Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)

MTUNZI: FEBIANI BABUYA 

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

Episode 3

“Jina lako unaitwa Karistus Dickson (KD) lakini unatambulika kama Dax na namba yako ya utambulisho ni 002?”

“Ndiyo mheshimiwa”

“Mhhh hizi ni taarifa zako kweli? Mbona zimeandikwa taarifa ambazo haziendani na mwonekano wako?”

“Hizo ni zangu mheshimiwa ndiyo maana nipo hapa na naapa kukutumikia mpaka pumzi yangu ya mwisho, nitatii na kufanya kila ambalo unalitaka lakini lengo kubwa ni kuyalinda maisha yako hata ikiwezekana kuyatoa maisha yangu kwa ajili yako”

“Una uhakika upo tayari kufa kwa ajili yangu?”

“Ndiyo mheshimiwa” mwanaume huyo alijibu akiwa amesimama kijasiri sana, raisi alimwangalia kwa umakini sana akiwa haamini hayo maneno hivyo alizunguka mpaka kwenye droo yake na kuitoa bastola ambayo ilikuwa imekokiwa kabisa.

“Hii ni bastola ambayo ina risasi zote sita na imeshakokiwa tayari, hivyo nahitaji ujipige risasi ili niamini kwamba kweli upo tayari kufa kwa ajili yangu” alimaliza maelezo yake huku akiwa anamkabidhi mkononi na mwanaume huyo hata hakujiuliza mara mbili, aliilengesha bastola hiyo kwenye kichwa chake kisha akaachia risasi lakini aligundua kwamba ndani hakukuwa na risasi yoyote ile, ina maana raisi alikuwa anampima kama kweli yupo tayari kufanya lolote kwa ajili yake. Mheshimiwa alimpigia makofi na kumpongeza mwanaume huyo wa kazi kisha akamgeukia ambaye alikuwa anaonekana mdogo kuliko mwenzake na kulishika faili lake bila kumpa ruhusa ya kuweza kuongea lololote.

“Donald Daniel (Double D (DD), jila lake la utani DONNY lakini jina la kazi ni Max na namba yake ya utambulisho ni 001. Ndiye mwanafunzi bora wa mafunzo ya miaka mitano ndani ya taifa la Tanzania akiwa ameyapatia mafunzo yake ndani ya taifa la Tanzania, Cuba, Uingereza pamoja na Urusi na huyu ndiye atakaye ichukua nafasi ya kuweza kuhakikisha usalalama wa mheshimiwa raisi mahali popote na kwa muda wowote ikilazimu hata kuweza kuyatoa maisha yake kwanza kabla mheshimiwa hajapata madhara” mheshimiwa raisi alibaki ameduwaa akiwa anasoma ripoti ya huyo kijana kutoka kwa mkurugenzi. Ni kama alikuwa haamini kile ambacho alikuwa anakisoma hivyo akawa anamwangalia kijana huyo mara mbili mbili.

“Hizi zilizo andikwa humu ni taarifa zako wewe?”

“Ndiyo mheshimiwa”

“Nataka unithibitishie kwa macho yangu sidhani kama inawezekana kweli wewe ndo uwe hivi, baadae kidogo kuna watu nahitaji ufanye nao mazoezi ya mapigano ndipo nitathibitisha kama hizi taarifa ni za kweli, na kama ni kweli basi kuanzia leo nawapa hiyo ruhusa ya kuweza kunilinda lakini kama ukishindwa basi wote nawaua kwa kuniletea taarifa za uongo pamoja na huyo mkurugenzi wenu. Mmenielewa?” 

“Ndiyo mheshimiwa” wanaume waliruhusiwa kuweza kutoka ndani ya ofisi ya raisi wa nchi na huo ndio ulikuwa mwanzo wao wa kukaa karibu na mheshimiwa raisi na kuwa walinzi wake rasmi.

ALEXIOS ARENA

Ulikuwa ni ukumbi mkubwa sana ambao ulikuwa unaendesha Kamari hususani za mapigano. Ni ukumbi ambao ulikuwa unajulikana mpaka na viongozi wa serikali ila walikuwa wanafumba macho na kuziba masikio kila jina hilo linapo tajwa bila kujulikana kwamba kwanini walikuwa wanafanya mambo hayo licha ya kujua kwamba ndani ya ukumbi huo kulikuwa kuna mambo mengi sana ya kutisha ambayo yalikuwa yanafanyika hapo. Sio kila mtanzania alikuwa anaweza kwenda kuingia ndani ya ukumbi huo kwani walikuwa wanahitajika watu wenye pesa za kutosha na ukwasi mkubwa ndio ambao walikuwa wanapata nafasi ya kwenda kutazama mapambano ya wanaume humo ndani.

Ni ukumbi ambao ulikuwa umeshamiri kwa uchezaji wa Kamari na wacheza Kamari maarufu ndani ya nchi ungewakuta humo ndani. Mapigano ambayo yalikuwa yanafanyika humo ndani yalikuwa ni ya mauaji, kama ungepanda ulingoni na ukashindwa kushinda basi moja kwa moja ulikuwa unauawa na hivyo ndivyo wanaume wa shoka walivyokuwa wanautafuta ugali na kuyaishi maisha ndani ya ukumbi huo wa kutisha. MLINZI ndiyo ilikuwa maana ya ukumbi huo mkubwa kwa tafsiri ya Kiswahili ambapo ilidaiwa kwamba muasisi wa ukumbi huo ndiye ambaye alipewa jina hilo lenye asili ya kigiriki ikiwa na maana ya kwamba ndiye ambaye alikuwa anausimamia ukumbi huo na kuhakikisha kwamba upo salama.

Wanawake walikuwa wanafanya biashara za kuuza miili humo ndani tena kwa dau kubwa mno kwa sababu maskini haikuwa sehemu yao sahihi zaidi ya kuishia kusimuliwa tu raha zipatikanazo ndani ya ukumbi huo, kulikuwa na makasino ya bei ghali sana humo ndani na kila kitu kilipatikana lakini chini kabisa ya ukumbi huo kulikuwa na ulingo wa mapambano ambapo walikuwa wanapatikana wanaume wa shoka haswa ambao walikuwa wanauana ili kuweza kutengeneza ufalme na pesa kwa ajili ya kuweza kuishi maisha mazuri.

Usiku wakati pambano moja likiwa linaendelea ndani ya ulingo wanaume wakiwa wanapimana mabavu, upande wa juu kabisa walikuwa wamekaa wanaume watatu ambao wote walikuwa wamejifunika vikoi na kubakia sehemu za uso tu kwa mbali wakiwa wanashuhudia mpambano ambao ulikuwa unaendelea chini. Kujifunika kwao ni wazi ilionekana kwamba hawakutaka kabisa kuweza kujulikana na mtu yeyote kwamba walikuwa wapo ndani ya ukumbi huo.

“Huu ni moja kati ya uwekezaji bora sana ambao umewahi kuufanya mheshimiwa” aliongea mwanaume mmoja akiwa anashushia wine taratibu kwenye bilauri la thamani ambalo liliwekwa kwenye sinia la bati.

“Unajua uongozi ni dhamana ya muda mfupi sana ila wengi huwa hawaelewi, ndani ya huo muda mfupi ndio ambao unaweza kuamua hatima ya maisha yako ya baadae itakuwaje. Kuna watu wanataka sifa tu za kusifiwa halafu mwisho wa siku wanakuja kutia huruma lakini kuna watu ambao ni wapambanaji haswa wanaamua kuziweka sifa pembeni na kuamua kuwekeza sana kwa ajili ya baadae yao na mimi ndicho nilicho kifanya. Nilikuwa mwenye furaha sana mbele ya kila mtu kitu ambacho kilifanya nipendwe sana na wananchi lakini sikuwa mjinga nilijua kuna siku nitatoka ofisini hivyo nikaanza kutengeneza mazingira ya uwekezaji kila kona ya nchi na kila kona ya dunia ili nikitoka ofisini nianze kuyaishi maisha bila wasiwasi na sasa tupo hapa leo mnajionea moja kati ya sehemu ambayo nimewekeza licha ya kutupa burudani lakini pia inatuingizia mabilioni ya fedha kwa siku moja tu pekee” mheshimiwa huyo ambaye alikuwa amekaa katikati yao aliongea kwa majivuno kweli kweli huku mbali kidogo na walipokuwa wamekaa wakiwa wamesimama wanaume ambao walikuwa wanaonekana ni watu wa kazi haswa kulingana na namna miili yao ilivyokuwa.

“Mara ya kwanza wakati unanikalisha chini na kunipa mpango wa kuwekeza pesa zangu hapa, niliona kama ni wazo la kijinga sana ila kwa sasa nimekuja kuelewa kwamba ni kwanini ulichaguliwa kuwa kiongozi wa hii jumuiya yetu ya watu ambao tutatengeneza pesa ambazo vizazi vyetu vitaishi maisha ya kifahari sana mpaka miaka zaidi ya miamoja ijayo” mwanaume mwingine ambaye alikuwa mnene kuliko wote aliongea akiwa anacheka kwa furaha sana.

Hao ndio ambao walikuwa wamiliki wa eneo hilo, mwanaume ambaye alionekana kuwa kiongozi wa hiyo sehemu alikuwa anaitwa Denis Kijazo, huyu alikuwa raisi ambaye ndiye alikuwa ametoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Teodensia Mpanzi. Mwanaume kibonge alikuwa anajulikana kwa jina la Madilu Mpagazi, huyu alikuwa ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa sana ndani ya taifa la Tanzania na alikuwa mfanya biashara mkubwa sana.

Mwanaume ambaye alikuwa wa tatu ndani ya sehemu hiyo alikuwa anaitwa Msafiri Kigoti, huyu alikuwa ni gavana wa benki kuu ya taifa la Tanzania, ndiye alikuwa anakamilisha hesabu ya wanaume watatu ambao usiku huo walikuwa ndani ya ukumbi mkubwa wa ALEXIOS ARENA ambapo wao ndio walikuwa wawezekezaji wakuu ndani ya sehemu hiyo.

“Akili ni nguvu kubwa lakini nguvu ya kweli ni pesa, akili bila pesa ni upigaji wa kelele tu kama hautakuwa na mzigo wa kutosha kwenye mifuko yako hivyo kwangu huwa natumia vyote, akili na nguvu ya pesa ndiyo maana niliweza kuja na wazo kubwa sana kama hili kwa sababu najua nchi hii kuna mafisadi wengi sana ambao wana pesa nyingi mno na hawana cha kufanyia. Sasa tunawezaje kuzichukua pesa hizo kwenye mifuko yao bila wao kushtuka? Ndipo nikatengeneza huu mchezo ili waje kula maisha huku kwa pesa kubwa sana na zingerudi tena kwetu bila kugombana nao kwani wengi ni vijana wangu na wanafanya kazi chini yangu hivyo usingekuwa ustaarabu kama ningetumia nguvu kuchukua pesa ambazo niliwaahidi, nilitengeneza mfumo ambao watazirudisha kwangu bila wao kujua na kwa sababu wengi wao ni watu wa starehe sana imekuwa rahisi hata kuliko nilivyo tarajia” Denis Kijazo aliongea huku akishuhudia ulingoni mtu akitolewa koromeo na mwanaume mwenzake ambaye alikuwa anaihusudu zaidi pesa.

“Uko sahihi ila unahisi huyu raisi wa sasa ataruhusu hili liendelee? Kumbuka hauko ofisini na wewe ndiye ambaye ulikuwa unatulinda na kulinda kila mali zetu zisiguswe na mtu yeyote yule. Wewe ndiye ambaye ulikuwa unahakikisha hatulipi kabisa kodi na kuwaacha maskini waendelee kulumbana na kupigiana kelele huko, vipi una imani na huyu mama kwamba hatatuzingua kwa sasa na kuanza kuingilia kwenye hizi biashara zetu?” Madilu Mpagazi alionyesha wasiwasi wake moja kwa moja mbele ya mheshimiwa huyo huku akiwa hana imani sana na hali ambayo ilikuwepo wakati huo.

“Upo sahihi, hilo suala nililiwaza kwa ukaribu sana kabla hata ya kufanya haya maamuzi, ni jambo ambalo hata mimi liliniumiza sana kichwa maana lilikuwa limeshika hatima nzima ya maisha yangu ya baadae na kama ningekosea basi ingekuwa hatari sana kwangu. Huyu raisi ni kijana wangu mimi ambaye nimemuweka mwenyewe pale Ikulu baada ya kutokea mpasuko mkubwa sana ndani ya chama kuweza kubishana juu ya nani ambaye alikuwa anastahili kuingia Ikulu huku kila mtu akitaka mtu wake akae pale, hata mimi nilikuwa na mtu wangu mwingine ambaye nilikuwa nimemuandaa kuingia pale ila kulingana na ile hali nilifanya kumteua bibie na kumpa nafasi ya kuingia pale Ikulu ili kuweza kuhakikisha mambo yanakuwa sawa ionekane kwamba kila mtu amekosa na hapo ndipo watu wakatulia baada ya kuona hata mtu wangu kakosa”

“Nilifanya hayo yote ili kurudisha imani zao kwanza maana ingekuwa ni hatari sana kama mpasuko ule ungeendelea ndani ya chama tungekuja kuvuana nguo wenyewe na kuanza kuuana wenyewe. Lakini yule bibie ambaye nimemuweka pale Ikulu ni kijana wangu mtiifu wa muda mrefu sana ambaye amepikwa kwenye mikono yangu mwenyewe hivyo nina imani kwamba atatii kila kitu na kwa hali yoyote ile lazima atafanya ambacho mimi nakitaka. Vijana wangu ambao wameshindwa tutawaingiza kwenye baraza la mawaziri, kijana wangu ambaye alitakiwa kuwa raisi anatakiwa kuwa waziri mkuu au anaweza kuingia tu kama waziri wa kawaida lakini hata nyie watu wenu ambao mlikuwa mnataka wakasimamie maslahi yenu nafasi zao zipo na nimelizingatia hilo vyema kabisa na kwa sasa ninavyo ongea na nyie nimesha mtumia listi ya watu ambao wanatakiwa kuingia huko kwenye nafasi za juu na sehemu ambazo wanatakiwa kuwepo hivyo uaminifu wake wa kwanza unaanzia hapo. Anatakiwa kuwaweka watu ambao nawataka mimi kwahiyo nadhani hamna haja ya kuogopa kila kitu kipo ndani ya mpango”

“Yes, hilo ni jambo la mhimu sana kuweza kufanyika na nikupongeze kwa hilo ila kuna jambo moja huenda lisiwe sawa sana. Vipi kuhusu yeye kufuatiliwa kwa umakini, tujue anawaza nini, anawazaje, anamtumia nani kufanya maamuzi yake na nani na nani ambao ni waaminifu sana kwake kiasi kwamba kama kutakuwa na hali ya sintofahamu tuweze kuishughulikia haraka sana. Kwenye haya maisha hatupaswi kumuamini mwanadamu moja kwa moja kwani wanadamu wanabadilika sana, tunaweza kuja kushtuka wakati tumeshachelewa ikawa ni tatizo sana kwa upande wetu” Gavana wa benki kuu mheshimiwa Msafiri Kigoti alikuwa makini sana kuhakikisha maslahi yao yanalindwa ipasavyo ndiyo maana alitaka uhakika wa kila kitu.

Episode ya 3 leo naihitimisha hapa, panapo majaliwa tukutane ndani ya sehemu zinazo fuata.

Wasalaam,

Febiani Babuya.

Previoua Next