HADITHI: SIKU ZA MWISHO
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WhatsApp: +255621567672
Email: [email protected]
UMRI: 18+
SEHEMU YA NNE
Alitoa sauti ya majuto na kelele za maumivu ila hazikudumu baada ya kupigwa kwenye shingo mpaka ikazunguka. Wengine ndipo walishtuka na kutambua kwamba walikuwa wamevamiwa hivyo wakahitaji kumshambulia mwanaume yule kwa pamoja ila hawakufua dafu kwa sababu aliivuta bastola yake na kuwatandika wote risasi za vichwa. Yule kijana msimuliaji aliogopa mno kiasi kwamba alibaki amejikunyata akiwa hana hata uwezo wa kukimbia kwakuwa alitambua kwamba naye ni lazima afe kwa namna yoyote ile. Aliinua uso wake kwa wizi ndipo akashangaa baada ya kumuona vizuri yule mtu, ni mtu ambaye alimuona kule kwa mama ntilie ila hakumtambua kwamba alikuwa ni nani, bwana mdogo huyo alikuwa ni mzuri mno kwenye kuyasimulia na kuyapanga maandishi kwenye maelezo ila alikuwa muoga kwenye uhalisia. Maisha ya watu kama ambao alikuwa akiwazungumzia yeye ni marahisi kuyaelezea kwa maelezo mafupi tu ila kuyaleta kwenye maisha ya kweli yanakuwa magumu isivyo kawaida.
“Unaitwa nani bwana mdogo?’’ ilipenya sauti nzito yenye mamlaka kwenye masikio yake.
“Steven” alijibu akiwa anatetemeka.
“Una familia?”
“Ndiyo, naishi na mdogo wangu”
“Unawajua watu ambao ulikuwa unawazungumzia kwenye ile simulizi yako?”
“Hapana, mimi yale niliyasoma kwenye kitabu tu”
“Leo umebahatika kukutana nao kwenye maisha yako” alibaki ameduwaa akiwa kama vile haamini.
“Wewe ni mmoja wao?”
“Ndiyo”
“Kwanini umenifuata mimi?” alianza kutetemeka kwa sababu alikuwa anaijua historia ya watu hao na namna walivyokuwa wanayafanya mambo yao hivyo hapo alitambua ni lazima ufe.
“Hilo swali nitakujibu siku nyingine ila nina maelezo mafupi ya kukupatia na baada ya hapo hautatakiwa kuja kuongelea haya mambo sehemu yoyote ile na ikiwezekana hii mitaa unatakiwa kuhama usiku wa leo”
“Kwanini nifanye hivyo?”
“Kwa sababu kuanzia sasa wewe unaenda kuwa mmoja wetu”
“Whaaaaat?” alibaki ameshangaa lakini bwana huyo aliingiza mkono mfukoni na kutoa bunda mbili za pesa na kadi ndogo.
“Hizo pesa ni milioni hamsini za kitanzania japo zipo kwa mfumo wa dola na hilo bunda dogo ni milioni tano za kitanzania. Hama hii mitaa bila kumuaga mtu yeyote na uende sehemu kubadilisha maisha yako na baada ya wiki piga kwenye hiyo namba kisha jitambulishe kwamba mimi ni Steven” kijana huyo ni kama bado alikuwa haelewi mambo yanavyo enda, alikuwa na maswali mengi mno kwenye ubongo wake lakini wakati huo huo alibaki amepigwa na bumbuwazi, wakati ambao alikuja kushtuka yule bwana hakuwepo sehemu ile, alikuwa ni yeye na anga tu wanatazamana, alizoa zile pesa na kukimbia nazo huku moyoni akiwa na furaha. Ipo hivyo siku zote, maskini akizipata pesa za ghafla jambo la kwanza huwa ni furaha bila hata kuwaza madhara ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na zile pesa ambazo amezibeba.
Zile risasi ambazo zilipigwa pale kutokana na makelele hazikueleweka zimetokea wapi hali ambayo iliwafanya watu wengi eneo lile kuzikimbia biashara zao kuhofia usalama wao jambo ambalo lilikuwa ni fursa kubwa kwa wezi wa mtaani pale. Muda mfupi baadae eneo lile lilikuwa limejaa polisi ambapo waliikuta miili ya vijana ambao walitambulika kama vibaka ikiwa haina uhai na mhusika asijulikane ni nani. Mtu ambaye alikuwa amefika lile eneo na kufanya yale yote alikuwa ni mwanaume mmoja ambaye alifahamika kama Mabanzi Mkwambe, alikuwa ni mwalimu wa Jabari huyu mtaalamu na ndiye ambaye alimfanikisha Jabari kujiunga na jamii yao ya the GL’s.
DODOMA
Mji mkuu wa taifa la Tanzania, eneo moja ambalo linazidi kukua kwenye upande wa biashara kila siku kutokana na upanukaji wa mji na uongezekaji wa huduma za kijamii na maendeleo kwa ujumla. Ni moja ya sehemu ambazo taifa linaziangalia kwa jicho pana kuwa kama moja ya sehemu kubwa za kibiashara kwa baadae kitaifa.
Eneo hilo kutokana na umuhimu wake limekuwa likikumbwa na baadhi ya changamoto kadhaa za kihalifu, sababu kubwa ni kwamba kuna watumishi wengi wa serikali hivyo hata mzunguko wa pesa upo. Sababu hiyo imepelekea eneo hilo kujazwa maafisa usalama wengi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kunakuwa safi kabisa na shughuli hizo za kihalifu zinaweza kupungua kama sio kudhibitiwa kabisa. Licha ya uwepo wa maafisa hao usalama ambao ni wengi lakini bado eneo hilo imekuwa ngumu kuweza kulirejesha kwenye hali ya amani kama mwanzo kwa sababu sio kila ambaye anatambulika kama afisa usalama basi kweli ni afisa usalama.
Imejitokeza jamii ya watu wengi, jamii ambayo inawagawa watu kwenye makundi matatu na ndiyo ambayo inafanya mambo yanakuwa magumu ndani ya eneo hilo. Jamii ya kwanza ni ya watu hao wa serikali ambao ni watu wa usalama, jamii ya pili ni wahalifu ambao nao wanaishi kwenye mgongo kama watu wa usalama pia na jamii ya tatu ni ya raia wa kawaida ambao kwa asilimia kubwa ndio wanategemea mamlaka kuweza kuwalinda nyakati zote. Uwepo wa jamii ya wahalifu ambao wanapora na kuua kwa kivuli cha kudai kwamba ni maafisa usalama kimefanya eneo hilo kutokuwa salama.
Mpaka wakati mambo yanakuja kuharibika zaidi, tayari ndani ya eneo hilo kulikuwa na miili ya watu hamsini ambayo haikuwa na uhai. Thelathini kati yao walikuwa ni watumishi wa serikali, kumi walikuwa ni wafanya biashara wakubwa na kumi ambao wanabaki walikuwa ni raia wa kawaida tu. Kuzuka kwa yale mauaji ndiko ambako kunafanya serikali ifanye maamuzi magumu, wale maafisa wa kule Dodoma kazi ilikuwa inaelekea kuwashinda ndiyo maana mpaka watu wote hao wakawa wanauawa mbele yao na hawana taarifa juu ya wahusika wa matukio hayo na hatua ambazo zilikuwa zinaenda kufuata baada ya hapo.
Timotheo Ganze, ndilo jina ambalo lilijitokeza kwenye ramani ya watu mhimu wa serikali ambao walitakiwa kwenda kuishughulikia hatari hiyo kwa taifa. Ni mauaji ambayo yalianza kukemewa kwenye mitandao ya kijamii, mauaji ambayo yalianza kuchafua taswira ya taifa kwa ujumla kwa sababu ilionekana kama serikali imetoa baraka kwenye mambo hayo ambayo yalikuwa yakifanyika.
Saa sita na dakika kumi na tano ndio muda ambao shababi mmoja ambaye alikuwa na begi lake dogo mkononi alikuwa anaingia ndani ya mji huo mkuu wa Tanzania. Alifika eneo hilo kwa ndege na hakuna hata mtu mmoja ambaye alikuwa ameenda kumpokea, bwana huyo muonekano wake ulikuwa nadhifu lakini usio na utulivu, kwa mwonekano wake alionekana kuwa kama mfanya biashara maarufu ndani ya eneo hilo la Dodoma. Baada tu ya kufika ndani ya eneo hilo alijua kwamba ana kazi moja kubwa, alitaka kuwa maarufu kwanza kwenye midomo ya watu na kazi yake ilikuwa inaanzia hapo.
Kwa watu ambao wanautafuta umaarufu wa haraka maeneo kama hayo, sehemu sahihi huwa ni kuanzia kwenye kumbi kubwa za starehe. Mwanaume huyo aliingia kwenye kumbi moja kubwa ya starehe na kuanza kutamba na kumwaga pesa, alizitumia pesa mpaka wenyeji wakamkoma hilo eneo. Mpaka inafika asubuhi ya kesho yake jina lake lilianza kutajwa kwenye midomo mingi ya wapenda starehe wakiambizana kwamba kuna bosi mpya wa kuangaliwa kwa umakini alikuwa ameingia jijini. Hakuishia pale tu bali hata kesho yake tena alienda sehemu nyingine ghali zaidi na kufanya yaleyale ambayo aliyafanya jana yake, umaarufu wake ndani ya siku mbili tu ukazidi kuwa mkubwa ungehisi kwamba alikuwa ni mtu ambaye alikuwepo hilo eneo kwa miaka kumi nyuma, pesa inaongea bwana.
Lengo lake kubwa alitaka kufahamika kila kona ya jiji kwakuwa aliamini kwamba wale wahalifu walikuwa wakidili na watu wengi wenye mafanikio, walikuwa ni watu ambao kwa mtazamo tu walionekana kuweka maslahi mbele kwanza kisha mwingine ambaye angeingia kwenye mikono yao basi wangemmaliza haraka ili kulinda siri zao. Umaarufu wa ghafla wa bwana yule kwenye kumbi za starehe uliwafanya baadhi ya watu kumuonea huruma kwani alikuwa anaingia kwenye dunia ambayo hakuwa akiitambua ila hawakuwa na taarifa za aina ya mtu ambaye walikuwa wanamuonea huruma.
Siku ya tatu ambayo alikuwa amedhamiria kuanza rasmi kuifanya kazi yake ndani ya hilo jiji, kuna kitu kama kilimshangaza japo hakuwa na uhakika nacho. Kwenye kasino moja kubwa ambalo alikuwa anaingia usiku huo alipishana na mtu wa makamo, ni sura ambayo alikuwa anahisi kuifahamu tangu hapo zamani lakini hakuwa na uhakika kwa sababu ya uharaka ambao ulitumika kuonana na mtu wake na kwa sababu ilikuwa sehemu ya starehe basi hakuona haja ya yeye kuumiza kichwa juu ya jambo hilo hivyo akawa anasogea ndani zaidi ya eneo hilo ambapo alipokelewa na wapambe kwa sababu jina lake walikuwa nalo kwa siku mbili za nyuma hivyo waliamini kwamba uwepo wa huyo mtu hilo eneo usingekuwa bure bali wangepata ulaji na unywaji kwa raha zao.
Sehemu ya nne inafika tamati hapa.
Febiani Babuya.
Comments