Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA MBILI

★★★★★★★★★★★★★★★★


Ankia akawa amefika hapo, naye Tesha akabadili mada upesi huku tukianza kutembea tena.

"Dah, kaka yaani nilikuwa sijategemea. Hilo ni bonge la mtoko, yaani halikufaa kuletwa Masai, au siyo Ankita?" Tesha akasema hivyo.

"Mmm... JC umegharamika kweli, yaani! Hiyo Dompo ilivyo tamu! Kweli tuje tupate kamshiko tufanye hii kitu kama hii," Ankia akasema hivyo.

"Yeah. Tutaenda sehemu nyingine nzuri siku moja," nikawaambia hivyo.

"Mwamba nikaona manoti tu unatoa, dah! Halafu ulikuwa unakataa eti siyo wa kishua," Tesha akasema hivyo.

"Ahahaha... siyo lazima kuwa wa kishua. Je kama nimeziiba, utajuaje?" nikamuuliza.

"Aa wapi. Ma' mkubwa kaniambia we' doctor. Ankia ulikuwa unajua jamaa ni doctor?" Tesha akamuuliza.

"Wewe... kweli?" Ankia akamuuliza hivyo.

"Uhakika. Anafanya kazi Muhimbili kabisa..."

"Wacha we! Mwanaume ana siri huyu!" Ankia akasema hivyo na kunisukuma.

Nikatabasamu kidogo.

"Tena anayo siri nzito kinoma. Ndo' umchune sasa. Oy JC, mkifika ndani mwonyeshe sugar mommy tiba ni nini," Tesha akasema hivyo kiutani.

Sote tukacheka kidogo, na masihara yakaendelea mpaka tulipofika getini kwao Tesha. Nikachukua mfuko aliobeba Ankia na kutoa nyama ya kitimoto kilo moja, nami nikamwambia Tesha apeleke hiyo kilo tatu kwao ili wakajikamulie pia. Akasema Mariam angefurahi kweli maana alizipenda, na ndiyo lililokuwa lengo langu. Ankia akaenda kufungua geti letu, nami nikamwambia Tesha asiseme kwa watu wa familia yake kwamba mimi ndiyo nilinunua hicho chakula, na ni kitu kilichofanya aniulize kwa nini. Nikamwambia tu aseme yeye ndiyo kanunua au hata asiseme lolote, maana kutokana na maelezo ya mama zake wakubwa kumhusu Miryam waliyonipa leo, sikufikiri hiki ni kitu ambacho dada yake angefurahishwa nacho; yaani kujua nimewanunulia kitu fulani. Lakini sikumwambia Tesha kuhusu hilo, naye akaridhia tu kwa hicho nilichomwambia na kwenda kwao baada ya kuagana kirafiki. Ankia wangu alikuwa ananisubiria getini, nami nikajiunga naye na kuelekea ndani. 

Mwanamke alionekana kutosheka kiasi na Dompo moja aliyokuwa amekunywa maana alikuwa na uchangamfu kweli, akinikumbushia kuhusu namna ambavyo watu walikuwa wanatutazama sana kwa macho yenye husuda, nami nikamsaidia tu kuingiza vitu vilivyotakiwa kuingia ndani na kufunga mlango. Nilipokuwa tu ndiyo nimemaliza kufunga mlango na kugeuka kumwangalia, nikakuta akiwa ameinama karibu na sehemu yenye 'extension' iliyochomekea nyaya za TV na king'amuzi, akionekana kutaka kuweka simu yake chaji. Kuinama kwake kulifanya shati lake lipande juu na kufunua mapaja yake mpaka kalio lililositiriwa kiasi tu na kiboksa-skinny chake. Mambo yangu ikaanza kupanda, bila kupenda. Alikuwa anahangaika kuichomekea simu waya sijui, nami nikawa namwangalia tu kwa matamanio kiasi. Akamaliza kuweka simu yake na kusimama vizuri tena, naye akaniangalia na kusema kitu fulani ambacho sikukazia fikira haraka.

"Mbona umesimama tu hapo?" akaniuliza hivyo tena.

"Naam?" nikawa kama nimeshtuka.

