FOR YOU
Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA TATU
★★★★★★★★★★★★★★★★
"Mamaaaa!"
Watoto walitoa vilio vya huzuni baada ya kuona mama yao akilegea na kuangushwa chini. Xander akiwa kwenye mwili wa Sandra bado alihisi maumivu tumboni mwake, lakini baada ya kuona mama yake amepigwa risasi alihisi uchungu hata zaidi. Casmir aliona hilo, na kwa sababu ya hasira kali iliyomwingia alitumia nguvu zake zote kumshinda jamaa uwezo na kumnyang'anya bunduki ile, kisha akamtandika risasi kifuani akiwa karibu naye; kitu kilichofanya damu zake zimrukie usoni. Kisha papo hapo akageuka na kufyatua risasi iliyompiga Luteni Weisiko na kumwangusha chini.
Mambo haya yote yalimwogopesha sana Azra. Alikuwa anapiga kelele nyingi sana huku amemng'ang'ania Salome. Sandra akiwa ndani ya mwili wa kaka yake akamfata pacha wake pale chini na kumsaidia anyanyuke, naye Salome akaenda hapo pamoja na Azra. Wote wakawa wanamwangalia mama yao akiwa amelala pale chini, akiwa ametulia tuli. Walilia sana. Casmir pia alikuwa akilia mno, naye akausogelea mwili wa mke wake na kumwangalia kwa huzuni nzito sana.
Watoto walipoanza kumsogelea, akawazuia na kuwaambia waondoke haraka sana.
"Lakini baba..." akasema Sandra (Xander).
"No. Xander, mwahishe dada yako hospitali hilo jeraha ni kubwa. Nahitaji kumwondoa mama yenu hapa. Salome mwangalie sana Azra... nendeni... now!" Casmir akawasihi huku akiwapa funguo za gari lake.
Salome akaanza kuwasaidia Xander na Sandra kutembea, huku Azra akiwa ametangulia mbele na funguo za gari. Walikuwa wakielekea kwenye gari la baba yao huku Casmir akiurudia mwili wa Alice pale chini, na wakati tu walipolifikia, sauti ya juu ya mlio wa risasi ikasikika. Ilifuatwa na kilio cha maumivu kutoka kwa Salome, ambaye alikuwa ametandikwa risasi mgongoni kwake. Wote wakaanguka chini, huku mapacha na Azra wakiwa wameshtushwa sana na jambo hilo. Casmir aligeukia upande wa nyumba na kumkuta Goko akiwa amesimama hapo, huku akiikoki bunduki yake kubwa ili afyatue risasi nyingine tena.
Lakini Casmir akaanza kufyatua risasi za kwenye bastola aliyokuwa nayo kumwelekea pia, huku Goko akirudi ndani ya nyumba kujificha ili zisimpate. Mapacha wakanyanyuka ili kuweza kuingia kwenye gari pamoja na mdogo wao, lakini ni hapa ndipo wakasikia mlio wa risasi ukifuatwa na kelele ya maumivu kutoka kwa baba yao!
Wote walipotazama upande huo, waliweza kuona baba yao akiwa amepigwa risasi mgongoni, na aliyemfyatulia alikuwa ni Luteni Weisiko kutokea pale chini. Kumbe wakati ule Casmir alipompiga risasi, ilimpata sehemu inayokaribiana na begani, siyo moyoni kabisa, hivyo hakuwa amekufa bali alipoteza tu fahamu baada ya kuanguka kwa nguvu. Watoto walibaki kumwangalia baba yao akidondoka chini, na hapo Goko akatoka kule ndani na kuanza kuuelekea mwili wa Casmir pale chini kuhakikisha kama alikuwa amekufa. Xander, akiwa kwenye mwili wa Sandra uliokatwa kwa kisu tumboni, alijua wazi wenyewe ndiyo wangefuata, hivyo akajitahidi kuwaondolea butwaa dada zake ili wakimbie haraka.
Goko alipofika karibu kabisa na mwili wa Casmir, akamtandika risasi nyingine mgongoni kuhakikisha hainuki tena. Watoto hawa watatu sasa wakawa mayatima. Goko akamfata Weisiko ili kumsaidia anyanyuke, lakini jamaa akamwambia awashughulikie kwanza wale watoto na asimpoteze yeyote.
Goko alipowaangalia watoto, aliwaona wakiwa wameingia kwenye gari tayari, na hapo hapo akaichukua bastola ya Weisiko na kuanza kufyatua risasi kulielekea gari hilo; hasa kwenye vioo na matairi. Kwa kuwa gari lilikuwa halijageuzwa bado ili kuondoka, risasi zilipiga tairi na kufanya lisiweze tena kutembea, huku ndugu hao watatu wakiwa wameinama kwa ndani ili risasi zisiwapate. Xander akawaambia wenzake watoke kupitia milango ya upande mwingine, na ni hapa ndiyo akatambua kwamba Sandra alikuwa amechunwa na risasi moja pajani.
Ilikuwa ni shida juu ya shida. Sandra, akiwa ndani ya mwili wa kaka yake akajikaza na kutokea upande wa pili wa gari pamoja na wenzake, nao wakaanza kukimbia kuelekea kwenye miti mingi; ikionekana kama msitu wa eneo hilo. Weisiko akajinyanyua na kuchana sehemu ya nguo ya Alice, kisha akaanza kujifunga sehemu ya jeraha lake akisaidiwa na Goko. Akamwambia hawakupaswa kuwaacha watoto hao watoroke, hivyo upesi wakabeba silaha zao na kuanza kuwafata huko huko.
Baada ya mapacha na mdogo wao kujitahidi kukimbia msituni hapo penye giza kwa sekunde kadhaa, mambo yalizidi kuwa magumu kwao hasa kwa sababu ya mwili wa Sandra (Xander) kuishiwa nguvu kutokana na kisu alichochomwa tumboni. Pacha wake alijitahidi kumkokota hivyo hivyo ili watoroke, lakini Xander alijua angewafanya wakamatwe upesi kwa sababu ya yeye kuwa mzito. Walifika sehemu fulani naye Xander akamwambia Sandra amwache nyuma ili dada zake wakimbie pamoja.
Sandra akawa anakataa, lakini Xander akamshawishi kwa kumwambia ni bora hata kama akifa yeye lakini ndugu zake wawe na nafasi kubwa ya kupona kuliko ikiwa wote watauliwa. Kwa hiyo akamwambia waelekee upande mmoja, halafu yeye atajitahidi kuelekea upande mwingine akiacha viashiria kwa wanaume wale ili wamfate yeye tu. Sandra akiwa kwenye mwili wa Xander alilia sana. Azra alilia pia mno, nao wote wakamkumbatia ndugu yao, kisha akawasihi wawahi haraka maana alijua wale wapumbavu walikuwa nyuma yao.
Sandra akaondoka na Azra kuelekea upande mmoja, kisha Xander, akihisi udhaifu mkubwa sana kwa sababu ya kupoteza damu nyingi kwenye mwili wa dada yake, akajitahidi kulivua sweta alilopewa na Valentina, kisha akapiga hatua chache kuelekea upande mwingine na kuliangusha chini makusudi, ili wale watu wakiliona upande huo waendelee kuufuata huo huo. Alijikongoja kilegevu tu huku akitumaini dada zake wangefika mbali sana, kwa sababu alijua yeye asingeweza. Akafika sehemu fulani na kujikalisha chini ya mti akiugulia maumivu makali ya kidonda chake kikubwa tumboni.
Weisiko na Goko walikuwa wamefika sehemu ile na kuliona sweta pale chini, na upesi Goko akamwambia Luteni wake huyo kwamba watoto watakuwa upande huo, hivyo wawawahi. Lakini Weisiko akamzuia kwanza. Kutokana na mafunzo yake, aliweza kubaini kwamba huo ni mpango wa kuwachengua, na kwa haraka akakisia kwamba watoto walijigawa na kwenda pande tofauti. Akaangalia upande ule ambao Sandra na Azra walielekea, naye akamwambia Goko afatilie ule ambao ulikuwa na sweta pale chini, halafu yeye angeenda huu mwingine. Balaa!
Goko akaanza kuelekea kule alikoenda Xander, huku Luteni Weisiko akitoka kwa kasi zote kuelekea kwa dada wale wawili. Goko alifika mpaka sehemu ya msitu ambayo ilimchanganya sana na hakujua aelekee wapi tena. Akawa anaangaza huku na huko akitumaini kuona jambo lolote, hasa kwa sababu alikuwa ameyazoesha macho yake giza la msitu. Kutokea aliposimama, mti wa nyuma yake ndipo alipokuwa amekaa Xander, na alikuwa akijikaza ili asitoe sauti yoyote ile, na akiomba Mungu mjinga huyo apitilize. Lakini eti ndiyo likasimama hapo hapo kabisa huku linajiuliza pa kwenda.
Kutokea upande mwingine wa msitu, Xander na Goko waliweza kusikia sauti za milio ya risasi, nao wote wakashtushwa na hilo. Goko aliwaza huenda ni Luteni Weisiko ndiyo amewapata vijana wale wengine, naye Xander ndiyo akatambua kwamba mpango wake wa kuwachengua wawili hawa haukufanikiwa na inawezekana ndugu zake walikuwa wamepatwa na baya. Maumivu yalimzidia, naye alijua hangeweza kuendelea kujificha, kwa hiyo kama angekufa, basi angekufa kibishi.
Chini hapo aliweza kushika jiwe kubwa kidogo, naye akaanza kujinyanyua taratibu huku akikaza kichwa chake sana ili asitoe sauti yoyote, lakini Goko akahisi kuna jambo fulani nyuma yake. Ile Xander alipotaka tu kumpiga nalo kwa nyuma, Goko akawahi kugeuka, hivyo likampiga sehemu ya bega huku naye akifyatua risasi iliyopiga hewani. Xander akadondoka chini kiudhaifu, naye Goko akajiweka sawa na kuikoki tena bunduki yake ili wakati huu asifanye makosa tena.
"Mmetusumbua sana nyie madogo... yote haya ya nini kama kifo kitawapata tu?" Goko akamwambia.
Xander akawa anajivuta-vuta hapo chini huku anamwangalia kilegevu, akiwa anajua huo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Lakini, mara ghafla akaona kama kitu fulani cheusi kinatokea nyuma ya Goko, na kilikuwa kinajongea taratibu sana kwa njia ya kuvizia. Akatoa macho kwa hofu kwa kuwa hakuweza kukiona vizuri, naye Goko akatambua hilo. Ile naye amegeuka tu, kitu hicho kikamrukia na kuanguka naye pembeni, jambo lililomwogopesha sana Xander (akiwa ndani ya mwili wa Sandra).
Akaanza kujivuta kutoka hapo huku akisikia sauti za Goko za maumivu, na kukuru-kakara zikitokea hapo. Hakuweza kujua kitu hicho ni nini, lakini ilionekana kama ni mtu; ila bado hakuwa na uhakika. Aliwaza labda ilikuwa ni mnyama, lakini bado alionekana kama mtu. Alijitahidi kujongea kwa nguvu ndogo alizobakiza, naye sasa akawa anakwenda ovyo ovyo tu bila kujua anakoelekea. Wazo lililokuwa kichwani mwake ni kwamba ingekuwa bora kufa kwa risasi, siyo kutafunwa na mnyama. Kwa hiyo bado akawa anajaribu kunusuru uhai wake masikini.
Ilifikia hatua akaishiwa nguvu kabisa na kuanguka chini. Alikuwa anapumua kwa shida huku macho yake yakifumba na kufumbua kilegevu sana kutokana na kuhisi kizunguzungu. Lakini kutoka masikioni mwake, aliweza kusikia sauti za vilio, na moja kwa moja akatambua sauti hiyo kuwa "yake." Yaani, sauti ya mwili wake, hivyo akajua huyo alikuwa ni Sandra. Akafumbua macho kwa nguvu, naye akaanza kujitahidi kufatilia upande sauti hiyo ilikotokea. Akajigeuza taratibu na kuanza kujiburuza, akiumia sana tumboni, lakini akawa anataka sana kumwona pacha wake.
"Usiniueee... pleeease... please usi... usiniueee...
Sauti hiyo ikawa inasema maneno hayo kwa kilio. Xander akaweza kujivuta mpaka sehemu ambayo ilimwezesha kumwona Sandra, akiwa amekaa chini huku ameviunganisha viganja vyake kama anaomba sana aonewe huruma. Huo ulikuwa ni mwili wake wa kiume, na chini yake akamwona Azra akiwa amelala tuli. Xander akaanza kulia kwa maumivu sana, akishindwa hata kunyanyuka ili kwenda kutoa msaada. Akasema kwa kutumia akili yake 'Sandra... Sandra...'
Xander akasikia sauti ya Luteni Weisiko ikisema, "Nisamehe... hii ni sehemu tu ya kazi yangu."
Hakuweza kumwona Luteni Weisiko, lakini sasa akajua kuwa huyo ndiye ambaye 'dada yake' alikuwa anamwomba asimuue.
Kutoka kichwani kwake, Xander akasikia sauti ya dada yake ikimwambia, 'Xander... popote ulipo... jua nakupenda sana pacha wangu. Tafadhali pambana usalimike... usisahau hili kamwe... for me....'
Xander alijua dada yake alikuwa anamkumbusha msemo wao waliopenda sana kuambiana, na kabla hajaweza kumjibu kwa kichwa, hapo hapo ikasikika sauti ya risasi, naye akauona mwili wake, ukiwa na dada yake kwa ndani, ukianguka chini karibu kabisa na Azra. Xander alihisi uchungu mwingi sana, kwa kutambua kwamba sasa alikuwa amebaki peke yake, na akiwa hana matumaini yoyote ya kupona. Aliumia sana moyoni.
Hivyo, akaona ni bora tu kama na yeye akienda hapo ili afe akiwa pamoja na ndugu zake. Akaanza kujiburuza tena, naye akavuta nguvu yote ndogo iliyobaki mwilini mwake ili amwite Luteni Weisiko, pale mkono fulani ulipouziba mdomo wake kutokea kwa nyuma! Xander alijaribu kufurukuta, lakini akawa hana nguvu za kufanya hivyo. Aliishiwa nguvu kabisa, huku akihisi mwili wake ulipoanza kuvutwa kwa nyuma, na giza zito likafunika macho yake.
Kutokea pale alipokuwa amesimama Luteni Weisiko, aliwaangalia sana watoto wale pale chini. Yeye aliona ni Xander na Azra, bila kujua aliyekuwa ndani ya mwili wa Xander ni Sandra. Alikuwa ameusikia mlio ule wa risasi aliyopiga Goko hewani muda ule amemkosa Xander (akiwa kwenye mwili wa Sandra), hivyo alikuwa amechukulia kwamba Goko alimkamata Sandra na kumuua.
Weisiko akawasogelea wawili wale pale chini na kuwatazama sana, naye akachuchumaa na kuushika uso wa Azra. Alimwangalia mno binti huyo mdogo, kisha akatoa simu maalumu za kijeshi (walkie talkie) na kupiga kwa mtu fulani. Baada ya kupokelewa, Luteni Weisiko akasema tu maneno haya:
"Mission Accomplished."
★★★★
WIKI CHACHE ZILIZOFUATA....
Mambo yalizidi kuwa mabaya sana ndani ya serikali. Kundi la Demba Group, ambalo lilikuwa lenye baadhi ya wanajeshi mahiri na waasi wakiongozwa na Luteni Weisiko na Kanali Jacob Rweyemamu kisiri, lilifanikiwa kuiua familia nzima ya Jenerali Pingu, ikiwemo na yeye pia, na Luteni Jenerali Geneya Oyayu. Waliacha ujumbe kuwa taratibu wangehakikisha viongozi wengi wanauawa pia. Haikujulikana waliweza vipi kufanya hivyo, lakini njia zao zilikuwa zenye urahisi fulani kutokana na wenyewe kuonekana kuwa wanajeshi walioaminika. Wanajeshi wengi waliingia kwenye msako wa hadharani nchi nzima ili kuweza kuwakamata, lakini waliambulia patupu.
Raisi alikuwa ametoa tamko kuhusiana na maovu hayo, kwa kusema kwamba angehakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa, lakini hofu ikazidi kutanda baada ya mabomu yaliyotegeshwa kwenye mabweni ya shule maalaumu za kutunza watu wenye ulemavu (upofu, viungo vya mwili, na akili), yaliyosababisha maafa ya watu 210 ndani ya siku moja; na yote yakilipuka sehemu tofauti ndani ya muda ule ule. Watu hawa walikuwa wakatili sana, na bado hawakuweza kukamatwa.
Wananchi wengi walianza kufanya fujo kwa sababu waliilaumu serikali kuwa iliangalia tu vitendo hivyo bila kufanya lolote zaidi ya kubwabwaja tu. Walishangazwa sana na jinsi ambavyo mambo haya yalikuwa yakiendelea bila serikali yao kufanikiwa kuwakamata waasi hao, hivyo wengi wakawa wakiandamana na kufanya fujo nyingi wakitaka Raisi ajiondoe madarakani kama Demba Group walivyotaka. Walijaribu kutulizwa sana lakini ghasia walizofanya zilisababisha taifa liwe chini ya msukosuko mkubwa kupita maelezo.
Raisi aliyekuwepo madarakani, alitoa video fupi iliyomrekodi yeye akizungumza maneno yaliyowalenga Demba Group, akitaka kujua kwa nini walitaka aondoke madarakani na ni nani ambaye walimtaka awe Raisi sasa. Jibu lilikuja kupatikana kupitia video iliyosambazwa mitandaoni, ya kundi hilo, na kiongozi wao aliyeficha uso wake akasema kwamba wenyewe walichotaka ni Raisi kujiondoa, mengine yangefuata, la sivyo visa vya kikatili kutoka kwao vingeendelea.
Muungano wa nchi za mashariki ulijaribu kutoa msaada maalumu kwa Raisi ili kushughulika na suala hili, lakini hiyo haikusaidia kwa lolote kwa sababu watu hawa walijua vizuri sana nyendo ambazo zingefuatwa, hivyo wenyewe wangetokeza njia zingine za kufanya maovu yao. Raisi alikuwa akipewa ulinzi mkubwa sana pamoja na viongozi wengi, lakini bado Demba Group wakafanikiwa tena kuwaua wabunge kadhaa na madiwani.
Hali hii ilitisha na ilichosha! Vurugu zilitanda kila kona, ilikuwa ni kama Taifa limeingia kwenye kipindi cha maafa, kwa sababu ijapokuwa hii ilikuwa vita, bado haikueleweka ni vita ya aina gani. Sehemu nyingi kama mashule na vyuo vilifungwa ili kuepushana na watu wengi kuendelea kuumia.
Kwa sababu mambo yalizidi kuwa mabaya sana, Raisi alitangaza kujiuzulu yeye mwenyewe, na kwa sababu haikuwa kipindi cha uchaguzi, kisheria sehemu yake ingepaswa kuchukuliwa na Makamu wake, mheshimiwa Paul Kalebu Mdeme. Huu ndiyo uliokuwa mpango mzima. Makamu huyu wa Raisi mpaka sasa alikuwa akijifanya yuko upande wa serikali yao, na Raisi pia, lakini kihalisi ni yeye ndiye aliyeongoza mambo yote hayo ili kuweza kuinyakua nafasi ya Raisi mapema.
Kwa hiyo baada ya Raisi kujiuzulu, Mdeme akaichukua ngazi ya uraisi kwa urahisi. Lakini mambo aliyokuwa amefanya kufanikisha yote haya yalikuwa ni mabaya kupita maelezo. Kabla ya kujiuzulu kwake, Raisi aliyepita alikuwa ametoa onyo la wazi kwa wananchi kwamba hata nani aingie madarakani, sikuzote watu hawangeridhishwa tu. Yeye alikuwa amejitahidi sana kulijenga-jenga taifa, na wengi walimpongeza kwa jitihada zake. Lakini matatizo haya yalipoanza, mazuri yake hayakuonekana tena. Ila alielewa fika kuwa hofu iliyokuwa imejengwa ilikuwa kubwa, na ndiyo maana akaachia tu cheo chake.
Baada ya Makamu Paul Mdeme kuwa Raisi rasmi, alitoa ahadi kwa wananchi kwamba mambo mengi yangekuwa sawa zaidi sasa, na hawangeacha kuwatafuta wabaya wao. Alisema hakujua ni kwa nini Demba Group walifanikiwa kufanya mambo yote hayo bila kukamatwa, ila kama kuna mtu au watu waliokuwa wanawaficha, hata kama ilikuwa chini ya mahandaki, wangewakamata tu. Akaongea kinafiki kwamba vifo vilivyotokea haviwezi kusahaulika, hivyo alijua kuwapata waasi hao na kuwaadhibu ilikuwa jukumu lake.
Wananchi hawakujali nani ni Raisi, walichokuwa wanaangalia sasa ni kama hali zingetulia kwa kuwa Demba Group waliahidi Raisi akijiondoa tu, wangeacha mambo hayo. Hakukuwahi kutokea tukio kubwa namna hiyo la uasi bila waasi kukamatwa, hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza. Kwa hiyo wengi bado walishangaa sana iliwezekanaje watu hao kutojulikana mpaka wakati huu. Wafiwa walifanya misiba kwa ajili ya wapendwa wao wengi waliopoteza uhai, na Raisi mpya alitoa msaada mkubwa wa njia ya rambirambi kwa pesa kwenye KILA familia iliyopatwa na matatizo hayo.
Mambo ambayo "Raisi" Paul Mdeme alikuwa ameanza kuyafanya yaliwafanya watu wamwone kuwa mwenye hisia-mwenzi sana (compassion), bila kujua kihalisi yeye ndiye shetani aliyesababisha vifo hivyo vyote.
Kwa kuwa sasa Paul Mdeme alikuwa na nguvu sana kama Raisi, alitumia uchochezi wake kuwapatia vyeo vya juu Kanali Jacob Rweyemamu na Luteni Weisiko. Ni mambo yaliyoshangaza baadhi ya watu jeshini kwamba Kanali Jacob alipandishwa cheo na moja kwa moja kuwa Jenerali wa jeshi la nchi baada ya kifo cha Jenerali Pingu, naye Luteni Weisiko akawa ndiye Luteni Jenerali baada ya Geneya Oyayu kuuawa. Lakini bado ukweli ulikuwa umefichika mpaka wakati huu, hivyo watu hawa wabaya wakawa juu zaidi na kuendelea kufanya mipango yao mingine ya kibinafsi.
Tokea Raisi aliyepita alipojiuzulu, Demba Group hawakusikika tena. Yaani walikuwa wametoweka tu mbele ya maisha ya watu baada ya Raisi mpya kuingia. Paul Mdeme alijitahidi sana kujifanya ni Raisi mwema kwa wananchi, ikionekana kuwa baada ya yeye kuingia aliweka mfumo mkali sana wa ulinzi uliowafanya Demba Group waogope, hivyo watu wengi walimsifu. Kihalisi, wanajeshi wale waliokuwa wakimuunga mkono kwa matendo hayo, ambao ndiyo walijifanya kuwa Demba Group, walikuwa wamepewa pesa nyingi sana kwa kazi zao. Hivyo nao wakaendelea kuwepo tu jeshini bila kutambulika, kwa hiyo ishu ya Demba Group ikaanza kuonekana kuwa historia.
Ndugu na marafiki wa familia ya Casmir waliwaombolezea sana kwa siku nyingi. Valentina na Raymond waliumia sana kujua kwamba hawangeweza kuwaona wapenzi wao tena. Sophia, Mecky, Lucas, Benjamin, Bernard, Hussein, na Ramla pia, walihuzunishwa sana na habari za vifo vyao. Waliowaua walifanya vilevile walivyoifanyia familia ya Kendrick; waliwarudisha kwenye nyumba ile ya mjomba wake Casmir na kuwaingiza, kisha kuichoma kwa moto. Kwa hiyo kihalisi miili iliyozikwa ilikuwa imekauka sana mpaka kufikia hatua ya majivu.
Kukawa na vipindi maalumu vya televisheni vilivyozungumzia maisha ya viongozi wa serikalini na jeshini waliokufa kwenye matukio hayo ya uasi. Na ingawa bado Demba Group hawakufichuliwa, ilitiliwa mkazo sana kwamba jambo hilo halingekuja kutokea tena chini ya utawala wa Paul Mdeme. Ahadi nyingi ambazo Raisi huyu mpya alitoa zilianza kutimizwa kwa kasi sana, hivyo watu wengi walizidi kumpenda, ilhali baadhi waliona makosa mengi pia kwenye njia zake za kuongoza mambo.
★★★
OFISI YA JENERALI
Jenerali Jacob Rweyemamu, akiwa amejaa mafanikio sasa baada ya "kupanda juu," akawa kwenye ofisi yake akifanya kazi fulani kwa utulivu mida ya jioni. Ni baada ya kujulishwa na msaidizi wake kwamba mgeni aliyekuwa anamsubiria amefika, ndipo akaachana na kazi zake na kuamuru mgeni huyo afike ndani ya ofisi. Baada ya msaidizi wake kuondoka, akaingia mwanaume aliyemfahamu vizuri sana, na kwa furaha akanyanyuka ili kwenda kumlaki. Mwanaume huyu akapiga saluti ya heshima kumwelekea Jenerali, naye Jenerali Jacob akasimama mbele yake akiwa anatabasamu na kumpiga-piga mabegani kirafiki.
"Luteni Jenerali Weisiko! Aah... inapendeza sana hahahahaaa," Jenerali Jacob akamsifia.
"General... habari za siku?" Luteni Jenerali Weisiko akamsalimu.
"Ni nnnzuri sana! Tena zinazidi kuwa nzuri kwa sababu yako. Unapiga sana kazi kijana wangu. Unastahili wake 10 kabisa," Jenerali Jacob akamwambia.
"Kama msemo wa mwanafalsafa, bado nipo nipo kwanza," Luteni Jenerali Weisiko akatania.
Jenerali Jacob akacheka na kumpiga-piga bega tena, kisha akamwambia waketi ili wazungumze.
"Singida wanasemaje?" Jenerali Jacob akamuuliza.
"Wako poa. Hawatangulizi mapenzi, ila vitunguu tu. Sebastian amenipa salamu zake nikufikishie pia," Weisiko akajibu.
"Hahahah... Unamwonaje Brigedia wetu huyo?" Jacob akauliza.
"Anapiga kazi... anawaongoza vizuri sana vijana wake na..."
"Nilikuwa namaanisha, na yeye anaweza kuwa asset nzuri upande wetu, au?" Jacob akamkatisha.
"Mmm... kiukweli... sina uhakika sana General. Bado na yeye ana mwelekeo wa Pingu-Pingu hivi. Kwa hiyo kwa masuala yetu sidhani kama itakuwa sawa kumwingiza," Weisiko akamwambia.
"Hmm... Okay. Lakini ninafurahi sana kwamba Mdeme ametuongezea na ally wengine. Viongozi wengi wanamkubali sana lakini kwenye hili game ni sisi saba tu. Yeyote atakayejaribu kutuzingua... you know the drill," Jacob akasema.
"Ndiyo Jenerali. Mambo yote tunayafanya kwa umakini sana. Mdeme kweli anajua kututunza," akasema Weisiko.
Jenerali Jacob akacheka.
"Ni nzuri sana ukifanya kazi ngumu na kuibuka mshindi. Vijana wetu wako vizuri sana. Mdeme alikuwa anahofia kwamba labda baadhi ya hao waliotumika wangetusaliti, lakini nikamhakikishia wote tunao mfukoni. Usiache kusisitiza umuhimu wa wenyewe kuwa kimya kuhusu mambo yote, la sivyo..."
"Ndiyo najua General. Nitahakikisha mambo yote yanakuwa sawa."
"Ulifanikiwa kumpata?" Jacob akauliza.
"Hapana, lakini nafikiri nimetambua alikoishia. Baada ya kukuta Goko amekufa, nilijua huyo msichana amemtoroka kwa hiyo nikafatilia trace zake za damu. Sehemu zilipoishia ni kwenye bonde refu sana kuelekea chini. Inaonekana alidondokea humo," Weisiko akaeleza.
"Inaonekana? Weisiko tunatakiwa kuwa makini sana. Vipi kama huyo binti alisalimika?"
"Hapana General, haiwezekani. Ilikuwa ni usiku, na nilikuwa nimemkata vibaya sana tumboni. Sijui alimshinda vipi akili Goko, lakini asingeweza kufika popote maana huo msitu ulikuwa ni dead end... na kudondokea kwake kule ni kifo moja kwa moja," akasema Weisiko.
"Okay sawa. Mlitumia akili kuweka miili ya watu wengine ichomwe ili ionekane ndiyo wenyewe. Kazi nzuri kwa hilo. Ninatumaini mambo haya hayatasikika tena," Jacob akasema.
"Ondoa shaka General. Huu ndiyo mwanzo tu wa kufurahia matunda ya jasho letu..."
"Hahahahah... kweli kabisa," Jacob akasema kwa furaha.
"Vipi kuhusu.... ameshafika India salama?" Weisiko akauliza kwa hisia.
"Ndiyo. Ameshafika," Jacob akajibu.
Weisiko akaangalia chini kwa utulivu.
"Nini hasa kilichosababisha ukashindwa Weisiko? Usiniambie ulikuwa soft..." Jacob akamuuliza.
"Hapana siyo hivyo. Ni kwamba tu..." akaishia hivyo.
"Alikukumbusha kuhusu Mary?" Jacob akasema.
Weisiko akatikisa kichwa taratibu kukubali.
"Well... nimefanya vile kwa ajili yako kwa kuwa uliniomba. Ila jambo hili linapaswa kuwa siri kati yetu, hata Mdeme hapaswi kujua. Nambiar anajua njia watakazotumia ili kumfanya awe kama tunavyotaka, kwa hiyo najua kila jambo litakuwa sawa," Jenerali Jacob akasema.
"Amefikia wapi?" Weisiko akauliza.
"Nimeongea na Nambiar akanijulisha wamempeleka Kerala kwenye sehemu ya siri sana kwa ajili ya hiyo ishu. Anaaminika, najua ata-deliver," Jacob akasema.
"Ni wapi kabisa?"
"Itakuwa bora usipojua. Focus kwanza kwenye mambo unayohitajika kufanya, yeye atakuwa salama. Ikiwa mambo yataenda vizuri, basi atakuwa msaada kwetu mbeleni. Trust that," Jenerali Jacob akasema.
Wawili hawa walikuwa wakizungumzia jambo fulani kubwa sana walilofanya kutokana na matukio yale ya kikatili waliyoshiriki kutenda. Na kama Jenerali Jacob alivyomwambia Weisiko, ilifaa kubaki kuwa siri ili kuja kuanza kuitumia kwa wakati unaofaa. Wakaendelea na maongezi yao mengine kuhusiana na kazi, kisha Luteni Jenerali Weisiko akamuaga Jenerali Jacob Rweyemamu na kuondoka jengoni hapo.
★
Siku zikazidi kwenda, na Taifa likaonekana kuanza kujinyanyua tena kutoka pabaya pale lilipokuwa kwa kipindi kile kifupi na kusonga mbele. Wenye kufanya maovu sasa ndiyo wakawa juu zaidi, wakifurahiwa na watu ambao hawakujua mabaya yao kwa sababu walijionyesha kuwa watetezi wazuri wa haki na walijali mahitaji yao, na muda ukazidi na kuzidi kusonga mbele kukiwa na mambo mengi sana yaliyojificha, ambayo muda ungekuja kuyafichua mbele ya safari......
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Huo ndiyo mwisho wa msimu wa kwanza. Sehemu zitakazoendelea zitaanzisha msimu wa pili.
Comments