Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)

MTUNZI: FEBIANI BABUYA 

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

Episode 4

“Vijana wangu wote ni watiifu sana kwangu labda kama huyu ndiye atakuwa wa kwanza kuanza kwenda kinyume na mimi na kama akifanya hivyo basi nitamfanyia kitu kibaya sana ambacho hatasahau kwenye maisha yake yote. Nimeshampa maagizo mkurugenzi wa usalama kwamba anatakiwa haraka sana kuweza kuwatuma vijana wa kwenda kuongeza ulinzi huko na tayari amefanya hivyo kwa kuwapa vijana hao wawili kazi lakini hao ndio ambao wataifanya hiyo kazi ambayo wewe ulikuwa unaiongelea hapa saivi”

“Mmoja wa vijana hao anajua kazi ambayo anaenda kuifanya kule Ikulu ila mmoja hajui na huyo ambaye hajui amepewa nafasi ya kuripoti kila kitu kwa mkurugenzi hivyo tutakuwa tunapata taarifa sehemu zote mbili huku mmoja akiwa anatoa taarifa bila kujua kwamba zinatumika kwenye nini na mmoja atakuwa anafanya kazi akiwa anajua kile ambacho anatakiwa kukifanya. Ondoeni shaka kama ambavyo nimewaambia tangu mwanzo kwamba kila kitu kipo ndani ya mpango”

“Hakika wewe ni mtu mwenye maono ya mbali sana mheshimiwa”

“HILI NI JIJI LA KAMARI ndugu yangu, namna unavyojua kuicheza hiyo Kamari yako ndiyo ambavyo unajihakikishia nafasi ya kuwa mshindi na bingwa ndani ya eneo lako, hahahaha hahahah” mheshimiwa alicheka sana huku akiitoa simu yake na kuipiga moja kwa moja Ikulu ambapo ilifika kwa mheshimiwa raisi moja kwa moja.

“Hongera sana kwa ushindi wako, kuna kijana anakuja na bahasha hapo ipitie vizuri kisha ufanye kama bahasha inavyo jieleza. Ni matumaini yangu utanifanya nijivunie sana uwepo wako, uwe na bahati njema” ni maelezo mafupi sana ambayo alikuwa amempatia mheshimiwa raisi Teodensia Mpanzi kisha akaikata simu yake bila kusubiri salamu wala jibu kutoka kwa mtu ambaye alikuwa amempigia simu. Wanaume hao watatu wote walinyanyuka na kupeana mikono kisha wakaanza kutoka ndani ya jengo hilo kubwa sana wakiwa na ulinzi mkali isivyokuwa kawaida kwani haikutakiwa mtu yeyote ajue kwamba ni akina nani ambao walikuwa hapo. Hawakuwa watu ambao walikuwa wanajulikana kwamba ndio walikuwa wamiliki halali wa eneo hilo, baada ya kufika kwenye lango kuu la kuingilia hapo ndani mwanaume ambaye alifungua geti la chuma ambalo lilikuwa hapo aliinama kutoa heshima huku kwenye mkono wake akiwa na shoka kubwa sana ambalo lilikuwa na cheni ndefu ambayo iliunganishwa mpaka kwenye surali yake ambayo ilikuwa mwilini huku usoni kwake akiwa na alama kubwa sana ya kovu ambayo bila shaka alikuwa amekatwa vibaya sana siku za huko nyuma.

Simu hiyo kutoka kwa mheshimiwa Denis Kijazo ilimkuta raisi Teodensia Mpanzi ndani ya chumba chake cha kulala usiku huo. Alichukizwa sana na kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kwani ilikuwa ni kama kukosewa heshima kwa kiasi kikubwa sana, mtu ambaye alimpigia simu wakati huo hakumpa hata nafasi ya kujibu, alitoa tu maagizo na kuikata simu hiyo kuonyesha kwamba alikuwa anatoa amri na sio ombi.

Hali hiyo ilimfanya raisi achukie sana, alivaa nguo zake haraka sana na kutoka usiku huo huo kwenda ofisini kwake ambako alimkuta kijana anamsubiri akiwa na bahasha mkononi mwake.

“Nani amekupa ruhusa ya kuweza kuingia kwenye hii ofisi?” alimuuliza kijana huyo ambaye alikuwa ameingia mpaka ndani ya ofisi hiyo ambayo hakuna mtu alikuwa anatakiwa kuingia bila ruhusa yake.

“Samahani mheshimiwa mimi nimegizwa hapa nilete hii bahasha na nimeambiwa nisipokukuta niingie moja kwa moja mpaka humu ndani kukusubiri”

“Kuanzia leo hii usije ukaonekana tena maeneo ya hapa Ikulu, hauna kazi tena ya kufanya hapa hivyo utoweke haraka sana na nitampa taarifa kiongozi wako ya kukufuta kazi, huwezi ukawa unaikosea heshima ofisi kubwa ya nchi unaingia kama kwako”

“Lakini mheshim…….”

“Toka humu ndani nisije nikakupiga risasi bure hapa mpuuzi wewe” mheshimiwa alikuwa na hasira kali sana wakati huo kwani aliona kama huyo mtangulizi wake na watu wake walikuwa wanamkosea heshima pakubwa sana. Baada ya kijana huyo kutoka alihema kwa nguvu na kutulia akiwa anaangaza kila sehemu humo ndani, kuna kifaa ambacho alikitoa kwenye mfuko wake wa koti na kukiwasha kikawa kinapiga alamu kuelekea kwenye sofa moja ambayo ilikuwa jirani na alipokuwa amesimama.

Alizamisha mkono wake pembezoni mwa sofa hiyo ndipo alipokutana na kifaa cha kunasa sauti, ina maana kijana huyo alikuwa amewahi hapo na kutegesha hicho kifaa ili kila ambacho raisi atakuwa anakizungumza au kuwasiliana na mtu kwa njia ya simu waweze kukipata haraka sana. Alikikanyaga chini na kukipasua huku akicheka kwa nguvu ila kwa hasira mno, aliinyanyua simu yake na kuipiga kwa walinzi wa nje ambapo alitoa taarifa kwamba kijana huyo ambaye alikuwa ametoka hapo alitakiwa kuwekwa chini ya ulinzi haraka sana na usiku huo hakuna mtu ambaye alitakiwa kutoka au kuingia ndani ya hilo eneo mpaka ambapo angetoa amri nyingine ya kipi ambacho kilikuwa kinatakiwa kufuatia.

“Huyu atakuwa wa mfano kutuma ujumbe kwao kwamba huenda wanacheza na mtu ambaye hawatakiwi kabisa kumchezea kijinga au kumgusa kwa lolote lile” aliongea akiwa anafoka pekeyake ndani ya ofisi hiyo na kusogea taratibu pale mezani ambapo kijana yule alikuwa ameiweka ile bahasha ambayo alikuwa ameambiwa kwamba alitakiwa kuifanyia kazi na kama maelezo yalivyokuwa yanajieleza ndani yake.

Baada ya kuifungua ila bahasha alishangazwa mno na jambo ambalo lilikuwa ndani yake, ilikuwa ni orodha ya majina na nafasi mbali mbali ambazo watu wa majina hayo walitakiwa kuteuliwa, alipigwa na butwa baada ya kuona yeye kama raisi anapangiwa kwamba nani na nani wanatakiwa kuteuliwa na wapi ambao wanatakiwa kutenguliwa. Alitabasamu akiwa na hasira sana na kwenda kuichoma orodha hiyo ambayo alipewa kisha akafungua droo yake baada ya kuingiza namba za siri ambazo alikuwa ameziweka, akaitoa bahasha ambayo alikuwa ameiandaa yeye.

“Hii ndiyo serikali ambayo naenda kuwa nayo mimi na hawa ndio watu ambao naenda kufanya nao kazi mimi ila sio watu wa kupangiwa. Kuna kosa moja kubwa sana umelifanya mheshimiwa kuhisi kwamba mimi unaweza kuniendesha unavyotaka na mimi naweza kukaa hapa nikafanya kazi zako eti kwa sababu tu wewe ndiye ambaye umenifanya nimekuwa hapa. Nimekuwa mtiifu miaka yote hii na kujifanya mjinga ila kiuhalisia mimi sio mjinga, mimi sio mtu ambaye unaweza kunifanyia kile ambacho wewe unakihitaji na kuamua kadri unavyo taka wewe”

“Mimi ndiye raisi wa nchi hii, mimi ndiye bosi wa taifa, mimi ndiye mtu mkubwa zaidi na mwenye nguvu zaidi ndani ya nchi hii, sasa wewe ni nani hasa mpaka uhisi kwamba unaenda kunipangia cha kufanya? Kama kuna kosa kubwa ambalo umelifanya kwenye maisha yako basi ni kunipa mimi hii nafasi ya kuwa raisi, nakuhakikishia wewe na mafisadi wenzako nitawanyoosha na mtajuta sana kuzaliwa kwenye taifa hili” alitamka kwa hasira akiwa anapigiza kwenye meza wakati huo alikuwa anaongea mwenyewe ndani ya ofisi yake hiyo.

Alikuwa anaongea na nafsi yake ila aliamini kwamba nafsi yake ilikuwa inaongea na huyo kiongozi ambaye alihisi kwamba anaweza kufanya jambo lolote lile ambalo yeye alikuwa anahitaji kulifanya. Aliinuka muda huo huo wa usiku na kumpigia simu msemaji mkuu wa serikali pamoja na watu wake watoe taarifa kwa vyombo vya habari kwamba ndani ya nusu saa ijayo mheshimiwa raisi alikuwa anatoa mkeka wa baraza la mawaziri ambao angeenda kufanya nao kazi na siku ya kesho yake angefanya mabadiliko mengine makubwa sana ndani ya maeneo mbali mbali ya kiutendaji.

“Hawa wajinga natakiwa kuwatoa watu wao wote kwenye mfumo kisha niwaweke watu ambao hawajulikani sana ambao nina imani wanaweza kunisikiliza na kunitii na hili litakuwa jambo kubwa sana kwangu kwa maana nitakuwa na watu wengi sana wa kunilinda lakini pia natakiwa kutengeneza timu yangu mwenyewe ambayo itakuwa na watu watakao yapigania maisha yangu kwa namna yoyote ile maana hawa mafedhuli hawataniacha kama nikicheza vibaya. Kitu cha kwanza natakiwa kuwafanya waanze kuniogopa kwanza na natakiwa kuonyesha mfano kwa hawa mafisadi ambao listi yao yote ninayo” baada ya kumaliza kujishauri tena mwenyewe, mheshimiwa aliishika bahasha yake na kutoka nje ya ofisi yake ambapo palikuwa na ulinzi mkali sana akawa anaelekea kwenye ukumbi wa mikutano ya Ikulu ili kwenda kutoa hiyo taarifa na mkeka wa watu ambao wangeenda kuwa mawaziri chini ya utawala wake.

Hiyo ni taarifa ambayo ilimshtua kila mtu hususani wale ambao huwa wanapenda sana kuitumia mitandao ya kijamii. Walishangazwa na tukio hilo kwani walizoea mambo hayo kuweza kuyaona mchana hivyo walishangaa sana kuona yanafanyika usiku tena usiku sana, ila hayo hayakuzuia mheshimiwa kuweza kutekeleza kile ambacho alikuwa amekikusudia kukifanya usiku huo.

Mheshimiwa raisi Teodensia Mpanzi alitoa listi nzima ya majina ya mawaziri kila mtu na wizara yake ambayo alikuwa amepangiwa. Listi hiyo nzima ilikuwa ya kushangaza kwani watu ambao waliteuliwa hapo hawakuwa watu ambao walikuwa na majina makubwa kabisa serikalini na kwa wale ambao walikuwa na majina makubwa walikuwa ni wachache sana hususani wale ambao walikuwa wanayapigania sana maslahi ya nchi na wengine akiwa amewatoa vyama vya upinzani jambo ambalo lilizua taharuki kubwa sana ila kwa bahati mbaya sana yeye ndiye ambaye alikuwa ni mwamuzi wa mwisho juu ya kila kitu.

Uteuzi huo ulimshtua zaidi raisi ambaye alikuwa ametoka madarakani Denis Kijazo, ni usiku huo huo alitoka kujinasibu kwa wenzake kwamba huyo alikuwa ni kijana wake na hakuwa na jambo lolote la kufanya mbele yake zaidi ya kutii kile ambacho alikuwa anakitaka yeye mwenyewe lakini kilichofanyika, kilikuwa nje kabisa na matarajio yake na mpaka wakati huo hakuwa akiamini kile ambacho kilikuwa kinaendelea.

Aliipasua kwa kuipiga risasi runinga ambayo ndiyo ilikuwa inatumika kuangalizia taarifa hiyo, baada ya kumaliza kuisikiliza orodha hiyo, alikuwa mtu mwenye hasira sana kiasi kwamba hata mdomo wake ulikuwa unacheza cheza huku akiwa anatabasamu. Kijana wake alikuwa ameenda kinyume na matarajio yake na maagizo yake kiufupi ni kwamba alikuwa amemsaliti tena vibaya sana kitu ambacho hakuwahi kukitegemea kwamba kinaweza kutokea kwani alimlea na kumtengeneza yeye mwenyewe hivyo aliamini kwamba angekuwa mtiifu mkubwa sana kwake.

“Huyu mshenzi nadhani bado hajanifahamu vizuri, hajui kwamba mimi ndiye mmiliki wa hii nchi, hajui kwamba kila kitu kwenye hii nchi kipo kwenye mkono wangu, hajui kwamba kila mtu ndani ya taifa hili ananitii mimi. Bado hajazaliwa binadamu wa kutaka kuweka ligi na mimi tena kijana ambaye nimempika kwa mkono wangu mwenyewe? Hilo kosa ambalo analifanya atalilipa kwa gharama kubwa sana ambayo itayafanya maisha yake yawe mafupi kuliko hata alivyokuwa ametarajia” aliongea bastola yake ikiwa kwenye mkono wake, aliitoa simu na kuitafuta namba ya raisi huyo kisha akapiga.

Ilimkutia raisi akiwa ndani ya ofisi yake baada ya kutoka kutoa orodha ya baraza jipya la mawaziri ambalo angefanya nalo kazi mpaka pale ambapo angeona kwamba kulikuwa kuna ulazima wa kuweza kulibadilisha tena, aliiangalia simu hiyo ambayo iliita mpaka ikakata, ilianza kuita tena, aliliweka koo lake sawa kisha akaipokea.

“Unataka vita na mimi?” ilikuwa ni sauti kutoka upande wa pili, sauti ambayo ilikuwa nzito lakini ya upole tena yenye utulivu mkubwa sana ndani yake.

“Unaongea ukiwa kama nani?” mheshimiwa raisi aliuliza kwa ujasiri ambao ulikuwa na majivuno ndani yake, upande wa pili ulikuwa kimya kwa muda kwanza kusikilizia kile ambacho kilikuwa kinatokea ikionyesha wazi mtu huyo wa upande wa pili hakuwa akiamini kile ambacho kilikuwa kinaendelea.

“Ushakuwa mkubwa sio?”

Episode 4 inafika mwisho tukutane sehemu inayo fuata.

Tchao.

Previoua Next