HADITHI: SIKU ZA MWISHO
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WhatsApp: +255621567672
Email: [email protected]
UMRI: 18+
SEHEMU YA PILI
Aliyekuwa nyuma alijitahidi kwenda baada ya kujitoa kwenye mshangao, kusogea kwake kwa nguvu likawa ni kosa kwake kwa sababu yule mwanaume aligeuka mkono wake ukiwa kiunoni. Alivuta kisu na kukizamisha kwenye moyo wa yule bwana na kukizungusha mara mbili habari yake ikawa imeishia hapo. Alihisi ujio wa mtu nyuma yake, aligeuka na kukutana na ngumi ya uso, yeye alirusha mkono wenye kisu kwenda pembeni kwa yule mwingine ambaye naye alikuwa anashambulia kwa ngumi ili wamuunganishie wote kwa pamoja.
Wakati anapigwa kwenye uso naye kisu kilizama kwenye mkono wa yule mmoja ambaye alikikutanisha na ngumi yake. Zile kelele za miguno zilitulia baada ya kufuatwa kwa kasi na kupigwa ngumi ya kifua, alihema akitaka kurudi nyuma ila alitulia baada ya kisu kuzungushiwa kwenye shingo yake. Alikuwa mmoja ambaye hakuwa bado anaamini yaliyokuwa yanatokea mbele yake, alimkimbilia yule bwana ambaye hakutumia nguvu kubwa zaidi ya kurusha kisu ambacho kilizama kwenye tumbo la yule mwanajeshi kiasi kwamba akakosa hata nguvu ya kuweza kusogea mbele. Alimfuata na kumsogelea yeye mwenyewe kisha akamziba mdomo na kukivuta kila kisu akakita kwenye shingo mpaka alipo hakikisha kwamba amekufa. Hakutaka jambo lile litambulike haraka hivyo ile miili aliisukumizia yote kwenye ule mfereji kisha akaharibu taa zote za umeme ambazo zilikuwa karibu na eneo hilo ambazo zingemfanya mtu yeyote kuiona miili hiyo. Alijifuta vizuri na kutoweka hilo eneo akiwa amekamilisha nusu ya kazi yake na kwa wakati huo ilikuwa imebakia nusu ya kazi ambayo ndiyo ilikuwa mhimu zaidi.
Tukio ambalo lilitokea nyakati zile halikuwa la kawaida kwa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, lilikuwa ni tukio baya, gumu na ambalo lilikuwa linaenda kuacha alama mbaya kwenye taifa hilo ndiyo sababu ambayo ilimfanya raisi wa taifa hilo kutangaza safari ya ghafla ya kwenda huko ili akawafariji wananchi wake ambao walikuwa wamemuweka madarakani. Ujio wake eneo hilo ulifanya jitihada za uokoaji kuwa kubwa zaidi na wananchi wake wakaanza kupata matumaini mapya japo hata ulinzi eneo hilo uliongezwa na kuwa mkali.
Raisi baada ya kufika eneo hilo yaliandaliwa mazingira kwa ajili ya yeye kufanyia mkutano wa haraka na vyombo vya habari ili kuweza kutoa angalau neno la pole kwa wananchi wa eneo hilo na taifa lake kwa ujumla. Ilitumika nusu saa helikopita iliyo mbeba raisi kufika eneo hilo na baada ya dakika zingine kumi alikuwa tayari amesimama mbele ya maiki kwa ajili ya kuweza kuongea. Wakati raisi anaanza kuongea mbele ya vyombo vya habari usiku huo huku kazi ya kuwaokoa watu pia ikiwa inaendelea, yule mwanaume ambaye muda mfupi ndiye alionekana kutega bomu hapo alikuwa amefika kwenye jengo ambalo alikuwa amefikia.
Nyakati hizo alikuwa dirishani akiwa anaifunga vizuri silaha yake, ni mtu ambaye alionekana kabisa kwamba alifanya tafiti za kutosha juu ya tukio hilo na kutambua kwamba kama tatizo likitokea basi ni wapi ambapo mtu wake atakuwepo kwa wakati huo. Alimaliza kuifunga vizuri na ndani yake akaweka risasi moja tu huku zingine zikiwa pembeni, hakuwa na shida ya kuweza kutumia risasi nyingi. Alitoa bablishi na kuitupia mdomoni mwake kisha akasogeza jicho lake kwenye silaha akiwa mtulivu, silaha yake ilikuwa inamtafuta raisi alipokuwepo ambapo ni sekunde thelathini tu zilitosha kumfanya raisi huyo kujaa kwenye kioo chake eneo ambalo lilikuwa ni mbali kidogo kutoka eneo la tukio. Alihema kwa nguvu na kufumba jicho moja kisha akafyatua risasi, alipokuja kulifumbua jicho lingine, raisi wa Jamhuri ya Afrika ya kati alikuwa anadondoka chini baada ya risasi kutoboa sikio lake na kuzama ndani ya kichwa.
Ilikuwa ni ghafla, ilizua taharuki kubwa hususani baada ya watu kugundua kwamba ni risasi ilikuwa imemdondosha raisi wao. Hakuna ambaye aliamini tena kwamba eneo hilo lingekuwa salama kwa wakati huo, lilionekana kuwa eneo hatari kwa maisha yao hivyo walianza kukimbia huku na huko kila mtu akihisi kwamba huenda ikafuata zamu yake. Ule mshtuko ulifanya viongozi wa usalama wa raisi pamoja na polisi kuhitaji mhusika apatikane haraka ambapo baada ya kuangalia kwa umakini waligundua kwamba ni wapi ambako risasi ilitokea hivyo mara moja walihitaji askari wazingire jengo lile kuhakikisha mhusika anapatikana huku raisi akiendelea kupata matibabu na kuwahishwa hospitalini kuona kama wangeweza kuokoa maisha yake.
Wakati ambao polisi wengi walikuwa wanalifikia jengo lile ili waweze kumtafuta mtu wao ndio wakati ambao ilisikika alamu ndani ya jengo hilo na kuwafanya watu ambao walitulia nyakati hizo za usiku kuanza kutoka na kukimbia kila sehemu hususani baada ya kusikia kwamba jengo hilo lilikuwa na bomu ndani yake kiasi kwamba nalo lingelipuka na kushuka kama lile la sokoni. Kuchanganyika kwa watu wengi ndiko ambako kulimfanya yule mwanaume kukamilisha kazi yake na kutoroka bila kupatikana. Polisi walianza kujazwa kila sehemu kuhakikisha mhusika haendi mahali, walizuia ndege zisiondoke, hakuna mabasi yaliruhusiwa kutembea ndani ya mji huo. Polisi walizagaa kila kona ila haikuwa kweli kufanikisha jambo lao kwa sababu mhusika hakuwepo tena muda ulikuwa umekwenda mno.
TANZANIA
TANDIKA SOKONI
Eneo hilo huwa lina amsha amsha muda mwingi kwa sababu ya shughuli zake ambazo zinaendelea. Ni eneo ambalo limekaa sehemu nzuri kibishara kwa sababu kuna mzunguko mkubwa wa watu kutoka maeneo mbali mbali hivyo kufanya biashara kuwa nzuri maeneo hayo.
Usiku wa saa tatu palikuwa pamechangamka kama kawaida wakati ambao akina mama ntilie walikuwa wakijitahidi kwenda na kasi ya eneo hilo kuhakikisha kwamba wanatengeneza pesa kwa biashara ya msosi. Wengi hawakuwa na vibanda au fremu kwa sababu zilikuwa ni ghali eneo hilo hali ambayo ilipelekea kuwa na maeneo ya wazi tu ambayo ndiyo yalikuwa yakitumika kufanyia biashara hiyo.
Hali hiyo ilifanya watu kujazana kwenye maeneo ya mama ntilie hao ili kujipatia milo ya jioni kabla ya kuendelea na shughuli zao na wengine wakiwa wanafunga kwa ajili ya kwenda kulala na wengine kustareheka kama ambavyo imezoeleka kwenye jiji kubwa la Dar es salaam. Kwenye viti vya mbao na meza moja ndefu ya mama ntilie mmoja walikuwa wameketi vijana kadhaa wakiwa wanakula huku wanapiga soga kuhusu taifa lao, pembezoni kwa kiti kimoja kirefu kulikuwa na mwanaume ambaye alionekana akiwa amevalia pama kubwa la kahawia kichwani huku mwilini akiwa na mavazi ya suti.
Umri wake ulionekana kabisa kuwa tofauti na vijana wale kwani yeye alikuwa ni mtu mzima kabisa. Hakuwa na maongezi na mtu yeyote yule kwa sababu hakuonekana kuwa sehemu ya utamaduni wa eneo hilo zaidi ya kulizingatia bakuli lake kubwa la supu na chapati tano ambazo alikuwa anaziendea taratibu bila haraka. Alionekana kuvutiwa na mazungumzo ya vijana wale kwa sababu zile habari zilikuwa zimetokea kwenye taifa lao, ni habari ambazo mpaka wakati huo zilikuwa zinayavutia masikio ya wengi kutokana na historia ya taifa ambako lilikuwa limetokaa na chanzo kikubwa zikiwa ni hizo habari ambazo wakati huo walikuwa wanautumia kuzielezea taratibu.
“Mimi naamini kwamba yale mambo yalitokea kwa sababu ya tamaa za wanasiasa, sehemu ambayo siasa inakuwepo kwa kiasi kikubwa na kuna maslahi basi wanasiasa huwa wapo tayari kuvuka ile mipaka ua ubinadamu na kuvaa uhusika wa ngozi za kutisha. Mara nyingi ukiwakuta kwenye hali kama hiyo basi sahau kabisa kuhusu wao kuuzingatia ubinadamu, mara nyingi hapo huwa wanaangalia zaidi kwenye mifuko yao na namna ya kudili na matumbo yao binafsi pamoja na kulimbikiza mali kwa ajili ya watoto wao ambao baadae ndio huwa wanakuja huku uraiani kuweza kututukana sisi kwamba hatufanyi kazi’’ aliongea kijana mmoja ambaye alivuta hisia za vijana wenzake ambao walikuwa pale kwa sababu ni yeye ambaye alionekana kuwa na akili nyingi na weledi kwenye kuelezea mambo yale.
“Unamaanisha kitu gani moja kwa moja ndugu yangu? Wote tunajua hapa kwamba wewe ndiye mwenye akili kutuzidi sisi sote hivyo ukiongea kwa falsafa namna hiyo unaanza kututesa sisi vichwa maji’’ alilalama kijana mwingine ambaye yale maelezo bila shaka yalimtupia habarini.
“Wote si mnakumbuka yale ambayo yalitokea miaka mitatu ambayo imepita?”
“Hilo sio swali la kuuliza, ni mambo ambayo kila mtanzania anayajua kwa maisha yake yote’’
“Una uhakika kila mtanzania anayajua kiundani’’
“Ndiyo kwa sababu hizo simulizi zilitapakaa kila sehemu, ndani na nje ziliongelewa kwa ukubwa, sasa unahisi ni mtu gani mjinga ambaye atakuwa hajazisikia habari maarufu ambazo zitaishi miaka na miaka?”
“Kuna utofauti wa kusikia na kujua kitu kiundani, kusikia ni kwamba unaweza ukapokea lolote ambalo masikio yako yataruhusu wewe ulipokee ndiyo maana kwenye maisha yako unashauriwa kusikiliza zaidi kuliko kusikia lakini kuelewa kiundani maana yake ujue taarifa zilizo nyuma ya hayo mambo na kuzijua taarifa kama hizo ndipo unaweza kuwa na muunganiko wa yale ambayo kweli yalitokea. Usipende kuamini maneno ya wanasiasa, wale huwa wanaongea lolote ili wakufurahishe kwa muda fulani waje kubeba kura yako na baada ya hapo wanakutupa kama hawakujui”
“Kwahiyo unamaanisha kwamba wanasiasa wote ni matapeli tu’’
“Sina maana hiyo lakini jambo la msingi ambalo unatakiwa kulizingatia kwenye maisha yako ni kwamba kumuamini mwanasiasa ni kuamua kujichosha na kupoteza muda wako kwa sababu they are all liars
(wote ni waongo)’’
Unahisi kijana huyu ana yapi ya kutueleza kiundani kuhusu hiyo miaka mitatu ambayo ilikuwa imepita? Sehemu ya pili inafika mwisho, tukutane ndani ya sehemu ya tatu kuweza kujua yale ambayo yalitokea kwenye hizo nyakati.
Febiani Babuya.
Comments