FOR YOU
Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI
★★★★★★★★★★★★★
"Mom, kwani lazima Sandra aende nami?" Azra akamuuliza Alice.
"Ndiyo unaweza ukapotea. Sandra ina maana hujanisikia au?" Alice akamuuliza Sandra (Xander).
"Ha..pana. Nimekusikia. Twende Azra," Sandra (Xander) akasema.
"Me siyo mtoto bwana! Siwezi kupotea," Azra akaanza kulalamika.
"Ngoja tu twende wote nami nahitaji kwenda," akasema Salome.
"Basi nenda naye tu Salome," akasema Sandra (Xander).
Salome akanyanyuka na kuondoka pamoja na Azra. Xander, akiwa kwenye mwili wa Sandra, akawa anamtazama sana pacha wake mpaka Alice akamshtukia.
"Mbona unamwangalia hivyo mwenzako?" Alice akamuuliza.
"Aa... hamna kitu," Sandra (Xander) akajibu.
Alice akaachana na hilo na kuanza kuangalia vitu fulani kwenye simu yake.
Xander bado akawa akijiuliza ni kwa nini alihisi kama alimsikia dada yake kichwani kwake. Hii ilikuwa mara ya pili; ya kwanza ikiwa kule chuoni wakati wapo darasani. Akataka kuona ikiwa naye angeweza kusikika kichwani kwa dada yake, hivyo akamwita kwa kutumia akili.
'Sandra...'
Sandra, akiwa kwenye mwili wa Xander, akanyanyua uso na kumtazama pacha wake. Alisikia! Lakini akamtazama kimaswali sana kwa kuwa hakuelewa kilichotokea. Xander akatabasamu kidogo, kisha akaona aongeze.
'Sandra, unanisikia vizuri?' akauliza kwa kutumia akili.
'Ndiyo,' Sandra akajibu kwa kutumia akili pia.
'Amazing!' Xander akawaza.
'Hii inawezekanaje?' Sandra akauliza.
'Sijui ila... inaweza kuwa njia nzuri ya kuwasiliana kati yetu...'
'Kwa hiyo mawazo yangu yote unayasikia?'
'Hapana... sijui. Em' jaribu kuwaza kitu bila kuniambia,' Xander akasema akilini.
Sandra akafanya hivyo.
'Umenisikia?' akamuuliza.
'Hapana,' Xander akajibu.
'Mmmm... basi inaonekana ni mpaka tuwe tunaambiana...' Sandra akasema kwa akili.
'Yeah. Hili jambo linaloendelea kati yetu linazidi kuchanganya sana!' Xander akasema kwa akili.
'Sana!' Sandra akakubali.
'Kwa hiyo... sasa hivi tutakuwa tuna...'
"Nyie vipi? Mbona mnaangaliana hivyo?" sauti ya Alice ikasikika.
Mapacha wakaacha kutazamana na kukuta mama yao anawaangalia sana. Wote wakabaki tu kimya na kuendelea na chakula kilichobaki. Alice akaingiwa na mashaka kwa sababu sasa akawa ametambua kuna kitu hakikuwa sawa kati ya wanaye. Azra na Salome wakaonekana wakirejea, naye Alice akasema anatoka kwanza kwenda kumwona rafiki yake kule kwenye ofisi yake. Baada ya wawili wale kufika, Alice akaondoka, akiwaacha wanamalizia chakula.
Alexander na Alexandra wakaendelea kufanyiana majaribio ya kuongeleshana kwa kutumia akili, na lilikuwa ni jambo lenye kustaajabisha sana. Sandra akamkumbusha Xander kwamba kesho angepaswa kutoka na mama yake na Azra kwa ajili ya shopping yao, hivyo angetakiwa kumchagulia mavazi mazuri na siyo yoyote tu.
Baada ya wote kumaliza chakula, wakaendelea kukaa hapo na kupiga story mpaka Alice aliporudi. Kwa kuwa yeye hangeendelea kula, akawaambia waondoke kuelekea nyumbani sasa ili kuweza kupumzika.
★★★
SIKU ILIYOFUATA
Ikiwa ni Jumamosi yenye upekee kwa Alice kwa sababu ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, maandalizi yalianza kufanywa mapema nyumbani kwao; usafi, mapambo, vifaa vya matumizi, vyakula, vinywaji, na burudani ndogo ambazo zingekuwepo. Mida ya mchana Alice aliondoka pamoja na Azra na Sandra (Xander) kuelekea kwenye moja ya duka lake kubwa la nguo ili kuchagua nguo nzuri za kuvaa, kisha baadae wakarejea nyumbani.
Marafiki wengi wa Alice walikuwa watu wenye maisha ya hali ya juu, lakini alialika pia na wale ambao hawakuwa na uwezo mkubwa sana kifedha. Sandra na Xander waliona ni bora kutoalika mtu yeyote, hasa rafiki zao, kwa kuwa waliona suala lao la kubadilishana miili kuwa tatizo ambalo lingewachanganya sana. Mpaka inafika mida ya jioni ndiyo watu wakaanza kufika kwa kuwa sherehe hii ililengwa hasa kwa ajili ya mida ya usiku.
Alice alipendeza sana kwa nguo alizovalia. Watoto wake wa kike walipendeza sana kwa magauni, huku Xander akichukia kuvalishwa gauni namna hiyo kwa kuwa ndani ya mwili wa pacha wake ilikuwa ni yeye. Sandra aliuvalisha mwili wa kaka yake nguo za kawaida tu kwa pendekezo la Xander, naye Azra alipendeza kupita maelezo. Alice akaamua kumpigia Casmir simu ili kuuliza ikiwa mume wake angefika, na wakati akifanya hivi, watoto wake wote walikuwa pamoja naye chumbani. Casmir akapokea, na kwa sababu ilikuwa ni kwa njia ya "video call," wote wakamwona akiwa ndani ya gari lililokuwa mwendoni pamoja na Kendrick.
"Uncle Kendrick!" Azra akamwita Kendrick kwa shauku.
"Azra! Umefutuka mtoto, unaenda wapi?" akasema Kendrick kupitia simu.
Wote wakacheka kwa furaha.
"Mwanagalie na huyo kadadaa! Alexandra umekua mkubwa jamani!" akasema Kendrick.
"Asante uncle K. Wewe pia unang'aa," akajibu Sandra (Xander).
"Ahahahah... unaongea kama mzee mzima hapo," Kendrick akasema.
"Nakuona uncle Kendrick," akasema Xander (Sandra).
"Nakuona pia mzee wa fujo," akasema Kendrick.
"Mmependeza sana wapendwa wangu," akasema Casmir.
"Baba, uko njiani eeh?" akauliza Azra.
Kendrick na Casmir wakaonekana wanaangaliana kifupi. Hii ikamfanya Alice ahisi kuna shida.
"Ndiyo sweetheart. Hapa ndo' tuko tunawahisha kuja," Casmir akasema.
Azra akafurahi sana.
"Mtafika saa ngapi?" akauliza Xander (Sandra).
"Aam... labda saa 1, saa 2..." Casmir akajibu.
Alice akatazama chini kwa kuvunjika moyo kiasi. Casmir akatambua hilo.
"Baba, Uncle Kendrick, msiache kuja na zawadi," Azra akasema.
Kendrick akajifanya kuziba mdomo kwa mshangao na kusema, "Ayaaa! Nimesahau! Sasa tutafanyaje?"
"Yaani usionekane hapa! Urudi huko huko mpaka ulete zawadi," Azra akaamuru.
"Basi sasa itabidi tu nirudi nyuma kweli..."
Kendrick akasema hivyo huku akionekana anarudisha mikono yake nyuma ya gari na kuirudisha akiwa ameshikilia boksi kubwa la zawadi. Wote wakacheka, huku Azra akifurahia sana.
"Kwa hiyo niahirishe tu kuja eti?" Kendrick akamuuliza Azra.
"Wee! Ole wako," Azra akamwonya.
Wote wakacheka tena.
"Sandra, nakuletea na Vaziri. Niliipata," Casmir akasema.
"Sawa. Asante," Sandra (Xander) akajibu kibaridi-baridi tu.
"Alice umependeza sana. Happy birthday," Kendrick akasema.
"Asante. Tunawasubiri kwa hamu sana," Alice akawaambia.
"Ndiyo sana. Mwahi kufika. Nyie ndiyo mtafanya party iwe party zaidi," akasema Xander (Sandra).
Casmir na Kendrick wakacheka.
"Alice my dear, happy birthday. Tuko njiani," Casmir akamwambia mke wake.
"Asante Casmir," Alice akajibu.
Kisha wote wakaagana na kukata simu. Watoto wakaelekea nje ya nyumba wakimwacha mama yao chumbani. Bado alihisi kama vile mume wake alikuwa anasema tu yote yale ili kumridhisha, lakini akajifariji tu kuwa hata kama nini kingetokea, angejitahidi kuwa sawa kwa ajili ya wanaye.
★★★
Baada ya simu kuwa imekatwa, ndani ya gari hili walilokuwemo Casmir na Kendrick kukawa na hali ya umakini zaidi. Kendrick akarudisha boksi lile la zawadi nyuma ya gari na kumtazama Casmir.
"Vipi kama tutachelewa?" Kendrick akamuuliza.
"Hapana Ken. Ni lazima tutawahi tu. Lazima nifike," Casmir akasema huku akiongeza mwendokasi.
"Yaani hata sielewi. Nini kinaendelea? Tunapofikiri tu tuko right on track, mambo yanaharibika," akasema Kendrick.
"Hii ishu imekuwa mbaya tena kwa njia ambayo inashangaza sana. Just... how?" Casmir akasema kwa mkazo huku anaupiga usukani kwa kiganja chake.
"Hapa Kanali atashangaa sana kwa hii ripoti. Unajua hawa Demba Group wanaanza kuonekana kama mashetani, maana wanafanya mambo yasiyoeleweka halafu wanatoweka tu, tena kwa watu fulani wanao... wanawalenga watu fulani kwa nini? Hawamtaki Raisi, si wamfate? Wale wanaume wamewakosea nini? Halafu wanafanyaje haya mambo bila kupatikana? Aagh... yaani me nashindwa kuelewa!" Kendrick akasema kwa kuudhika sana.
"Ningetakiwa kuwa nimetulia angalau kwa wiki hii na Alice wakati wanasakwa, ila sasa tena itabidi..." Casmir akasema kwa huzuni.
"Usijali Meja. Tufike kwa Kanali kwanza, then birthday, mambo mengine yatafuata," akasema Kendrick.
"Yeah. Baada ya birthday nataka kuhakikisha huu utumbo unamalizika haraka sana," akasema Casmir kwa uhakika.
"Nimeona kama Alexander anakuchangamkia. Ana Fever?" Kendrick akatania kidogo.
"Ahahah... sijui sana, lakini nimependa. Matumaini waliyonayo... yaani sitaki kuwaangusha kabisa," Casmir akasema kwa hisia.
Wawili hawa walikuwa na mzigo mzito sana kuhusiana na suala hili la Demba Group. Siku mbili zilizopita baada ya Kanali Jacob kuwahamishia jijini kwao, walikuja kupewa taarifa siku iliyofuata juu ya mauaji ya wapelelezi wale wa kijeshi waliowatuma kwenye mikoa ambayo walihisi Demba Group wamejifichia. Hawakuwa na jinsi ila kuondoka na kwenda huko kuchunguza mambo zaidi. Ila baada ya kuwa wamefika, leo tena wakapokea taarifa juu ya wanajeshi wengine 9 waliouawa na Demba Group.
Wanajeshi hao 9 walikuwa ndiyo wale ambao waliongoza msafara ule wa silaha siku ile Casmir alipoenda kuuchunguza, na wote waliuliwa kimya kimya na kuchorwa maandishi meusi juu ya paji la nyuso zao yaliyosomeka "Demba Group." Yalikuwa ni mambo yenye kushangaza sana, kwa sababu watu hao mpaka sasa hawakujulikana, na kwenye mauaji yote hayo hawakuacha kitu chochote cha kusaidia kuwafuatilia; kama tu msemo wa Kendrick, walikuwa kama mashetani.
Mambo haya yote yalimsumbua sana Casmir. Alikuwa amekwishapokea amri ya kuanza kazi baada ya yeye kuianza kisiri, na sasa wanajeshi wake aliowachagua wakauawa. Ikiwa ingejulikana kwa Raisi kuwa alifanya hivyo kabla ya kupewa amri, ingezua tatizo. Lakini Casmir alikuwa tayari kuwajibika. Hata kama angepewa adhabu. Alijilaumu sana kwa vifo vya wapelelezi wake. Alijiuliza watu hawa walijua vipi mipango yake na hatimaye kuikomesha kabla haijafikia hatamu nzuri.
Meja Casmir na Kapteni Kendrick walitakiwa kushughulika na mambo yote yaliyotokea haraka, lakini wakaamua kuyaacha kwanza ili Casmir atimize ahadi kwa mke wake ya kuwepo kwenye sherehe ya siku yake ya kuzaliwa. Hapo walikuwa wakitokea Singida upesi ili kuwahi jijini kwao. Walijua wangepaswa kwanza kwenda kwenye ofisi za Kanali ili kutoa ripoti ya ana kwa ana, na ndiyo maana Casmir alikuwa akiwahisha sana ili asiikose sherehe ya Alice.
★★
Ilifika mida ya saa 1 usiku, na wawili hawa wakawa wamefikia kwenye jengo hilo. Walielekea ndani upesi, wote wakiwa wamevalia suti nadhifu. Casmir alitambua kwamba ni kama wanajeshi wa ulinzi sehemu hii walikuwa wamepungua, lakini hakukazia fikira sana jambo hili na kwenda mpaka kwenye ofisi ya Kanali. Bado Kanali Jacob alikuwepo, hivyo wote wakaruhusiwa kuingia ndani. Casmir akaeleza hali halisi ilivyokuwa, na kusema kwamba ni makosa yake kwa kila kilichotokea, hivyo kama ni adhabu basi apewe; angekubali yoyote ile.
Kendrick naye vilevile akasema alistahili adhabu, lakini Kanali Jacob akawaambia hakukuwa na haja ya adhabu. Akasema kwamba walitakiwa kulificha jambo hilo lililowapata wanajeshi wale kwanza, ili "mission" yao ya kuwakamata Demba Group ikamilike. Meja na Kapteni wakashangaa. Walitarajia labda Kanali Jacob angekuwa mkali, lakini haikuwa hivyo. Tena akawakumbusha kwamba anajua ni muhimu sana kwa Casmir kuwa na mke wake leo, hivyo waende kujifurahisha, kisha wangerejea ili kupiga kazi kiusahihi zaidi.
Casmir na Kendrick hawakujua ikiwa wangepaswa kushukuru au la, lakini Kanali Jacob akaomba kuongea na Meja Casmir peke yake kwanza, kisha ndiyo wangeondoka. Kwa heshima, Kendrick akamwambia Casmir kuwa angemsubiri ofisini kwake (ofisi ya Kendrick), naye akapiga saluti na kutoka akiwaacha wawili hao humo ndani.
"Meja Casmir..." Kanali Jacob akaita.
"Naam Kanali..." Casmir akaitika.
"Unakumbuka kipindi kile cha zile fujo? Jinsi wanajeshi walivyoweka mgomo na kuharibu mambo mengi sana ya wazungu ili kuwafanya waache kutukandamiza?" Kanali Jacob akauliza.
Casmir akabaki tu kimya na kuangalia chini.
"Hivi kweli tulikuwa tunakandamizwa, au labda walikuwa tu hawaridhiki?" Kanali Jacob akauliza tena.
"Watu... huona mambo kwa njia tofauti na jinsi wengine huyaona. Wengine waliona wanatendewa vizuri, na wengine kinyume. Inapofikia wakati mtu amechukua hatua fulani kwa sababu ya maoni yake, basi huwezi... kuibadili akili yake kwa sababu anaona anachofikiri kuwa sahihi," Casmir akasema.
Kanali Jacob akamtazama kwa tabasamu la pembeni, naye Casmir hakupendezwa na jambo hilo.
"Sikuzote majibu yako huwa unayapangilia au? Ahahah... napenda sana akili yako. Ndiyo sababu General anaku-favour sana. Utafika mbali Casmir. Usipoteze matumaini," Kanali Jacob akamwambia.
"Hapana mkuu, sijapoteza matumaini. Najua maisha yana kusudi. Huko kote tulikopita, tulipo, na tunapoenda, hatuwezi kupanga sisi wenyewe. Wakati mwingine ni muhimu kuwa na imani kwamba kila kitu kitakuwa sawa hata ijapokuwa inaweza ikaonekana kama hakuna njia. Sijui ni kwa nini umenikumbusha jambo hilo, lakini ninakuhakikishia, ipo siku wale WOTE wanaohusika na haya watateketea vibaya sana. Imani tu," akasema Casmir kwa utulivu.
Kanali Jacob akamtazama kwa umakini, kisha akatabasamu na kutikisa kichwa chake.
"Ama kweli wewe ni mtu imara sana. Endelea hivyo hivyo, ipo siku utakaa kwenye kiti hiki... au cha General kabisa," Kanali Jacob akasema kwa njia yenye kejeli kiasi.
Casmir akatabasamu na kusema, "Asante mkuu."
"Okay. Waweza kwenda, najua mke wako anasubiri. Na kumbuka, usiseme kuhusu yaliyot..."
"Ndiyo najua Kanali. Nitafanya hivyo. Asante sana," Casmir akasema na kupiga saluti kwa heshima.
Kisha akatoka ofisini humo na kuelekea mpaka ofisini kwa Kendrick. Bado akili yake ilisumbuliwa sana na njia ya Kanali Jacob ya kufanya mambo. Hakujua ni kwa nini lakini ni kama Kanali alificha kitu fulani, ila hangeweza kutambua ni nini hasa. Akamkuta Kendrick akiwa amesimama na kijana fulani nje ya mlango wa ofisi yake, aliyekuwa kama msaidizi wa Kanali Jacob, ambaye pia alikuwa akiondoka jengoni hapo. Casmir akamwambia Kendrick waondoke upesi sasa ili kuwahi kule, na bila kuchelewa wakaelekea kwenye gari lake.
★★
"Huyo kijana ndiyo amekwambia hivyo?" Casmir akamuuliza Kendrick wakiwa mwendoni.
"Ndiyo. Amesema eti Kanali ana mkutano muhimu na watu fulani hapo ndo' maana hajaondoka mpaka sa'hivi," Kendrick akasema.
"Na ndiyo maana ni kama watu wote wamewafukuza. Hao watu watakuwa nani?" Casmir akauliza.
"Sijajua. Ila kuona kwamba sisi hatujui inamaanisha ni watu special, sisi mtumba," akasema Kendrick.
"Yeah."
"Kwa hiyo sisi ndiyo wakatuona makolo sana au? Kwamba tusijue kuhusu hilo?" akauliza Kendrick.
"Ahah... sidhani kama inajalisha. Kanali Jacob... ni mtu mtata sana. Kuna vitu vingi ambavyo anaficha. Na hiyo inakwambia kwamba kuna ishu nyingine itafanyika, labda hata ni viongozi wengine wanakuja kujadili hili suala tunaloambiwa tupige kimya kulihusu. Sisi tusubirie tu kupewa order... au labda kutimuliwa," akasema Casmir.
Kendrick akacheka kidogo. Casmir akaichukua simu yake ili kuiwasha, lakini haikuwaka.
"Aaagh... simu yangu imeshiwa chaji saa ngapi? Imezima halafu sijamtext Alice, yaani atanitafuna mzima mzima nikichelewa bila taarifa aisee. Mpigie basi hapo mwambie tupo njiani. Mwambie pia tulikuwa tumepitia zawadi kwa ajili yake ndiyo maana...."
"Aah shit!" Kendrick akamkatisha Casmir.
"Vipi?" Casmir akauliza.
Kendrick alikuwa anatafuta-tafuta kitu fulani mifukoni.
"Nafikiri nimesahau simu yangu ofisini," akasema.
"Dah! Uliingia na ofisini? Basi siyo mbaya..."
"Naihitaji kaka..."
"Uifate? Si utaikuta kesho?" Casmir akasema.
"Hamna bwana, naihitaji. Usifikiri ni wewe peke yako ndiyo unapenda ku-chat," Kendrick akamwambia kiutani.
"Ulishawahi kuniona na-chat?"
"Mm... unajikana eti? Hapo ukikuta Alice anakwambia uwahi ili akakupe malavii hadi maudende yanakutokaga heheheee..." Kendrick akatania.
"Ahahahah... mbwa wewe."
"Geuza bana niifate."
"Acha hizo Ken... unajua nawahi birthday ya Alice. Tumeshachelewa tena unataka niirudie simu yako... kisa ku-chat tu! Utaikuta kesho bwana..."
"Hamna siyo kihivyo Meja... sema... kuna jambo la muhimu nahitaji kufanya kwa simu ndiyo maana..."
"Nini? Umeshampatia Margaret au siyo?"
"Ahahahah... achana na habari zake huyo. Ila ni muhimu sana. Fanya kuniacha hapo hivi nichukue boda nirudi kule fasta..."
"Unajua hawaruhusu kufika maeneo yale na boda, umechanganyikiwa?"
"Hatutafika pale kabisa bana... ananifikisha pembeni natembea kwa guu mpaka kule."
"Mh! Yote hiyo kwa ajili tu ya simu? Si ungesubiri mpaka kesho ina maana ni muhimu kiasi hicho cha huo usumbufu wote?"
"Ndiyo kaka ni muhimu."
"Dah! Ahahah... haya bwana. Me yangu masikio nitajua tu ni nini."
"Ufe!"
Wote wakacheka, kisha Casmir akaegesha gari usawa wa sehemu ambayo ilikuwa na shughuli-shughuli za watu. Marafiki hawa wakaagana vizuri huku Kendrick akisema angejitahidi kuwahi kwenye sherehe ya Alice, kisha akashuka na kumsindikiza Casmir kwa macho alipoondoka eneo hilo. Akaangalia eneo hilo na kufanikiwa kuona taxi upande wa pili wa barabara, hivyo akafata moja na kuingia; akimwambia dereva ampeleke eneo fulani ambako angemwelekeza jinsi ya kufika.
★★
Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, dereva akawa anatambua walikuwa wakielekea kwenye makao ya kijeshi, hivyo akaonya kwamba asingeweza kumfikisha kule kabisa. Kendrick akamwambia asihofu kwa kuwa yeye ni mwanajeshi, na angemwelekeza sehemu nzuri ya kuegeshea ili asije akajikuta anaingia sehemu hiyo iliyozuiliwa na hivyo kukamatwa kimakosa. Wakiwa wanakaribia huko, Kendrick aliweza kuona gari mbili nyeusi zikiwa karibu na jengo lile. Akamwambia dereva asimame haraka, kisha akamlipa na kushuka.
Taxi ikaondoka, naye Kendrick akaanza kuelekea huko kwa umakini. Hakujua ikiwa kulikuwa na shida wala nini, lakini alielewa kwamba hakutakiwa kuwepo hapo kwa sababu aliambiwa kwamba mkutano huu uliwahusu wakubwa wake tu, hivyo akawaza kwamba labda ingeleta shida kama angeonekana tena hapo. Lakini akaamua tu kutowaza mambo mengi mno na kwenda pale kwa sababu kihalisi shida yake ilikuwa ni simu tu, kwa hiyo angeichukua na kuwahi birthday ya mke wa rafiki yake.
Baada ya kufika karibu na mwingilio wa eneo la jengo lile, akakuta wanajeshi wawili aliowajua vizuri wakiwa wanalinda bila shaka, na gari tatu nyeusi; mbili aina ya V8, na moja aina ya TOYOTA MARK X zikiwa pembeni. Aliweza kutambua kwa kuzipiga macho haraka kwamba V8 moja kati ya hizo ilikuwa na kibendera kidogo cha kupamba mbele ya gari, hivyo wazo la kwanza la mmiliki wake ingekuwa ni mtu kutoka serikalini na siyo jeshini; ingawa hakuwa mwenye uhakika na hilo. Akawasogelea wajeshi wale, nao wote wakapiga saluti ya heshima kwake; na yeye vile vile. Akataka kuwapita, lakini wakafanya kama kumzuia.
"Samahani mkuu. Tumepewa amri kuwa hatupaswi kuruhusu yeyote kuingia hapa," mmoja wao akasema.
"Ndiyo najua. Lakini kuna kitu cha muhimu sana nimesahau ofisini kwangu. Ninakwenda kuchukua kisha naondoka haraka," Kendrick akasema.
"Hiyo itakuwa kuvunja amri ya mkuu Kanali. Tusamehe sana lakini hakuna uwezekano wa kukuruhusu kupita..."
"Mimi ni superior kwenu. Mnajua hilo. Kwa nini mnanizuia wakati ninaweza kuwapa amri na mtapaswa kuifuata?"
"Hapana mkuu, siyo kihivyo. Ni kwamba amri ya Kanali ni ya juu zaidi... hata Luteni amesema tuhakikishe hakuna kitu kinaingia hapa, hivyo ni lazima amri itekelezwe."
"Luteni? Luteni Weisiko yuko hapa?" Kendrick akashangaa.
Wanajeshi wale wakatazamana, kisha wakamwangalia tena Kendrick.
Kendrick akajua bila shaka kulikuwa na mambo mengi ya siri yaliyoendelea hapo mpaka kufanya yeye azuiwe na watu ambao alipaswa kuaminiana nao, na mtu mwingine ambaye alikuwa chini yake. Lengo lake kufika hapa ilikuwa ni simu, lakini sasa akataka kulazimisha mambo ili ajue kilichoendelea hasa.
"Jamani... sijui niwaambieje. Ninahitaji sana kuingia ofisini kwangu... nimeisahau simu yangu. Kuna dada yangu yuko mkoa mwingine anajifungua leo, nahitaji kujua hali yake kwa sababu mtoto amekuja kabla ya wakati..." akadanganya.
"Si utumie simu ya mtu mwingine umpigie mkuu?"
"Ndiyo hicho sasa. Mimi sijaikariri namba ya kule na waliopo huko bila shaka wananitafuta kwa kuwa mimi ndiyo wanategemea nigharamie kila kitu. Nahitaji kujua mambo yanayoendelea huko kwa sababu nimeondoka upesi ili niwahi kufanya malipo lakini kwa bahati mbaya nikawa nimesahau vitu vyangu kwa sababu ya haraka. Ninawaomba mnisaidie siyo kama Kapteni wenu ila kama kaka na mzazi hapa... tafadhali..."
Kendrick alibuni uwongo huu haraka-haraka kiasi kwamba akawa hajawapa nafasi nzuri ya kukaa kutafakari mambo kwa kina kuelewa kuwa alikuwa anawadanganya tu.
"Goko... eeh... Rama... nisaidieni basi. Nahitaji kwenda kuchukua haraka. Kama vipi twendeni wote... au mmoja wenu anipeleke nichukue halafu niondoke... maana hata hivyo wengine si wako upande mwingine wa ofisi? Kwa hiyo tunafanya tu upesi halafu naondoka... come on guys..." akawashawishi.
Ilikuwa rahisi kwao kukubali maneno yake hasa kwa kuwa walimfahamu akiwa kiongozi hapo na alionyesha unyonge ijapokuwa yeye alikuwa mkubwa wao kiumri na hata kwa vyeo. Hivyo, Goko akamwambia Rama amsindikize Kapteni mpaka ofisini kwake ili achukue vifaa vyake haraka na kurudi naye ili hata ikitokea ameonwa basi awe karibu yake kusema alikuwa akimwangalia. Kendrick akashukuru, kisha akaanza kuongozana na Rama kuelekea ndani kule. Wakiwa wanaenda aliangalia mazingira ya hapo, naye hakuona mtu mwingine akilinda eneo la hapo; kana kwamba haikuwa sehemu ya kijeshi kabisa.
"Wanajeshi wote wa ulinzi wameondolewa?" Kendrick akauliza wakiwa wanaelekea ndani.
"Ndiyo. Luteni alituweka sisi tu na wengine wa kwao," Rama akajibu.
"Kwa hiyo amefika Luteni Weisiko, Kanali, na nani mwingine?" Kendrick akauliza.
"Wengine siwajui. Walikuwa watatu wote wamevaa suti. Ila kati yao kuna mbaba mwingine mnene nafikiri nilishawahi kumwona lakini sijui wapi tu..." akasema Rama.
"Viongozi viongozi..." akasema Kendrick kiudadisi.
"Inawezekana."
Kendrick akahisi ni kama Rama anaficha jambo fulani, ila anajifanya kila kitu kiko sawa.
"Nilifikiri anakuja Jenerali Pingu... kumbe wengine kabisa..." Kendrick akajifanya anajisemea.
Rama akabaki kimya akitembea sambamba naye.
Walifika kwenye ofisi ambayo ndiyo ilikuwa ya Kapteni Kendrick mwenyewe, naye akaingia na kumwacha Rama nje ya mlango. Alipofika mezani akachukua simu yake haraka, kisha akafikiria afanye nini ili aweze kufika sehemu waliyokuwepo watu wale ili ajue ni nini kilichoendelea. Akaikoki vizuri bastola yake na kuiweka kwenye mkanda wa kiuno chake, kisha akasogea mlangoni na kusema kwa sauti ya chini, "Rama, njoo mara moja kijana wangu."
Rama akiwa anafikiria labda mkubwa wake huyo alihitaji msaada na jambo fulani, akaingia upesi na kukuta pakiwa tupu sehemu hiyo ya ofisi. Lakini ghafla akahisi kitu fulani kimempiga na kwa mbali alihisi maumivu nyuma ya shingo yake, na papo hapo akalegea na kupoteza fahamu. Ilikuwa ni Kendrick ndiye aliyempiga hivyo, akiwa amejibanza nyuma ya mlango muda ule alipomwita kijana huyu. Akamvuta mpaka kwenye kona pembeni na kumlaza hapo, kisha akaichukua bunduki yake (ya Rama) na kuiweka ndani ya kabati yake na kuifunga kwa funguo.
"Nisamehe kijana wangu... lakini ni lazima nijue ukweli."
Kendrick akanena hivyo, naye akaitolea simu yake sauti, kisha akatoka kwenye ofisi yake na kuifunga kwa funguo kabisa. Akaanza kuelekea upande wa jengo ambako alijua bila shaka kikao hicho kilifanyikia, yaani ofisi ya Kanali. Hawakuwa wameachana sana kiofisi, hivyo ilikuwa rahisi kuifikia. Alipokaribia aliwaona wanaume wanne wakiwa wamevalia suti, pamoja na Luteni Weisiko, na kwa haraka akajibanza ukutani ili wasimwone. Akawachungulia tena ili kuwasoma vizuri, na upesi akatambua wale walikuwa walinzi maalumu wa mtu, au watu hawa muhimu waliokuja.
Kwa kuwa haingewezekana kuwapita hapo, na alijua bila shaka Goko kule nje angeanza kuona yeye na Rama wanachelewa, akatumia njia mbadala ili kuweza kufikia chumba kile. Kwa sababu alikuwa ametumia siku yake ya kwanza kufika kwenye jengo hili kulifahamu vizuri, alijua kwamba ofisi ya Kanali ilikuwa na uwazi juu ya dari, uliozibwa kwa njia fulani ambayo angeweza kufungua ikiwa angekuwa kwa juu. Hii ndiyo ilikuwa kama njia ya ziada ya kupitisha hewa, hivyo ikiwa angeweza kuingia humo basi angepata kusikiliza maongezi ya kikao hicho.
Upesi akatoka hapo na kuelekea upande mwingine uliokuwa na ngazi ili aelekee juu kisha atumie njia nyingine kufika juu ya dari la ofisi hiyo. Alitumaini kwamba hakuwa amechelewa sana, na kwamba kwa vyovyote ni lazima tu kulikuwa na nuksi hapa katikati. Mambo ambayo Casmir alimwambia kuhusu utendaji wa viongozi wao yalikuwa ni kweli, na ijapokuwa alimwambia kwamba walitakiwa tu kufanya wajibu wao na kufuata amri, alitaka sasa pia kujua mambo mengi sana yaliyoonekana kuwa na utata ndani yake.
Baada ya kufika kule juu, akafanikiwa kupenya ndani ya njia zile na kuingia mpaka sehemu ya karibu zaidi na chumba cha ofisi ile. Aliweza kuwaona wanaume wale wanne waliolinda pale nje ya mlango kutokea alipokuwa, pamoja na Luteni Weisiko, lakini akawapuuza na kujitahidi kusogea karibu zaidi kwa umakini wa hali ya juu. Kupitia njia hiyo iliyokuwa na matobo madogo kiasi, alianza kusikia sauti za watu humo ndani zikiongea pamoja kuhusiana na operesheni fulani ambayo hakuweza kuelewa kikamili ilikuwa nini.
"...lakini una uhakika tunaweza kumwamini huyu kijana katika hili?" mmoja wa watu hao akasema.
"Ndiyo. Asilimia mia," ikajibu sauti ya Kanali Jacob.
"Unajua hatuwezi kuafford makosa. Mipango yote imewekwa kwa umakini wa hali ya juu. Kinachobaki sasa ni kuhakikisha wote waliohusishwa wafutwe... hiyo inatia ndani na huyu kijana," ikasema sauti nyingine.
"Hapana mheshimiwa. Ninaelewa process nzima. Lakini nakuhakikishia, Weisiko hatakuwa tatizo. Wale wengine ndiyo tutakaowafuta kwa sababu wako keen sana na Jenerali. Tukiwamaliza hao ndiyo mambo yatakwenda bila shida kabisa..." akasema Kanali.
Kendrick akatilia mkazo maneno hayo. Kanali Jacob alimaanisha nini kwamba wengine wafutwe isipokuwa Luteni Weisiko? Mipango gani iliyokuwa ikiendeshwa kinyume na utaratibu ambao hawakutaka Jenerali Pingu afahamu? Na hawa watu ambao Kanali aliwaita "mheshimiwa," walikuwa ni akina nani? Wakati akiendelea kujiuliza, akasikia sauti ya mmoja wao ikisema, "Mwite." Akatega sikio vizuri zaidi na kusikia sauti ya mlango ukifunguliwa kisha kufungwa.
"Kazi uliyokabidhiwa ilikamilika jana. Kuna changamoto zozote zilizotokea kinyume na mpango mzima?" Kanali Jacob akasikika akisema hivyo.
"Hapana mkuu," Luteni Weisiko akasikika akijibu.
Sasa Kendrick akatambua aliyeingia alikuwa ni yeye.
"Umekuwa ukifanya kila jambo uliloambiwa kufanya, na mengi yamefanikiwa kwa msaada wako. Tunajuaje hautatugeuka mbeleni Luteni?" sauti ya "mheshimiwa" ikasikika.
"Mimi pia ninataka kile kile mnachotaka. Kila mtu anajua kupanda ngazi ni muhimu ili kufika juu, kwa hiyo niko tayari kufanya lolote chini yenu ili nifike juu. Na ikiwa nitashindwa, basi maisha yangu mnayo nyie," akasema Luteni Weisiko kwa uhakika.
Sauti za vicheko vya kuridhika vikasikika.
"Mnaona? Jamaa yuko vizuri sana. Anaelewa sehemu itakayompa faida ni ipi," akasema Kanali Jacob.
"Indeed. Sisi tuna motto moja. Maneno yakatwe, kazi ifanywe. Tunachotaka ndani ya masaa 24 ni kwa wale wote WALIOONA ile kitu watoweke. Sijali ni nani, ni wangapi, na wako wapi. Hakikisha unawamaliza wote kabla ya kesho kutwa, do you understand?" ikasikika sauti nyingine ikiongea kwa uzito.
Sauti hii haikuwa ngeni sana kwenye masikio ya Kendrick, lakini akawa bado hajatambua ni nani.
"Ndiyo mheshimiwa, imeeleweka. Jenerali Pingu anajifanya anajua sana kukaza, sasa atalazimika kulegeza tu," akasema Kanali Jacob.
"Mipango ya kesho?" ikauliza sauti ya "mheshimiwa."
"Kila kitu nyendoni. Mimi na Luteni Weisiko tuna vijana wetu watiifu ambao wako tayari kufa kwa ajili yenu wakuu. Kwa hiyo nyie mtakachotakiwa kufanya ni kunyoosha tu miguu na kuangalia maua mazuri yakimeremeta," akasema Kanali Jacob, nao wote wakacheka.
"Silaha za leo zimepita pia tayari?" akauliza mwanaume mwingine.
"Mapema. Kesho kazi inaanza," akajibu Luteni Weisiko.
"Na target wako wa kuwaondoa kimya kimya unawajua vizuri?"
"Nyayo mpaka nywele. Walikuwa 9, tayari nimeshawaondoa. Nimebaki na Meja na Kapteni kwa kuwa wenyewe ndiyo walilazimisha mizigo ile ifunuliwe, lakini Kanali akahakikisha hawasemi lolote kwa Jenerali. Ila sasa nitahakikisha hawasemi lolote tena milele!" Luteni Weisiko akasema.
Kendrick alibaa! Alishtushwa sana na kile alichosema Weisiko kiasi kwamba akajigonga hapo juu.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments