Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

FOR YOU

Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

Rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA TISA

★★★★★★★★★★★★★


Sandra alikuwa haamini kama kweli pacha wake alikuwa na uhusiano na mwanamke huyu mwenye elimu sana na aliyemzidi umri. Ingekuwa kawaida kusema ni Xander kwa hiyo bila shaka aliweza kumzuzua, lakini bado ilimshangaza. Baada ya kuondoka kwenye jengo la ofisi, akampigia pacha wake na kumwambia atoke huko aliko haraka sana ili wakutane kuongelea jambo fulani la muhimu. Akamwambia wakutane nje chini ya mti fulani, na ahakikishe anakuwa mwenyewe hata akihitaji kumkimbia Sophia.

Basi, baada ya yeye Sandra kuwa amekwenda hapo, akasubiri kwa dakika kama kumi hivi naye Xander akawa amefika. Alikuwa anatembea taratibu kama kawaida ya Sandra, naye alikuwa anatabasamu kama kawaida yake akiwa Xander.

"Yaani masela wanavyonitazaaama... wananiitaiiita... hahahah... tako lako linakuwa kubwa kila siku," Xander akasema baada ya kufika.

"Xander... kuna jambo nataka kukuuliza..."

"Na mimi nataka kukuuliza, hivi nyie wasichana mna matatizo gani? Yaani kamishe kadogo namna ile mpaka mzungushe kwa Tobias awaletee ujumbe, sijui mrudishe tena... yaani ina maana..."

"Tulikuwa na maana yetu."

"Maana gani?"

"Principal ananitaka. Mimi simtaki kwa hiyo ndiyo maana..."

"Anakusumbua? Kwa nini hukuniambia?"

"Kwa nini nikwambie?"

"Ahahah... okay. Kwo' kama angekuja na kunishika tako langu, yaani lako, ningemwachia tu maana ningefikiri na ye' unampa!"

"Em' toka huko! Sitaki mazoea naye kabisa. Sema sikuona haja ya hilo maana sasa hivi hatanisumbua tena..."

"Mmmm na Tobias ndo' Clerk..."

"Potezea hilo bwana. Nini kinaendelea kati yako na madam Valentina?"

"Madam Vale... ayaaa!"

"Kwa nini hukuniambia kama unatoka naye?"

"Kwa nini nikwambie? Hii ndiyo sababu sikutaka tubadilishane simu. Nipe bana amesemaje..." Xander akaichukua simu yake kutoka kwa dada yake.

"Ameniita ofisini akaanza kunipa romance. Ehehee... this is incredible. Kwa hiyo unamla madam Valentina?"

"Ndiyo, na ni kitu ambacho sikutaka ujue. Namlaani aliyenihamishia kwenye mwili wako."

"Vipi kuhusu Ramla?"

"Agh, Ramla anazingua. Madam V namwelewa sana."

"Ila wewe!"

"Ayaa... dah!" akasema Xander kwa kusikitika huku akiangalia simu yake.

Sandra akasogea karibu na kuona ujumbe wa Valentina kwenye simu hiyo. Ulisomeka: Xander, najua hatujawa pamoja kwa muda mrefu, lakini nimevunjika moyo sana na kilichotokea. Sijui kama kuna kitu nimefanya kukukwaza, ila naomba ujue nakuhitaji. Hata kama itakuwa kwa kipindi kifupi tu, ni sawa. Lakini bado nakuhitaji sana wakati huu.

"Ndiyo ameandika essay yote hiyo? Umeshamlaza mara ngapi?" Sandra akamuuliza Xander.

"Kwani we' umemfanyaje?" Xander akamuuliza akiwa amekerwa.

"Sijamfanya kitu. Amevunjika moyo kwa sababu sijamfanya kitu. Sijui huwa mnafanyaga nini ofisini kwake, lakini mimi nisingeweza kufanya hivyo. Si tulikubaliana hatutakiwi kufanya na yeyote chini ya hii hali?" Sandra akasema kwa sauti ya chini.

"Sijawahi kufanya naye ofisini kwake bwana. Ina maana umeshindwa hata kumpiga denda tu?"

"Ni rahisi kwako kusema... Raymond akitaka kukubusu utakubali?"

"Namkata ngumi ya pua!"

"Sasa je!"

Ujumbe mwingine kutoka kwa Valentina ukaingia. Ulisomeka: Nitakusubiri same place after hours. Please come.

Sandra alikuwa anatazama upande mwingine sana, kwa kuwa kuna jambo lilimkera sana kutokea hapo. Sasa akawa amechoka.

"Mbona huyo kaka ananiangalia hivyo?" Sandra akauliza.

"Nini?"

Xander ndani ya mwili wa Sandra akageuka na kumwona Isiminzile akiwa amesimama usawa wa maduka ya pembezoni mwa uzio wa chuo. Akamwangalia Sandra tena.

"Toka nimefika hapa namwona tu. Ananiangalia sana. Labda anakupenda!" Sandra akasema.

"Huyo ni Isiminzile. Ni rafiki yangu, kwo' igiza unamjua maana anafikiri wewe mimi. Mwite umsalimie... ni mwoga-mwoga," Xander akamwambia.

Sandra akatii na kumwita kwa ishara, lakini Isiminzile akaondoka tu kama haikuwa yeye aliyeitwa.

"Ish! Huyo mtu vipi?" Sandra akashangaa.

"Ana swaga za kiboya, achana naye. Sikiliza Sandra. Namkubali sana madam V. Sina jinsi ila kumwambia kinachoendelea..." Xander akasema.

"Nini? Yaani bado hata hatujawaambia wazazi wetu halafu unataka kumwambia mtu wa nje?"

"Sina jinsi. Mambo... yapo tight. Mama birthday kesho, anataka twende shopping najua tutakaa huko weee! Lazima tuongee na Valentina kabla ya huo muda maana mambo yatakuwa mengi kufikia kesho, si unajua mama atahitaji tuwe karibu naye zaidi?" Xander akasema kwa hisia.

"Mh! Ndiyo kusema unampenda sana?"

"Ahah... ananifanya najihisi tofauti tu. Tafadhali kubali Sandra... for me..."

Sandra akatabasamu na kusema, "For you. Sawa. Kwa hiyo tunaenda ofisini kwake sasa hivi?"

"Hapana. Ameniambia tukaongee kwake. Tukitoka tu hapa twende," Xander akasema.

"Haya sawa. Kwa hiyo wa kwanza kujua atakuwa madam Valentina. Lakini bado hatujui suluhisho la tatizo hili, sijui hata kama kuna suluhisho. Umeshafikiria itakuwa vipi kama tutakaa namna hii maisha yetu yote?" Sandra akaongea kwa hisia pia.

"Sijui kwa kweli. Lakini acha tu tuwe na imani. Mambo yatakaa sawa," Xander akasema.

Kisha akamshika Sandra kiganja kama kumtia moyo, nao wote wakapeana tabasamu la imani.


★★


Muda ulikwenda haraka. Mpaka inafikia mida ya saa 9 mchana, mapacha walijitahidi sana kukaa kwa ukaribu, wakiwa makini kutenda kwa njia "zao" za kawaida mbele ya wengine. Walikuwa wamekubaliana kubadilishana simu, lakini wangeambiana yaliyojiri kila mara ambapo wangetafutwa na watu waliowafahamu. Wakaahidiana kutoharibiana chochote kwenye simu zao, na nyakati ambazo wangekuwa sehemu moja, basi wangerudishiana simu mpaka muda ambao wangetengana tena.

Xander alikuwa amejibu ujumbe wa Valentina, akisema angekwenda kwake ili waongee vizuri. Lakini hakumwambia kwamba angeenda na dada yake ili kutomshangaza mapema. Raymond aliwasiliana mara kadhaa na Sandra, na hata Ramla bado alikuwa akijaribu kumwomba samahani Xander ili mambo kati yao yakae sawa, lakini kijana akaendelea kumpuuzia.

Baada ya muda fulani, Xander aliliona gari la madam Valentina likiondoka hapo chuoni, naye akamuuliza kwa ujumbe ikiwa ingekuwa sawa akimfata muda huo. Valentina akapiga simu, kwa hiyo ikabidi Sandra ndiyo aipokee ili wazungumze na kumfikirisha anayeongea naye ni Xander. Valentina akamwambia kwamba ndiyo alikuwa anaelekea nyumbani, hivyo kama alikuwa anataka kuja muda huu basi amfate. Xander (Sandra) akakubali, kisha akamwambia kaka yake kile madam alichosema.

Kwa kuwa hawakuwa na kipindi kingine, wawili hawa wakaondoka pamoja kwa pikipiki ya Xander. Kiukweli watu kadhaa siku hii hawakujizuia kuwaangalia sana kwa sababu walikuwa karibu mno siyo kama sikuzote. Aliyewakazia uangalifu zaidi alikuwa ni Isiminzile, kwa kuwa alijua alichokifanya, lakini hakujua atumie njia gani ili kutambua nini kiliendelea baina yao kwa sababu aliogopa. Mapacha wakaondoka zao haraka kuelekea kwa madam.

★★

Haikuwachukua dakika nyingi nao wakawa wamefika. Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Sandra kufika hapa. Kipindi cha nyuma alikuja hapo mara kadhaa hasa yeye na rafiki zake walipopita kumsalimu madam wao. Aliwatendea kwa urafiki sana nao walimpenda mno. Kwa hiyo Sandra alimjua kwa kadiri fulani mwanamke huyu, na kujua kwamba Xander alitoka naye sasa ni kitu ambacho kilimshangaza kwa kuwa alihisi ni kama hawakufaana kabisa. Ila yeye hakuwa mtu wa kuhukumu hata kidogo na kuyaona yao kuwa yao tu.

Baada ya kuegesha pikipiki nje, wakaelekea getini na kubonyeza soketi ya kengele. Walikuwa wamesimama kwa kusubiri huku Sandra akimwambia Xander asiogope sana. Jamaa akamhakikishia kwamba hakuogopa, ila wasiwasi tu ndiyo ulimjaa maana hakujua Valentina angechukulia vipi suala hili lote. Mlango mdogo wa geti ukafunguka, na wote wakamwona madam Valentina hapo. Alishtuka kiasi kwa sababu hakutazamia kuwaona mapacha wote hapo, na maswali yakaanza kupita kichwani kwake.

Xander, akiwa ndani ya mwili wa Sandra, akamkanyaga Sandra akiwa kwenye mwili "wake" mguuni kidogo ili aongee haraka, naye akasema, "Madam V..."

"Alexander..." akasema Valentina, huku akiwa na uso wenye kuonyesha hali ya kutopendezwa.

"Huyu ni pacha wangu... anaitwa..."

"Alexandra, najua. Ambacho sijui ni kwa nini umekuja naye," Valentina akamkatisha.

Xander aliona kweli mwanamke alikuwa amekerwa. Sandra akaona asogee karibu zaidi.

"Ambacho nataka kukwambia ni muhimu sana. Na Xander... I mean, Alexandra, anahusika pia," Xander (Sandra) akamwambia.

Valentina akawakaribisha ndani. Alijihisi kama mjinga kiasi kwa sababu vijana hawa bado walikuwa wadogo kwake lakini waliingia kwenye maisha yake kwa pamoja ghafla na kufanya ionekane kama walikuwa wanataka kucheza nayo. Ijapokuwa alimruhusu Xander maishani mwake, hii haikuwa ruhusa kwake kuanza kuingiza na watu wengine ambao aliona hawakupaswa kujua lolote; hasa kwa kuwa ndiyo walianza tu mahusiano. Wasiwasi pia ulimvaa akitaka kujua ni nini ambacho Xander alihitaji kusema kilichofanya na dada yake ahusike, mpaka kusababisha lile jambo lililomvunja moyo ofisini kwake asubuhi hiyo.

Walipofika ndani, Valentina akaenda kuketi kwenye sofa, akiwaambia mapacha wakae pia. Lakini wakawa wamesimama tu huku wanamtazama, naye akauliza shida ilikuwa ni nini. Xander, akiwa kwenye mwili wa Sandra, akamfata na kupiga magoti chini, karibu kabisa na alipokaa, huku akivishika viganja vyake. Valentina akashangaa.

"Alexandra... unafanya nini?" akamuuliza.

"Madam V... ni mimi. Mimi ni Xander," akamwambia kwa hisia.

Valentina akakunja uso kimaswali.

"Wewe ni Xander? Unamaanisha nini, sikuelewi..." Valentina akasema.

"Mimi ni Xander. Yule pale ni Sandra. Kuna kitu kimetokea kimesababisha miili yetu ibadilishane... sijui ibadilishanwe... ibadilishwe, ah damn it! We've switched bodies," Sandra (Xander) akasema.

Valentina akawaangalia wote kwa njia ya kawaida tu. Mapacha wakawa wanasubiri kusikia atasema nini.

"Okay kwa hiyo... wewe pacha wa kike ni Xander, na yule Xander nayemwona ndiyo wewe wa kike. Natakiwa tu kukubali like, 'sawa karibuni intertwined siblings' kirahisi tu. Ni mchezo gani mnanifanyia?" Valentina akaongea kistaarabu.

"Hapana madam, ni kweli. Mimi ni Sandra. Nimeingia kwenye mwili wa kaka yangu. Na huyo aliye kwenye mwili wangu ni Xander. Hatuwezi kukudanganya," akasema Xander (Sandra).

Valentina alianza kucheka kwa sauti ya chini huku akitikisa kichwa chake. Aliona anayemwambia hivyo ni Xander, lakini kiukweli hali hii yote ilikuwa yenye kushangaza sana. Hakuelewa vijana hawa wamepatwa na nini. Xander alikuwa anamtazama kwa hisia sana, akijua pia kwamba haingekuwa rahisi kwake kuelewa.

"Kwa hiyo... uliruka tu... mlirukiana halafu mkaishia kubadilishana miili?' Valentina akauliza.

"Siyo rahisi kuamini, naelewa. Lakini ni kweli. Jana usiku kwenye ile dhoruba, kuna kitu kilitokea. Tulikuwa tu tumelala pamoja kwa sababu dada'angu alikuwa anaogopa... tumeamka asubuhi tunajikuta hivi..." Sandra (Xander) akamwambia huku bado akiwa amemshikilia viganja.

"Dhoruba? Ile mvua ndogo ya jana ndiyo ilikuwa dhoruba?" Valentina akauliza.

Xander na Sandra wakaangaliana. Huyu alikuwa mtu wa pili kukanusha kwamba mvua ya jana haikuwa kubwa kama walivyodhani.

"Okay masihara kwisha. Xander, nilifikiri tulipaswa kukutana mimi na wewe peke yetu hapa. Sijui ni kituko gani mnataka kunifanya nionekane lakini sijapenda. Unanifanya nionekane kama mtoto mdogo. Kama unatafuta njia ya kuachana nami, niambie tu. Haya yote ya nini?" Valentina akauliza akiwa anamwangalia Xander (Sandra).

Xander, akiwa kwenye mwili wa dada yake karibu na Valentina, akamshika usoni kwa viganja vyake.

"Hapana siyo hivyo... Valentina... tafadhali niamini. Ni-test basi. Tu-test sisi wote. Kumbukumbu zetu ziko pale pale ila ni miili tu ndo' imebadilishwa. Please..." akamwomba.

Valentina akamtazama msichana huyu aliyekuwa anamwambia kwamba ndiyo mpenzi wake. Akamwangalia na "Xander," akiwa eti ndiyo "Sandra." Bado alihisi ni kama wanamchezea, lakini akaona afuate ushauri huu.

"Okay. Mara ya pili uliponishika na kunibusu, ilikuwa ni wapi, na ni nini kilifata baada ya hapo?" Valentina akauliza.

"Ilikuwa ofisini kwako. Na ilikuwa ni busu tamu sana ambayo sitasahau. Aam... principal aliingia, na mimi ikabidi niyaangushe mafaili yako chini... nikaanza kuyaokota ili kuficha... you know..." Sandra (Xander) akamwambia huku anatabasamu kwa mbali.

Valentina akamtazama sana, kisha akamwangalia yule aliyemwona kuwa Xander.

"Natumaini huwa haumwambii dada yako kila kitu ambacho mimi na wewe tumefanya," Valentina akamwambia, akiwa bado haamini.

"Hapana hajaniambia. Najua unaniona kama Xander, lakini mimi ni Sandra," Xander (Sandra) akasema.

"Ndiyo Valentina. Siwezi kumwambia Sandra kuhusu mambo yote yaliyotokea baina yetu. Lakini... kwa kuwa nahitaji kukufanya uamini... Unakumbuka mara ya pili tume... make love... nilikunong'oneza maneno gani sikioni ukasema nirudie?" Sandra (Xander) akamuuliza.

Valentina akabaki tu kumwangalia.

"Sandra" huyu akamsogelea sikioni na kumnong'oneza, 'Te amo, cariño.'

Kisha akajitoa sikioni kwake na kumwangalia tena machoni. Bado Valentina alikuwa amechanganyikiwa.

"Siwezi nikamwambia hivyo Sandra. Ni wewe tu," Sandra (Xander) akasema.

Valentina akamtazama sana "Xander" kule aliposimama. Hakuelewa nini kilikuwa kinaendelea.

"Madam, mimi ni Sandra. Unakumbuka wakati ule unatupa training usiku nyuma ya ile deck tuliona nini mpaka Asha akazimia? Na ukatuambia tusimwambie yeyote?" Xander (Sandra) akamuuliza Valentina.

Sasa Valentina akawa ameshibitishiwa hata zaidi kwamba huu ulikuwa ni ukweli. Lakini bado hakuelewa iliwezekanaje. Akawa anawatazama sana.

"Mh! Ni kitu chenye kushangaza sana. Kwa hiyo... miili yenu ime-switch vipi?" akawauliza.

"Hata sisi hatujui. Na bado hatujawaambia wazazi wetu. Xander alihofia labda utamchukia kwa kuwa kilichotokea asubuhi leo ofisini kwako... ilikuwa ni mimi. Yaani... wewe ulifikiri unanibusu mimi kama Xander na nilikuwa sijui kuhusu uhusiano wenu ndiyo maana nika-act namna ile. Sorry for that..." Xander (Sandra) akasema.

Valentina akamtazama aliyemwona kama Sandra.

"Xander..." Valentina akamwita.

"Naam..." akaitika, kwa sauti ya kike kabisa.

"Ahah... unbelievable!" Valentina akaongea kwa kustaajabu.

Xander akamkumbatia. Valentina bado aliona ni kama anakumbatiwa na Sandra lakini sasa hakuwa na jinsi ila kuzoea hali hii mpya. Xander akamwachia na kukaa naye karibu kwenye sofa.

"Kwa hiyo sasa, mtafanyaje?" Valentina akawauliza.

"Hatujui hii yote imetokea wapi na inaelekea wapi. Lakini tunahitaji msaada. Cha kwanza itakuwa ni kuwaambia wazazi wetu. Lakini tulikuwa tunataka kusubiri mpaka birthday ya mama ipite ndo' tumwambie kwanza maana atachanganyikiwa tukisema now. Baada ya hapo... nitahitaji msaada wa ukocha kidogo maana shindano la kuogelea limekaribia na Sandra anahitajika sana ili kushinda..." Sandra (Xander) akaeleza.

"Kwa kuwa uko kwenye mwili wake utahitaji kuzijua mbinu," Valentina akasema.

"Ndiyo."

"Kwa hiyo... utaogelea, ndani ya mwili wa dada yako, kwenye shindano la wanawake. Unajua kwamba kwenye vyumba vya maandalizi huwa..."

"Ndiyo tunajua madam. Lakini tutafanyaje? Xander alivyo na kichwa kibovu atafurahia sana kuona wadada wakiwa bila nguo au wakijipiga-piga makalio... na hata anaweza kuyashika-shika..." Xander (Sandra) akawa anasema kiutani.

"Sandra!" Sandra (Xander) akamkatisha.

Valentina akatabasamu kidogo.

"Usimsikilize huyu... I'd never do that," Sandra (Xander) akamwambia Valentina.

"Okay sawa nimewaelewa. Hii itakuwa challenge kubwa kwangu," Valentina akasema.

Sandra, akiwa anajua kwamba wawili hao wangehitaji kuzungumza peke yao, akamwomba Valentina amwelekeze vyumba vya haja vilipokuwa. Baada ya kuelekezwa na kwenda, Xander akamshika usoni Valentina.

"Valentina... najua hii ni ngumu kwako. Lakini ujue kwamba nakupenda sana hata kama niko kwenye mwili wa dada yangu. Hakuna kinachobadilika," akamwambia.

"Ndiyo. Najua. Ni ajabu kidogo kwa sababu... ahah... ni kama nayeongea naye ni Alexandra. Ijapokuwa mnafanana lakini ni wewe Xander, ukiwa kwenye mwili wako, ndiyo huwa unanifanya nasisimka. Hivi... sijui kama itakuwa rahisi," Valentina akamwambia.

"Usijali. Ninajua hiki kipindi kitapita. Cha muhimu ni kwamba bado tutakuwa wote madam wangu mtamu," Xander akamwambia.

Vakentina akacheka kidogo.

Xander akaifata midomo yake na kumbusu. Kwa mara ya kwanza kabisa akambusu mwanamke huyu akiwa ndani ya mwili wa pacha wake. Alijitahidi kumbusu kwa njia ile ile anayotumia akiwa kama Xander, lakini bado Valentina hakuhisi hilo; yeye aliona anapewa busu na Sandra. Baada ya Xander kukatisha denda hii, akampa tabasamu, naye Valentina akatabasamu pia lakini hakujihisi vizuri sana.

Baada ya Sandra kurejea hapo, mapacha wakazungumza na Valentina kuhusiana na jinsi ambavyo mambo yangekwenda baada ya birthday ya mama yao. Wangepanga muda fulani wa pekee ili Valentina amsaidie Xander kufanya mazoezi ya kuogelea, naye Xander akatania kwamba sasa wangetumia muda mwingi kuliko kawaida kwa sababu alionekana kuwa wa kike hivyo angemganda sana. Wakamwambia ikiwezekana wamshauri mama yao amwalike na yeye kwenye sherehe yake kesho nyumbani, ili akapate kupaona na ndani kwao kabisa, lakini Valentina akakanusha na kusema hangeweza, hivyo wao wafurahie tu.

Waliendelea kukaa hapo kwake mpaka kwenye mida ya saa 12 jioni, kisha wakaondoka kuelekea nyumbani. Valentina alibaki na vitu vingi kichwani kwake. Bado kuimeza hii hali yote haikuwa rahisi. Lakini akaamua tu kuacha mambo yawe jinsi yatakavyokuwa na kusubiri ambayo yangefuata. Akarudi ndani kupumzika.


★★★


Baada ya kufika nyumbani, mapacha walikuta mama yao pamoja na Azra wakiwa wamerudi tayari. Wakajitahidi sana kutenda kwa njia ya kawaida ili wasishtukiwe kwa kile kilichowapata. Alice akawaambia kwamba alitaka kuwatoa "out" wote ili kupata chakula sehemu fulani nzuri sana. Hili lilikuwa ni jambo lililomfurahisha sana Azra, ambaye bila kusubiri akaenda kujiandaa haraka. Salome, Xander na Sandra pia wakaenda kujiandaa kwa ajili ya matembezi hayo. Ilibidi Sandra amsaidie Xander kuvaa nguo nzuri na kumpamba usoni kiasi kwa sababu jamaa hakujua jinsi ya kutengeneza vizuri mwili wa dada yake. Walipokuwa tayari, wote wakaondoka, ikiwa ni mida ya saa 2 usiku.

Alice aliwaendesha mpaka kwenye hoteli kubwa sana ya kifahari jijini hapo. Baada ya kuegesha gari, familia hii ikaanza kuelekea ndani huko. Alice alikuwa amekwishalipia mapema sehemu waliyotakiwa kufikia kwa ajili ya mlo, hivyo walipofika tu sehemu za ndani, wakapokelewa na mhudumu maalumu aliyewaongoza kuelekea upande wa meza yao. Wanaume wengi waliwaangalia sana wanawake hawa (Alice, Salome, Azra, na Sandra (Xander), kwa sababu walikuwa wamependeza kwa mionekano yao ya gharama. Xander alikuwa anakerwa na jinsi wanaume walivyomtazama kwa njia ya utongozi kwa kuwa ni yeye ndiye aliyekuwa kwenye mwili wa Sandra, lakini Sandra akamwambia awapuuzie tu.

Wakafika kwenye meza yao, ambayo ilizungukwa na viti vyenye mtindo wa masofa vilivyokuwa virefu kuficha hadi vichwa vyao, nao wakaketi na kupewa mfululizo wa vyakula mbalimbali (menu) ili wachague walivyotaka. Wote walipomaliza kuchagua, mhudumu akaondoka kupeleka mahitaji yao kwa wapishi ili awaletee hatimaye. Lakini kuna jambo likamshangaza Alice kiasi.

"Sandra, umeagiza kitimoto? Nilifikiri huwa huli..." akamwambia Sandra (Xander).

Xander, akiwa kwenye mwili wa Sandra akasema, "Aam... sa'hivi huwa nakula. Ni nzuri."

Sandra akamkata jicho kwa sababu ni chakula ambacho hakupenda kula.

"Mama, hoteli nzuri sana hii. Kati ya zote ambazo umetupeleka, hii inafunika," Azra akasema.

"Hivyo ndivyo ulivyosema mara ya mwisho kwenye ile nyingine," Salome akamwambia.

"Hamna hii ni noma. Anaimiliki nani?" Azra akauliza.

"Anaitwa Juliana," akajibu Alice.

"Juliana wa Bushoke?" Sandra (Xander) akauliza.

"Ahahah... hapana. Juliana Kenneth. Sidhani kama mnamfahamu ni rafiki yangu pia," akajibu Alice.

"Nilikuwa najiuliza kwa nini tumekuja hapa siyo kwingine, kumbe una shosti? Angalau aone unamchangia kidogo," Sandra (Xander) akasema.

"Siyo hivyo wala. Nilikuwa nataka tu kumwona na yeye pia kwa sababu nilipanga kuongea naye. Ila ni ili nikukutanishe na mwanaye," Alice akamwambia Sandra (Xander).

Mapacha wakatazamana. Yeye Alice aliona anayemsemesha ni Sandra kumbe ni Xander.

"Kwa nini unataka kunikutanisha naye?" Sandra (Xander) akauliza.

"Ili akuoe," Alice akasema kiutani.

Sandra, akiwa kwenye mwili wa Xander, akacheka sana.

"Na wewe unacheka nini?" Salome akamuuliza.

"Hamna kitu dada. Kwa hiyo unataka kuni... unataka kumuozesha Sandra sasa hivi?" Xander (Sandra) akamuuliza Alice.

"Eeeh..." Alice akajibu.

"Mama, mimi sitaolewa na yeyote kamwe. Siwezi kuolewa. Haiwezekani kunioa," akasema Sandra (Xander).

Alice akacheka.

"Huyo kaka anaitwa nani?" Xander (Sandra) akauliza.

"Tristan," Alice akajibu.

"Wow, jina zuri. Ni mzuri?" Xander (Sandra) akauliza tena.

"Ish! Yaani Xander unauliza maswali utafikiri wewe ndiyo unaolewa!" akatania Azra.

"Hamna si namuulizia tu dada yangu jamani," akasema Xander (Sandra).

"Haolewi mtu hapa," Sandra (Xander) akasema, na wote wakacheka.

Baada ya muda mfupi, vyakula mbalimbali vikaletwa na vinywaji. Wote walikula kwa furaha sana; hasa Azra, aliyependa sana nyama ya kuku. Walikula huku wakipiga story kuhusiana na sherehe ndogo ya mama yao kesho, shule, michezo ya watoto, na maisha ya zamani ya Alice.

"Kwa hiyo kumbe lilikuwaga ni soko kubwa sana hapa?" Salome akamuuliza Alice.

"Halikuwa kubwa kihivyo. Lilikuwa dogo tu... kama vibanda vya mbogamboga na nyumba ndogo ndogo za kuuzia vyakula. Me pia nilikuwa nafanya kazi na mama kwenye mgahawa wake. Eh! Yaani palivyobadilika na kuwa hoteli kubwa hapa! Utadhani hakukuwahi kuwa na soko," Alice akaeleza.

"Kipindi hicho hata hatujafikiriwa kuzaliwa," akasema Azra.

"Ndiyo. Nilikuwa kama Sandra tu," Alice akawaambia.

"Ndiyo ulikutana na baba huku?" akauliza Xander (Sandra).

"Casmir nilikutana naye wakati nimerudi Pemba, nafikiri alikuwa kwenye masuala yao ya kuzuru. Ahah... ilikuwa kwenye daraja fulani hivi... nilikuwa nimebeba tray la mayai napeleka dukani kwa babu, nikapamiana na askari mmoja akasababisha mayai yote yapasuke. Badala aombe samahani yeye akaanza tena kuwa mkali, na mimi sikuwa nyuma. Nikaanza kumrushia maneno, eti akanitisha kunipiga, ndiyo akatokea Casmir akamkunja mkono wake kwa nguvu na kumwambia aombe msamaha...."

Watoto wakawa wameacha hadi kula, wakimsikiliza Alice kwa utulivu sana.

"Ahahah... baadaye tukawa marafiki. Akanipenda. Nikampenda. Tukaanza uhusiano. Alikuwa mwelewa sana na alinisaidia kwa mambo mengi sana... mimi pamoja na familia yetu. Mwishowe... akanioa. And... here we are," Alice akawaambia huku machozi yakimlenga.

Azra akamsogelea na kumlalia begani. Alice akaanza kuzilazalaza nywele za binti yake kwa upendo. Mapacha wakatazamana kwa hisia, wakiwa wameelewa kuwa mama yao alimkumbuka sana baba yao. Kisha Alice akawaambia waendelee kula na kupiga story nyingine.

Dakika chache baadaye...

"Mom, nataka niende restroom," Azra akasema.

"Okay. Sandra nenda naye," Alice akasema na kuendelea kula.

Lakini Xander, akiwa ndiyo Sandra, akawa amejisahau kwamba ni yeye ndiye aliyepaswa kunyanyuka, hasa kwa kuwa alikuwa anajibu ujumbe wa Valentina kwenye simu, naye Alice akamtazama kimaswali. Sandra, akiwa ndiyo Xander, akamwangalia pacha wake akiwa anataka kumsemesha kwamba ni yeye ndiye aliyeongeleshwa. Kutokea kichwani kwake, Sandra akasema kwa kuudhika, 'Alexander!' akiwa hajataka kuita hivyo kwa sauti.

Lakini Xander akanyanyua uso na kumwangalia Sandra. Alimsikia! Hakujua kivipi lakini aliweza kumsikia.


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next