Reader Settings

HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)

MTUNZI: FEBIANI BABUYA 

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

Episode 2

MIAKA 12 ILIYOPITA

Ndani ya nyumba za siri za shirika la kijasusi la taifa la Tanzania, vijana wawili walikuwa wanapokea kiapo kikali sana kwa spy master (Director General) kwa lugha rahisi mkurugenzi wao wa shirika la kijasusi mheshimiwa Philipo Tibaigana ambaye alikuwa na asili ya Kihaya. Nyumba hizo za siri ambazo ndizo walizitumia kuweza kula kiapo hicho zilikuwa pembezoni kabisa mwa jiji la Dar es salaam ambalo ndilo lilikuwa jiji kubwa zaidi la biashara ndani ya taifa la Tanzania hivyo mambo mengi yalikuwa yanafanyika ndani ya jiji hilo.

Vijana hao wawili walikuwa wanakula kiapo cha kwenda kumlinda raisi mpya wa taifa la Tanzania ambaye alikuwa ameshinda kwenye uchaguzi ambao ulikuwa umepita kwa kishindo japo kupita kwake nyuma kulikuwa na mambo mengi sana ndiyo sababu vijana hao walikuwa wanapewa kazi ya kuhakikisha raisi huyo anakuwa salama kwa namna yoyote ile. Baada ya kumaliza mafunzo yao ambapo walipelekwa ndani ya taifa la Uingereza, Urusi na Cuba, sasa walikuwa wameiva vya kutosha na walikuwa kamili gado kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaenda kuianza kazi yao hiyo ambayo ilikuwa ni mpya kabisa kwao ila hawakuwa na namna zaidi ya kuipokea amri kutoka kwa kiongozi wao ambaye ndiye alikuwa anawaapisha wakati huo.

Wanaume hao wawili walikuwa ni vijana wa umri wa kawaida tu ila uimara wao na mafunzo makali ambayo walikuwa wamefanikiwa kufuzu na kushika nafasi za juu miongoni mwa wengi ambao walikuwa wanatengenezwa kwa ajili ya kuja kudumisha ulinzi kwa viongozi wao ndiyo sababu kubwa ambayo iliwafanya wao ndio wapate hiyo nafasi ya kuweza kuchaguliwa kutekeleza majukumu ya taifa.

“Itifaki za nchi zinamtaka raisi wa kike kuweza kulindwa na mwanamke na hilo litafanyika lakini kuna mabadiliko kidogo yatafanyika, mlinzi wake wa kike atakuwepo lakini ninyi ndio ambao mtakuwa mnaongozana na huyo mlinzi kwa sababu sina imani na usalama wa mheshimiwa na sitaki tatizo lolote litokee nikiwa nipo kwani nitaonekana kama siwezi kuitekeleza kazi yangu vizuri kitu ambacho sijawahi kukubali nipate aibu ya kijinga kama hii hivyo nina imani mnajua ni kipi mtatakiwa kufanya si ndiyo?” aliuliza mheshimiwa huyo akiwa anawaangalia vijana hao wawili ambao walikuwa wamesimama kikakamavu sana.

“Ndiyo bosi” walijibu kwa pamoja kwa kujiamini sana.

“Mnajua kazi ya mhimu inayo wapelekea kule?”

“Kumlinda mheshimiwa raisi hata ikitulazimu kuyatoa maisha yetu itakapo hitajika kufanya hivyo”

“Nadhani sasa mshakula kiapo tayari na kazi iliyobakia ni nyie kutekeleza kile ambacho kipo mbele yenu. Kitu ambacho mnatakiwa kukikumbuka kila wakati kwenye vichwa vyenu ni kwamba serikali imetumia pesa nyingi sana kuweza kuwatengeneza nyie hapo ili mje kuifanya kazi hii, pesa hizo zingeenda hata kwa watoto yatima au wagonjwa lakini zinakuja kwenu kwa sababu ni jambo la mhimu sana kuilinda tunu ya taifa. Hakuna lolote ambalo unatakiwa kumuuliza wala kuhoji hata kama unaona anakosea hiyo siyo kazi yako wala siyo majukumu yako kuingilia kwa lolote. Haijalishi anaua ni mtu asiye na hatia, haijalishi anatukana mbele yenu, haijalishi anamtaka nani na hamtaki nani hamtakiwi kufanya upumbavu wowote wala kufanya kituko chochote maana sio majukumu yenu kabisa hivyo msije mkavuka mipaka maana mtakufa siku hiyo hiyo na nitawaua kwa mkono wangu mwenyewe, mnanielewa?”

“Ndiyo bosi tunakuelewa”

“Kumbukeni kwamba yule amechaguliwa na wananchi hivyo wananchi wanatarajia usalama wake kupewa kipaumbele kabla ya jambo lolote lile kutoka kwa vyomba vya ulinzi na usalama, hakuna kosa linatakiwa kufanyika. Naamini sana juu ya uwezo wenu, naamini sana kile ambacho mnacho ndani yenu, najua nyie ni wazalendo wakubwa hivyo mheshimiwa anatakiwa kuwa salama, hakuna kitu au mtu ambaye anatakiwa kugusisha hata mkono wake japo kwa bahati mbaya kwenye mkono wa mheshimiwa raisi. Wala hakuna risasi au kitu kilichorushwa kumpata hata kwa bahati mbaya ikiwa mpo hai na kama hilo linatokea basi litokee nyie mkiwa mmeshakufa tayari, mnanielewa?”

“Ndiyo bosi tunaapa kwa katiba ya nchi hii kuweza kumlinda mheshimiwa raisi hata kuyatoa maisha yetu pale ambapo itatubidi kufanya hivyo”

“Good. Kuanzia leo mnapewa majina mapya na namba zenu za siri ambazo ndizo zitakuwa code ambazo mtakuwa mnazitumia. Majina na hizi namba mnapewa kuendana na uwezo wenu na sio kigezo cha umri.”

“Sawa bosi” alimgeukia mmoja ambaye alikuwa anaonekana mkubwa kuliko mwenzie akiwa anamwangalia machoni kwa msisitizo.

“Wewe ndiye mkubwa kuliko mwenzako ukiwa na miaka ishirini na mitano tu lakini nina uhakika hata wewe mwenyewe unaelewa kwamba mwenzako amekuzidi kwa uwezo, hivyo kuanzia leo wewe jina lako ni Dax na namba yako ya siri ambayo utakuwa unaitumia kwenye mawasiliano ni 002” alimpatia vitambulisho vyake pamoja na kumbana na mashine kwenye mkono wake wa kulia ambapo tattoo hiyo ilijichora hapo japo alipata mauamivu makali ila hakushtuka maana hicho alichokuwa anapewa ndio ulikuwa utambulisho wake” kiongozi huyo baada ya kumalizana na kijana wa kwanza alimgeukia kijana wake wa pili.

“Una miaka ishirini na mitatu tu pekee lakini nakuamini na kukupa nafasi hii kubwa ya kuweza kumlinda mheshimiwa raisi wa nchi. Wewe ni miongoni mwa wachache sana ambao taifa limebahatika kuwapata kutokana na uwezo wako kuwa mkubwa sana kuliko hata umri wako hivyo hili jukumu la usalama wa raisi nalikabidhi kwenye mikono yako kwa sababu nakuamini sana. Wewe ndiye ambaye utakuwa unatoa ripoti kwangu na kunipa kila taarifa ya ambacho kitakuwa kinatokea na wewe ndiye ambaye utatakiwa kuwa wa kwanza kuyatoa maisha yako kama mheshimiwa atakuwa kwenye hatari yoyote ile ambayo inaweza kupelekea kuhatarisha maisha yake. Hakikisha hakuna kosa lolote lile ambalo linajitokeza hata kwa bahati mbaya. Umenielewa?”

“Ndiyo bosi, nakuahidi nitaifanya hii kazi kwa usahihi na uzalendo mkubwa mpaka pumzi yangu ya mwisho”

“Kuanzia leo jina lako wewe ni Max na namba yako ya siri ni 001” aliongea akiwa anamkabidhi vitambulisho vyake pamoja na kumbana na mashine ambayo ilikuwa kwenye mkono wake mpaka ilipo jichora hiyo tatuu ambayo ilikuwa na hiyo namba 001” baada ya kumalizana nao, kuna wanaume waliingia wakiwa kwenye suti zao kuwachukua vijana hao wawili ambao walikuwa wanaenda kuanza kuifanya kazi ya kuweza kumlinda mheshimiwa raisi wa nchi ya Tanzania ambaye alikuwa ameshinda uchaguzi wake ambao hata yeye hakuwahi kutarajia kama anaweza kufika hapo alipokuwa amefikia kwa siku hiyo.

Teodensia Mpanzi, ndilo lilikuwa jina la aliyekuwa raisi wa nchi ya Tanzania, mwanamama ambaye alikuwa ameyabeba maono ya watanzania wengi, mwanamama ambaye aliamini kwamba nchi ilikuwa inapaswa kwenda mbali zaidi ya pale ilipokuwa imefika huku akiwa ana imani kwamba watangulizi wake hawakuifanya kazi ambayo walitakiwa kuifanya ili kuhakikisha kwamba nchi inajengekea na kuwa moja kati ya mataifa makubwa na yenye nguvu sana duniani.

Alikuwa ameapishwa tayari na ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza tangu akabidhiwe ofisi yake, na ndiyo muda ambao waliingia walinzi wa Ikulu huku wakimpa taarifa mheshimiwa kwamba kulikuwa na ugeni wa wanaume wawili ambao walikuwa wameletwa hapo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba yupo salama muda wote lakini habari hiyo yeye hakuisadiki kabisa wala kuikubali. Alimpigia simu Philipo Tibaigana ili aweze kulijibia hilo na kujua kama alikuwa na taarifa juu ya ujio wa vijaan hao ambao aliambiwa kwamba muda mfupi wangeripoti hapo ofisini kuweza kuanza kuifanya kazi ya kumlinda yeye.

“Mzee wangu habari ya kazi?” alimsalimia kwa kumheshimu kwa sababu alikuwa amemzidi umri.

“Salama mheshimiwa, heshima yako kiongozi wangu”

“Nasikia kuna vijana wanakuja kunilinda hapa, kwamba haujaona walinzi wa kike kwamba wananitosha mpaka uniletee hawa vijana wako ambao sijui hata lengo lako la kuwaleta ni lipi? Unahisi kweli itafaa mimi kuendelea kukubakisha kwenye hiyo nafasi?”

“Naomba unisamehe sana mheshimiwa, najua kwamba unaweza ukampa nafasi hii mtu yeyote yule ambaye unamtaka wewe lakini mimi nimefanya hivyo kwa sababu za usalama zaidi na itifaki ya nchi. Walinzi wa kike ni wengi sana na wapo wa kutosha ila nina sababu za mhimu kukuletea hao vijana kwani ndio vijana pekee ambao wamepata alama za juu kabisa za haya mafunzo na serikali imetumia pesa nyingi sana kuwapa mafunzo kwenye nchi mbali mbali takribani miaka mitano hivyo wamebobea sana kwenye taaluma hii ndiyo maana nikawaleta kwako ukizingatia namna ulivyokuwa unafanya kampeni zako ulipokea vitisho vingi sana hivyo sitataka raisi wangu upate matatizo mimi nikiwa madarakani maana bado hatujui nani yupo upande wako na nani hayupo upande wako”

“Mhhhhh wazo lako ni zuri sana ila sidhani kama kweli haujui nani yupo upande wangu na nani hayupo upande wangu, sisi sio watoto wadogo. Najua unalielewa hili taifa ndani nje na wewe ni miongoni mwa watu ambao walikuwepo tangu enzi za mtangulizi wangu na unamjua vizuri namna alivyo kwahiyo ukisema hauelewi unakuwa unanipa sana mashaka. Nitawapokea na nitaangalia uwezekano kuhusu nafasi yako kama utaendelea kubaki au nikupe ubalozi mataifa ya mbali huko, uwe na siku njema”

“Asante sana mheshimiwa” kiongozi huyo wa shirika la kijasusi alijibu lakini hakuridhika kwani kwake aliona kama dharau, yaani licha ya kujitoa kwake kote bado alikuwa anatishiwa kupelekwa kuwa balozi kwenye mataifa ya mbali huko, kwake ilikuwa ni zaidi ya dharau hiyo maana raisi huyo ni kama alikuwa anahitaji kumtoa nje ya mfumo wake.

Teodensia Mpanzi baada ya kuikata simu hiyo ambayo aliipiga kwa mkurugenzi, alitoa amri kwamba vijana hao waingizwe ndani ya ofisi yake anahitaji kufanya nao mazungumzo ya siri akiwa yeye na wao tu pekee. Baada ya dakika kumi waliletwa vijana hao wawili na mlinzi wa humo ndani kisha baada ya kuwafikisha akawaacha wao wawili tu na mheshimiwa raisi maana yeye mwenyewe ndiye alikuwa ametoa amri iwe hivyo.

Aliwaangalia kwa umakini sana, vijana hao hawakuwa na sura za kutisha sana kwa mtazamo wao. Mkubwa zaidi angalau alikuwa ana sura ambayo ilikuwa imekomaa zaidi lakini ambaye alikuwa anaonekana mdogo sura yake ilikuwa kama barobaro mtaani japo wakati huo alikuwa kwenye suti ambayo ilikuwa imemkaa vyema sana.

“Nimepata taarifa zenu kutoka kwa mr Philipo Tibaigana lakini yule mhaya simwamini sana maana kuna muda huwa anapenda sana kusifia vitu ambavyo havitakiwi kusifika, nawaaminije juu ya uwezo wenu na kuwapa dhamana ya kuweza kunilinda ingali sijui hata uwezo wenu upoje?”

“Mimi nimepata mafunzo yangu ndani ya taifa la Tanzania lakini baada ya kufuzu nikapata nafasi ya kwenda Cuba kwa ajili ya mapigano. Huko nilifanya vizuri zaidi nikapata nafasi ya kwenda kupata mafunzo ya kijasusi ndani ya nchi ya Uingereza ambapo nilikaa mwaka mmoja ndipo nikafaulu vizuri na kufanikiwa kwenda kumalizia mafunzo yangu ndani ya nchi ya Urusi” Dax alitoa maelezo yake kikakamavu sana huku akiwa amemkabidhi mheshimiwa taarifa zake na wakati anaendelea kuyatamka hayo maneno mheshimiwa raisi alikuwa anaendelea kuzipitia taarifa zake na baada ya mwanaume huyo kumaliza mheshimiwa aliinua uso wake na kumwangalia usoni kwa umakini maana sifa zilizokuwa zimeandikwa pale kuhusu yeye ni kama hakuwa akiendana nazo kabisa.

“Jina lako unaitwa Karistus Dickson (KD) lakini unatambulika kama Dax na namba yako ya utambulisho ni 002?”

“Ndiyo mheshimiwa”

“Mhhh hizi ni taarifa zako kweli? Mbona zimeandikwa taarifa ambazo haziendani na mwonekano wako?”

“Hizo ni zangu mheshimiwa ndiyo maana nipo hapa na naapa kukutumikia mpaka pumzi yangu ya mwisho, nitatii na kufanya kila ambalo unalitaka lakini lengo kubwa ni kuyalinda maisha yako hata ikiwezekana kuyatoa maisha yangu kwa ajili yako”

“Una uhakika upo tayari kufa kwa ajili yangu?”

“Ndiyo mheshimiwa” mwanaume huyo alijibu akiwa amesimama kijasiri sana, raisi alimwangalia kwa umakini sana akiwa haamini hayo maneno hivyo alizunguka mpaka kwenye droo yake na kuitoa bastola ambayo ilikuwa imekokiwa kabisa.

Episode ya pili natundika daruga hapa.

Tukutane wakate ujao.

Tchao.

Previoua Next