MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA NANE
★★★★★★★★★★★★★★★★
Wiki moja ikawa imepita baada ya mambo hayo yote. Oh tena ni siku nane kabisa zilikuwa zimepita sasa toka nilipoanza kumsaidia Mariam na kuanza kushughulika na mke wake Chalii Gonga, yaani madam Bertha. Mambo bado yalikuwa yanakwenda taratibu, lakini nilijua tu matokeo yangekuja kwa kasi sana.
Suala la mke wa Chalii kuhusika na mauaji ya Joy niliendelea kulifungia kapuni na kufanya ionekane kwamba msiba huo ulikuwa umeshapita kwangu pia kama ilivyokuwa kwa watu wengine, na toka ile siku nimeenda kwenye ile hoteli kuonana na mwanamke huyo, hakuwa amenitafuta tena.
Najua alikuwa na mambo yake mengi labda pamoja na mume wake ambaye naye pia alikuwa amenikaushia tu toka mara ya mwisho tumeonana msibani kwa Joy, lakini nilijua angenitafuta tu. Nilielewa kwamba muda si mrefu angehitaji tu dawa kama niliyokuwa nimemtolea mfano, kwa hiyo angenitafuta tu. Na siyo kwamba nililala juu ya hilo.
Ndani ya hizo siku chache ambazo hakunitafuta, nilikuwa nimefanya experiment za ziada kutokeza madawa ya cocaine kwa kiasi kingi, ili ikitokea ameniita, niwe na jambo alilohitaji la kumpa. Lengo langu lilikuwa wazi si kwangu tu, bali na kwa askari Ramadhan. Tulikuwa tumekutana tena katikati ya wiki hiyo na kuzungumza kwa mapana zaidi.
Nilimwelewesha namna ambavyo nilitaka kujishikiza upande wa mke wake Chalii ili aniamini vya kutosha kuniweka ndani ya mambo yake haramu aliyoendesha, kisha nikishaelewa namna ambavyo mtandao wake unafanya kazi, nitumie kila njia kwa fursa ambazo ningepata ili kusomba ushahidi dhidi ya mwanamke huyo na mume wake, halafu nimkabidhi Ramadhan na maaskari wenzake ili waweze kuwaharibu wawili hao.
Na uzuri ni kwamba askari huyu alikuwa mwelewa sana, akisikiliza mawazo yangu na kuniongoza vizuri pia kwa mbinu za hivi ama vile, na jambo hilo lilibaki kuwa baina yetu sisi wawili tu; hata hakuwa amewaambia maaskari wenzake ili kweli njia hii ije kumletea faida kubwa yeye kama mpelelezi wa mauaji ya Joy.
Tukiweka hayo pembeni, upande wa pili wa vita yangu dhidi ya ugonjwa uliomsumbua binti Mariam ulianza kuonyesha kuzaa matunda mazuri. Hakukuwa na mabadiliko makubwa sana, lakini yalikuwepo baadhi ambayo yaliendelea kunipa matumaini kwamba njia niliyotumia kumsaidia binti huyu ingeleta manufaa.
Niliendelea kufanya michezo rahisi pamoja naye, na yeye alikuwa ameshanizoea mno kufikia sasa. Nilikuwa nimeanza na kumfundisha vitu rahisi kushika kama kugonga tano, kupangilia vifaa vyake vya kuchezea kwa utaratibu mzuri alipomaliza kuvitumia, nami nikawa nimeona badiliko dogo lakini lenye maana kubwa kiasi katika utendaji wake.
Kufikia sasa, Mariam akawa ameacha kutafuna-tafuna kucha zake na kutetemeka kwa kichwa kulikokuwa ni jambo la muda wote, kwa sababu akili yake ilikuwa imeanza kutafuta utulivu zaidi kupitia mazoezi tuliyofanya na hivyo nikaona hata mwili wake unaanza kutulia.
Kilichokuwepo hapa ilikuwa ni kuhakikisha naendelea kucheza naye kwa kubadilika, yaani kubadili michezo, ili mdogo mdogo tu nimsaidie mpaka apate utulivu mzuri zaidi wa kumwezesha kuongea vizuri tena na kufungua ufahamu wake wa kiakili.
Na familia yake iliniunga mkono sana, yaani hawakuwa na mbambamba. Waliamini kabisa kwamba mtoto huyu angepona tu, na hilo liliniongezea nguvu ya kuendelea kujitahidi kumpambania Mariam.
★★★
Sasa ikawa ni siku ya Jumamosi iliyokuwa na mambo mengi yenye kuburudisha kwa sehemu hii niliyokuwa. Nilitumia muda mwingi pamoja na familia yake Mariam, nikiendelea kucheza pamoja naye na kupatana zaidi na mama wakubwa.
Ni leo ndiyo siku ambayo hatimaye Tesha alikuwa ameweza kwenda kukutana na yule Winny, na alikuwa ameshajipanga vyema sana ili aende kujilia vyake kwa mwanamke huyo. Mie nilikuwa nawasiliana na Winny bado, na kama ni kitu ambacho sikuwa nimemweka Tesha wazi ni kwamba mwanamke huyo alinitaka.
Lakini nilikuwa nikimkwepa na kuendelea kumuunga mkono Tesha ili afanikiwe kumgalagaza kisha ndiyo mengine yafuate. Ilikuwa ni heshima ya kishkaji tu kumwachia mwenzangu meza kuu aliyotaka kulia chakula, na ndiyo leo ningeona matokeo ya kumwaga jasho lake kwa huyo manze. Angenisimulia tu!
Mimi kwa upande wangu sikuwa nimejihusisha na makutano ya kimwili pamoja na mwanamke yeyote yule kwa hizo siku. Ankia alikuwa ameingia kipindi cha hedhi, kwa hiyo sikutaka kumgusa. Basi tu, ndiyo niko hivyo. Ni Latifah na Soraya ndiyo ambao niliendelea kuwapiga kalenda tu.
Latifah alikuwa analazimisha tuonane tena, Soraya yeye alikuwa anaomba tukutane tena. Wote niliwakubali lakini kwa hizi siku nilikuwa tu nimewekeza akili yangu kwenye masuala mengine muhimu zaidi, kwa hiyo tamaa za mwili nilikuwa nimeamua kuziweka benchi kwanza.
★★
Basi, kwa hiyo nikawa hapo na akina Bi Zawadi mpaka jioni, nasi tukiwa sebuleni pamoja na Bi Jamila, Mariam, na mwanamama mwingine ambaye alikuwa ni rafiki kwa mama wakubwa, Tesha akawa amenipigia. Ilikuwa imeshaingia saa moja kabisa na bibie Miryam hakuwa amerejea nyumbani bado; sijui alikuwa kazini ama kwenye harakati zake nyingine, alijua mwenyewe. Na kiukweli alikuwa na mambo mengi ya kivyake mno mpaka alitisha.
Namaanisha hata pale kazini kwake, Soraya aliondoka mida ya saa kumi na moja kiukawaida, kumaanisha walifunga mapema tu, lakini yeye Miryam angerudi usiku kabisa mara kwa mara. Huenda alikuwa na mikutano na watu wake wengine, nani angejua? Na mimi sikuwa mtu wa kuanza kufatilia maisha yake japo nilijihusisha na mengi yaliyohusu familia yake kwa wakati huu.
Kwa hiyo nikapokea simu ya rafiki yangu na kumsikiliza. Alikuwa ananiambia kwamba mambo yalimwendea vyema sana kwenye date yake na Winny, naye angekuja kunisimulia kila kitu kilichotokea. Ndiyo mida hii alikuwa njiani kurejea huku nyumbani, naye akasema kwamba anampitia Shadya pale kazini kwake na kuja pamoja naye.
Baada ya Tesha kuniambia hivyo, akawa amenifanya nifikirie jambo fulani. Ikanibidi nitoke nje ili nimpange kuhusiana na jambo hilo, lililokuwa linamhusu Mariam pia, naye akacheka kidogo na kusema ananiunga mkono kwa hilo. Nikamaliza kuongea naye, nami nikarudi ndani tena.
Nikawa nimewaambia mama wakubwa kuhusu ujio wa Tesha na Shadya, nami nikawahusisha pia katika jambo hilo nililotaka kufanya kwa ajili ya Mariam. Walicheka, lakini Bi Jamila akawa hana uhakika sana ikiwa ni wazo zuri. Ilikuwa ni mchezo mdogo tu niliotaka kufanya pamoja na binti Mariam mwenyewe, nami nikamhakikishia Bi Jamila kwamba mambo yangekwenda vizuri tu.
Baada ya kuwa tumekubaliana, kilichobaki ikawa ni kumpanga Mariam mwenyewe, kisha kuwasubiri wakina Tesha wafike.
★★
Hazikupita dakika 40 naye Tesha akawa amenipigia kuniambia ndiyo wameshukia hapo Mzinga pamoja na Shadya, na mwendo wa mguu kuelekea huku nyumbani ndiyo ulikuwa umeanza. Nikamwambia poa, kisha nikasema ajitahidi kumtembeza Shadya taratibu na wakifika tu eneo la bar ya Masai anitumie ujumbe mfupi ili nijue wamekaribia, halafu ndiyo nifanye harakati niliyokuwa nimeipanga.
Alipokata simu, nikawaambia mama wakubwa kwamba mpango wangu ungetakiwa kuanza kazi sasa hivi kwa kuwa walengwa walikaribia kufika, nao wakanipa ruhusa ya kuanza kazi. Nikamchukua binti Mariam na kwenda naye pale kwa Ankia.
Binti alikuwa anatabasamu tu kwa sababu ya kujihisi uhuru mzuri wa kuambatana nami bila ya kuelewa kikamili tulichokuwa tunaenda kufanya ndani ya muda mfupi, nami nikamfikisha sebuleni na kumkuta Ankia akiwa pamoja na mama Chande.
Rafiki yake huyo ndiye aliyekuwa mwenye kufika hapo mara nyingi zaidi ya watu wengine waliofahamiana na Ankia, na japo tulikuwa tukiongea kawaida tu, sikujenga mazoea naye kabisa. Hata kuna siku Ankia alikuwa ameniambia kwamba kuna watu waliniogopa kutokana na kuhisi sifikiki kirahisi sana, ukiondolea mbali watu wa familia yake Miryam na Ankia mwenyewe, na mimi nilielewa mmoja wa hao watu kuwa ni mama Chande pia.
Kwa hiyo hata tulipoingia hapo ndani na binti Mariam, ni salamu tu ndiyo tuliyopeana na mwanamke huyo, nami nikamwambia Ankia anifuate chumbani mara moja ili nimpange juu ya ishu fulani. Nikaendelea kumvuta mkono Mariam kuelekea chumbani kwangu huku Ankia akitufata, nasi tukakaa kitandani baada ya kuingia na Ankia akawa amesimama karibu yetu akitutazama.
"Vipi JC? Mbona umekuja na Mamu?" Ankia akaniuliza.
"Kuna mchezo nataka tufanye. Nataka kuona kama Shadya anajua kukimbia," nikamwambia hivyo huku nikitabasamu.
"Mchezo gani?" akaniuliza tena.
"Una nguo ama labda... kanzu nyeupe? Yaani nguo ndefu nyeupe?" nikamuuliza.
Akatikisa kichwa kidogo kukanusha, lakini akasema, "Labda mashuka ndiyo ninayo meupe, ila..."
"Sa' na yenyewe si ni nguo Ankia!"
"Unataka ya nini kwani?"
"Chukua ile sabuni pale, huwa ina povu jeupe linalobaki ukilishindilia kwenye ngozi. Kampake Mamu upesi halafu mvalishe shuka jeupe mwilini... mzungushie yaani... ahahah... harakisha..." nikamwambia hivyo kwa furaha.
"Nimpake wapi? Sielewi JC, mnataka kucheza mchezo gani?" Ankia akawa hanielewi.
"We' kafanye tu hivyo Ankia, utaona. Harakisha sasa!" nikamwahisha.
Ingawa hakuelewa, akatii tu na kuifata sabuni yangu chini ya meza, kisha akamshika Mariam mkono na kuongozana naye chumbani kwake. Nikawa nimetoka kwenye cha kwangu na kufika sebuleni, nami nikasimama usawa wa sofa nikiwa makini na simu yangu.
Mama Chande alikuwa akitazama tu TV, na baada ya dakika chache Ankia akawa amemtoa Mariam chumbani. Nikatabasamu baada ya kumwona binti akiwa amefunikwa kwa shuka kuanzia shingoni mpaka kufikia miguuni, likiwa limekazwa kwa kuuzunguka mwili wa binti, lakini lilimruhusu atembee vizuri tu.
Ankia alikuwa ananiangalia huku akitabasamu, naye mama Chande akamwangalia binti kimaswali. "Kulikoni tena? Anaenda wapi huyo?" akauliza hivyo.
"Mi' mwenyewe sielewi," Ankia akasema na kunitazama.
"Mamu, njoo," nikamwita binti.
Akanisogelea huku akiniangalia usoni.
"Ankia, wahi... pakaa sabuni mikononi uje umpake huyu usoni," nikamwambia hivyo.
"Usoni tena?" mama Chande akauliza.
"Ahahah... ila JC! Nimeshaona unachotaka kufanya," Ankia akaniambia hivyo.
"Harakisha sasa, ndege wako njiani, nataka tuwakamate," nikamwambia hivyo.
Akacheka kwa mguno, naye akaelekea upande wa jikoni ili kuilowanisha sabuni.
Mama Chande akaomba kujua ni nini ambacho tulitaka kufanya, nami nikamwelezea kwamba tulitaka kumfanyia Shadya kamshtukizo kadogo kwa kumtengeneza Mariam aonekane kama mzimu. Akacheka na kuanza kusimulia visa kama vya namna hiyo ambavyo alifahamu, naye Ankia akarudi akiwa amejaza mikono yake povu jeupe.
Nikamwelekeza Mariam afumbe macho yake, na baada ya binti kutii, Ankia akaanza kumpakaa usoni. Lilikuwa povu zito ambalo liliacha weupe wake usoni hata baada ya kukauka, nalo likaupendezesha kweli uso wa Mariam kwa njia ya uzimu! Yaani mzimu beautiful!
Wanawake wakawa wanacheka baada ya Mariam kufumbua macho, na ndipo Tesha akawa amenitumia ujumbe kwenye simu akisema kwamba walikuwa wamefika Masai. Ikabidi nianze kuwaharakisha wanawake hawa, nikimwelekeza Ankia sehemu niliyotaka asimame pale nje pamoja na simu yangu ili arekodi video ya kile ambacho kingetokea.
Tukatoka ndani na kwenda nje, Ankia akiwa amewapigia simu mama wakubwa pale kwao ili waje nje pia kushuhudia, lakini kwa sehemu ambayo waja wasingewaona mpaka tukio likamilike. Mama Chande akatumia akili ya kwenda pale dukani kumwomba yule mwanamke muuzaji, ambaye sasa nilikuwa nimefahamu anaitwa Fatuma, azime taa ya nje kwa kitambo kifupi kwa sababu kuna ishu tulikuwa tunataka kuifanya.
Nilikuwa nimepata support kubwa kweli ijapokuwa jambo hili lilionekana kuwa la kitoto sana, lakini nilielewa kwamba watu hawa walitaka kuona tu itikio la Shadya lingekuwaje kwenye mchezo huu tuliopanga. Bi Zawadi na Bi Jamila walitoka ndani kwao na kusimama kwenye ukuta wa uzio lao, ambapo matobo yake yaliwawezesha kuona mpaka upande wa nje wa nyumba ya Ankia kwa kiasi fulani.
Ankia akawa ametoka kabisa na kwenda kujibanza nyuma ya kibanda kidogo upande wa pili wa barabara, palipokuwa na giza kiasi, nami nikawa nimesimama pamoja na Mariam na mama Chande mwanzoni mwa geti la nyumba yake Ankia kwa kificho. Kungekuwa na wapita njia kadha wa kadha na watu mmoja mmoja waliokuja dukani kwa Fatuma, nami nikaanza kuwaona Tesha na Shadya wakikaribia eneo hili la duka. Nikamwonyesha Ankia ishara ya dole gumba kuwa aanze kurekodi.
Nikamshika Mariam mabegani na kumwambia, "Shangazi kafika Mamu. Sasa... nikikwambia nenda, anza kwenda ukiwafata, sawa Maimuna?"
Mariam mwenye kufanana na mzimu akawa ananiangalia tu usoni, na mama Chande akacheka kidogo.
Nikaona Tesha na Shadya wamekaribia zaidi, nami nikamwambia Mariam, "Haya nenda," huku nikimgeuza na kumsukuma kiasi.
Mariam akatii bwana.
Najua Tesha alikuwa ameshajiweka tayari kwa kile ambacho kingetokea, kwa hiyo alikuwa anakuja na Shadya huku wakiongea ya kwao na yeye akijifanya kama vile haelewi somo. Mariam akatoka hapo nje na kusimama usawa wa duka la Fatuma, akiwaangalia wawili hao, nasi tukiwa tunachungulia tukamwona Shadya anamsimamisha Tesha kwa kumshika mkono huku akimwangalia Mariam kwa kukodoa.
Nikamwona Tesha akimtazama Mariam huku akijifanya kushangaa, nami nikamsikia anasema, "Toba!"
Kuna wapita njia wengine waliokuwa wanatokea upande walikotokea akina Tesha, nao pia wakasimama. Sasa sijui Mariam alipata wapi hii akili. Ghafla tu binti akachomoka na kuanza kukimbia kuwaelekea! Wee! Shadya akamsukuma Tesha na kuanza kukimbia kurudi Masai!
Tesha akabaki kusimama hapo hapo huku akicheka sana, nasi tukawa tunachteka pia kwa kushindwa kujizuia. Bi Zawadi alicheka mpaka machozi kumtoka, kwa kuwa Shadya alikimbia mpaka kufikia bar ya Masai!
Mariam alikuwa ameacha kuwakimbiza baada ya mwendo mfupi, naye akaanza kurudi mpaka alipomfikia kaka yake. Sisi wengine tukatoka na kwenda nje kabisa, baadhi ya watu wakiwa wamekuja ili kujua nini kilikuwa kinaendelea maana waliona Mariam alionekana kutaka kutafuna nyama ya mtu!
Tukawaelewesha kilichotokea hapo kihalisi, na wengi wao wakacheka pamoja nasi. Ilipendeza sana kumwona Mariam akifurahia mno kioja alichokuwa amefanya, kwa sababu yeye pia alicheka kwa furaha iliyotoka moyoni. Ikambidi Tesha amkimbilie Shadya ili amrudishe huku kwa sababu alikuwa amegoma kurudi, naye akatuacha tukiwa tumesogea dukani kwa Fatuma kuiangalia video aliyorekodi Ankia.
Hakuna kitu kilichokuwa kinawaua mbavu hawa watu zaidi ya kuona jinsi Shadya alivyomsukuma Tesha na kuanza kukimbia! Bi Zawadi, Fatuma, na Ankia walicheka mno. Tena Tesha alipofanikiwa kumfikisha Shadya hapo ndiyo kicheko kikalipuka kwa nguvu zaidi. Wanawake hawa waliongea sana, Tesha akakaa chini kabisa baada ya kuiangalia video hiyo, na Mariam akawa anamwangalia Shadya na sura yake iliyotisha huku akicheka.
Shadya alikuwa anasema ameishiwa nguvu miguuni, nami nikaelewa kwamba adrenaline kwenye mwili wake ilikuwa imepanda sana muda ule amekimbia na sasa ndiyo akawa anahisi nguvu kumtoka. Dah! Nilipenda sana. Akawa ananiambia nimemfanyia kitu mbaya sana na asingenisemesha daima, nami nikamwambia ningempa pole yake kwa kufanya atimue mbio namna ile, kisha nikawaomba wote kwa pamoja tuelekee ndani ili kutuliza hali.
Tukaelekea ndani kwao wakina Tesha, Shadya akionekana kuchoka vibaya mno, naye akafikia kukaa kwenye sofa kama vile ametoka kutua mzigo mzito. Muda ule tuko nje kabisa, ni Bi Zawadi pekee ndiye aliyekuwa ametoka kwa upande huu, yaani alimwacha Bi Jamila arudi kwa yule mwanamama mgeni aliyekuwa hapo mpaka wakati huu.
Mariam akawa ameondoa lile shuka jeupe mwilini mwake lakini ile sabuni usoni pake iliendelea kuwepo. Ankia akamfatia Shadya maji ya kunywa na kumletea, naye akaanza kunywa huku mama wakubwa, Tesha, Mariam, pamoja na huyo mwanamke mgeni wakiwa wanacheka kwa kuitazama ile video.
"Ahahaha... Mamu umeua! Ona Shadya anavyokimbia kama Chaplin!" Tesha akasema hivyo, na wengine wakacheka.
Nilikuwa nimekaa tu kwenye sofa pembeni nikitabasamu.
"Wee! Kwenye hali kama hiyo unadhani hata wewe ungebaki? We' si ulikuwa unajua ndiyo maana... kwani hujaona wale watu wengine wamekimbia?" Shadya akamwambia hivyo.
"Tena siyo kukimbia tu... Shadya umenisukuma! Yaani ilikuwa ni ile 'kufa mwenyewe huko!' Ahahahah aisee!" Tesha akasema hivyo.
"Shadya, mbona hukutuambia kama uliwahi kushiriki mashindano ya marathon jamani?" yule mmama mgeni akamuuliza.
Wengine wakacheka, naye Bi Zawadi akasema, "Mwenzangu! Ona hiyo miguu ilivyopauka, yaani katimua vumbi mpaka Masai huko! Hehehee nitalala nacheka leo."
Nikatabasamu na kumwangalia Mariam usoni. Nikaanza kuona kitu fulani kwenye uso wa binti huyo. Ni kama alikuwa anajaribu kuonyesha furaha yake kwa kuongea, lakini kwa sababu ya wengine kuendelea kuzungumza akawa anasita.
Hii ikanifanya nitamani kuwaambia wengine watulie ili Mariam aseme kitu fulani, lakini hiyo ingekuwa ngumu maana najua angebaki tu kimya kama ningefanya hivyo. Ingetakiwa kitokee kitu fulani cha kumsukuma yeye mwenyewe azungumze, na nilikuwa na hamu sana ya kuona hilo linafanikiwa.
"Mwanangu, nataka ni-edit kipande kidogo hii video nirushe tiktok. Itasumbua sana," Tesha akaniambia.
"Wee! Thubutu! Tena naomba muifute," Shadya akasema.
"Hakuna kuifuta. Leo Mamu kakuweza," Tesha akasema.
"Ifute! Ankia ifute," Shadya akaongea kwa mkazo.
"Subiri kwanza... nataka Miryam aje kuiona," Ankia akamwambia hivyo.
"Ahahaha... kweli Mimi inabidi aje acheke," Bi Jamila akasema.
"Sitaki, nimesema ifute. Ifute, ifute," Shadya akasisitiza.
"Mmm... we' naye! Kwani kuna ubovu gani Mimi akija kuiona?" Bi Zawadi akamwambia.
"Eti? Kwanza si na JC amekwambia atakupa pole?" Ankia akamwambia hivyo.
"JC ni mkuda tu na ye' naye. Kama vipi unipe tu pole yangu sasa hivi, ndiyo mtakuja kumwonyesha Mimi," Shadya akaniambia.
"Sasa pole gani unataka? Hela au?" Tesha akamuuliza.
Nikatabasamu kidogo na kutoa shilingi elfu kumi, na Shadya akaonekana kufurahi kwa jinsi alivyoniangalia.
"Hee! Baba, unataka kumpa yote hiyo kisa katimua mbio?" Bi Jamila akaniuliza.
"Eti mwanangu? Hapa anayepaswa kulipwa ni Mamu, hajatumia hata stunt double na akafanya improvisation. Usimpe huyo," Tesha akasema.
Kauli yake ikanifanya nicheke kidogo.
Shadya akamwambia, "We! Mimi hapa ndiyo wa kupewa pole, ningepata presha nikaanguka je? Si mngetoa zaidi ya hii pole anayonipa? Em' leta hapa."
Akaikwapua kutoka mkononi mwangu, huku wanawake wengine wakiguna kwa njia ya michambo. Shadya akaiingiza noti hiyo ndani ya nguo sehemu ya kifua chake, huku akiwa amekunja midomo yake kwa nyodo.
Nikamwambia Tesha, "Siyo mbaya akipoza koo kidogo maana najua ni lazima liwe kavu... kakisanua ile mbaya."
Wengine wakacheka kidogo, naye Shadya akasema, "Ila wewe Mamu wewe! Kwanza si mmnawishe huo uso mwishowe tuote vinyemela usiku."
"Eeh kweli, Tesha kamnawishe mtoto basi, yasije yakamwasha machoni hayo masabuni," Bi Jamila akamwambia.
Ni hapa ndiyo tukasikia honi ya gari nje ya geti, nasi kwa pamoja tukaelewa kwamba ilikuwa ni Miryam.
"Hah! Ngoja nikamfungulie Mimi aje kucheka hapa," Tesha akasema hivyo na kuelekea nje upesi.
Hii ilikuwa ni mida ya saa tatu kasoro sasa, na Ankia akamwambia Mariam, "Twende ukanawe uso my. Miryam asikukute hivi."
Lakini Mariam akatoka upande aliokuwa amekaa karibu na Ankia na kuja kwangu, naye akakaa karibu nami huku akiniangalia kwa shauku na kunishika mkononi kwa nguvu. Nikawa nimemwelewa.
"Ih, vipi tena Mamu?" Ankia akauliza.
"Anataka dada yake amwone akiwa hivi, ndiyo atanawa baadaye," nikamwambia.
"Aaa... ili Mimi acheke vizuri? Hahahah Mariam leo umetukosha sana jamani," akasema hivyo yule mwanamke mgeni.
Tulikuwa tunasikia jinsi geti lilivyofunguliwa, gari kuingia, na kisha likafungwa tena. Baada ya sekunde chache, Tesha akawa ameingia ndani tena akiwa amebeba mifuko miwili mikubwa yenye vyakula inaonekana, na dada yake ndiyo akafuata. Wote walikuwa wanatabasamu baada ya Miryam kuingia, nami nikamtazama kwa upendezi.
Wakati huu alikuwa amesuka nywele zake ndefu kwa mtindo wa rasta zilizokwenda pande tofauti, lakini mwanzoni tu mwa kichwa chake kufikia utosini, halafu kutokea hapo ziliachwa zile laini ambazo zilimwagikia nyuma mpaka kufikia mgongoni. Alizipamba kwa kuziwekea urembo wa vidude vidogo-vidogo vyeupe kwenye kila pande ya kichwa, na mtindo huo ulimpendezesha sana kuunganisha na sura yake hapo kati ambayo ilikuwa ni nzuri vibaya mno.
Leo alikuwa amevaa blauzi laini yenye mikono mirefu iliyofanana na ngozi ya twiga, pamoja na suruali nyeusi pana ya kitambaa laini ambayo pamoja na upana wake bado umbile hilo lilichoreka vizuri. Akiwa tu ndiyo ameingia kabla hata ya kutoa salamu, akawa amemwona Mariam pembeni yangu, naye akabaki akimtazama kimaswali. Wengine wakaanza kutabasamu na kucheka, ndipo Mariam akaniachia na kumfata dada yake upesi.
Tesha ndiyo akawa amerejea hapo baada ya kutoka kuipeleka mifuko ile jikoni, naye akaanza kusema, "Yaani Mimi hauwezi...."
Nikasimama na kunyanyua kidole changu kimoja kumwelekea, kwa njia ya kumzuia asiendelee kuongea, naye akatulia. Wengine wakaona hilo, nami nikarudisha umakini wangu kwa Mariam, hivyo wote wakamwangalia.
Mariam alikuwa amemshika Miryam mikononi huku akitabasamu na kupumua haraka-haraka, naye Miryam akamuuliza, "Mamu? Mbona... umepaka nini usoni?"
Mariam akanyanyua kidole juu, akipindisha shingo yake kiasi na kuonekana akitaka kuongea, nasi wote tukawa tumebaki kumtazama kwa matarajio mengi.
"Dada... hhh... dada... nihhh... nimemkimbiza... sshangazi!"
Nilipandwa na msisimko fulani mzuri sana baada ya kumsikia binti huyo akizungumza namna hiyo. Nikamtazama Tesha na kukuta ameachama kwa kushangaa, Bi Zawadi akiwa amefunika mdomo wake kwa kiganja, Ankia akiwa ndiyo anasimama kutoka sofani kwa njia ya mshangao, na hata Shadya akasimama pamoja na Bi Jamila.
Nikamwangalia Miryam na kuona akimtazama mdogo wake aliyekuwa anacheka kwa furaha, naye akasema kwa sauti ya chini, "Umefanyaje?"
"Nimemkimbiza... ssh.. Shadya!" Mariam akajibu.
Miryam alikuwa ameshika mkoba mkononi, lakini ukamdondoka kwa kile kilichoonekana kuwa mshangao. Sote hapo tulijawa na furaha sana yaani, sikujua kiwango cha furaha hiyo kwa wengine lakini mimi hapa, nilikuwa narukaruka sana ndani ya moyo wangu.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments