Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

Majanga yaliyomkumba mama yangu hayakutokana na uchawi wake wala makosa yake mwenyewe, bali na huruma yake isiyo na mipaka. Baba yangu alifariki wiki mbili kabla ya tukio hilo kutukumba, akichukuliwa na janga la mlipuko wa homa mbaya ya mapafu (Pneumonic plague). Uchawi/uganga wa mama haukuweza kupambana na ugonjwa huo uliokumba kijiji chetu cha Umba wakati wa majira ya baridi kali ya mwaka 1622. Wengi walikufa. Mazishi yalikuwa ya kila siku. Kilio kilikuwa sehemu ya upepo. Mama alikuwa bado anauguza huzuni ya kumpoteza mumewe na labda asingeweza kuvumilia tena kuona uhai mwingine ukizimika mbele yake bila kufanya kitu.

Nakumbuka kila kitu kuhusu usiku ule mbaya. Ulikuwa ni usiku wa mvua kubwa na radi kali zilizosikika mithili ya mapigo ya ngoma za kivita. Njinga, shangazi yangu, dada pekee wa marehemu baba alifika nyumbani kwetu akiwa amechakaa, nywele zake zikilowa mvua na uso wake ukiwa umejaa hofu. Hakujifunika hata kanga mabegani mwake licha ya baridi na upepo kuwa mkali sana huko nje. Alipiga mlango kwa nguvu, akishusha pumzi kama mtu aliyekimbizw mbio na jinamizi linalokula watu. Ilikuwa ni kama alikuwa anashindana na upepo au kukimbizwa na kitu kisichoonekana.

Mama alifungua mlango, akimtazama kwa mshangao. Kabla hata hajazungumza, alimvuta ndani haraka na kumwongoza hadi karibu na moto mdogo(fire place) uliokuwa uking’aa pembezoni mwa chumba. Niliweka kikombe cha chai mbele yake, nikitumaini kingemtuliza. Lakini Shangazi Njinga hakutulia. Macho yake yaliwaka kwa hofu, mwili wake ukitetemeka kwa wasiwasi. Alikataa kukaa, badala yake akapiga hatua zisizo na utulivu sakafuni, sketi yake ndefu ikiburuza chini, ikitiririsha matone ya maji ya mvua na kuacha alama za unyevu kwenye sakafu yetu ya mbao.

"Hakuna muda wa kukaa na kunywa chai," sauti yake ilipaza katikati ya mvua na radi.

"Sio wakati wake."

Aliinamia mbele, akamtazama mama kwa macho yaliyojaa uoga na shaka.

"Ni mtoto wangu, Kombo mdogo," alisema kwa sauti iliyojaa hofu, machozi yakianza kukusanyika kwenye kona za macho yake.

"Kombo mdogo... aliyependwa na kaka yangu mpendwa, Mungu amweke mahali pema peponi."

Sauti yake ilitetemeka, na kabla ya mama kusema neno lolote, alinyakua mabega yake kwa nguvu, akimtikisa.

"Najua unaweza kumsaidia!" alipaza sauti, macho yake yaking’aa kwa msukumo wa matumaini na hofu.

"Najua, Mekena! Na nakuambia, ikiwa hautamsaidia... tutaonana wabaya!"

Mwanga wa moto ulifanya kivuli chake kucheza ukutani, mithili ya mzimu uliokasirika. Kisha radi nyingine ilipiga, na upepo mkali ukatikisa milango na madirisha kana kwamba ulimwengu wenyewe ulikuwa ukishuhudia maneno aliyokuwa amesema.

"Njinga, tafadhali, tuliza munkari!"

Sauti thabiti lakini yenye upole ya mama yangu ilimfanya shangazi Njinga kusita, lakini ilikuwa ni kwa sekunde chache tu. Mvutano ulijaa hewani, na hofu ilianza kujikusanya ndani yangu kama wingu jeusi kabla ya dhoruba.

"Sijakataa kumsaidia Kombo," mama yangu aliendelea, sauti yake ikiwa thabiti lakini yenye uchungu wa ndani. "Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha anapona ikiwa iko ndani ya uweon wangu na kama pia inawezekana. Na najua unalielewa hilo, Njinga."

"Sielewi chochote!" Shangazi Njinga alinguruma kwa hasira, sauti yake ikitetemesha kuta za nyumba yetu ya udongo.

"Si wiki mbili tu zilizopita uliacha mume wako afe kwa ugonjwa huohuo? Kwa nini hukumsaidia Mekena? Kwa nini hukumsaidia ndugu yangu?"

Mama yangu hakusema neno. Alishusha kichwa, na macho yake ambayo siku chache zilizopita yalikuwa yameanza kupata nuru ya utulivu yakatawaliwa tena na uchungu mzito kwa kukumbushwa kifo cha mumewe mpenzi. Shangazi Njinga alikuwa kama amemwagia chumvi au pilipili kwenye kidonda kilichotoneshwa kwa kubanduliwa bandeji kwa nguvu na kubaki na ubichi ulioleta maumivu makali.

"Nilijaribu kila kitu," mama alisema kwa sauti ya chini, dhaifu kama upepo wa jioni.

"Nilijitahidi, lakini sikuweza kumwokoa."

"Labda kwa sababu wewe ndiye uliyemletea huo ugonjwa tangu mwanzo," Njinga alisema kwa sauti ya juu ikawa kama kisu chenye makali kwa mimi na mama yangu, kauli yake ikining'inia angani kama hukumu.

Nilihisi mwili wangu ukikakamaa.

"Shangazi Njinga!" niliingilia kwa ghafla, hasira ikiwaka ndani yangu kama moto wa nyika. Sikujali tena heshima za kimila, nilimshika mkono na kumvuta ili anitazame mimi badala ya mama.

"Unajua vyema zaidi. Wazazi wangu waliishi kwa upendo usio na kifani, kila mtu kijijini anajua hilo. Sitakaa kimya nikisikiliza ukichafua kumbukumbu yao!"

"Yolanda, tafadhali usiingilie," mama alinisihi, lakini sikuweza kufyata ulimi.

"Hakuna mtu anayeweza kuleta mlipuko wa ugonjwa kama huu kwa makusudi, na unalijua hilo, Shangazi!"

Njinga alikunja uso.

"Hakuna mtu ila mchawi, si ndivyo unavyomaanisha, Yolanda?" Sauti yake ilikuwa ya dharau, lakini macho yake yalikuwa makali, yakiwaka kwa hasira isiyofichika.

"Mama yako na wewe mna siri moja. Inawezekana hata wewe ni sehemu ya ibada zake za kipagani! Enhe, niambie yote, Yolanda, na wewe pia unafanya uchawi?"

Alinishika mabega na kunitikisa kwa nguvu, akinikodolea macho kwa msisitizo wa mtu anayetaka jibu.

Nilihisi damu ikiganda mwilini mwangu. Nilifumba na kufumbua macho kwa mshangao, nikirudi nyuma haraka, nikijiondoa kutoka mikononi mwake. Anajua.

Lakini amejuaje? Siri hii ilikuwa kati yangu na mama tu. Hata baba hakuwahi kujua…

Mama yangu alimpandisha macho kwa utulivu wa mtu aliyekabiliwa na dhoruba nyingi kabla ya hii. "Kwa nini unasema maneno makali kiasi hiki, wifi?" aliuliza kwa upole. "Unawezaje kumtuhumu dada yako mwenyewe?"

"Dada mkwe, si dada wa damu," Njinga alimsahihisha mama kwa sauti ya dharau.

"Na nimekuwa nikishuku mambo yako tangu zamani. Mekena, nakukumbuka ulivyonisaidia nilipozaa mtoto wangu wa kwanza, kwa namna fulani ukafanya nisihisi maumivu ya uchungu wa kujifungua hata kidogo. Na baadaye, nilipopata homa kali ya mafua, ulipambana kunitibu na wote tunajua kabisa bila zile dawa zako ningekuwa nimekufa mimi sasahivi."

Alinyosha mkono wake kwa ghadhabu, akipapasa kwa haraka mizizi na magome ya miti yaliyokuwa yakining'inia ukutani, pamoja na vikapu vidogo vya dawa na poda zilizopangwa kwa ustadi juu ya shelves za mbao.

"Hakuna daktari angeweza kunitibu kama ulivyofanya," alisema kwa ukali, sauti yake ikiwa na chuki iliyofichwa nyuma ya woga.

"Hivi kweli unataka kuniambia haujaingia kwenye ushirikina, Mekena?"

Mama yangu hakutikisika. Uso wake ulikuwa utulivu, bila hisia zozote za hofu wala hatia. "Miti na mimea ni neema ya Mungu," alisema kwa sauti laini lakini yenye msisitizo. "Maarifa ya kutumia rasilimali hizi ni zawadi, si dhambi."

"Wiki iliyopita nilikuona," Njinga alisema ghafla, sauti yake ikishuka kuwa ya kunong’ona. "Wakati mwezi ukiwa kamili."

Maneno haya yalituacha mimi na mama yangu tukitazamana, Nilitambua kuwa tulikuwa tunafikiria jambo lilelile tukikumbuka ibada yetu tuliofanya chini ya mwezi ukiwa kamili, tuliposoma maneno matakatifu karibu na moto wa usiku wa manane, tukiomba kwa miale ya mwezi mweupe.

"Najua wifi una... nguvu sana. Na sijali kama unachofanya ni dhambi au la. Ninachohitaji kwa sasa ni umsaidie mwanangu Kombo. Kama hukusababisha mlipuko wa ugonjwa huu, basi thibitisha. Mponye,wifi. Ukikataa..." Macho yake yalifinyana, lakini hakumaliza.

"Nikikataa, utafanya nini, wifi yangu mpendwa? Utabeba ushahidi dhidi yangu na kunishtaki kwa hakimu? Ili niadhibiwe kama wengine kwa ushirikina?"

Shangazi Njinga hakujibu chochote.. Ila tu Niliona jibu lake machoni, na mama yangu pia aliliona.

"Huna haja ya vitisho hivyo wifi," Mama alimwambia. 

"Ungeomba tu msaada wangu kwa ustaarabu, sisi ni familia moja. Nitajaribu kwa uwezo wangu wote kwa ajili ya mtoto wako, vile vile kama nilivyofanya kwa Kombo mume wangu. Lakini naomba uelewe kitu kimoja, kwa uganga au vyovote vile, kuna possibility ninaweza kutokuwa na nguvu ya kumsaidia, muamuzi wa mwisho ni Mungu."

"Akifa, ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, nitahakikisha unanyongwa!" Shangazi Njinga alielekea kwenye mlango wa kutokea wa mbao, akivuta kitasa kwa hasiraili atoke nje. 

"Chukua unachohitaji na uje mara moja. Nimemwacha mda mrefu lazima turudi haraka kumuhudumia mwanangu."

Alituacha mlango ukiwa wazi huku upepo mkali na mvua ikiingia ndani akitokomea kwenye giza bila kujali hajafunga mlango. Nilikimbia na kurudishia mlango ulikua mzito mnoo, kisha nikasimama kwa muda mrefu, mkono wangu ukiwa umeegemea kwenye mlango. Nilikuwa na hisia mbaya kwamba matukio ya muda uliopita yangebadilisha maisha yetu milele. Sikujua kwa vipi, au kwa nini, lakini nilihisi hilo hadi ndani mifupa yangu. Nikivuta pumzi ya kina, nikageuka kumtizama mama yangu. Nikapiga magoti mbele yake, nikishika mikono yake, nikimtazama macho yake meusi kama yangu. "Usiende kwake mama," nikamsihi. 

"Hauwezi kumsaidia zaidi ya ulivyopambana kusaidia Baba. Na kwa jinsi shangazi alivokuwa anaongea kama matokeo yatakuwa tofauti na anavyotaka, atakulaumu wewe."

"Yolanda, Kombo Junior ni mpwa wangu pekee," alisema kwa sauti ya chini. Akajiondoa mikono yake niliyokuwa nimeishika nikitetemeka, na akaanza kujiandaa, akichukua vijitawi vya mimea kutoka kwenye mafungu ya miti yaliyokauka yaliyokuwa yakining'inia ukutani, pamoja na unga kidogo kama poda na baadhi ya magome ya miti na kuyaweka kwenye chungu(cauldron) maalum. Chungu hicho kilikuwa kimepambwa kwa kuchorwa ua jekundu (red rose), lililochorwa kwa mkono ila kwa ustadi wa hali ya juu mnoo kwenye ubavu wake. Akaongezea na maji ya mvuke kutoka kwenye sufuria kubwa ya chuma iliyokuwa ikining’inia juu ya mahali pa moto (fire place).

"Mama tunapaswa kuondoka hapa kijijini haraka sana," niliendelea kumsihi mama huku nikimsaidia kufanya maandalizi pembeni yake, nilikuwa nikipima, nikikoroga, na nikiinua mikono yangu juu ya kila mchanganyiko ili kuusukuma na kuingiza nguvu za kichawi na mwanga wa uponyaji ndani yake.

"Tunapaswa kuondoka usiku huu, Mama. Siri yetu imejulikana, na ulishaniambia na kunitaadharisha jinsi ilivyokuwa hatari."

"Siwezi kuvunja kiapo changu," alisema mama. "Na naamini unajua hilo. Mtu anapohitaji msaada, na anaponisihi nimsaidie, nimefungwa kwa kiapo na kwa damu kujaribu. Na sioni njia nyingine zaidi ya kujaribu mwanangu." Akaniangalia machoni. "Unapaswa kuchukua nguo kwenye mkoba wako na uondoke uende Kaskazini Mlimani(Kilemajyaro). Chukua farasi. Ondoka usiku huu. Nitakutumia ujumbe wakati…."

"Sitakuacha ukabiliane na hili peke yako mama," nilinong’ona taratibu, kisha nikajitupa mikononi mwake kumkumbatia nikinusa nywele zake nyeusi tii kama kunguru, zinazofanana na zangu, ingawa zake zilikuwa zimefungwa nyuma huku zangu zikiwa zimeachwa na kufika kiunoni mwangu. "Usiniombe hivyo, Mama."

Lips za mdomo wake zikapinda kutengeneza tabasamu zuri la kuvutia ambalo ni la kwanza kuliona usoni mwake tangu kifo cha baba kilivotokea.

"Uu jasiri sana binti angu," alisema kwa upole.

"Na daima umekuwa mtu mwenye uthubutu. Sawa basi. Twende, tuharakishe kwa Junior."

Haraka haraka tukapakia dawa zetu, fuwele(crystals), na mishumaa ndani ya mfuko aina ya totebag, tukavaa makoti yetu ya zamani yaliyoshonwa nyumbani kwa mchanganyiko wa ngozi na sufi, tukafunika vichwa vyetu kwa boshori na scarfs kwenye mabega, kisha tukatoka nje kwenye giza kali lililoambatana na upepo wa baridi kali. Na kuchukua farasi hao mbio kwa shangazi.

 

Previoua Next