MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA SABA
★★★★★★★★★★★★★★★★
Tesha akaona aingilie kati. "Mimi, hakuna presha wala, ndiyo wameanza tu, kwa hiyo...."
Miryam akanyanyua kiganja chake kumkatisha. "Unataka kusema nini?" akaniuliza hivyo.
"Mtoto hawezi kuanza kutembea kabla hajasimama Miryam. Na akianza kusimama, kudondoka mara kwa mara ni lazima. Lakini atatembea tu. Huoni kwamba Mariam ameonyesha kudondoka sasa hivi nilipokuwa namfundisha kutembea tena?" nikamwambia hivyo.
Miryam akabaki kunitazama tu usoni.
"Una maana gani baba?" Bi Jamila akaniuliza.
Nikamwangalia na kusema, "Tulikuwa tunacheza... nikaigiza kununa. Ameonyesha anayajua maumivu ya kihisia kwa sababu ya mimi kumnunia kwa hiyo akamfata dada yake kunisema. Japo hajaongea, lakini amenisonta kabisa, si ndiyo?"
"Eeh... ni kweli!" Tesha akasema.
"Alishawahi kufanya kitu kama hicho... toka ameanza kuumwa?" nikawauliza.
"Ha..pana... sijawahi kuona. Eti?" Bi Zawadi akasema hivyo.
"Hata mimi sijawahi kumwona hivyo. Anacheza kama mtoto lakini... anune? Amfate Miryam kusema? Ahah... eh Mungu... hiyo inamaanisha nini JC?" Bi Jamila akaongea kwa matumaini.
"Inaonyesha amenizoea haraka... na akili yake ya kuelewa hisia inavizia," nikamwambia hivyo na kumtazama Miryam.
Tesha akamsogelea dada yake na kumshika mabegani huku akisema, "Sasa je! Si unaona Mimi? JC ni hatari! Mamu ashaanza kutoa cheche, fire linakuja. Oya... nakubali sana."
Miryam akawa ananiangalia kama vile bado hajaniamini.
"Wala hata usifikiri kila siku nitakuwa nakuja kumkwaza tu... ila sasa na wewe nisaidie kwenda na muziki," nikamwambia hivyo Miryam
"Kwendaje na muziki?" Miryam akaniuliza hivyo.
"Unamfata, unamdekeza kidogo, halafu akija kuniona tena tunaendelea na michezo yetu. Taratibu tu Miryam... wala usiogope dada. Taratibu," nikamwambia hivyo kwa njia ya kirafiki.
Lakini kiukweli, alikuwa amefanya mapigo yangu ya moyo yakimbie kwa kasi sana, nisielewe sababu kuwa aidha kumhofia yeye ama tu kuhofia kumwacha Mariam bila msaada. Hii kitu ikawa mpya sana kwangu maana kuogopa halikuwa jambo lililo ndani ya mfumo wangu kabisa. Mwanamke huyo akashusha pumzi ya utulivu, na ndiyo hapa nikawa nimepata nafasi ya kumwangalia vizuri zaidi. Alikuwa amevaa shati la kike la satini, lenye rangi nyekundu mchanganyiko na nyeupe kwa mtindo kama wa kumwagiwa rangi bila mpangilio, na kwa chini alivaa sketi ya blue-bahari iliyoishia magotini na kuiacha wazi miguu yake myeupee. Kichwani alikuwa amezilaza nywele zake ndefu kuelekea nyuma, huku mbele akiacha chache pembeni ya paji la uso wake. Na nakazia hili. Alikuwa mrembo sana!
Akaniangalia na kusema, "Sawa. Samahani nime..."
"Wala hata usiseme samahani. Kwani kuna mtu alijua ungekuja muda ambao nilitaka kumnunisha Mamu kwa makusudi?" nikaongea kiutani.
Mama wakubwa wakacheka kidogo, na ni hapa ndiyo simu yangu ikaanza kuita kutokea mfukoni mwa suruali. Nikaitoa kukuta mpigaji ni mke wake Chalii Gonga. Nikaitolea sauti na kuirudisha mfukoni upesi.
"Yaani ungekuwepo Mimi! Ungependa sana. JC ana vituko," Bi Zawadi akamwambia.
"Noma sana. Oy, si bado mnaendelea au Mamu kazira kimoja?" Tesha akaniuliza.
"Nitaishia hapa kwa leo. Angalau nimetikisa nyuzi ndogo," nikamwambia.
"Natamani hata mwendelee," Bi Zawadi akasema hivyo.
"Mimi... kaa basi, nanii... Zawadi anakaribia kuivisha," Bi Jamila akamwambia Miryam.
"Hapana mama... nahitaji kwenda dukani. Sijaingia huko tokea asubuhi," Miryam akamwambia.
"Ulienda Kongowe kufanya nini?" Tesha akamuuliza.
Miryam akatulia kidogo, kisha akasema, "Ni... kwa rafiki. Na... masuala ya kazi pia."
Nikamwangalia kwa uangalifu na kutambua kwamba alikuwa anadanganya ama kuna kitu tu alikuwa anaficha, na hakuwa mwongo mzuri sana huyu mwanamke japo kwa sababu watu wake wa familia walimwamini basi hilo halikuonekana wazi.
"Ngoja nikamwone huyu halafu ndiyo niende huko," Miryam akasema hivyo, akimaanisha kwenda kumwona Mariam.
Mama wakubwa wakakubali, naye Miryam akaniangalia machoni kwa njia ya kawaida. Nikampa tabasamu dogo la utakatifu, naye akanipita na kuelekea chumbani.
"Nimemaliza kufua. Nataka nikaoge, kaa sasa hapa kaka tu..."
Tesha akiwa ameanza kusema hivyo, nikamkatisha kwa kumwambia, "Hapana, ninaondoka sasa hivi. Kuna sehemu nilikuwa nimepanga kwenda."
"Ah... wapi nawe JC? Acha kuzingua..." Tesha akaniambia hivyo.
"JC, mbona ghafla? Na ndiyo namalizia kupika jamani..." Bi Zawadi akasema hivyo kwa kubembeleza.
"Usijali mrembo wangu, msosi nitakuja tu kuula. Sema... nilikuwa nimepanga kwenda sehemu hii saa saba, na ni suala la kikazi," nikamwambia hivyo Bi Zawadi.
"Eh! Bro? Ma' mkubwa kageuka mrembo wako lini tena? Tesha akaniuliza hivyo.
Sote tukacheka kidogo, naye Bi Zawadi akamwambia, "Usingekuwa unatunza minguo mingi sana ya kufua, ungejua."
"Poa basi. Kwa hiyo... vipi baadaye?" Tesha akaniuliza.
"Tutaongea. Ngoja niwahi, maana muda ushaanza kwenda. Asanteni warembo wangu, tutaonana baadaye," nikaaga na kuelekea mlangoni.
Mama wakubwa wakaniaga kwa shauku yao ya kiutu uzima, nami nikatoka kwao upesi na kuelekea upande wa nyumba ya Ankia. Nikakuta geti likiwa limefungwa kabisa, hivyo nikatoa funguo na kuanza kulifungua huku simu ikiwa sikioni nikiwa nimempigia huyo mwanamke ili tuongee. Ikiwa wazi kwamba Ankia alikuwa ameshaondoka, nikaelekea tu mpaka ndani bila ya jaribu langu la kwanza kumpigia huyo mwanamke kufanikiwa, nami nikarudia kwa mara nyingine tena. Hakupokea kabisa, kwa hiyo nikaamua kwenda nje tena kuichukua ile dawa niliyoweka darini na kurudi nayo ndani. Kichupa hicho kilikuwa cha moto mno kutokana na kuunguzwa haswa na jua, na dawa ile ikawa imekauka. Haikuwa na utofauti sana kama tu kuanika viazi mpaka vinapokauka na kuwa vyeupe. Isipokuwa tu haya yalikuwa ni madawa, na kukauka huku kukayafanya yawe na ule ukavu uliokithiri kiasi kwamba kama ungeyashika na kupekecha vidole, yangepukutika kabisa na kuwa kama unga. Ndiyo. Unga! Nikayatoa kwenye hicho kifaa na kuyaweka kwenye kingine ili yapoe, kisha nikaanza kuyapukutisha kwa makusudi ili kweli yawe unga. Wakati nikiwa nafanya hivi, simu ikaanza kuita, na kwa uhakika ilikuwa ni mtarajiwa wangu; mke wa Gonga.
Nikaweka simu sikioni baada ya kupokea, na kabla sijasema lolote, sauti ya mwanamke huyo ikasikika ikisema, "Njoo Royal Village Hotel. Ndani ya saa moja uwe umeshafika."
Ka!
Nikamuuliza, "Royal Village ya wapi... Makumbusho? Sinza?"
"Acha maswali. We' si mjanja? Njoo," akasema hivyo.
"Okay sawa, haina shida. Lakini... huo muda dear. Niko Mbagala, unajua ni mbali na usafiri sometime unaweza ukazingua, bora kama ungekuwa umeniambia mapema," nikamwambia hivyo.
"Wewe njoo Royal Village. Ukifika niambie," akasema hivyo.
"Yes madam," nikamjibu hivyo kizembe.
Akakata simu.
Nikacheka kidogo kwa mguno, kwa sababu nilijua vizuri kile ambacho nilikusudia kufanya, na angalau mambo yalikuwa yakienda kwa jinsi nilivyotaka yaende kwa mwanzo huu. Nikaingia chumbani na kujitengeneza vyema zaidi, uzuri nilikuwa nimeshaoga, kwa hiyo nikavaa jeans yangu nyeusi pamoja na lile T-shirt jipya kabisa nililonunua majuzi nimeenda Kariakoo, nami nikavaa na viatu vyangu vyeupe. Nikatia kacha aliyoninunulia Tesha pamoja na saa yangu kali mkononi pia. Hapo nikawa poa. Nikaiweka dawa ile kwenye kifuko kidogo na kukikunja vizuri kabisa, ndwii mfukoni.
★★
Safari ya kwenda kuitafuta hiyo Royal Village ikaanza baada ya kuondoka hapo. Watu kunikazia macho lilikuwa jambo la kawaida, kwa hiyo mpaka kupanda daladala za kwenda Rangi Tatu na kupanda za kwenda Makumbusho hadi kufika huko yaani ni kama nilikuwa nimeshibishwa kwa kutazamwa. Usafiri haukuwa wa tabu mno kwa muda huo na kwa hilo nikashukuru Mungu, sikuwa nimechelewa sana; saa tisa tu na nusu nikawa Makumbusho tayari. Kwa hiyo kama ilivyo ada, hapo kilichokuwepo ilikuwa kuita Uber ili nifike upesi kwenye hoteli aliyonitaka nifike mrembo wa Chalii Gonga, na hilo sikulikawiza. Nikabofya kwa simu yangu kutafuta "Uber driver," na mmoja akawa amefika sehemu niliyokuwa nikimsubiri nje kidogo ya stendi ya Makumbusho. Nikapanda, ikiwa ni IST ya silver, na mwendo ukaanza. Hoteli ya Royal Village ikaonekana kuwa karibu kutokana na mwendo wa haraka wa usafiri huu, nami nikafikishwa kwenye malango ya jengo hilo refu lenye maghorofa mengi na kushuka baada ya kulipa.
Nikaelekea ndani huko, kukiwa na eneo pana lenye mandhari maridadi sana. Watu walioonekana walijiwekea mionekano yenye hadhi ya juu, magari yalikuwa mengi na ya kifahari, nami nikaishia kwenye mti mmoja ufananao na mnazi na kutoa simu yangu. Nikampigia mke wake Chalii Gonga mara mbili bila ya yeye kupokea, nami nikaona nitulie kwanza. Kwa ufahari wa hoteli hii kwa kiasi chake, inaonekana huyu mwanamke alikuwa anataka tu kunionyesha kwamba yeye ni wa gharama sana, ama kuna jambo lingine lililokuwa likiendelea hapo lililofanya ndiyo iwe sehemu ya kuniitia. Kwa vyovyote vile, ningepaswa kuwa makini kwa kile nilichotaka kufanya, kwa sababu nilikuwa nimekuja hapa kama mtu mwingine kabisa tofauti na nilivyokuwa kihalisi.
Nikaiacha sehemu hiyo niliyosimama na kwenda upande wa ndani wa jengo hilo, na kama ilivyo kawaida ya hoteli kubwa, hapa pia palikuwa na mwonekano maridadi sana. Watu wengi walikuwa sehemu kwa sehemu wakifanya mambo yao, nami nikatumia muda mfupi kutalii huku na kule. Bado tu mke wa Chalii hakuwa amenipigia, hivyo nikajaribu tena kumtafuta bila ya kupata fanikio. Nikiwa nimeamua kutafuta sehemu ya kukaa kwa muda mfupi ili kusubiri ndiyo mwanamke huyo akanipigia. Nikapokea.
"Umefika?" akasikika.
"Ee, uko wapi?" nikamuuliza.
"Njoo ghorofa ya saba. Ingia room namba 101," akasema hivyo.
"Ndiyo nitakukuta humo?" nikamuuliza hivyo.
Simu ikakatwa. Khh!
Hakutaka mazungumzo marefu, au siyo? Nikaona isiwe kwere, nami nikaelekea kwenye milango ya lifti kuchukua lifti. Hoteli hii ni kubwa na pana sana, yenye maghorofa mengi yenye vyumba, kumbi, na huduma za gharama. Nikaingia na kukutana na mwanadada mweusi aliyevaa hijab, akionekana kuwa mfanyakazi hotelini hapo maana alivalia suti nyeusi ya kike pamoja na kitambulisho alichovaa shingoni mpaka kufikia kifuani.
Nikamwambia, "Habari yako?"
Akajibu, "Salama tu."
Alionekana makini sana, nami nikabonyeza kitufe cha namba ili lifti iendelee kupanda mpaka kufikia ghorofa ya saba. Sikumsemesha tena mwanamke huyo na wala hatukuangaliana, lakini ghafla tu akanyoosha mkono wake kwa chini kunielekea. Nikauangalia na kukuta umeshikilia kadi kwenye vidole viwili, yenye rangi ya shaba iliyo na ufanano na kadi za benki, nami nikamtazama usoni. Hakuniangalia hata mara moja, akiwa na uso makini kweli, nami kwa haraka nikawa nimetambua kwamba huyu alikuwa ametumwa.
"Nini?" nikamuuliza hivyo.
"Shika. Utafungulia mlango," akanijibu hivyo bila kuniangalia.
Nikatulia kidogo nikitazama kadi hiyo, kisha nikaipokea. Lifti ilipofika ghorofa ya tano, milango ikafunguka, na mwanamke huyo akatoka. Wakaingia watu wengine pia waliotaka kuelekea juu zaidi, nami nikabaki nikimuwaza huyo mtu aliyetumwa anipe hii kadi/funguo. Sijui hata alijuaje kwamba ningeingia kwenye lifti hiyo! Kwa vyovyote vile, haya maigizo ningesonga nayo hivyo hivyo mpaka nifike kule nilikotaka kufikia, nami kweli nikawa nimefika ghorofa la saba. Nikatoka na kutembea kuelekea korido, nikipita vyumba na kuangalia namba milangoni.
Nikiwa natembea nikatoa simu yangu na kuiweka katika mfumo fulani maalumu, kisha nikailaza na kuiweka mfukoni tena. Nikawa nimefika chumba namba 101. Hapa hapakuhitaji hodi maana funguo nilikuwa nimekabidhiwa. Ilikuwa kama kuingia chooni tu. Nikapitisha kadi ile pale ilipotakiwa kupitishwa, na mlango ukatoa sauti ya kufungua lock. Nikausukuma na kuingia ndani humo nikiwa makini sana, nami nikakuta mazingira yenye kutegemeka lakini kwa asilimia kadhaa tu.
Chumba hicho kilikuwa na mwonekano mzuri kutokana na vifaa vingi vya gharama na mpangilio wake safi, na ndani hapo nikakutana na sura mbili. Moja niliifahamu, nyingine ilikuwa ngeni. Niliyoifahamu ilimilikiwa na mke wake Chalii mwenyewe, Bertha, ambaye alikuwa ameketi kwenye sofa ndani hapo kwa kukunja nne kama malkia vile. Alikuwa amevaa nguo kama gauni lenye rangi ya kijivu lililoishia mapajani, lililoubana mwili wake kama linautesa, likiacha miguu yake myeupe wazi mpaka kufikia chini alikovaa viatu vya kuchuchumia vyenye rangi nyekundu.
Wakati huu alikuwa amesuka nywele za rasta nene ambazo aliziachia zimwagikie mgongoni, na lipstick yake nyekundu ilipendezesha sana mdomo kwenye huo uso wake. Na alimfanana kweli Rose Ndauka. Pembeni yake alisimama mtu mwingine, mwanaume mwenye mwili mkubwa na mpana sana wa mazoezi. Alikuwa mweusi, mwenye ndevu nyingi kutokea kwenye timba mpaka kidevuni. Alivaa nguo kama mwanajeshi fulani hivi, nami nikapata picha kwamba jamaa alikuwa ndiyo bodyguard wa bibie.
Nikaingia tu kitakatifu na kuanza kuwafata, lakini baunsa akanionyesha ishara ya kiganja kwamba nisimame. Nikatii. Mwanaume huyo akanifuata na kunifikia karibu zaidi, naye akaanza kunipekua mwilini kwa kupapasa, naye akatoa simu yangu mfukoni pamoja na kile kimfuko nilichokuwa nimewekea ile dawa. Akavitazama kwa umakini na kuniangalia.
"Hayo ni madini kaka. Ikiwa unaelewa. Kila mtu ana yake, au siyo?" nikamwambia hivyo kwa ujasiri.
Akawa ananitazama kwa umakini sana, kisha akarudisha vitu vyangu mfukoni na kumgeukia malkia.
"Yuko safi," jamaa akamwambia hivyo kwa sauti ya besi nzito.
Bertha akasimama taratibu, na ni hapa ndiyo nikawa nimetilia maanani uwazi wa duara katikati ya kifua chake uliofanya kionekane kwa juu, na jinsi nguo hiyo ilivyokificha kwa chini ilikuwa kama vile imekibeba nusu kidogo tu kuangusha balaa kama uwazi huo ungeachia kidogo. Akatembea kwa mbwembwe kiasi kunielekea, akiwa ameunganisha vidole vyake usawa wa tumbo vyenye makucha marefu yaliyopakwa rangi ya blue-bahari, naye baunsa wake akasogea pembeni mwanamke huyo aliponikaribia.
"HB wa Masai huyo! Inaonekana unapenda kujiweka vizuri sana," Bertha akaniambia hivyo.
"Asante, ila siyo zaidi yako. Unajua sana kupendeza," nikamwambia.
"Mwingi sana wa maneno we' mtoto. Haya... sema haraka ulichomaanisha kwenye simu jana. Nina mambo mengi ya kufanya," akasema hivyo.
"Sawa. Kwanza... nataka kuomba radhi kwa...."
"Kwa kuniita mjinga?" akanikatisha.
"Aa.."
"Tena hicho ni kidogo, hadi ukathubutu kunitukana kwa kusema nitakalia chupa ya moto. Unakumbuka?" akaniuliza hivyo kwa sauti tulivu.
"Bertha... naomba tu..."
"Usilitaje tena jina langu, mbuzi wewe!" akaniambia hivyo kiukali.
"Samahani. Naomba unisamehe," nikaweka upole.
"Unajua kwamba ninaweza kukufanya jambo baya sana na hakuna mtu atakayekusaidia?"
"Ndiyo. Naelewa," nikamwambia.
"Hapana. Hauelewi. Haujui umegusa wapi we' mtoto. Nipe sababu nzuri... moja tu... yaani moja tu ya ni kwa nini nisiukate ulimi wako hapa sasa hivi kwa kunitukana namna ile," akaongea kwa hisia kali.
"Ndiyo maana niko hapa Be... aa... boss. Ndiyo maana niko hapa. Sitaki kugusa upande wako mbaya maana nimeelewa sasa kwamba una nguvu sana boss... sina... sitaki yaani unifanye niwe adui kwako... boss," nikajing'atang'ata kwa makusudi.
Akacheka kidogo na kumwangalia baunsa wake, ambaye naye alikuwa anatabasamu kibabe, kisha akanitazama na kusema, "Eti boss. Nani boss wako hapa? Unanifanyia kazi gani mimi we' mtoto wa mwanamke malaya?"
Nikainamisha uso, nikiwa nazuia hisia zangu za hasira kutokana na maneno yake, na ikiwa angethubutu tu tena kunirushia kashfa ya namna hiyo, ningebadilika hapo hapo haijalishi matokeo.
"Si ulikuwa unajiona mjanja? Mbona umekuja kunipigia magoti sasa?" akaniuliza hivyo.
"Kama nilivyosema... sitaki niwe adui yako. Nimejifunza. Na... najua unamkubali sana Gonga... kwa sababu zako wewe mwenyewe, maana mnajua mlikotoka na vitu mlivyoshare... ila me naweza kukupa vitu vizuri zaidi ya vile anavyoweza kukupa. Na siongelei pesa," nikamwambia.
Akatulia kidogo, kisha akauliza, "Ila?"
Nikamsogelea karibu zaidi na kusema, "Vibe."
Akacheka kwa mguno, kisha akauliza, "Sasa wewe utanipa nini mimi ambacho sijawahi kupata, ama kufanyiwa labda? Unafikiri hako kasura kako kananihangaisha mimi?"
"Usinichukulie poa kwa sababu ya sura yangu. Nikikwambia naweza kukupeleka high kuliko hata kwa msisimko unaopata kwa heroin je?"
Sura yake ikageuka kuwa makini kiasi, naye akauliza, "Una maana gani?"
"Niruhusu nikuonyeshe."
"Nionyeshe, kwani we' unaogopa nini? Nionyeshe kama we' mwanaume kweli," akaniambia hivyo kwa mkazo.
Nikatabasamu tu, na nafikiri kwa sababu ya mimi kutabasamu akadhani nilikuwa namfanyia masihara, kwa hiyo akaudhika na kuikaba shingo yangu kwa kiganja chake.
"Unataka kucheza na mimi, si ndiyo?" akaniongelesha kiukali.
"Tulia. Usiwe na papara. Si unataka nikupe?"
"Ni nini hicho... nionyeshe..."
Nilikuwa namwangalia tu kwa macho makini, nikiona namna ambavyo suala la madawa lilimfanya awe dhaifu sana, nami nikaona niache kumtesa. Kutoka kwenye mfuko wa suruali yangu nikakichomoa kile kimfuko nilichokuwa nimeweka ile dawa, nami nikakiinua mbele ya uso wake, na macho yake yakakitazama kwa mkazo.
"Nini hiki?" akaniuliza.
"Hii ni coke," nikamwambia hivyo.
Akanitazama usoni kwa umakini na kuniachia shingo. "Coke? Cocaine?" akauliza kwa sauti ya chini.
"Ndiyo. Na una makucha marefu boss! Shingo imekwanguka hapa," nikamwambia hivyo kwa kujiamini.
"Wewe... umetoa wapi hii?" akaniuliza.
"Nimeitengeneza," nikamwambia.
Akionekana kutoniamini, akauliza, "Umeitengenezaje?"
"Kama nilivyokwambia... me ni mjanja," nikasema hivyo.
Akakishika kimfuko hicho na kukiangalia kwa umakini, kisha akasema, "Hii siyo coke wewe. Na kama ni coke basi kuna sehemu unatoa. Niambie ni wapi, usijichetue eti umetengeneza. Umeinunua kwa wakala gani?"
"Najua bado huamini ila hii ndiyo point ya mimi kuja hapa."
"Kwamba utakuwa unaniuzia coke?"
"Hapana. Kwamba nitakuwa nakutengenezea coke nzuri sana bila gharama yoyote. Ndiyo faida niliyokwambia ningekupa ukiniweka upande wako," nikamwambia hivyo.
"Ahah... nani anakupa mawazo kwamba nina upande wowote ambao naweza nikakuweka wewe? Na ni nani aliyekupa wazo ufikiri kwamba nafagilia hivi vitu?"
Nikaweka uso makini, nami nikamwambia, "Nina akili pia Bertha. Nimeshakuelewa. Najua una mambo kubwa, na mimi hapa... bado niko chini chini, ndiyo maana kuwa na watu wakubwa kama wewe najua itanipa faida kama ambazo na we' nataka upate. Nina mwonekano mzuri, eh? Nina mvuto yaani halafu najua sasa kutengeneza vibe la ukweli kama hili. Nipe tu nafasi, nitakufanyia manuva, huwezi amini."
Akabaki kuniangalia kwa mkazo kiasi, kisha akasema, "Kilichokubadilisha ghafla ni nini?"
"Sihitaji mpaka kusomewa manual kuelewa maana ya kilichompata Joy. Unajua jinsi ya kutia tiki maneno yako aisee, na umetisha sana... salute. Sitaki tu na mie yanikute kama hayo ndo' maana nimejileta mapema kutoa dhabihu," nikamwambia hivyo.
Akatabasamu kwa njia ya kuhukumu, kisha akapiga hatua chache kukielekea kitanda huku akiyatazama hayo madawa kama vile amepata madini.
"Unaogopa sana kufa eh?" akauliza hivyo yule baunsa.
"Ah kufa najua nitakufa, ila sitaki kufa kama mlivyom...."
"Ishia hapo hapo," Bertha akanikatisha.
Nikatulia.
"Sitaki tena kukusikia unaongelea suala la huyo mwanamke, unanielewa?"
"Ndiyo, nimeelewa," nikamjibu.
"Wewe... ahah... una bahati sana. Yaani kwa jinsi ulivyonisemesha sjku ile nilikuwa nimepanga nikufanyie kitu kibaya zaidi ya nilichokifanya kwa huyo mwanamke. Ila naona akili imekusogea ingawa moto sikuwa nimekuwashia bado," akaniambia hivyo.
"Na ni kweli, akili imenisogea. Sitarudia. Nisamehe tena," nikamwambia.
Akanitazama usoni kwa umakini, kisha akasema, "Njoo hapa."
Nikamfata mpaka kufikia aliposimama, huku baunsa wake akiwa ametulia tu pembeni akituangalia.
"Nipe uhakika kwamba hii kitu ni OG," akaniambia hivyo huku akinionyeshea hayo madawa.
"Hauwezi kujua kwa kuambiwa. Ni tamu balaa, lakini ndo' mpaka uonje. Nilichofanya kuitengeneza ni project moja kali sana, na nimeiongezea madini kuifanya iwe nzuri kuliko kawaida. We' mwenyewe utaona," nikamwambia hivyo.
Akawa ananitazama kwa yale macho makini, na yule baunsa wake akasogea karibu nasi na kuniuliza, "Umeiwekea madini gani labda? Sumu?"
Nikatabasamu kidogo na kufungua kiganja changu kumwelekea Bertha, nikiwa namwomba anipe dawa hiyo, naye akanipatia. Nikaifungua kwa uangalifu na kisha kulamba kidole changu kimoja kidogo, halafu nikachovya kwenye hiyo dawa na kisha kuiweka ulimini mwangu.
Nilikuwa nafanya hivi huku nikitazamana sawia na mwanamke huyo aliyekuwa makini kweli, nami nikamumunya dawa hiyo na kisha kuonyesha msisimko kwa kutetemesha uso huku nimefumba macho.
Oh siyo jambo la kushangaa wala kwamba JC pia aliwahi kutumia kitu kama hiki, ingawa ulikuwa umepita muda mrefu tokea mara ya mwisho nimetia madawa ndani ya mfumo wangu, na kwa wakati huu hali ilinilazimu nifanye hivi ijapokuwa nafsi haikutaka.
Nikiwa nahisi mwili unapandisha kasi ya nguvu sana kiuchangamfu, nikamwambia Bertha, "Hakuna sumu humo. Vibe tu."
Baunsa wake akafanya kama mimi nilivyofanya pia, naye akatikisa kichwa kwa msisimko kuonyesha vibe kweli imemwingia.
"Mh! Shemeji... ni hatari," baunsa akasema hivyo.
Inaonekana walikuwa na ukaribu zaidi mpaka jamaa kumwita Bertha shemeji, na mwanamke huyo akanitazama usoni kwa umakini.
"Umeitengenezaje hivi? Yaani nimeilamba tu ikanigonga..." jamaa akaniuliza.
"Me mtu wa manuva kaka, mkemia mkemia. Hii weka kwenye ulimi, ama fizi, ama puani, hata kunani, yaani utajiona kilele cha mlima Kilimanjaro," nikasema hivyo.
Jamaa akacheka kidogo, naye akamwambia Bertha, "Kitu safi sana. Huyu white yupo vizuri kama anavyojitangaza."
"Ah, uhakika kamanda," nikamwambia hivyo.
Nilikuwa nimeanza kuhisi nguvu zikiikimbia miguu maana ni kweli kwamba niliifanya dawa hiyo iwe kali, lakini nikatulia tu ili nione itikio la mke wake Chalii.
Bertha akasema, "Tuliza makeke dogo. Unaongea sana, na mimi sipendi mtu anayeongeea mno."
"Sawa. Niko kimya. Nakusikiliza," nikamwambia.
"Kwa hiyo unaweza kutengeneza coke wewe mwenyewe, si ndiyo?" akaniuliza.
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Sawa. Nataka nipime vitu fulani. Nitakufatilia. Kuna business naendesha kwa hiyo... kama uko vizuri namna hii... nitakuweka sehemu. Umeelewa?" akaniambia hivyo.
Kauli aliyoitoa ikanifanya nibaki kumtazama kwa umakini. Ni ile hisia unayopata unapojua kwamba unaelekea kushinda jambo fulani, lakini bado unakuwa hujui ni mambo gani yanahusika zaidi katika kuutwaa huo ushindi.
Alipoona nimekaa kimya tu, akauliza tena, "Umenielewa HB wa Masai?"
Nikatabasamu kidogo na kusema, "Nimeelewa."
"Utakuwa unanipa nachotaka kwa muda wowote napokitaka, na si umesema hauhitaji malipo?" akaniuliza.
"Ndiyo. Yote itakuwa kwa ajili yako boss," nikamwambia.
"Usiniite hivyo. Niite madam," akaniambia hivyo kibabe.
"Madam," nikasema hivyo kiutiifu.
Akanisogelea karibu zaidi na kusema, "Kuwa makini sana na unayotaka kufanya ukiwa upande wangu kijana. Nikinusa mchezo wowote wa kipuuzi..."
"Haiwezi tokea. Niamini,* nikamwambia.
"Hapana... bado sijakuamini," akaniambia hivyo.
Nikainamisha uso tu na kutulia. Alikuwa sahihi kutoniamnini bado maana nilikuwa na lengo la kumpindua vibaya mno, na pamoja na ushenzi wake wote lakini alikuwa makini, na mimi ningehitaji kuwa mwerevu kweli nikiwa nimeshajiingiza kwenye himaya yake.
Akawa ananitazama kwa njia ya kibabe kama kawaida yake, naye akasema, "Ila tutaona. Nenda. Nikikuhitaji nitakupa maagizo."
Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa, na yule baunsa akanitikisia kichwa kwa njia ya kuaga.
Nikageuka na kuuelekea mlango, nami nikatoka ndani ya chumba hiki kimya kimya bila kuwaangalia watu hao tena. Nikaanza kujiona kama vile nimeingia ndani ya kisa chenye uzito zaidi ya nilivyotarajia, lakini ndiyo nilikuwa na hamu kubwa ya kutaka kufika hatua za mbele zaidi ili malengo yangu yatimie.
Likizo yangu fupi ingejaa uhondo mkubwa sana ambao sikuwa nimeutarajia, na hilo lilinisisimua. Bertha angelipia kwa kifo cha Joy tu, lakini pamoja na hilo, nilikuwa nataka kuhakikisha na mambo yake mengi haramu yanaanguka pamoja naye. Na ingekuwa kwa mwendo wangu kama kawaida; taratibu.
Nikatoka kwenye jengo la hoteli hiyo na kuamua kwenda Makumbusho upesi. Safari ilikuwa moja tu ya kurudi tena Mbagala, ingawa kuwa huku kulinifanya nivutwe na wazo la kwenda kumwona mama yangu.
Sikuwa nimesahau mazungumzo yetu mapema ya leo, ambayo yalikaribia kuelekea kwenye pande ambazo sikutaka yaende kwa wakati huu, hivyo kama ningesema nipite kumsalimu mzazi wangu huenda masuala hayo yangezushwa tena na kunivuruga tu. Ndiyo. Yalikuwa ni mambo yenye kuvuruga akili ambayo nilijua ipo siku tu ningetakiwa kuja kuyapa za uso, lakini kwa sasa nilitaka akili yangu ikazie fikira zaidi yale ya kule Mbagala.
Hisia za hatia kutokana na kifo cha Joy ndiyo zilikuwa zimenisukuma kufika huku na mke wake Chalii Gonga, lakini sasa kukawa na mengine zaidi yaliyojiongeza. Mwanamke huyo pamoja na mume wake walionekana kufanya mambo mengi haramu, na mimi wala hata nisingejishughulisha nao endapo kama baadhi ya hayo mambo yasingeniathiri.
Gonga alifikiri nahusika na kifo cha Joy, na mhusika halisi alikuwa mke wake ambaye alijionyesha wazi kwangu kwamba ni yeye ndiye aliyekuwa amemuua. Sijui kwa nini tu Chalii Gonga hakuona kwamba mke wake ndiye aliyekuwa msababishi, ama labda alijua lakini na yeye alikuwa anamhofia mke wake. Sijui ni yale mambo ya kufichiana siri nyingi labda? Ama tu ni kutafuta watu wa kurushia lawama hata kama ukijua fulani ndiyo mbaya maana unakuwa huwezi kumgusa kwa sababu moja au nyingine.
Kwa vyovyote vile, wawili hao walikuwa wameuvuta umakini wangu kwao, na walikuwa wameupata kweli kweli. Lilikuwa ni suala la kuwakamata tu katika udhaifu wao na kuugeuza uwe nguvu yangu ili niitumie kuwamaliza; Chalii Gonga wanawake, na madam Bertha madawa. Kwisha kazi.
★★
Nikawa nimechukua usafiri wa daladala kuelekea Mbagala, na nikiwa njiani, simu yangu ikaita. Nilikuwa nimetunza jina la mpigaji kwa maandishi ya kichina, lakini nilielewa huyo kuwa askari mpelelezi Ramadhan Hamisi. Nikapokea.
Akawa ameniuliza ikiwa ningeenda kituoni muda huo kama nilivyokuwa nimemwambia, nami nikamjulisha kwamba bado nilikuwa njiani kutokea Sinza hivyo kama ingemfaa basi ningefika hapo baadaye. Akasema hakuna shida, lakini tubadili sehemu ya kukutana maana muda huu alikuwa anatoka kituoni na kwenda Temeke mara moja, kwa hiyo ikiwa ningeweza kwenda huko tungekutana na kuongea.
Nikamwambia haina shida na kumwomba anipangie sehemu hususa na kunielekeza namna ya kufika. Akaniambia atanitumia ujumbe, kisha simu ikakatwa. Wito mwingine huo niliopaswa kuitikia upesi. Uzuri ni kwamba nilikuwa na jambo fulani la kumpatia askari huyo ili aweze kuona uzito wa yale niliyotaka kufanikisha katika suala la kutafuta haki ya kifo cha Joy, na nilitaka aniunge mkono kwa hatua nilizotaka kuchukua; na hiyo ni kama tu angekuwa mwelewa maana hawa watu huwa wana mambo ya kikuda sana.
Nilikuwa nimesimama kutokana na abiria kuwa wengi ndani ya gari, mpaka tumefika maeneo ya Uhasibu ndiyo nikapata nafasi ya kukaa. Nikatoa simu yangu tena na kukuta ujumbe kutoka kwa mpelelezi Ramadhan, naye akawa amesema kwamba nichukue usafiri wa kuelekea Tandika, kisha usafiri mwingine kuelekea Kijitonyama na nishukie kituo cha Ali Maua halafu nimjulishe. Dah!
Bado nilikuwa naona kama ni ngumu kuelewa somo maana kuna kauchovu nilikohisi mwilini kalikonitaka nirudi tu Mzinga na kupumzika, lakini hiki hakikuwa kitu cha kuepuka tena. Askari mwenyewe hata nilikuwa simwelewi, mara aseme anaenda Temeke halafu ananiambia tukutane tena Ali Maua. Ila nikamjibu kifupi tu kwamba nimeelewa.
★★
Vuuu hazikupita dakika nyingi sana nami nikawa nimeshuka. Niliamua kushukia Sabasaba na kuvuka barabara ili nikapande daladala za Temeke. Sikuwa mkongwe bado wa haya maeneo lakini angalau nilionekana kama mwenyeji kwa kwenda moja kwa moja kwenye kile nilichohitaji.
Nikawa nimesimama ndani ya usafiri kwa mara nyingine tena, na macho yangu yalinionyesha wazi ni jinsi gani watu ndani humo walinitazama sana. Sasa unakuta kuna ile naamua kumwangalia mtu fulani moja kwa moja usoni, halafu anaangalia pembeni kidogo kama vile hana habari na mimi, kisha tena anaendelea kuniangalia akiona nimegeukia kwingine! Nakuwa nashindwa kuizuia ile hisi ya kupenda sana jambo hilo japo nimeshazoea na kuliona kuwa la kawaida.
Nikiwa naelekea Tandika, Tesha, Ankia, pamoja na Bi Zawadi wakawa wamenipigia na kunisalimu. Bi Zawadi alikuwa ananiambia ni kama vile Mariam alijihisi upweke sana pale nyumbani baada ya mie kuondoka, maana alitoka nje ubarazani kwao na kuchungulia upande wa nyumba ya Ankia ili aangalie kama nipo. Nikafurahi sana na kumwambia asiwaze kwa sababu nisingekawia sana kurudi jioni, nami ningeendelea kucheza na binti huyo.
Basi, nikawa nimefika Tandika, nikaulizia daladala ambazo zingenipeleka Kijitonyama na kuelekezwa zilipokuwa, nami nikafanikiwa kuzipata na mwendo ukaanza kuelekea huko. Nilikuwa nimeshaongea na konda, nikimwomba anishushie kituo dha Ali Maua, na mwendo wa dakika kadhaa ukanifikisha huko hatimaye.
Nikatoka kwenye gari na kusimama pembezoni mwa barabara ya lami, kisha nikampigia mpelelezi. Akapokea, nami nikamjulisha kwamba nimefika. Akaniambia nisimame hapo hapo nilipokuwa naye angenifikia. Haya. Nikatulia.
Upande wa pili wa barabara kulikuwa na uwazi zaidi uliotoshea kusimamisha biashara ndogo ndogo pamoja na pikipiki za mabodaboda. Walikuwepo boda wanne pamoja na wanawake watatu waliouza vitafunwa kama mihogo ya kukaanga, sambusa, na viazi vya kukaangwa; ingawa wenyewe walikaa pembeni zaidi.
Nikavuka barabara na kwenda upande huo, magari yakiwa yanapita huku na huko, na mabodaboda wale wakiwa wameshaanza kuwasha pikipiki kabisa, lakini nikawatuliza kwa kusema kuna mtu namngoja. Nikasimama pembeni yao, nami nikaanza kupiga nao story.
Niliongea nao kwa uchangamfu wa kadiri, nao wakaonyesha utashi wao wa kuongea pia. Nilikuwa naua muda tu, nikiwafanya wanione kuwa bonge moja la mtoto wa mjini kwa ujuzi wa mambo mengi niliyozungumzia, na ndipo gari jeupe aina ya Toyota Land Cruiser, kama tu yale ambayo watanzania tumeyazoea kuwa ndiyo ambulance, likawa limefika upande ule nilioshukia na kusimama.
Nikiwa nakisia kuwa bila shaka gari hilo lilimhusu mhusika niliyemsubiria, nikaamua kuwaacha mabodaboda wale na kuvuka barabara tena ili nilifate. Kabla sijalifikia, simu yangu ikaanza kuita, nami nikaona mpigaji kuwa huyo huyo afande. Nikapokea.
"Hello..." nikasema hivyo.
"Uko wapi?" Ramadhan akauliza.
"Ni mimi nakuja nyuma ya gari," nikamwambia.
Inaonekana alinitazama kupitia kioo cha pembeni mlangoni mwa gari, naye akakata simu.
Nikawa nimefikia mlango wa mbele upande wa dereva, nami nikamkuta mwanaume mtu mzima wa miaka ya thelathini na kitu akiwa ananiangalia kwa njia ya kawaida. Alikuwa mweupe wa kadiri, mwenye mwili mkubwa na nadhani alikuwa mrefu kunifikia. Alikuwa na kipara lakini kutokea kwenye timba aliacha ndevu hafifu kiasi mpaka kidevuni, na mavazi yake yalikuwa ya kiraia; si kiaskari.
"Habari za kazi bwana Ramadhan?" nikamsalimu.
Akiwa ananiangalia machoni sawia, akasema, "Ni nzuri. Ndiyo wewe eh?"
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Ingia kwenye gari tuongee," akasema hivyo.
Nikazungukia upande wa pili wa gari na kuingia kukaa siti ya pembeni na askari huyu. Kiukweli nilikuwa nina msisimko kutokana na yale niliyokuwa nimepanga kufanya, na mpaka kufika hapo tayari nilikuwa nimejipanga vya kutosha kiakili ili na huyu mtu anielewe.
"Kwanza pole na kazi mkuu. Najua una mambo mengi," nikamwambia hivyo.
"Ndiyo mambo ni mengi. Kutenga muda kwa ajili ya kila kitu sometime ni ngumu, hapa pia ninahitajika kufika mahala. Kwa hiyo kama vipi hii kitu tuipe spidi," akaniambia hivyo.
"Sawa, sitakula muda wako."
"Uliniambia huyo Joy alikuwa rafiki yako?"
"Ndiyo, na... tumefahamiana kwa muda mfupi tu lakini mazoea yalikuja kiuwepesi. Najua kuingiliana kwa vitu vingi kikazi kunaweza kufanya iwe ngumu kufanikisha uchunguzi wa mauaji ya huyu mwanamke, na ndiyo maana nataka kusaidia ili kuhakikisha haki inatendeka kwake na... kwa watu wa familia yake."
"Unamjua aliyemuua?" akaniuliza hivyo.
Nikatikisa kichwa kukubali, nami nikasema, "Lakini bado sijawa na ushahidi wa kutosha. Nataka tusaidiane... mimi na wewe... mpaka aje kukamatwa na...."
"Subiri. Kama unamjua aliyemuua, niambie ni nani, sisi tutafatilia ili..."
"Hapana kaka, nisikilize tafadhali. Najua mna hizo taratibu lakini kwa hili suala mambo ni tofauti. Ona... mazingira yote yanayozungukia kifo cha Joy ni mapana sana. Yanahusisha mambo mengi ambayo ndiyo yamenifanya nikutafute namna hii. Watu waliosababisha hilo ni wakubwa, yaani wana njia nyingi haramu za kubadili hata hali mbaya kwa upande wao ziwe nzuri."
"Hakuna mtu mkubwa zaidi ya sheria. Hata awe nani lazima apewe adhabu kwa kosa la kuua. Au unataka kumaanisha tuwaogope sasa?"
"Hapana, sina maana hiyo..."
"Sasa unataka tufanye nini? Si ni bora uniambie hao ni akina nani ili wafatiliwe mpaka wabainishwe na kuchukuliwa hatua? Najua ndiyo, mazingira ya kifo cha huyo mwanamke ni tata ndiyo maana mpaka sasa hivi hata upande wetu haujapata kitu... mpaka inaweza kusahaulika. Kama unawajua na hauna ushahidi wa kutosha, nipointie wako wapi, uchunguzi ufanywe, basi."
"Lengo langu siyo kuwakamata tu kwa kifo cha Joy. Hawa watu wanajua kuficha mambo vizuri, wanaendesha mambo illegal na hakuna mtu ambaye amewagusa mpaka leo... na ninamaanisha hata maaskari pia. Wana mambo zao haramu, sehemu zao haramu, lakini sijazijua bado, kwa hiyo muda pia unahitajika siyo kuingia tu kichwa kichwa. Bwana Ramadhan... kuwakamata mtawakamata tu. Lakini mimi nataka wakomeshwe kabisa kwa maovu yote wanayofanya... waporomoke, siyo waingizwe ndani siku mbili wametoka... maana wana huo uwezo kwa sababu wako makini. Ninataka kufanya hivi... kwa njia fulani ambayo italeta matokeo mazuri baadaye, lakini ni kama tu utani-support na kuiacha iwe kama... upelelezi wetu sisi wawili," nikaongea kwa kusihi.
Alikuwa ananiangalia kwa macho yenye umakini, naye akaniuliza, "Sisi wawili? Ni njia gani unaongelea?"
Nikashusha pumzi kiutulivu, nami nikatoa simu yangu na kuanza kubofya. Nikamwekea rekodi moja ya sauti ambayo nilichukua muda ule niko kule hotelini kuonana na mke wake Chalii Gonga. Ndiyo. Muda ule niliiweka simu katika mfumo maalumu wa kurekodi sauti kabla sijaingia ndani ya kile chumba mpaka wakati nilipotoka, na ilikuwa imekula nafasi kubwa ya memory kwenye simu.
Kwa hiyo nikaanza kumsikilizisha askari huyu, huku nikielezea jinsi mambo yalivyokuwa, na nani alikuwa nani, na mimi nilijiingiza katika sakata hilo kwa sababu gani. Kuna nyakati fupi ambazo mpelelezi huyu alikuwa akitabasamu na kutikisa kichwa kuonyesha namna alivyoona jambo hili lote kuwa kama mchezo wa kitoto, lakini nikamsihi kwa bidii mpaka nikaona ameanza kunielewa. Mwishowe uamuzi wa hatamu ungekuwa wake, nami nikamuuliza kwa mara nyingine tena anaonaje kuhusu wazo hili nililokuwa nimemfikishia.
Akaniangalia tu kwa utulivu, naye akasema, "Yaani ili kuwakamata wanaharamu inabidi tuungane mkono kufanya mambo haramu pia, eh? Huoni kwamba unaweza ukajiweka hatarini?"
"Najua. Hatari ipo, lakini siyo kwangu tu, bali kuzungukia wengine naowafahamu pia. Ndiyo maana nakuomba tusaidiane ili tulimalize hili jambo kiaina bila mtu mwingine yeyote kuumia. Si unajua wakati mwingine ni vyema kutuma mwizi ili mwizi akamatwe? Ndiyo tutakachofanya mkuu," nikamwambia hivyo.
Akacheka kidogo na kutikisa kichwa, kisha akasema, "Unajiamini sana. Sawa. Nimekubali. Itabidi tuje tukutane tena ili tupange hii ishu vyema zaidi, umeelewa?"
"Kabisa. Nashukuru kwa kukubali kaka," nikamwambia hivyo.
"Mhm... sawa, lakini uwe makini. Uko vizuri pia, ungefaa hata kuwa askari."
Nikatabasamu na kusema, "Asante. Siyo mbali sana kufika huko maana hata sa'hivi niko kama askari wa mchongo."
"Eeh, naona. Ila nisije tu kukukuta siku moja unawatengenezea watu wengine madawa. Hatutaelewana," akaniambia hivyo.
Nikatabasamu kidogo na kusema, "Hamna, siwezi. Hii ni kwa ajili ya mission tu."
Akatabasamu kidogo, kisha akawasha gari lake na kusema anaelekea pande zingine kikazi kwa hiyo angeniacha eneo la Mawasiliano. Nikamkubalia, naye akatuondoa hapo.
Tukiwa mwemdoni ndiyo akapata nafasi fupi ya kuuliza majina yangu kamili na nilikotokea, nami nikawa nimemweleza yale aliyotaka kujua. Nilifarijika rohoni kwamba zoezi la kumshawishi askari huyu lilikuwa limefanikiwa, na sasa ambacho kingefuata ilikuwa ni moto tu!
Niseme nilikuwa tu na nyota nzuri, hasa kwa siku ya leo. Vita yangu dhidi ya wauaji wa Joy ingepata ushindi kwa msaada wa mtu mwenye nguvu kisheria kama askari Ramadhan, na matendo ya watu kama Bertha yangekomeshwa kimtindo kabisa. Lingekuwa ni suala la muda tu, tena mfupi sana.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments