Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: SIKU ZA MWISHO 

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA 

WhatsApp: +255621567672

Email: [email protected] 

UMRI: 18+

SEHEMU YA KWANZA

*******************

THE DARKNESS OF AN ANGEL

SIKU ZA MWISHO

JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

BANGUI

Saa mbili na dakika hamsini na tano za usiku kwa saa za Jamhuri ya Afrika ya kati, kwenye jengo moja refu la ghorofa kumi na tano alionekana mwanaume mmoja. Ni ndani ya mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya kati uitwao Bangui.

Taifa hilo ambalo linapatikana katikati kabisa mwa bara la Afrika lilikumbwa na balaa zito nyakati hizo za usiku wa mapema katikati kabisa ya mji. Kwenye lile jengo la ghorofa ile ndani ya floo ya tisa, mwanaume mmoja alikuwa kwenye haraka kubwa akionekana kwamba alikuwa anawahi mahali. Alikuwa anayabadilisha mavazi yake akiingia kwenye mavazi ya kawaida. Mezani palikuwa na silaya ya masaafa marefu aina ya SVD Dragunov ambazo huwa zinatumiwa na wadunguaji mashuhuri duniani.

Pembezoni mwa hiyo silaha kulikuwa na bastola mbili, kisu kimoja, ramani pamoja na begi la mgongoni. Bwana huyo alikuwa anajitahidi kwenda na muda na wakati ambao haukuwa rafiki kabisa kwake, aliifungua ile silaha haraka haraka kisha akaipulizia spray ikaanza kusinyaa kisha akairushia kwenye kapu la taka. Alibeba passport zake za kusafiria na kuziweka mfukoni, bastola alizipachika kiunoni pamoja na kile kisu, alibeba vitu vyake na kuiweka kofia usoni kiasi kwamba akawa haonekani vizuri.

Alisogea dirishani na kuchungulia nje ambako aliona kuna kashikashi kubwa ikiendelea huku watu wakiwa wanakimbizana kuelekea kila upande kila mtu akionekana kabisa kwamba alikuwa anayapambania maisha yake. Polisi walitapakaa kila sehemu, walikuwa wanabadilishana kupigiana simu kila mahali huku gari za wagonjwa zikiwa za kutosha eneo hilo, halikuonekana kuwa salama kwa nyakati hizo. Bwana huyo baada ya kuridhika na alichokuwa akikiangalia kwa wakati ule, alivuta droo na kubeba pesa zote akazifukia kwenye begi lake na kulirudishia mgongoni mpaka alipo hakikisha kwamba kila kitu kimemridhisha basi akafungua mlango na kutoka nje.

Nje ya floo yake hapo hapakuwa na mtu, palikuwa na utulivu wa kutosha hivyo hakuna mtu hata mmoja ambaye alikuwa anamuona ikawa rahisi kwake kufanya ayatakayo. Alisogea kwenye kifaa cha alarm akakibonyeza, kilipiga kwa sauti kuwapa tahadhari watu kwamba eneo hilo halikuwa salama kwa wakati huo na kama wangeweza basi kila mtu alitakiwa kuyapigania maisha yake. Japo eneo hilo halikuonekana kuwa na watu wengi kwa wakati ule ila waliokuwepo walitoka nje kwa hofu wakitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kinaendelea.

“Bomb! Bomb! Bomb!” bwana yule alitamka maneno hayo kwa sauti kubwa kiasi kwamba kila ambaye alikuwa karibu alisikia, kila mtu alianza kuropoka huku watu wakiwa wanakimbia kwenda chini kuyaokoa maisha yako kwakuwa hali haikuonekana kuwa sawa. Hali ile ilifanya msongamano wa kushuka kwenye ngazi wakati watu wakiwa wanajitahidi kuyaokoa maisha yao kuwa mkubwa hivyo naye akajumuika pamoja na watu hao tena akionyesha kuwa na hofu kubwa. Wakati wamefika floor ya kwanza walipishana na polisi wengi wakiwa wanapandisha kwenye hilo eneo ila alijifanya naye ni mhanga kama walivyokuwa wengine. Kuna polisi mmoja wakati anapandisha alimshtukia bwana huyo ikabidi asimame na kugeuka kuweza kumwangalia, alionekana kuwa tofauti kidogo na watu wengine kwani wenzake walionekana kukimbia wakiwa nusu utupu ila yeye alikuwa amejipanga kama mtu ambaye anasafiri. Hakufanikiwa kurudi kwa sababu wenzake walimuita ili wakaone tatizo.

Mwanaume huyo alihema baada ya kufanikiwa kutoka salama eneo hilo ambapo alikatisha kwenye vichochoro kadhaa mpaka alipofanikiwa kufika kwenye barabara kubwa akaita usafiri ambao alihitaji umpeleke moja kwa moja kwenye uwanja wa ndege ambao upo umbali wa kilomita nane tu kutoka ndani ya mji mkuu wa taifa hilo. Zilitumika dakika kumi na tano tu wakawa wamefika kwenye uwanja huo wa ndege wa Bangui M’poko International Airport, alilipa pesa na hakutaka chenji hata pale ambapo dereva huyo wa gari alipo jaribu kumuita, hakuonekana kama ni mtu ambaye alimjali bwana huyo zaidi ya kutokomea ndani ya uwanja huo wa ndege ambao ndio mkubwa zaidi ndani ya Bangui.

Tiketi alikuwa nayo tayari kwenye mkono wake hivyo alipitia kwenye ukaguzi tu ambapo muda mfupi baadae aliingia kwenye usafiri na baada ya dakika kumi na tano ndege ikaanza kukata anga kuiacha ardhi ya Bangui nyuma huku akionekana kuhema na kushukuru kwa kila ambalo lilitokea kue nyuma, silaha zote ambazo alikuwa nazo mwilini alizitelekeza uwanja wa ndege upande wa vyooni ili zisije kutumika kwenye muunganiko wa jambo ambalo bila shaka alikuwa amelifanya usiku huo wa mapema ikamletea shida ya kuweza kutoka ndani ya eneo hilo.

SAA MOJA NYUMA

Katikati kabisa ya mitaa ya Bangui lilitokea jambo la kutisha, jambo ambalo halikuwa la kawaida na wala halikutarajiwa kuweza kutokea. Ndani ya jengo la soko kubwa ambalo ndilo lilikuwa linatumiwa na watu wengi kwa ajili ya shughuli za kila siku za kibiashara, ulitokea mlipuko mkubwa ambao ulilidondosha jengo hilo. Kudondoka tu kwa jengo hilo hakukutosha kuleta simanzi miongoni mwa watu bali jambo ambalo lilitishia amani zaidi ni idadi ya watu ambao walikuwa ndani ya jengo lile. 

Kudondoka kwake kulisababisha msiba wa taifa, msiba ambao ulileta simanzi kubwa miongoni mwa watu na wakazi wa Bangui. Jengo lilienda na maisha ya watu mia tatu na hamsini kwa hesabu za haraka haraka lakini wakati huo pia walikuwa wanaendelea na uokoaji na kuendelea kulifukua jengo hilo. Kushuka kwa jengo hilo haikujulikana sababu yake haswa ilikuwa ni nini kwa sababu halikuwa jambo la kawaida lakini dakika kadhaa nyuma kabla ya jengo hilo kushuka, alionekana mwanaume mmoja akiwa ndani yake.

Mwanaume huyo ndiye yule ambaye baadae alionekana kwenye lile ghorofa akiwa na silaha ya udunguaji. Bwana huyo alikuwa na begi dogo tu akiwa anafanya manunuzi ya bidhaa kadhaa ndani ya jengo hilo hivyo hakuna mtu ambaye alikuwa na muda naye. Kila mtu alikuwa anajali kufanya yale ambayo yalimpeleka pale hivyo akaipata nafasi nzuri ya kutimiza lile ambalo alililenga kulifanya. Alishuka mpaka upande wa chini kabisa wa jengo hilo ambako kulikuwa na utulivu, eneo hilo ndilo ambalo lilikuwa na nguzo kubwa ambazo zilikuwa zimelishikilia jengo hilo, alitazama kila upande mpaka pale ambapo alikuwa na uhakika kwamba hakuna mtu hata mmoja ambaye alikuwa anamtazama ndipo akajisogeza kwenye kona moja iliyokuwa na kiza.

Kwenye kona hiyo aliiweka ile begi ambayo alikuwa nayo na kubonyeza rimoti kwenye mkono wake, bila shaka alikuwa amehifadhi bomu ndani ya ile begi yake. Baada ya kuhakikisha kila kitu kinaenda kama ambavyo alikuwa amepanga, hakuhitaji kukaa hilo eneo tena zaidi ya kuondoka haraka kwani alijua jambo ambalo lilikuwa linafuata muda mfupi baadae. Baada ya kutoka kwa dakika kumi mbele alikaa sehemu na kulitazama jengo lile kwa mbali kisha akaitazam rimoti ambayo ilikuwa inasoma sekunde kwa kasi kubwa.

Zilikuwa zimebakia sekunde kumi na tano tu na baada ya kugota kwenye sifuri, ulisikika mlipuko mkubwa ambao ulisambaa kila sehemu na kuzua taharuki. Upande mmoja wa lile jengo ulishuka huku moto ukiwa wa kutosha japo haukudumu kwa kufukiwa na zile kuta nyingi za jengo lile, upande ambao hakukuwa na mlipuko ulianza kutitia taratibu japo watu wengi walifanikiwa kukimbia ambao walikuwa upande ule ila bado kuna ambao walikufa pale pale na majeruhi wengi walipatikana.

Bwana yule alitabasamu akiwa anahakiki saa yake na kutoa bablish kwenye mfuko wake akaanza kutafuna taratibu na kuingia kwenye kona moja. Akiwa anakatiza kwenye hizo kona mbele yake walitokea wanaume wanne na wakati anawasogelea ndipo aligundua kwamba hawakuwa wanaume tu bali walikuwa ni wanajeshi ambao walikuwa ndani ya magwanda yao. Ule mshtuko ambao aliuonyesha kwa kuwaona bila matarajio ndio ambao hata wao uliwashtua, wanaume hao walionekana kabisa kwamba walikuwa wanawahi kutoa msaada kwenye lile jengo kwa sababu walikuwa karibu ndipo wakakutana na mtu ambaye yeye alionekana kutokea kule tena akiwa na furaha kubwa.

Haikuwa kawaida kwa raia wa kawaida nyakati kama hizo kuwa kwenye furaha au kutokuwa na hofu, maana yake alikuwa ni zaidi tu ya raia ndiyo sababu baada ya kumkaribia bwana huyo, walimtaka asimame ili waweze kumalizana naye kwanza kwa kumhoji ama kumkamata ili baadae waweze kumhoji vizuri lakini hata yeye alikuwa nje ya muda kwa sababu kuna kazi ambayo alitakiwa kuifanya muda mfupi ambao ulikuwa unafuata kuanzia wakati huo hivyo watu hao wangempotezea muda na kumuingiza kwenye hatari.

Wanaume hao walimpa ishara ya kusimama hapo alipokuwepo, walimzunguka kila upande huku mmoja akimsogelea ili aweze kumkagua tena kwa sifa ambayo ilijionyesha mbele ya uso wake. Aligusisha mkono wake kiunoni karibu na zilipo sehemu za siri, ule mkono ulidakwa na kuvutwa kwa nguvu, alipigwa ngumi ya kwenye kwapa karibu na bega akatoa ukelele wa maumivu. Ngumi ya pili ilitua kwenye shingo yake ambayo ilipinda akasukumiwa kweye mfereji mdogo wa maji machafu akiwa ni marehemu. Lilikuwa ni suala la sekunde nne tu tukio zima kuweza kukamilika, wenzake walibaki kwenye mshangao wakiwa kama ni watu ambao hawakuwa wakiamini yale ambayo yalitokea pale nyakati kama zile.

Ndo kwanza naufungua ukurasa wa kwanza kabisa wa simulizi hii. Huyu mtu ni nani na anafanya nini ndani ya taifa hilo ambalo anaonekana mgeni nalo na shida nini mpaka anaonekana anakimbia?

Ungana nami mwanzo mpaka mwisho ili tuweze kwenda sawa na simulizi hii mpya.

FEBIANI BABUYA.

Next