Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

NOTE:
HADITHI HII NI YA KUTUNGA TU HAIHUSIANI NA MAISHA YA MTU YEYOTE, MAMLAKA WALA SEHEMU YOYOTE ILE NA HAILENGI KABISA KUMCHAFUA MTU YEYOTE YULE, KILA KILICHOPO HUMU NDANI NI CHA KUTUNGA TU NA KUFIKIRIKA.

STORY: GEREZA LA HAZWA
STORY WRITER: FEBIANI BABUYA
STORY TELLER: Bux the story teller
EMAIL: [email protected]
WHATSAPP: 0621567672


UKURASA WA KWANZA

ANZA NAYO..............

Wakati nyie mnalala sana mkiwa mnausaka usingizi wa pono watu wenye ndoto zao ambao wanaiogopa njaa kuliko kitu chochote kile wapo macho kuzitafuta na kuzisaka ndoto zao kuhakikisha mwana haramu ambaye anaitwa tumbo anaridhika kwa namna yoyote ile hata kwa kumlazimisha. Ni wanadamu ambao wanaamini mikono yao ndiyo msaada wao wa pekee wa kuweza kuendelea kuwa hai na kupunguza mateso pamoja na dhihaka za kuchekwa na wanadamu wasiokuwa na uoga wowote mbele ya dunia ya Muumba, hao ndio watu ambao wanaweza kuiishi hii dunia yenye kila aina ya vioja vya ajabu na vya kutisha pia, kwao hawaamini katika bahati juhudi kwanza ndizo zinazo wapa imani ya kujikwamua kwenye maisha magumu sana ambayo wanayapitia wakiamini hakuna kitu kirahisi kukipata kwenye ulimwengu ni lazima ulipie ndipo ukipate unacho kitaka. 

Wanalipaje na hawana pesa? Basi jasho lao ndilo malipo ambayo wanatakiwa kulilipa ili tu wafanikishe moja ya ndoto zao za kuwa na maisha angalau kupata hata milo miwili mpaka mitatu kwa siku “the bright future is only for the brave people” ni kauli ambayo inawapa muongozo wa nini wanatakiwa kukifanya kwenye maisha yao kama tu watahitaji kuipata ahueni ya maisha wakiamini ujasiri wao na ushujaa wao ndicho kitawapa kesho iliyo njema, hawana mashamba ya kusema wajifariji kwamba kama wakitaka mali basi wataipata shambani, yes, hayo ndiyo maisha halisi kwao.

ARUSHA, TANZANIA

Ndani ya machimbo ya moja ya madini adimu zaidi ulimwenguni na yanapatikana ndani ya nchi moja tu ulimwengu mzima ambayo ni Tanzania pekee kuna wanaume wapo ndani kabisa sehemu ambayo ilikuwa na kiza cha kutosha, tochi zilizofungwa kwenye vichwa vyao zilikuwa ni sehemu ya kuwasaidia kuona vitu ambavyo vipo mbele yao. Sio kwamba walikuwa sehemu ambayo haina umeme kiasi kwamba watashindwa kuona nini kilichopo huko hapana bali ni moja ya njia za kuweza kuzisaka na kuzifikia ndoto zao, wapo mgodini ndani kabisa ambako hata mwanga wa jua huwa ni ndoto kuonekana, mtu anakuwa kama yupo dunia ya peke yake tofauti kabisa na hii dunia ya kawaida ambayo kila mwanadamu anaiishi. Kama mtu angeshtuka kutoka usingizini akajikuta hiyo sehemu basi angehisi moja kwa moja kwamba ulikuwa usiku wa manane sana kulingana na aina ya kiza kizito ambacho kilitanda ila ni muda ambao usingeamini kwamba ilikuwa ni jioni ya kawaida kwenye dunia ya huku nje ambayo watu walikuwa wanaendelea na shughuli zao za kila siku hasa kwa wale wasaka tonge na wengine wale ambao kwao kazi ni mwiba uwachomao sana hawakuacha kuendelea kupiga majungu na jingi kwenye vijiwe mbali mbali na kuendelea kuijutia zamani zao badala ya kuiwaza na kuijenga kesho yao  iliyo bora.

Ndani ya mgodi ambao unajulikana kwa kuwa na madini ya Tanzanite ndimo wanamo onekana wanaume wa kazi wakiwa hawaongei sana ila vitendo vyao vinajionyesha majembe mazito, uma, nyundo na machepeo ndivyo vitu vinavyo ongea zaidi huko, wanaume hawalali kuhakikisha maisha bora yanakuja kupitia imani zao za ufanyaji kazi kwa bidi. Vijana zaidi ya watano kila mmoja akiwa upande wake wanapambania kombe chini ya ardhi ambako kama ikitokea namna yoyote kukajifunika basi hadithi zao zinakuwa zimeishia huko huko chini ila hakuna namna wanaweza kuyafanya maisha yakawa malaini kwao kwa mlo wao wa siku moja kwa siku zaidi ya kujitoa mhanga. Ni zaidi ya masaa matano wakiwa wanafanya kazi kwa bidii sana.

“Hey Alen una tatizo gani man” ni sauti ya mmoja wa wale vijana watano ambao walikuwa ndani ya mgodi baada ya kusikia mwenzake yupo kimya sio nyundo wala chepeo ambayo ilikuwa inasikika upande aliokuwa.

“Ni kichwa tu kidogo Kani usijali hakuna tatizo” alimjibu mtu wake huyo ambaye ni wazi walikuwa wanajuana kama sio kuwa marafiki kabisa.

“Oya kama uko vibaya pandisha juu huko chapu gusa kamba pale usije kutupatia kesi mwanangu nadhani unayajua maisha yetu yalivyo hata mia mbovu tu kuipata mpaka tujitoe maisha yetu humu ndani” alionekana kumjali mwenzake kama sio kumtaka atoke asije akaleta ugumu wa kazi kama akizidiwa huko chini yakawa mambo mengine.

“Napumzika dakika moja tu kisha naendelea man usiogope” alimaliza kwa kuongea huku akipigiza nyundo moja kwenye jiwe kama sio chuma maana mlio ulio sikia ni dhahiri lilikuwa ni jiwe limepitiwa na nyundo, baada ya kufanya hivyo aligeuza macho yake huku akiivua tochi kwa kuwaangalia wenzake ambao walitawanyika kidogo ilikuwa inaonekana miale ya mwanga tu kutokana na kiza kizito kilicho kuwepo. Alipoona kila mtu anaendelea na majukumu yake aliinama chini na kuokota vipande vidogo vidogo vya kutosha ambavyo alivitawanyisha kwa nyundo yake, alitoa nailoni ndogo kwenye nguo yake ya ndani akawa anaichana kidogo anakikunja kipande kimoja kimoja kisha anakimeza mpaka alipo kamilisha vinne. Akatulia kidogo kisha akachukua vipande vilivyokuwa vimebakia akavua suruali yake na kuvifunga sehemu zake za siri kwenye hicho kinailoni ambacho aliviweka ndani vipande hivyo kisha akajivalisha kwenye uume wake na kuvifunga kwa kikamba kidogo ambacho alikuwa amekihifadhi kwenye mfuko wake. 

Ni wazi alipata maumivu makali alikuwa akiikunja sura yake kila anavyoikaza kamba ili iwe sawa na uume wake ila hakuwa na namna hiyo ndiyo ilikuwa njia ya pekee kwake, mkono wake ulilowa alijua ni damu inatoka baada ya sehemu zake za siri kupata majeraja kutokana na kubanwa sana na vipande hivyo vya mawe na kamba iliyokazwa sana kwenye uume wake hata hivyo hakujali sana alikuwa akiuma meno yake tu huku anaendelea na zoezi lake vizuri mpaka alipohakikisha amekamilisha baada yah apo akajifuta damu mkononi kwenye mchanga uliokuwa chini. Alikuwa na wasiwasi sana kiasi kwamba jasho lilikuwa linamtoka mno kwenye mwili wake wote aliivaa tochi yake tena kwenye kichwa chake akaendelea kupiga kazi machozi yakiwa yanamtoka alikuwa na mawe manne kwenye tumbo lake hiyo haikutosha kweye sehemu yake ya thamani zaidi kwenye mwili alikuwa amejifunga mawe ambayo yalikuwa yakimletea maumivu makali lakini alichagua kuichagua hiyo njia ya kuumia kwani alikuwa anaamini hakuna njia rahisi kabisa kwenye utafutaji.

“Kichwa changu mimi nakufaa nakufaaa jamani msaada” yule mwanaume ambaye jina lake alifahamika kama Alen alisikika akipiga makelele ya kuomba msaada kwa kudai kwamba kichwa chake kinamuuma sana na alikuwa akilia kwa sauti kali, ni hali iliyo washtua wenzake wa mle ndani lakini aliyekuwa na muda naye ni mmoja tu wengine waligeuka tu mara moja kisha wakaendelea na kazi zao za utafutaji walifunzwa kwenye utafutaji kuwa na roho ngumu zaidi ndiyo siri pekee ya mafanikio huruma zingewachelewesha kufika kwenye safari zao ndefu za maisha ndiyo sababu hawakuwa na huruma na mtafutaji mwenzao waliamini huyo kama anakufa atajua yeye na hata akiishi hakuna kitu atawasaidia. Kani kama jina lake lilivyo itwa na Alen alimkimbilia msaka tonge mwenzake akamkuta chini akiwa na joto sana kwenye mwili wake huku akiwa anatoa machozi kuonyesha wazi hali yake ni mbaya hata mwili wake ulikuwa umechemka mno baada ya kumgusa kwenye kichwa chake.

Akamkokota mwenzake kwa mwanga wa tochi anafanikiwa kufika mpaka sehemu ya kuingilia humo ndani ambapo kwa mbali aliuona mwanga wa nje, kuna kamba ya kutolea ishara aliigusa na kuivuta kwa nguvu kisha akakaa pembeni ya mwanaume mwenzake kwa dakika kama mbili mpaka ngazi iliposhuka alijua wakati wa kutoka sasa umefika. Mwanaume alimshika bega mtafutaji mwenzake na kupandisha naye juu ambako huko waliumizwa na mwanga wa kawaida wa dunia yetu ya kila siku baada ya kukaa huko chini kwa muda mrefu ila hawakuwa na namna ni aina ya utafutaji waliyo ichagua. 

Kani alipiga kelele kwamba mtu huyo amezidiwa sana akicheleweshwa hapo lazima atakufa hivyo wafanye haraka kumpa msaada, ililetwa gari ndogo ya hapo machimboni ili kumuwahisha mtu huyo hospitali, kwa namna alivyo lala na hali yake ilivyo onekana hakuna mtu ambaye alipata ujasiri wa kuweza kumkagua mwili wake kwa maana alivaa nguo chache sana hivyo alipandishwa kwenye gari moja kwa moja na kuwahishwa hospitali ili kupewa matibabu ya haraka kuweza kuiponya nafsi yake.

Kani kama alivyo julikana alijitahidi sana kuomba amsindikize mtu huyo hospitali ili awe kama mwangalizi wake lakini hakuipata hiyo nafasi walimwambia yeye aendelee na kazi yake huyu wagemshughulikia mwenyewe basi kishingo upande alirudi ndani ya shimo akiwa anasikitika juu ya hali ya mwenzake ambayo ilibadilika ghafla tu.

HOSPITAL
Yes, mwili wa mgonjwa ulifikishwa salama akiwa anaonekana kuzidiwa na kuhema kwa shida sana, madaktari walimpokea na moja kwa moja alipokelewa na kupelekwa moja kwa moja kwenye chumba cha wagonjwa mahututi ambacho kinajulikana kama ICU (an Intensive Care Unit). Uongozi wa machimboni haukuwa na namna zaidi ya kuweza kusubiri vipimo vya madaktari ili wapate majibu mgonjwa wao ana shida gani kwa sababu kama kuna chochote kingetokea wao ndio watu ambao walitakiwa kujibu kuhusu hiyo kesi, ndani ya nusu saa tu daktari ambaye alikuwa amewapokea na ndiye ambaye alikuwa akishughuika na masuala yote ya ICU aliwapa taarifa kwamba mgonjwa wao hana tatizo lolote isipokuwa anaonekana kufanya kazi kwa muda mrefu sana bila kupumzika hivyo hali ya mwili ilibadilika na kufikia kwenye hiyo hali ambayo alikuwa nayo sasa hivyo atalala hapo ila kesho asubuhi waje kumchukua mtu wao atakuwa sawa kabisa akiwa kwenye afya nzuri pia daktari aliahidi kwamba mtu huyo akizinduka tu atarudi kwenye hali yake ya kawaida na atabadilishiwa wodi.

Asubuhi na mapema wale watu walikuwa wamefika hapo kwa sababu huyo mwanaume kama yupo sawa alihitajika kurudi maeneo ya kazi akajumuike na wenzake kama ilivyo siku zote ila cha ajabu daktari waliye mkuta jana aliwapa taarifa ambazo zilimshtua kila mmoja wao, waliambiwa kwamba mtu huyo tangu jana daktari alipoweza kutoka kwenye ile wodi alivyorudi hakumkuta huyo mgonjwa kabisa na hakujulikana ameelekea wapi, alidai kwamba walipitia mfumo wa kamera za ulinzi kwenye hiyo hospitali zote lakini cha ajabu zote zilizima kabisa hakuna hata moja ambayo ilikuwa imewaka kwa muda huo kwahiyo kwa lugha raisi tu ni kwamba mgonjwa alikuwa amepotea kwenye mazingira ya kutatanisha mpaka muda huo hospitali haikuwa na taarifa yoyote ambayo alikuwa ameandikisha sababu kubwa ni kwamba alikuja akiwa amezimia hivyo walisubiri aamke ndipo waweze kuziandika na kuzirekodi taarifa zake kwa usahihi.

Uliwahi kusikia wapi mgonjwa ambaye amezimia anatoroka?....... ni nani yeye hasa mpaka apotee kwenye mazingira kama haya? ...., unavyohisi atakuwa amepotelea wapi mwanaume huyu……….

Ndo kwanza tunaufungua ukurasa wa kwanza kabisa kwenye kigongo hiki ambacho kinaitwa GEREZA LA HAZWA……lina nini hili gereza? wanafungwa akina nani humo ndani? linahusikaje na hadithi hii? Na ni kiumbe gani kinakuja kuwa kiumbe cha hatari mno mpaka wanahitaji kukifunga kwenye hilo gereza?.......majibu utayapata humu ndani ungana na kalamu yangu tena mwanzo mpaka mwisho.

Wananiita 

Bux the story teller

chao

Next