Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: SIKU ZA MWISHO 

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA 

WhatsApp: +255621567672

Email: [email protected] 

UMRI: 18+

SEHEMU YA TATU 

“Mhhh kwenye lugha hapo ndo unaanza kuharibu sasa, turudishe kwenye mjadala wa kwanza tujue ni jambo gani ambalo ulihitaji kulimaanisha na sisi tupate kulielewa kiundani kama wewe’’ kijana mmoja ambaye alionekana kuwa na hamu kubwa ya simulizi ya stori hizo hakutaka maada ihame, alikuwa anataka naye apate mambo kadhaa ya kwenda kutambia mtaani kwake ili wajue kwamba alikuwa na za ndani kuliko wenzake.

“Una haraka sana ndugu yangu ila binafsi huwa naamini kwamba kama zisingekuwa tamaa za wanasiasa basi yale mauaji yasingetokea, ile familia ya Gavin Luca isingeweza kuacha maafa makubwa namna ile. Mimi nilifanikiwa kukisoma kile kitabu kwa rafiki yangu mmoja mtoto wa tajiri ambaye aliweza kukinunua niseme tu kwamba kuna mambo ya kutisha ambayo hii dunia haiyajui na siku ambayo ulimwengu unafanikiwa kuyajua mambo hayo basi nafasi ya wanadamu kuendelea kuishi inakuwa ni ndogo mno” jambo ambalo aliliongea lilionekana kuwa la mhimu kwa wenzake kiasi kwamba wote waliacha kula na kumzingatia yeye, lakini haikuwa hao tu bali hata kwa watu wengine ambao walikuwa pembeni walianza kusogea na kujazana eneo hilo ili kuipata hiyo simulizi ambayo kila mwanadamu wa Tanzania alikuwa akiihusudu na kuipenda lakini ni watu wa kuhesabika walibahatika kuzipata taarifa zote za watu hao.

“Ina maana kwamba muda wote una simulizi ya hawa watu ambayo sisi hatukuipata na umetukaushia kaka? Aaaaah! Sio kweli bwana’’ alilalama kijana mwingine huku akiwa anavua shati yake na ndani akibakiwa na vest nyeupe ambayo mbele yake ilibandkwa picha ya Gavin Luca akiwa ameushika upanga. Yule msimuliaji baada ya kuona vile, alitabasamu na kumuuliza yule kijana mwenzake.

‘Kwanini una picha ya huyo mtu kwenye nguo yako?”

“Kwa sababu ni shujaa wa kweli ambaye hakuhitaji kwenda kulia lia ili asaidiwe, ni mwanaume pekee ambaye aliamua kuinyoosha serikali kwa upumbavu wao ambao huwa wanawafanyia watu wengine. Kama ningefanikiwa kukutana na mtu huyo kabla ya kifo chake basi ningekubali mimi kuuawa kwa niaba yake. Hakuna mtu mwenye akili timamu hapa duniani halafu asiwe shabiki mkubwa wa Gavin Luca na ndiyo maana mpaka leo ndani ya soko la Afrika nguo zake ndizo nguo ambazo zimeuza zaidi kuliko nguo za aina zozote zile kuwahi kutokea” alijinadi kijana huyo na wenzake wakacheka ila walimtaka kijana mwenzao azingatie zaidi ni yapi ambayo yalikuwa ndani ya kile kitabu cha THE DARKNESS OF AN ANGEL.

“Mle ndani yameandikwa maisha yake yeye, maisha ambayo aliyaishi, maisha ambayo yalimfanya yeye kuwa kiumbe hatari zaidi duniani na namna ambavyo alianza kuua watu. Kuna vitu ambavyo wanadamu wengi huwa hawavielewi na hata kama wakivielewa basi huwa wanavielewa muda ukiwa sio rafiki kwao. Mtu yeyote anapo zaliwa huwa anakuwa malaika kabisa kwa sababu hana dhambi yoyote ile ila maisha ya dunia na maisha ambayo yeye anaamua kuyaishi ndiyo ambayo yanaweza kumfanya akawa tofauti na vile ambavyo wengi walikuwa wanamtaka awe au ambavyo asili iliamua awe.

Dunia huwa inaanza kuwabadilisha watu taratibu, ulimwengu huwa unawafanya watu wanakuwa wa tofauti na kipindi wakibadilika ndipo huwa yanaanza kutokea mambo ya kutisha ambayo huwa yanaufanya ulimwengu usiwe sehemu salama kwa ajili ya maisha ya watu. Kitabu kinazungumzia upande wa giza wa malaika, upande ambao wanadamu wengi huwa wanakuwa nao kulingana na maisha ambayo dunia inawachagulia wao kuweza kuyaishi. Bwana yule alizaliwa akiwa kama malaika, alitamani kuwa mtu safi ambaye hakutaka kuwa sehemu ya kuyakatisha maisha ya mtu mwingine lakini angeweza vipi kuyaishi hayo maisha ingali familia yake mwenyewe iliuawa? Tatizo kubwa lilianzia hapo hivyo yule mtu ambaye alitakiwa kuwa malaika aliamua kutuonyesha ule upande wake wa pili wa giza unakuwaje pale ambapo dunia inamlazimisha kuyafanya mambo ambayo huenda hata yeye mwenyewe hakuwa nayo.

Lakini pia kile kitabu kinatoa somo moja kubwa ambalo ndilo huwa linawafanya wanadamu kuonekana wana roho mbaya kupita ile kawaida ya mwanadamu anavyotakiwa kuwa, KISASI. Kisasi huwa ni haki kama kinatakiwa kulipwa lakini ubaya wa kisasi ni kwamba ni ugonjwa wa milele, ni ugonjwa ambao huwa unaishi siku zote za maisha ya mwanadamu. Mwandishi mle ndani kupitia akili ya Gavin Luca anaelezea kwamba unapo lipa kisasi au kutengeneza kisasi unatakiwa kutambua kabisa kwamba umetengeneza tatizo la milele ambalo litaenda kizazi kimoja mpaka kingine. Leo wewe ukilipa kisasi unatakiwa kulazimika kufanya jambo moja kubwa ambalo ndilo limefanya yeye aone kwamba kisasi huwa kinamfanya binadamu kutoka kwenye ubinadamu wake.

Unapolipa kisasi unatakiwa kuhakikisha unaua kizazi kizima cha huyo mtu ambaye alikukosea kwa sababu kama akibaki mtu hata mmoja kwenye kizazi hicho basi ni lazima naye baadae atakuja kurudi kwako na kuhitaji kulipa kisasi cha wapendwa wake na vivyo hivyo na kwako pia nawewe baadae kama ukibaki utatamani kulipa kisasi. Sasa hilo huwa linaenda vizazi na vizazi na ametolea mfano kwamba Gavin mwenyewe aliwahi kufanya kosa kubwa la kumsamehe mtu na baadae akaja kuwa sehemu kubwa ya majuto yake na alijua lazima kuna mtu mwingine ambaye angekuja kurudi baadae.

Sasa hayo maisha ya baadae hayapo kwenye kitabu na ndiyo ambayo hata yeye mwenyewe yalimfanya akaja kufa. Jambo pekee ambalo ni kubwa na halipo ndani ya kitabu ni kuhusu siri za familia yake na familia yake kwa ujumla ambayo kwa baadae ilikuja kujitokeza na wote tunajua kabisa kwamba mwisho wake haukuwa mzuri mpaka hii leo yeye mwenyewe ni marehemu’’ ilikuwa ni simulizi nzuri na ya kuvutia mno. Ndani ya muda mfupi eneo hilo lilikuwa limefurika watu wakiwa makini kusikiliza habari hizo za ndani kabisa watu wakasahau hata kula na hata wauzaji wenyewe walibaki wamesimama wakisikiliza kwa kumakini mkubwa.

“Unasimulia matukio kama ulikuwepo ndugu yangu, nahitaji tuipate simulizi nzima ambayo ipo humo ndani kwa sisi ambao hatuna uwezo wa kukipata kitabu lakini tunatamani kujua kwamba je ile familia mpaka leo bado ipo, na kama ipo iko wapi? Ni muda mrefu umepita na hakuna taarifa zozote kuhusu wao na wala hawajawahi kusikika mahali popote na serikali kwa sasa haijawahi kuzungumzia tena habari hizo” aliuliza kijana mwingine ambaye alikuwa moja ya wale ambao walivutiwa zaidi na yale maelezo.

“Kuhusu familia naweza kukuhakikishia kwamba bado ipo hai lakini kujua kwamba ni wapi ilipo! Nina imani hata raisi wa taifa hili hawezi kukupa jibu la hilo swali lako”

“Mhhhhh umejuaje kama ipo hai?’’ kijana huyo alitabasamu baada ya kuulizwa swali la namna hiyo, alijikohoza kidogo na kumwangalia muulizaji.

“Nina mgonjwa nyumbani hivyo nawahi kwa sasa, kesho nawaahidi kwamba nitawasimulia simulizi nzima na nitawapa taarifa kwamba nilijua vipi kwamba hii familia iko wapi na nitawapa sababu za msingi za familia hii kuweza kupotea mpaka leo’’ kauli yake ilifuatiwa na yeye kunyanyuka hapo na kuanza kuondoka, watu walianza kulalamika na wengine wakiwa wanatukana kwani aliwapa hamu kubwa ya simulizi halafu akaikata njiani, watu walikuwa tayari kumpatia pesa aweze kukaa na kuendelea lakini aliondoka hapo na kuahidi kwamba angerudi kesho yake. Hakuwasikiliza walalamikaji ambao waliondoka wakiwa wanalaani na kushusha matusi mazito ya nguoni kwa kijana huyo’’

Kumaliza kwake mazungumzo kwa ghafla kuliwafanya watu kuanza kutawanyika lakini pia ilikuwa hivyo kwa yule mwanaume ambaye umri wake ulikuwa wa makamo akiwa anayasikiliza yale maelezo kwa umakini. Hakuna ambaye alikuwa amemshtukia hata kidogo huenda kwa sababu ya kunogewa na ile simulizi hali ambayo iliwafanya watu kuwa na mawazo yote upande huo. Alikuwa amemaliza kula, baada ya kuona yule kijana anaondoka alilipa pesa ambayo hakutaka hata kupatiwa chenji yake kisha akatoweka kwa uharaka kwenye eneo hilo. Hakuwa anaenda upande wowote mwingine zaidi ya kumfuatilia yule kijana ambaye alikuwa msimuliaji wa simulizi ile na alionekana kabisa kwamba alikuwa makini kwenye upande wa utulivu wa akili yake, hakuwa sehemu ya wale vijana ambao walikuwa wakikurupuka.

Kijana yule alikuwa anatembea taratibu kwa sababu alikuwa akiifahamu ile mitaa ya Tandika, hakuwa mgeni sana maeneo yale. Kwenye kukatiza mitaa alikutana na watoto wa mjini, watoto ambao huwa wanaamini kwamba mitaa yote ya jiji ni yao na wao ndio ambao wana haki nayo.

“Toa pesa uende zako mtoto wa kike wewe’’ alifoka dogo mmoja ambaye kimtazamo alikuwa mdogo kwake.

“Acheni zenu, yaani mniibie kwenye mitaa yan….” kabla ya kufanikiwa kumalizia sentensi yake alikoswa na upanga ambao ulimpuliza kidogo kwenye paji la uso, hapo alitambua kwamba ameingia kwenye mikono ya panya road hivyo aligeuka ili akimbie ila hakujua kama kuna wengine wawili walikuwa nyuma yake wakiwa wameshika bisibisi kwenye mikono yao. Kijana ambaye mwili wake ulikuwa na mavazi ya hovyo aliirusha bisi bisi moja na kutaka kuitoboa shingo ya kijana huyo ambaye alikubali kwa sababu hakuwa na namna ya kufanya lakini kabla ile bisibisi haijafika kwenye shingo yake ule mkono ulidakwa na kuvunjwa.

Sehemu ya tatu mpaka hapa, sina la kuongeza tena.

Febiani Babuya.

Previoua Next