"Nimekuuliza mbona umeufunga mlango? Hauendi kujimwagia kama kawaida yako?" akasema hivyo.

"Ah... nimeona uvivu hata kwenda kujimwagia... feni itanihusu," nikamwambia hivyo na kusogea usawa wa sofa.

"Tukae kidogo... bado mapema..."

"Ishaingia saa sita mbona... na we' si unapendaga kulala mapema, vipi leo?" 

"Sijachoka kihivyo," akaniambia hivyo na kunipita.

Alikuwa akielekea upande wa chumba chake, kalio lake likitikisika si mchezo, nami nikamwambia, "Kumbe unataka kuchoka ndo' ulale?"

"Eee, bado nimechangamka," akajibu.

"Nikusaidie?" nikamuuliza.

Akawa ameufikia mlango wake na kunigeukia, naye akatabasamu na kuuliza, "Unisaidieje?"

Nikamfata mpaka kufikia hapo aliposimama na kusema, "Kukuchosha."

Akasema, "Haya... nichoshe."

Alikuwa ananiangalia kwa macho yenye uvutio, nami nikamshika kiunoni kwa nguvu na kumvuta kwangu. Alipodhani nataka kumbusu, mimi nikamgeuza na kumfanya anipe mgongo, kisha nikamsukumia ukutani na kumkandamiza hapo kiasi.

"Ah... JC... mbona hivyo?"

Akasema hivyo kwa deko, nami nikaishika shingo yake kutokea nyuma na kukivuta kidevu chake ili nimtazamishe kwangu. Unajua ni pombe tu ndiyo ilinipandishia mzuka namna hiyo la sivyo nisingejishughulisha naye kabisa. Kwa hiyo hiki kingekuwa cha kuchoshana haraka tu. Tukatoka ukutani mpaka kwenye sofa, tukapigana ndondi nzito haswa. Pombe ilikuwa inazunguka vizuri mwilini kwa kuwa sikudhani kama ningeweza kukata dakika nyingi sana nikicheza naye tu namna hiyo, ila kucheza naye kwa mara nyingine kuliridhisha sana, nami nikaona nimwache tu hapo sofani na kwenda zangu jikoni. 

Nilichukua chupa tupu ya maji ili nikojoe humo maana choo kilikuwa nje na mlango nilikuwa nimeshafunga. Kisha nikaenda pamoja nayo chumbani na kuiacha huko. Nikaitoa feni na kuipeleka hapo sebuleni, kisha nikaiwasha na kuielekeza kwa mwenye nyumba wangu. Alikuwa amelala kwa kujiachia huku jasho kama lote likimtoka, nayo feni ikaanza kutupuliza vizuri nilipokaa karibu yake pia. Akajinyanyua baada ya dakika chache na kuelekea chumbani kwake bila kusema lolote, nami nikamwahi kabla hajafikia mlango.

"Si umechoka sasa?" nikamuuliza.

Akatikisa kichwa kidogo kukanusha.

"Aaaa... kwa hiyo tuendelee? Njoo," nikamwambia hivyo huku nikimvuta.

"Hamna, natania tu... nimechoka..." akawa anakataa huku akicheka.

"Twende nikumwagie uji mwinginee..." nikamwambia kwa sauti nzito ya mchezo.

"Iih wewe... sitaki..." akasema hivyo huku akicheka.

Akakimbilia chumbani kwake na kufunga mlango, nami nikasema, "Njoo tuchoshane bwanaa..."

"Choka wewe tu. Mtu mwenyewe hata huchoki, sijui binadamu wa aina gani..." 

Akasikika akisema hivyo, nami nikacheka kidogo. Alifikri sijachoka kwa sababu ya muda niliotumia, lakini kimwili nilikuwa nimechoka sana. Tayari ikawa imeingia saa saba usiku, nami nikaona tu nizime taa na kuibeba feni, maana Ankia hakutaka kutoka tena. Kwa hiyo tungekuja kuonana kukishakucha, na nilikuwa sijasahau mipango mingine ya kushughulika nayo kwa siku hii ambayo ingefuata; mipango ya kumsaidia binti Mariam. Nikaingia zangu chumbani na kulala.

 

★★★

 

Asubuhi na mapema ya saa tatu tu nikawa nimeamka. Oh hii kwangu ndiyo ilikuwa mapema sana kwa hizi siku za mapumziko yangu huku, na cha kwanza nilichokuwa nataka kufanya kabla ya mengine ni kujisafisha kinywa na mwili; hasa kwa kuwa nililala bila kujimwagia usiku uliopita. Nikapitia jumbe mbalimbali kwanza kwenye simu na kujibu chache, kisha nikachukua vifaa vya usafi na kutoka ndani ya chumba. Nilidhani labda Ankia angekuwa hajaamka bado kutokana na uchovu wa usiku lakini mwanamke huyo alikuwa na bidii. Tayari alikuwa ameshaamka, ameshafanya usafi, bila shaka mapema sana, nami nikatoka nje na kumkuta akiwa anamalizia kufua mashuka yake pamoja na yale ambayo niliyaondoa kitandani kwangu usiku ule nimefanya na Joy. Na nilikuwa nimeyaweka tu pembeni ili kuja kuyafua baadaye, ila Ankia akawa ameniwahi. 

Tukasalimiana vizuri kabisa, nami nikamshukuru kwa kunisaidia kufua, kisha nikamwacha na kwenda upande wa sinki kuosha domo. Nilitazama upande wa nyumba yao kina Tesha na kuona kwamba gari la Miryam halikuwepo, kumaanisha tayari alikuwa ameenda kazini kwake. Nikaelekea bafuni kuoga kisha kurudi ndani tena kujitengeneza vyema pia kwa sababu nilitaka kuondoka. Ankia alikuwa ameshamaliza kufua na wakati huu alikuwa anatengeneza chai jikoni. Nikavaa jeans yangu na T-shirt jeupe la mikono mifupi, na ndiyo nilipotoka akaniuliza ninakwenda wapi. Nikamwambia tu naenda huko Mbagala kukutana na mtu kifupi kisha ningerudi. Alikuwa anasisitiza ninywe chai kwanza, yaani amalize kuichemsha kisha afate chapati upesi kwa ajili yetu, lakini nikamwambia asijali; ningekunywa chai huko huko tu, kwa hiyo asiharakishe chochote. 

Basi, nikahakikisha niko vizuri kichwani, na kufikia wakati huu nilikuwa na uhitaji wa kunyoa kiasi ama kuchonga nywele. Lingekuwa jambo la kufanya baadaye. Nikatoka na kumkuta Ankia sebuleni, akiwa amesimama usawa wa sofa huku akitazama jambo fulani kwenye TV, nami nikafika karibu yake na kusimama pia. Akaniambia kwamba kiukweli, bila unafiki wowote, nilijaliwa kuwa na sura nzuri sana, na hata ile kumwambia tu kwamba ninatoka kwenda kukutana na mtu fulani ilimfanya ahisi wivu kwa kukisia kwamba ni mwanamke, japo tulikuwa tumeshakubaliana kwamba hakupaswa kuziacha hisia za namna hiyo zimtawale. Mimi nikamwangalia tu kwa kumwelewa, nami nikaona nimpe busu laini tu ya kupoza roho. Akauliza ikiwa nilihitaji anitunzie chakula kwa ajili ya mchana, nami nikasema ningemjulisha kwa njia ya ujumbe endapo kama ningechelewa. Nikamwachia elfu kumi nikimtania kwamba kama akitaka basi akanunue Dompo aje kupigia ndani, naye akafurahi sana na kunibusu tena, kisha ndiyo nikaondoka zangu.


★★


Sikupata shida kufika Mzinga na kuchukua usafiri wa kuelekea Mbagala, na kama kawaida, nilivuta macho ya wengi. Nikafika Mbagala, nami nikakunja kona mpaka kufikia Zakhem, kisha nikachukua bajaji kuelekea Kijichi. Ndiyo, Kijichi. Mpango ulikuwa kwenda kukutana na bibie Miryam ili nizungumze naye kuhusiana na mdogo wake, Mariam, na nilitaka mazungumzo yetu yaende vizuri sana maana yule mwanamke alionekana kupenda vitu vilivyonyooka; masihara pembeni yaani, na kwa jambo hilo sikutaka ahisi labda namchezea. Kwenye bajaji niliyopanda niliketi nyuma pamoja na wadada wawili kwenye miaka ya ishirini na kitu mpaka thelathini hivi, wenye mionekano mizuri kweli kwa jinsi walivyovaa na kusuka. 

Dereva wa bajaji alikuwa mwongeaji sana, akihamishia mpaka mazungumzo yao kunielekea mimi kwa kuwaambia waniombe namba maana mimi ndiye niliyekuwa mwanaume mzuri wa kutoka nao, lakini walionekana kuniogopa kutokana na jinsi nilivyoonyesha kutokuwa na habari nao. Ile tumefika kituo cha Upendo hatimaye, nikashuka, nikalipa, kisha nikawasemesha hao wanawake. Nikamwomba huyo mmoja simu yake niandike namba, naye akacheka tu. Dereva akawa anawapampu wachukue namba la sivyo wangepoteza bahati eti. Mwenzake na huyo dada aliyeona aibu hakupoteza muda na kunipa ya kwake, nami nikaandika namba yangu na kumrudishia, kisha nikamwambia 'nitext,' halafu nikaanza kuondoka. Nilifanya hivyo kwa sababu kiukweli wanawake hao walikuwa wazuri, ila sikuwa na nia yoyote ile ya kutoka nao. Nia yangu ilikuwa nyingine tu.

Nikafika pale kwenye duka la bibie Miryam, na hapo nje nikakuta gari lake pamoja gari lingine jeusi aina ya Toyota Kluger. Bila shaka angekuwa na mgeni wa masuala yao ya kibiashara, nami nikaelekea mpaka ndani huko. Nikamkuta Mamacita Soraya akiwa ameketi kwenye kiti chake mezani kwa mapokezi, na tabasamu aliloachia lilitosha kueleza ni namna gani alivyokuwa amefurahi kuniona. Akiwa amevaa ushungi kichwani kama kawaida yake, uso wake mweupe ulipendeza sana. Nyusi zilizotindwa vyema na lipstick ya zambarau mdomoni, pamoja na macho yake makubwa kama ya kiarabu yalivutia mno. Nguo aliyovaa ilikuwa kama gauni la njano lakini lenye mtindo wa sari lenye kubana kufunika mwili wake wote kutokea kifuani, na kwa sababu ya kukaa sikuweza kumchora vizuri.

"JC!" akaniita kwa shauku tulivu.

"Mambo vipi Cute Soraah?" nikamwambia hivyo.

"Hee! Umelitoa wapi hilo jina?"

"We' kwani umeliandika wapi?"

"Hahah... umeshanitafuta mpaka Facebook?"

"Ndiyo maana yake. Una tupicha tukali kweli, siyo rahisi kuamini una miaka 30..."

"Ahahaha... kwa nini?"

"Unaonekana mdogo kweli. Upo sahihi kujiita Cute... na me sa'hivi nitakuwa nakuita Soraah."

Akacheka kidogo kwa haya.

"Ama ni la mume wako tu kukuita?" nikamuuliza.

"Hamna... niite tu hivyo. Napenda."

"Eti eh?"

Akatikisa kichwa kukubali.

Ni hapa ndiyo simu yangu ikatoa mtetemo kutokea mfukoni mwa suruali yangu kuashiria kuna ujumbe umeingia, nami nikaitoa ili kuona ni nani.

"Na me itabidi nikutafute FB nijue una miaka mingapi," Soraya akaniambia hivyo.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Itakuwa vizuri."

Nikaona ujumbe huo ulioingia kwenye simu kutoka kwa namba ngeni, aliyetuma akisema 'mambo,' nami nikakisia kuwa huenda ni yule mwanamke wa kwenye bajaji.

"Na wewe lazima uwe na tupicha tuzuri FB. Nitakuona," Soraya akasema hivyo.

"Hamna hata, mbaya," nikamwambia hivyo kiutani.

"Mh... labda umdanganye mtu ambaye hajawahi kukuona," akasema hivyo na kucheka kidogo.

Nikamjibu aliyenitumia ujumbe 'saf, nan?' naye akajibu, 'me naitwa Winny tumekutan kw bajaj.' Nikaona Soraya ananitazama tu kwa utulivu, nami nikampa tabasamu hafifu na kumjibu huyo "Winny" kwamba ningemtafuta baadaye maana kuna jambo nilikuwa nashughulika nalo.

"Sawa. Vipi... boss wetu yupo na mgeni?" nikamuuliza hivyo na kuweka simu mfukoni.

"Eeeh. Umekuja kuonana naye?" 

"Ndiyo, nimekuja kuongea naye. Itabidi kusubiri eh?"

"Ee, ila ngoja tu nimpigie nimwambie ana mgeni hapa mwingine..."

"Hapana, acha tu. Nitasubiri. Na sisi tupige story zetu kwa huo muda. Za nyumbani?" nikamuuliza hivyo.

"Nzuri tu. Ndo' ukanichunia jana..."

"Mh? Saa ngapi?"

"Jana, si niliku-text mida ya saa nne hivi, lakini hukujibu," akaniambia hivyo.

"Kweli? Itakuwa hazikufika labda. Pole," nikamwambia hivyo.

"Haina shida."

"Basi ukaumia?"

"Wala hata..."

"Hahah... sema tu... nitafidishia hilo kwa chochote utakachotaka."

"Mh... ahahaa... wanaume bwana..."

Nilipenda sana alivyofanya macho yake aliposema hivyo, na kiukweli niliweza kuhisi uvutio wangu kumwelekea ukiongezeka. Nikaanza kumtamani sana mwanamke huyu, ikiwa ni hisia iliyojijenga upesi sana.

"Mbona sasa ukanitafuta saa nne usiku kabisa?" nikamuuliza.

Akaniangalia tu na kutabasamu kiasi.

"Ulikuwa unataka tuimbiane na nyimbo za kupeana usingizi eti?" nikamuuliza kiutani.

Akapandisha nyusi zake kukubali, nami nikacheka kidogo kwa kuelewa alikuwa anatania pia. Hapo hapo mlango wa ofisi ya Miryam ukafunguka, nasi sote tukautazama. Tabasamu nililokuwa nalo usoni likaondoka, nami nikaweka uso makini zaidi baada ya kumwona Festo akiwa anatoka ndani huko. Yule yule mchumba Festo aliyedhaniwa kuwa ndiyo mimi hapa mara ya kwanza kabisa nimefika nyumbani kwake Miryam, ndiyo alikuwa hapo. 

Miryam pia akatoka ofisini na kusimama baada ya kuniona sehemu hiyo, nami nikaendelea kujituliza tu. Kulikuwa na ukimya mfupi ulioijaza sehemu hiyo hali nyingi tofauti kifikira, kwa sababu niliona Festo akinitazama kwa macho yenye udadisi, kisha akamwangalia Miryam pia. Bibie Miryam alikuwa ananitazama tu kwa umakini, yeye bila shaka akijiuliza kwa nini niko hapo, lakini Festo akiwa kama anahukumu kwa nini niko hapo. Nikawaza sijui jamaa bado alikuwa anafukuzia manzi huyo, manzi mwenyewe alikuwa mgumu kweli kulainika! Ni lazima tu Festo hakuwa amefika hapo kibiashara, bali lengo lake lilikuwa kuongea zaidi na Miryam kumshawishi waweze kuungana kimahusiano. Ilieleweka alikuwa amemwelewa. Lakini mimi nisingejua undani wa mambo yaliyoendelea baina yao, na hayakunihusu. Ila kwa jinsi Festo alivyoniangalia, ilikuwa ni kama vile fahali mpya kaingizwa kwenye zizi lenye fahali mwingine, na hiyo ilifanya nijiulize sababu ni nini. 

Jamaa akaniangalia tena, kisha akasogea karibu nami na kusimama. Nikiwa namwangalia tu kwa utulivu, akaninyooshea mkono wake kwa njia ya salamu. Nikaupokea, tukaitingisha kwa pamoja bila kusemeshana chochote, kisha mwamba akaondoka. Alikuwa nadhifu kweli, nguo zake zikionekana wazi kuwa za gharama, nami nikamwangalia Miryam usoni. Kama kawaida yake, katika uzuri hakuangusha hata kwa kidogo alichoweka mwilini. Alikuwa amevaa blauzi nyeupe yenye mikono mirefu pamoja na sketi ndefu ya jeans ya blue, na nywele zake alizibana kwa nyuma. Bado aliniangalia kwa macho yenye subira tu, nami nikawa natafuta salamu iliyofaa kumpa kwa wakati huu.

"Dada... JC ndiyo kafika. Anataka mfanye mazungumzo," Soraya akaingilia kati ukimya wetu.

Miryam akanitazama usoni tena, kisha akatikisa kichwa kukubali na kuingia ofisini kwake. 

Nikamwonyesha Soraya ishara ya mapigo ya moyo kudunda kwa nguvu, naye akacheka kidogo bila kutoa sauti, kisha nikaenda zangu ofisini kwa bibie. Sikuwa na hofu, ila kwenye kuongea na huyo mwanamke kuhusu suala la familia yake kungehitaji busara. Sikuwa nimeisahau motto yake hata kidogo: sipendi michezo isiyo na faida. Kwa hiyo hapa ningehakikisha namwonyesha kuwa sikuja kufanya mchezo, ili kutokea hapa aanze kunichukulia 'serious.' Nikaingia ofisini humo na kwenda kukaa kwenye kiti sehemu ya meza yake mkurugenzi, huku yeye akiwa amekaa kwenye chake cha kibosi. Alipendeza sana huyu mwanamke kwa namna alivyojiweka tu yaani. Kawaida. Hakupenda makuu, lakini alionekana kupenda sana maendeleo ndiyo maana hata na sehemu hii ya kikazi alikuwa ameipanua vizuri sana. Nilihisi kama vile niko kwenye kampuni kabisa.

Akiwa ananiangalia kwa macho yenye subira, nikamwambia, "Habari za kazi dada yangu?"

"Ni nzuri. Mbona umekuja hapa? Kuna tatizo lolote?" akaniuliza hivyo.

"Ha..pana... siyo hivyo. Hamna tatizo. Kwa nini unafikiri mimi kuja ni mpaka kuwe na tatizo? Sura yangu imeandikwa 'matatizo' au?" nikamwambia hivyo kiutani.

Nikaona anatoa tabasamu hafifu na kuangalia chini, nami nikacheka kidogo kwa kupata kitulizo kiasi.

"Sawa. Niambie," akasema hivyo.

Nikasafisha koo kidogo na kusema, "Nimekuja ili tuzungumze kuhusu mdogo wako... Mariam."

Akabaki kimya na kuendelea kunitazama kwa utulivu.

"Sijui ikiwa... mama zako walikwambia kuhusu maongezi yetu jana?" nikamuuliza.

"Ndiyo waliniambia. Wewe unataka kipi kutoka kwa Mariam?" akaniuliza.

"Nataka kumsaidia. Mdogo wako ana kasoro ndogo kwenye ubongo wake ambayo nina imani inaweza kushugulikiwa na kuondolewa kwa njia ya... ya kwake yaani. Nimemwangalia nikaona ana njia tofauti za kuitikia mambo...."

"Ni kasoro gani unayoongelea?" akanikatisha.

"Sijawa na uhakika sana, ila nafikiri mdogo wako atakuwa amepatwa na kitu kinachofanana na ASD," nikamwambia hivyo.

"Ndiyo nini hiyo?" akauliza.

"Autism Spectrum Disorder. Ni ugonjwa unaozuia maendeleo ya utimamu kwa mtu unaosababishwa na tofauti zinazojitokeza kwenye ubongo. Wanaokuwa na hii kasoro huwa wana matatizo ya kuwasiliana, ama tabia na mapendezi yanayojirudia-rudia, na... njia zao za kujifunza zinakuwa tofauti sana na ukawaida wa watu wengine. Hii huwapataga sanasana watoto wadogo kwa sababu ubongo wa mtoto bado unakuwa unaendelea kukua mpaka anapofikisha miaka kama 15, ndiyo unakuwa umekomaa. Ubongo wake Mariam tayari ulikuwa umeshakomaa alipopatwa na shida kama hii, kwa hiyo nafikiri tunaweza kumsaidia arudishe utimamu wake mzuri licha ya kwamba muda umepita..." nikamwelezea.

Akawa ananitazama tu machoni kwa umakini.

"Unaonaje kuhusu hilo?" nikamuuliza.

Akaangalia chini kiasi, kisha akanitazama na kuuliza, "Wewe... ni daktari kweli?"

Swali lake likaniacha namwangalia tu usoni kwa ufikirio, kwa sababu ilikuwa wazi kwamba mpaka kufikia hapo bado alikuwa haniamini; haijalishi hata kama suala la mdogo wake kuokolewa asigongwe kwa gari lilitoka kwangu. Bila shaka aliambiwa na mama zake wakubwa kwamba mimi ni tabibu, lakini bado bibie alikuwa na mashaka yake kunielekea.

Nikashusha pumzi kiitulivu, nami nikamwambia, "Ndiyo. Mimi ni daktari."

"Unajua... Mariam nimeshampeleka hospitali na... wanasema nimwache wodi za vichaa. Kwa haya uliyoniambia unamaanisha kwamba mdogo wangu siyo kichaa, si ndiyo?" akaniuliza.

"Ndiyo. Mariam siyo kichaa, anaumwa tu kwenye ubongo."

"Sasa kwa nini walikuwa wananiambia mdogo wangu ni kichaa, sijui... amepoteza kabisa utimamu wa akili?"

"Hapana, hajapoteza utimamu wa akili. Unajua labda kwa kipindi hicho... Mariam ndiyo alikuwa amepatwa tu na hiyo shida ghafla kwa hiyo hata hao waliomwangalia inaonekana hawakumwelewa vizuri. Madaktari wengine ni wajinga, wana... wanafanya vitu haraka-haraka bila kuchunguza vizuri," nikamwambia hivyo.

Akapiga ulimi wake mdomoni na kuangalia pembeni.

"Ila usijali. Mariam anaweza kusaidika. Ninaomba tu unipe ruhusa ili niweze kumsaidia," nikamwambia hivyo kwa upole.

"Unataka kumpa msaada gani sasa? Kama ni madawa ameshatumia mengi mpaka nikaogopa angejazwa sumu mwilini."

"Hapana, usijali. Msaada naotaka kumpatia ni wa kisaikolojia. Nataka nicheze na akili yake kwanza, nimwelewe vizuri zaidi, kisha ndiyo nitampa msaada unaomfaa YEYE. Hawezi kufanana na wagonjwa wengine, kwa hiyo atakuwa na njia tofauti ya kupona," nikamwambia.

Macho mazuri ya mwanamke huyu yakawa yananitazama bila kukwepesha hata kidogo, nami mpaka nikahisi ajabu kiasi.

"Unanipa uhakika kwamba... atapona?" akaniuliza hivyo.

Sauti yake tamu sana ilijaa matumaini aliponiuliza hivyo, nami nikasema, "Ndiyo. Atapona."

Akaangalia chini kiasi akionekana kutafakari vitu.

"Nitahitaji kwenda naye hospitali kwanza... tuonane na daktari aliye-specialize zaidi kwenye magonjwa ya hivi ili nijue mambo ya kufanya kwa uhakika," nikamwambia.

"Hospitali gani?" akaniuliza hivyo.

"Muhimbili," nikamjibu.

Akaniangalia kwa macho yenye umakini.

Najua alikuwa anajaribu kusawazisha wazo la mimi kwenda na mdogo wake sehemu ya mbali, ile hali ya kutoniamini bado ikionekana wazi, nami nikamwambia, "Tutaenda pamoja na Tesha, ukiona ni sawa. Maana wewe unakuwa kazini. Unaonaje?"

Akatikisa kichwa kukubali.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Sawa basi... nashukuru. Uta... fanya unachotaka kumwandaa ili labda kesho twende huko... nitakuwa nimeshawasiliana na huyo daktari."

"Gharama ya haya yote haitakuwa nyingi?" akaniuliza.

"Hapana, wala... sifanyi hivi ili unilipe. Unafikiri kila kitu ni pesa tu?"

"Nilidhani wewe ndiyo unafikiri hivyo. Kwamba mtu akikusaidia basi ni lazima anataka kulipwa. Au nakosea?" akaniuliza hivyo kwa umakini.

Ohohoo, povu! 

Pozi likaniisha kidogo kwa sababu nilielewa maana ya kauli hiyo vizuri sana. Alikuwa ananiunguza, tena kunichoma kwa ule moto mkali wa kumbukumbu ya kile nilichomfanyia mara ya kwanza tumekutana. Si nikakumbuka kweli nilitoa elfu mbili na kujaribu kumpatia kama malipo kwa ule msaada alionipa? Inaonekana hiki ni kitu ambacho bado kilifanya awe na shuku kunielekea japo hakuniona kuwa mtu mbaya, oh nasema hivyo kwa sababu sikuwa nimesahau namna alivyonikumbatia ule usiku alipotoa shukrani kwa ajili ya msaada niliompa mdogo wake, na hapo kiukweli nikawa nimejifunza somo muhimu. Shukrani zetu zilitofautiana, na ya kwake ndiyo iliyofaa zaidi. Mimi kumpa hela siku ile amenisaidia labda kulifanya ahisi nimemdharau hata kama sikuwa na nia hiyo, lakini yeye aliponikumbatia kwa shukrani japo nilikuwa nimelewa, alionyesha ni kitu kilichotoka moyoni mwake, na ni jambo lililonigusa sana usiku huo. Kwa hiyo hapa kiukweli alikuwa amenipa fundisho dogo lakini lenye maana kubwa sana, nami nikatabasamu tu na kutikisa kichwa kuonyesha uelewa wa kauli yake kwa njia nzuri.

Akashusha pumzi na kusema, "Okay. Nashukuru pia kwa... jitihada yako. Nitamwandaa Mamu baadaye ili kesho mwende. Tesha atakuwa nanyi."

Nikatikisa kichwa kukubali, nami nikasema, "Asante kwa kukubali. Ngoja niende sasa. Tutaonana... labda baadaye... au... kesho..."

Alikuwa ananitazama tu machoni kwa mkazo kama vile ananishangaa kutokana na kubabaika kwa yale niliyosema, nami nikasimama tu ili niondoke. Nikampungia kiganja kwa chini kama kumuaga, naye akatikisa kichwa kukubali. Nikatoka hapo ofisini nikiwa nimefarijika kutokana na kukubaliwa ombi langu, japo mwanamke huyo alinipiga bomu zito kiasi la rohoni. Ile ndiyo nimegeuka tu na kutazama upande wake Soraya, nikakunja uso kimaswali kiasi baada ya kukuta kuna mtu mwingine aliyekuwa amesimama usawa wa meza hiyo ya mapokezi, naye hakuwa mwingine ila yule Joshua! 

Nikamtazama machoni kwa mkazo kiasi, nikiwa najiuliza kwa nini alikuwa amekuja hapo. Kumwona mwanaume huyo kazini kwa Miryam ilinifanya nipatwe na hisia mbaya kwamba huenda alikuwa amekuja kumfanyia fujo dada mkubwa na huku tena, wakati alipewa msamaha wa kutofungwa jela na Miryam mwenyewe. Alisimama kwa utulivu huku akiniangalia kwa njia ya kawaida, nami nikamwona Soraya akimwonyesha ishara ya kumruhusu aje upande huu wa ofisi. Jamaa akatembea taratibu na kufika karibu zaidi na niliposimama. Nikawa namwangalia kwa ujasiri machoni, na kwa sababu alizozijua yeye, wakati huu hakuwa akinitazama kwa njia ya chuki kama vile alivyoniangalia mara ya mwisho tumeonana.

"Niaje mtu wangu?" akanisalimia hivyo.

Mh? Ilikuwa ni kama kumpiga kofi kidogo Shetani ili kuona ikiwa atakurudishia la kwake kwa utani, lakini mimi sikutaka kufanya matani yoyote na huyu mtu. Sikuwa na uhakika, lakini kwa kumwangalia tu, nilihisi ujio wake hapa ulikuwa wa nia mbili; yaani bado singeweza kuamini kuwa alikuja hapa kwa lengo la kusaka amani. Zamu hii angekuwa anataka nini kutoka Miryam?

 

★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next