FOR YOU
Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
Rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA PILI
★★★★★★★★★★★★
Ikiwa ni mida ya saa 3 usiku, familia ya mapacha hawa ilikuwa mezani ikipata mlo wa mwisho wa siku kabla ya kwenda kupumzika. Alikuwepo Alexander, Alexandra, mama yao aliyeitwa Alice, mdogo wao mwingine wa kike aliyeitwa Azra ambaye alikuwa na miaka 14, na msaidizi wao wa kazi aliyeitwa Salome. Walimtendea Salome kama mmoja wa familia yao kwa kuwa alifanya kazi hapo kwa muda mrefu sana, hata watoto walimwita dada yao mkubwa.
Alice alikuwa mwanamke mrembo, mweupe sana, akiwa na mwonekano kama mhindi, na mwenye mwili wenye unene wa wastani. Ni kutoka kwake ndiyo watoto waliutolea weupe, maana hata Azra alikuwa mweupe sana na mwenye sura nzuri. Alice alimiliki maduka matatu makubwa ya nguo na bidhaa nyingi za urembo sehemu mbali mbali jijini hapo, na alijulikana kwa wengi wa wateja wake kama "Alicious."
Hapa mezani palikosekana mtu mmoja tu, naye alikuwa ni baba ya watoto hawa. Walikuwa wamekwishazoea kupata milo bila yeye kuwepo, na ijapokuwa mara nyingi Alice angesema kwamba mume wake alikuwa akijitahidi, alishindwa kutenga muda mwingi pamoja na familia yake kutokana na kuwa bize sana na kazi yake. Siyo kwamba labda wazazi wao hawakupatana; walipendana sana. Lakini kazi ya baba huyo ilimnyima muda wa kutosha kuwa pamoja nao, hivyo hawakuwa na budi ila kuzoea maisha hayo.
Sikuzote Alice alikuwa mama mwelewa na aliyewapenda sana watoto wake. Mara nyingi aliwaelezea kwamba baba yao anapigana sana kwa ajili yao na taifa lote kwa ujumla, kwa hiyo ijapokuwa hakuonekana mara nyingi mbele yao, hawakupaswa kusahau kuwa aliwapenda sana.
Hili ni jambo ambalo lilimfanya Xander apoteze kabisa ukaribu na baba yake, kwa sababu aliona ni kama baba yake alichukulia kazi kuwa muhimu zaidi ya familia. Ingeonekana labda mara nyingine anamhukumu vibaya, lakini kiukweli baba yao alikosa muda wa kuwa pamoja na watoto wake kwa kipindi kirefu mno. Wasichana wenyewe walikuwa waelewa na walionyesha kumkubali sana baba yao, lakini Xander hata hakujali kuhusu habari zake.
Wakawa wanafurahia chakula huku wakipata na maongezi. Walikuwa wanazungumzia kuhusiana na sherehe ya mama yao ya siku yake ya kuzaliwa, ambayo ingefanywa hapa hapa nyumbani siku chache mbele. Alikuwa akitimiza miaka 45. Alice alitaka sherehe hii ifanywe kwa njia rahisi tu bila kuhusisha mambo mengi kupita kiasi kama watu wanaofanya mambo kujionyesha mali zao. Angealika marafiki kadhaa na ndugu waliokuwa karibu ili waifurahie pamoja naye. Ilikuwa wazi kwao kwamba huenda baba yao angeikosa, ijapokuwa aliwaambia kwamba angejitahidi kufika. Kama kawaida Xander aliona huo kuwa uwongo tu, lakini akaona siyo mbaya kuwaacha wengine waote.
Sasa wakawa wanamzungumzia Sandra.
"Kwa hiyo mashindano ni tarehe 9? Hiyo ni Jumamosi ya wiki ijayo, si ndiyo?" Alice akamuuliza Sandra.
"Ndiyo," akajibu Sandra.
"Birthday party ya mama ni Jumamosi, na mashindano yako Sandra ni Jumamosi. Hadi raha," akasema Azra.
"Ahahah... yeah," Alice akamwambia Azra.
"Yaani... I'm really nervous! Nimepangwa kuwa namba nne, kwa hiyo natakiwa kuwa faster sana," akasema Sandra.
"Hiyo inamaanisha nini?" akauliza Azra.
"Yaani... kwenye timu ya uogeleaji, wakati wa mashindano na vyuo vingine..."
"Blah, blah, blah, blah..." Xander akamkatisha Sandra kiutani.
Sandra akamsukuma kichwa kwa kidole chake, naye Xander akawa anacheka.
"Acha basi nawe mwenzio amwelezee mtoto," Alice akamwambia Xander.
"Mtoto! Hivi mama unajua huyu ana miaka mingapi? Au basi ngoja tu nisikwambie," Xander akaongea hivyo kiutani.
"Achana naye huyu. Em' Sandra endelea," Azra akasema.
"Endelea Sandra," akasema Salome.
"Bichwa lako wewe, ole wako unikatishe tena," Sandra akamwonya Xander.
"Blah..."
Xander akasema hivyo kiutani huku anamwangalia Sandra, naye Sandra akamkata jicho kali. Akaziba mdomo na kuendelea kula.
"Yaani... ni kama tu mpira wa miguu. Kunakuwa na yule anayetegemewa kufunga magoli. Lakini yule anayemsaidia kutengeneza nafasi ya kufunga ndiyo huwa anatoa pasi eeh... ndiyo kama mimi sasa. Yaani namba yangu ni ya kuhakikisha nakuwa na kasi sana ili wa mwisho kuingia amalize vizuri..." Sandra akamwelezea Azra.
"I swear dogo alikuwa ameshasinzia uliposema tu kufunga magoli," Xander akatania.
"Hamna! Mwaya Sandra nimeelewa," Azra akasema huku anamwangalia Xander kwa jicho kali.
Xander akafanya kama kumzomea.
"Mama... baba ni lazima atakuwepo si eti?" Sandra akamuuliza Alice.
"Mhm... sahau," akasema Xander.
"Ndiyo atakuwepo. We naye mbona unakuwa hivyo?" Alice akasema.
"Ah, me mama naongelea hali halisi kwa jinsi inavyoonekana. Like, hii siyo mara ya kwanza baba ata-miss event kubwa kwenye career anayotengeneza binti yake. Akiikosa hii itakuwa mara ya tatu... kwa hiyo inabidi Sandra azoee hilo na asitarajie mengi," Xander akasema.
Wote wakamwangalia sana kama wanatafakari alichosema. Sandra akahuzunika kwa kuwa maneno ya pacha wake yalikuwa na ukweli ndani yake.
"Atakuwepo. Alikuahidi atakuwepo. Wewe jitahidi tu kuwa the best kama siku zote, sawa?" Alice akamwambia Sandra.
Sandra akakubali na kuingiza chakula mdomoni mwake.
"Mama, Sandra is the best. Hakuna asiyejua hilo. Lakini zamu hii haitakuwa kama kipindi cha nyuma, kwa sababu hii ni national. Anahitaji support ya familia nzima maana itakuwa baab kubwa. Vyuo mbalimbali nchini vinashindanisha waogeleaji bora zaidi. Lakini kama tu mzee atakavyo-miss birthday party yako, na event ya Sandra..."
"Xander, enough!" Alice akamkatisha kwa uthabiti.
Watoto wote wakamwangalia mama yao kwa hofu.
"Nimesema atakuwepo. Usimvunje moyo dada yako, ukoje lakini?" Alice akasema kiukali.
"Angalau mimi naweza kuhandle mama, lakini Sandra huwa anaumia. Hasemi, lakini anaumia. Hii siyo tu kuhusu mashindano yake, ni muda mrefu kiasi gani baba hajaonyesha sura yake hapa? Anatumikia taifa mpaka anasahau wanae? Na siyo kwamba labda hata ni mbali sana... mbona wenzake huwa wanarudi kwenye familia zao? Yeye ndo' analipenda taifa sana kuliko watu wooote nchini..."
"Xander nenda chumbani kwako," Alice akamkatisha.
"Usimpe dada yangu matumaini fake. Kama haji, haji tu..." Xander akaongea kwa hisia na kuondoka hapo akiwa ameudhika.
Machozi yalikuwa yanamlenga Sandra, aliyehisi huzuni moyoni mwake. Azra na Salome wakawa kimya tu wakielewa kuwa hali ya hewa hapo ilikuwa imekwishavurugika. Alice akamwangalia sana Sandra, kisha akamwambia aendelee kula. Lakini Sandra akanyanyuka taratibu na kusema alikuwa ameshiba, hivyo naye akaelekea chumbani kwake. Alice alihisi huzuni sana moyoni mwake mpaka hamu ya kula ikamtoka. Muda fulani baadae, wote wakawa kwenye vyumba vyao tayari kwa kulala.
★★
Nyumba yao ilikuwa kubwa, pana, na yenye ghorofa juu ambalo ndiyo lilikuwa na vyumba vyao vya kulala. Alice na mume wake walikuwa na chumba chao kikubwa, Alexander na Alexandra wote walikuwa na vyumba vya peke yao, naye Azra pia alikuwa na cha kwake. Vyote vilitengenezwa kwa umaridadi mzuri na vilijaa vitu vyao vingi vizuri. Salome alikuwa analala kwenye chumba kizuri sehemu ya chini ya nyumba hiyo, na sehemu ya sebule ilikuwa pana sana yenye sehemu ya masofa na meza, sehemu ya kulia chakula, ya mapishi na vyombo, na vyumba kwa ajili ya mashine za kufulia nguo.
Kwa nje kulikuwa na kiwanja kipana chenye bustani nzuri na majani yaliyokatwa vizuri chini, sehemu ya kuegeshea gari za wazazi na pikipiki ya Xander, nayo ilizungukwa na uzio wenye kuta ndefu zenye ulinzi wa vyuma vya umeme. Karibu na getini, kulikuwa na nyumba ndogo iliyojengwa pembeni kwa ajili ya walinzi wao. Walikuwa ni walinzi wenye mafunzo ya jeshini, nao waliilinda vizuri sana nyumba hii pamoja na mbwa wao mkali sana aliyewazoea wao tu na familia hiyo.
Xander alikuwa chumbani kwake akiandika kazi ile ambayo madam Valentina alikuwa amempatia kufanya. Alizama kwenye utafiti mwingi sana kwenye laptop yake wa mambo aliyotaka kujua kuhusu kile alichoandika, hivyo hakutilia maanani wakati simu yake ilipoita sana. Baada ya kuangalia mpigaji baadae, akapuuza na kuendelea kuandika. Kidogo hii ilimsaidia kupotezea kilichotokea mezani na mama yake kwa sababu mambo aliyoandika yalimfanya azame sana kiuandishi na kihisia pia. Sandra yeye aliwahi tu kulala baada ya kuwasiliana na mpenzi wake, Raymond, nao Azra na Salome walikuwa mbali kiusingizi pia.
Alice alikuwa chumbani kwake akifikiria vitu fulani. Usingizi haukumjia kabisa kwa sababu ya kumwaza mume wake. Ilikuwa imepita miezi mingi sana bila kuonana naye, na kiukweli alimkosa sana. Mara nyingi waliwasiliana kwa njia ya "video call," lakini bado alimhitaji karibu yake. Alijua maneno ya mwanaye yalibeba ukweli fulani, na ilionekana kwamba hakuwa na jinsi ila kuyakubali tu maisha haya jinsi yalivyo, ila sasa yalikuwa yameanza kumchosha. Hata leo Sandra alimwonyesha kwamba yeye pia anavunjwa moyo sana na baba yake.
Hiyo ilikuwa ni kwa nini? Kwa sababu kipindi cha nyuma walikuwa familia yenye ukaribu sana, na baba yao alijitahidi kuwaonyesha upendo wake kwao kwa kuwapatia muda wake mwingi ili wautumie pamoja kama familia. Lakini baada ya yeye kupokea majukumu ya juu zaidi kazini, mambo mengi yakabadilika. Akiwa amekaa kitandani huku akiwaza kilichotoka kutokea kwenye meza ya chakula na mwana wake, simu yake ikaanza kuita, na kwa uhakika wa kutosha ilikuwa ni mume wake. Akapokea, nayo ilikuwa ni kwa njia ya video call kama kawaida.
"Hey honey... uhali gani?" mume wake akamsalimu.
"Salama tu. Za huko?" Alice akamjibu.
"Safi. Pole nimechelewa kukusemesha..."
"Usijali..."
"Nimetoka kuwatafuta watoto lakini hakuna hata mmoja aliyejibu. Wote wameshalala eeh?"
"Ndiyo... inawezekana."
"Alice... kila kitu kiko sawa? Mbona kama hauna furaha?"
"Yeah... nimechoka tu that's why..."
"Alice niambie. Nini tatizo?"
Alice akashusha pumzi na kuangalia pembeni.
"Ni Xander?" mume wake akauliza.
"Ndiyo. Ni Xander. Ni Sandra. Ni Azra. Ni sisi wote..." Alice akasema kwa njia ya kuudhika.
"Alice unajua kwamba line..."
"Your line of duty begs you to be there, I know. Lakini itaendelea kuwa hivi mpaka lini Casmir? Watoto wanakumiss sana... mimi pia. Ni miezi mingi imepita hujakanyaga nyumbani. Mbona wengine huwa wanarudi makwao hata kama ni kwa muda mfupi? Eeh? Casmir... inachosha. Hata kama mambo ni mengi jamani me najua kuna muda wa kupumzika tu. Badala uutumie kuwa na familia wewe unaendelea kuhakikisha mambo yako vizuri tu huko, vipi sisi?" Alice akamwambia kwa huzuni.
"Wow... Leo haitawezekana kujitetea hata kidogo," mume wake, Casmir, akasema.
Alice akatikisa kichwa kwa kusikitika.
"Nisamehe my wife. Nimekuwa mbinafsi sana. Natanguliza mambo mengi badala ya nyie... na najua ninawaumiza. Ila nataka ujue kwamba jambo hili halitaendelea kuwa namna hii tena. Nakuahidi. Nitafanya yote niwezayo kuwa pamoja nanyi tena..."
"Mara ngapi umetoa hiyo ahadi Casmir?"
"Najua. Najua. But this time nakuhakikishia sitaivunja. Believe me," mume wake akasema.
"Sawa. Utakuwepo kwenye mashindano ya Sandra si ndiyo?"
"Sitakosa. Ni tarehe tisa, lazima nitakuwepo. Nilikuwa ndiyo nataka niongee naye kumwambia kwamba nitamletea na ile swimsuit ya Vaziri Gemini anayoitakaga..."
"Ahah... umemnunulia?"
"Ndiyo. Niliagiza original tokea South Africa. Kazuri, katamtosha..."
"Okay sawa. Atafurahi sana."
"Look... najua Xander anaweza kuku..."
"No, no, no, usijali. Xander yuko poa. Ni kwamba tu wote tumekumiss sana... basi," Alice akasema.
"Hajakusumbua kwa maneno yake makali huyo dogo?"
"Ahahah... hapana. Tafadhali Casmir, timiza ahadi yako. Alexandra anahitaji sana kukuonyesha achievement zake. Anajali hilo sana. Usimwangushe," Alice akamwomba.
"Sitamwangusha. Wewe pia mke wangu. Nakuahidi nitakuwepo kwenye birthday yako," Casmir akasema.
Machozi yakaanza kumlenga Alice, naye akauliza kwa hisia, "Kweli?"
"Ndiyo. Nitakuwepo. Nakupenda sana Alice," Casmir akasema.
"Ahah... Nakupenda pia Casmir..." Alice akamalizia kwa hisia.
Baada ya hapo wakatakiana usiku mwema, naye Alice akajilaza na kuanza kuutafuta usingizi.
★★★
Asubuhi na mapema Alice aliwahi kuamka. Alikuwa na kawaida ya kuamka mida ya saa 2 asubuhi, lakini asubuhi hii aliwahi kuamka ili aweze kuongea na Xander. Sikuzote mapacha waliamka mapema na kuwahi chuoni pamoja, hasa kwa kuwa walitumia pikipiki ya Xander kwenda wote. Alice akashuka kutoka juu ya ngazi na kumwona Azra pamoja na Sandra pale sehemu ya sebuleni. Walikuwa na mionekano iliyomwambia kwamba walikuwa tayari kuelekea chuoni na shule.
Walipomwona mama yao, Azra akamkimbilia na kumkumbatia, kisha akamsalimu. Mama yao alimdekeza Azra sana kwa kuwa ndiye alikuwa kitindamimba, hivyo sikuzote alimtendea kama bado ni mtoto mdogo mno. Sandra yeye akamsalimu kutokea pale aliposimama, kisha Alice akaanza kumwelekea huku akiwa amemshikilia Azra kiunoni wakitembea pamoja. Akamuuliza kama alikuwa anamsubiri kaka yake, lakini Sandra akamwambia kwamba tayari Xander alikuwa ameshaondoka.
Kidogo hii ilimhuzunisha Alice kwa sababu Xander kuondoka mapema bila dada yake kulimaanisha bado alikuwa na hasira kutokana na mazungumzo yao ya jana usiku. Azra akamwambia mama yake kuwa aachane naye kwa sababu alikuwa ananunanuna kama mtoto mdogo wakati ni mkubwa. Sandra akamwambia mama yake kwamba yeye angechukua usafiri mpaka chuoni, lakini Alice akakanusha na kusema kwamba kwa kuwa aliwahi kuamka leo, basi angewapeleka binti zake hawa sehemu zao za masomo kwa gari lake mwenyewe.
Wote wakafurahi sana, kisha Alice akarudi juu kuvaa nguo nadhifu, na baada ya muda mfupi wakaondoka pamoja kwenye gari lake aina ya Camri nyekundu. Walianzia kwenye shule ya sekondari aliyosomea Azra. Shule hii ilikuwa ya kibinafsi na nzuri sana. Mtoto wa kike alikuwa kidato cha pili, naye alijulikana shuleni kuwa mtoto wa kishua sana. Mama yake sikuzote alimpatia pesa nyingi ya kutumia, lakini hakuwa aina ya msichana mwenye kujidai au mwenye nyodo. Alipenda watu wote, wala hakubagua watu kwa misingi ya hali zao. Alikuwa mwenye urafiki pia na alisoma kwa bidii.
Baada ya kumwacha Azra shuleni kwao, sasa Alice akaanza kumpeleka Sandra chuoni. Njiani mama huyu alimwambia kuhusu maongezi yake na baba yao usiku wa jana, naye akamwambia jinsi alivyomhakikishia kwamba angekuwepo siku ya mashindano yake. Sandra akaomba samahani kwa sababu alikwazika jana na kutenda kwa njia ambayo hakuiona kuwa sahihi baadae. Mama yake akamwambia alielewa ni jinsi gani alimpenda baba yake, hivyo hakupaswa kuhisi hatia.
Lakini bado akawa ana wasiwasi kuhusu mwenendo wa Xander. Hakujua angeshughulika naye jinsi gani. Kwa hilo Sandra akamwambia mama yake asiwaze kwa kuwa Xander alimwelewa sana, hivyo angezungumza naye vizuri halafu mambo yangekaa sawa. Alice akamshukuru kwa hilo na kusema naye angemtafuta mwana wake huyo kwa simu ili kutuliza hali. Akamfikisha binti yake chuoni na kuagana naye, kisha akaanza kuelekea kwenye mizunguko yake.
★★
Wakiwa bado chuoni mida ya mchana, Xander pamoja na rafiki zake; Mecky, Benjamin, na mwingine aliyeitwa Bernard, walikuwa wamekaa ndani ya chumba cha darasa ambacho hakikutumika kwa wakati huu (yaani hakukuwa na kipindi). Walikuwa wanapiga story za hapa na pale, kisha Ramla pamoja na rafiki zake wengine wawili wakaingia. Kwa madoido Ramla alienda moja kwa moja mpaka alipoketi Xander na kumkalia, nao rafiki zake Xander wakaanza kuwatania rafiki za Ramla kuwa na wao wawakalie.
Waliendelea kuongea mambo yenye kufurahisha mpaka pale Sandra alipofika kwenye chumba hicho, naye akamfata Xander moja kwa moja. Akamwambia alihitaji kuongea naye, lakini Xander akaweka mgomo na kuendelea kumsemesha Ramla sikioni huku akimtekenya. Sandra akiwa ameudhika kiasi, akamvuta Ramla na kumsukuma pembeni, jambo lililowashangaza wote. Kisha akamvuta mkono Xander pia na kuanza kumlazimisha waondoke. Waliobaki hapo wakaanza kuwaongelea mapacha hawa, hasa Ramla akisema ipo siku angekuja kumnyoosha huyo Waziri wa Afya kwa sababu eti "alijisikia sana."
Sandra alimkokota pacha wake mpaka kwenye chumba kingine kisichokuwa na kipindi kwa wakati huo na kumbananiza kwenye kona ili yale aliyotaka kumwambia mtu mwingine asisikie. Ijapokuwa Xander mara nyingi alitenda kwa njia ya kutojali, Sandra alimwelewa vizuri sana. Na pia Xander alimpenda sana na kumheshimu pacha wake kwa sababu walikuwa na aina fulani ya ukaribu ambao ulikuwa wenye nguvu mno.
"Xander... kwa nini unafanya mambo kama mtoto aliye... spoilt sana? Kisa tu cha jana ndiyo kinakufanya unakosa adabu?" Sandra akamwambia.
"Sijui... unaongelea nini..." Xander akasema kikejeli.
"Mama amekupigia mara ngapi leo? Kwa nini hupokei?"
"Na wewe Sandra usinipande. Siku yangu imeanza kwenda fresh kwo' hayo masuala potezea..."
Xander akasema hivyo, kisha akampita na kuanza kuondoka.
"Alexander!"
Sandra akamwita kwa jina lake lote. Xander akasimama. Hii ilikuwa ni kwa sababu sikuzote kama Alexandra angemkasirikia, basi angemwita jina lake lote. Hivyo hapa jamaa akatambua kuwa dada yake alikuwa amekasirika, hivyo akamgeukia na kumtazama tena usoni.
"Njoo hapa..." Sandra akamwambia.
Xander akatabasamu na kumfata tena.
"Naona umeanza kuleta swaga za mama," Xander akasema.
"Xander mama anaumia pia. Siyo wewe na mimi tu. Lakini anapata wakati mgumu hata zaidi ukitenda namna hii. Tumebarikiwa kuishi maisha ya kizungu, sikatai..."
Xander akacheka.
"...lakini hiyo siyo ruksa kumsemesha mama namna ile, au kutopokea simu zake. Unataka tu kusababisha matatizo maana unajua akikasirika anavyokuwaga..." Sandra akaendelea kusema.
"Mbaya kuliko mjeshi?"
"Xander nisikilize. Acha kujifanya kama mtoto... you're better than this. Mpigie simu mama, maana ameniambia amekupigia mara tatu lakini hukupokea. Na mimi ni makosa yangu maana nilikuwa sijaongea nawe mapema. Mpigie... mwombe samahani. Najua unajisikia vibaya na unaogopa utasema nini, lakini fanya hivyo. Hata kama ni kwa shingo upande. Usisahau... for me, for you..." Sandra akasema.
"Aaah Sandra usianze sasa..."
"Come on say it!"
Xander akashusha pumzi, kisha akasema, "For me... for you."
Alexandra akatabasamu, kisha akaanza kuzivuruga nywele za pacha wake kichwani.
"Aagh! Usifanye hivyo. Hata yule dogo alisema, 'you don't mess with a black man's do!' Xander akalalamika.
"Ahahahah... na wewe ni black man? Kwenda huko!" Sandra akamwambia na kumsukuma pembeni.
Wawili hawa wakacheka pamoja na kuanza kutoka kwenye chumba hicho. Sandra alianza kumwambia kuwa alitoka kwenye mazoezi ya kuogelea hivyo angeenda kupata chakula kisha ndiyo angeelekea nyumbani. Xander akamwambia kwamba naye baadae angeenda kwenye mazoezi ya mpira, hivyo atamrudisha nyumbani kisha ndiyo aelekee huko.
Mapacha hawa sikuzote walitatua vikwazo vyao kwa kurekebishana, na hasa Alexandra ndiye aliyemrekebisha mara nyingi pacha wake na kufanya ionekane kana kwamba yeye ni mkubwa zaidi kwa Alexander. Kihalisi, Alexandra alimwacha mwenzie kwa dakika 9 kiumri, kwa hiyo tunaweza kusema alikuwa mkubwa kwake! Walikuwa na msemo huo waliotumia pindi ambazo walirekebishana au kutiana moyo. Ulirithishwa kwao na bibi yao kipenzi, ambaye alipoteza maisha miaka kadhaa nyuma kwa kuwa umri wake ulisonga.
For me... for you, ulikuwa ni msemo ambao bibi yao huyo aliwaachia kuwakumbusha kwamba hata kuwe na hali gani, wanapaswa kukumbuka sikuzote kufanya mambo kwa ajili ya mmoja na mwenzake. Walipaswa kuyaona matatizo waliyopitia kuwa "yao" wote hata kama aliyeyapitia alikuwa mmoja, na hivyo kusaidiana kuyatatua kwa ajili ya mmoja na mwenzake. Hivyo kuusema mara nyingi kuliwafanya wajikumbushe umuhimu wao kuelekeana wakiwa mapacha, nao ungewapa amani ya akili kufanya maamuzi sahihi na kukumbuka upendo wao wa dhati kuelekeana.
★★
Upande wa madam Valentina. Alikuwa ofisini kwake akipitia kazi alizokuwa amewapa wanafunzi wake za somo alilofundisha siku iliyopita. Zilikuwa zimekusanywa na kupelekwa kwake muda wa saa 5 asubuhi, na sasa ilikuwa ni saa 7 mchana akiwa ameketi kwenye kiti chake cha ofisi akizipa alama. Hakuwa na kipindi cha darasani siku hii, hivyo aliamua kusahihisha kazi hizo mapema na angeisoma kazi ya Alexander mwishoni, kwa sababu alipenda uandishi wake na alitaka kuona ikiwa "challenge" aliyompa aliitendea kazi vyema.
Baada ya kuifikia, alishtuka sana kukuta kichwa cha habari kuwa "The Life of Madam Valentina," yaani Maisha ya Mwalimu Valentina. Alikunja uso wake kimaswali sana kwa kuwa hiki ni kitu ambacho hakutarajia kabisa. Xander alitakiwa kuandika insha nzuri iliyohusiana na mtu fulani aliyempenda au kumkubali sana kama madam Valentina alivyomwambia, kwa hiyo kuona jina lake hapo kulishangaza hasa kwa sababu hakuwa na ukaribu wowote na kijana huyo.
Akaanza kuisoma kwa umakini kazi ya kijana huyo. Alijisemea maneno "Oh my God" karibia mara ishirini kadiri alivyoendelea kuisoma. Mambo yaliyoandikwa humo yalikuwa ni kuhusu maisha yake, na yaliandikwa kwa usahihi kabisa. Karibia kila kitu! Jina lake lote, umri wake, shule alizosomea, chuo, vitabu alivyoandika, marafiki zake, baadhi ya wanaume ambao aliwahi kutoka nao kimapenzi kipindi cha nyuma, sehemu alikoishi zamani na wakati huu, mambo aliyopenda kama chakula, mavazi, vinywaji, burudani, na hata kitu ambacho hakudhani kijana huyo angeandika; kwamba alikuwa na tattoo ya ua la waridi kwenye paja lake!
Valentina alianza kudondosha machozi baada ya kufikia sehemu ambayo ilieleza jinsi wazazi wake na mdogo wake wa kiume walivyopoteza maisha yao kwenye ajali ya gari, na jinsi mwanamke huyu alivyojitahidi kusonga mbele licha ya magumu aliyokabiliana nayo maishani. Akaeleza kwamba vitu hivi vyote ndiyo vimemjenga Valentina wa leo, na kwamba vinamtia moyo hata yeye (Xander) kuwa imara ijapokuwa kuna mambo yenye kuvunja moyo ambayo sikuzote maisha huleta; haijalishi mtu ana hali gani.
Valentina akaifunika kazi ya Xander na kufumba macho yake. Alihisi ni kama kijana huyu alikuwa ametumia hadubini kuyachunguza kwa undani maisha yake, na hasa vitu ambavyo alitaka sana kusahau. Alihisi huzuni, na hasira, na kupendezwa na akili ya kijana huyo, vyote kwa wakati mmoja. Hakuendelea tena kufanya kazi zingine hapo. Akabeba tu makaratasi ya wanafunzi wake hao na kuyaweka kabatini, kisha akachukua mkoba wake na kuondoka chuoni hapo.
★★
"Nakupenda Xander..."
"Nakupenda pia mama..."
Hilo ndiyo lilikuwa hitimisho la maongezi ya simu baina ya Xander na mama yake. Alikuwa amefuata ushauri wa Sandra na kumpigia simu Alice, kisha akamwomba samahani kwa yaliyotokea usiku wa jana. Alice alimkumbusha kuwa bado alipendwa na baba yake, na hata kama mambo hakuyaona kuwa sawa, la muhimu ni kwamba sikuzote walikuwa pamoja kama familia. Akamwambia asahau hayo na ajitahidi kuwa mtulivu zaidi, ndiyo akamwambia maneno hayo mwishoni.
Sasa Xander alikuwa akimsubiria pacha wake ili ampeleke nyumbani kama alivyoahidi. Alikuwa amekwenda sehemu ya pembeni kidogo wakati alipokuwa akiongea na mama yake kwenye simu, hivyo akarejea kwa rafiki zake waliokuwa wamekaa pamoja kwenye mabenchi mapana yenye meza sehemu za nje ya jengo la chuo (ndani ya uzio wa kulizunguka). Walikuwepo wakina Benjamin, Bernard, kijana mwingine aliyeitwa Lucas, na Hussein; wote wakiwa ni marafiki wa Xander. Walikuwa wakiongelea mambo kadha wa kadha, naye Xander alipofika, Bernard akamwomba amwachie laptop yake kwa leo halafu angeirudisha kesho.
"Aa... hapana. Nina mambo nataka kufanya..." Xander akakataa.
"Acha hizo mwanangu. We si unakuwa nayo kila siku, me nataka tu nikaicheki movie ya Vampire Diaries bado sijaiona..." Bernard akasisitiza.
"Vampire Diaries? Ni series siyo movie bwege wewe..." Hussein akasema.
"Si ndo' apo mwanangu! Hawezi kuimaliza yote leo na mimi kutoa PC mpaka unipe dada'ako," Xander akasema.
"Mchukue tu," akasema Bernard.
"Eeh afu' kweli hivi Asha bado yupo?" Benjamin akamuuliza Bernard.
"Duh, ngoma imehamia kwako bradha. Bernard dada yako ana target nyingi nyuma," Lucas akasema.
"We mwanangu usizingue bwana nipe nika..."
"Ningekupa Bernard, ila kuna research nafanya baadae na nimeshazoea kutumia PC. Wewe si uidownload uwe unaangalia kwenye simu yako..." Xander akamwambia Bernard.
"Nafasi kaka. Mapicha kama yote halafu sitaki kufuta. Unaringa kishenzi wewe..." Bernard akasema.
"Aaaa... siyo kihivyo, siyo kihivyo wewe. Hauitoi hapa kirahisi-rahisi japo utaona kama nakudis..." Xander akamwambia.
"Kichwa kama Temba," Bernard akasema.
Wote wakacheka pamoja.
Ni wakati huu ndiyo wakaanza kuona vijana wengine wakitoka nje ya geti kwenda kushuhudia jambo fulani lililoonekana kuwa zito. Kwa fikira za haraka wote wakadhani ni ajali labda, hivyo nao wakatoka hapo upesi kwenda kuona kilichotokea. Walipofika kwa nje, waliweza kuwaona wanachuo wenzao wakiwa wamesimama kwa njia ya kuzunguka wakiangalia watu fulani, na baada ya kukaribia hapo wakamkuta rafiki yao, Mecky, akiwa anafokeana na mwanachuo mwenzake huku wameng'ang'aniana nguo zao kwa njia ya kupigana.
Xander akaingilia kati na kujaribu kuwaachanisha, na vijana wengine wakamsaidia. Akamuuliza Mecky shida ilikuwa ni nini, naye akasema kwamba kuna "dogo" hapo aliyekuwa anataka kumharibia pikipiki yake, yaani pikipiki ya Mecky mwenyewe, na alipotaka kumdhibiti ndiyo huyo jamaa akaanza kumzingua akisema eti aache kuonea. Xander akamtazama huyo "dogo" na kumtambua. Alikuwa kijana mdogo ambaye alimwona mara kadhaa hasa mwaka huu wa chuo. Mecky na huyo jamaa walianza tena kurushiana maneno, hivyo Xander akamvuta Mecky pembeni ili kuzuia vurugu zaidi.
"Mecky mwanangu mbona hivyo?" Xander akasema.
"Fala tu huyo anaingilia vitu havimhusu eti anajikuta anajua kupigana, ningemwonyesha," akasema Mecky akiwa na hasira.
Watu walianza kuondoka kuendelea na mambo yao, huku yule jamaa aliyekuwa karibu kupigana na Mecky akiondoka zake pia. Rafiki zake Xander wakasogea karibu nao.
"Kwa hiyo huyo dogo alikuwa anataka kuiharibu pikipiki yako?" Xander akamuuliza.
"Alikuwa anaikagua-kagua ya nini? Yake?" Mecky akauliza.
"Kwa hiyo kuikagua ndiyo anaiharibu?" Xander akasema.
"Aa-aaa mwana, we humjui huyo dogo ndiyo maana. Kwao Sumbawanga huko anaweza akawa anataka kunitia alama usiku waanze kunijambia yeye na bibi yake," Mecky akasema.
Wenzake wakacheka sana.
"Siyo vizuri hivyo Mecky..." Xander akamwambia.
"Kweli mwanangu siyo fresh... Ulimuuliza alikuwa anaangalia nini au ukaja tu juu kama kawaida yako?" Benjamin akamuuliza pia.
"Sitaki aishike. Mamae zake na huyo taahira mwenzie wanikute sasa ntawacharaza wote juu ya dari..."
"Ai! Basi mkuu... basi," Hussein akasema huku anamkejeli kumpa "massage" mgongoni ili atulie.
Mecky akaielekea pikipiki yake akiwa analalamika na kuanza kuifuta-futa. Xander alikuwa anamwangalia yule "dogo" akiwa anaelekea barabarani, ikionekana anaenda kuchukua usafiri ili aelekee kwao. Akaamua kupotezea tu kilichotokea na kurudi eneo la ndani.
★★
Baada ya muda mfupi, Sandra alimaliza kipindi alichokuwa nacho na kumkuta pacha wake akimsubiri. Wakaondoka pamoja kuelekea nyumbani. Lakini wakiwa njiani, Sandra akamwambia wapite kwenye soko fulani la karibu ili anunue kitu fulani kwa ajili yake. Xander akatii na kumpeleka huko, na baada ya kufika, Sandra akaingia kwenye soko hilo na kumwacha pacha wake kwenye pikipiki akimsubiri. Simu ya Xander ikaita, na mpigaji alikuwa ni Ramla. Akapokea.
"Xander jamani, umeondoka hata kunicheki hamna?" Ramla akasikika upande wa pili.
"Pole my... nilikuwa namwahisha Alexandra nyumbani," Xander akasema.
"Siyo vizuri bwana, me sijapenda," Ramla akalalamika kwa deko.
"I'm sorry. Nita...."
Kabla hajamalizia maneno yake, aliweza kumwona kijana yule, "dogo," ambaye ndiye alihusika zaidi kwenye ugomvi uliotokea baina ya rafiki yake na yule jamaa mwingine. Alikuwa akitokea upande huo wa soko huku mikononi mwake akibeba mfuko mkubwa ambao kwa haraka Xander alitambua ulikuwa na matunda mengi ndani yake.
"Xander mbona huongei?" Ramla akasikika kwenye simu.
"Aa... nipo, nipo..."
"Me nataka kukuona. Unanifanyia vibaya kweli siku hizi..."
"Usijali... baadaye naenda kwenye mechi. Ntakupitia. Jiandae vizuri. Sawa?" Xander akasema haraka-haraka huku akitoka kwenye pikipiki yake.
"Kwa hiyo mechi ndiyo ita..."
"Just do it. Nitakupigia. Baadaye," Xander akamkatisha na kukata simu.
Alikuwa akimwahi kijana huyo ili waongee.
"Oya..." akamwita.
"Dogo" akageuka na kusimama. Alikuwa anamtazama Xander kwa njia ya kawaida, lakini Xander aliona unyonge fulani hivi usoni kwake. Akamkaribia na kumtazama kwa makini. Alikuwa kijana mdogo tu, makadirio ya umri ikiwa ni miaka 19 mpaka 20 hivi. Alikuwa na mwili mwembamba, na kiurefu alimfikia Xander shingoni. Akaangalia chini kwa njia fulani kama anataka kuuficha uso wake.
"Unaitwa nani?" Xander akamuuliza.
"Isiminzile," akajibu kwa sauti ya chini.
"Simi... what?" Xander akauliza akiwa hajamsikia vizuri.
Isiminzile akabaki tu kimya.
"Okay. Nitakuita Simi. So, Simi... unaenda nyumbani?" Xander akamuuliza.
Akatikisa kichwa kukubali.
"Usiniogope. Mimi ni rafiki. Ulikuwa unafanya nini mpaka Mecky akakutendea namna ile?" akamuuliza.
"Niliishika pikipiki yake," akajibu.
"Uliishika pikipiki yake. Yaani uliishika tu. Haukuichokonoa wala nini?"
"Hamna. Nilikuwa namwonyesha Musa CDI..."
"Ndiyo nini?"
"Ni... box fulani lina-control ignition system ya pikipiki ili kuiwasha. Hauwezi kuiona kwa nje ndiyo nikawa namwonyesha inavyokaa na kufanya kazi..."
"Aaaa... ukatumia pikipiki ya Mecky kumwonyesha jamaa yako mfano?"
"Ndiyo."
"Sawa. Alikuuliza ulichokuwa unafanya au akaanza tu kukulaumu?"
Isiminzile akabaki tu kimya. Xander akashusha pumzi na kumshika begani.
"Pole dogo langu. Nimekuonea huruma sana pale. Ila watu wengine wanakuwaga wakuda, na Mecky ni mmoja wao. Wakati mwingine usiguse kitu cha mtu bila ruhusa yake sawa?" Xander akamwambia kwa upole, kama kaka kwa mdogo wake.
Kijana huyu akamwangalia sana Xander. Alimtazama kwa njia fulani mpaka Xander akajiuliza ikiwa alikuwa amemwelewa au la.
"Xander!"
Xander akageuka nyuma baada ya kusikia sauti ya pacha wake ikimwita. Akamwonyesha kwa ishara kwamba anakuja, kisha akamgeukia Isiminzile. Lakini akashangaa kukuta kijana huyo akiwa ameanza kuondoka bila hata kusema lolote. Akajiuliza ikiwa alikuwa sawa kweli, lakini akaona aachane naye maana labda alisumbuliwa na hali iliyomkuta leo chuoni. Akarejea kwenye pikipiki yake na kupanda, huku Sandra akiuliza alikuwa anazungumza na nani yule.
Walipoianza tena safari ya kuelekea nyumbani, ikabidi Xander amsimulie kilichotokea nje ya chuo muda ule ili kumwelewesha kijana huyu alikuwa nani.
★★
Isiminzile alifika kwao kwenye mida ya saa 9 alasiri. Aliishi kwenye nyumba yao pamoja na mama yake, kaka zake wawili, mdogo wake mmoja wa kike, na bibi yao mzaa baba. Baba yake alikuwa amekufa miaka kadhaa nyuma kwa kuumwa na nyoka. Walikuwa na maisha ya kawaida tu, lakini kuna mambo mengi sana yenye kuvunja moyo ambayo familia yao ilipitia.
Mama yake Isiminzile alikuwa mlevi sana; wa vilabuni. Alipenda kutukana-tukana mno na hakujali wanae hata kidogo. Kaka yake mkubwa na Isiminzile ndiye aliyeiandalia mahitaji familia hii kwa kufanya kazi ya ujenzi, na bibi yao pia alisaidia kwa shughuli ya kuuza mbogamboga na matunda kwenye kibanda chake kidogo ambacho hakikuwa mbali na nyumba yao. Kaka yake mwingine naye pia alifanya kazi za vibarua, lakini hakuwa mkaaji wa nyumbani sana kwani alipenda kukesha kwa marafiki zake tu na kulala nyumbani hapo mara moja moja. Mdogo wake wa kike alisoma pia sekondari kidato cha tatu, naye alikuwa aina ya binti unayeweza kumwita "mcharuko." Alipenda wanaume wenye pesa, naye alikuwa amekwishaanza tabia za ovyo ovyo tu tokea alipokuwa darasa la saba.
Yaani kwa familia hii, wapole walikuwa ni Isiminzile na kaka yake mkubwa, ambaye alijitahidi sana kuwaonyesha upendo bila kuchoka. Ni yeye ndiye aliyejitoa kugharamia masomo ya Isiminzile na mdogo wake wa kike, na mara kadhaa hata alisaidiwa na baadhi ya ndugu wa ukoo walioishi mbali ili kuitunza familia hiyo. Hakuwa ameoa bado, kwa sababu aliona familia yao kuwa jukumu la kwanza kabla ya mambo yote.
Isiminzile alikuwa aina ya kijana mtulivu, lakini aliyesumbuliwa na tatizo la kushuka moyo. Alijiona kuwa kama hafai, kama anabaguliwa sana, na ijapokuwa alikuwa na akili sana hata kaka yake kumwambia mara nyingi kwamba angekuja kufanikiwa na kuisaidia familia yao, bado alihisi kama... hatoshi. Bibi yake alikuwa mkali mkali mara nyingi aliyechunguza-chunguza sana mambo, lakini kati ya watoto wale wote, aliwapenda sana Isiminzile na kaka yake mkubwa. Hao ndiyo aliwaona kama matunda mazuri ya uzao wa mwanae, hivyo mara nyingi aliwafanyia mambo kwa upendo na unyenyekevu.
Kijana alimkuta bibi yake sehemu ya kibandani, naye akampatia mfuko ule uliokuwa na matunda mengi. Bibi yake alikuwa amempatia pesa kidogo siku iliyotangulia ili leo amletee matunda hayo, naye angeyatumia kwa ajili ya kuuza, lakini baadhi kwa ajili ya kula pia. Aliweza kuona usoni kwa mjukuu wake kwamba hakuwa sawa. Akamuuliza shida ilikuwa ni nini, lakini hakujibu na kutaka kuondoka. Bibi yake akamshika mkono na kumkalisha, akimuuliza kiukali wakati huu SHIDA ILIKUWA NINI.
"Kuna mtu chuoni leo... alitaka kunipiga," akamwambia.
"Kisa?" bibi akamuuliza huku amekunja sura.
"Niliishika pikipiki yake... akakasirika."
"Kwa hiyo alikuwa anataka kukupigha kwa sababu umeishika pikipiki yake?"
Isiminzile akatikisa kichwa kukubali.
"Kwa nini unashika vitu visivyo vyako?"
"Mimi bibi sijafanya chochote kibaya, lakini sikuzote hata nikifanya lolote lile lazima tu nionewe. Kuishika kuna tatizo gani? Nilikuwa tu namwonyesha mtu jinsi pikipiki inavyofanya kazi, huyo jamaa akaanza kuniambia mara mimi mchawi eti nataka sijui... yaani aagh..." Isiminzile akasema kwa hisia za huzuni.
"Nini?" bibi yake akauliza.
"Me bibi ngoja nikale maana njaa inani..."
"Subiri! Amekwambiaje?" bibi yake akamkatisha.
"Amesema mimi mchawi nitamroga."
"Kwa nini amesema hivyo?"
"Si anatujua... anajua sisi ni watu wa Sumbawanga kwa hiyo eti ananiitaga me mchawi... tokea muda mrefu huwa wananiambiaga hivyo wakisema ni utani lakini mimi huwa nachukia sana..." Isiminzile akasema.
"Huyo kijana anakujua?"
"Eee... mitaa ya huko mbele yeye ndiyo anakaa... yule Mecky. Tunasoma chuo kimoja..."
Bibi yake akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa.
"Yaani bibi... muda mwingine huwa nawaza sijui kwa nini mimi tu. Vijana wengine kama huyo wana vitu vizuri vizuri tu hata hawavistahili lakini wanavyo... sisi ndiyo wavirakani tu..."
"Usiseme hivyo. Huyo mkaka ana vitu gani ambavyo wewe huna?"
"Vingi tu. Sura na mwonekano wa kiume zaidi. Ana nguvu, anapendwa na wengi, ana swagger, ana... ana pikipiki... yaani hata hafanyi kazi ngumu lakini inaonekana maisha kwake ni rahisi zaidi... Mimi sijawahi hata kuwa na girlfriend... nani atamtaka jamaa kama mimi mwenye kifua cha panzi? Ila nitafanyaje... kuna watu tu hatujazaliwa na bahati..." Isiminzile akafunguka.
Bibi yake alimtazama kwa huruma nyingi, lakini akihisi hasira sana kumwelekea mtu aliyekuwa anamwonea mjukuu wake. Isiminzile akataka kunyanyuka ili aelekee nyumbani, lakini bibi yake akamkalisha tena. Akamtazama kwa wasiwasi kiasi kwa sababu bibi huyu alimwangalia kwa njia iliyo makini sana. Kisha akaishika shingo ya Isiminzile na kumsogelea karibu zaidi.
"Je nikikwambia kwamba bahati hiyo unaweza kuipata, utanisikiliza?" bibi akasema.
Isiminzile akabaki kumtazama bibi yake kimaswali kiasi. Hakuelewa alimaanisha nini, ila alimwamini, hivyo akakubali kumsikiliza na kutega sikio kwa umakini.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments