Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

 

A Story by Elton Tonny

 

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

 

R-rated 18+

 

Enjoy!

 

 

★★★★★★★★★★★★★★★★

 

 SEHEMU YA KUMI NA NNE

 

★★★★★★★★★★★★★★★★

 

 

Mama Chande akaendelea kusema, "Ile jana nilipata taarifa eti Joy alikuwa amevamiwa, akapigwa, lakini hakujua amepigwa na nani. Yaani wakaenda mpaka polisi... akawa amehojiwa. Aliulizwa kama alifahamu watakaokuwa wamefanya hayo kwa sababu mapolisi waliona hao watu walimlenga yeye kabisa, lakini akasema hajui. Leo ndo' tunapata hizi taarifa. Jamani!" 

 

Nikamwangalia Ankia kwa ufupi, akiwa bado ameinamisha tu uso wake, nami nikauliza, "Ameuawa vipi?"

 

"Nasikia sijui amechomwa na visu, sijui amekatwa na mapanga... eh, yaani bado sijaelewa," mama Chande akasema.

 

Nikafumba macho kwa ufupi, kisha nikafumbua na kuuliza, "Wapi?" 

 

"Nasikia alikuwa huko mitaa ya Buza. Jamani dada wa watu alikuwa mzuri! Alikuwa rafiki yetu sana, akija anatuchangamkia kweli, yaani ni kama tumetoka mbali kweli japo tumekutania huku tu. Sijui hao watu walikuwa wanamtaka nini! Na ni kweli kama mapolisi walivyosema, walikuwa wanamlenga yeye hata kwenye hiyo ya kupigwa. Nimeogopa sana jamani yaani... ah! Ankia... jikaze dada, ndo' maisha... yamempata mwenzetu, tuombe tu yasitufikie na sisi! Hei..." mama Chande akasema hayo kwa huzuni.

 

Safari ya kwenda bafuni kuoga ikawa imekatikia hapo hapo, nami nikakaa kwenye mkono wa sofa pembeni yake Ankia na kutulia hapo kwanza. Maswali kadhaa yalipita kichwani kwangu, na sikuweza kujizuia kuhisi vibaya sana moyoni kutokana na tukio hili kunihusu mimi pia kwa njia fulani. Nikakumbuka namna ambavyo Joy alikuwa akiongea kwa huzuni sana jana aliponipigia na mimi nikampa bega la baridi kwa kudhani alikuwa ananifanyia tu kituko kingine. Nikawaza kuwa huenda kwa njia kubwa nilisababisha kilichompata kitokee, kwa sababu nilichukulia vitisho vya mke wa Gonga kuwa hewa tu. Na sasa akawa amethibitisha kwamba hakutania. Aisee! Nilijua kabisa kwamba ingekuwa ni yeye ndiye aliyefanya hayo, na kama haikuwa yeye, basi ningehakikisha nafanya utafiti wa ndani zaidi kujua ni nani aliyemwondoa mwanamke yule duniani. 

 

Sehemu hii sasa ikawa imejawa na simanzi kutokana na hii ishu, nami sikusema lolote lile na kuendeleza utulivu wangu tu. Mama Chande akasema kwamba amesikia mapolisi walikuwa wanafatilia sakata hilo la mauaji ya Joy ili wawapate waliohusika, nami nikawa nimeingiwa na wazo lililonitia wasiwasi kiasi. Tesha alisema kitu kuhusu mke wa Chalii Gonga kuwa mtu mwenye hila sana, na kama ilikuwa yeye ndiye amemuua Joy, uwezekano wa kuligeuzia suala hilo kwangu ulikuwepo. Si alikuwa anataka kunikomesha? Huwezi jua, ningeshangaa tu mapopo hao wanafika mlangoni hapo na kusema niko chini ya ulinzi kwa sababu mimi ndiyo muuaji! Huyo mwanamke angeweza kunikamatisha kinamna hiyo kabisa kwa kutumia hila zake, na hili lilikuwa ni wazo la kutochukulia kirahisi hata kama uhakika wa mambo kwenda namna hiyo haukuwa wa asilimia mia. 

 

Nikiwa bado nawaza mengi, nikasikia sauti ya mlio wa simu yangu kutokea chumbani, nami nikanyanyuka kwenda kuona mpigaji ni nani. Nikakuta ni Tesha, na baada ya kupokea, rafiki yangu huyo naye akawa amenipa taarifa za kifo cha Joy. Ila yeye kama kawaida yake ndiyo alikuwa na habari kamili. Akaniambia kwamba Joy aliuawa maeneo ya kule Buza baada ya kuwa ametoka kwenye ile hoteli yake Chalii Gonga kwenye mida ya jioni kabla giza kuingia, sehemu ya mauaji hayo ikiwa ni kwenye ghetto lake lililokuwa maeneo ya huko huko. Nikamuuliza ikiwa alisikia kuhusu kuvamiwa kwake pale Kongowe, na alipokubali, nikauliza Kongowe alivamiwa akiwa kwa nani. Akasema alivamiwa akiwa kwenye nyumba isiyo ya kwake, ila hakuwa na uhakika sana ni ya nani. Akaeleza kwamba alikisia hayo yote yalihusiana na suala la mke wa Chalii Gonga kujua kuhusu Joy kutoka na mume wake, naye akaeleza namna alivyohuzunika sana kwa sababu Joy aliuliwa vibaya kwa kukatwa na visu mara nyingi mno mwilini. Roho iliniuma. 

 

Tukaagana na Tesha baada ya yeye kuniambia yupo njiani kurudi kutokea Tandika. Mimi kiukweli nilivurugwa mno na msiba huo. Nikawa hadi nashindwa kuacha kumtafakari mwanamke yule japo nilijitahidi kiasi kuondoa fikira zangu zote kwake. Mpaka mama Chande na mwanaye walipoondoka, nikakaa na Ankia kidogo na kumsikiliza alipotoa maneno yake yenye kuonyesha huzuni kuelekea kifo cha rafiki yake, nami nikajitahidi kumbembeleza kwa upole mwingi. Hapa kilichokuwepo kwa Ankia hiyo kesho ilikuwa kwenda msibani ili kuwaunga mkono ndugu na marafiki zake Joy, na mimi pia nikamwambia ningekwenda. Nikiwa nimeshatafakari mambo mengi kuhusiana na hali hii, nikawa nimejiweka vizuri kiakili ili nifanye jambo fulani ambalo lingesaidia kurudisha haki ya kilichompata Joy. Siyo kwamba labda nilijiona kuwa na hatia sana ama kama mpelelezi mahiri mno, hapana, bali ikiwa kama ni kweli mke wake Chalii Gonga ndiye aliyekuwa amehusika na suala hilo, nisingemwacha salama. Ningehakikisha analipia.

 

 

★★★

 

 

Asubuhi ikafika. Niliamshwa mapema kwa sababu ya simu yangu kuita mara kadhaa, na baada ya kuichukua nikaona mpigaji kuwa Tesha. Baada ya kupokea, jamaa akaniuliza ni muda upi tungeenda pamoja na Mariam kumwona daktari huko hospitali, akisema kuwa dada yake alimwambia kuhusu suala hilo, na wakati huu Miryam alikuwa anamwandaa Mariam kwa ajili ya kwenda huko. Nikamwambia ni muda siyo mrefu ningefika hapo kwao ili tushughulike na jambo hilo, naye akakubali. Kwa hiyo nikaamka na kuanza kufanya maandalizi. Nikaoga, nikavaa vizuri, hii ikiwa ni saa tatu kasoro, na mwenye nyumba wangu alikuwa chumbani kwake tu mpaka wakati ambao nilikuwa nimemaliza kuuweka mwili wangu safi. Nikaona niende huko chumbani kwake kumwona, nami nikamkuta amejilaza tu kitandani kwake huku akionekana ku-chat kwenye simu ama kusoma; alijua yeye. Nilielewa kwamba tayari alijua nimeingia, lakini hakuniangalia hata mara moja, akionekana kuwa makini kweli, nami nikamsemesha.

 

"Ankia... umeamkaje?" 

 

Akanitazama usoni, naye akasema, "Kawaida tu. Unataka kutoka?"

 

"Ndiyo."

 

"Sawa. Nisamehe sija... sijachemsha chai...."

 

"Usijali, we' pumzika mpaka utakapojisikia kunyanyuka," nikamwambia.

 

"Unaenda wapi?"

 

"Natoka na Tesha kumpeleka Mamu hospitali," nikamjulisha.

 

"Aaa... sawa."

 

"Na wewe? Umepanga kwenda msibani mida gani?"

 

"Baadaye. Si na wewe utakuja?"

 

"Ndiyo, nafikiri Tesha ata...."

 

Kabla sijamaliza kumjibu, simu yangu ikaanza kuita, nami nikaitoa na kuangalia mpigaji kukuta ni Chalii Gonga. Nikakaza macho kwa umakini.

 

"Vipi?" Ankia akauliza.

 

Nikamwangalia na kusema, "Ee... labda nitakuja na Tesha. Tukishatoka hospitali. Sipajui kwo' kuja naye lazima... ngoja nipokee simu," nikamwambia hivyo.

 

Akatikisa kichwa kukubali, nami nikatoka chumbani hapo na kusogea mpaka kufikia mlango wa kuingilia sebuleni. Mawazo yakiwa ni mengi kichwani kutokana na kujua mambo mazito yaliyokuwa nyuma ya mtu huyu aliyenipigia, nikapokea na kuiweka sikioni.

 

"Oya dogo langu..." sauti ya Chalii Gonga ikasikika.

 

"Naam kaka," nikaitika.

 

"Mbona nakutafuta sana lakini unanikaushia?"

 

"Mambo mengi tu. Vipi kwani?"

 

"Umesikia kilichompata Joy jana?"

 

"Ndiyo nimesikia."

 

"Unaweza kuniambia nini kinaendelea?" akaniuliza hivyo.

 

Nikakunja uso kimaswali kiasi na kusema, "Kwa nini uniulize mimi hivyo?"

 

"Nimeuliza tu... labda ukawa unajua kitu fulani..."

 

"Ah... sijui. Hilo jibu linatosha au?"

 

"Mhm... usipandishe jazba mdogo wangu..."

 

"Sijapandisha jazba. Ongea point yako," nikamwambia hivyo kwa sauti makini.

 

"Nimeanza kusikia Joy kapigwa hiyo juzi. Sijui unanielewa? Na alipopigwa, mtu wa kwanza kupigiwa ilikuwa wewe. Nataka kujua alitaka nini kutoka kwako... ama labda na wewe pia ulihusika kwenye hiyo ishu," akaniambia hivyo.

 

"Ishu gani? Kumpiga? Kwa nini nimpige Joy?"

 

"Ndiyo uniambie..."

 

"Nisikilize Chalii. Wewe si una watu wako? Fanya utafiti mwenyewe uujue ukweli, sawa? Kama unafikiri mimi ndiyo nimemuua Joy, thibitisha, halafu uje kwangu umlipizie kisasi. Sawa?"

 

"Mbona unaenda mbali sana? Mimi nataka tu kujua ukweli."

 

"Ndiyo maana nimekwambia fanya uchunguzi. Ukikuta nimehusika... nifanye chochote unachotaka. Si alikuwa mtu wako? Utaamua mwenyewe cha kufanya. Nimemaliza. Kuna kingine?" nikamwambia hivyo kwa ujasiri.

 

Akacheka tu na kusema, "Usijali. Uchunguzi nafanya. Sikutaka kuamini ni wewe ndiyo umemuua Joy, ila nikikuta ni wewe... utajuta mdogo wangu."

 

"Ah... utajua mwenyewe. Hivyo vitisho vyote ungevitunza kwa ajili ya wahusika halisi na si mimi Chalii. Hapa unapoteza tu muda wako... na naomba usinisumbue tena," nikamwambia hivyo kwa kukereka.

 

Kabla hajasema lolote tena, nikakata simu na kushusha pumzi kwa nguvu. Kuna mtu aliyekuwa anazungusha mchezo huu wa mauaji ya Joy kunielekea mimi, na tayari nilijua huyo kuwa mke wake Chalii. Hako kajinga kalikuwa kanataka kuniharibia wakati wangu mzuri niliokuwa nimekuja kujijengea huku, na kitendo cha Chalii Gonga kunipigia wakati huu na kuanza kutema vitisho ndiyo kilichochea kuni za moto kwenye nia yangu ya kutaka kupambana nao na kuwaangusha. Wote kwa pamoja walikuwa wameshanigeuza mimi kuwa adui yao, na ningewaonyesha urafiki mzuri wa kuwa adui yangu. 

 

Nikaweka suala hilo pembeni na kutafuta namba za daktari fulani pale Muhimbili, kisha nikampigia na yeye akapokea. Daktari huyu alibobea kwenye masuala ya maendeleo na ukuzi wa ubongo, hivyo alikuwa ni mtaalamu wa mambo mengi yaliyohusisha kichwa. Nikamwambia kuhusu ishu ya Mariam, nikimwomba nafasi ya kuonana naye kwa asubuhi hii ili anipatie ushauri mzuri kuhusu hali ya "mdogo wangu," naye akaridhia. Akaniambia niende tu na nikifika nimjulishe hasa kama nisingemkuta kwenye ofisi yake, nami nikamshukuru kwa hilo. Nikaweka simu mfukoni baada ya kumalizana naye, nami nikaelekea nyumbani kwao Tesha. Sikuwa hata nimempa Ankia kwa heri nyingine tena maana nilihisi kuvurugwa kiakili kiasi, na baada ya kufika getini pale, nikaligonga na kusubiri lifunguliwe. Dakika moja nyingi nalo likawa limefunguliwa, na sikuwa nimetarajia mfunguaji awe bibie Miryam mwenyewe. Nikatoa tabasamu hafifu kama kumpa salamu, naye akawa ananiangalia kama vile anasubiria niseme kitu fulani. Nikampa hilo.

 

"Za asubuhi dada?" nikamsalimu.

 

"Nzuri. Karibu," akaniitikia na kuachia uwazi zaidi ili niingie.

 

Nikapita na kuingia sehemu hiyo ya ndani ila nje ya nyumba yao, na nilikuta Bi Jamila akiwa ameshikilia mpira mrefu wa maji uliounganishwa kwenye bomba hapo nje, akimwangalia maua yaliyotunzwa kwenye vyombo kuzungukia nyumba yao. Mwonekano wa Miryam uliniambia kwamba bado, ama labda hakuwa na mpango wa kwenda kazini kwa leo, kwa sababu alikuwa ndani ya T-shirt nyeusi yenye mikono mifupi pamoja na khanga kutokea kiunoni, na nywele zake hakuwa amezitengeneza vizuri kimtoko; zikiwa na mvurugo kiasi wa kazi za asubuhi nadhani. 

 

Nikasimama usawa wa gari lake na kumwamkia Bi Jamila. "Mama, shikamoo?"

 

Akaniangalia na kuitikia, "Marahaba baba. Hujambo?"

 

"Sijambo. Naona unawaogesha watoto," nikamjibu.

 

Akacheka na kusema, "Ee wanangu hawa wanapenda kweli maji, kila asubuhi na jioni lazima waoge."

 

"Ni vyema. Hapo lazima wanenepe mno," nikamwambia kiutani.

 

Alipotabasamu kidogo, nikamwangalia Miryam na kukuta ananitazama kwa yale macho yake yenye udadisi fulani hivi, nami nikashindwa kujizuia kutabasamu na kuangalia chini. Hata sikujua sababu ni nini!

 

"Nini?" akaniuliza hivyo.

 

Nikatikisa kichwa kuonyesha kwamba hamna kitu, nami nikamtazama machoni kwa mara nyingine.

 

"Ingia ndani. Mariam yuko tayari ila anapaswa anywe chai kwanza. Tesha ndiyo bado hata hajaoga," Miryam akasema hivyo.

 

"Dah! Halafu kameniwahisha kweli, kumbe bado hata hajaamka!" nikasema hivyo kiutani.

 

"Nini? Nani?" akaniuliza hivyo.

 

"Mdogo wako, tumeongea muda si mrefu, nikadhani na yeye alikuwa tayari tayari. Kwa hiyo nakaa kuwasubiri," nikasema hivyo.

 

"Yeah... au unapotezewa wakati?"

 

"Hapana. Nataka nitumie muda wangu wote nitakaokuwa hapa kumsaidia Mamu... kwa hiyo yeye ndiyo mmiliki wa wakati wangu," nikamwambia hivyo.

 

Itikio alilotoa baada ya mimi kusema hivyo lilikuwa kunishusha na kunipandisha mara moja kama vile anajaribu kunisoma, nami nikatabasamu kidogo.

 

"Mbona unaniangalia hivyo?" nikamuuliza.

 

Akaachia tabasamu hafifu la kuhukumu fulani hivi, naye akanipita na kuanza kuelekea ndani ya nyumba. Nikajizuia kutotabasamu zaidi kwa sababu ni wazi kwamba mwanamke huyu bado aliniona kuwa mtu asiyeeleweka, labda sijatulia kiakili, huenda akiniona kama Tesha vile, na mimi nikaridhia tu kuwa angalau mambo baina yetu yalikuwa sawa. Nikaingia ndani kwao na kumkuta Mariam, akiwa amekaa upande wa 'dining,' na akipata kiamsha kinywa pamoja na Bi Zawadi. Mwanamama huyo akanisalimu kwa uchangamfu wake na kunikaribisha ninywe chai, nami nikashukuru na kusema nilikuwa sawa kabisa, kisha nikakaa sofani kumsubiri binti. Miryam alikuwa ameenda chumbani nadhani, na hakutoka tena tokea aliponikaribisha ndani hapo. Tesha akaja kutokea upande wa bafuni, akiwa amevaa pensi ya kijani pekee, huku mwili wake ukionekana kulowana, akiwa ametoka kuoga, nasi tukasalimiana vizuri na jamaa kwenda chumbani kwake kuvaa nguo ili tuondoke. 

 

Nikapata mazungumzo mawili matatu pamoja na Bi Zawadi kuhusiana na masuala ya dawa za kienyeji na za hospitali, na mwanamke huyo alionekana kupenda sana matumizi ya dawa za kienyeji zaidi ya za hospitali kwa jinsi alivyozisifia. Nilimtazama Mariam kwa usomi mwingi alipokuwa akila, nikiona jinsi alivyofurahia kupata chakula kwa njia kama ya mtoto mdogo. Akawa ameshiba, Bi Zawadi akamsaidia kunawa, kisha wakaja upande wa masofa hapo sebuleni na kukaa. Binti alikuwa akionyeshwa mimi ili anisalimie, lakini akawa anaangalia chini tu kama hataki. Nilielewa kwamba bado hakuwa amejenga uzoefu kwangu, na njia ya kwanza ya kufanikisha kumsaidia vizuri ingenihitaji nijenge mazoea naye ili akishaweza kujiachia zaidi kwangu, ndiyo nianze kumwekea tiba akilini. Wakati ambao Bi Jamila ndiyo alikuwa amerudi kutoka kumwagilia maua yake, Tesha naye akawa ametoka chumbani, akiwa amevaa vizuri sana, naye akamwita dada mkubwa ili apewe funguo za gari.

 

Kweli Miryam akawa ametoka na kumpa Tesha funguo, naye akamsihi mdogo wake awe makini sana na Mariam mpaka tutakaporudi. Nikamuuliza Miryam angekwendaje kazini, naye akasema angechukua usafiri. Basi kwa kuwa mambo yalionekana kunyooka kwa sehemu hiyo, tukatoka kwa pamoja, Mariam akaingia siti za nyuma ya gari, Miryam akafungua geti, nasi tukaingia mbele ya gari na Tesha kulitoa nje. Niliona jinsi gani Mariam alimpenda sana dada yake, kwa kuwa aliweka uso wake kwenye kioo huku akimtazama sana huko nje kana kwamba ni mtoto asiyetaka kumwacha mama yake, nami nikaweka hilo akilini ili nije kulitumia katika msaada niliotaka kumpatia. Kila jambo lingekwenda taratibu tu mpaka ningehakikisha huyu binti amekaa sawa tena.

 

 

★★

 

 

Vuuu, mwendoni kuelekea hospitali. Gari hili lilikuwa modeli ya zamani ya 'manual' kwa hiyo kulikuwa na gia ya kusukuma na kurudisha nyuma karibia kila dakika, na Tesha alitia mbwembwe kweli kwenye kuendesha ili kunionyesha kwamba alijua sana. Na alijua. Alikuwa dereva mzuri. Nikamwangalia Mariam nyuma na kumwona akiwa ameshika simu ya Tesha akitazama katuni ambazo kaka yake alimwekea ili binti atulie, nami nikamtazama rafiki yangu.

 

"Oya unaona navyoweka vitu hapa?" akaniambia hivyo kwa kujisifu.

 

"Naona. Miryam ndiyo alikufundisha kuendesha?" nikamuuliza.

 

"Hamna, nimejifunzia Arusha. Miezi miwili tu Veta nikatoka nimeiva," akasema.

 

"Aaa sawa."

 

"Na wewe mtoto wa kishua? Unajua kuendesha?"

 

"Ahahah... ndiyo, najua."

 

"Ulijfunzia chuo gani?"

 

"Hamna, me sikujifunzia Veta wala popote. Nilichukua tu gari la mtu nikaanza kuendesha mwenyewe mpaka nikaweza."

 

"Aa wewe... unazingua."

 

"Kweli tena."

 

"Una leseni?"

 

"Ee."

 

"Uliitolea wapi sasa kama hukwenda chuo?"

 

"Ahahahah... shortcut tu. Yaani me nimeweza gari mdogo, nilipofika legal age nikamtafuta askari mmoja wa usalama barabarani... hadi nilishamsahau jina ila, yaani, yule ulikuwa unampa hela tu anaenda anakutengenezea leseni, fwii unaingia barabarani," nikamwambia.

 

"Kweli eh? Nishagasikia wanafanya hivyo ila siku hizi sidhani sana maana kuna kushikwa kwingi..."

 

"Ee, ndiyo hivyo. Me nilipita nayo namna hiyo."

 

"Ulikuwa unatoa shi'ngapi?"

 

"Kwa ajili ya leseni? Laki tatu tu."

 

"Laki tatu tu, au siyo? Kama buku tatu yaani."

 

"Wee, nilihangaika kuipata! Hata kipindi hicho mambo hayakuwa easy sema ukishajuana tu na watu si unajua vichochoro vinajinyoosha..."

 

"Ahehehe... mwana me napenda sana hizi manual. Kucheza hapa mbele nakubali mno, yaani auto zinakera, unaweza hata ukanyoosha miguu hapa juu maana nyepesi mno," aksema hivyo.

 

"Na dada yako anapenda za hivi eh?" 

 

"Da' Mimi? Sijui sana. Hii ni ya kuenzi tu unajua? Angeweza hata kuiuza na kuchukua nyingine ila anapenda mno kutunza kumbukumbu," akaniambia hivyo.

 

"Unamaanisha nini?" nikamuuliza.

 

"Hili lilikuwa gari la baba," akaniambia hivyo.

 

"Aaa..."

 

"Eee, walikuwa tight sana na da' Mimi."

 

"Sawa. Inaonekana ya zamani, lakini anajua kutunza."

 

"Ina muda. Sema mzee alipoenda, Miryam akaichukua. Sa' siunajua ye' mrembo kwa hiyo na gari lazima itarembwa tu hata kama ishazeeka," akasema hivyo.

 

Nikacheka na kumwambia, "Kweli. Hivi... yule jamaa, Joshua, umeshamwona tena?"

 

"Toka walipomwachia? Sijamwona. Wa kazi gani kwanza? Akae huko huko, next time akileta bangi zake nitamtoboa kabisa..."

 

Nilikuwa nimekumbuka namna ambavyo huyo Joshua alimtukana Miryam siku ile kuhusu mwanamke huyo kutumia gari hili aliloliona kuwa la kizee, na sasa baada ya mimi kuelewa kwa nini mwanamke huyo alilitumia, kweli kashfa za jamaa zilizidi kuonekana kuwa mbaya sana. Lakini kitendo cha kumwona jana ofisini kwake Miryam akijionyesha kuwa mtakatifu na sasa Tesha kuonekana hajui kuhusiana na hilo, kilifanya nielewe kwamba kuna jambo lililokuwa likiendelea ambalo kijana huyu, labda na familia yao wote kwa ujumla, walifichwa kwanza, kwa hiyo nikaona nisimwambie kuhusiana nalo. Bila shaka dada yake alikuwa anapanga mambo fulani bila kuwaambia wengine, ama huyo Joshua alijipeleka huko kazini kwa Miryam yeye mwenyewe. Ningeona. 

 

"Tuachane na habari za huyo mjinga. Oya, hivi... hii ishu ya Joy mwanangu unaionaje?" akaniuliza hivyo.

 

Nikawa makini zaidi na kusema, "Iko hivyo tu. Kauliwa... labda shauri ya yale mambo uliyoniambia."

 

"Yale yake na Chalii Gonga, au ile ishu nyingine?"

 

"Ishu gani?"

 

"Acha kujitoa akili JC. Mke wake Chalii si kakuita ile juzi kukutisha eti atafanya kitu kibaya, halafu kweli kimetokea. Hujahisi labda ni yeye?"

 

Nikamwangalia Tesha. Kijana alikuwa na akili nyepesi, lakini nikamwambia, "Huwezi kuwa na uhakika. Labda tu tuyaache jinsi yalivyo."

 

"Dah! Me naacha kwenda Masai kwa wiki kabisa. Nisije kujikuta naamkia motoni kesho tu. Sijasema mbinguni maana najua nishakataliwa huko," akasema hivyo  

 

Nikacheka kidogo na kusema, "Kweli kaka, hilo ndiyo la muhimu kufanya. Jiweke kushoto kabisa."

 

"Fact," akasema hivyo.

 

Mawazo yake Tesha kuhusiana na jambo hilo yalifanana na ya kwangu, lakini sikutaka kuchangia sana upande wa mawazo yangu kwa sababu sikuhitaji kijana huyu avutwe kiundani zaidi kwa yale niliyofikiria kufanya. Ndiyo, bado nilikuwa na mpango wa kumtafutia haki Joy endapo kama kweli mke wake Chalii alihusika na kifo chake, lakini nilitaka Tesha akae pembeni kabisa na suala hili. Ingekuwa bora kwa ajili yake.

 

 

★★

 

 

Mwendo wa kupita robo tatu ya saa kuelekea Muhimbili ukatufikisha hospitalini huko, nasi tukaelekea majengoni baada ya kuegesha gari. Sikudhani ningekuja kurudi hospitalini hapa mapema namna hiyo, yaani baada ya kuingia tu kwenye siku za likizo, lakini Mariam aliustahili umuhimu wa kilichofanya nirudi tena hapa. Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeshawasiliana na yule daktari, nikampigia simu tena kumjulisha kwamba tulikuwa tumefika, naye akasema kwamba niende tu moja kwa moja mpaka ofisini kwake. Tulipita majengo ya chuo cha Muhimbili na aisee! Watoto! Kuna wanawake warembo ukanda huo wa wanavyuo mpaka Tesha alikuwa anashindwa kujizuia kuwaangalia. Ujio wangu kwa sehemu hiyo kama kawaida ulivuta macho ya baadhi ya watu walionifahamu na wasionifahamu, na wale walionijua wangenipa salamu kwa kupunga mikono na mimi pia kuwarudishia. Mariam alitembea kwa ukaribu sana na Tesha, akiung'ang'ania mkono wake ili asijikute anapotea kwenye mazingira hayo mapya kwake. Alikuwa amependezeshwa kiasi na dada yake isingekuwa rahisi kwa yeyote aliyemwona kwa mara ya kwanza kudhani ana tatizo kwenye akili yake.

 

Kwa hiyo tukasonga mbele zaidi, tukipita majengo ya kantini, majengo ya vyumba vya madaktari, mpaka kufikia upande wa hospitali yenyewe. Kama kawaida watu walikuwa ni wengi, nami nikawapeleka ndugu hawa moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya yule daktari. Tukaingia na kumkuta daktari huyo akiwa anajaza ripoti fulani, na baada ya kuniona, akatabasamu kiasi na kunisalimu pamoja na niliokuja nao. Daktari huyu aliitwa Roshan Sotto, mhindi, naye alikuwa mtu mzima karibu kufikia kama miaka 60 hivi. Alipomaliza kuandika ripoti ndiyo akaanza sasa kunisemesha kirafiki, akiuliza naendelea vipi huko nilikokuwa nimeenda. Nikamwambia niliendelea vizuri tu, naye akasema kiukweli nilikuwa nimetia pengo fulani hapo hospitalini kwa kuondoka, akinitania ni namna gani muuguzi mmoja wa kike hapo hospitalini aliyeitwa Latifah alivyonitafuta sana. Karibia kila mtu aliyenifahamu hapa hospitali aliniita mimi na Latifah mume na mke. Tulizoewa namna hiyo. Kwa hiyo daktari Roshan aliponikumbusha kumhusu, nikacheka sana na kumwambia kwamba nilijitahidi kuingia tena huku kisiri ili asinione maana kama angeniona ndiyo angening'ang'ania mpaka basi. 

 

Baada ya kuweka utani pembeni, umakini ukawa kwa Tesha na Mariam. Walikaa kwenye viti kutazamana na daktari Roshan, mimi nikiwa nimesimama, na baada ya utambulisho wa ndugu hawa wawili, Tesha akaombwa aelezee hali ya mdogo wake ilikuwa vipi. Akaeleza kila kitu kwa namna nilivyofahamu pia, naye daktari Roshan akajaribu kumsemesha Mariam. Binti hakujibu hata mara moja, nami nikamwambia daktari kwamba kutokana na namna ya Mariam ya kuitikia kwa vitu fulani na dalili kadhaa alizozionyesha, nilifikiri alikuwa na tatizo lililofanana na ASD, na ndiyo nilikuwa nimekuja kupata uhakika kutoka kwake ili apendekeze tiba sahihi zaidi ya kumpa. Daktari Roshan akanyanyuka, akafata kifaa fulani cha kielektroni kwenye chumba cha pembeni ndani humo humo na kumfata Mariam, kisha akamvalisha kichwani na kuanza kusoma namba-namba na maherufi-herufi, akimpima, na baada ya kumaliza akamtolea na kurudi kukaa kwenye kiti chake. 

 

Akamuuliza Tesha, "Huyu mdogo wako, amekuwa hivyo kwa muda gani?"

 

Tesha akasema, "Ni... miaka kama mitatu na miezi kadhaa. Inaelekea miaka minne."

 

Daktari Roshan akasema, "Sawa. Sasa ni hivi... aam, utasamehe na Kiswahili changu, ila si kibaya sana..."

 

Nikatabasamu kidogo, naye Tesha akasema, "Haina shida doctor."

 

"Her brain isn't damaged... aah... ubongo wa Mariam uko sawa... kabisa, hakukuwa na kitu kama... uvimbe au shimo dogo kutokana na ugonjwa, ama accident... ajali, kwa hiyo bila shaka... alikuwa na tatizo kwenye... mishipa midogo iliyosawazisha taarifa kwenye ubongo wake..." daktari akaelezea.

 

Aliongea kwa kutumia kauli za wakati uliopita lakini sote tulielewa alimaanishia wakati huu aliotoka kumpima binti, na alielekeza maneno hayo kwangu. Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.

 

Akaendelea. "Yaani... kwa wakati huu mishipa hiyo haikuweza kusawazisha... vizuri... taarifa mbalimbali ubongoni mwake, na... ni kweli... tatizo lililompata lilifanana na ASD."

 

"ASD ndiyo nini? Au... utanielezea baadaye JC?" Tesha akaniuliza.

 

"Yeah, nitakwambia. Ngoja nimuulize kuhusu tiba. Kwa hiyo doctor Rosh... what approach should be taken towards her treatment?" nikasema hivyo.

 

"It depends. Matibabu kwa ajili ya ugonjwa... wa ASD, yanalenga kupunguza... dalili zilizoingilia utaratibu mzuri wa kuishi au kutenda kwa njia kawaida... mtu aliyeathiriwa. ASD inawapata na... kuwaathiri watu... kwa njia tofauti, hiyo ilimaanisha kwamba waathiriwa hawawezi kuonyesha dalili zilezile... so... na njia za kuwatibu... haziwezi kufanana. Unaelewa pia... Tesha?" daktari Roshan akamuuliza hivyo.

 

"Ndiyo doctor," Tesha akajibu. 

 

"Yes. Matibabu hayo ya ndani... tabia, maendeleo ya kiakili, kielimu, psychology, mazungumzo, na vitendo. Yanaweza kumix kwa... kwa pamoja... ama kukazia fikira kimoja tu kati ya hayo, ikitegemea na hali ya mwathiriwa. Kwa hiyo cha msingi kufanya kwa ajili ya binti huyo... ingekuwa kuangalia nini... kinavuta zaidi akili yake, kisha kutafuta njia za kumfanya akaze fikira... zake... kuzungukia kitu hicho... au vitu hivyo, ili ubongo wake... urudi kwenye ukuzi mzuri wa awali..."

 

Blah, blah, blah kutoka kwa daktari mwenzangu zilikuwa nyingi sana, lakini nilielewa zaidi sasa kwamba Mariam angehitaji vitu viwili tu kwenye jambo moja; michezo ya kiakili, na mafundisho ndani ya hiyo hiyo michezo ya kiakili. Ningeweza kujua tayari alipenda mambo yapi yaliyoichezesha vyema akili yake, kwa hiyo ningeyatumia hayo hayo kwa njia ya kidaktari zaidi ili akili yake itiki. Daktari Roshan alieleza kwamba kwa jinsi hali yake Mariam ilivyokuwa, angehitaji msaada wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu ambao wangemwangalia kwa ukaribu. Hii ingemaanisha akae sehemu fulani hususa mbali na kwao, kama tu wodi za vichaa, lakini ya peke yake, na nilijua hiki ni kitu ambacho dada yake asingekubaliana nacho; achilia mbali tu na gharama ambazo zingehitajika kuwalipa wataalamu hao. Kwa hiyo nikiwa na uhakika wa mambo ya kufanya sasa kutokea hapo, nikamshukuru tu daktari huyu na kumwambia tungeshughulika vyema kumpatia msaada binti huyo ili kusaidia hali yake irudi kuwa sawa tena, nasi tukamuaga upesi ili aweze kuangalia mahitaji ya wagonjwa wengine waliokuwa wakimsubiri. 

 

Hivyo tukaondoka hatimaye sehemu hiyo ya hospitali, ikiwa ni mida ya saa sita kasoro sasa, nami nikawa natembea pamoja na ndugu hawa wawili kuelekea nje huku nikimwelezea Tesha vitu alivyotaka kujua. Kwa hiyo baada ya kuwa ameelewa vizuri hali ya mdogo wake, nikawaongoza ndugu hawa wawili kuelekea kwenye jengo la maabara moja hospitalini hapo, nami nikamwomba Tesha anisubirie nje kwa ufupi tulipofikia mlango wa kuingilia ndani hapo. Nikaingia na kumkuta mwangalizi wa sehemu hiyo ambaye ndiyo nilikuwa na lengo la kumwona. Huyu hakuwa mwingine ila mwanadada Latifah, mke wangu wa hospitali. Yeye ndiyo alikuwa msimamizi kwa sehemu hii na kwa sababu nilikuwa na nia ya kupata vitu fulani kutoka kwenye maabara hii, kuonana naye ilikuwa lazima. Kama ingekuwa ni ndani ya uwezo wangu basi ningefanya kila kitu kumkwepa kabisa maana nilijua kama angeniona ndiyo angening'ang'ania mno, na sikuwa nimekosea. Aliponiona tu ndani hapo, akaacha mambo aliyokuwa anafanya na kunifata kwa kasi huku akifurahi mno, naye akanikumbatia. Alikuwa mweusi wa maji ya kunde, mwembamba kiasi na mwenye miguu mirefu iliyoupa mwili wake umbo la umiss maridadi. Alikuwa na midomo minene na mizito kama vile iko tayari kudondosha udende muda wowote. 

 

Ijapokuwa tulikuwa tumebambikiziwa ndoa ya kiutani hapa hospitalini, mimi na Latifah tulikuwa tumeshafanya michezo mingi sana kwa sababu alinielewa mno. Kwa wengine tulijionyesha kuwa wapenzi wa kikazi tu, lakini nilikuwa nimeshampigisha kazi nyingi sana huyu mwanamke kiasi kwamba alitamani hata nimwoe!Kwa hiyo hata na hapa akaanza kudeka kwangu, akisema amenikosa, akiniambia mimi mbaya, nimeondoka bila kumuaga ili nimkimbie na niende kwa wanawake wengine. Nikampiga fix-fix za uwongo tu kumtuliza. Tukajuliana hali, kisha nikamweleza lengo langu la kuja hapo. Nilihitaji vifaa vichache vya maabara pamoja na kemikali kiasi za kugawanyisha virutubisho vya madawa, naye akaniuliza vya kazi gani. Nikamwambia kuna dawa nilikuwa nataka kutengeneza, na singechukua muda mrefu sana na vifaa hivyo ningevirudisha. Akakubali ila akaniomba nimjali kidogo kwanza, unaelewa, lakini nikamwambia haingewezekana maana kuna Serikali ilikuwa inanisubiri hapo nje, lakini akasisitiza tu na kutaka kunibusu mdomoni. Nikamzuia, nikimkumbusha kwamba kuna CCTV camera humo, lakini akaendelea kulazimisha. 

 

Alikuwa mkaidi kweli, lakini mara zote alipoona niko makini alitulia, na mimi nikamwonyesha kweli kwamba sikuwa na muda wa kufanya kile alichokuwa anakitaka. Nikamwambia kama hataki kunipa basi tu mimi niondoke, ndiyo akashusha makeke na kuninifatia vifaa hivyo, naye akaniwekea kwenye mfuko na kuniletea. Nikamuaga na kurudi kwa wenzangu baada ya kumwambia nahitaji kuwahi msibani, nikimwahidi kumtafuta baadaye, ahadi ambayo sikujua ikiwa ningeitimiza. Tesha na mdogo wake walikuwa wamesimama kwenye kingo ya pembeni karibu na ngome zilizoshika ukuta, nami nikamwambia nilikuwa nimepata nilivyovitaka kwa hiyo tuondoke hapo hatimaye. Tulipokuwa tumefika eneo lenye zile kantini, nikawaongoza ndugu hawa kwenye kantini moja ili tupate chakula chepesi. Nilihisi njaa kiasi na hata Tesha hakuwa amekunywa chai pia, kwa hiyo nikaagiza na kuwaagizia ndugu hawa msosi mtamu, nasi tukala kwa pamoja. 

 

 

★★

 

 

Tulipomaliza kula na kujisafisha, tukaondoka hospitalini hapo hatimaye. Mwendo ungekuwa mmoja tu wa kuturudisha nyumbani ili Mariam akapumzike, na Tesha alikuwa analalama kuhusu kuondoka bila namba ya pisi yeyote wa hapo Muhimbili. Nikamwambia wa huko wangemsumbua tu kwa kumnyonya mno hela mpaka angekauka. Lakini malalamiko yake ya kutaka pisi kali yakanifanya nikumbuke kitu fulani. Winny. Mmoja wa wale wadada niliokutana nao kwenye bajaji jana. Nikamwambia Tesha kuhusu mwanamke huyo, nikisema ni mzuri na nilichukua namba yake. Masikio yakamsimama jamaa akinitaka nimpatie, lakini nikamwambia atulie kwanza; mpaka nimtafute Winny mwenyewe, nimpange kuhusu rafiki yangu, halafu ikiwezekana niwakutanishe. Jamaa akakubaliana na hilo.

 

Tukiwa tumekaribia kuifikia Mbagala, simu yangu ikaanza kuita. Mpigaji? Soraya. Tabasamu hafifu likaniponyoka, na sikuwa na mpango bado wa kumwambia Tesha lolote kuhusu mimi na yule mwanamke, lakini jicho la mwewe la jamaa likaona jina la huyo Mamacita hapo akinipigia, naye akaanza kunisema sasa. Nikamwambia acha zako wewe, huyu anapiga kunisalimia tu, nami nikapokea na kumsikiliza mtoto mzuri. Alinijulia hali, akaniambia yuko kazini, na alitaka tuje tukutane tena. Yaani leo leo, maana kama tu msemo aliokuwa ametumia jana, ni kwamba bado "aliwashwa." 

 

Sikujibu kauli zake za kimapenzi moja kwa moja, lakini kitendo cha mimi kusema kwa leo haitawezekana maana nilibanwa na mambo mengi, kikafanya Tesha ashtukie dili. Nikamwambia tu Soraya ningemtafuta baadaye maana hapa nilikuwa na mpango wa kuelekea kwenye msiba wa rafiki, naye akaridhia. Baada ya mazungumzo pamoja na Soraya, Tesha akaanza kunichokoza sasa. Alitaka kujua. Ajue, ajue, ajue! Nikamwambia dogo tulia, Soraya anataka tu tuelekee kule kwenye mambo zetu lakini mimi nampiga chenga, ila Tesha hakutaka kukubali. Na akasema haina shida, mimi hata nikimficha, angejua tu. 

 

Kwa hiyo baada ya dakika kadhaa kupita kutokea hapo, tukawa tumefika Mzinga hatimaye na kuendelea kuelekea nyumbani. Kwa kuwa tulikuwa tumekula kule hospitali, hapo ilikuwa ni kumwacha tu Mariam nyumbani kisha sisi tugeuke tena kuelekea msibani. Lakini tulipofikia eneo la Masai, nikamwambia Tesha anishushie hapo kwanza. Akaniuliza nilitaka kwenda kunywa bia au, nami nikamwambia hapana, kuna deni nilikuwa naenda kulipa hapo, hivyo yeye ampeleke mtoto nyumbani kisha akigeuka atanikuta hapo ili tuondoke. Hakuwa na neno. Nikashuka na kwenda kule ndani baa. Hii ikiwa ni saa saba mchana, bado Masai ilikuwa imetulia, ikiwa wazi kwamba hata muda wa jirushe haukuwa umefika. 

 

Lengo langu kuja huku lilikuwa kumtafuta Bobo, nami nikawa nimemwona. Bobo alikuwa amesimama usawa wa kaunta akizungumza na wanawake wawili, bila shaka wahudumu wa hapo. Alikuwa akiwapa maelekezo sijui, na aliponiona, akanipa ile salamu yake ya uchangamfu. Nikawasalimu wanawake, nao wakaitikia na kuendelea kunitazama. Bobo akaanza utani wake, akimsukumia mmoja kwangu ili nikamtandike, lakini nikacheka tu na kumwambia ni yeye ndiye aliyefanya nikaja hapo. Nilitaka tuongee kibinafsi, na kwa hilo akasema hakuna noma. Tukasogea pembeni kabisa na kusimama kwa ukaribu.

 

"Oy, si unajua kilichomkumba Joy?" nikamuuliza.

 

"Ee, najua. Dah mwanangu! Wamemchana vibaya yaani! Wanaingiza vipisi kwenye jeneza. Inatisha kinyama," Bobo akasema.

 

"Aisee! Kwa hiyo... utaenda msibani?"

 

"Nitaenda kuchungulia tena. Unajua... nilienda kuona tukio baada tu ya kusikia na... mambo kule hayaeleweki. Huo mwili wake wenyewe ungetakiwa kuachwa kwa mapolisi huko, lakini wameona waipe tu familia yake heshima ili uzikwe. Mwanangu, Joy hakuwa wa kufa kihivyo... tukiwapata waliomuua, hata mimi nitachangia kuwachinja."

 

"Labda ni masuala ya makundi, si unajua? Ikiwa kuna kundi linalopingana na kundi la Chalii labda kumuua Joy ilikuwa kukomoana..."

 

"Ah, mwana una akili! Umekuja juzi tu tayari umeshaotea hivyo..."

 

"Nimeshaona mengi."

 

"Ee, inawezekana masuala ya makundi. Sijui sana, ila... maneno ni mengi, si unajua? Maaskari wanaweza kuja hadi hapa kuipekenyua Masai wakijua Joy alipenda kutimkia na huku, kwo' tumejiweka sawa pote hapa ili hiyo ikitokea maelezo yanyooke. Sijaelewa undani wa kilichompata ila... Chalii na yeye anawatafuta hao mbwa wal'omuua. Si unajua alikuwa demu wake?"

 

"Najua."

 

"Ndo' hivyo. Amepanga fanya kitu mbaya akiwanasa. Me nasubiri mchezo tu," Bobo akasema.

 

Nikatulia kidogo kutafakari mambo. Aidha Bobo alijua ama hakujua kwamba Chalii Gonga alinishuku mimi pia mpaka kunipigia simu leo kunitisha, lakini hicho siyo kilichokuwa kimenileta hapa.

 

"Wewe unaenda huko?" akaniuliza.

 

"Ee, ndo' tunaenda sa'hivi na Tesha," nikamwambia hivyo.

 

"Aaa, isingekuwa ya biashara na mimi ningeunga. Ulikuwa umekuja kunipitia?"

 

"Hamna. Nilikuja kwa sababu... nataka tuwe washkaji Bobo. Tight yaani. Nimekuangalia... nimekusoma... wewe uko poa sana. Japo uko upande mbaya lakini naona unajua upande sahihi wa mambo ni upi," nikamwambia.

 

"Ehehe... sikuelewi mwanangu, sijui ndo' unaongea nini," akasema hivyo.

 

Nikacheka kidogo na kusema, "Nataka unisaidie kitu, lakini iwe baina yetu."

 

"Nambie kamanda... usikonde," akasema.

 

"Una namba za mke wa Chalii?"

 

"Mke... Bertha?"

 

"Yah."

 

"Aaaa... kumbe!" akasema hivyo.

 

Nikatabasamu kidogo.

 

"Ah! Mwanangu umezunguka kichizi. Si ungesema tu?"

 

"Ndiyo nimekwambia sasa."

 

"Ah, maji laini mbona? Unamkubali eh?"

 

"Sana. Sema shida... kama unavyojua..."

 

"Ah... wewe Chalii asikuumize kichwa. Sikiliza nikwambie. Huyo manzi huwa ni mtata, lakini we' kama mjanja pale unaingia vizuri mbona? Halafu tena wewe... yaani yule unakula mapema. Si ile juzi alikuita ye' mwenyewe hapa?" Bobo akasema.

 

"Mh! Habari zinasambaa haraka!" nikasema.

 

"Hahaha... watu tuna macho. Yaani wewe Chalii asikupe presha wala, usimwogope. Namba nakupa... ukitaka huyo mutoto unakula vizuri sana... ila uende na swaga zilizonyooka, maana..." akasema hivyo huku akitoa simu.

 

"Anaweza akazingua, namwelewa. Usihofu. Najua pa kumtekenyea. Sema tu Chalii asijue, au siyo?"

 

"Uhakika. Ila ukimla chukua video uje unionyeshe. Nataka kuona kama ana mabaka au ngozi ya tembo!" Bobo akasema hivyo.

 

Nikacheka kidogo na kutoa simu yangu, nami nikaanza kuandika namba ya mwanamke yule na kisha kuitunza. Nikabadilishana namba na Bobo ili tuwe tunawasiliana pia, naye akanisevu kama alivyopenda kuniita, "Mchina." Ilikuwa sawa kwangu kuigiza kwa Bobo kwamba nilimtaka kimapenzi huyo Bertha ili anipe namba yake, na nilipeleka maigizo haya mbali kwa kufanya ionekane kuwa nilimhofu sana Chalii, lakini nilikuwa na lengo lingine kabisa kwa kufanya haya yote. Baada ya kuwa nimeipata namba, sasa ingekuwa ni kula sahani moja na huyo Bertha.

 

 

 

★★★★★★★★★★

 

 ITAENDELEA

 

★★★★★★★★★★

Previoua Next