Ni siku ya Ijumaa, siku ambayo ilikuwa imetawaliwa na jua kali sana ndani ya wilaya ya Korogwe, mkoa wa Tanga. Wilaya hii ilikuwa imetawaliwa na eneo la tambarare kwa ukubwa wake, licha ya baadhi ya maeneo kuwa na misitu na baadhi ya miti. Lakini kwa maeneo ya mjini, hayakuwa na miti mingi sana, hasa katika pembe ya barabara kuu iliyokuwa ikiunganisha mkoa wa Moshi–Arusha na Pwani–Dar es Salaam.
Wilaya ya Korogwe ni wilaya ya pili kwa kuwa na maendeleo ya wastani, ukiachana na wilaya ya Tanga mjini ambako ndio makao makuu ya mkoa.
Pembezoni mwa barabara hiyo iliyokuwa ikiunganisha mkoa wa Tanga, Arusha, na Dar es Salaam, alionekana kijana mmoja akiwa anatembea kwa unyonge sana, huku akionekana amechoka sana. Ukizingatia jua lilivyokuwa kali, ilikuwa ni zaidi ya taabu mbele ya barabara hiyo, huku mgongoni akiwa amebeba mfuko mmoja mdogo ambao ulionekana kuwa wa zamani sana. Mifuko hii ilikuwa ukiubeba mgongoni, huku ukiwa na kamba ambazo zilitumika kama mikanda ya begi, na ndani ya mfuko huo alionekana akiwa amebeba nguo.
Licha ya kijana huyu kuonekana akitembea barabarani, lakini hata mavazi yake yaliwakilisha kile kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake. Alitembea kwa umbali mrefu kidogo mpaka akafika sehemu moja iitwayo Mwembeni, sehemu ambayo ndio anaingia mjini Korogwe.
"Hapa sina hata hela, ila lazima nifike jijini Dar kwa njia yoyote ile. Pia nitakula nitashiba, ngoja uone. Kwanza nikale kwenye kibanda kile mgahawani pale," aliwaza yule kijana huku akikisogelea kibanda kwa kujiamini kabisa. Wakati huo hakuwa hata na shilingi mia mfukoni, zaidi ya mfuko wake wa kubeba mgongoni.
Baada ya kufika ndani ya mgahawa ule, alitafuta meza ambayo kuna mzee mmoja nae alikuwa akipata chakula.
"Mzee, shikamoo!"
"Marhaba, kijana," aliitika huku akiendelea kula, na hakutaka maongezi zaidi. Kwani kwa muonekano wa yule kijana, aliona kabisa kaja eneo lile kwa ajili ya kumuomba hela ili na yeye apate chakula. Kwani mara nyingi alizoea kuona vijana wengi wenye tabia hiyo kuja sehemu ile na kuomba hela.
“Karibu kaka, nikuletee chakula gani?” aliongea mhudumu.
“Weka msosi kama anao kula huyu mzee,” aliongea vile kwa makusudi, maana aliona huyu mzee kama alikuwa akidhania kuwa atamuomba hela. Kwa hiyo, aliagiza vile ili kumkomoa.
“Kaka, chakula chake hicho ni elfu kumi. Utaweza kulipa?”
“We mhudumu, mteja si kakuagiza. We, lete kama alicho omba. Unahoji maswali ya nini?” aliongea yule mzee huku akitaka kuona kweli kama atamudu bei ya chakula.
Ndani ya muda mfupi, mhudumu aliweka chakula kwenye meza, na jamaa huyu bila ya kupoteza muda aliamka na kunawa mikono na kuanza kula msosi huu kwa mbwembwe zote mpaka akamaliza. Huku yule mzee aliekuwa akila chakula bado alikuwepo pale pale kwenye ile meza akichati na simu yake kubwa, na yote alifanya vile kutaka kuona kama huyu kijana ataweza kulipia kile chakula. Maana ukizingatia jinsi mavazi yake yalivyo chanika chanika, halafu ale chakula cha zaidi ya elfu kumi, ilikuwa ni kichekesho na alitaka kuona mwisho wake.
Kijana baada ya kumaliza kula chakula kile, aliagiza maji ya buku ya uhai na kisha akanywa kidogo. Na pale pale, yule mhudumu alikuja kwa lengo la kuchukua hela.
Lakini kabla hajakaribia meza waliokuwepo, aliitwa na mteja mwingine kwa ajili ya kuchukua hela.
"Mzee," aliita yule kijana, na yule mzee akaangalia na kuitika. Lakini cha kushangaza, yule kijana alifumba jicho moja kwa sekunde mbili na kisha kuliachia. Na bila ya kuongea chochote, alinyanyuka na kuchukua maji yake na kutoka ndani ya ule mgahawa. Lakini wakati anakaribia kutoka, mara yule mhudumu alimwita.
"Wee kaka, mbona hujalipia na unataka kuondoka?"
"Nishamwachia yule mzee hela, na inayobaki tumia mrembo ee," alisema yule kijana. Basi yule dada alimfuata yule mzee na kumuomba ampe hela alioachiwa. Na kumbuka, kijana hakutoa hela yoyote pale, zaidi ya kula na kuondoka.
"Anhaa, kweli kaniachia elfu ishirini, na inayobaki kasema... inayobaki tumia mremboo," aliongea yule mzee huku akitoa walleti. Kitu kilichomshangaza yule mhudumu maana hela katoa kwenye walleti, lakini hakutaka kujihangaisha sana zaidi ya kupokea na kufurahia. Kwani yule kijana alikuwa ametumia elfu kumi na moja, kwa hiyo iliyobaki ilikuwa elfu tisa.
Yule mzee baada ya masaa mawili kupita alijikuta akiwa amekaa pale pale hotelini, lakini ni kama mtu alierudiwa na kumbukumbu.
"Duuh! Hivi yule kijana alilipa?" alijiuliza huku akinyanyuka na kumfata yule mhudumu na kumuuliza.
"Ndio alilipa, mbona tena hela alikuachia wewe au ushasahau na kanipa mpaka chenchi."
"Unasema hela nimetoa mimi?" aliuliza yule mzee kwa mshangao.
"Mhmh, ndio mzee. Tena hela si umetoa kwenye walleti yako wewe?"
Yule mzee bila kujiuliza alitoa walleti yake na kuanza kuhesabu hela zake, lakini alijikuta akipagawa maana ni kweli kuna upungufu wa shilingi elfu ishirini.
"Umesema ameondoka saa ngapi?"
"Muda mrefu kama masaa mawili yaliopita."
"Duuh!.. Basi asante kwa chakula," alisema yule mzee huku akijikuta akipata mfadhaiko kwani hela yake kamlipia yule kijana huku akiwa hana kumbukumbu ya aina yoyote ile.
"Daah! Leo nimeumbuka. Yule dogo lazima atakuwa mchawi. Yule sio bure. Ila siku nitamkamata tuu. Hela yangu haiendi buree. Ila atakuwa yupo vizuri maana kama ni chuma ulete, asingeniweza. Nimezindikwa vya kutosha na pia hirizi yangu ipo kiunoni. Iweje ameniweza?"
Yule mzee alikubaliana na yalio mtokeo na kuondoka zake...... Yule kijana ni nani? Swali hilo likabaki kwenye kichwa chake.
*******
1995 - DAR ES SALAAM, 1800 HOURS PM
Katika moja ya maeneo ambayo yanasifika kama sehemu (Neighbourhood) ambazo matajiri wengi huishi ndani ya jiji la Dar es Salaam ni Masaki na Osterbay. Na hili sio kwa hapa Tanzania tu, lakini pia kwenye nchi nyingi na majiji makubwa huwa na maeneo ambayo yamejitenga kama maeneo ambayo wanaishi walio nazo. Kwa mfano tu, China kuna Central Park. Hii ni moja ya sehemu ambayo inaaminika matajiri wengi wanaishi. Kwa hiyo, sio jambo la kushangaza sana, ni jambo la kawaida kwa watu kuonesha uwezo wao wa kipesa pale wanapokuwa nazo. Yapo maeneo mengi ndani ya majiji tofauti makubwa duniani ambayo matajiri wengi wamejitenga na watu wa vipato vya chini.
Ndani ya eneo hili la Masaki, wakati familia nyingi zikiwa ndani ya mageti yao katika maeneo haya tulivu, kuna familia moja ambayo haina muda mrefu tangu ihamie maeneo hayo. Alionekana dada mmoja ambae alikuwa akisukumwa nje na mlinzi wa nyumba hiyo baada ya kupata maelezo kutoka kwa bosi wake huyo ambaye alifunga ndoa hivi karibuni na kuhamia maeneo hayo ya ushani. Kwani baba yake alikuwa tajiri mkubwa aliekuwa akihusika na biashara za usafirishaji wa mizigo (Cargo Transit And Swift Logistic Company), kampuni ambayo ilikuwa ikisifika sana kwa usafirishaji wa mizigo ambayo makao yake makuu yalikuwa maeneo ya Mikocheni, nyuma kidogo kabla hujakaribia jengo la Airtel, ambalo kwa miaka hiyo ya tisini jengo hilo halikuwepo.
Na moja ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ni kijana Samiri ambae alikuwa ndio CEO (Mkurugenzi Mtendaji) wa kampuni hiyo, huku baba yake akiwa mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo kubwa Afrika Mashariki.
Tukirudi huku Masaki, baada ya mwanadada yule kufukuzwa, alijikuta akilia sana huku akianza kukumbuka siku alio kutana na Samir katika biashara zake za uchangudoa. Lakini kutokana na matakwa ya mteja wake kutotumia kondomu, basi alijikuta akibeba ujauzito bila mategemeo. Lakini kama ilivyokuwa kwa wadada wengi wapatapo ujauzito wa kutotarajia, basi huwa wanachukua maamuzi ya kutoa mimba hizo. Na wazo hilo lilimjia Irene, mwanadada ambae alipata ujauzito kutoka kwa Samir. Lakini kilicho muhuzunisha na kuchukua maamuzi ya kuicha mimba ikue ni baada ya kuambiwa na daktari wakati akitaka kutoa mimba hiyo kwamba kama atatoa mimba hiyo, kuna asilimia tisini za kutoweza kupata ujauzito tena na asilimia kumi za kupata ujauzito tena. Ndipo daktari alipo mshauri kwenda kujifikiria kwanza kama atoe ujauzito huo asipate mtoto maisha yake yote ama auche. Ulikuwa ni uchaguzi mgumu sana kwake, ukizingatia na hali ya maisha alio kuwa nayo. Alijikuta akilia sana usiku mpaka alipo kuja kuamka na kupata wazo la kumtafuta mtu alie mpa ujauzito huo kuona kwamba ni kipi atamwambia, kama angeweza kukubali ujauzito huo. Japo alikuwa na uhakika mdogo sana wa kukubaliwa na huyo mwanaume alie mjua kwa jina la Samir, kwani alijulikana sana kwa utajiri alio kuwa nao pamoja na kupenda maisha fulani ya kuonekana pamoja na kununua dada poa kila anapojisikia.
Irene hakupata shida kupata sehemu anayoishi Samir. Alifanikiwa kufika nyumbani hapo na aliruhusiwa na kuingia ndani na kumkuta Samir na mke wake Shani, ambae licha ya kuwa wachumba wa muda mrefu, ndio walioana siku chache tuu zilizo pita. Baada ya Irene kumkuta Samir, Samir kwanza alishtuka kwani anamkumbuka vizuri Irene, japo hakumfahamu jina, ila alimkumbuka kwa kumnunua na kulala nae hotelini.
"Samahani jamani kwa kuwaingilia na jioni hii," aliongea Irene.
"Hakuna shaka, karibu," walimkaribisha Irene, aliekuwa akiendelea kushangaa mandhari ya kuvutia ya nyumba hiyo na kujisemea kuwa kuna watu wanaishi sehemu nzuri sana.
"Nina mazungumzo na wewe kaka."
"Okey, hapa au nje ya hapa?" aliongea Samir.
"Hata hapo nje tafadhali," alisema Irene. Basi Samir alitoka na Irene mpaka nje kwa ajili ya mazungumzo, huku mke wake japo alitamani kusikia kilichokuwa kinakwenda kuongelewa, ila alijikuta akikubaliana na mume wake kuongea na huyo mwanamke.
"Nadhani unanikumbuka vizuri?" alianzisha maongezi Irene.
"Ndio, sura yako inakuja kuja hivi."
"Sitaki kwenda mkato mkato. Nimekuja sio kwa ajili ya kukubebesha hili swala, ila nimekuja unipe ushauri na kama utapata moyo wa kunisaidia maana hapa nilipo nimchanganyikiwa sijui cha kufanya."
"Mbona unanitisha dada? Jambo gani hilo?"
"Siku ile ulivyokuja kupata huduma kwangu, kama unakumbuka, ulikataa kutumia kondomu, na mimi sikutarajia lakini nimepata ujauzito wako."
"Whaat!!!.. Wewe dada una kichaa?" aliongea Samir kwa mpayuko ulio sababisha hata mke wake alie kuwepo sebuleni kuja kuangalia kinachoendelea.
"Mume wangu, nini tena?"
"Shania, hakuna kitu mke wangu. Kuna jambo limenishangaza hapa."
"Mhmh, haya," Shania alirudi ndani na kuwaachaa.
Lakini Samir pale pale alienda mpaka getini na kumuita mlinzi aitwae Juma.
"Wewe Juma, unaruhusu je watu wa ajabu ajabu wanaingia nyumbani kwangu?" alisahau kama yeye mwenyewe ndo alimruhusu.
"Bosi, samahani sitorudia tena," Juma alijibu na kuomba msamaha japo hakufanya kosa.
"Sasa sikia, nenda kamtoe pale kimya kimya mke wangu asijue haraka sana. Usilete watu vicha vichaa ndani kwangu."
Juma bila kupinga oda ya bosi wake alikwenda kumburuza Irene kimya kimya na kumsukumia nje ya geti.
Samir alijikuta akipata hasira na wasiwasi juu ya jambo lile. Haraka haraka aliingia chumbani kwake na kuvuta droo na kutoa kiasi cha pesa, huku mke wake akimuangalia tuu.
"Mume wangu, unapeleka wapi hizo pesa?"
"Subiri nakuja kukuhadithia mke wangu," huku akitoka nje.
"Juma yuko wapi?"
"Nishamtoa nje."
"Sikia, hebu nifungulie haraka haraka," Juma alifungua na Samir akatoka nje. Na bahati ni kwamba Irene hakwenda mbali.
"Sikia we kahaba, naomba usije ukakanyaga nyumbani kwangu kuanzia leo. Sitaki kujua unacho ongea ni cha kweli ama uongo. Shika hii pesa utajua mwenyewe cha kufanya," aliongea Samir na kumtupia zile hela chini.
Irene alijikuta akilia sana, ila upande mwingine alipata nafuu baada ya kupata zile hela kwani pia haikuwa nia yeye kwenda kukubaliwa kwa mimba ile. Ila alitaka tu kubahatisha kama anacheza mchezo wa bahati nasibu, maana ni naninage kukubali mimba ya mwanamke anajiuza.
“Samahani sana kaka kwa kusababishia mawazo na kukukosesha amani. Lakini jisikie huru kabisa. Sikuja kukuambia tulee hii mimba, ila nimekuja unipe msaada wa kimawazo. Lakini nakuhakikishia hii mimba nitaelea lakini hakika mwanangu hatokuja kujua kama wewe ndio baba yake, japo huo ndo ukweli kama hii mimba ni yako. Naomba usahau kuhusu hili. Nitaitumia hii pesa kama moja ya matumizi kwa mwanao atakapo zaliwa. Kwaheri," aliongea Irene maneno hayo na akaondoka zake, huku Samir nae baada ya kumwangalia mwanadada huyo mpaka alipo yokomea ndipo akaondoka zake.
ITAENDELEA KESHO SAA NNE USIKU USIKOSE SIMULIZI HII YA KUELIMISHA NA KUCHEKESHA KWA WAKATI MMOJA
Comments