Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: SIKU ZA MWISHO 

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA 

WhatsApp: +255621567672

Email: [email protected] 

UMRI: 18+

SEHEMU YA TANO 

Lakini kabla ya utulivu kuchukua nafasi yake, zilisikika kelele kutoka upande wa juu ya eneo hilo. Ni vyumba vya VVIP ndiko ambako kelele zilikuwa zinatokeea. Kelele hizo zilikuwa zimetoka kwa mwanamke mmoja mrembo mno tena akiwa uchi kabisa. Mdada huyo alikuwa anakimbia kana kwamba alikuwa amekutana na mabomu ya boko haramu ana kwa ana jambo ambalo halikuonekana kuwa la kawaida. Timotheo alihisi kuna kitu hakipo sawa hivyo alikimbilia kwenda kwenye ile sehemu kuweza kujua ni kipi kilitokea huku yule mdada ambaye alikuwa anakimbia akishikwa na walinzi ili aweze kusaidia kutoa maelezo kwamba ni jambo gani ambalo lilikuwa limetokea mpaka awe kwenye hali kama ile.

Baada ya kufika kwenye kile chumba, kulikuwa na tukio la kutisha, ni mwanaume mmoja mbavu kidogo alikuwa ameuawa kwa kuzamishiwa kisu kwenye moyo wake. Mwili ulikuwa na majeraha na sehemu kadhaa ambazo zilikuwa zimeiva bila shaka ni kwa nguvu ya ngumi ambazo zilikuwa zinapenya kwenye ule mwili ila haikujulikana kwamba alipigwa na nani na kwa sababu zipi basi hapo ikalazimu yule binti aitwe. Binti yule akiwa analia na kutetemeka alidai kwamba walikuwa wakifanya mapenzi humo ndani mpaka alipo ingia mwanaume mmoja, yeye hakupata nafasi kubwa ya kushuhudia yaliyo tokea kwa sababu yule bwana ambaye aliingia humo ndani alimzimisha na kubaki na huyo mwanaume wake ambaye alikuwa akifanya naye mapenzi. Muda mfupi baadae baada ya yeye kurejewa na fahamu zake ndipo alizinduka na kukutana na hayo mauaji ambayo yalionekana kumtisha na kumnyima raha.

Sasa muuaji alikuwa nani? Timotheo alishtuka na kugundua kwamba haikuwa bahati mbaya kupishana na yule mtu ambaye yeye alihisi kwamba aliwahi kumfahamu kwenye maisha ya huko nyuma. Akiwa sehemu kama ya watu wa kawaida ambao walikuwa kwenye eneo lile muda ambao hata polisi walikuwa wanaingia aliamua kutoka nje haraka, hakukuwa na shida kuweza kutoka kwa wakati huo kwa sababu kila mtu alikuwa kwenye taharuki, mauaji yalileta hofu ndani ya eneo hilo huku watu wengine wakiwa wanaondoka ili wasije kuhusika kwenye hiyo kesi hivyo ilikuwa rahisi kwake. Alifanikiwa kufika mpaka nje lakini hakukuwa na dalili za kuweza kumuona yule mtu wake ambaye alikuwa anahisi alimuona.

Hali hiyo ilimfanya arudi ndani, kurudi ndani alimfuata meneja moja kwa moja na kumvutia pembeni ili apate msaada. Bwana huyo aligoma hivyo alimshawishi meneja na kudai kwamba anafuatilia kesi ya mauaji ndipo alipo amua kukitoa kitambulisho na kumuonyesha, hata meneja mwenyewe alishtuka, alikuwa ni afisa wa ngazi za juu wa usalama wa taifa. Shida yake kwa meneja huyo ilikuwa ni kuhitaji video za marejeo kwa sababu kuna mtu alikuwa anahitaji kumuona ili aweze kujiridhisha kama mawazo yake yalikuwa sahihi na sio kuishi kwa hisia tu. Hakukuwa na namna nyingine kwani alihitaji kuona video ile kabla haijatua kwenye mikono ya polisi ambao mpaka wakati huo ndo kwanza walikuwa wameanza kuukagua ule mwili wa marehemu.

Kwenye video ambayo alikuwa anaiangalia, watu ni wengi ambao walikuwa wanaingia na kutoka kwenye yale maeneo lakini alishtuka kwa mara nyingine baada ya kumuona yule mwanaume ambaye alihisi anamfahamu. Mwanaume yule aliingia ndani ya ile sehemu na kutoka baada ya dakika kumi tu tena mwili wake ukiwa msafi kabisa, hakuna sehemu hata moja ambayo ilikuwa na tone hata la damu. Alitabasamu kwa wakati mmoja lakini moyo wake ni kama ulishikwa na ganzi kwa wakati huo huo kwa mara nyingine tena kwa sababu ya jambo ambalo alilishuhudia. Aliitoa simu yake mfukoni ili kuweza kujiridhisha zaidi asije kuwa anahisi vibaya, hisia zake zilikuwa sahihi kabisa.

OTHMAN CHUNGA, yule mtaalamu wa zamani, moja kati ya viongozi wa familia ya Gavin Luca ndiye ambaye alionekana kwenye hiyo sehemu, umri kidogo ulikuwa unazidi kwenda ila mwonekano wake haukuwa haba kwa sababu ya mazoezi ambayo yalikuwa yanalishwa kwenye mwili wake. Timotheo alijihakikishia kwamba ni kweli yule alikuwa ni Othaman ndiyo maana hata sura yake haikuwa ngeni. Alijikuta akiwa na maswali mengi ambayo hata majibu yake hayakueleweka kwamba yalikuwa ni yapi na angeyapatia kwa nani.

Othman alikuwa na shida gani na huyo mtu mpaka amuue? Othman alikuwa wapi kwa nyakati zote hizo na ni sababu ipi ilimfanya aje kutokea nyakati kama hizo na eneo kama hilo ambalo lilikuwa na kamera na alijua kabisa kwamba sura yake itaonekana? Familia yake nyingine ilikuwa wapi kwa wakati huo na muda wote ambao ulikuwa umepita? Hakuwa na majibu ya maswali yake na aligundua kuendelea kupoteza muda kwenye eneo hilo ilikuwa ni kuendelea kuuweka wazi utambulisho wake kwa watu ambao hawakutakiwa kumjua kwamba yeye ni nani na alikuwa Dodoma kwa sababu ya kufanya jambo gani japo aliondoka kinyonge ndani ya hilo eneo akimtaka meneja huyo asije kumtambulisha yeye kwa mtu yeyote yule hata hao askari wa polisi kwa sababu hawakupaswa kumjua.

Timotheo kuwa na wasiwasi alikuwa sahihi kwa upande wake kwa sababu ya ujio wa hao watu wapya, ni watu ambao walikuwa na historia ndefu mno na ya kutisha ndani ya taifa lao. Ndiyo ilikuwa familia maarufu zaidi kwenye historia nzima ya taifa la Tanzania kwahiyo aliona kuna hatari kubwa ambayo ilikuwa inakuja kwa mara nyingine baada ya miaka kadhaa tu ya amani ndani ya mipaka ya Tanzania. Ilikuwa imepita miaka mitatu, miaka ambayo ilifanya watu wasahau yale maswaibu na shida ambazo walizipata huko nyuma, zile zama za kuhofia kila siku kuokota miili ikiwa haina uhai zilikuwa zimeisha, zile zama hazikuwepo tena kwa wakati huo na ndio muda ambao familia hiyo ilipoteaga moja kwa moja kwenye masikio na macho ya watu.

Ni wakati ambao haikutambulika familia hiyo iliendaga wapi kiasi kwamba hakuna taarifa hata moja ambayo iliwahi kuvuja kutoa utambulisho wa sehemu ya uwepo wa hao watu hivyo kutokea kwa Othman tena eneo ambalo alijua kwamba lilikuwa na kamera nyingi kama hilo, ilikuwa ni ishara mbaya kwa mtu kama yeye ambaye alikuwa anatambua namna mambo kama hayo yanavyokwenda. Alikumbuka kitu kuhusu mtu huyo, sura yake haikutakiwa kufika kwenye mikono ya polisi hivyo alirudi haraka kwa yule meneja na kuudai ule mkanda wote ambapo aliondoka nao kabla hata wale polisi hawaja unasa rasmi naye akatoka eneo hilo.

Timotheo kwenye tafiti yake ambayo ilikuwa inafuata aliyapata majina ya watu wanne, majina ya watu ambao waliaminika kwamba walikuwa ndio wahusika wakuu wa yale matukio ya mauaji ndani ya Dodoma. Kazi yake ya kutamba kwenye kumbi za starehe iliweza kumrahisishia upatikanaji wa taarifa hizo ambazo alizipata kwa malaya mmoja muuza mwili ambaye alidai kwamba alikuwa akitumiwa na watu hao pale ambapo wangehitaji kufanya naye mapenzi au kama kungehitajika kuteka watu hususani wa serikali ambao mbele ya wanawake huwa wanatekwa kirahisi tu.

Taarifa hizo kwake zilikuwa za dhahabu, zilimfanya kuona kazi yake imekuwa nyepesi kuliko hata ambavyo alifikiria hivyo alikuwa anasubiri usiku uende ndipo aweze kuvamia eneo ambalo aliambiwa kwamba watu hao walikuwa wakipatikana. Saa saba na dakika hamsini na tano usiku, kabla ya muda mfupi ambapo aliambiwa kwamba kesho yake watu hao walikuwa wanapanga kumuua mkuu wa mkoa wa Dodoma ndipo aliweza kutua miguu yake kwenye nyumba ambayo walidaiwa kuwepo hao watu.

Timotheo alikuwa ni mtu mmoja ambaye kazi yake ilikuwa zaidi ya uwepo wa watu hata kumi ndiyo maana licha ya kuiona hatari ambayo ilikuwa mbele yake, bado alihitaji hiyo kazi kuifanya mwenyewe bila uwepo wa mtu mwingine yeyote yule. Kwenye apartment moja kubwa ya kifahari ndilo eneo ambalo alipewa taarifa kwamba hao watu wake walikuwepo, alifika akiwa amejiandaa kwa ajili ya kukabiliana na kila hali ambayo angeikuta hapo japo yale ambayo aliyakuta yalikuwa ni tofauti na yale ambayo yeye aliyatarajia. Kwanza geti la eneo hilo lilikuwa wazi kabisa, hakukuwa na dalili zozote za uwepo wa mtu getini hali ambayo haikuwa ya kawaida ukizingatia ulikuwa ni usiku wa manane.

Aliitoa bastola yake na kuingia kwa tahadhari ambapo mlango wa ndani pia ulikuwa wazi kama getini, jambo hilo lilimpatia taarifa na kuelewa kwamba mazingira hayo kwa wakati huo hayakuwa salama, ilikuwa ni hatari kubwa ambayo huenda ilikuwa mbele yake. Alitembea haraka haraka mpaka mlangoni ambapo aliingia kwa sarakasi moja na kuibukia upande wa pili lakini palikuwa patupu. Taa ya ndani ilikuwa imewaka ila hakuona mtu kwa sababu macho yake yalikuwa yakiangaza kila kona kuweza kutambua kama kulikuwa na hatari yoyote aweze kukabiliana nayo vizuri.

Alianza kutembea taratibu mpaka alipohisi kwamba amekanyaga kitu kwa buti lake ikamlazimu kuangalia sehemu hiyo ilikuwa na nini. Alijikuta akishtuka kwa hofu baada ya kutambua kwamba ameukanyaga ni mwili wa mtu. Hata baada ya kuangalia vizuri, aligundua kwamba haukuwa mwili tu bali ilikuwa ni miili. Eneo hilo lilikuwa na miili ya watu wanne ambao waliuawa kikatili sana huku ikiwa imerundikwa sehemu moja, aliangalia kwa umakini na kutambua kwamba miili hiyo bado ilikuwa ya moto maana yake muuaji hakuwa mbali, alikuwa mazingira hayo hayo na hivyo kupelekea hata yeye usalama wake kuwa mashakani japo hakuonekana kulijali hilo zaidi ya kuhitaji kumpata muuaji huyo kabla hajafanikiwa kutoroka.

Alitoka nje haraka akiwa anaonekana kuwahi jambo, aliangaza upande wa mbele na hakuona mtu hivyo akataka kuzunguka upande wa nyuma wa apartment hiyo ili aweze kuona kama mtu wake alikuwa huko ila baada ya kusogeza hatua mbili mbele alisikia sauti ya mguno nyuma yake. Aligeuka kwa kasi kubwa akiwa ameinyoosha bastola yake akafanikiwa kuona jambo la kushangaza ambalo lilimshtua kwenye moyo wake. Othman Chunga ndiye ambaye alikuwa amesimama mbele yake akiwa ameiweka mikono yake nyuma. Alijikuta akiwa na maswali mengi ila hakuelewa ni swali gani lilikuwa sahihi kuanza nalo, hakuona ni jambo lipi alipaswa kuongea na bwana yule ukiacha tu kutokuelewa uwepo wake eneo hilo na kwamba tarifa hizo yeye alikuwa anazipatia wapi.

“Othman upo chini ya ulinzi”

“Wewe hapo ndo unataka kunikamata mimi?”

“Una haki ya kubaki kimya mpaka pale mwanasheria wako atakapofika, unakamatwa kwa kuhusika na mauaji ya watu watano” alitabasamu akiwa anamsogelea Timotheo ambaye alikuwa akirudi nyuma taratibu japo mkononi yeye ndiye alikuwa na bastola.

Sehemu ya tano sina la ziada mpaka wakati ujao.

Febiani Babuya.

Previoua Next