MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA TISA
★★★★★★★★★★★★★★★★
Mariam alikuwa na sauti nzuri, na hapo alipoongea alikuwa ameitoa yote. Hii ilimaanisha nini? Michezo tuliyokuwa tumeianza ilikuwa inamsaidia binti huyo kurejesha utaratibu mzuri kwenye ubongo wake, na hasa sasa nikawa nimetambua zaidi kwamba ni furaha aliyokuwa akiipata kwa kucheza hivi ndiyo iliyokuwa inafunika ile huzuni iliyosababisha akaanza kuumwa.
Wengine walikuwa wanamwangalia binti kwa kustaajabu, yeye mwenyewe asielewe kwamba hiyo ilikuwa ni pindi yenye kugusa nyoyo za wapendwa wake kwa kiwango kikubwa, naye akaushika mkono wa Miryam na kuanza kumvuta kuelekea pale Ankia alipokuwa amesimama.
Walipomfikia Ankia, Miryam akawa amesimama pembeni yangu, naye Mariam akamwambia Ankia, "Mwonyeshe."
Ke! Yaani sisi tulikuwa tumemezwa na butwaa la kuona binti ameanza kuongea vizuri lakini yeye alikuwa anataka tu kumwonyesha dada yake kilichofanya afurahi namna hiyo. Ankia akaninyooshea simu yangu ili nitoe lock, nami nikaiwekea kidole ili ifunguke. Ilipofunguka, Ankia akaweka ile video ya Shadya, naye Miryam akaanza kuiangalia.
Mariam akaendelea tu kucheka na makeup yake usoni, naye akasema, "Ona... anakimbia upande-upande kama bata!"
Oh Mungu! Nilijihisi vizuri sana aisee. Wiki moja tu nikawa nimefanikiwa kuanza kumkarabati vyema huyu binti.
Miryam akawa anacheka kwa pumzi, lakini kwa ile njia kama vile alikuwa anataka kulia. Najua video ilikuwa imemfurahisha lakini niliona furaha yake kuu kuwa kusikia mdogo wake akizungumza tena bila kujikwaa sana, naye akamwangalia usoni kwa hisia. Hata akacheka kidogo kwa pumzi, nami nikaona machozi yakimlenga.
"Mariam..." Miryam akamwita hivyo.
"Bee..." Mariam akaitika.
"Umenifurahisha sana. Nani ameku... nani amekuchora hivi halafu... ukamkimbiza shangazi?" Miryam akamuuliza tena.
Mariam akaniangalia na kunisonta, akionekana kutaka kusema jina langu lakini kukawa na ugumu fulani, hivyo akaishia kuachama tu.
"Ni wewe?" Miryam akaniuliza.
Nikamwambia, "Ni sisi wote tumechangia."
"Kasoro aliyekimbia kama bata," Tesha akasema hivyo.
Wanawake wengine wakacheka kidogo, naye Shadya akamwambia Tesha "Na we' nitafute sasa!"
Miryam akamshika Mariam usoni, kisha akamkumbatia kwa upendo.
Ilikuwa ni pindi yenye kugusa sana moyo ambayo kiukweli sikuwa nimetarajia ingefika hapa kwa muda mfupi namna hiyo. Yaani wazo langu mapema ilikuwa ni kufanya tu kioja pamoja na Mariam ili aendelee kuchangamka, lakini sikutarajia uchangamfu wake uonyeshe matokeo mazuri mapema mno kama haya ya sasa. Mama wakubwa walikuwa wanatokwa na machozi kabisa. Walikuwa watu wa hisia sana, nao wakawasogelea Miryam na Mariam kujiunga nao kwenye kumbatio.
"Jamani! Hadi raha," akasema hivyo yule mama mgeni.
"Umeona eh?" Shadya akamwambia hivyo huku akitabasamu.
Wanne hao wakiwa wameendelea kukumbatiana namna hiyo, Miryam akapandisha macho yake na kuniangalia. Nikawa namtazama kwa utulivu tu, naye akashusha pumzi na kuwaachia wenzake ili kumbatio hilo livunjwe hatimaye. Ankia akanisogelea na kunipiga kidogo begani kwa njia ya kusifia, naye Tesha akanipigia saluti ndogo ya kishkaji.
"Ahah... umependeza sana," Miryam akamwambia hivyo Mariam.
"Asante," Mariam akamjibu hivyo.
Sisi wengine tukacheka kidogo, na Tesha akasema, "Yaani dada ungekuwepo... ungegalagala kwa kucheka."
"Nataka kujua ilikuwaje. Nataka Mariam anisimulie," Miryam akasema hivyo kwa sauti yake tamu.
"Njoo... hapa..."
Mariam akamwambia hivyo Miryam na kumkalisha dada yake sofani. Akanivuta mkono pia ili nikae hapo hapo, hivyo nikawa nimekaa pamoja na dada hawa wawili, Mariam akiwa katikati. Akaanza kuongea.
Alijitahidi sana kuzungumza ijapokuwa maneno mengi aliyatafuta mno kichwani, na wote tulikuwa tukimsikiliza alipoongea kwa furaha na kufurahi pamoja naye. Miryam mpaka akajikuta anadondosha chozi kutokana na furaha aliyokuwa akihisi, naye Mariam akamalizia kumsimulia kwa kusema Tesha alicheka mpaka akakaa dhini.
"Yaani nyie ngojeni tu. Mmenigeuza kituko chenu leo ila na nyie nitakuja kuwaonyesha," Shadya akasema hivyo.
"Aaa, bado unalalama nini Shadya? Si pole umepewa?" Tesha akamwambia hivyo.
"Hata kama. Mnanicheka sana," Shadya akasema kwa njia ya kuudhika.
"Ahahah... Basi tunaacha kukucheka. Mamu... twende nikakusafishe uso uje ule. Unajua nimekuletea nini?" Miryam akaongea hivyo.
Mariam akatikisa kichwa kuonyesha hajui.
"Kitimoto," Miryam akamwambia.
Mariam akatabasamu kwa furaha, naye akasimama upesi.
Miryam akasimama pia, na ni wakati huu ndiyo akawa ametilia maanani uwepo wa yule mmama mgeni hapo ndani na kumsalimia, kisha akawasalimu na mama zake wakubwa na Ankia. Wakampa pole ya kazi, naye pia akaomba radhi kwa kuchelewa lakini wakamwambia kwamba haikuwa na shida.
Ankia akawa amemwambia Miryam kuwa mimi na yeye tungeondoka sasa kwenda kwetu, lakini Miryam akakataa. Akasema tutulie kwanza ili tupate chakula pamoja kisha ndiyo twende, kwa sababu alikuwa ameleta cha kutosha. Ankia na mimi tukawa wapole. Kwa hiyo akaondoka pamoja na mdogo wake baada ya kutuambia tutulie hapo, nasi tukakaa kuwasubiria.
Kilichofuata ilikuwa ni maongezi zaidi yenye kufurahisha kuhusiana na Mariam, na hata mara kwa mara Tesha angemtania Shadya, aliyekuwa amenuna kimasihara bado. Dada wale wawili wakawa wamerejea, wakati huu Miryam akiwa amevaa dera pana la zambarau na kilemba kilichofunika nywele zake kwa mbele, na Mariam alikuwa safi zaidi kwenye uso wake.
Miryam akaelekea jikoni, na Ankia akamfata kwenda kusaidiana naye kuandaa vyakula. Oh inaonekana bibie Miryam alikuwa ameleta vyakula vilivyotengenezwa tayari maana harufu nzuri ilikuwepo hewani baada ya wao kwenda kuifungua ile mifuko aliyokuja nayo.
Sisi tukiwa sebuleni tukiendelea kujaribu kumfanya Mariam aendelee kuzungumza, wanawake hao wawili ndiyo wakaanza kutuletea sahani za mmoja mmoja zenye vyakula pendwa kama chips kavu, kipande cha nyama ya kuku, na nyama za kitimoto kwa wingi. Na ilikuwa kama ameotea yaani kuleta msosi mtamu namna hiyo kwenye siku ambayo mdogo wake alikuwa ameanza kuzungumza tena, na baada ya kila mmoja kupewa yake na Ankia kutunawisha, makamuzi yakaanza.
Tukala huku tunapiga story, na hiki ni kitu ambacho lazima nikiseme kwa mkazo, kwamba kila mara ambayo ningemwangalia Miryam na yeye kunitazama, macho yetu yangetulia yakiangaliana kwa sekunde chache, kama vile yanatafakariana, na bibie ndiyo angevunja utizami huo na kuendelea kula taratibu.
Ilinifanya nione mtazamo mpya ndani ya mwanamke huyo kunielekea, yaani bado hakuwa ameniambia kitu chochote lakini macho yake tu yalitoa shukrani za dhati kwa yote niliyokuwa nafanya ili kumsaidia mdogo wake.
Nikawa najihisi vizuri sana rohoni, nikitazamia kwamba huenda hii hata ingeanza kutengeneza msingi mzuri wa urafiki baina yangu na huyo mwanamke, na sijui kwa nini tu lakini nilitamani sana tuwe marafiki. Tena hiyo ilikuwa ni kutokea mara ya kwanza kabisa nimekutana naye. Ningepaswa tu kusubiri kuona.
★★
Kwa hiyo tukawa tumemaliza msosi na kukaa hapo mpaka mida ya saa tano. Mariam alikuwa binti aliyezoea kulala mida ya saa tatu, saa nne, kwa hiyo hapo tayari alikuwa zake chumbani amesinzia muda mfupi tu baada ya sote kumaliza kula. Kwenye hii mida ya saa tano, yule mwanamke aliyekuja kuwatembelea mama wakubwa akaona aage hatimaye.
Alikuwa anafahamiana sana na marehemu mama yao wakina Tesha, na alikuwepo kusaidiana na akina Bi Zawadi na Bi Jamila katika kipindi ambacho wazazi wa ndugu hawa walikuwa wamepoteza maisha, na leo alikuwa amekuja kuwasalimia. Sikujua sana ila inawezekana hata huo mlo mtamu ambao Miryam aliuleta ulikuwa kwa ajili ya ujio wa mwanamke huyo.
Kwa sababu aliishi maeneo ya Toangoma, Miryam akawa amemwitia usafiri wa bodaboda fulani aliyejuana naye aje kumchukua na kumpeleka barabarani pale Mzinga ili mama wa watu akapande daladala. Mimi na Ankia tukatumia nafasi hii pia kuaga na kutoa shukrani kwa ukarimu wa familia hii, nao wakatupa heri nzuri ya usiku pia.
Wanawake hawa, hasa mama wakubwa, walikuwa wanapenda sana Tesha na mimi tulipoongea vitu vilivyowachekesha, nasi tukatoka nje baada ya yule bodaboda kufika tukiwa tunawafurahisha wote kwa story zetu. Yule mama akapanda zake boda, huyoo akasepa. Sisi, yaani mimi na Ankia, tukazungukia upande wetu huku tukiendelea kuzungumza na hawa majirani zetu kwa shauku.
Tulikuwa tumeshazoeana sana na mama wakubwa, walinipenda kweli, hasa kutokana na kuwa na utani pamoja nao wa kuwafanya wajihisi vijana. Kwa kuwa nafasi ilikosekana ya kuongea na Tesha kuhusiana na ishu yake na Winny, akawa ameniambia angenisimulia kesho, nami nikaridhia.
Sikuwa nimeongea lolote pamoja na Miryam kuhusiana na mdogo wake kwa wakati huu, kwa hiyo ningepaswa kusubiri tu maana najua alikuwa na nia ya kutaka kujua kiundani zaidi kuhusu maendeleo ya mdogo wake kutokea hapo. Nilifurahia sana usiku huu, yaani kama Ankia asingekuwa kipindi cha P, angekoma huko ndani!
Tukaingia zetu tu ndani na kwenda kujipumzisha, nikiwa na hamu na yale ambayo siku ya kesho ingeyakaribisha.
★★★
Pakakucha hatimaye, ikiwa ni Jumapili takatifu kwa wengi. Nilikuwa nimeamka mida ya saa kumi na mbili alfajiri lakini nikajirudisha tena usingizini, na sasa nikawa nimeamka mida ya saa tatu asubuhi. Sikutoka kitandani, bali nikavuta simu yangu iliyokuwa inaita kwa muda fulani sasa.
Nilikuwa nimeona uvivu tu kuichukua mapema, na sasa nilipoangalia mpigaji nikakuta ni Soraya. Kunipigia mapema ya saa tatu namna hii haikuwa kawaida yake, yaani hata hakuwa na kawaida ya kunipigia kwa sababu tulizoea kuwasiliana kwa sms, lakini nikapokea na kusikilizia.
"Halloo..." sauti yake ikasikika.
Nilikuwa nimelaza uso kwa upande huku simu ikiwa sikioni kwa juu, nami nikiwa nimefumba macho nikamjibu, "Halloo."
"JC jamani... mbona unanitesa?" akaongea kwa sauti ya kubembeleza.
"Ih, me nimekufanyaje tena?"
"Ina maana hujui?"
"Nisingeuliza."
"Sawa. Basi asubuhi njema," akasema hivyo.
"Na kwako pia," nikamwambia hivyo.
Akatulia kidogo, kisha ndiyo akakata simu.
Nikatabasamu kiasi na kuiweka simu pembeni.
Soraya alikuwa anafikiri ningeanza kumbembeleza lakini akawa amekosea namba. Siyo kwamba labda sikumtaka tena ila najua alikuwa ameshadata na mimi kwa hiyo hata kama ningefanya nini, najua angerudi mwenyewe tu. Nikaamua kunyanyuka ili nikafanye usafi wa mwili kisha mengine kama kunywa chai yafuate.
Hiyo wiki yote iliyoisha sikuwa nimefanya mzunguko mwingine wowote mbali na Mbagala zaidi ya nilipokwenda kukutana na yule askari mpelelezi Ramadhan, kwa hiyo nikawa nafikiria labda leo ingefaa kama nikitoka kwenda sehemu kupiga mbili tatu pamoja na Ankia na Tesha. Uzuri kulikuwa na mechi ya Simba kwa hiyo kwenda kuitazama na kuburudika pamoja na hao marafiki zangu lilikuwa wazo zuri.
Ankia tayari alikuwa ameshaamka na kufanya usafi, na wakati huu alikuwa akikanda unga wa ngano ili atengeneze mkate mkubwa. Tena angeukaangia, sijui kuubanikia, kwenye sufuria, nami nikampongeza na kusema nasubiri kwa hamu kunywa chai pamoja na mautashi yake ya kupika.
Nikaendelea kukaa sebuleni kwa muda fulani mpaka pale marafiki wawili wanawake wa Ankia walipokuja kumtembelea sijui, ama labda kwa biashara zao wajuazo wenyewe. Mimi nikaingia chumbani bila hata ya kuonana nao maana nilitoka sofani wakiwa ndiyo wameukaribia mlango, kwa hiyo nikajichimbia chumbani kwangu na simu yangu nikisoma mambo fulani.
Nilipomaliza, nikaweka tu simu pembeni na kuamua kutafakari vitu. Upande wa vita yangu dhidi ya tatizo la Mariam ulionekana kuanza kunipa ushindi, lakini kwa upande wa vita yangu dhidi ya mke wa Chalii Gonga bado ulisua. Mara kwa mara askari Ramadhan alikuwa amenitafuta kuuliza kama kuna maendeleo yoyote au jambo jipya, nami nilimjulisha kwamba bado kumetulia.
Ila huu ukimya wa Bertha uliniwazisha kiasi. Inawezekana alikuwa akifuatilia mambo fulani kuhusu mimi bila mimi kujua, huenda kwa hizo siku chache zilizopita akiwa ametumia watu wake kunichunguza. Nilikuwa na uhakika kabisa kwamba hakuna sehemu yoyote ile ambayo ningejikamatisha vibaya kwa lolote, kwa hiyo hata kama angenifatilia hangeona nuksi yoyote. Hata makutano yangu na huyo askari yalikuwa ya siri na yaliyopangwa kwa akili.
Ingekuwa rahisi kusema ah ninajipa presha tu bila maana yoyote lakini huwezi kuwa na hakika sikuzote kwamba mambo yatakuwa sawa tu na kutofikiria njia mbadala za kuepuka matatizo ambayo hufikirii yatatokea, kwa hiyo nikawa nawaza nini nitafanya hiki kikitokea, au nini nifanye kile kisipotokea. Hata yale madawa niliyotengeneza nilikuwa nimeyaweka sehemu salama na kwa kificho ili Bertha akiyaomba tu, ayapate, na kutokea hapo ndiyo mipango ianze kazi kwa kasi.
Bwana, nikiwa nimejilaza tu kitandani hapo simu yangu ikaanza kuita, na mpigaji alikuwa ni Bi Zawadi. Nikapokea na kumsalimia, naye akaniuliza ikiwa nilikuwa na kazi. Nikakanusha hilo, ndiyo akaniomba niende hapo kwao sasa hivi maana kuna jambo la muhimu alikuwa anataka ashiriki nami. Nikamwambia anipe dakika chache tu nami ningekuwa nimeshafika. Simu ikakatwa.
Nilikuwa nawaza kwamba bila shaka jambo hilo lingekuwa linamhusu Mariam, na kwa kufikiria pale nilipomwacha binti huyo kihali hiyo jana, ingekuwa muhimu kwenda kuona hali yake iko vipi kwa sasa. Hivyo, nikatia nguo safi mwilini na kujitengeneza vyema kama kawaida yangu, nami nikatoka chumbani.
Hapo sebuleni nikakuta Ankia akiwa amekaa pamoja na wale marafiki zake wawili. Wote sikuwahi kuwaona kabla; mmoja alikuwa mweusi wa maji ya kunde, mwingine alikuwa mweupe. Na nadhani wote walikuwa waislamu maana walivaa hijab vichwani, na nguo ndefu kama mabaibui au kanzu za kike. Wee!
Hawa nawajua. Huwa wanavaa kitakatifu kwa nje ila ndani sasa! Tena na hako keupe kalikuwa kameweka na pini iliyozunguka tobo moja la pua, ndiyo nikajua hapo kwisha kazi!
Lakini mimi nikawa makini tu na kufika usawa wa sofa alilokalia Ankia, nami nikamwambia, "Natoka."
"Ih, wapi tena?" Ankia akauliza.
"Warembo wangu wananiita," nikamjibu hivyo.
Ankia alielewa namaanisha mama wakubwa hapo jirani, naye akasema, "Chai je?"
"Ngoja nikawasikilize kwanza. Mambo vipi?" nikasema hivyo na kuwasalimu hao wadada.
"Safi..."
"Poa..."
Wakajibu huku wakiniangalia kwa umakini.
Nikamwangalia Ankia na kusema, "Badae.'"
"Haya," akanijibu.
Mimi huyoo nikatoka hapo kama vile najali muda. Sijui hao wanawake walifika hapo wakiwa na dhumuni lipi lakini macho yao yalionyesha kutaka masilahi fulani. Ah potelea pote, akili yangu ikakazia zaidi mwito wa warembo wangu Bi Zawadi na Bi Jamila.
Nilipotoka na kufika getini kwao Tesha, nilimwona yule Fatuma wa dukani akiwa amekaa kwenye kiti hapo nje pamoja na mwanaume kijana, wakionekana kuongea, nami nikagonga geti na kusubiri lifunguliwe.
Nikamwona huyo Fatuma akiwa anamwonyeshea huyo kijana kwa kidole kunielekea mimi, kisha akaanza kucheka huku huyo kijana akinitazama. Kwa haraka nilitambua kwamba alikuwa anamsimulia kile kituko cha usiku wa jana, nami nikakaza tu na kutazama muda kwenye simu.
Ikiwa inaelekea kuingia saa tano sasa, mlango mdogo wa geti hilo ukafunguka, na ni Tesha ndiye aliyekuwa amenifungulia. Tukasalimiana vizuri sana kirafiki, nami nikaingia na kukuta pickup ya Miryam ikiwa hapo nje, kisha tukaanza kuelekea ndani pamoja. Tesha akawa amegusia kwangu kuhusu kwenda kuitazama mechi ya siku hii baina ya Simba na Singida, nami nikampa uhakika kwamba tungekwenda kuiona kwa pamoja baadaye.
Tulipoingia tu ndani hapo, nikakuta mama wakubwa wakiwa wamekaa sofa moja, na Mariam akiwa amekaa kwenye lingine pamoja na bibie Miryam.
"Ah warembo wangu hao! Shikamoo ziende kwenu jamani," nikawapa salamu.
Wakaniitikia huku wakitabasamu kwa furaha, na baada ya Mariam kuniona, akatoka sofani na kunifata mpaka niliposimama huku akitabasamu.
"Vipi Mamu?" nikamwambia.
"Poa. Sh..kamoo," akaniamkia.
"Marahabaa. Hi-five," nikasema hivyo na kunyanyua kiganja changu juu.
Mariam akagongesha kiganja chake hapo kirafiki.
Nikamwangalia Miryam na kuona anatutazama huku akitabasamu kiasi, nami nikamwambia, "Za asubuhi?"
"Safi. Karibu," akanijibu.
Hako kasauti sasa! Na alikuwa amependeza kweli kwa nguo aliyovaa ingawa hakuonekana kutaka kutoka kwa siku hii.
"Karibu ukae baba," Bi Jamila akaniambia hivyo.
Nikaketi kwenye sofa pembeni yake Tesha, naye Mariam akakaa kwenye mkono wa sofa hilo hilo karibu nami. Nadhani alikuwa na hamu ya kuona tungefanya michezo ipi kwa leo. Kulikuwa na harufu ya nyama niliyovuta upesi baada ya kukaa hapo, nami nilielewa ilitokea jikoni.
"Shadya ametoka?" nikawauliza.
"Aende wapi wakati sasa hivi anatrend tiktok? Yuko jikoni anajua akitoka tu nje atavamiwa na paparazzi," Tesha akasema hivyo.
Mara ghafla Shadya akatokea jikoni akiwa ameshika kijiko cha kupakulia mboga na kusema, "Halafu Tesha naomba unitoe mdomoni mwako, sawa?"
Wote tukacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Si ni JC ndiyo kakuulizia jamani?"
"Si ungemwambia tu niko jikoni, paparazzi wametokea wapi? Wewe! Nitakukoa na hili likijiko!" Shadya akamwambia hivyo Tesha huku akimnyooshea kijiko kweli.
Tukacheka tena kwa pamoja maana inaonekana vita ya Tesha na Shadya bado haikuwa imeisha.
Miryam akawa anacheka bila kutoa sauti, naye Bi Zawadi akamwambia Tesha, "Mwache mwenzio bwana, atakuja akukoe kweli."
"Yaani hili!" Shadya akasema hivyo.
"Ahah... shikamoo," nikamsalimu Shadya.
Akasonya kidogo kuondoa kero ya Tesha, kisha akaniambia, "Marahaba mwaya. Karibu."
"Asante," nikamjibu hivyo.
Tesha akaniangalia machoni kwa njia ya kuudhika lakini kikejeli, nami nikamwelewa. Ni ile kwamba mimi ndiyo niliyekuwa msababishi wa kumfanya Shadya awe kituko jana, lakini Tesha ndiyo alikuwa anarushiwa vijembe kwa kumtania kidogo tu halafu mimi mastermind nikawa natendewa vizuri.
Nikatabasamu kidogo na kumwambia, "Siyo makosa yangu, we' ndo' unamchokoza sana."
"Aa wapi, we' umemkuna tu jana kwa kale kamsimbazi ndo' maana anakufagilia," akanijibu hivyo.
Ilikuwa kidogo tu nimwambie 'acha ujinga,' lakini nikajituliza na kumwangalia Bi Zawadi. "Cheupe wangu vipi?" nikamsemesha.
"Safi tu," akanijibu hivyo.
"Haya niambie. Kuna ishu gani mpya weye? Ama... ni ya sisi wawili tu, tutaongea baadaye?" nikamuuliza hivyo.
Bi Zawadi akacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Ishu gani tena? Mtufahamishe."
"Hamna wala. Nilikuita tu... uje tunywe supu pamoja. Shadya anatengeneza makongoro. Unayajua?" Bi Zawadi akaniuliza.
"Ahaa... ee nayajua. Basi nikafikiri labda kuna tatizo," nikasema hivyo.
"Hapana baba, tunapenda tu ukiwepo hapa. Umetusaidia sana kurudisha sehemu kubwa ya furaha kwenye hii nyumba," Bi Jamila akaniambia hivyo kwa upole.
Nikatabasamu na kumwangalia Miryam, ambaye alikuwa ameweka macho makini kwenye simu yake. Ni kama vile akili yake ilikuwa mbali kiasi kwa sababu fulani, kwa hiyo nikarudisha umakini wangu kwa mama wakubwa.
"Wengine wakajaribu na kushindwa mpaka kulegea, eti ooh mwanenu ni chizi, kichaa, aende wapi wapi sijui... si huyu hapa umemsaidia? Tena hata mwezi haujaisha," Bi Zawadi akasema hivyo.
"Kweli. Kila daktari na dawa yake, halafu ya JC ndiyo original sasa. Kama masihara tu kaanza, cheki sasa hivi! Nakubali sana mwanangu. Sana," Tesha akaniambia hivyo.
"Ah usiwaze... tuko pamoja," nikamwambia hivyo.
"Siyo rahisi kupata mtu kama wewe siku hizi ambaye... ambaye anaweza kujitoa, akatumia muda wake kufanya mambo mengi kama unayofanya kwa ajili ya Mamu bila kutegemea malipo. Yaani... JC umenigusa sana. Jana Mariam kuanza kuongea... ni kitu nilichokuwa nasubiri kwa hamu kuja kukiona. Kama umeweza kumfikisha hapo basi ina maana utamfikisha mbali zaidi. Unastahili malipo makubwa zaidi ya yale yote ambayo Mimi alitoa kujaribu kumsaidia mdogo wake lakini watu wakamfanyia ulaghai tu... baba, yaani tunakushukuru sana," Bi Jamila akaongea hayo kwa hisia.
Nikajikuta hadi nakosa la kusema na kubaki nikitazama tu chini, nikiwa nahisi amani sana moyoni kupokea shukrani hiyo ya dhati.
Tesha akasema, "Ni kweli bro. Wote hapa tunakukubali sana. Mama zetu hawa, Mamu, mimi hapa, Mrs. Paparazzi kule..."
Sote tukacheka kidogo.
"Na Miryam pia. Tena dada anakukubali kichizi yaani, usimwone amekaa tu hivyo amebunda, anakuelewa sana. Huwa anasema hapa 'yaani JC ni jembe kali sana!'"
"Tesha..." Miryam akamwita hivyo kwa sauti ya chini kama kumwonya.
Wengine wakacheka kidogo, nami nikashindwa kujizuia kutabasamu na kucheka kidogo kwa pumzi. Nilijua Tesha alikuwa anaongeza chumvi tu, lakini alionyesha kwamba uthamini wa familia yake nzima kunielekea aliujua.
Mariam akanishika begani, nami nikamwangalia. "Tutacheza... mm..muziki... baadaye?" akaniuliza hivyo.
Nikatabasamu na kumwambia, "Leo tutapumzika, sawa? Mpaka kesho. Nataka nikufundishe mchezo mwingine kesho. Utaupenda... sawa?"
Akatabasamu na kutikisa kichwa kidogo kuonyesha uelewa.
"Hamtacheza leo?" akaniuliza hivyo Bi Zawadi.
"Ee, leo mapumziko, kesho tutaendelea. Nimemnywesha-nywesha maziwa akayazoea, sasa hivi nitaanza kumpa msosi mgumu kidogo ili akae sawa zaidi. Si mnaelewa?" nikawaambia hivyo.
"Ndiyo baba, inaeleweka. We' endelea tu na utaratibu wako, ujue sisi tutakupa support yote," Bi Jamila akaniambia hivyo.
"Da' Mimi, mbona uko kimya tu? Mpe maua yake mwana huyu, tena mpe ya kimombo. Oya, dada anajua kiingereza huyo!" Tesha akasema hivyo.
"Usinambie," nikatoa jibu hilo.
Mama wakubwa wakacheka kidogo, nami nikamtazama Miryam machoni na kuona ananiangalia kwa macho yenye utafakari. Niliona wazi kwamba akili yake ilikuwa imemezwa na jambo tofauti na hili lililokuwa likiendelea hapa japo alikuwa msikivu wa mada nzima, na hakuna mtu yeyote ambaye aliona hilo isipokuwa mimi.
Nikiwa bado namwangalia mwanamke huyo, sauti ya Shadya ikasikika kutokea jikoni ikisema, "Mimi... tayari."
Nikajua tu kiongozi wa mapishi ndiyo alikuwa anaitwa ili kwenda kusababisha zaidi huko jikoni, naye Miryam akanyanyuka tu na kupita upande wangu kuelekea huko. Ah mwanamke alikuwa na mguu huyu! Niweke tu heshima pembeni aisee, yaani Miryam alikuwa moto!
Moja kati ya wale wanawake waliobarikiwa karibia kila kona ya miili yao halafu sasa alijua kujitunza. Harufu yake iliyopitishwa na upepo aliponipita ikanifanya hadi nifumbe macho kuisikilizia zaidi, ila nikajitoa mbali kote huko kifikira na kuirudisha ile heshima niliyokuwa nimeiweka pembeni kwa muda mfupi. Kama nilivyokuwa nimesema awali, huyo alikuwa wa kumwacha tu hivyo hivyo.
Kwa hiyo sisi wengine tukaendelea kuongea mambo kadha wa kadha kupisha muda, na tukimsaidia Mariam aendelee kutia jitihada ya kuongea, ndipo Shadya pamoja na Miryam wakaanza kuleta supu za nyama ya kongoro kwenye mabakuli mapana ya udongo.
Walianza kwa kuwapatia mama wakubwa supu zao na ya Mariam, nao wakaamua kushuka chini na kukaa ili wanywe kwa kujinafasi, naye Mariam akaenda kukaa pamoja nao hapo chini pia. Shadya na Miryam wakatuletea supu mimi na Tesha; Shadya akimpa Tesha yake, na Miryam akinipatia ya kwangu.
Alipokuwa ameinama kiasi kunipatia bakuli hilo, nikalipokea huku nikimtazama usoni kwa umakini, na macho yake mazuri yakaniangalia pia. Ilikuwa kama nimemezwa na hali ya kutaka kupata maana yoyote ile ya utizami wake kwangu mpaka nikawa sikazii fikira ni jinsi gani bakuli hilo lilikuwa likiunguza viganja vyangu. Sikuona ujumbe wowote ule kwenye macho yake zaidi tu ya uzuri yaliyokuwa nao, naye akaacha kuniangalia na kurudi tena jikoni.
Ni hapa sasa ndiyo nikahisi jinsi mikono yangu ilivyochomwa. Woi! Nikaliweka bakuli kwenye mkono wa sofa na kujikausha, nikiwa nakaza maumivu, ndiyo baada ya kutulia nikaanza kunywa thupu. Na ilikuwa "thupu" tamu sana.
Miryam na Shadya wakarudi sebuleni tena wakiwa na mabakuli yao pia na kuketi pamoja kwenye sofa la pembeni. Nyama za kongoro zilikuwa nyingi, naye Tesha akawa ameniambia kwa sauti ya chini kwamba Shadya ndiye aliyekuwa ameagiza ziletwe ili wazipike, akihisi huenda mwanamke huyo alitumia hela yake kujumuisha na pole niliyompatia jana kuzinunua.
Ilikuwa nyama nyingi sana yaani ilikuwa ni kunywa, kutafuna, na kushiba kabisa kama kiamsha kinywa. Ilivyo laini na yale mamifupa sasa! Tukaendelea kujinoma taratibu, na niligundua kwamba bibie Miryam alikuwa amejiwekea kiasi kidogo sana, hivyo yeye ndiyo akawa amewahi kumaliza na kurudisha chombo chake jikoni.
Kidogo tu nikawa nimetumiwa ujumbe kwenye simu, nami nikautazama na kukuta ni Ankia ndiye aliyeutuma. Alikuwa ananifahamisha kwamba ametoka pamoja na wale marafiki zake kwenda mahala fulani, na alikuwa amerudishia tu mlango wa kule ndani si kuukaza kwa funguo. Nikamjibu tu poa, tutaonana baadaye, nami nikaweka simu pembeni.
Tukaendelea kufurahia supu na maongezi mepesi ndani hapo, huku nikiwa makini kutambua mbadiliko mwingine wowote wa kitabia kwa binti Mariam kadiri alivyoendelea kula, na ndipo tukasikia geti huko nje likigongwa.
Tesha akataka kuacha kula ili aende kuona ni nani yupo huko nje, lakini Miryam akamzuia na kusema yeye ndiyo angeenda kufungua. Alitoa kauli ya kwamba anaenda kufungua, siyo kuona ni nani yupo huko nje, na hiyo ikanifanya nitambue kwamba kuna mtu aliyekuwa anamtarajia afike hapo; labda mgeni wake.
Akatoka ndani, sisi tukiendelea tu kutulia hapo na mama wakubwa, kisha baada ya sekunde chache bibie Miryam akarudi tena. Alianza kuingia yeye, kisha nyuma yake wakafata watu wawili. Kila mmoja hapo ndani, hata mimi, tulishangaa sana baada ya kumwona Joshua akiwa hapo! Yaani ilikuwa ni ujio mmoja wa ghafla sana ambao hakuna yeyote hapo alikuwa ameutegemea kabisa.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments