Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA SITA

★★★★★★★★★★★★★★★★


Nikatoka hapo varanda na kurudi ndani, nami nikamkuta Miryam akiwa sebuleni tena, akiwa amekaa kwenye mkono wa sofa alilokalia Bi Zawadi na Bi Jamila, wakati huu wote wakipata mazungumzo. Harufu nzuri sana ya chakula alichokuwa anaandaa mwanamke huyo ilipenya vizuri zaidi puani mwangu, nayo ikaongeza hamu yangu ya kutaka kuonja mahanjumati yake. Mazungumzo yao yalikuwa kama mabishano mepesi baina ya Shadya na bibie Miryam mwenyewe, nami nikawa nimekaa sofani karibu na Tesha kwa mara nyingine.

"Hapana, unakosea. Ni nje, siyo ndani. Hivi unafikiri ukimwambia nani hivyo atakubali?" Shadya akamwambia hivyo Miryam.

Miryam akatabasamu kiasi na kutikisa kichwa kidogo.

"Ametoka ndani ya... ametoka nje ya... eh! Pana ugumu hapo..." Tesha akasema hivyo kwa utafakari.

"Me naona kama vile Mimi yuko sahihi," Bi Jamila akasema.

"Mm-mm, haiwezekani. Basi tumuulize msomi... daktari, JC," Shadya akasema hivyo.

Mimi nikawa bado sijaelewa na kuendelea kuwaangalia tu kwa utulivu.

"Kwani nani hapa hajasoma? Au Mimi siyo msomi?" Bi Zawadi akamuuliza hivyo Shadya.

"A-aah, ye' anao wa kivyake. JC yeye anao kama wa kwangu... na mimi ningekuwaga daktari," Shadya akasema hivyo.

"Daktari wa porojo," Tesha akasema hivyo.

Mama zake wakubwa wakacheka.

Nikiwa bado sijaelewa, nikauliza, "Ni kuhusu nini?"

Shadya akasema, "Kuna mama mmoja pale juu ile juzi amefumaniwa na mume wake akiwa na hawala. Ametoka nje ya ndoa, si ndiyo?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Sasa je!" Shadya akamwambia hivyo Miryam.

Miryam akatabasamu kiasi na kusema, "Hujaelezea vizuri kwa nini tunapingana."

Nikamwangalia Tesha, naye akasema, "Yaani eti... sawa si kama hivyo huyo mwanamke kafumaniwa? Sasa, huwa kuna hiki kitu kwamba mtu kama huyo tunasema ametoka nje ya ndoa. Da' Mimi anasema kwamba kwa Kiswahili fasaha inatakiwa kuwa ametoka ndani ya ndoa, Shadya hataki. Hapo inakaaje?"

Nikamwangalia Miryam usoni, naye alikuwa ananiangalia kwa macho yenye subira.

"Eti JC, si ni kutoka nje ya ndoa? Utatokaje ndani ya ndoa... hai-make sense," Shadya akaniambia hivyo.

Nikamwangalia na kusema, "Hapana Shadya. Miryam yuko sahihi."

"Si nimekwambia!" Bi Jamila akamwambia hivyo Shadya.

"Eeh, hata me naona kama dada yuko sahihi. Ni kutoka ndani ya ndoa, si ndiyo?" Tesha akaniuliza.

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Mmm... JC na wewe!" Shadya akasema hivyo.

"Ahahah... Kiswahili tunakikuza na kukiharibu sisi wenyewe maana maneno mengi tunayaongea kimazoea. Ukiangalia hata kwa mfano... tuseme labda mtu akaja hapa na kupiga hodi, ikiwa utasema "toka nje," ataelewaje?" nikamuuliza hivyo Shadya.

"Atajua unamfukuza," akajibu hivyo.

"Eee... ndiyo ilivyozoeleka. Lakini kwa ufasaha zaidi, unamaanisha kwamba atoke nje, aingie wapi...?"

"Ndani," Tesha akamalizia maelezo yangu.

"Umeona?" nikamuuliza hivyo Shadya.

Bi Zawadi na Bi Jamila wakacheka kidogo, naye Shadya akacheka kwa mguno.

"Miryam ndiyo ana maana hiyo. Mtu akifanya usaliti kwenye ndoa, ameenda nje ya ndoa yake, kwa hiyo anakuwa ametoka ndani ya ndoa. Umeelewa?" nikamwambia Shadya.

"Mhm... haya bwana, nyie mpeane pambe tu," Shadya akasema hivyo.

Sote tukacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Ni kweli bwana. Kwa hiyo... kama da' Mimi anavyosema, inapaswa kuwa "amekwenda nje ya ndoa," siyo "ametoka nje ya ndoa." Dah, kweli maana, huwezi kutoka nje kama tayari uko nje, au siyo? Ni lazima uwe ndani ili uende nje. Yeah, hiyo ndiyo imepafektika! Nimeipenda hii sana, ngoja niweke na status WhatsApp."

Wengine wakacheka kidogo, nami nikamtazama Miryam machoni na kukuta anatabasamu. Shadya akaanza kuridhia ukweli wa mambo, na nilipenda sana namna ambavyo hali ya kirafiki baina yangu na familia hii ilivyozidi kuongezeka hatua kwa hatua. Miryam aliponitazama na kukuta namwangalia, tabasamu lake likafifia kiasi, naye akanyanyuka na kuelekea jikoni. Nikajikuta natabasamu tu, kwa sababu ingawa sikuwa nimejenga ukaribu naye wa kirafiki zaidi, kuna haka kahali kapya ka mazoea ya mbali kalikokuwa kameanza kujijenga kati yetu, na ilinifanya nitake kukakuza zaidi ili ikiwezekana nije kuwa hata na urafiki pamoja naye. Ila huko bado palikuwa mbali sana kufika. Huyo mwanamke alikuwa wa kivyake mno, kwa hiyo alikuwa ni wa kumwacha tu. Hivyo hivyo.

Basi, muda si muda nikaanza kumwona bibie Miryam akiwa anaandaa meza upande wa 'dining' kwa ajili ya vyakula, akiweka vyombo kwa ajili yetu sote pamoja na vyakula alivyotengeneza. Akatukaribisha, nasi tukaenda na kukaa vitini ili tuyape matumbo yetu upendo. Nikapakua kwa upande wangu na kuanza kula, na aisee! Huyu dada kweli alijua kupika. Yaani vyakula vilivyokuwepo havikuwa tofauti na vyovyote ambavyo nimewahi kula lakini upishi wake ndiyo uliokuwa mpya kwenye ladha niliyopata. Wali wa nazi, maharage sijui aliyachanganyia maziwa na vitu gani, pamoja na nyama laini iliyoungwa kwa kiungo fulani kilichofanya ionekane kuwa na rangi ya kahawia iliyokoza na tamu vibaya mno. Nikamaliza zamu ya kwanza na kuongeza bila kusukumwa, na Bi Jamila alipouliza nimeonaje, nikamwambia kwa kweli nimeona. Sikumsemesha Miryam moja kwa moja lakini nikasifia upishi wake, nikisema anajua sana na wala hata haringi. Nikamwona tu akitabasamu kiasi huku akiendelea kula taratibu na kumlisha binti Mariam, akimtendea vizuri sana kwa njia fulani utadhani alikuwa kama mama yake. 

Baada ya kushiba, nikatoa shukrani na kurudi tena kukaa sofani. Tesha akajiunga nami pia, kisha wakubwa wakafata, nami nikamwona Miryam akimnawisha mdogo wake kabla ya kumleta upande wetu tena na yeye kurudi mezani kupasafisha. Sisi wengine tulikuwa tunaendelea na maongezi yenye kufurahisha, lakini sijui kwa nini tu jicho langu la pembeni lilikazia fikira zaidi upande aliokuwepo Miryam. Nadhani nilipendezwa tu na ile kuanza kumjua vizuri mwanamke huyo. Alikuwa mnyenyekevu sana. Ni yeye ndiye aliyehangaika kuiandalia familia hiyo mahitaji yao na hata kuwabebea mizigo mingi mizito, lakini bado hata kwa mambo madogo tu alijishusha na kuwafanyia pia. Katika kila 'sense,' alikuwa dada na mwanamke bora, na utu wa namna hiyo ulimfanya apendeze sana. 

Hii ikiwa ni saa nne usiku sasa, Mariam alionekana kuwa na usingizi baada ya kushiba, hivyo Bi Jamila akaongozana naye kuelekea chumbani ili wakapumzike pamoja. Shadya alikuwa amesema kwamba kwa sababu mume wake alikuwa safari na hangerudi mpaka wiki ijayo, angetumia muda huo kuwa huku zaidi, kwa hiyo hata na leo angelala hapa. Miryam akamaliza usafi na kuja tena sebuleni, naye akakaa sofa moja na Bi Zawadi na kuchukua laptop yake iliyokuwa chini ya meza ndogo hapo sebuleni, akianza kupitia mambo yake humo ya kikazi labda. Sikumaliza dakika kumi na tano baada ya hapo nami nikawa nimetoa heri ya kuaga kwa mara nyingine tena, nao Bi Zawadi na Shadya wakaipokea vizuri na kunitakia usiku mwema pia. Niliona kwamba, nilipoaga tu, Miryam aliondoa umakini wake kwenye laptop na kunitazama, kisha akaiweka mezani kabisa. Niliposimama pamoja na Tesha ili kwenda nje, mwanamke huyo akasimama pia, ikionyesha alitaka kutoka pamoja nasi pia ili labda aongee nami, hivyo nikatangulia kutoka mpaka varandani na kusimama. Tesha akatoka, kisha dada yake akafata nyuma yake. 

"Oy, wingu limetanda... sijui itashuka?" Tesha akaniambia hivyo.

Nikaangalia juu na kusema, "Yeah, inaweza ikanyesha. Angalau ianze kutuondolea vumbi."

"Na joto ndiyo liongezeke kubabake..."

Tesha aliposema hivyo, akajishtukia na kumwangalia Miryam usoni. Nafikiri alihisi hiyo "kubabake" haingesomeka vizuri kwa dada yake, na kweli Miryam akawa anamwangalia kwa njia ya kuonyesha amekerwa.

Tesha akatoa simu yake na kuvaa ndala, kisha akaiweka sikioni na kuigiza amepokea huku akisema, "Eeh oya nakusikia..."

Akalielekea gari, nami nikatabasamu na kumwangalia Miryam usoni, ambaye alikuwa na tabasamu hafifu huku akitikisa kichwa taratibu.

"Utaenda msibani kwa Joy?" nikamuuliza hivyo.

Hilo swali lilikuja ghafla tu yaani hata sijui kwa nini niliuliza hivyo.

"Bee?" akaitika.

"Msibani... kwa Joy?" nikauliza tena.

"Aaa... mimi kwenda? Sidhani. Kwanza hata nilikuwa simfahamu, na... nina mambo mengi," akaniambia.

Nikabana midomo yangu ili tabasamu langu lisionekane wazi, kwa kuwa nilichokuwa nataka tu ilikuwa ni kusikia kasauti kake kazuri, nami nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.

"Nilikuwa nataka nikuulize..." akaniambia.

"Ndiyo, niulize chochote," nikamwambia hivyo kwa umakini.

"Hayo mazoezi utakayokuwa unafanya na Mamu... ni vitu practical sana, au? Maana... mdogo wangu hayuko vizuri sana na interaction pamoja na watu asiowafahamu, so... nataka tu kujua ni approach zipi unazotaka kutumia pamoja naye, zaidi tu ya kusema kwamba mtafanya michezo," akaongea hayo.

Nilikuwa nimebaki kumtazama usoni tu, na kwa kiasi fulani nikawa nimezubaa. Sababu? Sauti yake. 

Nafikiri akawa ameona hilo, naye akauliza, "Umenielewa?"

Nikatazama pembeni kiufupi nikiwa najaribu kuisawazisha vyema taarifa ya maneno aliyotoka kusema, nami nikamwambia, "Ndiyo, nimeelewa. Yaani... nakuelewa. Najua unahangaikia hali njema ya mdogo wako, na nakuhakikishia mambo nayotaka kufanya pamoja naye hayatapita mipaka... hayatakuwa ya gusa-nikuguse, no. Kuwa na amani kabisa."

Akaangalia chini kiasi na kusema, "Sawa. Usichukulie vibaya lakini... labda hata ukafikiri nakuona kama mhuni sana."

"Ahahah... usijali, ninaelewa. Kila kitu tutakifanyia hapa hapa kwako hasa kwa sababu ni sehemu aliyoizoea, kwa hiyo atakuwa kwenye mazingira salama. Nitaanza na vitu vyepesi tu ili anizoee haraka, kisha tutaendelea na mengi zaidi. Itakuwa vizuri kama siku moja ukija kutuona pia," nikamwambia hivyo.

"Sister anatupenda mno JC, yaani hataki hata tujikwae," Tesha akadakia.

"Yeah, ni jambo zuri sana," nikamwambia hivyo.

"Mpaka kero," Tesha akatania.

Nikamwangalia Miryam usoni na kuona anatabasamu, naye akasema, "Sawa, basi... ndiyo hivyo. Nashukuru pia kwa jitihada zako japo... sikulipi."

"Ahah... ondoa shaka," nikamwambia.

Kuna kitu kilichokuwa kikinisukuma nitake kumuuliza kuhusu suala la Joshua kwenda kazini kwake ile jana, ikiwa imeingia tu akilini wakati huu ambao angalau tulikuwa tumepata mazungumzo mafupi, lakini nikaona niache tu hasa kwa sababu sidhani ingekuwa busara kumuuliza kitu kama hicho na Tesha akiwa hapo; na labda hata Miryam angeniona kuwa mfukunyuku. Sauti ya bajaji ikasikika ikifika nje ya geti na kuendelea kuungurumia hapo hapo.

"Atakuwa Ankia huyo," Tesha akasema hivyo.

"Ndiyo, halafu funguo ninazo... ngoja nimwahi," nikasema hivyo.

Nikavaa vya miguuni na kumwomba Tesha anitolee ule mfuko wa vifaa nilivyochukua hospitali leo ndani ya gari la Miryam, naye akaufungua na kunitolea. Nikamwona Ankia kupitia matundu ya ukuta akiwa upande wa geti la nyumba yake, nami nikamwambia nipo huku. Ankia alipomwona Miryam, akaamua kuja upande wetu ili aweze kumsalimia. Tesha akamfungulia mlango mdogo wa geti, naye Ankia akaenda kupeana salamu fupi za kirafiki pamoja na Miryam, kisha ndiyo tukaondoka kwa pamoja kuelekea "kwetu." Ankia alionekana kuchoka sana. Hakuwa na mpango wa kupika maana alikuwa ameshakula, nami nikamwambia kweli apumzike tu maana hata mie nilikuwa nimeshakula. Akaona uhitaji wa kwenda kujimwagia maji kisha ndiyo arudi kupumzika, nami nikamwacha aanze ili mimi nipange vitu fulani kwanza ndiyo nikajimwagie pia. 

Nikaingia chumbani kwangu. Kitu cha kwanza kabisa kufanya ikawa ni kupiga simu kwa namba ya yule askari mpelelezi ambayo dada yake Joy alinipatia huko msibani. Ikapokelewa, nami nikaanza kuzungumza na mtu huyo kwa kujitambulisha na kusema dhumuni la kumpigia. Aliitwa Ramadhan Hamisi, akiwa ni mwenye sauti yenye amri kwelikweli, na alipouliza nimepata wapi namba yake, nikamweleza kuhusu Adelina kunipatia, nikionyesha kwamba nina ukaribu na familia ya mwanamke huyo. Kwa sababu alitaka tuongee vizuri zaidi ana kwa ana, akaniuliza niko maeneo gani, na nilipomwambia Mbagala akasema sawa; kesho niende kwenye kituo cha polisi kilichopo Mbagala Maturubai sijui, nikaonane naye hapo, kwenye mida ya saa tisa alasiri. Alisema kabisa kwamba angepita huko ili ndiyo tuonane, kumaanisha labda yeye hakufanyia kazi kwenye kituo hicho, nami nikakubali tu kisha kumuaga. La kwanza hilo nikalimaliza, na la muhimu ingekuwa kutafuta eneo la kituo hicho baadaye.

La pili, ilikuwa ni kutoa vifaa nilivyochukua hospitali pamoja na dawa, kisha nikaingia mtandaoni ili kutafuta ujuzi hususa wa kutengeneza madawa fulani. Baada ya kujua mambo niliyohitaji kufanya ili zoezi nililotaka kufanikisha likamilike, nikatunza kumbukumbu fupi kwenye simu, kisha nikaweka vifaa hivyo pembeni ili kesho niamkie kwenye matengenezo hayo ya kisayansi. Dakika si nyingi naye Ankia akawa amerejea kutoka bafuni na kunishtua ili nikajimwagie pia, hivyo nikaenda kufanya hivyo na upesi kurudi ndani. Nilikuwa na mpango wa kuiwahi asubuhi ya mapema kwa kesho, kwa hiyo nilipoingia tu ndani nikafunga milango na kumtakia Ankia usingizi mnono, kisha nami nikaenda kulala.

 

★★★

 

Asubuhi ikafika kama kawaida yake. Kweli nikawa nimeiwahi mapema kama nilivyodhamiria, nami bila kutoka nje hata mara moja nikaanza kushughulika na ishu yangu ya kisayansi kabla ya mengine kufuata. Nikachukua ma-conical flask na kemikali, nikaichanganya na dawa zilizokuwepo na kutengeneza dawa ya mwanzo kwa ajili ya mchanganyiko niliotaka kuupata, kisha nikaiweka pembeni. Ilitakiwa  kuongezea na soda ya Coca cola ili mchanganyiko huu ukamilike. Kidogo tu baada ya kumaliza mchakato huo wa mwanzo, nikamsikia Ankia akiwa ameanza kufanya usafi wa ndani, nami nikatulia tu na simu yangu nikisubiri amalize ndiyo nitoke. Akawa amekuja chumbani baada ya muda mfupi na kunisalimia, akisema kuwa anataka kwenda kuemea vile ambavyo tungetumia kwa ajili ya kunywea chai na mboga kwa ajili ya usiku. Alikuwa na mpango wa kwenda msibani akishamaliza kupata kiamsha kinywa, kwa hiyo akaniaga na kuondoka. 

Nilikuwa na mipango kadhaa ya kushughulika nayo kwa leo, binti Mariam akiwa ndiyo mpango wa kwanza. Nikaamua kutoka hatimaye kwenda kujisafisha, kisha nikarejea ndani na kuvaa nguo nyepesi. Nikachukua hela, moja kwa moja mpaka dukani pale nje ili ninunue soda niliyohitaji. Wakati huu nilipofika hapo, yule mwanamke muuzaji alinisalimia kwa uchangamfu na hata kunisemesha kiasi, akiniuliza kwa nini nilipenda kukaa ndani tu badala ya kutoka hata hapo nje kuongea na wenyeji. Nikamwambia hapana, kutoka nilitoka, ila sikuwa na mazoea ya namna hiyo kwa sababu nilipotoka ilikuwa kwa ajili ya jambo fulani hususa nililokusudia kufanya; kama hivyo kuja kuchukua soda. Akacheka kidogo na kunipa soda yangu, naye akasema kwamba toka nimefika hapo na kumwokoa Mariam siku ile, nilikuwa nimewaogopesha waume za watu eti kwa kuwa wengi wa wanawake mtaani hapo walinizungumzia sana, wakitaka mazoea, lakini kwa sababu nilionekana mkali basi hawakuweza kusogea. Nikatabasamu kirafiki na kumwacha tu japo alionekana kutaka kuendeleza mazungumzo, na alionekana kuwa mbea kweli! 

Nikarudi chumbani na kurudia zoezi langu la kisayansi. Zamu hii nikawa natenganisha virutubisho fulani ndani ya soda hiyo ili nipate nilichohitaji kwa ajili ya jaribio langu. Kwa maneno mengine, nilikuwa naiondoa 'cola' kwenye soda, ili ibaki 'coca.' Kisha baada ya kufanikiwa, nikaichanganya na ile kemikali-dawa niliyoitengeneza mara ya kwanza, na mchanganyiko wangu ukawa umemalizika. Sasa kilichokuwa kimebaki ilikuwa kuikausha dawa hii, aidha kwa kuichoma na moto au ipigwe na jua, nami nikaona uchaguzi wa pili ndiyo uliofaa. Nikiwa nimeiweka ndani ya chombo chake, nikapeleka nje na kuiweka juu ya dari kabisa ili itandikwe jua kali mpaka ikauke. Nilipoangalia upande wa pili kwa jirani yetu, sikuliona gari la Miryam, hivyo nikaelewa lazima bibie angekuwa ameshakwenda kazini. Baada ya hapo nikarudi ndani na kuingia chumbani tena kuichukua simu, kukuta 'missed call' moja kutoka kwa mama yangu. Nikatabasamu kiasi na kurudi tena sebuleni, nami nikakaa sofani na kumpigia.

Alipopokea, nikasema, "Damastee..."

Sauti yake ikasikika akicheka kidogo, naye akaniambia, "Ni Namasté mwehu wewe!"

"Ahahahah... mama na wahindi bwana! Ilikuwaje ukazaliwa Tanzania na siyo Mumbai?"

"Ilikuwa kwa bahati mbaya tu..." akasema hivyo.

Nikacheka kiasi.

"Ndiyo umenigaya hivyo?" akaniambia.

"Aa wee... nikugaye wewe tena? Haiwezi tokea."

"Mm... hata kunijulia hali tu mimi mama yako jamani..."

"Sorry... mambo yamekuwa mengi kidogo."

"Mambo gani? Wakati umeenda huko kupumzika?"

Ni wakati huu ndiyo Ankia akawa amerejea hatimaye, naye akiwa ameshika mfuko mkononi, akanipita na kuelekea jikoni baada ya kuona nilikuwa nazungumza kwenye simu.

"Kuna maisha huku mama, siyo kwamba nimekaa tu muda wote. Ila pole, nimekuweka pembeni sana. Za huko?" nikaendeleza mazungumzo na mama. 

"Nzuri tu. Wewe?" akauliza.

"Fresh. Kuna vitu nafanya kidogo huku angalau na mimi najiona shujaa wa kihindi kama wa tamthilia upendazo," nikamwambia.

Akacheka kidogo na kusema, "Wewe ndiyo Amitabachani kutokea zamani sana. Najua hiyo inamaanisha unatoa msaada kwa mtu. Endelea tu hivyo hivyo kusaidia watu, Mungu anapenda sana, na atakuzidishia."

"Amen," nikamwambia.

"Umeshamwona Jasmine?" akaniuliza.

"Ee ndiyo, nimemwona juzi hapa aliweka picha zake status. Aisee amekuwa bonge!"

"Ahahaha... ni kweli. Shauri ya ujauzito, na ninamwombea sana Mungu amfanyie wepesi aje kujifungua salama."

"Ishaenda hiyo mama. Jasmine atajifungua salama kabisa, afya yake iko poa," nikamwambia hivyo.

"Sawa kabisa. Halafu... kuna kitu nilikuwa nataka nikwambie," akasema hivyo.

Ankia akawa amerejea hapo pamoja na sahani iliyowekewa chapati, na vikombe pamoja na chupa ya chai. Akaviweka mezani na kisha kuelekea jikoni tena.

"Mh? Kizuri au kibaya... maana hiyo gia uliyoiingiza naielewa hahah," nikamwambia hivyo mama kwenye simu.

"Siyo kibaya... ila sijui we' ndiyo utachukuliaje," akasema.

Ankia akawa amerejea hapo tena na kopo la kutunzia sukari na kijiko, naye akaanza kumimina chai kwenye vikombe.

"Hauhitaji kuomba ruhusa mama, we' niambie tu. Kuna nini?" nikamwambia hivyo.

"Stella alikuja hapa," mama akaniambia hivyo.

Kauli hiyo ikanifanya niondoe sura nyepesi usoni na kuwa makini zaidi.

"Alikuja hiyo juzi tu hapa nyumbani. Halafu alikuja na...."

"Mama ishia hapo hapo," nikamkatisha kwa sauti makini.

Ankia akanitazama usoni.

"J..." mama akaniita kwa sauti ya kubembeleza.

"Hapana mama... tuta... tutaongea baadaye. Ndiyo nataka kunywa chai... kuna na chapati, karibu," nikasema hivyo.

Nikamwona Ankia akitabasamu na kuendelea kukoroga sukari kwenye chai.

Niliweza kuhisi mama akishusha pumzi upande wa pili wa simu, kisha akasema, "Sawa. Ukipata nafasi utanijulisha ili tuongee. Mapumziko mema."

"Haya," nikajibu hivyo, nayo simu ikakatwa.

Ankia akasogeza meza yenye chakula karibu zaidi na nilipokaa, naye akakaa sofa moja nami na kuuliza, "Mama JC huyo?"

Nikamwangalia na kutabasamu kiasi, nami nikatikisa kichwa kukubali.

"Kwa jinsi ulivyo mzuri hivi, mama yako si ndiyo mwisho?" akasema hivyo.

"Ahahah... acha mambo yako bana. Hizi ungezileta na supu, au ulikosa?" nikabadili mada.

"Hamna, sema... hela haikutosha..."

"Aaa, unazingua. Si ungeniambia? Unajua navyopenda kula chapati na supu..."

"Basi nisamehe mume wangu... sitarudia," akaongea kwa sauti ya deko eti.

"Yaani wewe..."

Makamuzi yakaanza baada ya hapo, nami nikajitahidi kumpigisha story mwanamke huyu mbali na suala la mama yangu mzazi. Ankia alikuwa na udadisi lakini sikutaka kupita huko kwa wakati huu, kwa sababu kuna maisha niliyokuwa nimeyaacha kwa kitambo kifupi huko nyuma na ndiyo kuja Mbagala ilikuwa kwa lengo la kuishi mengine. Sababu nilizijua mimi mwenyewe na sikutaka kuzipitia tena kwa muda huu niliokuwa likizoni, na ingetakiwa kubaki kuwa namna hiyo hiyo. Labda.


★★


Kwa hiyo tulipomaliza chai, Ankia akaondoa vyombo nikiwa nimemtekenya-tekenya kiasi pia, nami nikaenda chumbani kuvaa suruali na T-shirt nadhifu ili nielekee kwa mgonjwa wangu hatimaye. Nikainywa soda ya Coca cola iliyokuwa imebaki kwenye chupa na kwenda sebuleni tena. Ankia alikuwa na mpango wa kwenda tena kule msibani hasa kutokana na kufahamiana vyema na ndugu za marehemu. Kwa hiyo nilipofika sebuleni, nikamkuta hapo, naye akawa amenipatia funguo za nyumba yake za ziada. Akasema alikuwa tu amesahau kunipa mapema lakini hii ilikuwa muhimu sana kwa nyakati ambazo tungekuwa sehemu tofauti kimaeneo, na hivyo kila mmoja wetu kuwa na funguo ingeepusha usumbufu wa kuhitaji kusubiriana. Na ilionyesha kwamba aliniamini sana. Tukaagana, nami nikatoka na kuiangalia ile dawa niliyoweka juu ya bati. Bado ilikuwa kwenye hatua za mwanzo za kukauka. Nikatoka hapo mpaka kufika nje kwenye geti la jirani yetu, nami nikagonga na kusubiri. Kidogo tu na mlango wa geti ukafunguka, ikiwa ni Tesha ndiye aliyefungua, akiwa ndani ya jezi yake ya Simba na pensi ya kijani.

"Oy, oy," akaniambia hivyo kwa shauku.

"Nakuona mkali," nikamwambia.

"Karibu bro," akanikaribisha.

Nikapita na kuingia ndani hapo, nami nikaona rundo kubwa kiasi la nguo pale varandani, pamoja ndoo na mabeseni yaliyowekewa nguo na maji yenye sabuni. Bila shaka ni Tesha ndiye aliyekuwa akifua maana mikono yake ilionekana kulowana kiasi, na kamba za kuanikia nguo tayari zilikuwa na nguo chache zilizoanikwa.

Nikamgeukia, naye akanisogelea na kusema, "Oy furushi hilo... nina miezi sijafua."

"Ahahah... ndiyo inabidi ukomae," nikamwambia.

"Ah... kufua naonaga kero kinyama. Eh, oya... yule mtoto kichaa..."

"Nani? Winny?"

"Ee. Mwana, demu anatoa zile vibe za wale wanawake wanaofanyaga kuuzia telegram sijui?"

"Ahahahah... kweli? 

"Ah, siyo poa. Jana nilikuwa namchatisha, nikawa nampanga, unajua alichosema? Eti nikitaka anipee, matunzo kwanza ni lazima, ndiyo maua atachanua!"

"Ahahah... Mbagala, tumefika Mbagala," nikamwambia hivyo kiutani.

"Ahahaaa... anaonekana anapenda sana bata, sasa me nataka nije nimmwagie laana mpaka akome!"

"Umemwelewa, eh?"

"Ah, yuko vizuri. Sema nikitaka kupanda pale ndo' kujipanga kwanza."

"Ndo' ujipange sasa."

"Nishaanza mbona... si unaona nafua?"

"Hahah... haya bwana."

"Ngoja niumalizie huu mkasa wa nguo tuje tuongee. Mamu ameshaamka, si ndiyo unataka kwenda kuanza kum...?" akaniuliza.

"Yeah, ndiyo. Mama wakubwa?" nikauliza pia.

"Wako ndani hapo. Ingia tu, nitafata," akasema hivyo.

Nikamwacha kweli akiendelea kupalangana na furushi hilo hapo nje, nami nikafungua mlango wa kuingilia ndani hapo huku nikisema, "Hodi, hodii..."

Nikawakuta mama wakubwa wakiwa wamekaa kwenye sofa walilopendelea kuketi, nao wakanikaribisha vizuri kabisa. Nikakaa sofani pia, nami nikawaamkia na wao kuniitikia vizuri tu.

"Za hapo kwenu?" Bi Jamila akaniuliza.

"Nzuri tu mama, sijui hapa?" nikamjibu hivyo.

"Kwema. Umekuja muanze mazoezi na Mamu eh?" Bi Jamila akaniuliza tena.

"Ndiyo," nikajibu.

"Yuko chumbani. Mamu... njoo..." Bi Zawadi akamwita.

"Nina hamu kubwa kuona namna utakavyomsaidia, JC," Bi Jamila akaniambia hivyo.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Ndiyo. Mdogo mdogo tu mpaka kieleweke."

"Ahahah... umemwona mwenzio anafua hapo?" Bi Zawadi akaniuliza.

"Eeh... dah! Me kufua zote kama hivyo siwezagi yaani. Anajitahidi," nikawaambia.

"Hamna, yaani Tesha mvivu sana kufua. Anarundika nguo, matokeo ndiyo hayo, anakuja kufua zikiwa nyingi," Bi Zawadi akasema.

"Ni kitu ambacho wanaume tunacho, yaani sijui kufua tunaonaje tu!" nikasema.

"Ih, kumbe hata na wewe?" Bi Zawadi akaniuliza.

"Yeah, naonaga kero kufua. Kwa hiyo huwa situnzi nguo chafu kabisa maana kwanza sipendi uchafu ukomaze nguo. Nafua kila wiki yaani zikiwa chache," nikawaambia.

"Ee hiyo ndiyo busara. Tesha angekuwa anafanya hivyo asingekuwa anahangaika na minguo ujazo," Bi Zawadi akasema.

"Kulikuwaga na kadada alikuwa anatoka nako ndiyo kalikuwa kanakuja kumfulia. Wakawa wameachana sijui, ndiyo maana sa'hivi anasota," Bi Jamila akaniambia hivyo kwa sauti yake ya kistaarabu.

Nikacheka kidogo.

"Halafu hako kadada nilikuwa sikapendi!" Bi Jamila akaniambia.

"Ih, kweli? Kwa nini sasa?" nikamuuliza hivyo kwa njia ya kuomba nipewe ubuyu zaidi.

"Kalikuwa na nyodo kupita nyodo! Yaani kuna kipindi walikafukuzaga huko kwao sijui kwa kutoelewana, ndiyo Tesha akakaleta hapa mpaka hali itulie. Sasa kalipokaa-kaa hapa, kakawa hakasikii, hata ukikaambia kafanye hivi hakataki... kanajiona kamefika sasa, yaani hakaambiliki... mpaka Tesha mwenyewe akaja kukatimua," Bi Zawadi akaniambia.

"Aisee!" nikasema hivyo.

"Kuna wakati waliwahi hadi kusemana hapa na huyu, kisa kalimtania kwamba eti amezeeka mno kwa hiyo hafai kujitengeneza kama mwanamke kijana," Bi Jamila akaniambia hivyo.

"Aaa... jamani!" nikaonyesha mshangao wa kumpamba Bi Zawadi.

Akaweka sura yake ya deko, naye akasema, "Tena siyo kwamba alikuwa anatania. Alinisema kabisa kwamba eti mimi mzee sana, kwa hiyo hata kupaka vipodozi na lipstick hainifai. Eti mimi hapa hata namzidi mama dangote umri? Mbona ye' anajipambaga? Au kwa sababu ya kuonekana mzee basi...."

"Aliyekwambia we' mzee nani?" nikamkatisha kwa hiyo kauli.

Wote wakaniangalia kwa pamoja.

"Hivi haujui ukitembea tu hata hapo barabarani unaweza ukasababisha watu wajikwae wakikuona?" nikamwambia hivyo Bi Zawadi.

Mwanamke huyo akaachia tabasamu hafifu huku akiniangalia kwa macho yaliyoonyesha furaha, na Bi Jamila akamwangalia.

"Huyo alikuwa anakuonea gere tu. Yaani wewe kama ungekuwa na ngozi nyeusi bado ungeweza kufanya hadi magaidi wasahau bunduki kwa kukutazama, sasa ndiyo umebarikiwa kuwa mweupe yaani ndiyo kabisaa! Ungewafanya hadi wasahau na vita," nikampamba namna hiyo.

Akaweka kale kasura kake ka maringo, naye akasema, "Weewe! Unasema kweli?"

Bi Jamila akacheka kidogo kwa pumzi na kuangalia pembeni.

Nikamwambia Bi Zawadi, "Siyo kwamba kwa sababu mimi ndiyo nimesema, ila ni kwamba mpaka ukweli wenyewe unajua ni kweli. We' ni Zawadi cheupe, mrembo."

"Kumbe ni kweli, alikuwa ananionea gere," Bi Zawadi akasema hivyo kwa nyodo kabisa.

"Haya JC, ndo' umeshampa na kichwa huyu. Utakuja kumkuta amevaa suruali za Mimi," Bi Jamila akaniambia hivyo.

Sote tukacheka pamoja.

"Na sisi tulio weusi, tunakaa kundi gani?" Bi Jamila akauliza.

"Wewe ni mrembo black beauty. Hata bila makeup unang'ara sana," nikamsifia namna hiyo.

Bi Jamila akacheka kidogo na kusema, "Haya bwana, ya leo kali."

Nikacheka kidogo kwa kufurahia maongezi yetu haya yaliyokuwa yanaongeza zaidi mazoea. Bi Zawadi alipenda sana hali ya urembo kama mwanamke kijana, na inaonekana alipenda kusifiwa kwa kuwa alikuwa na mwonekano mzuri japo alikuwa na umri mkubwa. Akawa amemwita Mariam kwa mara nyingine tena, naye binti akaja sebuleni hapo baada ya sekunde chache. Alikuwa amevaa dera, nywele zake ndefu zikiwa zimesukwa kwa mtindo wa Yebo rasta fupi, na mkononi alishikilia mdoli wenye kufanana na paka. Mama zake wakubwa wakamwelekeza aje kukaa kwenye sofa nililoketi, naye akaonyesha kukubali japo kwa njia ya kujihami na kuja kukaa pamoja nami. 

Nikaanza kumsemesha vitu ambavyo nilijua asingejibu, nikimwambia mambo mengi kwa njia ya kirafiki na kwa uchangamfu ili mazoea yaanze kweli kujengeka. Nikaanza kufanya michezo rahisi ya watoto pamoja naye, nikijaribu kumfundisha na kumkaririsha kwa kuirudia-rudia, na mama zake wakubwa walikuwa wananiunga mkono sana kwa kujumuika pamoja nasi. Mariam akaanza kujiachia zaidi kwangu. Alipenda michezo ya 'shuadina' na 'mapera' zaidi kwa kuwa ilichezwa kwa kuimba, na tabia yake ya kupiga-piga makofi kila mara alipocheka ilionyesha furaha ya kina ndani yake. Hakuwa na maneno hususa ya kuzungumza kila mara nilipomjaribu kwa kuuliza jambo lolote upesi ili nilazimishe furaha yake imsukume aongee. Lakini najua uwezo wa kuongea vizuri ulikuwepo, sema kwa wakati huu ulikuwa umefungwa, hata mara ya kwanza mimi kuja hapa niliita jina lake bila kukusudia na yeye akaitika kabisa, na shikamoo aliweza kuisema vizuri kabisa, kwa hiyo ndiyo ningetakiwa kuwa na subira ili mazoezi haya yaje kutia tiki mbele zaidi ya hii safari. 

Tukaendelea kucheza ndani hapo, huku Tesha akija ndani mara kwa mara pia na kurudi tena kufua, na Bi Zawadi akaanza kutengeneza chakula cha mchana ilipoingia mida ya saa sita. Wakati huu, nikawa pamoja na Mariam upande wa 'dining,' akiwa ameleta makopo yake na vijiti ili anifundishe kupika wali. Alikuwa amechukua na mchele kabisa, akiniongoza mwenyewe ili nisije kuunguza na mboga ya majani kwenye kopo lingine, naye Bi Jamila akawa anatutazama tu huku akicheka. Mariam alianza kunizoea upesi sana kiasi kwamba akafata mtandio chumbani na kuja kunifunika nao kichwani; sababu ikiwa kwamba na mimi ni mwanamama mpishi kwa hiyo lazima nionekane kuwa kama maman'tilie kabisa! Nami kweli nikauvaa na kuendelea kuigiza pamoja naye. Vitu nilivyokuwa nafanya hapo ndani viliwafurahisha sana mama zake wakubwa, na Mariam mwenyewe alikuwa makini kweli kwenye kuhakikisha mapishi yake "yanaiva."

Tukiwa tunaendelea na mambo yetu pamoja na binti, Tesha akawa ameingia ndani tena, lakini wakati huu pamoja na bibie Miryam. Sikuwa nimetegemea kabisa kumwona hapo muda huo, naye akamwamkia Bi Jamila na mwanamama huyu akaitikia huku akisimama kutoka sofani. Miryam hakuwa ameniona kutokea sehemu aliyokuwa amesimama, nami katika kubaki nimemtazama, nikajisahau kwa kuwa niliondoa umakini wangu kwa binti Mariam. Alikuwa akiniita kwa ishara za mikono ambazo niliziona, lakini sikuzipa umakini kwa muda huo mfupi, ndipo akanipiga begani kwa nguvu kiasi. Nikamwangalia kwa kushangaa kidogo, nikalishika bega kuonyesha nimeumia, naye akawa ameweka sura ya kununa. Nikaweka uso wa kununa pia na kutazama pembeni, kwa njia ya utoto ili iendane na yake pia.

Bi Zawadi akatoka sehemu ya jikoni baada ya kusikia Miryam akiongea hapo, naye akafikia sebuleni na kumuuliza, "Mimi, vipi? Mbona umewahi, unaumwa au?"

"Hapana, nilikuwa nimeenda hapo Kongowe mara moja, ndiyo nikaona nipite. Shikamoo?" Miryam akaongea hivyo.

"Marahaba mama," Bi Zawadi akamwitikia.

"Za hapa?" Miryam akasema hivyo.

Wakati akiwa anajibiwa, Mariam alikuwa akinivuta mkono ili niendelee kupika pamoja naye, lakini nikamwonyesha kwamba nimenuna bado. Akaniacha na kwenda upande wa dada yake.

"Na Mamu amekula?" Miryam akauliza.

"Eee, chai kanywa. Huyu hapa, yuko na...." 

Kabla Bi Jamila hajamaliza kuongea, Mariam akawa amemfikia dada yake na kuanza kuivuta nguo yake kwa chini huku akimwangalia kwa njia ya kukwazika. Nikaelewa tu kwamba hapo binti alikuwa anataka kunisemea, nami nikabana tabasamu langu na kuendelea kujifanya nimenuna. 

"Nini Mamu? Umekuwaje?" Miryam akamuuliza kwa kujali.

Nikamwona Mariam akinyoosha kidole chake kuelekea upande wangu, nao wote wakaniangalia. Ilimbidi Miryam achungulie kiasi ili aweze kuniona, naye akaniona nilivyokuwa nimejifunika kichwa kwa mtandio huku nikionyesha madoido ya kununa. 

Wengine wakaanza kutabasamu, naye Miryam akakunja uso wake kimaswali na kuniuliza, "Wewe... ndiyo unafanya nini sasa?"

Nikiwa naendelea kuigiza kimaringo, nikamwambia, "Usinisemeshe... nimenuna."

Bi Zawadi, Bi Jamila, pamoja na Tesha wakacheka kidogo na kumwangalia Miryam, naye bibie akaonekana kutonielewa vizuri na kuwatazama kimaswali.

"Wameanza kucheza na Mamu," Tesha akamwambia hivyo.

Miryam akamtazama Mariam, naye akasema, "Mamu... usiwe hivyo... kwani mmefanyaje? Mbona amekasirika?"

Nikamwangalia Mariam na kuona kweli alionyesha hisia za kuumia, nami nikatabasamu tu. Hilo kwangu lilikuwa goli la kwanza kuelekea kwenye ushindi. Binti akachukua mdoli wake na kuelekea chumbani, akionekana kukasirika kweli. Miryam alionekana kuchanganywa sana na jambo hilo, naye akanitazama usoni tena kwa umakini. Nikatoka hapo nilipokuwa nimekaa na kuutoa mtandio kichwani, nami nikaenda waliposimama wenzangu.

"Za saa hizi dada?" nikamsalimu Miryam.

"Unafanya nini we' kijana? Umesema unataka kumsaidia mdogo wangu lakini nakuja kukuta unataka kumliza?" Miryam akaongea kwa hisia kali kiasi.

Tesha na mama wakubwa wakawa makini zaidi, nami nikasema, "Hapana Miryam... siyo unavyodhani."

"Ila nini? Me sitaki mdogo wangu ajazwe presha ya aina yoyote, nilikwambia ni ngumu kwake kwa watu ambao hajawazoea. Hii michezo haimpi faida yoyote, sioni ikimsaidia, kwa hiyo kama ni sawa kwako... nakuomba uache," akaniambia hivyo.

Wengine wakabaki kututazama kwa utulivu baada ya Miryam kuniambia hivyo. Sijui ikiwa alitibuliwa huko Kongowe alipotoka ama labda tu alikuwa na hasira kunielekea isiyoeleweka sababu yake, lakini njia aliyotumia kunisemesha ilionyesha kwamba alimjali sana Mariam; yaani kupita kiasi, kiasi kwamba angekuwa tayari kuondoa jambo lolote lile ambalo lilisababisha mdogo wake huyo aumie bila kujali nani wala nini. 

Lakini bado hakuwa ameelewa vizuri nilichokuwa nakifanya, kwa hiyo nikaweka uso makini pia na kumwambia, "Hapana. Siyo sawa kwangu... kwa hiyo siwezi kuacha."

Kauli hiyo ikafanya wote waniangalie, kwa sababu ilianza kuonekana kuwa mabishano baina yangu na dada mtu. Hali ikageuka kuwa nzito baina yangu na mwanamke huyu, naye akanikazia macho kana kwamba alikuwa na hasira kali sana na mimi.

 

★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next