SURA YA PILI
Kigoma, Tanzania — 2016
Mwanga wa alfajiri uliingia taratibu ndani ya nyumba ya matofali ya udongo, ukichungulia kupitia pazia la kitenge lililozeeka. Sauti ya jogoo ilisikika kutoka nje, ikichanganyika na mlio wa mawimbi ya Ziwa Tanganyika yaliyopiga taratibu ukingo wa maji. Mbali kidogo, sokoni, wanawake walikuwa wakifungua vibanda vyao, wakitayarisha samaki wa kukaanga na maandazi ya asubuhi.
Ndani ya chumba kidogo kilichokuwa na kitanda cha mbao na kabati la zamani, Hadija aliketi kwenye godoro huku akifunga mkufu wa shanga shingoni mwake. Alikuwa amerudi Kigoma baada ya kumaliza masomo yake, na leo alikuwa na jambo muhimu sana la kuwaambia mama yake na wadogo zake.
Alijishughulisha na kazi za asubuhi — alifagia uwanja, akapiga deki, na kusaidia mama yake kutandika samaki sokoni. Baada ya kazi hizo, waliketi kwenye mkeka nje ya nyumba, wakinywa chai ya rangi na vitumbua.
"Mama," Hadija alianza kwa sauti ya upole, akimwangalia mama yake aliyekuwa akichungulia barabara kana kwamba anangoja mteja wa dagaa. "Nina jambo nataka kukuambia."
"Sema mwanangu," Mama Asha alijibu bila kumtazama, macho yake yakiwa yamejaa mawazo.
"Nikiwa Dar es Salaam, nilikutana na kijana mmoja. Anaitwa Juma. Ni mtu wa kazi, ana ndoto kubwa, na ananipenda kweli. Alisema atakuja Kigoma kunichumbia mara tu atakapopata nauli."
Mama Asha alisimama taratibu, akimgeukia binti yake.
"Juma? Anafanya kazi gani?" aliuliza, akikunja uso.
"Ni mchoraji. Lakini pia alikuwa akifanya kazi za mjengo ili kujikimu. Ana moyo mzuri, mama. Ana nia ya dhati ya kunioa."
Mama Asha aliguna, akifuta mikono yake kwenye khanga aliyovaa.
"Mapenzi hayawezi kulisha familia, Hadija. Unasema anafanya mjengo? Atakuletea matofali badala ya chakula?"
"Lakini mama, mapenzi ni zaidi ya pesa..." Hadija alijaribu kusema, lakini mama yake alikatisha mazungumzo.
"Tutazungumza baadaye," alisema, kisha akarudi sokoni.
Hadija alibaki akitazama nyuma ya mama yake, machozi yakianza kumtoka taratibu.
---
Simba Anaingia Kijijini
Wiki chache baada ya Hadija kurejea Kigoma, hali sokoni ilibadilika. Habari zilienea haraka kwamba mfanyabiashara mkubwa kutoka Dar es Salaam alikuwa amefika mjini kwa shughuli za biashara ya samaki.
Alikuwa Rashid — mwanaume mwenye umri wa miaka 38, mrefu, mweusi, na mwenye mwili uliojengeka vizuri. Alivaa suti za gharama, akitembea na walinzi wawili kila mahali alipoenda. Magari mawili ya kifahari yalikuwa yakiendeshwa barabarani kama msafara wa kifalme kila alipohama eneo moja hadi jingine.
Siku moja, Rashid alikwenda sokoni kutafuta samaki wakavu wa kusafirisha Dar es Salaam. Alipokuwa akitembea kati ya vibanda, macho yake yaliangukia kwa msichana mmoja aliyekuwa akimsaidia mama yake kupanga dagaa kwenye sinia.
Hadija.
Macho ya Rashid yalibaki yamekodoa, moyo wake ukipiga kwa kasi. Hakuwahi kuona msichana mzuri kiasi kile. Uso wake ulikuwa na utulivu wa asili, macho yake makubwa yalimwangalia kila mtu kwa heshima, na mwili wake ulikuwa umefungwa kwenye khanga iliyomkaa kama alizaliwa kuivaa.
Alimsogelea taratibu, akijifanya anatafuta samaki.
"Shikamoo mama," alisema kwa sauti nzito, akimgeukia Mama Asha.
"Marahaba, karibu," Mama Asha alijibu kwa bashasha, akimtambua Rashid mara moja kutokana na sifa zake mjini.
"Natafuta dagaa wa daraja la kwanza," Rashid alisema, lakini macho yake hayakutoka kwa Hadija hata sekunde moja.
Hadija alihisi mwili wake ukitetemeka chini ya macho ya Rashid. Alijua aina ya wanaume kama hao — wenye pesa nyingi na tamaa kubwa.
---
Mtego Unategwa
Siku zilizofuata, Rashid alirudi sokoni kila siku bila sababu ya msingi. Alimletea Mama Asha zawadi — sukari, unga, na hata pesa za matumizi. Hatimaye, aliamua kusema kilicho moyoni mwake.
"Mama Asha," Rashid alianza siku moja, wakiwa wamekaa kwenye kibanda cha mama huyo. "Nimependa sana binti yako. Ningependa kumuoa."
Mama Asha aliguna kwa mshangao, lakini kabla hajasema chochote, Rashid aliweka bahasha nene mezani.
"Hiyo ni shukrani ya kutaka nafasi ya kumjua zaidi," alisema, macho yake yakiangaza tamaa kali.
Mama Asha alifungua bahasha taratibu — ilikuwa imejaa noti mpya za elfu kumi.
Alimgeukia Hadija, ambaye alikuwa amesimama kando, macho yake yakiwa yamejaa woga.
"Hadija, usiwe mjinga," mama yake alisema baadaye walipokuwa nyumbani. "Huyu mwanaume ana pesa. Ataweza kutusaidia. Unataka kung’ang’ania yule Juma wa mjengo badala ya mtu kama Rashid?"
Hadija alilia usiku kucha, akifikiria maneno ya mama yake. Hakutaka kuamini kwamba maisha yake yalikuwa yamegeuzwa bidhaa ya kuuzwa sokoni.
Na wakati huo huo, Juma alikuwa anajitahidi Dar es Salaam, akihangaika kutafuta pesa ya safari ya kwenda Kigoma, bila kujua kwamba mtu mwenye fedha nyingi tayari alikuwa ameanza kumvua mpenzi wake kutoka mikononi mwake.
---
Kivuli Cha Kisasi Kimeanza Kuingia
Siku iliyoamuliwa Rashid aje rasmi nyumbani kwa Mama Asha kutoa posa, basi la Juma lilikuwa limeondoka Ubungo kuelekea Kigoma.
Safari ya mapenzi ilikuwa imeanza.
Lakini safari ya kisasi ilikuwa karibu zaidi.
Comments