Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

STORY:

UKURASA WA PILI

Baada ya mgonjwa kuweza kutoweka kwenye moja ya hospitali huko ndani ya jiji la Arusha ambako alikuwa amepelekwa ili kuweza kupata matibabu hatukuweza kujua kwamba alikuwa ameelekea wapi na hali yake ilikuwaje kwa sababu kwa mara ya mwisho alionekana kabisa akiwa amezimia na hali yake ilikuwa mbaya sana kiasi kwamba alikuwa amepoteza fahamu.

 

Moja ya basi bora kabisa ambalo lilitoka Arusha majira ya asubuhi na mapema sana na sasa majira ya saa mbili za usiku lilikuwa linaingia ndani ya jiji pendwa zaidi nchini jiji la Dar es salaam, lilifika stendi walianza kushuka abiria mbali mbali ambapo kuna mwanaume mmoja ambaye alikuwa na begi lake mgongoni pamoja na kofia ambayo ilikuwa imeuziba uso wake vizuri alikuwa amekaa konani kabisa kwenye siti ya mwisho alibaki amekaa humo ndani mpaka pale alipo hakikisha kwamba watu wote wametoka ndipo naye alipo amua kutoka huku akiwa anaificha sana sura yake ni wazi hakuhitaji mtu yeyote yule aweze kumuona sura yake na alikuwa makini sana kwa kila hatua yake moja ambayo alikuwa anaipiga.

 

Alishuka kwenye gari na kuchukua usafiri wa bajaji akiwa makini sana kuulinda uso wake kwa kofia ambayo alikuwa ameivaa usoni kwake, bajaji hiyo ilimfiksha mpaka maeneo ya usalama ambapo aliomba usafiri huo uweze kumuacha huko mbele angeendelea mwenyewe na safari yake, mwanaume alishuka na kuanza kuikata mitaa ya jiji majira ya usiku wa mapema huo lakini alihisi kama kuna watu walikuwa wakimfuatilia kwa muda kidogo tangu pale alipoweza kushuka kwenye ile bajaji, aliigusa kofia yake kidogo na kutabasamu kisha akawa anaendelea na safari yake kama ilivyokuwa kawaida yake. Hatua kama saba alizozipiga alipotea kwenye hilo eneo ambalo alikuwa anaonekana yupo haukupita muda sana wakatokezea wanaume watatu waliangaza huku na huko walishangaa kutomuona mtu yeyote yule ilikuwa ni ghafla sio muda sana waliona kabisa kuna mtu hilo eneo.

 

“Kama ikitokea siku ukiwa karibu na huyo mtu ni kiumbe cha ajabu sana kinapokuwa kwenye uhalisia wake unapaswa kujihadhari kwa namna yoyote ile ambayo unaweza ili kuhakikisha maisha yako yanakuwa salama kama ukichezea hata sekunde moja tu ukafanya uzembe wowote basi jiandae kubadilishiwa jina lako halisi na kuitwa marehemu” ni kauli ambayo mmoja wa hao wanaume aliikumbuka vizuri siku moja wakati anapewa onyo na kiongozi wake na alionekana kuwa mkuu wa msafara huo wa watu watatu ambao walikuwa hapo usiku huo jiji likiwa limetulia mubashara.

 

“Jiangalieni na muwe makini hayupo mbali na hapa” aliongea ikiwa ni kuwatahadhalisha wenzake alionekana kumjua huyo mtu kwa uchache wake, bahati mbaya ni kama taarifa hiyo alichelewa sana kuitoa mmoja kati yao alikuwa anaenda chini akiwa amelainika kama tambi zilizopikwa, walimkimbilia na kumgusa walipigwa na butwaa uti wa mgongo wa mwenzao ulikuwa umevunjwa hauwezi hata kufanya kazi tena alikuwa ameshaanza kuwa wa baridi maana yake dunia hayakuwa makao yake tena.

 

“Vipi mnanitafuta mimi” mshtuko walioupata kwa kusikia sauti la kutisha ni kama walikuwa ndotoni, ni sauti iliyoshiba ambayo ilisikika kutoka kwa mtu ambaye alikuwa yupo nyuma yao.

 

“Mpige risasi kwenye mbavu haraka” aliyekuwa anapewa maagizo ya kupiga risasi huyo binadamu mwenzao utoaji wa risasi kwenye bastola yake ulikuwa mdogo sana kiasi kwamba ilimpelekea yeye kupiga magoti akiwa amejishika eneo la shingoni, yule mwanaume ambaye ndiye aliyekuwa anatafutwa alionekana kuwa na pete kwenye mkono wake iliyotumika kufanyia hayo mauaji japo haikueleweka pete imeweza vipi kuichana chana shingo ya mtu mpaka akadondoka na kupoteza maisha kwa sekunde kadhaa tu.

 

“Nenda kamwambie huyo aliyewatuma kwangu aje anitafute yeye mwenyewe”ni kauli moja tu ambayo aliweza kuitamka kwa mwanaume mmoja tu ambaye alikuwa amesalia na kuachwa hai kati ya hao watatu ambao walikuwa wapo hilo eneo, alibaki akitetemeka mno aliyo yashuhudia kwa wenzake kwa hizo sekunde chache kwenye mwili wake yalimfanya kuelewa nini maana ya hofu. Alimshuhudia mwanaume huyo akiondoka na kupotelea ambako alikujua yeye mwenyewe na hakuwa na cha kuweza kumfanya chochote kile, alijipapasa kwenye mwili wake baada ya kujigundua kwamba alikuwa ni mzima wa afya aliitupa bastola yake chini na kuanza kukimbia kwa nguvu sana hakuweza kuamini kama kweli aliweza kuachwa akiwa hai na mzima wa afya ya kutosha alishukuru MUNGU kwa hilo hakujua aina ya mtu ambaye alikuwa anamhangaikia usiku huo ni bora angebaki hata kuuza miguu ya kuku na kashata huko Tandika hii michezo ya wanaume alikuwa haiwezi.

 

 

Siku zilikatika, wiki ziliishaa, miezi ilienda na miaka ilikuwa inakimbia kwa kasi kubwa kama ilivyo kawaida kwa muda haujawahi kusimama hata siku moja kila siku huwa unakimbia kwa kasi, miaka mitano ilikuwa imepita tangu matukio yote hayo yaweze kutokea ndani ya Arusha na Dar es salaam. Kwenye moja ya Apartment kubwa ya kifahari alionekana bwana mmoja akiwa amesimama eneo la dirishani akiwa anaangalia nje kupitia kioo kikubwa kilichokuwa hapo akiwa anashuhudia kwa namna mji ulivyokuwa unavutia majira hayo ya usiku ulio tulia. Alionekana kuwa mtu ambaye mawazo yake yalikuwa yanakumbuka mbali sana, aligeuka na kuangalia upande wa pili ambako kulikuwa na mlimbwende kama sio mrembo kwa lugha ambayo ni rahisi zaidi, mwanamke ambaye tungesema ni sumaku kwa namna muumba alivyo tulia na kuvigawa viungo ambavyo viliufanya mwili wake kuwa sehemu ya kiburudisho cha macho kwa kila ambaye alikuwa ana uwezo wa kuona basi asingeweza kupita akakosa kuisaliti nafsi yake kwa kugeuza shingo yake na kumshuhudia huyo mwanamke jinsi alivyokuwa mzuri wa haja na alipendelewa uzuri wa kipekee ambao kwa hadithi ya neno moja moja ilitakiwa ramani nzima ya Afrika kuweza kumaliza kilomita za kumuelezea namna alivyokuwa ni mwanamke mzuri sana, sifa kubwa zilienda kwa MUNGU kwa uumbaji wake kiufupi ni kwamba MUNGU fundi sana.

 

Mwanamke huyo alikuwa kwenye tabasamu zito lililo mfanya meno yake ambayo yalikuwa ni meupe kwa asilimia mia moja na nukta zake yaonekane vizuri sana lakini hilo halikuwa tu la kumfanya atabasamu sana hivyo lahasha bali kiumbe kilichokuwa karibu yake ndipo lilipokuwa tabasamu lake kubwa, alikuwa akicheza na binti mdogo wa kike ambaye usingesita kusema alikuwa ana miaka miwili mpaka mitatu pale unapo muona, kama yeye alivyokuwa amependelewa kuwa mzuri basi hata yeye alimshukuru MUNGU kumpendelea mtoto mzuri kama huyo aliye mpata, aliye mfanya mpaka yeye mwenyewe asadiki kwamba hii dunia kuna watu wanabarikiwa kuwa wazuri akijisahau kwamba yeye ndiye mama wa huyo mtoto (hahahahha binadamu hawaridhiki kabisa bwana). Ilionekana kuwa moja ya familia iliyokuwa na furaha kubwa mno, hao wawili ndio ulikuwa moyo wa huyo mwanaume ambaye alikuwa pembezoni kabisa mwa dirisha kubwa la vioo akiwa anamuangalia mkewe na mwanae wa pekee wakiwa kwenye furaha kubwa mno na hilo ndilo lengo la kila baba bora kwa familia yake ni bora yeye alale njaa lakini sio kuona familia yake inalia au kutoa chozi (he was a good father indeed).

 

Hapo alipokuwa amesimama alikuwa anaongea na nafsi yake mwenyewe akiwa anajikumbushia namna alivyo mpata huyo mwanamke na aliweza vipi kukutana naye mpaka ikafikia hatua akawa mke wake kabisa wa ndoa. “Ilikuwa ni siku moja nikiwa nimetoka kwenye mishe mishe zangu za kila siku, kuvaa na kupendeza kila siku ilikuwa sehemu ya maisha yangu, nilibahatika kuwa miongoni mwa wale vijana waenda gym basi hata mwili wangu ulikaa vyema sana sikuwa na tatizo la kimwonekano. Ni usiku mmoja nilikuwa nimeenda na gari yangu kwenye hoteli moja japo nilikuwa makini sana kuulinda uso wangu usije ukapatikana kwenye kamera hata moja na mara nyingi nilikuwa ninatembea na barakoa pale ambapo naingia sehemu ambayo inaweza kuwa tatizo kwangu kuonyesha sura yangu.

 

Nilijibanza kwenye kona moja ambapo nilipata kinywaji changu ila kwa bahati mbaya sana nilijikuta sina waleti yangu ambayo ilikuwa na pesa nilihisi nimeibiwa ila nikakumbuka nitakuwa nimeidondoshea kwenye gari yangu, mhudumu alinijia juu na kusema kwamba mimi nilikuw atapeli na nisingeweza kutoka kwenda kwenye gari bila kulipia vinginevyo ilitakiwa nikamatwe kama ningeshindwa kulipa kitu ambacho kingenifanya nijulikane haraka na sikutaka hilo lifanyike lakini kwa bahati iliyokuwa njema pembeni yangu alikaa mwanamke mmoja mzuri sana tena sana ambaye nisingeweza kumuelezea nikamaliza nilishangaa ananilipia na kutabasamu hahhhaaa kilicho fuata ilibaki kuwa historia” alitabasamu sana baada ya hisia zake kumkumbusha namna alivyoweza kukutana na mwanamke huyo japo hakutaka hisia zake ziweze kuendelea kwa muda huo ili kuweza kujua kwamba ilikuaje mpaka akafikia hatua kabisa ya kumuweka ndani, alimshukuru sana MUNGU kumpendelea familia yenye furaha sana.

 

“MUNGU ni mkubwa sana sasa hivi hata mimi naishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine” alitabasamu baada ya kuweza kuyatamka hayo maneno yake kisha akazamisha mkono wake mfukoni na kuitoa simu akaanza kuhangaika kuitafuta namba moja ambayo kwa muda huo ilionekana kuwa ya mhimu, baada ya kuipata alipiga ikaite kwa sekunde kadhaa tu kisha ikapokelewa.

 

“Halo”ni sauti kutoka upande wa pili uliokuwa umepokea simu bila shaka ilitoka kwa moja ya watu waliokuwa na njaa kali sana ndiyo sababu alikuwa tayari kuipokea simu kwa wepesi akihisi huenda ni ya chochote kitu cha kuliweka tumbo lake sawa.

 

“Kani uko wapi saivi?”

 

“Nani wewe?” sauti ya upande wa pili iliuliza kwa msisitizo mzito

 

“Alen”

 

“Whaaaaaaat?”

 

“Yes, uko wapi?”

 

“Mimi bado nipo Arusha ndugu yangu umeniharibia maisha yangu yote kwa ajili yako nilifungwa jela na kufukuzwa ka……”

 

“Kesho nahitaji uwepo Dar es salaam”

 

“Kufanya nini?”

 

“Acha jeuri kama umeyapatia maisha mjinga wewe wakati una shida kibao” upande wa pili mtu huyo alimeza mate kwani alikuwa ameambiwa ukweli kabisa wa maisha yake.

 

“Daaaah kaka sema sina nauli”

 

“Nakutumia, utanitafuta ukifika stendi” Baada ya simu kukatwa iliingia meseji ambayo huwa inabeba zaidi ya asilimia 99 ya furaha ya binadamu mwenye shida, shilingi laki tano ilikuwa imethibitishwa kwenye laini yake hiyo, hakuamini hicho kitu ndani ya chumba chake kidogo ambacho alikuwa ametandika godoro chini akiwa hajatia chochote tumboni alimshukuru MUNGU kwa hilo alinyanyuka na kukimbilia kwa wakala kabla mwenye pesa hajairudisha kwake, alienda kutoa pesa yote akiwa anacheka cheka njia nzima. Alienda kwenye moja ya migahawa bora sana akaagiza chakula cha bei kubwa akiwa anafidia siku alizo teseka, alikula akashiba vizuri baada ya hapo alienda club na kuchukua mwanamke mmoja mrembo sana akawa anakunywa pombe baadae aliingia naye chumbani kupunguza uzito aliokuwa nao ikiwa ni kama kulipiza kwa namna wanawake wazuri walivyokuwa wanamkataa kwa sababu hakuwa na pesa kwenye maisha yake yote basi alijisikia fahari sana siku hiyo. Asubuhi na mapema sana alikuwa ndani ya gari akiwa anaelekea zake kwenye moja ya jiji ambalo kwake ilikuwa ni ndoto kwenda kuliishi.

 

 

Huyu mwanadamu ambaye alionekana kuwa kiumbe cha hatari sana ni nani hasa?, kipi kimemfanya atafutwe sana namna hiyo? Tuna mengi sana ya kuyajua na kuyaelewa humu ndani kikubwa twende taratibu tutaelewana tu……. sehemu ya pili haina cha kukuongezea kwa sasa mpaka wakati ujao.

 

Bux the story teller

 

Chao

Previoua Next