FOR YOU
Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
★★★★★★★★★★★★★★★★
Kendrick akatulia kidogo akisikilizia ikiwa walikuwa wamemsikia alipojigonga, lakini wakaendelea kuongea tu.
"... mpumbavu anajiona sana anajua kutoa lecture za maisha. Ni vyema wamerudi huku, hii kazi kwa Luteni itakuwa rahisi zaidi...."
Kanali Jacob akawa anaendelea kuzungumza tu, naye Kendrick akaanza kujirudi taratibu nyuma ili aondoke hapo haraka. Hakujali tena kilichoendelea baada ya kutoka hapo, kwa kuwa alijua alikuwa amepangiwa kifo pamoja na rafiki yake ndani ya saa 24. Hivyo alipaswa kuhakikisha anamwonya Casmir upesi kisha wamwambie na Jenerali Pingu pia kuhusu haya yote.
Akafanikiwa kufika chini kule na kuanza kuelekea nje, na alipokaribia pale aliposimama Goko, akaanza kujifanya kama ameumia hivyo akawa anachechema. Baada ya Goko kumwona, akamwahi na kuanza kumuuliza nini kilitokea maana yeye na Rama walikuwa wamechukua muda mrefu mno; na Rama alikuwa wapi. Kendrick akamdanganya kwamba kuna shida kule ndani, kwamba inaonekana kuna mtaalamu wa mauaji ya kimya-kimya (assassin) aliyeingia na kutaka kuwadhuru, lakini yeye akafanikiwa kumponyoka, hivyo Goko awahi ili kutoa msaada maana waliopo kule bado wanahangaika naye.
Goko akatoka nduki na bunduki lake akiwahi kwenda kutoa msaada, akiwa ameamini kabisa kile ambacho Kapteni wao huyu alikuwa amesema, naye Kendrick akaharakisha mpaka kwenye magari yale pale nje na kuanza kuangalia kama kuna mlango ulio wazi. Yote yalikuwa yamepigwa funguo, hivyo, akiwa kwenye Mark X ile nyeusi, akavunja kioo na kuifungulia kwa ndani, kisha akaingia na kuanza kujaribu kuliwasha gari kwa kuziunguza nyaya za "ignition system." Akafanikiwa kuliwasha na kuliondoa hapo haraka sana, akiendesha kama anashindana vile!
Kendrick alichoka sana kiakili. Akaanza kuyarudia tena maneno ya watu wale aliyotoka kusikia, na baada ya kutafakari kwa kina, akawa ameitambua sauti ile iliyotoa amri ya kwamba yeye na wengine wafe kabla ya kesho kutwa kufika. Ilikuwa ni sauti ya Makamu wa Raisi, a.k.a mheshimiwa Paul Kalebu Mdeme. Akajiuliza maana yao kufanya yote haya ilikuwa ni nini. Alihofia mambo mengi mno; hasa familia zao.
Akatoa simu yake upesi na kupiga namba ya Casmir ili aweze kumwonya mapema kuhusu mambo yote aliyosikia, lakini akawa hampati. Alijaribu sana mpaka kumbukumbu ilipomjia kuwa simu ya Meja wake huyo ilikuwa imezima, kwa hiyo huenda alikuwa ameshafika nyumbani na kuiweka moja kwa moja ipate "charge." Akaamua kupiga namba ya Alice, nayo ikaita. Hakupokea mara ya kwanza na ya pili, lakini ya tatu akapokea.
"Alice..."
"Yaani wewe mbwa wewe ndiyo ukaamua kutokuja leo eti? Nikikata simu hapa usinisemeshe tena kamwe..." Alice akaongea kimasihara upande wa pili.
"Alice... nisamehe sana shemeji kwa kutofika. Lakini nahitaji kuongea na Cas sasa hivi! Ni muhimu sana tafadhali..." Kendrick akasema kwa presha.
"Kuna tatizo gani?" Alice akauliza.
"Ni kuhusu maisha yake... yako hatarini. Please mpe simu muda hautoshi..."
Kukawa na sekunde kadhaa za ukimya, kisha sauti ya Casmir ikasikika...
"Ken vipi?"
"Kaka ondoka haraka sana hapo! Mambo yamechacha..." Kendrick akasema.
"Kuna matatizo gani tena? Mbona umemfanya Alice ameogopa sana?"
"Samahani. Lakini maisha yako... labda hata ya familia yako nzima yako hatarini. Kaka, Kanali amefanya mpango kutuua mimi na wewe ndani ya masaa 24!" Kendrick akamwambia.
"Nini?" Casmir akashangaa.
"Ondoka haraka sana hapo maana tunavyoongea hivi inawezekana wameshaanza ku-move..."
"Ken, subiri. Nini... umetoa wapi taarifa hizi maa..."
"Nisikilize Casmir! Hakuna muda wa kuanza kuuliza maswali. Fanya haraka sana utoke huko. Hakikisha unaondoka na familia yako hata ukihitaji kuwaburuza sawa tu lakini mwondoke haraka. Nitakueleza kila kitu. Niamini Meja..." Kendrick akasema kwa heshima.
Simu ilikatwa, naye Kendrick akawa anatumaini kwamba Meja Casmir alikuwa amemwelewa vyema na kuanza harakati za kuondoka haraka sana. Kwa mbali aliweza kusikia mlio wa helicopter, naye akawa makini zaidi kwenye kuendesha huku anaangalia juu ili asije kutunguliwa kutokea angani. Alikokuwa anawahi ni kwenye nyumba yake, ambako aliishi mama yake na wasichana wale wawili ambao walikuwa ni ndugu wa kiukoo.
★★
Baada ya mwendo wa kama nusu saa, alifika maeneo ya nyumba yake na kuliegesha gari nje. Akawahi mpaka getini na kuanza kugonga kwa fujo akiwaita wadada wale ili wafungue upesi. Mlango mdogo wa geti ukafunguka, naye akaingia ndani haraka akimpita dada mmoja hapo ambaye ndiye alimfungulia, na akiwa anashangaa kwa nini kaka anapita kama anakimbizwa. Kendrick alifika mpaka ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwa mama yake, kisha akamwamsha akisema walihitaji kuondoka haraka sana.
Mama yake alikuwa anamshangaa mno, hasa ukitegemea ilikuwa usiku na hakujua mwanaye alikuwa anataka waende wapi. Akamuuliza tatizo lilikuwa nini, lakini Kendrick akamwambia tu kwa ufupi kwamba ikiwa wangeendelea kukaa hapo basi wangeuawa. Wadada wale wawili walikuwa mlangoni wakitazama mambo haya, naye Kendrick akawageukia na kuwaambia wamsaidie mama yake kujiandaa haraka ili waondoke kwa kuwa maisha yao yalikuwa hatarini. Akawaambia akihakikisha amewapeleka sehemu salama zaidi, ndiyo angeanza kufanya jitihada za kupambana na watu waliotaka kumdhuru.
Upesi akaelekea chumbani kwake haraka akiwaacha wanawake wanajiandaa. Aliwaambia wasibebe makolokolo yoyote bali wavae tu nguo nadhifu na yeye angeenda kuwapatia kila kitu walichohitaji mbele ya safari. Akiwa anaweka vitu vichache vya muhimu kwenye begi lake dogo, simu yake ikaita. Ilikuwa ni Casmir ndiye aliyepiga.
"Meja..." Kendrick akasema baada ya kupokea.
"Ken, tumeshatoka kule, lakini Alexandra hatuko naye," Casmir akasikika upande wa pili.
"Nini? Amekwenda wapi?" Kendrick akauliza.
"Alitoka kwenda kukutana na rafiki zake, lakini tumemtafuta na kumwambia asirudi nyumbani ila atukute kule kwenye ile nyumba ya mjomba wangu ya zamani... si unapakumbuka?"
"Ndiyo napakumbuka..."
"Basi nilikuwa nafikiri na wewe uje tukutane huko ili tupange mambo vizuri, halafu tuhakikishe tunawapeleka mahala salama zaidi..."
"Sawa kaka, nitafanya hivyo. Lakini Sandra akichelewa je? Umemwambia uzito wa suala hili?"
"Ndiyo nimemwambia na amesema ameelewa. Ana akili, ninajua atawahi..."
"Okay basi, na sisi tunaelekea huko sasa hivi. Umeongea na Jenerali kuhusiana na haya tayari?"
"Bado. Familia kwanza Kendrick. Wakiwa salama ndiyo tutajua jinsi ya kushughulika na hao washenzi. Wahi tafadhali..."
"Ondoa shaka Meja..."
Casmir akakata simu.
Kendrick akajisawazisha na kujiuliza ikiwa kuna jambo lolote la muhimu alisahau. Hapana. Alipoangalia kabati yake tena, akatuliza macho yake hapo kwa sekunde chache, kisha akavua begi na shati lake na kwenda kuifungua. Akatazama kwa makini ndani hapo, kisha akachukua vazi lingine na kuvaa, halafu akavaa na jaketi jeusi kwa juu. Akabeba begi lake na kutoka chumbani kuelekea sebuleni ili aondoke na wapendwa wake, pale aliposimama ghafla baada ya kukuta jambo lenye kushtua sana.
Luteni Weisiko alikuwa amefika. Alikuwa amesimama nyuma ya mama yake Kendrick, huku ameweka bastola nyuma ya kichwa chake. Mama yake Kendrick alikuwa anatetemeka kwa hofu huku analia kwa sauti ya chini. Hofu ilimwingia zaidi Kendrick kwa kuwa wadada wale wawili walikuwa wamelala chini, bila kuonekana kwa damu zozote, na hiyo ikamwambia kwamba walikuwa wamepigwa sehemu fulani mwilini na kupoteza fahamu haraka au maisha kabisa. Pembeni yake Weisiko walikuwepo wanajeshi wengine wawili, mmoja wao akiwa ni yule Goko, nao walikuwa wameelekeza bunduki zao kwa Kendrick.
"Kapteni Kendrick. Habari za wakati huu?" Weisiko akamsalimu.
"Luteni, nakuomba umwache mama yangu," Kendrick akamwambia.
"Nami nakuomba utoe bastola yako na kuirusha pembeni Kapteni," Weisiko akamwambia.
"Kwa nini unafanya hivi? Eeh? Unawaumiza watu wasio..."
"Bastola yako. Tupa chini pembeni," Weisiko akamkatisha kwa mkazo.
"Kenddd... hhh... Kennnn..." sauti yenye utetemeshi ya mama yake ikasikika.
Kendrick akatoa bastola yake na kuitupa pembeni. Luteni Weisiko akatoa ishara ya kichwa kwa Goko kuwa amfate Kendrick, naye akatii na kumfata. Akaanza kwa kulitoa begi mgongoni kwake, kisha akampapasa mwili mzima akitafuta kama alikuwa na silaha nyingine lakini akakosa. Kendrick alikuwa anamtazama mama yake kwa huruma, kwa sababu alijua kwa vyovyote vile watu hawa wasingemwacha akiwa hai. Akaanza kujilaumu moyoni mwake kuwa yeye ndiye amemsababishia mama yake mambo haya wakati angetakiwa kumalizia siku za uzee wake kwa amani.
Goko akamwambia Weisiko kuwa Kendrick hakuwa na chochote tena mwilini.
"Kwa mambo yote Kapteni, ninataka tu ujue kwamba hili suala si la kibinafsi. Niko hapa kutimiza wajibu tu," akasema Weisiko.
"Kuua watu wasio na hatia kwa tamaa za kibinafsi za wengine toka lini imekuwa ni wajibu wa mwanajeshi? Nyie vijana wote hamstahili kuitwa watumishi wa nchi hii. Nyie ni mashetani. Na ipo siku... IPO SIKU... yote mnayofanya yatawarudia..." Kendrick akasema kwa hisia sana.
Weisiko akang'ata tu meno yake huku anamwangalia Kapteni wake, na papo hapo akafyatua risasi iliyopasua kichwa cha mama mzazi wa Kendrick mbele ya macho yake. Mwili wake ukadondoka chini kwa kishindo kikubwa. Kendrick alifumba macho yake huku machozi yakitiririka kwa kuhisi huzuni kubwa sana. Kwa mtu mwenye mafunzo ya kivita kama yeye ilikuwa jambo la kawaida kuona watu wakifa, na hata alihusika kuwafundisha wanajeshi kuwa wanapaswa kujikaza sana kifo cha mwenzao kikitokea, lakini kifo kama cha namna hii kilimuumiza sana. Hakuweza kujikaza, akaanza kulia kwa uchungu.
"Nilitaka kufanya mambo kwa njia rahisi. Bila kuumiza mwingine yeyote. Lakini wewe kuja jengoni leo kumebadili hilo. Sina namna nyingine..."
"Huna namna??? Mshenzi wewe!!!" Kendrick akafoka kwa hasira.
Goko akamshika mikono kwa nguvu, na yule mwanajeshi mwingine akawahi kumsaidia. Kendrick sasa akawa anapumua kwa kasi huku akijaribu kujivuta, lakini wakamzidi nguvu kwa pamoja.
"Nakulaani Weisiko... ninalaani kizazi chako chote na yote ambayo unafikiri utayapata kwa kufanya unyama huu. Nilikuwa mwalimu wako... nilikutendea kama mdogo wangu... lakini umechagua ku..."
Kabla Kendrick hajamaliza kuongea, Weisiko akamfyatua risasi kifuani! Akaongeza mbili nyingine zilizompata sehemu ya tumbo na upande wa kushoto wa kifua akilenga moyo. Wanajeshi wale wawili wakamwachia na kumlaza hapo chini baada ya maneno yake kukatishwa kikatili namna hiyo.
"Usisahau kwamba hata mwanafunzi anaweza kuja kumzidi mwalimu. Lala salama... Captain," akasema Weisiko huku akirudisha bastola yake kiunoni.
Luteni Weisiko akatoka ndani ya nyumba hiyo pamoja na wanajeshi wake hao. Wakaenda mpaka kwenye gari walilokuja nalo; Weisiko akiingia na kuketi, lakini wanajeshi wale wakichukua madumu mawili ya mafuta na kurejea kwenye nyumba ile. Walienda na kuanza kuimwagia mafuta nyumba, mmoja nje, mwingine ndani; na baada ya kumaliza madumu yote mafuta, Goko akafyatua risasi kutokea nje kuelekea mlangoni iliyofanya moto mkali uanze kuwaka. Wote wakarudi upesi kwenye gari lao na kuondoka kutoka eneo hilo.
★★★
MASAA MAWILI KABLA YA KENDRICK KUPIGWA RISASI
"Happy birthday to you! Happy birthday to you! Happy birthday, Happy birthday... Happy birthday to you!"
Makofi yalisikika na vigelegele vya shangwe kutoka kwa familia na rafiki za Alice, waliokuwepo kwenye sherehe hii nzuri ya siku ya kuzaliwa kwake. Sasa ulikuwa ni wakati wa yeye kupuliza mishumaa na kutoa maneno ya kile ambacho angetamani kitokee (wish), lakini ijapokuwa alitakiwa kufurahia, hakujihisi vizuri kwa sababu mume wake hakuwa amefika bado. Watu wakawa wanamwambia apulize mishumaa midogo-midogo iliyowaka ambayo iliyozungushiwa kwenye keki yake kubwa, lakini yeye akawa anawaza tu mume wake yuko wapi kwa sababu aliahidi angewahi kufika, lakini mpaka sasa hakuwa amefika.
Watoto wake walimwangalia kwa huruma sana kwa kuwa walijua aliumia mno. Kwa kupoteza matumaini, akaona tu ainame kuelekea keki yake ili apulize, na hapo hapo sauti ikaanza kusikika ikiimba "happy birthday to you." Wote walitazama kutokea getini na kumwona Casmir akiwa amesimama huku anaimba wimbo huo kwa ajili ya mke wake. Wengi walifurahi sana kumwona, hasa watoto wake na mke wake pia. Alice alifurahi mno mpaka machozi yakaanza kumlenga kwani alikuwa amemkosa sana mume wake.
Azra pamoja na Sandra (akiwa ndani ya mwili wa Xander) wakamkimbilia baba yao na kumkumbatia kwa furaha. Kidogo hii ilimshangaza sana Casmir kwa sababu hakutegemea "Xander" angemkumbatia, bila kujua kihalisi aliyekuwa ndani humo ni binti yake. Xander akiwa ndani ya mwili wa Sandra akabaki tu kuwaangalia, nao dada zake wakaanza kutembea pamoja na baba yao kuelekea mpaka aliposimama Alice huku Casmir akimwimbia wimbo huo wa 'birthday,' na mikononi alibeba zawadi kubwa iliyofungwa kwa karatasi za urembo, kisha akaiweka chini na kumwambia Alice, "Make a wish."
Alice akainama kuelekea keki na kuipuliza mishumaa, na marafiki zake wote wakamshangilia sana. Yeye akamkumbatia mume wake kwa furaha sana huku Casmir akiomba samahani kwa kuchelewa. Kisha wakaanza kukata keki kwa pamoja, na wa kwanza kulishwa alikuwa ni Azra. Wakafata mapacha, kisha baba yao, na marafiki zao wote pia. Kila mmoja aliyelishwa alimlisha Alice pia, hivyo alikula keki nyingi sana.
Casmir hakuwa amechelewa mno kwani hata chakula walikuwa hawajala bado, hivyo ni wakati huo ndipo watu wakaanza kufata misosi huku wakiburudishwa na muziki. Casmir alikuwa akiongea na baadhi ya watu waliofahamiana naye sana, na baada ya hapo akaenda kuketi pamoja na familia yake ili wapate chakula na vinywaji pamoja. Maongezi yao yalitawaliwa zaidi na Azra, Sandra (ndani ya mwili wa Xander), na Alice. Xander akiwa ndani ya mwili wa Sandra hakuzungumza sana, na hii ilikuwa mpya kwa Casmir kwa sababu alizoea Sandra kuwa mchangamfu kwake, lakini sasa Xander ndiyo akawa mchangamfu kwake badala.
"Sandra, nakumbuka competition yenu ni Jumamosi. Najua umeshajiandaa vyema. Sijaisahau na Vaziri yako ipo kwenye gari," Casmir akamsemesha.
Xander akabaki kimya tu akiwa amejisahau kwamba alipaswa kujibu kwa kuwa mwili wa dada yake ndiyo ulikuwa unasemeshwa, hivyo ikabidi Sandra amshtue kwa kutumia akili.
'We Xander! Baba amekusemesha, mjibu!' akaongea kwa kutumia kichwa.
Sandra (Xander) akashtuka na kukuta wengine wanamtazama.
"Aaa... ndiyo. Nimeshajiandaa. Asante," akajibu.
"Nitajitahidi kuwepo pia," Casmir akasema.
"Sawa," Sandra (Xander) akajibu.
"Baba, siyo kujitahidi. Ufike bwana. Hii ni muhimu sana kwangu, nahitaji wote mwepo," akasema Xander (Sandra), akiwa amejisahau pia.
"Ahahahah... muhimu kwako? Siyo kwa dada yako?" akauliza Casmir.
"Oh, namaanisha... ndiyo, ni muhimu kwa Sandra... kwa sisi wote. Ataumia sana usipofika, si eti Sandra?"
"Yeah, yeah, nitaumia. Usiache kuja," akasema Sandra (Xander) bila kuwaangalia.
Mbadiliko huu wa tabia kati ya mapacha ulizidi kumchanganya Alice, ambaye bado alikuwa akijiuliza ni nini kilikuwa kinaendelea kati ya wanaye hawa. Casmir yeye alikuwa anaishangaa tabia mpya ya Sandra, ya kutojali, bila kujua kihalisi aliyekuwa humo ni Xander.
"Okay. Niliongea na Rojas wakati ule nimeenda Moshi, akaniambia nikusalimu. Unamkumbuka?" Casmir akamwambia "Sandra."
"Ndiyo, namkumbuka," Sandra (Xander) akajibu.
"Ndiyo nani huyo?" Alice akamuuliza Casmir.
"Ni jamaa fulani anaye... em' Sandra mwambie mama yako," Casmir akasema huku akiingiza chakula mdomoni.
Xander akaingiwa na wasiwasi kwa sababu alipaswa kujibu kuhusu mtu huyo asiyemfahamu kwa kuwa wazazi wake walifikiri wanaongea na Sandra. Lakini kabla hajaropoka, msaada ukaingia kichwani kwake...
'Rojas ni mkuu wa TUSA,' sauti ya Sandra ikasikika kichwani kwake.
"Aaam... Rojas ni mkuu wa TUSA. Anajuana na... baba pia... na mimi..." Sandra (Xander) akajibu bila kuwa na uhakika sana.
Alice aliweza kuhisi kuna hali fulani ya sintofahamu hapa katikati, naye akataka kuthibitisha zaidi.
Akamuuliza Sandra (Xander), "Kirefu cha TUSA ni nini?"
Sandra (Xander), akamwangalia kwa ufupi Xander (Sandra), naye Alice akatambua hilo. Kutokea kichwani kwa Sandra alimsemeshea Xander kirefu cha neno hilo.
'TUSA ni Tanzania University Sports Association...'
"TUSA kirefu chake ni Tanzania University Sports..."
'Association!'
"Association," Sandra (Xander) akasema.
Alice akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa, akijifanya kama hakuhisi lolote na kuendelea kula tu.
Waliendelea kupata mlo, na baada ya kutosheka wote wakanyanyuka na kuendelea na vitumbuizo vingine vichache kwenye sherehe hiyo. Alice alikuwa akiwatazama mapacha wake mara kwa mara ili kuona matendo yao. Kwa sababu aliwajua vizuri sana, angeweza kuona kwamba walikuwa wamebadilika kwa kiwango fulani kilichomfanya akose amani. Hivyo akaona amwambie Casmir kuhusu jambo hilo ambalo lilikuwa linamsumbua sasa. Akamwomba waende ndani ya nyumba ili wazungumze kwa ufupi. Casmir akafurahi sana akifikiri mke wake anaenda kumwambia ni jinsi gani alivyokuwa amem-miss sana.
Wakafika mpaka ndani na kuelekea kwenye chumba chao. Walipoingia tu Casmir akambana mke wake kwa nyuma huku akiibusu shingo yake kwa fujo nyingi, kitu kilichofanya Alice acheke kwa furaha. Akamgeukia mume wake wakiwa wameshikana kwa ukaribu namna hiyo, kisha Casmir akaanza kumpiga busu ya upendo. Alice aliifurahia busu hii iliyogeuka kuwa denda taratibu, lakini siyo kitu kilichokuwa kimemleta hapa. Baada ya kujitoa mdomoni mwake, akamwambia anataka waongee.
"Kunimiss sana kusifanye tuwaache wengine nje ili tu tujinome huku," Casmir akatania.
"Ahahah... hapana, siyo hivyo. Kuna jambo fulani nahitaji tuzungumzie. Ni kuhusu Alexander na Alexandra," Alice akasema.
"Ndiyo..."
"Unajua... sijui tu nikuelezee vipi, ni kama kuna jambo fulani wanaficha... au wanatuficha..."
"Kwa nini unasema hivyo?"
Simu yake Alice ikaanza kuita. Alikuwa ameishikilia mkononi lakini akaipuuza.
"Behavior zao zimebadilika. Wakati mwingine mpaka wananiogopesha..." akamwambia mume wake.
"Kwani kuna jambo baya wamefanya?"
"Hapana. Ni tabia... yaani... zimebadilika. Nawajua vizuri... na hizi siku mbili wamekuwa wanaonyesha tabia tofauti sana na jinsi ninavyowajua."
"Umejaribu kuongea nao?"
"Ndiyo nilijaribu kuongea na Sandra lakini alisema kila kitu kiko sawa. Pamoja na yote, lakini bado sikuridhika kwa kweli..."
Simu ilikuwa imeacha kuita muda huu, kisha ikaanza tena kuita. Alice akaitolea sauti bila kuangalia mpigaji.
"Labda unawaza kupita kiasi. I'm sure wako fine. Jeez, yaani hata Xander amenikumbatia leo..." Casmir akamwambia.
"Ndo' hicho Casmir. Hujiulizi inawezekanaje Xander akukimbilie kukukumbatia halafu Sandra abaki kukuangalia tu? Me naona kuna kitu hakiko sawa Cas..."
"Mh... okay usiwaze sana. Tutaongea nao ili kujua mengi zaidi. Lakini sasa weka worries zote pembeni darling... enjoy party yako!" Casmir akasema na kumtekenya kidogo.
Alice akacheka na kumsukuma nyuma kidogo. Simu yake ikaendelea kuita tena.
"Pokea simu, utanikuta nje sawa?"
"Haya..."
Casmir akatoka chumbani hapo na kuelekea kwa wengine. Alice alipoiangalia simu yake, akakuta mpigaji ni Kendrick. Akachekea kwa chini na kusonya kidogo, kisha akapokea huku akitabasamu....
★★
Casmir alifika mpaka nje na kukuta watu kadhaa wakiwa bado wanajifurahisha kwa muziki na vinywaji. Akamwona Azra, ambaye alikuwa amekaa kwenye viti vya nje karibu na mwingilio wa mlango wa ndani akibofya simu yake ya kioo. Akamfata hapo na kumshika begani.
"Baba..." Azra akamgeukia.
"Wewe, hausikii usingizi?" Casmir akamwambia.
"Ahah... hapa mpaka kukuche... ndiyo wamesema hivyo..." Azra akajibu.
"Mmmm... yaani utaweza kweli kukesha? Na unavyopenda kulala hivyo? Halafu kuna baridi, kwa nini usivae...."
Kabla hajamaliza kuongea, Alice akafika nyuma yake na kumwambia kwamba Kendrick alikuwa anataka kuzungumza naye. Baada ya Casmir kuona uso wa mke wake ukionyesha wasiwasi, akajua kulikuwa na shida. Akamuuliza ni nini kilikuwa kinaendelea lakini Alice akamwambia tu rafiki yake huyo alisema kuna jambo la muhimu sana alihitaji kumwambia. Akaichukua simu upesi na kurudi ndani ya nyumba haraka, huku Alice akimfuata taratibu.
"Ken vipi?" Casmir akasema baada ya kuiweka sikioni.
"Kaka ondoka haraka sana hapo! Mambo yamechacha..." Kendrick akasema upande wa pili.
Ni wakati huu Alice akawa amemfikia mume wake huku akionyesha sura ya wasiwasi.
"Kuna matatizo gani tena? Mbona umemfanya Alice ameogopa sana?" Casmir akauliza.
"Samahani. Lakini maisha yako... labda hata ya familia yako nzima yako hatarini. Kaka, Kanali amefanya mpango kutuua mimi na wewe ndani ya masaa 24!" Kendrick akamwambia.
"Nini?" Casmir akashangaa.
"Ondoka haraka sana hapo maana tunavyoongea hivi inawezekana wameshaanza ku-move..."
"Ken, subiri. Nini... umetoa wapi taarifa hizi maa..."
"Nisikilize Casmir! Hakuna muda wa kuanza kuuliza maswali. Fanya haraka sana utoke huko. Hakikisha unaondoka na familia yako hata ukihitaji kuwaburuza sawa tu lakini mwondoke haraka. Nitakueleza kila kitu. Niamini Meja..." Kendrick akasema kwa heshima.
Casmir akakata simu, naye akamshika mkono Alice na kuanza kwenda naye chumbani haraka sana. Alice alikuwa haelewi kinachoendelea.
"Alice, kuna jambo fulani haliko sawa. Maisha yetu yanaweza kuwa hatarini... tunahitaji kuondoka haraka!" Casmir akamwambia.
"What? What's going on? Nani anataka..."
"Listen, nahitaji uniamini katika hili. Wakusanye watoto tuondoke haraka sana. Kendrick amenionya kuwa wanaotaka kutuumiza wako karibu, kwa hiyo hatuna muda wa kupoteza. Please Alice... fanya haraka... Azra, mapacha, Salome..."
"Sawa, sawa, nafanya hivyo..." Alice akasema na kutoka chumbani upesi.
Casmir akaanza kuchukua vitu vya muhimu ambavyo angehitaji kwa ajili ya safari hiyo ya ghafla. Kichwani kwake yalipita maswali mengi sana ambayo hayakuwa na majibu sahihi. Kwa nini Kanali alitaka kuwaua? Tena hata na familia yake nzima? Kendrick alitoa wapi taarifa hizo? Ijapokuwa tahadhari hii ilikuja kwa kushtukiza sana, alimwamini Kendrick. Alijua rafiki yake angekuwa na vigezo vilivyojitosheleza vya kuamini kwamba maisha yao kweli yalikuwa hatarini, hivyo jambo la muhimu kufanya ilikuwa kutii onyo hilo haraka iwezekanavyo.
Casmir akiwa anaweka vitu kwenye begi dogo, wakaingia watoto wake pamoja na mama yao. Akashangaa kutomwona Sandra hapo.
"Alexandra yuko wapi?" akauliza.
"Ameondoka baba," akajibu Xander (ikiwa ni Sandra).
"Ameenda wapi?! Xander unawezaje kumwacha dada yako aondoke usiku huu wote?" Casmir akauliza kwa ukali.
"Amechukua tu gari akaniambia ameenda pale kona kuna rafiki yake anakutana naye..."
"Kona wapi?!" Casmir akafoka.
"Casmir, tulia. Cha muhimu sasa tumtafute, tumpate, tuondoke, sawa?" akasema Alice.
"Mama, baba, nini kinaendelea?" akauliza Azra.
"Kuna watu wanataka kutuumiza. Tunahitaji kuondoka upesi ili muwe sehemu salama..." akajibu Casmir.
"Wakina nani?" akauliza Azra.
"Ni wale waasi... Demba Group?" akauliza Xander (Sandra).
"Umemtafuta Sandra?" Casmir akauliza.
"Ndiyo, lakini hapokei simu..." akajibu Alice.
"Eh, Mungu wangu!" Casmir akaishiwa nguvu.
"Xander mpigie simu dada yako mpaka apokee... Azra twende kumsaidia Salome kuweka vitu vyetu," Alice akasema.
"Salome yuko wapi? Msiweke vitu vingi sana tusichelewe..." Casmir akasema.
Alice na binti yake mdogo wakatoka na kuwaacha "Xander" na baba yake chumbani humo. Xander (yaani Sandra) akawa anaipigia sana simu yake mwenyewe, kwa kuwa sasa walikuwa wamebadilishana simu na kaka yake kutokana na yeye kuwa mbali naye. Casmir baada ya kukamilisha vifaa vyake muhimu akatoka pamoja na mwanaye na kufika mpaka sehemu ya sebule. Wanawake nao wakaja hapo wakiwa wamebeba mabegi yenye vitu vichache. Baadhi ya watu waliokuwepo sehemu hiyo wakawa wanawashangaa.
"Xander..."
"Bado hapokei mama!" akajibu.
"Casmir... isije ikawa kwamba...." Alice akaishia hapo.
"No, hapana. Yuko sawa. Tutampata tu. Mpigie rafiki yake," akasema Casmir.
Sandra, akiwa kwenye mwili wa Xander, akawaza ni wapi ambapo Xander angekuwa amekwenda. Akasogea pembeni.
"Alice vipi? Mbona kama mnataka kuondoka?" rafiki yao mmoja akawauliza.
"Party imeisha. Jamani... kila mmoja anaweza kwenda nyumbani sasa, party imekwisha. Usiku mwema. Harakisheni," Casmir akaongea kwa sauti ya amri.
Wote waliokuwepo walibaki kushangaa tu, na mmoja baada ya mwingine wakaanza kujiondokea. Baadhi waliwauliza shida ilikuwa ni nini, nao wakawaambia tu kulitokea dharura ghafla. Sandra alitambua sasa baada ya kufikiria sana kuwa Xander hakukutana na "rafiki" yoyote, bali madam Valentina, hivyo akampigia madam ili kuuliza ikiwa bado alikuwa naye. Hakuwa amefanya hivi mapema kwa sababu ya kuchanganywa na hali nzima, ila sasa akakumbuka. Simu ya madam Valentina iliita bila kupokelewa mara ya kwanza, kisha mara ya pili akapokea.
"Hallo... Madam V..."
"Ndiyo... Alexandra mwenye besi..." akasema Valentina upande wa pili.
"Samahani... Xander yuko kwako?"
"Ndiyo..."
"Tafadhali naomba kuongea naye... ni muhimu sana..."
Baada ya sekunde kadhaa...
"Sandra vipi?" Xander akasikika (ikiwa ni sauti ya kike).
"Xander, toka huko haraka njoo nyumbani!" Sandra akamwambia kwa sauti ya chini.
"Mzee ameshaanza kumtafuta mdoli wake eeh?"
"Acha masihara. Kuna shida imetokea. Wahi nyumbani sasa hivi..." Sandra akasema kwa mkazo.
"Yeah... actually... sidhani kama n'tarudi leo maana huku mambo ni fire!"
"Xander... maisha yako yapo hatarini! Unapaswa kuni..."
"Xander, umempata dada yako?" Casmir akamkatisha huku anamfata.
Ikabidi akate simu haraka ili baba yake asije kuanza kuuliza "Sandra" alikuwa anafanya nini kwa mwalimu wake usiku huu wote ikiwa angeichukua simu.
"Hapana... ngoja niendelee kumtafuta..." akamjibu baba yake.
"Sasa tunafanyaje?" akauliza Alice.
Kufikia sasa, watu wote walikuwa wamekwishaondoka nyumbani hapo, hivyo Casmir akasema waende tu kwenye gari upesi na Sandra wangempata mbele kwa mbele. Wakawahisha mpaka ndani ya gari lao na kuliondoa hapo haraka sana. Casmir alikuwa ameongea na na walinzi wa nyumbani kwake kuwaambia wafunge nyumba vizuri kisha waondoke pia, naye angewatafuta baadae. Wakiwa ndiyo wameianza barabara tu, simu ya Xander (yaani Sandra) ikaita, na mpigaji alikuwa pacha wake. Akawaambia wazazi wake kwamba "Sandra" alikuwa anapiga sasa, naye Casmir akamwambia ampe Alice apokee kisha aweke sauti ya juu.
"Halloo..."
"Sandra... uko wapi?" akauliza Alice.
"Mama... niko huku kwa..."
"Unawezaje kuondoka bila kusema unakoenda? Una matatizo gani wewe siku hizi? Unajua kwamba lolote baya linaweza kukupata? UKO WAPI?!" akauliza Alice kwa hisia kali.
"Mama punguza jazba... niko kwa rafiki yangu. Kwani shida gani mpaka unafoka hivyo wakati hii siyo mara yangu ya kwanza?"
"Uliaga? Uliaga?"
"Basi Alice, inatosha. Sandra, uko wapi?" Casmir akauliza.
"Niko huku... mitaa siyo mbali sana na chuo..."
"Kote huko umeenda kufanya nini? Oh God... Sandra... nisikilize kwa makini. Kuna watu wanataka kutudhuru, na wanaweza kuwa popote pale muda wowote ule. Nahitaji kuwapeleka kwenye usalama. Sandra unanielewa? Maisha yako yapo kwenye hatari! Nataka ufanye kile ambacho nitakwambia haraka sana..." Casmir akasema.
"Ndiyo baba... nakusikiliza..."
"Unakumbuka nyumba ya babu yako Daudi ilipo? Kule tulipokuwaga tunawapeleka mkiwa wadogo kumtembelea?"
"Mjomba wako yule?"
"Ndiyo..."
"Yeah... napakumbuka. Lakini baba..."
"Nisikie. Nataka uje huko haraka sana. Ndiyo tunakoenda sasa hivi. Usiende nyumbani, na uhakikishe huongei na yeyote kuhusu hili. Sandra unanielewa dear? Harakisha mpenzi..." Casmir akaongea kwa hisia.
"Sawa baba. Nakuja..."
"Sawa," akasema Casmir.
"Kuwa mwangalifu Sandra. Nakupenda," akasema Alice huku machozi yakimlenga.
"Nakupenda pia mama..."
Kisha simu ikakatwa. Ndani ya gari hili walilokuwemo palijaa hali nzito ya wasiwasi. Casmir na Alice walimwaza sana binti yao. Sandra, akiwa ndiye Xander ndani ya gari, alimwaza pia kaka yake ambaye alikuwa mwenye mwili wake. Azra aliogopa, na Salome pia alikuwa na wasiwasi mwingi.
"Casmir... kwa nini usiongee na watu unaofahamu juu ya hili? General Pingu bila shaka anaweza kukusaidia, au marafiki zake wengine ambao..."
"Hapana Alice. Siyo rahisi kama unavyodhani. Sijui wa kumwamini. Ninaweza kuongea na mtu nikifikiri ni msaada kumbe ndiyo tatizo lenyewe. Singetaka kuwaweka nyie hatarini. Nataka kuhakikisha hamfikiwi na yeyote ndiyo nianze kudili na hawa wapumbavu sasa..." akasema Casmir.
"Baba nani anataka kutuua?" Azra akauliza.
"Sijui mpenzi. Lakini watu wanaoshirikiana naye pia tulidhani ni marafiki, kumbe ndiyo maadui. Isingekuwa ya Kendrick sijui ingekuwaje..."
"Kendrick yuko wapi?" Alice akauliza.
"Atakuwa amekwenda kwa mama yake, ndiyo yuko karibu zaidi. Ni yeye tu ndiyo ninayemwamini... wengine wote sijui... yaani sijui imekuwaje hivi... eti Meja nakimbizwa na... ahah... I can't believe this!" Casmir akaongea kwa masikitiko.
Alice na wengine walibaki kimya, wakimwonea Casmir huruma sana.
★★
Waliendelea na mwendo kwa zaidi ya dakika 30 bila kusemeshana lolote, nao wakawa wamefika eneo ilipokuwepo ile nyumba. Azra alikuwa amesinzia pamoja na Salome wakati huu. Wengine waliweza kuona nyumba ile ndogo kiasi ikiwa imetawaliwa na giza, na pembeni mwake hakukuwa na nyumba zingine kwani ilijitenga sana. Pande za huku kulikuwa tu na miti mingi iliyofanya paonekane kama msitu, lakini haikuwa ule wa kina sana.
Baada ya kuwa amesimamisha gari, Casmir akatoa simu yake na kumtafuta "binti yake" tena. Wakaongea, naye Sandra (Xander) akamwambia alikuwa njiani. Baada ya hapo, akaona ampigie na Kendrick ili kumwambia jambo la muhimu pia.
"Meja..." Kendrick akasikika baada ya kupokea.
"Ken, tumeshatoka kule, lakini Alexandra hatuko naye," Casmir akasema.
"Nini? Amekwenda wapi?"
"Alitoka kwenda kukutana na rafiki zake, lakini tumemtafuta na kumwambia asirudi nyumbani ila atukute kule kwenye ile nyumba ya mjomba wangu ya zamani... si unapakumbuka?"
"Ndiyo napakumbuka..."
"Basi nilikuwa nafikiri na wewe uje tukutane huko ili tupange mambo vizuri, halafu tuhakikishe tunawapeleka mahala salama zaidi..."
"Sawa kaka, nitafanya hivyo. Lakini Sandra akichelewa je? Umemwambia uzito wa suala hili?"
"Ndiyo nimemwambia na amesema ameelewa. Ana akili, ninajua atawahi..."
"Okay basi, na sisi tunaelekea huko sasa hivi. Umeongea na Jenerali kuhusiana na haya tayari?"
"Bado. Familia kwanza Kendrick. Wakiwa salama ndiyo tutajua jinsi ya kushughulika na hao washenzi. Wahi tafadhali..."
"Ondoa shaka Meja..." Kendrick akasema.
Casmir akakata simu na kumwangalia mke wake. Alipotazama saa, ilikuwa ni kasoro dakika chache itimie saa 8 kamili usiku. Akamwambia Alice asubiri kwanza ndani ya gari, kisha yeye akashuka na kuanza kuelekea kwenye nyumba ile huku akiwa makini. Mikononi alishika bastola kwa ajili ya tahadhari, naye akazunguka nyumba hiyo kwa umakini akiangalia kama kuna nuksi yoyote. Mjomba wake Casmir, yaani Daudi, alikuwa amekufa siku nyingi na nyumba hii hakumwachia yeyote. Wapo ndugu kadhaa ambao waliendelea kuishi hapo lakini baadae ikaachwa tu bila kuwa na yeyote wa kuitunza kwa sababu ilikuwa ya siku nyingi mno.
Baada ya kuhakikisha pako salama, akarejea kwenye gari na kuwaambia washuke ili kwenda kule ndani ya nyumba. Azra akiwa na usingizi sana akaamshwa pia na kutembea pamoja na wengine mpaka ndani kule. Baada ya kuwa wameingia, walikuta vifaa vingi vikiwa vimechakaa na vumbi likitawala sehemu kubwa. Alice akamuuliza Casmir ikiwa lilikuwa wazo zuri kwenda hapo, lakini mume wake akaweka wazi kuwa sehemu hii ilikuwa salama zaidi kwa wakati huu kwa sababu maadui zao wasingejua wapo huku.
Basi, Salome pamoja na "Xander" wakafanya-fanya usafi wa kadiri sehemu fulani za makochi yaliyokuwa ya zamani sana, kisha Alice akaketi huku Azra akijilaza hapo pia akiwa amemlalia mama yake mapajani. Kwa kuwa walibeba mashuka machache na blanketi, wakayatumia kumfunika Azra na kujifunikia pia mwilini. Casmir alikuwa anawaangalia wote kwa huzuni sana, akiwaza imekuwaje mpaka wakajikuta kwenye hali hii ghafla. Lakini akajifariji kuwa kila kitu kingekuwa sawa; cha muhimu kwanza ni kuwasubiria wakina Kendrick na "Sandra."
Zilipita dakika kadhaa wakiwa hapo, na kufikia wakati huu ni Casmir na Xander (yaani Sandra) ndiyo walikuwa macho bado. Wengine walikuwa wamepitiwa na usingizi kutokana na uchovu wa usiku. Kulikuwa na giza ndani hapo na mwanga pekee uliokuwepo ulitoka kwenye tochi ya simu ya "Xander." Casmir akamtazama mwanaye, ambaye alikuwa ametulia tu kwenye kiti huku amekunjia mikono kifuani.
"Unajua muda mrefu sana umepita, sikuwa hata nimetambua kwamba umenizidi urefu," Casmir akamsemesha.
"Ahahah... ndiyo. Hadi na ndevu nitakuzidi," Xander akatania, ikiwa ni Sandra ndiyo anaongea.
Casmir akatabasamu kidogo, kisha akasema, "Mama yako alikuwa anawaza kuhusu nyie wawili. Anasema hizi siku chache ni kama mmebadilika sana kitabia. Siwezi kujua mengi kwa sababu nakuwa mbali, lakini... nilitaka tu kujua ikiwa kila kitu kiko sawa."
"Ndiyo baba, kila kitu kiko sawa. Ni kwamba tu mama... anatupenda sana, kwa hiyo... hata kitu kidogo tu kinamhangaisha," Sandra akaficha ukweli.
Casmir akabaki kimya kwa ufupi, kisha akasema, "Unakumbuka kipindi kile tumeenda Serengeti?"
"Ndiyo! Nakumbuka... ahahah... wakati tumelala kwa tent wale nyani wakaanza kutufanyia fujo jinsi Azra alivyokung'ang'ania yaani..."
Casmir akacheka kidogo.
"Yeah ilikuwa ni kipindi ambacho nilifurahia sana. Kuwa pamoja nanyi. I wish siku zingerudi nyuma wakati ambao nilitumia muda wangu mwingi na nyinyi..." Casmir akasema kwa huzuni.
"Usijali baba. Cha muhimu ni kwamba tunajua upendo wako kwetu haubadiliki... hata ukiwa mbali kiasi gani..." Xander (Sandra) akasema.
"Mhmm... nilifikiri bado ungekuwa unanichukia kwa sababu ya hilo," akasema Casmir.
"Hapana baba... sikuchukii."
"Najua kwa sababu ya... hali tuliyopo... inawezekana... Ulikuwa sahihi kuniambia niachane na hii kazi... nisingeendelea nayo huenda haya yasingetupata..."
"Hapana baba siyo..."
"Ndiyo ukweli Xander. Nimetumia muda mwingi kutumikia wengine, kwa faida gani? Ili familia yangu ije iwekwe shabaha? Hakuna wa kulaumu kuhusu hili isipoku..."
"No, baba nisikilize. Haya siyo makosa yako. Sisi sote tunakupenda sana. Inaweza ikaonekana kama Xander anakuchukia, lakini siyo hivyo. Anakuwa anataka tu ujiingize zaidi kwenye maisha yake. Naweza kusema kati ya sisi wote yeye ndiye anakupenda zaidi..."
"Ahah... unavyojiongelea ni kama unasemea mtu mwingine..."
"Aam... yeah, napenda kufanya hivyo. Sote tunakupenda baba. Tunajua utapambana kwa ajili yetu no matter what. Pambana Meja... ninajua utashinda..."
Sandra akiwa ndani ya mwili wa Xander aliongea maneno hayo yaliyomtia sana moyo baba yake. Casmir akafarijika sana na kuhisi amepata nguvu zaidi kwa sababu alifikiri anayemwambia hivyo ni mwana wake ambaye kwa kipindi kirefu alihisi anamchukia.
"Kwa hiyo baada ya hapa tutaenda wapi?" Xander (Sandra) akauliza.
"Mimi na Kendrick tuliwahi kuwa na sehemu fulani iliyojificha chini ya ardhi kipindi kile wahamiaji haramu na waasi wamevamia. Nafikiri hiyo itakuwa ya kuanzia," Casmir akajibu.
"Ahahahah... tutaishi mapangoni sasa..."
"Ndiyo, kwa muda mfupi tu lakini. Na haitakuwa mbaya sana kwa sababu mtapata supply nyingi nzuri tu. Sema roho inaniuma kwa sababu Sandra anaweza kukosa competition yao Jumamosi na alikuwa amejiandaa sana..."
Maneno ya Casmir yalimhuzunisha sana Sandra kwa kuwa baba yake hakujua ilikuwa ni yeye ndiyo yuko hapo. Akaanza kuona ni kama hakukuwa tena na sababu ya kumficha baba yake ukweli wa kile kilichowapata yeye na Xander, hasa ukitegemea hali hiyo hawakujua jinsi ya kuitatua. Akanyanyuka ili amfate baba yake na kumweleza ukweli, pale alipohisi kitu fulani. Akatulia kwanza, na baada ya Casmir kumwangalia, akatambua kwamba mwanaye alikuwa anafikiria kitu fulani. Kisha Casmir akamwonyesha kwa ishara ya kidole kuwa asiseme lolote na ainame chini taratibu. Hii ilikuwa ni baada ya Casmir kusikia hatua za mtu fulani nje.
Baada ya Xander (Sandra) kuinama, Casmir akawa anaelekea dirishani ili kuchungulia nje, akiwa ameishika bastola yake kwa utayari. Akachungulia upande ule ambao aliegeshea gari lake lakini hakuona chochote kulizunguka. Sandra akiwa ndani ya mwili wa Xander akawasogelea mama yake, mdogo wake, pamoja na Salome, kisha akawaamsha polepole akiwapa tahadhari kuwa wakae kimya na kujiweka tayari kwa lolote. Wakajitahidi kuuondoa usingizi na kujiweka tayari, wakimtazama Casmir kwa umakini.
Casmir akahisi hatua zimefikia mlangoni, hivyo akawahi upande huo na kujibanza ukutani, huku akiwapa ishara ya mkono wengine kuwa wasogee mwishoni mwa kona ya nyumba wajifichie hapo. Wote wakatii na kuelekea huko, huku Azra akiwa amemkumbatia Alice kwa hofu. Casmir akaendelea kujibanza karibu na mlango akisubiri jambo fulani litokee, na papo hapo mlango ukagongwa. Akawaza kwamba huenda ilikuwa ni Kendrick au Sandra ndiye aliyefika, lakini bado alihitaji kuwa na uhakika kwa sababu ingeweza kuwa adui. Ila kabla hajafikiria la kufanya...
"Baba..."
Akasikia sauti hiyo ikiita, aliyoitambua upesi kuwa ni sauti ya binti yake kipenzi, Sandra. Alice pia alisikia, naye akaanza kufurahi sana pamoja na wengine.
"Sandra!" Casmir akasema akihisi faraja moyoni mwake.
Alice akatoka pale alipokuwa na kusogea mpaka karibu yake Casmir. Casmir akaanza kuufungua mlango upesi akiwa anataka kumwingiza binti yake ndani haraka, lakini papo hapo, Sandra, akiwa kwenye mwili wa Xander ndani hapo akatoka pale alipokuwa na kusema kwa sauti kubwa...
"Baba subiri!"
Tayari Casmir akawa ameshaufungua mlango na kukuta "binti" yake amesimama huku kichwani kwake akiwa amewekewa bastola! Aliona mkono tu ukiwa umetokezea upande wa ukutani, kisha mwenye mkono huo akajitokeza pia. Casmir akamtambua upesi, naye alikuwa, si mwingine, ila Luteni Weisiko mwenyewe.
"Habari za wakati huu Meja..." Luteni Weisiko akamsalimu.
Casmir alichoka. Alice aliogopa sana na kuanza kulia, huku mapacha nao wakiangaliana kwa huzuni sana....
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments