MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
★★★★★★★★★★★★★★★★
"Joy..." nikaita hivyo huku nikimwangalia Ankia.
Ankia akaniangalia kiumakini pia.
"Njoo JC... nakuombaaa..." Joy akaendelea kulia.
"Wewe, umekuwaje? Nini shida?" nikamuuliza.
"JC nakuomba... nakuomba uje..."
"Nije wapi? Umefanyaje? Sikuelewi..."
"Hhh... njoo... nimepigwa... njoo JC..." akasema hivyo.
"Umepigwa na nani? Uko wapi?" nikamuuliza.
Hakujibu kitu na kuendelea kulia, nami nikamwangalia Ankia kimaswali. Akanionyesha ishara kwamba niweke mfumo wa kipaza sauti kwenye simu, nami nikafanya hivyo ili amsikie pia. Joy akawa akisikika vyema zaidi sasa namna alivyolia.
"We' Joy... niambie uko wapi..." nikasema hivyo.
"Hhh... Kongowe... nipo... hapa...."
"Nani amekupiga, amekupiga wapi? Eleweka basi..."
"Njoo JC... nakuomba... uje unitoe huku... JC nimeumia..."
Khh! Nikaona mwanamke huyo ananichanganya tu, hivyo nikakata simu na kuangalia pembeni kwa kuudhika.
Ankia akasema, "JC... mbona umekata simu? Joy... Joy anaonekana kuwa na shida... ameumia..."
"Me siyo mtoto mdogo Ankia. Tumia akili na wewe basi..." nikamwambia hivyo kwa kuudhika.
"Una maana gani?" akaniuliza.
"Huyu mwanamke anataka kunipanda. We' ndo' ulimpa namba yangu?" nikamuuliza.
Akabaki kunitazama tu usoni.
"Nijibu Ankia," nikamwomba.
"Ee... alichukua namba yako kwangu... hiyo juzi. Aliichukua aliponisimulia mliyofanya chumbani kwako..." akaniambia hivyo.
"Achana na hayo. Huyu mwanamke anataka kunizoea vibaya, na mimi hiyo juzi nilikuwa nimelewa ndo' maana nikafanya naye. Asa' hapa ataanza kunisumbua kijinga tu..."
"Je kama amepigwa kweli? Labda yuko kwenye hali mbaya..."
"Asingekuwa ananifahamu angempigia nani?" nikauliza.
"Sijui, labda mabwana zake..."
"Awapigie hao hao sasa..." nikasema hivyo kwa kuudhika.
Simu ikaanza kuita tena, ikiwa ni Joy, nami nikakata upesi. Nikaiwekea namba hiyo ya Joy kizuizi (block) ili isinisumbue tena, haijalishi alikuwa anamwaga vipi machozi huko alikokuwa. Ankia akatulia tu, akiona namna ambavyo hali hiyo ilikuwa imenikera sana, nami nikamwambia afanye kujiandaa kabla ya Tesha kuja ili tuelekee Masai kujichangamsha kidogo, kisha nikatoka hapo na kuelekea chumbani kwangu.
★★
Tesha hakukawia kuja hapo kwa Ankia baada ya mimi kuipuuzia simu ile iliyonikera kutoka kwa Joy, na alikuwa amevaa kwa njia ya kawaida ya kinyumbani tu. Hata mimi pia nilitinga nguo zangu za kawaida tu japo ningeonekana kupendeza mno kama kawaida yangu. Ni Ankia ndiye aliyejiwekea mwonekano matata. Alivaa nguo kama shati laini tu lenye mikono mirefu, jeupe, lililoishia sehemu ya chini ya mapaja yake, pamoja na kikaptura cha skinny nyeusi kifupi sana alichovaa kwa chini, na hapo ndiyo nikawa nimengundua kumbe huyu mwanamke alijua kujiachia. Kwa hiyo tukasepa zetu kwenda Masai kwenye mida ya saa mbili kasoro.
Tesha akatuambia kwamba dada yake alikuwa nyumbani, hasa kwa sababu leo ilikuwa Jumapili kwa hiyo alishinda hapo tu. Akaeleza pia kwamba hapo nyumbani kwao angalau kwa wakati huu mambo yalikuwa vizuri tu kama nilivyoyaacha tokea Joshua aondolewe. Dada yake hakuwa mbanizi sana ila alimwambia Tesha awahi kurudi, ishu za kuingia ndani usiku mno hazikufaa, nami nikamwambia kweli leo tusingekaa muda mrefu. Ankia akawa amemwambia kuhusu suala la Joy kunitafuta, naye Tesha akasema nilifanya la maana kumpuuzia kwa kuwa angenisumbua mno; na tayari alikuwa ameshanishauri juu ya sababu iliyofanya kwa nini kumpuuzia Joy iwe muhimu.
Basi tukafika Masai, na kukaa sehemu iliyokuwa na viti vifupi vya mbao, vikizunguka meza pana ya mbao kwa pande mbili. Watu walikuwa wengi sana leo, ikiwa kawaida ya wikiendi. Mhudumu alipofika, nikamwambia aketi karibu nami ili kumpa maagizo kwa njia ambayo asingesahau, na baada ya kuelewa akaondoka. Tukaendelea kutulia tu, huku baadhi ya watu waliopandwa na pombe wakiwa wameshaanza kucheza, Ankia akininong'oneza sikioni kuhusu namna watu walivyotuangalia na kunifahamisha fulani ni fulani, na muda si mrefu vinywaji vikaletwa; chupa tatu za Dompo baridi, pamoja na glasi. Zikagawanyishwa kwetu na huyo mhudumu, kisha akaondoka. Tukamimina kila mtu kwenye glasi yake na kuanza kunywa, tukifanya maongezi yenye kufurahisha, na taratibu muda ukawa unaenda.
Hazijapita dakika nyingi, wakaja wanaume vijana wawili wakiwa wamebeba sinia pana lenye vyakula hapo. Kulikuwa na chips kavu nyingi, mishikaki ya ng'ombe mingi pia, pamoja na nyama za kuku. Tesha akanitumia ujumbe kuuliza ikiwa tungekula halafu tukimaliza tukimbie, maana alihofia hakukuwa na pesa ya kutosha, na kuniuliza ikiwa ni Chalii Gonga ndiye aliyelipia. Nikamwambia hapana, sikuwatoa hapa na Ankia kwa udhamini wa mtu yeyote; hii yote ilikuwa mimi, na yeye ajitahidi tu kufurahia kisha tuondoke mapema. Makamuzi yakaanza baada ya sisi wote kunawishwa mikono. Nilielewa kuna vitu vingi sana vingesemwa hapo Masai hata kuhusu haka kajambo kadogo tu tulikofanya, maana Tesha alisema fitina nyingi zilijaa sana sehemu hiyo. Niliangaliwa, yaani niliangaliwa mpaka ilikuwa inakera! Tukakata muda hapo mpaka imefika saa nne na nusu hivi, 'vibe' la Dompo likiwa limenipanda kiasi, nami nikaletewa jambo jipya.
Mhudumu yule aliyetuhudumia jana pale VIP hadi Tesha akaanza kumchokoza, akawa amekuja hapo tulipokuwa na kuniinamia sikioni, kisha akasema, "Nimeambiwa nikuletee hii."
Alinishikisha kitu kama karatasi kwenye kiganja changu, nami nikaitazama kwa njia ya kawaida tu. Hakuondoka. Akasimama nyuma yangu kama vile anasubiria jibu. Nikaifungua hiyo karatasi, ikiwa ni bandiko dogo la kwenye chupa ya bia, na upande mweupe ulikuwa umeandikiwa maneno 'njoo VIP, NINA SHIDA NA WEWE.' Aya?! Huyu angekuwa nani? Chalii Gonga? Hapana, yeye angenipigia tu simu. Huyu angekuwa mtu nisiyemfahamu, ama labda nilimfahamu lakini kwa hapo nisingejua ni nani. Fikira za haraka ikawa kwamba ni Joy, nami nikamwangalia Tesha na kukuta ananitazama kwa yale macho ya kuuliza 'vipi?'
Nikampa ishara huyo mhudumu kuwa ainame nimsemeshe, naye aliponikaribia nikamuuliza, "Nani amekupa hii?"
"Mke wake boss... boss wetu," akajibu hivyo.
"Bosi? Mke wake Chalii?" nikamuuliza.
Akatikisa kichwa kukubali.
"Nani, yule Joy?" nikauliza tena.
"A-ah... siyo Joy... mke wake boss kabisa... sijui anaitwa nani," akaniambia hivyo.
Dah! Kizungumkuti.
Ankia akaniuliza vipi, hapo tumacho twake tukiwa tumeshaanza kuwa lege, nami nikamwambia kuna mtu huko VIP ananiita, mke wa Gonga. Ankia aliposikia hivyo, akaniambia niende tu kumwona, maana alimjua lakini hakuwahi hata kuongea naye, ila nafsi yangu ikawa inapingana na hilo.
Nikamwambia yule mhudumu, "Nenda kamwambie hivi... ninakula. Kama anataka kuniona... yeye ndiyo aje hapa. Asipoweza, basi. Nenda."
Mhudumu akaondoka zake.
"Hadi mke wa Gonga ashaanza kutuma wajumbe!" Ankia akaniambia hivyo sikioni.
"Unamjua vizuri?" nikamuuliza.
"Ee, yupo hivi mwembamba kidogo, ila ana kashepu... mzuri mzuri... anapendaga kukaa huko juu akijaga hapa," akasema hivyo.
Nikapiga tu fundo dogo la wine.
"Si ukamwone?" Ankia akasema hivyo.
"Ah... ili iweje?"
"Atakuwa anakutaka."
"Me simtaki sasa. Hebu kula tuondoke bwana."
Ankia akacheka na kunilalia mgongoni, kisha akaendelea kula. Tesha akanitumia ujumbe kuniambia kwamba niwe mwangalifu sana kwa jambo lolote lile ambalo ningejiingiza kufanya na watu wake Chalii Gonga, nami nikamwambia asijali, nilikuwa macho. Dogo pia alikuwa makini hata ingawa kwenye kukubali bia za ofa kutoka kwa watu hao lilikuwa jambo rahisi kwake. Ni baada tu ya dakika kama mbili kupita na yule mhudumu akawa amerudi tena. Zamu hii akanipa kikaratasi kingine tena, nami nikahisi kukerwa. Alikuwa ameshaanza kunichoresha kwa watu maana wajanja wangejua tu kwamba alikuwa anatumwa kwangu, na mimi nilitaka hiyo ikome. Nikaifungua karatasi na kusoma.
"Njoo, pametulia zaid huku. Kuna ishu muhm natak tuongee. Nitagharamia order zako zote hata ukitaka. We njoo"
Ikasomeka hivyo. Nikawaangalia wenzangu na kuona wananitazama usoni kwa umakini, nami nikasimama na kumwambia huyo mhudumu aende zake; sikuhitaji msindikizaji, VIP nilipajua. Nikatoka na tembea yangu ya kujiamini, nikiwapita watu walioserebuka hapo, na nilipofikia usawa wa sehemu ya DJ nikakuta ni Bobo ndiye anaongoza mitambo. Alikuwa pia ameshika maiki na kufanya kama u-MC, na baada ya kuniona nakuja upande wake, akaelekeza sifa kwangu.
"Oyo, oyo, vibe kama lotee... mchina, mchina, kasimama mchina... kelele kwakeee!"
Bobo alikuwa anasema hivyo huku akinionyeshea kwa watu, na kweli shobo zikaanza kutoka kwa watu ambao hata sikuwafahamu; wanawake wakiwa wanatoa sauti za shangwe. Nikacheka kidogo nilipomfikia na kumwambia 'acha basi mwanangu,' naye akagongesha kiganja chake kwenye changu kabla ya kumpita na kwenda upande wa vyoo. Baada ya kutoa haja ndogo ndefu kweli, nikatoka hapo na kuelekea VIP, yaani moja kwa moja mpaka ndani.
Nilipoingia, nikakuta ndani humo kukiwa na utupu wa watu isipokuwa ya mwanamke mmoja aliyekuwa amekaa kwenye sofa upande wa mbele zaidi. Alikuwa amekaa kwa utulivu tu, simu ikiwa kiganjani, na macho yake yakiwa kwangu. Alikuwa mzuri kwa kiasi chake, mwembamba lakini kutokea kiunoni mpaka miguuni alikuwa na unawiri mzuri, akiwa amevalia gauni refu lenye kubana mwili wake, jeusi, na lilikuwa na mpasuo mrefu kufikia juu ya hip yake uliolionyesha vizuri sana paja lake jeupe. Sura yake ilitaka kufanana na ya mwigizaji Rose Ndauka, ingawa huyu alikuwa mweupe. Alishonea wigi la nywele za kizungu kichwani, na midomo yake ilikuwa minene ikionyesha mtapakao wa lipstick nyekundu iliyong'aa. Alivutia kwa mwonekano aliokuwa nao, wadhifa wa kuwa mke wa mwenye Masai na hoteli kubwa huko Buza ukimfaa kabisa, lakini hakuwa Hamisa Mobeto! Nilimwona kuwa wa kawaida, na nilitaka kujua alichohitaji kuzungumza nami ili niondoke haraka.
"Ingia. Mbona umesimama huko? Njoo."
Akasema hivyo, sauti yake ikiwa na utulivu tu, nami nikauachia mlango na kusogea mbele kidogo.
"Wewe ndiyo unaniita?" nikamuuliza.
"Ndiyo, ni mimi. Mpaka kusumbuana sana... si ungekuja tu mara ya kwanza nilipomtuma huyo?" akasema hivyo.
"Sikujui, ndiyo maana."
"Kwani sasa hivi umenijua? Ama ni ile tu kwamba... nitalipia kila kitu ulichoagiza ndiyo imekunyanyua?"
"Sikuja hapa nikitarajia kulipiwa chochote na mtu yeyote, unanielewa? Ongea shida yako niondoke," nikamwambia hivyo kwa sauti makini.
Akaachia tabasamu la kuhukumu fulani hivi, nami nikaona ana dharau tu.
"Unaitwa nani?" akaniuliza.
Nikabaki kimya tu.
"Mimi ni Bertha. Naimiliki hii sehemu na mume wangu...."
"Unataka nini?" nikamkatisha.
"Mhm... una kiburi sana inaonekana..."
"Ah..." nikafanya hivyo na kupiga ulimi mdomoni, nami nikageuka ili niondoke.
"Unajua kwamba mpenzi wako amevamiwa?" akaniuliza hivyo.
Nikageuka na kumtazama.
"Eee. Wamemvamia... wamempiga vibaya sana... hadi polisi wameitwa," akasema hivyo.
"Sielewi. Mpenzi wangu gani?" nikamuuliza.
"Lazima utakuwa nao wengi kwa hiyo kukuchanganya ni rahisi..."
Nikaendelea tu kumwangalia, naye akasimama na kuanza kuja upande wangu. Oh alikuwa mrefu, na ulizidishwa kwa viatu vya kuchuchumia alivyovaa.
Akanikaribia na kusema, "Kwa hiyo huna habari yoyote kama Joyce amevamiwa?"
"Joyce? Joy?“
"Mmm."
"Amevamiwa wapi?"
"Huko Kongowe."
"Ih! Kwa hiyo umeniita hapa kuniambia kwamba Joy amevamiwa, sijui amepigwa, kwa nini?"
"Si ni mpenzi wako?"
"Siyo mpe.... aisee! Watu mkoje? Joy ni mpenzi wangu? Haya, sawa. Ni mpenzi wangu. Akipigwa inakuhusu nini? Wewe unataka nini?" nikamuuliza kwa kuudhika.
"Nataka ujue kwamba mimi ndiyo nimewatuma hao watu wakamvamia," akaniambia hivyo kwa sauti kuu.
Kauli hiyo ikavuta umakini wangu.
"Isingekuwa ya mazingira, ningehakikisha wanamuua! Wewe kijana ni mjinga sana. Unashindwa vipi kujua kwamba mpenzi wako anatembea na mume wangu na ukamdhibiti? Tena kwa jinsi navyosikia ni kwamba unajua kabisa, lakini umetulia tu. Kwa nini, kwa sababu unamwogopa Gonga?" akaongea kwa hisia kali.
"Unasikia kutoka kwa nani?" nikamuuliza hivyo kwa sauti ya chini.
"Nisikilize. Sipendi mchezo. Sawa? Kama unafikiri Gonga ndiyo wa kuogopa, umekosea. Niogope mimi hapa. Kila kitu anachofanya Gonga kinapita kwangu, na sitaki aguswe na malaya yeyote yule. Yeye ni mume wangu tu. Usipoangalia na wewe nitakuja nikuumize vibaya mno kwa sababu unaendekeza unafiki tu wa kipuuzi. Huna hata aibu? Yaani mwanamke wako anatoka na mwanaume wangu halafu umekaa tu?" akasema hivyo kwa mkazo.
Ka! Huyu mwanamke alikuwa mjinga, ama? Nikabaki nikimtazama kwa mkazo sana.
"Nimekwambia ni mimi ndiyo nimemfanya hivyo ili usihangaike kutafuta nani kampiga... wala nini. Na ushahidi hauna kama ni mimi, na ninakuambia ili nikuonye... wewe na huyo malaya wako. Habari zenu zote ninazo. Nikija kusikia tena... nawaua nyie wote. Unanielewa?" akasema hivyo.
Nikatazama chini nikiwa najaribu kuelewa hali ya mtu huyu mbele yangu.
Akanipiga begani kidogo na kusema, "Wewe! Unanielewa?"
Nikamnyooshea kidole kwa njia ya hasira na kumkazia macho kiukali.
Akabaki kunitazama kwa ujasiri.
"Na wewe nisikilize. Kama una kawaida ya kutengeneza drama kwa kufanya vituko vya kijinga, na unataka kuitengeneza na mimi hapa... nitaicheza. Unanielewa? Sipendi ujinga. Unanipotezea muda kuniambia vitu visivyonihusu, sijui umefanyaje, sijui utafanyaje, ili iweje? Kama unataka kufanya, fanya! Nimekuzuia? Sitaki ujinga. Narudia tena, sitaki ujinga. Hunijui, sikujui, ila ukitaka kunijua na mimi... endelea kunichokonoa," nikamwambia hivyo kwa hasira.
"Mhm... kwa hiyo unajifanya unaniweza mimi si ndiyo?"
"Na nitakuharibu vibaya mno! Niguse tena uone," nikamwambia hivyo kiukali.
Akabaki kuniangalia tu.
"Hivi wewe... yaani unaonekana.... eti 'nimempiga mpenzi wako,' kwa hiyo unataka nikusaidie nini? Ama unafikiri nitakupigia magoti? Tena yaani... waambie na hao waliompiga Joy waje kwangu... walete kwangu na mimi wanipige, sawa?" nikamsemesha kwa ujasiri.
Akawa ananiangalia kama vile bado hanielewi sijui, na mimi hapo tayari nilikuwa nimeshapandwa na hasira pia.
"Mtu kweli unakosa kazi, unakaa kufanya michezo ya kipumbavu tu? Tuko kwenye movie hapa? Haya ni maisha, darling. Hata upige na kuua malaya wangapi, mume wako atatoka nje tu! Unang'ang'aniza ujinga, eti 'nakuambia ili nikuonye,' mimi ndiyo natoka na mume wako? Unashindwa kutafuta suluhisho linalofaa unaendekeza ujinga tu wa Sinema Zetu? Utaendelea kukalia chupa ya moto tu, mjinga wewe!" nikamwambia hivyo kwa hasira.
Alikuwa amenikera sana. Hii ilikuwa nje ya matarajio yangu kabisa. Akanisukuma kifuani kwa mikono yake, kama kutaka kunifukuza, lakini nikaishika mikono hiyo yenye bangili nyingi kwa nguvu sana, halafu nikamvuta mpaka karibu na uso wangu. Akaniasa nimwachie huku akitukana.
"Nakwambia hivi... waite hao watu wako na mimi wanivamie, sawa? Uone kama Gonga ataacha kulala na wanawake wengine. Ikikupa faida yoyote kuumiza watu wengine kwa sababu ya vitu unavyoshindwa ku-control... niite mwehu. Nitakula makapi yako kila siku! Mjinga wewe!" nikamwambia hivyo.
Kisha nikamsukuma mpaka akadondokea kwenye meza na kukaa huku akiniangalia kwa hasira.
Nikaufungua mlango, na kabla sijatoka nikamwambia, "Na sikuja ili unilipie chochote. Hauna hata hela wewe, unazitoa tu kwa mume wako afu' unajifanya eti 'kila kitu kinapita kwangu,' 'nitakuumiza!' Uje ujaribu kunisogelea tena uone."
Alibaki akiniangalia kama vile kweli alikuwa amekalia chupa ya moto, nami nikatoka hapo na kurudi kwa wenzangu tena. Nilikuwa nimeshaudhika sana, na baada ya kufika pale walipokuwepo marafiki zangu, nikakuta ni Ankia na Tesha wakiwa wametulia vile vile. Ankia akaniuliza mke wake Chalii Gonga alitaka nini, nami sikujibu hilo, nikamwomba tu Tesha aniitie yule mhudumu ili nilipe, tuondoke. Ilikuwa imeshafika saa tano na nusu hivi, na baada ya huyo dada kuja tukapiga mahesabu na kujua gharama iliyonihusu hapo ilikuwa 83500. Nikatoa wallet na kumpatia elfu tisini, naye Tesha akanionyesha ishara ya kushangaa kwa mdomo. Mhudumu huyo akaondoka, akiwa anatakiwa kurudi na chenji na mzigo mwingine.
Ankia akaniuliza mbona kama hela ilipita hata vile ambavyo tulichukua, na ndiyo hapo hapo akapata jibu. Mhudumu aliporejea na chenji, akawa ameleta na mfuko uliowekewa nyama ya kitimoto iliyotengenezwa vizuri sana, ikiwa imegawangishwa kwenye vifungo viwili. Moja ilikuwa kilo, na nyingine kilo tatu. Nikampatia Ankia abebe huo mfuko, nasi tukaanza kuondoka. Bila shaka watu walijiuliza kwa nini tunaondoka mapema sana, ila sababu zilikuwa zetu kujua. Kwa sababu Ankia alikuwa anamalizia kuagana na rafiki yake aliyekutana naye langoni, mimi na Tesha tukawa tumetangulia nje, na ndiyo kijana akapata nafasi ya kuniuliza yaliyojiri kule VIP.
"Umemwona huyo mwanamke?" akaniuliza hivyo.
Nikatikisa kichwa mara moja kukubali.
"Alikuwa anataka nini?"
"Ah... ananichanganyia habari tu. Anaanza kuniambia eti sijui katuma watu wampige Joy kisa anatoka na mume wake..."
"Wewee... kweli?"
"Ndiyo hivyo kaka. Asa' me inanihusu nini? Eti anasema anajua me ni mpenzi wa Joy, kwa hiyo ananiambia ili kunionya. Ana akili kweli?"
"Ahahee... mwanangu siyo poa. Mabalaa yashaanza kukutafuta mapema hata wiki haijaisha!"
"Ananiogopesha sasa unafikiri?"
"Kwani ni kweli alivyosema?"
"Hata kama ni kweli, hanibandulii chochote. Siogopi mtu Tesha, nayemwogopa ni Mungu tu. Sijui watu wana matatizo gani... mimi kuja hapa sijui nawazuia wasile kwao? Tayari washaanza kusambaza me mtu wake Joy, wakati hata sijui anatokea wapi! Fitina za hapa ulizoniambia ndiyo nimeanza kuziona... mpaka natamani nisirudi tena," nikamwambia hivyo kwa kuudhika.
Tesha akanisimamisha karibu na nguzo, naye akasema, "Oy, tusimame hapa, tumsubirie huyu. Sikia. Me nilikwambia. Masai ndo' palivyo. Yaani mtu akishakugusa tu kidogo, ndiyo atataka hadi afunue na nguo yako auone mwili wote."
"Unafikiri kwa huyu mwanamke ni hicho Tesha? Basi tu, sijui ana akili gani yaani... nilikuwa hata simwelewi..."
"Huwa anavuta," Tesha akasema hivyo kwa sauti ya chini.
"Bangi?"
"Unga."
"Kumbe?"
"Ee. Bobo si mwana? Huwa ananiambia. Kamemganda sana Chalii, na hata wakigombanaga... akikapa tu unga kanatulia. Sasa kakiwa high huwaga kanafanya vituko hapa ama kule... Chalii muda mwingine anakafungiaga wanasema..." Tesha akaniambia.
"Ahaa... kumbe ni addict?"
"Eee. Usikute hapo kalikuwa kamepiga. Kanajionaga matawiii, shauri nasikia kwao kwanza wana hela sana..."
"Aaa, kumbe ka kishua?"
"Ndo' hivyo. Ila ishu zake siyo, sometime huwa hadi nasikia kanampelekaga Chalii kombo na ye' anaanza kufanya vitu kwa sifa.... wana akili zile zile tu, sijui walitoana wapi mpaka kufaana... yaani mwanangu! Me huwa najichekesha kwao tu lakini sijiwekagi karibu kabisa. Kuna mambo mengi figisu huko, unashangaa tu umekuja kuuziwa kesi. Kisa? Ulionwa umeingia VIP na mke wa Gonga. Kakishapeleka maneno ya kijinga kwa mume wake huko kakamroga-roga kwa uwongo? Ohooo... unajikuta kwa Maimuna mzee. Kuwa makini," Tesha akasema hivyo.
Nikaangalia pembeni kiufupi nikiwa natafakari maneno hayo. Alikuwa sahihi kabisa. Tena hata nilipomwambia huyo mwanamke hana hela, nilisema hivyo kwa sababu ya hasira zilizonifanya kutongalia vitu kwa umakini, lakini si ajabu kwamba kweli mwanamke huyo ndiye aliyekuwa mwenye nguvu zaidi hata ya Chalii Gonga. Kwa vyovyote vile nisingetaka kujiingiza kwenye shida zaidi na watu hao, japo nilikuwa tayari kupambana nazo kama wangezileta kwangu, kwa hiyo kuanzia wakati huu ningepaswa kujitahidi kuweka kigingi kikali kuzuia mazoea yasiyo na faida yoyote pamoja na watu hao; hasa huyo Chalii Gonga.
Nilihisi kabisa kwamba mwanaume huyo angekuja kuniletea shida endapo kama ningejiingiza kwenye mambo aliyojihusisha nayo, haijalishi ikiwa na mke wake alihusika, hivyo huu ndiyo ungekuwa mwanzo wa mwisho wa ukaribu wowote uliokuwa umejitengeneza baina yangu na mwanaume huyo. Sikutaka kuangalia faida zozote zile za muda mfupi ambazo ningepata kutoka kwa mtu aliyefanya mambo haramu mpaka kutembea na mabastola, bali kukazia fikira hasara ambazo zingenipata kwa kuweka ukaribu naye ndiyo kungenisaidia niwe makini kwa muda wote ambao ningekuwa huku.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments