MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA TANO
★★★★★★★★★★★★★★★★
Nikatoa elfu kumi na kumpatia Bobo ili apige pombe mbili tatu, naye akaonyesha kukubali sana pigo zangu na kusisitiza nisije kusahau kuchukua mkanda wa video nikifanikisha kumvua nguo mke wake Chalii. Na mimi nikamwambia atunze jambo hilo kuwa siri yetu pekee, naye hakuwa na neno. Hazijapita dakika nyingi sana Tesha akafika hapo nje, naye akaegesha gari na kuja ndani ili asalimiane na Bobo pia. Wakazungumza kidogo kwa utani, kisha ndiyo tukamwacha Bobo hapo na kurudi garini ili kwenda msibani.
Kabla ya kuingia ndani ya gari, nikaenda kwenye duka moja lenye huduma ya kutoa pesa kwa wakala wa benki ya CRDB, nami nikatoa kiasi cha shilingi laki mbili kwenye akaunti yangu kupitia simu, na nikanunua bahasha ndogo hapo hapo, kisha nikaiweka pesa hiyo ndani na kurudi garini. Tesha akaniambia kwamba alimwacha mdogo wake kwao vizuri na kuwaeleza mama zake wakubwa kiufupi kuhusu yale ambayo daktari Roshan alituambia kumhusu Mariam; akisema wangemjulisha Miryam kuhusiana nayo maana yeye alikuwa ameenda kazini, na walinitumia shukrani kwa jitihada niliyoweka leo. Ankia angekuwa ameshatangulia huko msibani, hivyo jamaa akawasha gari na mwendo ukaanza kuelekea Buza.
Tukiwa bado njiani ndiyo nikachukua nafasi hiyo kumtafuta yule Winny, nami nikaongea naye na kumpiga swaga laini mpaka akaeleweka. Alionekana kupenda ucheshi sana kwa hiyo niliweka utani mwingi, na ndiyo nikawa nimemwambia kwamba kuna ndugu yangu aliyekuwa akitamani sana kujuana naye ili waweze kuwa marafiki pia. Niliingiza tu na uwongo kwamba huyo ndugu yangu alishawahi kumwona pia wakati fulani, na baada ya kuiona picha yake ya WhatsApp profile kwenye simu yangu akamtambua na kutaka nimpe namba. Basi, akawa amekubali nimpe Tesha namba yake, lakini kabla ya hilo nimrushie picha zangu na za Tesha kwa WhatsApp. Sijui alikuwa anataka kutulinganisha? Tukafanya hivyo, naye Tesha akasema na yeye huyo Winny atume picha za kwake nyingi ili tumwone. Maungano yakawa yamefanikishwa hapo, mambo yetu vijana kama inavyokuwa.
Baada ya dakika kadhaa, tukawa tumeingia Buza, naye Tesha akapeleka gari hadi msiba wa Joy ulipofanyikia. Sikujua sana ikiwa ndiyo palikuwa kwao au kwa ndugu zake waliokuwa huku tu, lakini kwenye hiyo nyumba tulipofikia tulikuta watu wengi kiasi. Wanawake walikuwa upande wa ndani zaidi na wanaume walikaa kwenye viti sehemu ya nje zaidi, na ujio wetu hapo ulifanya fikira za wengi zielekezwe kwangu. Hakukuwa na viti vya kutosha lakini hadi tukapishwa na wanaume watu wazima ili tukae, na kuna wanawake kadhaa waliokuja na kutupa salamu kwa mikono huku wakipiga na magoti kwa heshima kabisa. Kwa hiyo tukakaa tu kwa utulivu, na Tesha akampigia simu Ankia ili kumwambia kwamba tulikuwa hapo nje. Kwa ufahamu wangu wa misiba, bila shaka leo ikiwa ni siku ya pili tokea kifo cha Joy basi hii ya kuja hapa ilikuwa kutoa tu pole na kuunga mkono wafiwa, na labda kesho ama kesho kutwa ndiyo wangezika.
Muda si muda, Ankia akawa ametoka nje na kuja mpaka upande wetu. Alikuwa amevaa T-shirt ya mikono mirefu nyeusi na kitenge kwa chini, kilemba kichwani, na alishika khanga moja mkononi sijui kwa masilahi gani. Watu walimwangalia mpaka alipokuja kufikia nilipokaa, halafu akachuchumaa kama vile amepiga magoti karibu kabisa na mimi, huku mikono yake akiiweka mapajani kwangu. Akaongea nasi, akisema yuko na wanawake wengine wakitengeneza chakula cha jioni kwa ajili ya wote walioko hapo, nami nikamuuliza ni ndugu gani wa karibu zaidi na Joy aliyekuwa hapo.
Akasema ni mama yake mzazi pamoja na baba wa kufikia, na dada zake wawili wa damu pia. Akatuonyesha huyo baba wa kufikia, mzee wa miaka iliyokimbilia 70 hivi ambaye aliketi mbele zaidi pamoja na wanaume wengine walioonekana kuwa marafiki zake. Hapo ndiyo palikuwa kwa wazazi wao, lakini mwili wa Joy ungesafirishwa kama siyo kesho, basi kesho-kutwa kwenda Nachingwea; ndiyo iliposomeka kuwa kwao kihalisi na mwanamke huyo ili akazikwe huko. Jeneza lake lingeletwa baadaye hapo nyumbani na lingelala mpaka kufikia wakati wa usafirishaji.
Ingawa najua nilikuwa nimepita kwenye mstari uliopinda sana pamoja na mwanamke yule niliyekutana naye na kumjua kwa kipindi kifupi, nilikuwa nimehuzunishwa sana na kifo chake. Achilia mbali tu kukisia ni nani aliyemsababishia kifo, ila ni ile hali ya "kujuana" zaidi kutokana na kushiriki mapenzi pamoja naye usiku ule iliyofanya nihisi ukaribu naye kiasi, na alikuwa mtamu kweli! Nikatoa ile bahasha mfukoni na kumpatia Ankia, nami nikamwambia ampelekee mama yake Joy na kumpa; iwe kama rambirambi yetu sisi watatu kuielekea familia hiyo. Ankia akakubali na kusema angeenda kuwaambia kwamba mume wake ndiyo aliyeitoa hiyo rambirambi, eti mimi yaani, nami nikatabasamu tu kidogo na kusema sawa. Mwanamke huyo akaondoka zake kurudi sehemu ya ndani, nasi tukaendelea kusubiri tu hapo nje.
★★
Baada ya dakika kama kumi tu, Ankia akawa ametoka tena, zamu hii akiwa na mwanamke mwingine pamoja naye. Huyu alikuwa mrefu kiasi, mwenye mwili ulionawiri na ngozi rangi ya chocolate, akiwa amevaa nguo kama kijora ya kijani kibichi huku kiunoni akijifunga khanga, na alikuwa na rasta ndefu kweli mpaka kufikia kiunoni. Sura yake ilikuwa na ufanano wa mbali kiasi na sura ya Joy, nami nikawa nimetambua huyo ni dada yake. Ankia akaja naye mpaka upande wetu lakini hakutufikia kabisa, kisha akaniita kwa ishara ya kiganja kuonyesha alitaka nimfate. Nikanyanyuka, na sijui ni kwa nini lakini idadi ya wanawake waliokuwa wakija nje ilizidi kuongezeka tu, na walielekeza macho yao upande wetu. Nikawafata wanawake hao pembeni waliposimama, nami nikasimama karibu yake Ankia. Kwa ukaribu huo, huyo dada yake Joy alionekana kuwa mrefu kiasi cha kunipita, lakini macho yetu yalilingana.
"JC... huyu ni Adelina. Ni dada yake Joy. Adela, huyu ndiyo JC," Ankia akatutambulisha.
"Ahaa... sawa. Habari yako kaka?" Adelina akanisalimu.
Alikuwa na sauti nzuri tu kutoka ndani ya midomo yake minene, nami nikajibu, "Salama dada. Poleni kwa msiba."
"Asante sana. Tunashukuru pia kwa rambirambi yako. Ni ukarimu mwingi sana ulionao kaka," Adelina akaniambia hivyo.
"Oh, haina shida... tuko pamoja. Mama anaendelea vipi?" nikamuuliza.
"Ah... amepigika yaani. Sisi wote. Unajua... kufa huwa ni... inatokea... lakini mtu akifariki kama mdogo wangu alivyofanywa... inaumiza kwa kweli," Adelina akasema hivyo, na machozi yakaonekana kumlenga.
Ankia akamshika begani kama kumpa faraja.
"Pole sana," nikamwambia hivyo Adelina.
"Asante. Ni mama ndiyo ameniambia nije nikupe shukrani kwa niaba yake... ameishiwa nguvu bado, yaani hata kutoka nje ameshindwa," Adelina akaniambia.
"Aaa sawa... haina shida. Utamwambia mimi ni rafiki yake Joy pia, kwa hiyo tuko pamoja," nikasema hivyo.
"Sawa," akaitikia.
"Naweza ku... kukuomba jambo fulani, dada?" nikamuuliza hivyo.
"Ndiyo, unaweza," akasema hivyo.
Nikamwangalia Ankia kiufupi, naye akajiongeza.
"Ngoja niende ndani, utanikuta," akamwambia hivyo Adelina.
Adelina akatikisa kichwa kukubali, naye Ankia akatembea.
Nikamwangalia mwanamke huyu na kusema, "Mmeshazungumza na mapolisi tena kuhusiana na yaliyotokea?"
"Hapana... bado wanafatilia. Sijui kama watawakamata waliomuua mdogo wangu ila... naombea kwa Mungu wawakamate," akaniambia hivyo.
"Yes, hata mimi pia. Kwa hiyo mlikuwa mmeachiana mawasiliano labda na maaskari au... yaani, askari aliyeshughulikia huo uchunguzi?"
"Ndiyo, tumepewa namba zake za mawasiliano."
"Ahaa... sawa. Naweza kuomba unipatie tafadhali?" nikamwambia hivyo.
Akanitazama usoni kiudadisi kiasi.
"Kama wewe ulivyoniambia dada, hata mimi nataka waliomfanyia Joy hayo wakamatwe. Ninataka kusaidia, na ndiyo maana nahitaji namba ya huyo askari ili niende sambamba na uchunguzi wao," nikamwambia.
"Kwa nini? Kuna kitu fulani unajua?" akaniuliza.
"Hapana, ila nataka kuhakikisha haki kwa ajili ya mdogo wako inapatikana. Kama unavyojua... hawa maaskari wanaweza wakasinzia, na mimi nina uwezo wa kuharakisha huo uchunguzi tukawagundua wauaji, kwa hiyo... nikipata chochote kile, inakuwa vizuri kama nina namba zao ili niwapasie tu taarifa. Si unaelewa?" nikamwambia hayo.
Akatikisa kichwa kukubali, naye akasema, "Sawa. Ngoja nikafate simu ndani nije nikupe."
"Sawa, nashukuru. Nakusubiri hapa," nikasema hivyo.
Mwanamke huyo akaelekea kule ndani tena, nami nikabaki kusubiri hapo hapo nilipokuwa nimesimama. Tesha alikuwa akinitumia ishara za mikono kuuliza 'vipi,' nami nikamwambia kwa ishara atulie tu ningemwelezea. Kusimama hapo kulinifanya nione namna ambavyo baba wa kufikia wa kina Joy alivyoniangalia sana, na najua angedhani labda nafahamiana sana na Adelina baada ya kuniona napata maongezi pamoja naye. Dakika mbili hivi naye dada mkubwa wa Joy akarejea tena, zamu hii akiwa na simu mkononi, naye akaja kwangu tena ili anipe namba. Nikafungua simu yangu pia, nami nikamsikiliza aliponitajia namba za huyo askari/mpelelezi, kisha nikazitunza kwenye simu.
"Asante dada," nikamshukuru.
"Usijali. Hivi... unaitwa nani kweli?" akaniuliza.
"JC."
"J..C. Sawa. Nataka nikuombe kitu, samahani lakini..."
"Usiwaze. Niambie," nikamkatisha.
"Naomba na mimi unipatie namba yako kama hutojali... ikitokea umepata lolote basi na mie unaweza kuniambia, si ndiyo?"
"Okay, haina shida. Nitajie zako nikubipu."
Akafanya hivyo, nami nikazitunza zake na kumpigia, kisha akatunza zangu pia.
"We' haukai huku?" nikamuuliza.
"Ee, me nakaa Mbezi. Wewe je? Mnaishi wapi na mke wako?"
"Mke? Aa huyu Ankia? Tupo Mbagala huku..."
"Aaa ndiyo mmejuana na Joy huko eh?"
"Ndiyo."
Akatikisa kichwa kidogo kuonyesha uelewa na kusema, "Sawa. Haya, baadaye. Tuta... wasiliana."
"Haya."
Akaondoka baada ya hapo, nami nikawa nimeridhika baada ya kuzipata namba za huyo askari. Taratibu tu, na mpango niliokuwa nao ungezaa matunda yake. Nikarudi pale kwenye kiti changu na kukaa, naye Tesha akanisogelea karibu zaidi.
"Vipi? Nani huyo?" akaniuliza.
"Dada yake Joy," nikamjibu.
"Ahaa... lizuri kweli. Mlikuwa mnapeana hadi manamba kila mtu kakuona bonge la fisadi."
"Kwenye kipi labda? Je kama tunajuana?"
"We' usikimbie maana, watu washasoma mambo kivingine. Ndiyo maana nampendaga Dulla Makabila, kashaimba hivi vitu hadi msibani vinatokea. Utasababisha Joy aghairi kufa!" akasema hivyo.
Nikabana cheko yangu na kumwambia, "Acha ujinga, tuko msibani. Na nilikuwa naongea naye mambo ya maana siyo upuuzi."
"Hahah... haya bana. Kwa hiyo hapa tunasubiri maiti iletwe halafu ndiyo tunaosha, au siyo?"
"Ee lakini... si tunaondoka na Ankia?"
"Akijichelewesha je?"
"Tutaongea naye," nikamwambia hivyo kwa utulivu.
Baada ya dakika chache kupita, nikatoka hapo na kwenda pembeni kidogo, kisha nikatoa simu na kupiga kwa namba za mke wake Chalii Gonga. Nilikuwa nataka nianze kukichokonoa kichuguu alichokuwa amejifichia huko aliko, ama labda kama ni kasri la kifalme, basi niyavunje malango yake. Piga ya kwanza, hakupokea. Ya pili, ya tatu, kimya. Nikaona nimweke pembeni kwanza ili baadaye nije kuendelea kumchokoza, labda kwa sasa alikuwa bize kutafuta watu wengine wa kuua.
★★
Basi, kutokea hapo tukaendelea kusubiri tu mpaka ilipofika mida ya saa kumi jioni. Mida hiyo ndiyo mwili wa Joy, au niseme "vipande" vya Joy ndiyo vikawa vimeletwa. Ulikuwa ndani ya jeneza jeupe lenye msalaba kwa juu, likiwa limebebwa kwenye pickup nyeupe ya Toyota Hilux iliyoonekana kuwa ya gharama. Wanaume wakaanza kuchangamka kuliondoa hapo ili liingizwe ndani ya nyumba, vilio kutoka kwa wanawake vikisikika kutokea huko ndani jeneza lilipokuwa linapelekwa, na kama ni kwenda kushoto zaidi na matarajio yangu ambayo sikuwa nayo kabisa mpaka kufikia sasa, basi ilikuwa ni kumtambua dereva aliyeendesha gari hilo. Aliposhuka, mimi na Tesha tukatazamana kimshangao kiasi, kwa sababu ilikuwa ni Chalii Gonga.
Oh, hii ndiyo ilikuwa mara yangu ya pili kumwona kutokea mara ya kwanza kule kwenye baa yake, maana hata aliponipa elfu kumi kama nauli ya kuja kwenda kukutana naye, nilimpiga chini, na baada ya yeye kuniona, akanipungia kiganja chake hewani huku akiniangalia kwa umakini, nami nikamtikisia kichwa mara moja tu kurudisha salamu yake. Sikufikiri ningemwona hapo leo, lakini jinsi ambayo alijichanganya na watu wa familia yake Joy hapo ilinifanya nitambue kwamba alikuwa akifahamiana nao. Na si ajabu aligharamia mambo mengi yaliyoendeshwa kwenye huu msiba. Baada ya kuona ameongea machache pamoja na baba wa kufikia wa akina Joy, yeye pamoja na aliokuja nao wakarudi kwenye gari, kisha wakaondoka hapo. Alitendewa kama taita hapo, na sidhani ikiwa kuna yeyote kati ya watu wa familia hiyo waliofikiri mke wa Chalii alichangia kwa kiasi fulani katika mauaji ya Joy, ijapokuwa hata na jamaa hakuonekana kujua, na mimi bado sikuwa na uhakika. Yote kwa yote, ingefahamika tu.
Baada ya Chalii kuondoka, wanawake wakaanza kusambaza sahani zenye wali na maharage kwa wazee-wazee, kisha watu wazima vijana, nami nikamwambia Tesha kwamba kiukweli sikujihisi vizuri sana kula msibani. Akauliza kwa nini, nami nikamwambia iko hivyo tu. Akasema nisiwe hivyo, nikipokee tu chakula kikiletwa na nile mpaka kiishe, la sivyo ningemkasirisha Joy huko mbinguni kwa kuacha kula kwenye msiba wake. Akanifanya nitabasamu kwa hisia, kwa sababu alinifanya nitilie maanani ukweli kwamba ingawa Joy aliuwawa vibaya, angalau alikuwa amepumzika. Kwa amani. Labda. Tukaletewa misosi pia. Msosi ambao uliletwa kwangu, ulibebwa na Adelina mwenyewe, naye Tesha akapewa na Ankia. Cha kushangaza kwa upande wangu ni kwamba, Adelina alifikiri Ankia ni mke wangu, si ndiyo? Lakini yeye ndiyo akanipa chakula. Na pamoja na kwamba alikuwa mkubwa zaidi yangu, nilipokipokea akashuka mpaka chini kwa kupiga goti moja ili kunionyesha heshima. Nikabaki nikimwangalia mwanamke huyo kwa umakini, sura yake bado ikionekana kuwa na simanzi lakini akijitahidi mno kuwa imara, nami nikamshukuru na kumwacha aende. Tesha sasa! Akaanza mambo yake. Nikamwambia komea hapo hapo!
Tukala, tukamaliza, sahani pembeni. Saa kumi na mbili haikukawia kufika, na baadhi ya watu walikuwa wameshaondoka baada tu ya kula. Ikiwa inakimbilia kuingia saa moja usiku, Ankia akaja, naye akatuambia kwamba kama ni kuondoka hapo basi mimi na Tesha tutangulie na yeye angekuja baadaye. Kuna vitu bado alikuwa anataka kusaidia kufanya hapo nyumbani kwao Joy, kwa hiyo akanipa funguo za nyumba yake na kutuaga. Kukawa hamna noma kwa hilo, nasi tukaingia kwenye gari ili kurudi Mzinga. Saa mbili usiku tu ndiyo inaingia nasi tukawa tumefika pande za maskani yetu. Nilikuwa nimeshamuungishia Tesha namba ya Winny ili waanze kuwasiliana pia, na kwa kuwa mwanamke huyo alikuwa ametuma picha zake maridadi sana, Tesha akasema ndiyo keki ambayo angeanza nayo kuila kabla ya zingine. Kwa kuwa nilihitaji kumwona Mariam kwanza, nikaamua kwenda naye pale kwao ili nimjulie hali binti huyo pamoja na mama zake wakubwa. Bado mfuko wa vifaa nilivyochukua hospitali leo uliokuwa ndani ya gari hilo, nami nikauacha tu humo mpaka kufikia wakati wa kuondoka ndiyo ningeuchukua.
Nikafikiria kwamba huenda Miryam bado angekuwa kazini, lakini tulipofika ndani, tukawakuta wanawake wote wa hapo wakiwa sebuleni, kutia ndani Shadya. Bibie Miryam alikuwepo sebuleni pia wakati tunaingia, kisha akaelekea upande wa jikoni; ikionekana alikuwa anapika. Wanaume tukapokewa kwa salamu nzuri sana, nasi tukakaa kwenye sofa moja huku Tesha akianza kuelezea namna ambavyo mambo yalikuwa huko msibani; kuanzia wakati tulipofika mpaka tulipoondoka. Wakawa wanachangia mada kuhusiana na janga lililomkumba Joy, na kutokea hapo sasa ndiyo Tesha akaanza kupewa somo la kujitahidi kuachana na masuala ya kukesha Masai, kwa sababu mama zake wakubwa hawakutaka aje kujikuta kwenye hali kama ya Joy, na kwa wakati huu Tesha alikuwa msikivu kweli, akiunga mkono pointi zao kwa kusema angekuwa mwangalifu sana. Kwa upande wangu mimi nilikuwa kimya tu, nikimtazama binti Mariam sanasana. Alikuwa amekaa chini karibu na miguu ya Bi Zawadi, akiwa anatazama katuni kwenye TV huku amekilaza kichwa chake kwenye paja la mwanamke huyo, na Bi Zawadi alikuwa akizilaza-laza nywele laini za binti taratibu kama kumbembeleza.
"Kwa hiyo kesho ndo' watafanya na ibada eh?" akauliza hivyo Shadya.
"Eee kesho. Halafu hazikiwi hapo Buza. Ankia amesema mwili wa Joy utapelekwa huko Nachingwea... ndiyo kwao kabisa," Tesha akamwambia.
"Aaa kumbe?" Shadya akauliza.
"Eeeh," Tesha akasema.
"Ankia je? Mmerudi naye?" Bi Jamila akaniuliza hivyo.
"Ye' amebaki huko. Kuna mambo anamalizia kufanya, atakuja baadaye," nikamjulisha hilo.
"Si mngemsubiria? Masuala ya usiku siyo mazuri kwa wanawake mnajua," Shadya akasema.
"Ye' mwenyewe ndo' katuambia tutangulie. Sidhani kama atachukua muda mrefu sana..." Tesha akasema.
Ni wakati huu ndiyo bibie Miryam akawa amerudi tena sehemu hii ya sebule, naye akakaa kwenye mkono wa sofa walilokaa mama wakubwa na Mariam kwa chini. Wakati huu ndiyo nikaweza kumchora vyema zaidi. Alivaa nguo kama Punjabi yenye rangi ya zambarau, pamoja na kilemba kilichofunika nywele zake. Ingawa suruali ya nguo hiyo ilikuwa pana, umbo lake lilichoreka vizuri hasa alipokaa namna hiyo kwa kunyanyua mguu mmoja juu kiasi, nasi tukaangaliana kwa njia ya kawaida tu machoni na kisha kuwatazama wengine.
"Mariam anapenda katuni eh? Naona ametulia kweli," nikasema hivyo.
Binti akanitazama usoni, nafikiri kwa sababu alisikia nimetaja jina lake.
"Ahahah... sana. Muziki, katuni, anapenda sana. Si unakumbuka ulivyomkuta anacheza "Kwikwi?"" Bi Zawadi akasema hivyo huku akiigiza vipapatio kwa mikono yake.
Nikatabasamu kidogo na kusema, "Ndiyo nakumbuka. Na alikuwa anapatia."
Bi Zawadi akacheka kidogo, nami nikamwona Miryam akitabasamu kwa hisia.
"Hapo ukimtolea anaanza kulia," Shadya akasema hivyo.
Wote tukacheka kidogo pia, nami nikiwa nasugua-sugua magoti yangu kwa viganja, nikasema, "Sawa. Basi, ngoja me niwaache jamani."
"Ih? Wapi tena?" Tesha akaniuliza.
"Naenda ndani tu," nikasema hivyo.
"Kwani hapa nje?" Shadya akauliza.
Nikacheka kidogo kwa pumzi.
"Tulia bwana, sister anataka kuturekebishia matumbo," Tesha akasema.
"Ndiyo baba, kaa tu. Kwanza... Ankia bado si hajarudi? Utaenda kukaa mwenyewe?" Bi Zawadi akaniuliza.
Nikatabasamu tu.
"Au umechoka sana?" akauliza Bi Jamila.
"Hapana, sijachoka wala," nikajibu.
"Eeeh... kaa tu baba'angu. Mimi anaandaa mirosti huko. Si unakumbuka nilivyosema kuhusu mapishi yake?" Bi Jamila akaniambia hivyo huku akimzomea Bi Zawadi kiutani.
Shadya na mimi tukacheka kidogo, nami nikamwona Miryam anamtazama mama mkubwa wake kimaswali kiasi; bila shaka akijiuliza kauli yake ilimaanisha nini, naye Bi Zawadi akamwangalia mwenzake kwa njia ya kununa.
"Ee mwanangu, kaa uonje mapishi ya sister. Anajua huyu!" Tesha akamsifia dada yake.
"Eti Mimi, wananisema me sijui kupika. Eti unanizidi," Bi Zawadi akamwambia Miryam hivyo kama anadeka eti.
"Aa wapi! Akuzidi nani? Wewe ndiyo unajua bwana. Waambie wakuache," Miryam akambembeleza eti.
"Anakupa kichwa tu. Ngoja JC ale chake leo uone kama atagusa chako tena," Bi Jamila akamwambia mwenzake hivyo kwa utani.
Eh! Kauli hiyo ya Bi Jamila ilikuwa inalenga suala la chakula, lakini ilikuja kwa njia ambayo iliingiza jambo lingine akilini, na nafikiri Miryam pia alielewa kwa njia hiyo hiyo kwa sababu nilimwona akishtuka machoni kiasi na kumtazama Bi Jamila kimaswali, kisha akanitazama kwa njia ya kuhukumu. Nikaangalia pembeni na kujikaza nisicheke, kwa kuwa najua hata Miryam alidhani kilichoongelewa kuliwa kilikuwa chake kingine! Aisee! Hii familia ilinipa raha sana. Wengine hawakuelewa mambo kwa njia hiyo, lakini kwa namna tu ambayo Miryam aliniangalia ilionyesha alielewa vitu vingi kwa mapana mno, na alikuwa na akili iliyonolewa vizuri sana.
Tesha akaniangalia kwa umakini, kisha akauliza, "Vipi kaka? Umefurahi sana eh?"
Nikaibana cheko yangu zaidi na kumwambia, "Ee... ndiyo... ahah... sawa. Nita... nitakaa kukionja."
Niliposema hivyo, nikamwangalia Miryam usoni, naye akatazama pembeni akiwa kama ameudhika vile, nami nikaelewa kwamba alikuwa ameshasoma kile ambacho kilipita akilini mwangu pia. Nikainamisha uso na kuweka kiganja changu kwenye paji ili nijisitiri zaidi kutocheka. Bi Jamila alikuwa amenifurahisha mno bila yeye mwenyewe kutambua umbali wa furaha hiyo, na maongezi zaidi yalipokuwa yakiendelea, simu yangu ikaita. Nikatoa ili nione mpigaji kukuta ni mke wake Chalii Gonga. Muda mwafaka kwake wa kunitafuta ukawa sasa hivi, hivyo nikaomba wenyeji wangu samahani ya kuwapisha ili niende nje kuzungumza na simu, nami nikatoka hapo ndani upesi.
Nikiwa varandani nikapokea. "Hello?"
"We' nani?" sauti ya mke wake Chalii ikasikika ikisema hivyo.
"Huwezi kukisia? Hata sauti tu hujaitambua?"
"Bwana, sema we' ni nani. Nimekuta umenipigia. Sema we' ni nani, una shida gani..."
"Me JC," nikamwambia.
"Nani?"
"JC."
"Wa wapi?"
Nikabaki kimya tu baada ya yeye kuuliza hivyo.
"Aaa... lover boy wa Joy?" akasema hivyo.
"Mmm... ndiyo mimi."
"Ehe... kulikoni?"
"Naomba kukutana na wewe tafadhali," nikamwambia kwa sauti ya upole.
"Unataka nini?"
"Nataka tu tongee."
"Kuhusu?"
"Mambo mengi. Sikia... juzi ile tulivyoongea... nilikuja juu sana. Najutia kuongea kwa hasira mbele yako, eh? Nataka mambo yanyooke kati yetu..."
"Ahhahaaa... Naona umepunguza kibesi leo. Yamekukuta yapi huko HB wa Masai?"
Nikakunja ngumi yangu na kumwambia kwa sauti tulivu, "Sina haja ya kuzunguka popote. Nilitafakari tu uliyoniambia... na nimeona uko sahihi. Mimi sikuwezi, na sitaki uje uniumize wala nini maana... me bado mdogo, sitaki kutengeneza maadui. Ni bora zaidi nikijiweka upande wako badala ya kuwa dhidi yako... na naweza kuwa rafiki mzuri kwako kwa saabu' naweza kukupa vitu vyenye faida."
"Mhm... ahahah... a-ah. We' unaweza kunipa nini mimi? Unafikiri nahangaishwa na kasura kako? Mimi ni malikia. Nimeshaona wengi zaidi yako, em' niambie una nini cha kunioffer mimi..."
"Wala sijafikiria masuala kama hayo. Naongelea vitu vitamu hata zaidi ya heroo dada'angu," nikamwambia hivyo.
"Unamaanisha nini?"
"Nipange. Tukutane hata kesho sehemu yoyote unayotaka wewe. Nitakuonyesha," nikamwambia.
"Kwa hiyo we' kijana unataka kunifanyia mimi mchezo wa kipuu...."
"Hapana, Bertha. Niko serious. Ndiyo maana nimekwambia wewe mwenyewe unipange tukutane unapotaka. Nataka niwe upande wako, sawa? Na lazima nikupe kitu kizuri kama zawadi ya urafiki... au hata kama siyo urafiki basi tu iwe njia ya kuomba msamaha. Nimekuelewa sana... na... ukikuta nazingua, una ruksa ya kunifanya chochote unachotaka," nikamwambia hivyo kwa uhakika.
Nilikuwa makini sana kuhakikisha maneno hayo hayasikiki kule ndani kwa kuongea kwa sauti ya chini, naye akauliza, "We' ni mjanja eh?"
Nikajibu, "Ndiyo. Me ni mjanja."
Akatulia kidogo, kisha akasema, "Haya. Tutaona. Nitakutafuta. Usinitafute mpaka nikutafute. Sijui umenielewa?"
Nikatabasamu kidogo, nami nikamwambia, "Poa. Nitasubiri. Nishtue tu muda wowote unipange."
Akakata simu.
Raa! Hapo nikawa nimechukua, nikaweka, halafu sasa ikawa imebaki tu kufanya Waah! Angalau nilikuwa nimeweza kuipika vizuri akili ya mwanamke huyo ili aone kwamba nina kitu kizuri cha kumfaidisha nacho katika mambo aliyopenda zaidi; madawa. Ningehakikisha namchanganya mwanamke huyo mpaka ingeeleweka kwake kwamba si yeye tu ndiye aliyetakiwa kujiona wa kuogopwa, bali kuna watu ambao hawakutaka kuogopwa, lakini walistahili kuogopwa. Achana na mimi kabisa nikiwa nimekaza nia kwenye jambo fulani, na huyo Bertha angelipia kwa kucheza na mimi. Kila kitu kingekwenda taratibu tu, lakini angejikuta anaanguka chini kwa kasi sana!
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments