Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

ENDELEA..........

 

Kani kwa mara ya kwanza alikuwa anashuka ndani ya jiji la Dar es salaam ambalo kwake lilikuwa ni geni mno hakuwahi kufika zaidi ya kusikia tu watu wakiwa wanalinakshi kwa uzuri wake wa kuvutia na umaridadi wa maisha ambayo watu waliomo ndani yake huwa wanayaishi kila siku, majira ya jioni wakati kiza kinaanza kuingia taratibu ndio muda ambao alikuwa anashuka stendi. Namba alikuwa nayo kwenye simu yake aliitoa kwenye mfuko wake kwa umakini sana na kuweza kuipiga iliita kwa mara ya kwanza na kukata, ikaitwa kwa mara ya pili kwa muda mrefu ndipo ilipoweza kupokelewa.

 

“Vuka hiyo lami kwa mbele utaona kuna gari nyeusi ingia humo” maelekezo aliyo yapata ilionekana mtu ambaye alikuwa akimuelekeza alikuwa anamuona moja kwa moja bila wasiwasi wowote ule basi alivuka na kweli hatua kama hamsini kutoka sehemu aliyokuwepo aliona kuna gari moja zuri sana la kifahari mno alisita kwenda ila aliamua kuufuata moyo wake na maamuzi yake, hatua mbili kabla hajafika mlango ulifunguliwa kana kwamba alikuwa akisubiriwa kwa muda mrefu kisha akaingia ndani ya gari. Ndani ya hiyo gari alikuwa amekaa mwanaume mmoja mwenye ndevu ambazo bila shaka zilichongoka na kukaa kwa usahihi kwa matunzo ambayo yalionekana kufanyika kwenye hizo ndevu, mustachi uliipamba sana sehemu ya juu kidogo ya mdomo wake na kuonekana kama alikuwa mhindi flani hivi, Kani ilimchukua kama dakika mbili kuweza kumtambua vizuri mtu ambaye alikuwa mbele yake alikuwa amebadilika mno na wala hakutegemea kama ndiye yule rafiki yake wa miaka mitano huko nyuma ilihitaji umakini wa hali ya juu na kwa mtu ambaye anamjua kiundani sana kuweza kumtambua kwamba ndiye alikuwa yeye mwenyewe.

 

Alen ndiye mwanaume aliyekuwa ndani ya gari hiyo ya kifahari walikumbatiana kwa furaha sana huku Kani machozi yakiwa yanamtoka kwa miaka mitano ambayo ilikuwa imepita alipitia mambo magumu sana ambayo yalimpelekea mpaka kuipoteza kazi yake.

 

“Ulikuwa wapi miaka yote hiyo ndugu yangu” Kani aliuliza akiwa anashangaa namna gari hiyo ilivyokuwa ya kifahari mno na hakuwahi hata siku moja kupanda wala kufikiria kama atakuja siku moja kuwa sehemu ya maisha hayo ya kifahari na kuyaishi kwenye uhalisia wake.

 

“Namba zinasoma kwa kasi kubwa sana ndugu yangu na miaka inazidi kukatika tu lakini wanadamu bado tupo, hilo ni swali ambalo nitakujibu siku nikipata muda ila kwa sasa nilihitaji kukusaidia ujitoe kwenye hiyo hali ya maisha ambayo ulikuwa nayo kwa muda mrefu sana nina imani umepitia shida za kutosha kwa sababu yangu mimi na hilo ndilo limenisukuma sana kuweza kulipa fadhila kwa wema wako ambao siwezi kuusahau kwa namna ulivyo nisaidia wakatii ule hakukuwa na mtu yeyote yule ambaye angeweza kusimama na kunikumbuka, kwa sasa twende sehemu ambayo ndiyo utafikia na utakuwa unakaa halafu kesho nitakupeleka sehemu ukafanye manunuzi ya nguo kidogo uanze kuendana na kasi ya mji” maneno hayo ya Alen Kani hata hakuwa anayasikia vizuri mawazo yake yalikuwa yapo mbali sana kushangaa namna mtu ambaye alikuwa naye kwenye machimbo ya madini miaka kadhaa nyuma leo alikuwa anaongea akiwa siriasi sana maisha yalikuwa yamebadilika mno kwa kiasi kikubwa.

 

 

“Ahhhh…. sawa” alijibu kwa kigugumizi, Alen alitabasamu tu kuona hiyo hali alimjua mwenzake huyo kwa ushamba hususani anapofika sehemu ambayo anakuwa haijui kabisa au ni ngeni kwenye maisha yake, alinyanyua gia na kuanza kutoka kwenye hilo eneo kwa spidi ya kawaida ikionekana wazi hakuhitaji kumuumiza mgeni wake.

 

“Hivi kaka wewe wazazi wako na asili yako kabisa huwa ni wapi?” ni swali ambalo lilionekana kumshtua sana Alen baada ya kuulizwa na Kani walionekana kuwa watu ambao walikutana na kusaidiana tu ila walikuwa hawajuani kiundani sana.

 

“Sikumbuki sana nilikuwa mdogo mno ila ninacho kijua mimi wakati naanza kujitambua nilijikuta naishi kwenye kituo cha watoto yatima mpaka pale nilipo ona kwamba nina uwezo wa kujitegemea nikaamua kuondoka hiyo sehemu nadhani hata siku ya kwanza niliwahi kukwambia hivyo” Alen alijibu lakini ni wazi hakupendezwa kabisa na hilo swali ilimbidi kufungua muziki taratibu kwenye gari akiwasha skrini ndogo ambayo iliuchukua umakini wa Kani wote na maswali yakawa yameishia hapo. Nusu saa ilipita waliingia Sinza kwenye mjengo ambao haukuwa mkubwa saana ila ulikamilika kwa mtu kuweza kujiita ana maisha mazuri ya kuvutia, mlango ulifunguliwa wakaingiza gari ndani kisha wakafunga geti, muda wote Kani macho hayakubanduka kwenye skrini ambayo ilikuwa ipo mbele ya gari mpaka pale alipokuja kushtuliwa na Alen kwamba walikuwa wamefika mwisho wa safari yao ndipo alipoweza kushuka ndani ya gari wakaongozana mpaka ndani ya nyumba.

 

“Kani kuanzia leo hapa ni kwako na ndipo utakapokuwa unaishi kwa sasa, yale magari mawili ambayo umeyaona pale nje ni yako yote ila kuhusu wafanyakazi utaamua wewe kama utawaleta au la itakuwa ni juu yako mwenyewe” Kani aligeuka kutoka kwenye mshangao aliokuwa nao wa kushangaa vitu vya thamani vilivyokuwepo ndani ya sebule hiyo na kumwangalia Alen kwa taharuki, hakuwa anaamini kwamba hivyo vitu humo ndani vilikuwa ni mali yake yeye na alikuwa anaruhusiwa kuvitumia kadri atakavyo, alijikuta analegea na kupiga magoti chini akiwa anatoa machozi huyo mwanaume mbele yake hakuwa ndugu, kaka wa kuzaliwa wala hawakutoka sehemu moja ya kuzaliwa ila leo ndiye aliyekuwa kama ndugu yake ndani ya jiji hili, ni binadamu wachache sana huwa wana moyo wa aina hiyo. Alen alimfuata rafiki yake huyo wa machimbo akamnyanyua na kumkumbatia.

 

“Kama ningekuwa na uwezo ningeurudisha muda nyuma uzaliwe wakwanza kwenye familia yetu kisha nifuate mimi nikuite kaka wa damu kabisa tumbo moja nadhani ningekuwa mwanadamu ambaye ningekuwa nina bahati kuliko binadamu yeyote yule hapa duniani, asante sana kaka” Kani aliongea kwa kumaanisha macho yake yalitoa ishara za msisitizo kuhusu hilo jambo wakati huo alikuwa amekumbatia sofa moja maridadi sana ambalo lilipita kwenye mkono bora wa fundi seremala.

 

“Hahahahahah Kani bado hujaachaga masiara yako, hivi ni vitu vidogo tu usijali, wewe ndiye binadamu pekee uliuona umuhimu wangu wakati ule mimi ni kapuku sina hata mia mbovu, ukanipeleka mpaka kazini kwako na kunisaidia sana sehemu ya kulala kwahiyo haya ninayo yafanya wewe ndiye unastahili pongezi kwani huenda kama sio wewe mimi leo nisingekuwa hapa” Alen aliongea kwa kumaanisha mashavu ya Kani yalituna kwa cheko kisha akakaa chini akiwa ana furaha sana, kilicho fuata alionyeshwa mazingira yote ya nyumba na namna ya kutumia vitu mbali mbali humo ndani, vyakula vilikuwa vipo vya kutosha kwenye friji alikula sana baada ya Alen kuondoka na kuahidi kwamba angekuja kesho yake kumchukua akabadilike kuanzia mavazi mpaka muonekano.

 

Sauti za kengele ndizo zilizo weza kumshtua kutoka kwenye usingizi mkali na mnono ambao alikuwa amelala, hakuwahi kwenye maisha yake kulala sehemu nzuri na bora kama hiyo leo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa hakuhitaji kuukosa usingizi huo hata kwa sekunde moja, alimlaani sana mtu ambaye alikuwa amehusika na kuikatisha safari yake ya usingizi, alitoka taratibu sebuleni na kwenda kuufungua mlango, alitabasamu baada ya kumuona Alen akiwa kwenye moja ya suti nzito mno hakuhitaji maelezo mengi alimhitaji watoke sasa akatengenezwe. Walipanda kwenye gari haraka sana wakaitafuta moja ya saloon kubwa Kani alienda kutengenezwa kuanzia uso wake na kufanyiwa masaji na watoto wakike ambao walinona mno, mate yalikuwa hayamkauki mdomoni na aliapia angerudi kuwatafuta, baada ya kumaliza safari yao ilienda kuishia ndani ya Mlimani City ambako walipanga kwenda kununua nguo za kutosha kwa ajili yake. Walifika na kushuka kwenye gari walianza taratibu kutembea kuelekea ndani Alen akiwa ametangulia mbele wakati anayakaribia malango ya kuingilia alijifanya kama anaishika kofia yake vizuri akaikutanisha mikono yake miwili na kuibonyeza kidogo tu saa ambayo ilikuwa kwenye mkono wake ghafla umeme kwenye sehemu zote ambazo zilikuwa karibu na hapo walipokuwa ulikata kwa dakika moja na kurudi haraka sana halikuwa jambo la kawaida liliwashangaza watu wote ambao walikuwa wapo karibu kutokana na sehemu hiyo kuto katika umeme hata kama umeme wa tanesco ungekata basi huwa kuna jenereta za kutosha ambazo huwa zinafanya sehemu hiyo kuwa yenye umeme muda wote.

 

 

Baada ya kumalizana na shoping yao ndani ya Mliman City siku ile maisha yaliendelea kama kawaida Kani akijitahidi sana kuwa mwenyeji wa jiji hili na kwa msaada wa rafiki yake Alen haikuwa kazi ngumu sana ilifika sehemu akawa ni mwenyeji kila sehemu japo alikuwa ana maswali mengi sana juu ya maisha ya rafiki yake kwanza alikuwa haelewi Alen alipoteaje ndani ya Arusha na kuja kuwa mtu tajiri kiasi hiki? Alijaribu kujijibu mwenyewe kwamba huenda mwanaume huyu alibahatika kuyapata madini lakini alilipinga hilo kwa sababu ilikuwa sio rahisi mtu kutoka na madini ndani ya yale machimbo na hata siku ambayo rafiki yake huyo aliondoka alikuwa kwenye hali mbaya mno kiasi kwamba asingekuwa na uwezo wa kufanya hicho kitu, swali la pili lilikuwa ni maisha ya mtu huyo kiujumla muda wote ambao alikuwa amekuja ndani ya jiji la Dar hakuwahi kabisa kuijua sehemu ambayo alikuwa akishi Alen lakini swali la tatu hakuelewa kwanini rafiki yake huyo alikuwa anakwepa sana kupiga picha kwenye uso wake na alikuwa makini sana kuweza kulikwepa hilo jambo hata hivyo aliamua kuuachia muda uamue kwa sababu hakuhitaji kulazimisha mambo wakati mhusika yeye mwenyewe hakuwa tayari kabisa kumwambia japo alitamani sana kuyajua majibu ya maswali yake.

 

“Kani nina imani utakuwa na maswali mengi sana juu yangu kwamba nimeyapataje haya maisha, kwanini sijawahi kukupeleka nyumbani? Muda ukifika utajua kila kitu ila kwa leo nataka kwa mara ya kwanza ukaione familia yangu ili hata siku nikipata tatizo wapate mtu wa kuwafariji” ni maneno ambayo yalimuacha Kani mdomo wazi alitetemeka kidogo hicho ndicho kitu ambacho alikuwa anakiwaza muda sio mrefu kwenye akili yake sasa alijiuliza huyo mtu kwanini amwambie hayo mambo muda huo kwamba alikuwa ameshajua anacho kiwaza? Hakupata jibu.

 

“Itakuwa ni vizuri sana ndugu yangu maana sijui hata familia ya rafiki yangu mpaka najisikia aibu muda mwingine” alijibu tu kama kujifariji ila kiuhalisia hata alicho kijibu alikuwa hajakijua, Alen alimwangalia kwa umakini sana Kani kiasi kwamba alikuwa ni mtu ambaye alikuwa anayapima macho yake kisha akatabasamu, waliingia kwenye gari na kuondoka kwa mwendo wa taratibu kabisa. Maeneo ya posta pembezoni kabisa mwa bahari ndipo gari ilipo enda kusimama nje ya mjengo mmoja ambao bila shaka mmiliki hakuwa mtu wa kuhesabu pesa kwa mkono lazima mashine ndizo zilikuwa zinafanya hiyo kazi ya kuhesabu ndipo walipoweza kufika, ilikuwa ni miongoni mwa majumba ya kifahari sana ndani ya eneo hilo Kani aliutazama huo mjengo bila kuumaliza alijikuta anameza mate na kikiri moyoni kwamba ukiachana nayeye kudumu hapa duniani ila dunia hii hii ina watu ambao walikuwa wanaishi kweli.

 

Baada ya kuingia ndani walikaribishwa na tabasamu la mwanamke mmoja mzuri mno ambaye alienda kumkumbatia Alen na kumpiga busu zito kwenye paji lake la uso.

 

“Welcome back my husband” ni sauti tamu ambayo ilipenya kwenye ngoma za masikio ya Kani na kujikuta akitabasamu akiwa haamini yule rafiki yake kapuku wa machimboni leo alikuwa anapokelewa na sauti nzuri laini kama hiyo mbele yake maisha yalikuwa yanakimbia mno, naye hakunyimwa haki ya kuisikia sauti hiyo baada ya kugutuliwa na sauti 

 

“Karibu nyumbani shemeji” alijikuta anababaika hata kujibu huku akipokea mkono wa mwanamke huyo kabla hajakaa sawa ilisikika sauti yenye kicheko cha kitoto iliyokuwa na furaha sana ikiwa inakuja upande wao.

 

“Daddy” mtoto wa Alen alikuja na kumkumbatia baba yake kipenzi, ni kitendo kilicho muacha Kani mdomo wazi hakuweza kuamini kama rafiki yake alikuwa amefikia hatua mpaka ya kuwa na mtoto kabisa, alijikuta anainama chini kwa mshangao, kwake dunia ilikuwa ina siri kali ila wanadamu ndio walikuwa wenye siri zaidi ya mifuko iwekwayo ndani ya nguo ya mtu.

 

Ni mwanzo kabisa ndani ya GEREZA LA HAZWA ukurasa wa tatu tunaweka nukta tupumzike kidogo.

 

Bux the story teller.

Previoua Next