Reader Settings

Irene, baada ya kurudi kwenye chumba chake alichopanga maeneo ya Sinza, alifungua zile hela na kuanza kuzihesabu. Alizikuta ni milioni mbili na hamsini. Kwanza, alishukuru sana kwa hela hiyo na kuona ni msaada mkubwa sana ambao amepata. Ndipo alipoamua kuacha biashara yake ya kujiuza na kuanzisha biashara ya kuuza mkaa katika eneo la Tegeta. Biashara hiyo ilimwezesha kujipatia kipato, huku kiasi kidogo alichokuwa akipata akikitunza benki kwa ajili ya mtoto wake atakayejifungua. Baada ya miezi tisa, alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume ambaye alimpa jina la Peter.

Mtoto Peter, maendeleo yake ya ukuaji hayakuwa mabaya, na hatimae alifikisha umri wa miaka sita na kuanzishwa shule kwenye darasa la kwanza. Siku zilizidi kusonga, na hatimae Peter alifikisha darasa la saba. Ndipo mama yake Irene alipopata ajali ya kugongwa na gari. Ilikuwa ajali moja ya kusikitisha sana kwani alifia hapo hapo. Lakini kilichowashangaza wengi ni mazingira halisi ya ajali hiyo, kwani ilionekana kama mgongaji alidhamiria kumgonga mama Peter. Baada ya ajali hiyo kutokea, gari halikusimama, na namba za gari hakuna aliyeweza kuziona.

Ilikuwa ajali mbaya sana, ajali ambayo ilimfanya Peter kuwa yatima kwani mama yake alishawahi kumwambia kuwa baba yake alikwisha kufariki. Mtoto Peter alilia sana na kuhuzunika kumpoteza mama yake, hasa kwa wakati huo ambapo bado alikuwa akimhitaji sana, kwani alikuwa bado darasa la saba. Majirani walimuonea sana huruma, walijitahidi kumfariji, lakini kumfariji huko hakukuzaa matunda. Haikuwa na jinsi, kwani mama yake alikuwa amekwisha kufariki.

Baada ya siku chache, Irene au Mama Peter alizikwa katika makaburi ya Sinza. Maisha kwa mtoto Peter yaliendelea, na uzuri ni kwamba mama yake alikuwa amemuwekea pesa benki. Kwa hivyo, Peter hakupata shida sana ya matumizi. Baada ya miezi kadhaa kupita, Peter alifanikiwa kumaliza darasa la saba na kuanza kuendeleza biashara ya mama yake ya uuzaji wa mkaa. Mara nyingi, pesa aliyokuwa akiipata aliitunza kwani bado alikuwa na safari ndefu ya kusoma. Kutokana na msaada wa majirani zake, walimfanya Peter asijisikie kuwa mpweke sana.

Baada ya miezi kadhaa, matokeo ya kidato cha kwanza yalitoka, huku Peter akiongoza katika somo la hisabati na sayansi kwa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata A kwa kila somo. Ilikuwa habari njema sana kwa kijana Peter na kwa wale ambao walikuwa wakimpenda. Lakini bahati pia ikamwangukia Peter kwani wanafunzi wote ambao walifanya vizuri katika masomo ya sayansi walipata ufadhili chini ya kampuni ya R&J Foundation, kuwalipia ada na matumizi kwa kipindi chote cha masomo. Moja ya wanafunzi waliopata ufadhili huo alikuwa Peter. Sheria ya mkataba huo ilikuwa kusomea katika shule za serikali au za jeshi, kwa shule yoyote ile yenye bweni.

Kwa upande wa Peter, baada ya kwenda ofisini kwa ajili ya kukamilisha usajili wa ufadhili huo, alikutana na mwanamama mrembo ambaye, japo umri wake ulikuwa umeenda, alionekana kama kijana kwa uzuri wake pamoja na mavazi aliovaa yaliyokuwa ya bei ghali. Peter alikaribishwa vizuri na kujieleza pamoja na historia yake. Baada ya hapo, alichagua shule ya Makongo Sekondari, lakini akikataa kukaa hostel kama sheria za ufadhili huo zilivyoelekeza.

"Kukaa hostel za shule au kutokaa bado hakutakuwa na mantiki kama mwanafunzi mwenye mfadhili hatafanya vizuri katika masomo yake. Mimi naona nitafanya vizuri zaidi kama nitakaa nyumbani na kwenda shuleni asubuhi," alisema Peter.

"Okey, ni sawa lakini lazima uelewe kwamba kama itatokea umefanya vibaya katika masomo yako, tutaacha kukufadhili," alimjibu mwenye ofisi.

"Hakuna shida," Peter alifurahi sana. Hatimae, mwezi wa kwanza alianza kusoma katika shule hiyo ya Makongo, shule ya jeshi iliyopo kati ya Mbezi Beach na Mwenge ndani ya eneo la Lugalo.

Tukirudi kwa kijana tuliyemuona Korogwe

Baada ya kutoka mgahawani, alichukua barabara kuu huku akidhamiria kutafuta stendi ya mabasi. Alipouliza, aliambiwa stendi ipo mbele. Ndipo alipoamua kunyoosha miguu pasipo kujali jua lililokuwa likimwakia. Alitembea huku akipoozea na maji aliyochukua pale mgahawani.

"Japo Mungu hakunijaalia uwezo wa akili, lakini alichonipa namshukuru. Asante Mungu, nimeshiba," alisema huku akizidi kusonga mbele mpaka akafika eneo liitwalo Majengo. Ndipo aliposimamisha mtu na kuuliza kuhusu stendi ya mabasi. Baada ya kuelekezwa, alifuata barabara hiyo hatimae aliingia stendi. Lakini wakati anatembea, alikuwa akiyafikiria mawaidha aliyokuwa akipewa na mama yake kabla hajafariki.

"Mwanangu, najua una uwezo wa kumpumbaza mtu kwa muda mfupi na kumfanya afanye kile unachotaka, lakini isiwe chanzo cha wewe kuanza kuwadhulumu watu na kufanya uhalifu. Hakikisha unajipatia kipato kilicho halali. Shida zako zisikufanye ukiuke sheria za ulimwengu. Kumbuka, kile ulichojaliwa na Mungu ni kama zawadi, lakini sio siraha ya kuwachapia watu," alikuwa akimwambia mama yake.

Hayo ni maneno ambayo kijana huyu, ambaye bado hatujapata kumjua jina, aliyakumbuka. Alikuwa akimwambia mama yake, "Mama, nisamehe sana, lakini sina jinsi. Lazima nitumie uwezo wangu nilio nao ili nifikishe Dar kutafuta maisha."

Alipoingia stendi, moja kwa moja aliinyoosha kwa wakata tiketi na kudhamiria kukata tiketi. Lakini wakati huo hakuwa na hata shilingi mia mfukoni, zaidi ya mavazi yake yaliyochakaa huku baadhi ya sehemu zilionekana zimechanika.

"Dogo, unaelekea Dar? Njoo nikukatie tiketi chapu. Gari linafika sasa hivi," aliongea moja ya watu wanaokata tiketi. Lakini kilichomfurahisha kijana huyu ni mkataji tiketi yule kutombagua kutokana na mavazi yake.

"Dogo, unaitwa nani?"

"Unasema?"

"Jina lako nani?"

"Naitwa Bahati Masumbuko."

"Dogo, kweli wewe kwa muonekano wako, masumbuko kakuzaa kwa bahati."

"Hata mimi naona broo."

"Poa, toa hela chapu. Tiketi yako hii hapa, na gari lile ndio linaingia."

"Broo..." Aliita kijana huyu ambaye jina lake ni Bahati Masumbuko, na pale pale akachezesha jicho lake kwa staili ya ajabu kama vile anakukonyeza.

"Dogo, shika tiketi yako. Nilisahau kumbe ulianza kutoa pesa," aliongea yule jamaa huku Bahati akipokea tiketi yake na kwenda kupanda gari.

"Nisamehe sana broo, mimi sio mchawi, ila inanibidi kufika Dar kutafuta maisha. Nitakuja kukulipa," alijiongelesha mwenyewe Bahati huku akiingia ndani ya basi.

Baada ya masaa mawili, yule mkata tiketi alijikuta kama anatoka usingizini kwani ndipo alikumbuka kuwa yule dogo hakutoa pesa na gari ilishaondoka.

"Yule dogo nilimuachia achia je, au mchawi? Ngoja nimpigie Ayubu achukue hela aache uhuni (Ayubu ni konda), au alilinipa sikumbuki," huku akitoa simu na kuanza kupiga.

Simu ilimshtua Ayubu ambaye alikuwa bize akiangalia movie ya Majuto kwenye TV ya gari. Aliichomoa na kuweka sikioni baada ya kuona ni rafiki yake.

"Oya mzee, kuna dogo sijui nimemuachia achia vipi. Nimemkatia tiketi lakini hela hajatoa. Anaitwa Bahati Masumbuko. Hebu fanya mpango uichukue."

"Una uhakika hajatoa au umesahau? Kama ametoa?"

"Nina uhakika, ila sikumbuki vizuri."

"Sasa una uhakika halafu hukumbuki vizuri? Jibu sahihi ni lipi? Ndo maana nakwambia uache kuvuta bangi mchana wewe."

"Oya Ayubu, hebu muulize tu kama amenipa au hajanipa."

"Poa, ngoja nimcheki."

Konda wala alikuwa anamkumbuka vizuri Bahati kutokana na muonekano wake wa mavazi. Halafu, isitoshe, kapanda gari ya Luxury.

"Dogo, vipi eti ulipokata tiketi ulitoa hela?"

"Wewe konda, na wewe sasa kaingia je humu kama hajatoa pesa au kisa anamavazi yaliyochakaa ndio kinachokutia wasiwasi?" Alijibu mama mmoja aliyekuwa na rafudhi ya kitanga Tanga.

"Mama, mimi nimeuliza tu maana aliempa tiketi kanambia ana uhakika ila hakumbuki vizuri kama alitoa hela."

"Sasa ushasema ana uhakika na hakumbuki vizuri? Jibu ni kwamba kijana ametoa pesa mfyuu..."

"Wewe dogo, ulitoa hela?"

"Nilitoa ndio," alijibu Bahati Masumbuko na kumfanya konda atulie na kurudi zake mbele huku safari ikiendelea.

"Hapa nikifika kwanza, niitafute Milimani City niingie, kisha niitafute Kariakoo ndio mambo mengine yaendelee," aliwaza Bahati Masumbuko huku akijikuta anafurahi kwani ndoto zake za kuliona jiji la Dar muda si mrefu zinaenda kutimia. Hayo yalikuwa ndio mawazo ya bwana Masumbuko. Hakuwaza nani atampokea, atakaa kwa nani, au atalala wapi na kuishi vipi.

Ndani ya muda wa saa moja kuelekea na nusu, ndio muda ambao basi alilopanda Bahati Masumbuko lilikuwa likiingia stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani, yaani Ubungo. Basi ilijiegesha kwenye eneo lake na kuruhusu abiria watoke kwani walikuwa wamefika.

Bahati nae aliamshwa kutoka usingizini kwani alikuwa amesinzia tokea muda mrefu, na hata gari lilivyofika hakujua limefika muda gani.

"Wewe amka, gari lishafika Ubungo," aliongea mama aliyekuwa amekaa pembeni yake huku akichukua begi lake na kutoka nje.

Bahati alijikuta akianza kushangaa baada ya kuona upande wa pili taa zinawaka kwenye jengo lililopo hapo Ubungo. Alichukua kijimfuko chake na kutoka haraka mpaka nje ya basi na kuanza kuendelea kushangaa.

Peter alianza shule kidato cha kwanza

Na siku kadiri zilivyokuwa zikisogea, alijikuta akifahamika haraka sana kutokana na uwezo wake wa akili darasani, huku akionyesha ubingwa wake zaidi katika somo la Mathematics (hesabu) na komputa (tarakishi). Ndani ya miaka miwili tu, Peter alikuwa moto sana kwenye somo la komputa na hisabati kwani alikuwa ameshajua kila kitu kuhusu komputa.

"Vipi Peter?"

"Safi, niambie kaka."

"Vipi baadae, nataka nije getoni kwako unisaidie kunielekeza maswala ya Excel na Publisher. Yananizingua kinoma," aliongea jamaa mmoja anayefahamika kwa jina la John ambaye yeye alikuwa kidato cha nne na Peter cha pili.

"Poa, hakuna shida. Wewe njoo," alimjibu huku wakitembea mpaka walipofika eneo la Smart Area, eneo ambalo hapo shuleni hauruhusiwi kutembea zaidi ya kukimbia.

Peter wakati huo alikuwa akiishi Mbezi Beach ambako alipangishiwa apartment (nyumba) na wafadhili wake baada ya Peter kuonyesha uwezo mkubwa darasani. Japo Peter alikuwa akilipiwa kila kitu, lakini hakuacha kufanya biashara yake ya mkaa ambayo ilikuwa kama urithi kutoka kwa mama yake Irene. Na kila pesa aliyokuwa akipata kwenye biashara hiyo, nusu alikuwa akiweka benki na nusu alikuwa akitumia kwenye matumizi yake madogo madogo.

"Baada ya muda wa jioni kukaribia, John alikuja nyumbani anapoishi Peter."

"Mzee, ndio maana uko vizuri kwenye komputa. Kumbe una madesktop himu ndani."

"Ndio mzee, naanza maandalizi ya kozi nitakayosoma nikimaliza shule tuu. Maana sina mpango wa kusoma kidato cha tano na cha sita. Nataka nipitie diploma kwanza."

"Unataka usome kozi gani sasa mzee?"

"Nataka nipige Computer Science."

"Duuh, kweli mzee, wewe fuata kipaji chako. Kitakutoa kimaisha."

Basi, John alielekezwa na Peter mpaka pale alipoelewa, ndipo aliondoka.

Baada ya miaka saba kupita, Peter alikuwa kichwa cha kuotea mbali sana katika maswala ya komputa, na wakati huo alikuwa chuo kikuu akimalizia kuchukua degree yake ya Computer Science katika chuo cha Dar es Salaam.

Siku moja, ikiwa ni wikiendi, Peter alikuwa maeneo ya Mlimani City ambapo yeye alikuwa upande wa nje kwani tayari alikuwa ameshanunua kilichomleta pale. Kwani siku hiyo alikuja kununua simu ya ndoto yake, simu aina ya Samsung Galaxy Note 10. Ila wakati yupo anajiandaa kuondoka, mara aliona gari moja zuri sana likiingia mahali hapo na kwenda mpaka kupaki mita kadhaa kutoka miguuni mwake. Alijikuta akiangalia gari hilo, lakini alijikuta akipata kushangaa zaidi baada ya kumuona moja ya msichana mrembo sana akiwa amevalia gauni jekundu akishuka kwenye gari hilo. Wakati anaendelea kushangaa, alishuka mwanaume ambaye Peter alimjua kwani alikuwa maarufu sana nchini, ambaye watu walipenda kumuita Bosi Samir.

"Huyu mtoto atakuwa wa huyu bosi. Huyu demu nitafanya jua chini nilale nae."

"Aiyaaa... Mamaaaa, simu yanguu jamani mwiziii..." Peter alijikuta akiropoka kwani simu aliyokuwa amenunua muda si mrefu uliopita ilipakuwa kwa kushangaa kwake.

Previoua