Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)

MTUNZI: FEBIANI BABUYA 

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

Episode 1

USIKU WA KUTISHA

Usiku wa manane mvua ikiwa inanyesha mithili ya kufunguliwa kwa koki iliyopo huko angani, alionekana mwanaume mmoja akiwa ndani ya nguo nyeusi na begi jeusi kwenye mkono wake huku koti lake jeusi refu ambalo lilivuka magotini likikamilisha mwonekano wake wa kuwa moja kati ya wanaume ambao walikuwa wanatisha mno.

Akiwa na kofia yake kubwa aina ya pama kwenye kichwa chake, alikuwa anatembea haraka haraka tena kwa uangalifu mkubwa akionekana wazi kuwa mtu ambaye alikuwa makini sana na begi lake ambalo lilikuwa kwenye mkono wake ili lifike salama mahali ambapo alikuwa anatakiwa kulifikisha usiku huo.

Akiwa kwenye huo mwendo wake wa haraka baada ya kufika katikati ya barabara ndogo ambayo ilikuwa imezungukwa na majengo marefu sana ambayo yalikuwa yamejengwa kwa mawe magumu mno huku pembezoni kukiwa na vichochoro vingi ambavyo vilielekea maeneo tofauti tofauti. Alihisi kwamba hilo eneo ni kama kulikuwa na ugeni, nafsi yake ilimpa taarifa hiyo kwamba walikuwepo watu wengine ukiacha yeye.

Masikio yake yalimtekenya na kumpa taarifa hiyo kupitia mlango wake wa hisia na alikuwa akiziamini sana hisia zake kwa kuamini kwamba zisingeweza kabisa kumdanganya kamwe hivyo akawa na uhakika kwamba alikuwa kwenye hatari majira hayo ya usiku wa kiza totoro, huku taa kwa mbali zilizokuwa zimezunguka kwenye majengo ya karibu yake zikiwa zinatoa mwangaza ambao ulimsaidia kuona kila kitu ambacho kilikuwa pembeni yake.

Alisimama na kuyafumba macho yake kisha akayaweka masikio yake kwenye hali ya utulivu na usikivu mkubwa isivyo kawaida ili aweze kujua kwamba huyo mgeni au hao wageni walikuwa wamejifichia wapi na wangetokea wapi ili aweze kujihami mapema kabla hajapata madhara yoyote yale. Akiwa amesima hapo na begi lake mkononi ambapo mkono mmoja alikuwa ameuweka kiunoni sehemu ambayo ilikuwa na kisu kikali sana, alihisi kwamba kuna kitu kilikuwa kinakuja alipo kwa kasi kubwa sana kiasi kwamba sikio lake lilicheza kumpa ishara hiyo hivyo aliinama kwa kasi mithili ya mwanga wa radi ambavyo huwa unajitokeza machoni radi ikipiga kisha ungetoweka haraka.

Kuinama kwake kulimsaidia kupishana na shoka la chuma ambalo lilienda kukita kwenye moja ya kuta za majengo marefu ambayo yalikuwa karibu na alipokuwa amesimama. Alihema kwa nguvu kwa tumaini la kushukuru kuweza kupona kwenye dhahama hiyo na kuamua kugeuka kwa kasi kubwa ila wakati anageuka alitumia muda mwingi sana ambao ulimuingiza matatizoni.

Alihisi kifua chake kinamuwasha maana spidi ambayo ilitumika kumkita hapo ilikuwa ni kama umeme unavyo safari kwenye njia zake, alitema damu maana alipokea mishindo mikali ya haraka haraka ya mabuti ambayo yalitoka kwa mtu ambaye alikuwa ana nguvu kubwa sana miguuni na mtu huyo alionekana dhahiri alikuwa amedhamiria kuweza kumuua moja kwa moja.

Mwanaume huyo licha ya kurushwa mbali karibu na kuta za mijengo hilo, mgongo wake ulikuwa umelenga jiwe ambalo lilikuwa lipo kwenye msingi mkubwa wa jengo moja na kama angekita hapo basi moja kwa moja alikuwa anaupoteza uti wa mgongo wake, hakuwa tayari kufa kifala sana namna hiyo hivyo aliutanguliza mkono wake baada ya kujipinda kidogo tu na mkono wake ndio ambao ukakita kwenye jiwe hilo la msingi wa hiyo nyumba. Mkono wake ulikuwa na gloves lakini nguvu ambayo ilitumika kukita kwenye huo ukuta ilifanya koti lake kujivuta kidogo na kuufanya mkono wake uonekane ambapo mkono huo ulikuwa na tattoo (tatuu) iliyokuwa inasomeka 002 mbele yake pakiwa na alama ya nyoka.

Mwanaume huyo alitua chini na kukiweka sawa kifua chake na kuifuta damu ambayo ilikuwa kwenye mdomo wake kisha akageuka kumwangalia mtu huyo ambaye alikuwa amemvamia ndani ya hilo eneo. Kwa bahati mbaya sana mtu ambaye alikuwa mbele yake hakuwa akionekana sura kwani sura yake ilikuwa imefunikwa na kitambaa cheusi huku naye akiwa amevaa mavazi kama yake mpaka kofia kichwani ilikuwa ni kama yake. Kitu pekee ambacho walikuwa wametofautiana ilikuwa ni kwamba mvamiwaji uso ulikuwa wazi na mvamiaji uso wake ulikuwa umefunikwa wote na kumfanya asitambulike kabisa kwamba alikuwa ni nani.

“Tunafahamiana kabla?” mvamiwaji aliuliza swali ambalo halikuwa na majibu, alitabasamu kidogo na kukitoa kisu chake ambacho mara ya kwanza hakufanikiwa kukitoa. Mwenzake alikuwa amesimama tu anamwangalia bila wasiwasi kwenye macho yake. Aliyakanyaga maji ya mvua chini kwa nguvu na kuyafanya yapande juu kuelekea alipokuwepo mvamiaji kisha akakirusha kisu kwa kasi kikiwa kinapita kwenye yale maji huku naye akija kwa nguvu sana kwa hatua ambazo zilikuwa zinapigwa kwa umakini sana.

Mwanaume ambaye alikuwa mbele yake hakukikwepa kile kisu bali alikiacha kikazama kwenye bega lake, wakati huyo mvamiwaji naye alikuwa amefika eneo alilokuwepo ambapo aliituma ngumi yake eneo ambalo lilikuwa na kisu ili akizamishe zaidi ndani. Mvamiaji ni kama alishtuka kutoka kwenye tafakari ambayo alikuwa nayo kwa muda ambao alikuwa hapo hivyo aliteleza kwenye maji kusogea nyuma kidogo ya alipokuwa na kufanya ngumi hiyo ipige hewa.

Mvamiwaji alizunguka teke la chini ambapo mvamiaji aliruka sarakasi ya nyuma na miguu yake ikatua kwenye ukuta na mikono ikidaka sehemu ya jiwe akawa amegeuka miguu juu na mikono uelekeo wa chini akimwangalia mwenzake ambaye aliishia kuyasambaratisha tu maji ambayo yalikuwa chini na hakufanikiwa kumpata mtu wake. Mvamiwaji alichukia sana kiasi kwamba akavua mpaka koti lake na kulirushia pembeni ila wakati anafanya hayo yote mvamiaji alikichomoa kisu kwenye bega lake na kukirudisha kwa mwenye nacho kikiwa kinaenda kwa mwendo mkali ambao ulipatikana kutokana na spidi ya mrushaji kuwa kubwa sana. Mwanaume huyo alijitahidi sana kukikwepa kisu hicho kikaishia kumbaraza kwenye shavu lake ila wakati anapambana kukikwepa kisu hicho mvamiaji alikuwa ameshuka pale juu kama kimbunga.

Alitua kwenye mbavu ya mvamiwaji ambapo ngumi mbili zilitosha kumfanya agugumie kwa maumivu makali ambayo yalijitawanya kila sehemu ya mwili wake. Alirudi nyuma akiwa anayumba yumba, mvamiaji alidunda kwa mkono mmoja na kujibetua na meteke mawili ambayo mvamiwaji aliyaona na kuyakwepa kwa kuinama ila wakati anainuka mvamiaji huyo alizungusha teke la chini na kumzoa mwanaume huyo ambaye angedondokea mgongo kwenye maji ambayo yalikuwa hapo chini yametuama ila hakufanikiwa kuiona ardhi baada ya kushindiliwa mateke mawili ya shingo ambayo yalimburuza mbali sana kwenye maji ambayo yalikuwa hapo karibu.

Alipata maumivu ambayo ilikuwa ni siri yake ndani ya mwili wake namna ya kuweza kuyaelezea, akiwa anatoka damu kwenye mdomo wake na puani huku kifua kikiwa kinawaka moto pamoja na shingo yake, aliinuka kwa maumivu huku akiunguruma kupiga kelela za hasira, aliinyoosha shingo yake mpaka ilipokaa sawa akageukia ule upande ambao alikuwepo mvamiaji ambaye kwa namna alivyokuwa anamshambulia alionekana kwamba alikuwa hapo kuweza kumuua.

Ila wakati anageuka tu, umeme ulikatika ghafla sana hata yeye mwenyewe alibaki kwenye mshangao maana lilikuwa ni tukio la haraka sana ambalo hata yeye hakuweza kulitegemea kwamba lingetokea majira hayo na wakati kama huo. Kukatika kwa umeme huo kwake ilikuwa ni ahueni maana angepata muda wa kupumzika japo gizani ingekuwa ni ngumu kumuona adui yake ila aliamini kwamba angekuwa makini na wakati huo angepumua kwanza kwani mtu ambaye alikuwa anapambana naye kama sio umeme kukatika basi ni wazi angemuua mapema mno.

Alitulia na kuweza kusikilizia kujua adui yake alikuwa wapi lakini hakusikia kitu zaidi ya mvua ambayo ilikuwa inaendelea kushuka kwa wingi. Akiwa anahitaji kupiga hatua moja umeme ulirudi tena lakini alishangaa baada ya kugundua kwamba mtu ambaye alikuwa amemvamia kwenye hilo eneo hakuwepo, ikimaanisha kwamba ni muda mrefu sana alikuwa ametoweka hapo. Aligeuka kwa pupa sehemu ambayo begi lake lilidondokea baada ya kupigwa lakini begi halikuwepo kwenye hilo eneo ishara ya mhusika ambaye aliingia hapo kutoweka nalo.

Aliogopa sana na kubaki akitetemeka kwenye mdomo wake, hakuwa anaamini kwamba alikuwa amelipoteza begi kizembe sana namna hiyo na begi hilo lilionekana kuwa la mhimu sana. Akiwa kwenye huo wasiwasi mkubwa aligundua kwamba mita kadhaa kwa chini kutoka alipokuwa amesimama yeye kulikuwa na karatasi nyeupe ambayo ilikuwa na maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwa damu ikiendelea kunyeshewa na mvua pale chini.

Aliisogelea karatasi hiyo na kuiokota ila baada ya kusoma kilichokuwa kimeandikwa hapo, aliiachia ghafla sana na kuanza kurudi nyuma huku akiwa anatetemea mwili mzima mpaka meno yake kwa namna alivyokuwa ameogopa na kushtuka kwani halikuonekana kuwa tukio la kawaida kwake kuweza kuona hali kama hiyo. Karatasi hiyo ilikuwa na maandishi ambayo yalikuwa yanasomeka “KAMARI YANGU YA MWISHO NDIYO KAMARI YAKO YA KWANZA”

Aliogopa sana kwa sababu hiyo ilikuwa ni kauli ambayo alikuwa anaitumia mwanaume mmoja ambaye yeye mwenyewe alimuua kwa mkono wake miaka kadhaa ambayo ilikuwa imepita. Aliangaza ile sehemu ambayo shoka lilikita muda ule lakini hakuliona hivyo aligundua kwamba mhusika alikuwa ameondoka na shoka lake na kilikuwa ni kitendo cha haraka sana, alisogea hatua kadhaa na kukiokota kisu chake na kukipachika tena kiunoni huku akiwa anaitoa simu yake mfukoni akionekana kwamba kuna mtu wa mhimu sana ambaye alikuwa anahitaji kumpatia taarifa za tukio hilo ila kwa bahati mbaya sana simu ambayo alikuwa anahitaji kuitumia kufanyia mawasiliano ilikuwa imevunjika na hapo akakumbuka kwamba ilipasuka baada ya teke zito kuzama hiyo sehemu hivyo aliamua kutoweka haraka sana hilo eneo.

Rasmi tunaanza kuifunua episode 1, ni mwanzo tu wa yale mengi ambayo tunakwenda kuyafunua ndani ya simulizi hii mpya. Nipe muda wako, jicho lako na umakini wako ile twende sawa ndani ya simulizi hii.

Kwenye kalamu nipo mwenyewe.

Tchao.

Next