Siku zote tokea nikiwa mdogo, nilijua na kutambua kuwa mimi ni mchawi.
Utambuzi wa neno hili haswa kwa mataifa ya magharibi ukiacha nchi za Afrika, umekuwa mpana zaidi kadiri siku zinavozidi kwenda. Kwa lugha yetu ya Kiswahili hatuna utajiri mwingi wa maneno yanayoonyesha utambuzi yakinifu wa neno hili Mchawi.
Katika ulimwengu wa uchawi, maneno yana nguvu sana na si tu katika uchawi wenyewe, bali pia katika jinsi yanavyounda ufahamu wetu kuhusu wale wanaotumia sanaa za kichawi. Lugha za watu wa mataifa mabalimbali hujaribu kufafanua, lakini hakuna neno moja linaloweza kuelezea kikamilifu upeo wa uwezo wao.
Miongoni mwa majina mengi yanayotolewa kwa wale wanaotumia uchawi yanatofautiana kati ya nchi na nchi, na kila moja lina uzito wake na historia yake. Kwa mfano Mchawi wa kuvutia (enchantress) ni mwanamke ambaye uchawi wake hujidhihirisha kupitia mvuto na haiba, akiweza kufunga mioyo na akili za wale wanaomkabili. Mchawi mkuu (sorceress), kwa upande mwingine, ni mtumiaji wa uchawi wa nguvu za asili, uwezo wake ukiwa si wa kuvutia bali wa mamlaka ya kweli inayotokana na asili flani. Neno mchawi wa giza (witch) mara nyingi huhusishwa na mambo yaliyofichwa na maarifa yaliyokatazwa, ingawa si wote wanaobeba jina hilo hutembea katika giza. Katika hili inaaminika kuwa kuna wachawi wa aina mbili: wanaotumia Nguvu za Giza na wale wanaotumia Nuru(hawa ni wale waliozaliwa nao).
Utajiri wa maneno ya kingereza una maneno kama Magician(mwanamazingaumbwe), Sorcerer(wa kiume), Sorceress(wa kike), Enchanter(wa kiume), Enchantress(wa kike), Wizard(wa kiume), na Witch(wa kike) ambao hawa wote kwa lugha yetu ya Kiswahili tunawaita wachawi tu.
Kila jina, kila cheo, ni zaidi ya neno tu ni hadithi, urithi, alama inayobaki katika ulimwengu.
Leo, yeyote mwenye azimu ya kujifunza na kuitumia Sanaa ya Wenye Hekima anaweza kujiita na kwa haki kukubalika kama mchawi. Lakini kwa wakati wangu nikiwa nakua, hakukuwa na vitabu vilivyoandikwa ili kutuongoza katika kujifunza. Siri na maarifa yote ya taaluma hii yalifichwa kwa siri kwenye vitabu vilivyofahamika kama Vitabu vya Tahajia (Grimoires) na vilikuwa vikihifadhiwa kwa usiri mkubwa mnoo. Wakati ule, mtu alikuwa mchawi tu ikiwa alizaliwa na wazazi ambao ni wachawi au kuwa adopted na mzazi ambae nae ni mchawi. Na hata hivyo, wakati ule watoto hawa hawakuambiwa au kufundishwa siri zote za kichawi. Hata mimi siri nyingi nimejifunza badae sana baada ya kuwa mkubwa.
Mama yangu alikuwa mwanamke wa hekima, mpole, mwenye moyo wa huruma, na mchawi wa nuru (white witch). Tangu nikiwa mdogo sana, alinifundisha jinsi ya kuunganisha nafsi yangu na nguvu za jua, mwezi, nyota, na asili yenyewe ya duniani. Lakini zaidi ya yote, alinifundisha umuhimu wa kunyamaza na kutunza siri zetu kama hazina isiyopaswa kuguswa na mtu yeyote. Kwa sababu ulimwengu haukuwa tayari kutupokea na kuishi na sisi katika jamii moja.
Adhabu kwa wale waliotuhumiwa kutumia sanaa zetu zilikuwa kali, ingawa mama hakuwahi kuniambia moja kwa moja jinsi gani zilivyokuwa za kikatili. Niligundua ukweli huo mwenyewe nilipotimiza umri wa miaka ishirini na moja, kwa njia ambayo sitaisahau kamwe katika maisha yangu. Somo hilo la uchungu lilitia muhuri wa moto ndani ya moyoni mwangu, alama isiofutika hata baada ya karne tatu kupita. Na kutokana na siku hiyo, mara ya kwanza kabisa nilimuona Michael Nsebo.
Comments