Bahati mbaya binamu yangu alikuwa amekwisha kufa tokea sisi tuko njiani yani hata kabla hatujafika nyumbani kwa shangazi yangu. Na vile tunafika tu tulikaribishwa na mwanamke mwenye macho yalijojaa roho mbaya na ya kikatili aliyewahi kutuita ndugu, pamoja na kundi la wananchi aliowahamasisha kutoka usingizini, wote wakiwa na mienge(torches) huku wakipiga kelele,
"Wakamate! Wakamate wachawi hao!"
Mikono yenye ukatili ilinivuta kwa nguvu hata nilipojaribu kukimbia. Mashtaka yalirindima usiku huo, watu walikuwa na hasira kana kwamba sisi ndio tuliosababisha vifo vilivotokea hapo kijijini. Watu wengine walisimama kuangalia huku mimi na mama yangu tukizingirwa na kusukumwa kama wezi vile, kisha tukakokotwa juu ya matope yaliyojaa barafu na mawe yaliyoniumiza kwenye magoti. Nilipiga kelele sana kuomba msaada kwa majirani zangu, lakini hakuna hata mmoja aliyenijali. Na moyo wangu ukaganda na kufa kwa hofu kubwa. Baridi ilikuwa kali kama theluji iliyokuwa ikinichapa na upepo usoni mwangu.
Ilikuwa safari ndefu, safari ndefu zaidi ya zote maishani mwangu. Vibanda na baadhi ya nyumba za masikini zilibaki nyuma yetu tulipokuwa tukivutwa na kusukumwa mbele, kuelekea kwenye mtaa alikuwa akikaa Hakimu alieteuliwa na kanisa la Katoliki kwa ajili kutoa hukumu pale kesi za wanakijiji zinapoibuka. Hadi tukafika kwenye mitaa ambayo nyumba zake zimejengwa na mawe, nyumba moja iliyokuwa kati ya nyumba nzuri za matajiri katika mtaa huo ilikuwa ni ya Hakimu. Hatimaye, tukasimama mbele ya nyumba ya hakimu mwenyewe, mimi na mama yangu tukitetemeka dhidi ya upepo mkali wa baridi huku washtaki wetu wakigonga na kubisha mlango kwake kwa nguvu.
Mwanaume huyo baada ya muda alitoka akiwa amevaa mavazi ya kulalia, alionekana bado ana usingizi na sura yake ilionyesha kukereka na hasira kali.
"Haya yote ni nini?" aliuliza, huku ndevu zake nyeupe zikimulikwa na mienge ya watu.
"Wachawi wawili!" alipiga kelele yule jamaa aliyemshika mama yangu kwa nguvu.
"Wale walioleta mlipuko wa tauni juu yetu sote, Mheshimiwa."
Macho ya yule mzee yakapanuka, kisha yakakunjamana tena alipotuangalia kwa makini. Nyuma yake, niliweza kuona mwanga wa moto mkubwa katika mahali pa kuotea, na niliuhisi ukipasha uso wangu joto. Nilitamani kwenda kunyoosha mikono yangu karibu na huo moto. Vidole vyangu vya mikono vilikuwa tayari vimepooza kwa baridi.
"Mnayo ushahidi gani dhidi yao?" hakimu aliuliza.
"Haya mashtaka ni kutoka kwa mwana familia mwenzao," alisema mwingine, akimnyooshea Shangazi yangu kidole.
"Njinga si dada yangu," mama yangu alisema, sauti yake ikiwa tulivu na upole bila wenge hata katikati ya machafuko hayo. Sitaweza kusahau uso wake, mzuri na mtulivu. Macho yake, yenye ujasiri, hayakuonyesha dalili yoyote ya hofu.
"Yeye ni dada wa mume wangu."
"Mume wako aliyekufa kwa tauni!" yule mwanaume alipiga kelele.
"Na sasa mpwa wako naye amechukuliwa pia."
"Wengi wamepoteza maisha kutokana na tauni, bwana. Hakika huwezi kuwashtaki kwa kila familia iliyofiwa ukisema ni uchawi?" alijibu Hakimu
Mwanaume huyo alimkazia mama yangu macho kwa hasira. "Njinga Kombo anatoa ushahidi, Mheshimiwa. Amewaona kwa macho yake wakifanya ibada zao za ushirikina."
"Uongo huo!" Nilipiga kelele. "Shangazi yangu amepagawa na huzuni! Hajui asemalo!"
"Kimya." Amri ya hakimu ilinifanya nitetemeke. Alisogea mbele, akitazama mfuko wa kitambaa ambao mama yangu bado alikuwa ameshikilia mikononi mwake.
"Una nini hapo, mwanamke?"
Mama alinyanyua kidevu chake, akimkabili kwa macho yake. Niliweza kuona mawazo yakizunguka nyuma ya macho yake, jinsi alivyotuangalia na kutuhukumu, ingawa tulikuwa wageni kwake.
"Ni mimea tu," alisema kwa upole, "iliyotengenezwa kuwa chai."
"Anasema uongo," yule mwanaume alisema.
"Njinga Kombo alisema mwanamke huyu alikuwa akimletea mtoto wake mdogo dawa ya kumponya. Lakini aliogopa kuwa mchawi huyo angejichelewesha makusudi ili mvulana huyo apatwe na majanga zaidi, na hofu yake ikathibitika kuwa ya kweli. Ndani ya huo mfuko kuna dawa za kichawi, Mheshimiwa. Si kingine, naapa."
"Hii si dawa wala uchawi," mama yangu alimwambia. "Ni chai ya tiba tu, nakuambia."
"Je, wewe ni tabibu, mwanamke?" hakimu aliuliza kwa ukali.
"Unajua kuwa mimi si tabibu."
"Nipe mfuko huo."
Mikono iliyokuwa imemshika mama yangu ililegeza mshiko na kumpokonya mama ule mfuko na kumkabidhi hakimu. Hakimu aliufungua, akitazama kilichomo ndani yake, na mimi nikatetemeka na kuogopa baada ya kukumbuka fuwele(crystals) tulizoweka ndani ya ule mfuko. Amethisto inayong’aa na Lapis ya bluu iliyokolea, kwa ajili ya nguvu za uponyaji. Na mishumaa, tuliyoitengeneza kwa mikono yetu wenyewe na kuichonga kwa alama za kichawi ili kusaidia kumponya Junior. Tulikuwa tumepanga kuizungushia pembeni mwa kitanda chake, ili iangaze usiku kucha kumlinda dhidi ya maamgamizi tauni.
Hakimu aliona yote haya, na alipoinua macho yake tena, yalikuwa yamepoa. Yalikuwa baridi kiasi cha kunifanya nihisi baridi zaidi licha ya joto la moto uliokuwa nyuma yake. "Wafungeni minyororo. Tuwahukumu kesho. Labda wakikaa usiku mmoja hapa uwanjani, itawafanya wakiri makosa yao na kutusaidia kutokupoteza muda."
Akaondoka, akiacha mlango wazi, kisha akarejea baada ya muda mfupi akiwa na ufunguo mkubwa, ambao alimkabidhi mmoja wa wale wanaume. "Hakikisha unawafunga vizuri."
"Hapana Jamani!" nililia. "Msifanye hivi! Hatujafanya kosa lolote. Hakimu, tafadhali, nakuomba…."
Mlango wake ulifungwa hata sauti yangu ya kuomba hakuipatiliza, nilijikuta nikivutwa kwa nguvu na kikatili huku nikiburuzwa bila huruma nikijitahidi kupambana na watesi wangu. Lakini jitihada zangu hazikufua dafu.
Na muda si mrefu nikajikuta nikilazimishwa kuinama mbele, kwenye frame ilitengenezwa kwa mbao ikiwa ina matundu matatu, mawili ya kuweka mikono na moja la katikati la kuweka shingo ambapo unakuwa umekaa style ya kuinama. Kifuniko kizito cha mbao kilishushwa na kufungwa kwa nguvu ili kuzuia mikono yangu na shingo isitoke huku majirani zangu wenyewe wakinishikilia kwa nguvu, na nikasikia sauti ya mnyororo na kufuli vikibana kwa nguvu.
Comments