Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

 

ENDELEA..................

 

Walikuwa kama familia moja, ilikuwa ni furaha kubwa sana kujumuika pamoja sasa swali moja lilikuwa limejibiwa kwake bila hata yeye kuuliza kwa kuweza kujua mahali ambapo rafiki yake alikuwa anaishi tena alibahatika kuijua na familia yake kabisa, sasa ilikuwa ni kawaida kwa Kani kwenda kwa Alen siku ambazo alikuwa ana muda wa kutosha kwa sababu mpaka muda huo alikuwa tayari ana biashara zake ambazo Alen alimfungulia hivyo kuna muda ilikuwa inamlazimu sana kuwa busy kusimamia hiyo miradi ambayo ilikuwa imefunguliwa tayari. Ulipita muda mrefu sana akawa mzoefu wa jiji tayari na alikuwa ameanza kijisimamia kwa kila kitu maisha mazuri yakiwa sehemu yake kwa kupitia mgongo wa rafiki yake ambaye alimsaidia miaka kadhaa nyuma kwake wema ulikuwa ni akiba kubwa ambayo ilikuwa imezaa matunda mema. 

 

Siku moja alikuwa anatamani sana kuweza kumshukuru rafiki yake kwa namna alivyo msaidia na kuyabadilisha maisha yake, aliwaza sana kumshukuru yeye tu lakini aliona haitakuwa sawa kwa sababu alihitaji watu wengi waone anavyo shukuru njia pekee kwake ambayo aliona watu wengi wanaweza kuona ni kupitia mitandao ya kijamii ambako huwa wanakutana watu wengi sana hapa ulimwenguni kwa muda mfupi. Alipanga atafanya kila namna ili ampige mtu huyo picha au wapige wote bila yeye kujua kitu chochote kile hivyo alinunua kamera moja nzuri na kubwa akawa ameihifadhi juu ya friji wakati huo alimpigia simu Alen kwamba alikuwa akimhitaji kwa muda huo kulikuwa na dharura ya mhimu sana mwanaume hakuona tabu alikuja kumsikiliza rafiki yake. Kabla hajaenda kufungua mlango aliitegesha kamera yake vizuri kabisa na kwenda kumfungulia mlango Alen baada ya kugonga.

 

“Kani umeniita ghafla sana umenishtua kuna nini?” Alen aliuliza kama kulikua kuna usalama humo ndani lakini Kani aliiangalia saa yake na kutoa kicheko

 

“Angalia kuleeeeee” alionyesha kidole wakiwa wapo karibu na ndipo Alen alipo geukia ule upande ambao ulikuwa na kamera yeye hakuweza kujua chochote kile muda huo kamera hiyo alipiga picha za kutosha (kosa kubwa sana).

 

“Nimekununulia zawadi ya saa hii hapa kaka, nashukuru sana kwa wewe kuwa sehemu ya maisha yangu sijui ningekuwa naishi vipi mpaka leo, sihitaji kujua kwa sasa kwanini ulitoroka hali iliyo nifanya nifukuzwe kazi kwa kusingiziwa kuiba madini na pia nilifungwa kwa muda wa miaka mitatu jela mpaka nilipo onekana sina hatia maisha yangu yalikuwa yameelekea shimoni ila umekuja na kunipa tumaini jipya kwenye maisha yangu asante sana kaka” Kani aliongea kwa uchungu mkubwa sana wakati anamshukuru rafiki yake, ni kweli maisha yake yalibadilishwa sana na mwanaume huyo kwake alidai alimuita hapo ili kumkabidhi zawadi ya saa ikiwa ni kama sehemu ya shukrani kwa kila alicho fanyiwa kwenye maisha yake, Alen alifurahi kiasi chake japo moyoni alikuwa kawaida sana kwake ilikuwa kawaida kwa sababu aliwajua sana binadamu hasa pale unapo onekana wa mhimu kwao basi watakunadi kwa kila aina ya maneno matamu ila sio ajabu hao hao kesho ndio wanakuja kukufanya ujutie kuwafahamu basi aliipokea saa hiyo na kumkumbatia rafiki yake wa ukubwani na kumpiga piga mgongoni.

 

“Asante Kani” alitamka kwa tabasamu na kutoka humo ndani akawasha gari na kuondoka kwani hata kazi yake ilikuwa haijulikani kabisa hapa mjini. Kani aliufunga mlango na kuanza kushangilia zoezi lake lilikuwa limeenda sawa, aliifuata kamera yake na kuangalia kweli kulikuwa na picha zaidi ya kumi ila kuna picha mbili tu ndizo alizo zipenda yeye, alizihamisha vizuri kwenye simu yake hakuchukua muda alienda moja kwa moja kwenye kurasa za mitandao na kuanza kuzisambaza hizo picha kwa maelezo mazuri sana ambayo yalikuwa yameandikwa kwa mbwembwe.

 

“MAISHA YANGU YAMEKUWA KAMA HADITHI YA KUFIKIRIKA KWA ZAIDI YA MIAKA 20 ILIYO PITA NIMEISHI NDANI YA JANGWA BILA MAJI ILA MUNGU ALIVYO WA AJABU AKAMTUMA MJA WAKE NA KUJA KUNIPATIA DAWA YA KIU NIKAPONA, SINA CHA KUKULIPA ILA NINASHUKURU KWA KILA KITU ULICHO NIFANYIA KWENYE HAYA MAISHA YANGU ALEN, I LOVE YOU BRO” maneno yalisomeka vizuri kabisa akiwa ameyaweka kwa herufi kubwa ili kwa kila msomaji atakaye iona picha hiyo asiache kuyasoma hayo maelezo. Lengo lake alitaka kumfanya rafiki yake aone ni namna gani alikuwa anathamini na kuheshimu kwa kila alichoweza kufanyiwa, fikra zake alijua atamfurahisha sana Alen kama ataona hicho kitu ila huenda alikuwa anafanya kosa kubwa sana kwenye maisha yake bila yeye kujua na kama angefanikiwa kujua madhara ya hicho alichokuwa anakifanya ni bora angejiua yeye mwenyewe.

 

Baada ya kuona ameiweka vizuri kama alivyokuwa anahitaji yeye basi aliichapisha na kuiruhusu kwenye mitandao mbali mbali ambayo kwake aliamini kwamba watu wengi wataiona na kumpongeza kwa Kumkumbuka mtu aliyeweza kumtoa mbali. Baada ya kuichapisha picha hiyo ilichukua dakika moja tu kuna alama nyekundu ilitokea kwenye hiyo picha mpaka yeye mwenyewe alibaki anashangaa hakuwahi kuona hicho kitu, baada ya sekunde thelathini tu picha hiyo ilifutika na kwenye kila ukurasa ambao alikuwa ameisasisha ilikuwa imefutika, mawazo yake yaligoma kuamini hicho kitu alihisi huenda alikosea ikamlazimu kurudia tena kuipakia cha ajabu ilikuwa inagoma. Alitaka kutafuta moja ya namba kwenye simu yake apige simu hiyo mahali ili aulizie hicho kitu lakini simu ilikuwa haifanyi kazi kabisa huku akiwa inapiga alama nyekundu, alibaki anatokwa jasho hakuelewa inawezekana vipi maajabu kama hayo kumtokea yeye majira hayo ya usiku wa mapema kabisa hiyo, alivyokuwa anazidi kulazimisha simu hiyo kufanya kazi ilianza kutoa moshi hatimae ilipasuka kwa mlipuko mdogo wa moto ambao uliifanya ibaki nyeusi kabisa na umeme ulizima nyumba yote.

 

Alikimbilia kufunga mlango ili kama kuna hatari awe salama alijikuta anarudishwa kwenye sofa kwa nguvu hakujua amepigwa na kitu gani kwenye mwili wake alihisi maumivu makali ambayo yalimfanya agugumie kama jogoo lililo ona tetea mbele yake.

 

“Nani wewe nani wewe, unavamiaje kwenye nyumba za watu aaaaagh” alikuwa anaongea mwenyewe hakusikia mchakacho wala sauti ya mtu yeyeote ambaye alikuwa akimjibu humo ndani. Ghafla taa ziliwaka mbele yake kulikuwa na watu watatu ambao wote walivaa suti zao nyeusi ila hawakuonekana kuwa watanzania kwa mwonekano wao tu ni wazi hawakuwa na uswahili mwingi kama ilivyo kwa wazawa wengine.

 

“Hey hey mnataka nini nyie watu, kawatuma nani hapa, hey nitawaua mimi” alikuwa akijitetea baada ya kuona mwanaume mmoja alikuwa anasogelea ile sehemu ambayo alikuwa amedondokea yeye hata hivyo hakujibiwa kitu chochote kile, alitaka kunyanyuka akimbie ngumi ilitua kwenye shingo yake akarudi tena chini na kutulia bila kupiga makelele alizimishwa kisha mwanaume huyo akambeba wakamuingiza kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi humo na gari yao ambayo walikuja nayo na walikuwa wameiacha nje ya nyumba.

 

 

 

Kani alishtuka kutoka kwenye usingizi mzito shingo yake ilikuwa na maumivu mno, mwanga mkali uliyaumiza macho yake ilimlazimu kuyafumba kisha kuyafumbua tena kwa mara nyingine ndipo alipoweza kuona sakafu nzuri sana na chumba kikubwa chenye kila kitu cha kukifanya kuwa bora kupita maelezo, alishtuka baada ya mbele yake kuwaona wanaume wenye suti nyeusi wakiwa wapo kama watano hivi mmoja wao alikuwa amekaa kwenye kiti ambapo mbele yake kulikuwa na meza ya kioo na meza hiyo ilitumika kuwekewa bastola na kisu kimoja kikali mno. Kwenye mwili wake alikuwa amevalishwa nguo nyeupe ni kama za wafungwa ila zakwake hazikuwa na mistari na namba, akiwa anashangaa na kurudi nyumba kwenye kitanda kizuri alichokuwa amelala alikuwa anajivuta taratibu nyuma mpaka pale alipofika mwishoni kabisa kwa ukuta hakuwa na sehemu ya kwenda tena kuna kijana mwenzie kama yeye aliingizwa humo ndani akiwa amekunjwa vizuri alisukumiziwa mbele hakuulizwa chochote ila alikuwa analia sana na alionekana alikuwa amelia kwa muda mrefu sana, yule mwanaume ambaye alikuwa amekaa kwenye kile kitu aliichukua bastola yake na kuigeuzia upande ambao alikuwa yule kijana bila hata kuangalia wakati huo macho yake alikuwa ameyakaza kwenye uso wa Kani alimmiminia yule kijana risasi kumi na mbili kwenye mwili wake halafu akaonyesha ishara ya mwili wa kijana huyo utolewe kwa mkono wake lilikuwa ni jambo la haraka hicho kitu kilifanyika kwa wepesi mkubwa, Kani alikuwa akitetemeka hakuwahi kushuhudia mtu akiuawa kwenye maisha yake leo kijana mwenzake kichwa chake kiligeuzwa mpira kwa kupigwa risasi nyingi mno aliogopa isivyo kawaida.

 

“Unaitwa nani kijana?”

 

“Naitwa Kani”

 

“Kwenu wapi?”

 

“Moshi”

 

“Unamjua huyo uliye naye kwenye picha?” alirushiwa picha kubwa ambayo yeye alikuwa ameipiga kwa siri na Alen mpaka hapo alijua kwamba watu hao waliibeba ile kamera ndiyo maana walikuwa wana hizo picha.

 

“Ndiyo namjua” alikuwa akijibu jasho likiwa sehemu ya mwili wake.

 

“Unamjuaje?”

 

“Ni rafiki yangu”

 

“Jitahidi kuwa na kichwa chepesi elezea vizuri umemjuaje na unamjua vipi yeye” sauti nzito ilimsisitizia kiasi kwamba hakuwa akiombwa kutoa hayo maelezo ilikuwa ni lazima afanye hivyo kwa sababu ya usalama wake, hakuwa na kitu ambacho angeweza kukipinga ni kwa muda mfupi sana alitoka kushuhudia mwenzake akiuliwa hapo japo hakuweza kujua kama naye alikuwa na kesi kama hiyo ya kwake au kulikuwa na mambo mengine nyuma yake.

 

“Anaitwa Alen jina lake jina lingine silijui na wala sijui alizaliwa wapi ila ninacho kikumbuka ni jioni moja majira ya saa mbili za usiku nilikuwa nimetoka kwenye harakati zangu za kila siku za kuweza kutafuta mkate ili nipeleke mkono wangu kinywani, wakati nimetoka kuchukua mikate na juisi kwa ajili ya kuimaliza jioni yangu vizuri nikalale kwenye valanda moja ya duka kubwa nilisikia mtu akiwa anaunguruma, mara ya kwanza nilihisi huenda itakuwa ni mlevi ila nilivyo karibia nilikuta kuna mwanaume amejiviringisha akiwa anatetemeka kwa baridi mno kwenye mwili wake, midomo ilimkauka sana ni wazi ulipita muda mrefu sana bila kuweza kuyapata maji. Nilimuamsha na kumuuliza nini lilikuwa tatizo kwake alinieleza kwamba ana njaa kali sana na ndiyo mara yake ya kwanza kuweza kuingia ndani ya jiji la Arusha, ni mwanaume mwenzangu hivyo niliingiwa sana na huruma nikaamua kumpatia kile chakula ambacho nilikuwa nimekibeba kwenye mfuko, alikifakamia mno akanywa na juisi kisha akadai na maji alikunywa yote akapata na nguvu za kuongea.

 

“Asante sana ndugu yangu hapa kama ungechelewa hata dakika tano tu nahisi nilikuwa ninakufa nilikuwa na njaa kali mno” aliniambia hivyo nikiwa bado namshangaa.

 

“Kwani nyumbani ni wapi ndugu yangu?”

 

“Sijawahi kujua chochote mpaka wakati najielewa nilijikuta kwenye kituo cha kulelea watoto yatima huko Dar es salaam hivyo namimi ni yatima lakini nikaamua kuondoka kwenye kile kituo baada ya kuona umri wangu wa kuweza kujitegemea umeweza kufika niliamua kuondoka na kwenda kuyaanza maisha yangu katika kuhangaika ndo nikawa nimeingia kwenye hili jiji la Arusha nina siku tatu hapa sikuwa nimekula chochote namshukuru sana MUNGU kuweza kukupitisha kwenye hii njia ambayo nilikuwa naenda kufa huku watu wote wakiwa wananipita kama hawamuoni mwanadamu mwenzao kabisa” aliongea kwa msisitizo akiwa anamalizia maji ambayo nilimpatia. Kwa sababu niliona ni msakatonge mwenzangu basi nikamchukua moja kwa moja na kwenda naye nyumbani ambako nilianza kuishi naye, mimi nilikuwa nashinda kwenye machimbo ya madini basi nikamuunganisha nayeye akawa anaenda siku moja moja mpaka pale alipo zoea na kuwa mmoja wa wachimbaji kule na hapo alipanga kachumba kadogo ambako alikuwa anakaa pekeyake japo bado tulibaki kuwa karibu sana kama marafiki na tulisaidiana kwa kila kitu mpaka ile siku ambayo aliumwa ghafla sana tukiwa shimoni kuendelea na uchimbaji, nilifanya jitihada za kuweza kumtoa na nilifanikiwa, alipelekwa kwenye hospitali ambapo huko ndiko inako daiwa alipotea mpaka ilipo pita miaka mitano ndipo alipo nitafuta na kuniambia nije DAR, nilifanikiwa kufika salama akanipa maisha mazuri sana akaniunganisha na familia yake lakini nilikuwa natafuta nafasi ya kuweza kumshukuru ndipo nilipo piga picha za siri ambazo leo hii nilikuwa nataka kuzisasisha mtandaoni kutoa shukrani zangu kwake” alitulia baada ya kuwapa maelezo mafupi ya namna anavyo mjua mwanaume huyo.

 

 

Hili game ndo kwanza linaanza, ulishawahi kuona mtu wa kawaida anaishi bila kuhitaji kamera yoyote ile iweze kuipata picha yake? Kwanini? Unadhani huyu binadamu Alen ni nani na hawa watu ni akina nani mpaka wanaonekana kumtafuta kwa nguvu zao zote namna hii?.......ukurasa wa 4 unaishia hapa huenda wakati utaamua kutupatia majibu juu ya huyu mchimba madini Alen ni nani hasa na kwanini anaishi kwa kujificha sana hivi.

 

Bux the story teller.

Previoua Next