Alfajiri ilipowadia, ilikuja na hakimu, na pembeni yake kulikuwa na mwanamke aliyekuwa na huzuni na macho mekundu kwa kulia. Nyuma yao alikuja mwanamume aliyekuwa amevaa mavazi ya kikuhani kama ma father wa kikatoliki. Alikuwa na uso wenye umri mkubwa, mwembamba na mkali, na pua iliyopinda na kuchongoka iliyomfanya afanane na ndege aina ya bundi mwenye njaa kali. Ngozi yake ilikuwa imepauka kama vile haina damu na virutubisho vya ya kutosha, kana kwamba alikuwa mgonjwa au mtu dhaifu sana mwenye afya mgororo. Walipokaribia, sikuweza kuona chochote ila miguu yao, kwa kuwa sikuweza kuinua kichwa changu vya kutosha kuwaangalia juu zaidi.
"Ms Mekena," hakimu alisema, "wewe na binti yako mmeshtakiwa kwa kosa la uchawi. Je, unakiri makosa yenu?"
Sauti ya mama yangu ilikuwa dhaifu sasa, na niliweza kusikia maumivu ndani yake.
"Nitakiri tu endapo utamwachia binti yangu. Hana hatia yoyote."
"Hapana," yule mwanamke alisema kwa sauti ya juu. "Lazima muwauwe sasa, Nzogere. Wote wawili!"
"Lakini sheria—" alianza kusema.
"Sheria! Unajali nini kuhusu sheria wakati mtoto wetu mwenyewe amekuwa mgonjwa ghafla? Unahitaji ushahidi gani zaidi?"
Moyo wangu ulianguka kwa maneno yake. Alitulaumu kwa ugonjwa wa mtoto wake, kama vile shangazi yangu alivyokuwa ametufanyia. Hakuna mtu anayeweza kutuokoa sasa.
Nilisikia hatua zikisogea upande alikuwa mama yangu, nikahisi hakimu atakuwa alikwenda karibu na mama yangu. Aliinama karibu na kichwa chake, akasema,
"Tafadhali Ondoa laana hii nyumbani kwangu. Iondoe sasa hivi, nakusihi tafadhali."
"Sijawaletea laana yoyote wewe wala familia yako, bwana," mama yangu alimwambia. "Ikiwa ningekuwa na uwezo wa kumsaidia mtoto wako, ningefanya hivyo kwa furaha. Kama ambavyo ningefanya kwa mume wangu mwenyewe na mpwa wangu. Lakini siwezi."
"Waueni!" mke wake alipiga kelele. "Koku alikuwa mzima hadi mlipowakamata hawa wawili! Wameleta laana hii kwake jana usiku, wakamfanya awe mgonjwa zaidi, nakwambia, na wakikaa hai kwa muda mrefu, watamuua! Waueni, mume wangu. Hilo ndilo njia pekee ya kumwokoa mwanetu Koku!"
Kuhani yule mwenye afya ya kuzorota alisogea mbele, mavazi yake meusi na kamba kiunoni zikining’inia chini na kuburuza kwenye theluji yenye unyevunyevu hapo uwanjani. Hatua zake zilikuwa nzito kana kwamba ana mtihani mkubwa wa kufanya maamuzi ya haki ili hali kila mtu aridhike na hukumu itakayotolewa. Alikwenda kwanza kwa mama yangu upande wa kushoto, hakusema chochote, na sikuweza kuona alichofanya. Lakini sekunde chache baadaye alikuja kwangu akainama na kunishika kiganga mkono wangu kama vile anasali,na alinishika kwa muda mfupi tu.
Ghafla akiwa amenishika mkono…Mshtuko fulani, hisia ya msisimko na umeme ilipenya mkononi mwangu na kupanda hadi kwenye mkono wangu mwingine, ikinishangaza na kuniogopesha sana kiasi kwamba nilipiga kelele kwa uwoga.
"Usimdhuru binti yangu tafadhali!" mama yangu alipaza sauti.
Kuhani aliondoa mkono wake, na hisia hiyo ya ajabu ilitoweka pamoja na mguso wake, ikiniacha nikiwa na wasiwasi na kuchanganyikiwa. Nikijiuliza moyoni Ilikuwa ni nini?
"Nahofia kuwa uko sahihi," kuhani alisema kwa hakimu na mkewe. "Lazima wafe, la sivyo mwanao atakufa. Na nahofia hakuna muda wa kesi. Lakini Mungu atakusamehe kwa hilo."
Hakimu akatembea mbali na sisi, mgongo wake ukituelekea, akisema kwa sauti ya chini, "Basi sina chaguo lingine." Na wote watatu wakaondoka, lakini kwa muda mfupi tu.
"Mama," nilinong’ona. "Ninaogopa sana."
"Huna cha kuogopa kutoka kwao, Yolanda."
Lakini mimi nilikuwa naogopa sana, mapigo ya moyo yalikuwa yakidunda mpaka kifua kikawa kinauma. Sijawahi kuhisi hofu kama ile niliyohisi wakati huo, na ndani ya muda mfupi yule kuhani alirudi, na akaja na watu wengine kadhaa. Wanaume wakubwa, wenye nguvu. Watu walianza kujaa hapo uwanjani kuja kushuhudia familia yangu ikiteketezwa kwa mashtaka yasiyo ya kweli. Mimi na mama yangu tulitolewa kwenye magereza ya wazi. Watu walitupigia kelele na kutuita wauaji na majina mengine mabaya. Waliturushia vitu. Uchafu na chakula kilichooza, hata wakati wanaume wale walipofunga mikono yetu nyuma ya migongo yetu na kututupa kwenye gari lililokuwa likivutwa na farasi mmoja.
Nilijikokota karibu na mama yangu, ambapo alikaa wima na kwa fahari kwenye gari hilo, na nikasogea karibu yake na kuegemea bega lake, kichwa changu kikiwa kwenye bega lake, mikono yangu ikikazwa kwenye minyororo nisiweze kumkumbatia.
"Uwe imara," aliniambia. "Uwe jasiri, Yolanda. Usiruhusu waone unatetemeka kwa hofu mbele yao."
"Ninajaribu mama," nilinong’ona.
Comments