MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Nikiwa nafikiria kurudi ndani kwanza kutokana na kiatu changu kukatika, Ankia ndiyo akawa amerejea. Alipendeza sana kichwani kwa kusuka nywele ngumu zenye mtindo wa mawimbi kama tambi, na zilikuwa nyekundu. Mkononi alishika mfuko mdogo ulioonyesha kitu kama karatasi, au bahasha nyeupe iliyotuna.
Alipofika karibu zaidi akasimama huku akitabasamu. "Vipi JC? Mbona umesimama hapa?" akaniuliza.
Nikiwa na uso makini, nikamwambia, "Nilikuwa nataka kutoka... ndala ikakatika. Inabidi nianze kuvaa zile mpya."
"Ee... pole."
"Umependeza."
"Asante. Zimenikaa vizuri?"
"Sana. Shi'ngapi hapo?"
"Elfu ishirini na tano."
"Ahaa... umependeza sana. Leo lazima nikutekenye," nikamtania.
"Ahahah... haya twende ndani. Nimeleta chips, saa nne sa'hivi, nisingeweza kuja kupika. Au? Ulikuwa unaenda wapi?" akaniuliza.
Alikuwa anaongea huku akitembea kuelekea kule ndani, lakini nikabakia hapo nikiwa nimeweka uso makini. Bado akili yangu ilikuwa imetekwa na suala la muda mfupi nyuma kuhusu Joshua.
"JC... vipi?" Ankia akarudi na kuuliza hivyo.
Nikamwangalia na kusema, "Poa. Namtafuta tu Tesha."
"Kumbe hamkuwa wote? Labda
atakuwa Masai... si kulikuwa na mechi leo?"
"Hapana. Masai hayupo."
"Kwao je?"
"Ndo' nilikuwa nataka niende ila... nimeahirisha," nikasema.
"Kwa nini? Kuna nini kwani?" akauliza.
"Twende ndani, nitakwambia," nikasema hivyo na kuanza kuelekea upande wa ndani pamoja naye.
Kweli nikawa nimemwelezea Ankia kilichotokea baada ya Joshua na mke wake kufika hapo nyumbani kwao Tesha, nami nikamjulisha kuwa bado watu hao walikuwa hapo ndiyo maana sikutaka kwenda nilipogundua hilo. Nilikuwa tu nataka kuhakikisha Tesha yuko poa maana mpango ulikuwa niondoke pamoja naye lakini akawa ameniacha tu, ikionekana ni hasira ndiyo zilimlemea.
Ankia akanituliza kwa kusema huyo kijana angekuwa poa tu maana alikuwa mjanja; labda alienda kwa mademu zake ama huko Mbagala kunywa pombe. Lakini na mwanamke huyu alishangaa sana suala la Miryam kumleta Joshua hapo baada ya kila kitu alichokuwa amewafanyia, ila akanishauri niachane na mambo ya hiyo familia maana hayakunihusu. Ila mimi sasa!
Tayari nilijua rangi za kweli za huyo Joshua, vitu vibaya sana ambavyo hata Ankia sikumwambia. Nisingeweza kuacha kujali hali ya Mariam huku nikijua kabisa kwamba kaka yake alikuwa na mpango wa kumuua, sijui na wakati huu alikuwa amepanga nini! Je kama alitaka kumuumiza Tesha? Mama wakubwa? Miryam?
Ningehitaji kuhakikisha naukomesha huo mchezo wake upesi ili asije kuleta shida kwa watu hao niliokuwa nimeanza kuwajali sana, yaani kwa maneno mengine, ningejitahidi kuilinda familia hiyo dhidi ya Joshua. Si alitaka watu wausikilizie muziki wake? Wakwangu angeucheza!
★★
Baada ya Ankia kuandaa vyakula mezani, tukala pamoja, chips kavu na mishikaki mitano-mitano. Ah hiki ni chakula pendwa na chepesi sana kupata kila kona ya eneo lolote, na angalau baada ya kushiba nikawa nimetulia zaidi kimwili. Nilikuwa nahisi uchovu-uchovu tu uliotokana na njaa, joto, bila kusahau mechi niliyocheza na Soraya pia, hivyo nikaamua kwenda kujimwagia ili kupunguza fukuto baada ya msosi kukaa mahali pake.
Mpaka inafika saa sita, sikuwa nimempata Tesha. Bi Zawadi alinipigia simu kuniuliza ikiwa nilikuwa na mwanaye huyo, lakini nikamwambia hapana. Walimpenda sana na walitaka kuhakikisha yuko salama, kwa hiyo nikawahakikishia angekuwa vizuri tu na angerudi, kwa hiyo wasijali.
Lakini mimi ndiyo nilikuwa najali zaidi, siyo kuhusu Tesha tu, ila wote hapo kwao. Nilikuwa nimemuuliza Bi Zawadi kama Joshua na mkewe waliendelea kuwepo hapo kwao, lakini akaniambia walikuwa wameondoka mida ya saa nne usiku huo, kumaanisha si muda mrefu sana uliokuwa umepita tokea nilipomsikia jamaa akiongea na jambazi mwenziye kwenye simu, ndiyo akawa ameondoka.
Nikaulizia tu na hali ya Mariam kwa muda huo, nami nikajulishwa kuwa binti alikuwa ameshapumzika usingizini. Sikutaka kuuliza mengi sana yasiyonihusu, kwa hiyo tuliachiana hapo tu.
Tesha sikuweza kumpata kabisa kwa simu. Bora hata mwanzoni ilikuwa ikiita mpaka kukata, lakini wakati huu haikupatikana kabisa. Dah! Sikuwa na namna ila kusubiri tu, nami nikakaa sebuleni mpaka saa nane kasoro usiku ndiyo hatimaye jambo jipya likaja.
Niliweza kusikia geti likigongwa huko nje, nami sikuwa na uhakika kama lilikuwa letu au la jirani, kwa hiyo nikatoka ili kwenda tu kuangalia ikiwa ilikuwa ni Tesha. Ankia alikuwa chumbani kwake lakini inaonekana alikuwa macho bado, kwani nilipoanza kufungua mlango wa kuingilia ndani hapa akawa ametoka chumbani na kuja kuniuliza naenda wapi. Nikamwambia naenda kuangalia ikiwa Tesha ndiyo amerudi, naye akasema poa.
Nikatoka mpaka nje, nikachungulia upande wa pili wa nyumba na kumwona bibie Miryam, ndani ya nightdress, akiwa hapo nje kwenye ubaraza wao. Alikuwa ndiyo ametoka ndani nafikiri, akitaka kwenda kufungua geti, nami nikadhani bila shaka ni kwake ndiyo paligongwa. Lakini geti lilipogongwa tena, nikatambua lilikuwa la kwetu.
Miryam akaonekana akienda kwenye geti lao na kufungua, kisha akaenda nje kabisa. Geti letu likaendelea kutoa kelele tu, nami nikaenda hapo na kukuta ni Tesha. Lakini hali niliyomkuta nayo haikuwa nzuri kabisa.
Alikuwa amechafuka kwenye suruali, huku akiwa anayumba kilevi na kofia yake kama kibandiko kichwani. Kuangalia jinsi alivyokuwa akiyumba lakini kwa kupindia upande mmoja kukanifanya nitambue kwamba alikuwa amepigwa.
Nikamwona Miryam akitokea pembeni yake na kumshika mkono, ikiwa wazi anataka ampeleke kwao, lakini Tesha akagoma.
"Hhh... sss... JC... kaka nifungulie..." Tesha akasema hivyo.
Hakuwa akitoa machozi, lakini alikuwa analia. Ile kulia ya kiume siyo kwa sababu umeumia mwilini, ila moyoni.
Miryam akaniangalia kifupi, kisha akamwambia mdogo wake, "Tesha... twende ndani. Ni usiku sasa hivi, na mimi hii tabia siipendi. Twende!"
"Niachie Mimi... nenda mwenyewe. Si unawajali hao mbuzi zaidi yetu... waambie wakae hapo... basi..." Tesha akasema hivyo.
Ikanibidi nirudi ndani upesi kwenda kuchukua funguo za hili geti letu, naye Ankia akawa ameniuliza kulikoni. Nikamwambia Tesha amerudi, lakini alikuwa vibaya, nasi sote tukatoka tena na kwenda nje. Tulikuta Miryam akiwa anamfokea mdogo wake lakini kwa sauti ya chini, nami nikafungua geti na kutoka.
"...maneno gani? Hebu jiangalie Tesha. Unafanya maisha yako yawe mabaya kisa hasira, unafikiri itakufikisha wapi?" Miryam akaendelea kumwambia hivyo.
"Mimi... niache... wewe fanya mambo yako... maana haujali hisia zangu..."
"Mimi sijali hisia zako Tesha? Unaniambia hivyo?" Miryam akamuuliza kwa hisia.
Nikamshika Tesha mkononi na kuuliza, "Tesha nini kimetokea?"
"Ah... sss... mwanangu..." akasema hivyo na kupiga ulimi mdomoni.
"Ulikuwa wapi? Umeanguka?" Ankia akamuuliza hivyo.
Tesha akawa anababaika, akionekana kuwa na maumivu.
"Umefanyaje? Nani amekupiga?" nikamuuliza hivyo kwa uthabiti.
"Amepigwa? Umepigwa Tesha?" Miryam akamuuliza hivyo na kusogea karibu zaidi.
"Ah... mwanangu nimekabwa... njiani..." Tesha akasema hivyo.
"Na vibaka? Sehemu gani?" nikamuuliza.
"Si huko Mbagala mwanangu... nilikuwa narudi... ah... mwanangu wamechukua simu yangu..." Tesha akaongea kwa kukaza hisia.
"Umetembea kutokea Mbagala?" Ankia akamuuliza hivyo.
"Jamani! Tesha umeona sasa mambo ya usiku? Nikwambie mara ngapi unisikilize?" Miryam akasema hivyo kwa huzuni.
"Ni kweli Tesha, usiku siyo mzuri... jamani, tuingieni ndani..." Ankia akasema hivyo.
"Twende Tesha ukalale..." Miryam akamwambia hivyo na kuuvuta mkono wake, lakini Tesha akaweka mgomo.
"Tesha... msikilize dada'ako..." Ankia akasema.
"Mbona yeye hanisikilizi? Anawaleta... ah... Ankia, sister anazingua... ona mpaka nimejikuta kwenye hii hali..." Tesha akasema hivyo.
"Yaani unanilaumu mimi kwa sababu ya upuuzi wako? Me nilikutuma uende huko? Ukoje wewe?" Miryam akasema hivyo na kusukuma kichwa cha mdogo wake kwa kidole.
"Miryam..." nikamwita hivyo kwa sauti ya chini.
"Nini?" akaniitikia hivyo.
"Nitaenda kulala naye. Yuko vibaya kama unavyoona... mwache tu, mtaongea asubuhi. Sawa?" nikamwambia hivyo kwa upole.
Miryam akamtazama mdogo wake, nikiona machozi yakiwa yamemlenga.
"Oya... twende ndani..." nikamwambia hivyo Tesha na kuanza kumvuta.
"Dah... JC, simu yangu..." akasema hivyo kwa huzuni.
"Twende kwanza upumzike... tutatafuta nyingine..." nikamwambia hivyo.
Nikamkokota vizuri mpaka ndani, Ankia na Miryam wakiwa wanatufata kwa ukaribu, nasi tukafika chumbani kwangu. Tesha akajitupia kitandani na kulala kifudifudi, huku uso wake akiugeuzia ukutani, na mwili wake ungeshtua kila mara kwa ile njia ya kulia kwa pumzi.
Nikawa namtia moyo tu ajikaze, na nikiangalia kama kuna sehemu aliyokuwa ameumia vibaya, huku wanawake wakiwa wanatutazama tu pale mlangoni, nami nikamwomba Ankia aifate feni sebuleni na kuileta huku, kisha aiwashe mpaka mwisho.
Akatii na kuileta, akiiwasha na kuielekeza upande aliolala Tesha, nami nikatoka kitandani na kusimama kumtazama dada mtu. Alikuwa anamwangalia mdogo wake hapo kitandani kwa macho yaliyojaa huzuni, na nilitambua kuna kiasi cha machozi kilichokuwa kimemtoka lakini akawa ameyafuta macho yake.
"Tumwache alale sasa, pombe ikimtoka mambo yataeleweka zaidi, eti Miryam?" Ankia akamwambia hivyo.
"Muda mwingine natamani hata nimkate masikio," Miryam akasema hivyo kwa sauti ya chini.
Ankia akatabasamu na kuniangalia.
Nilikuwa namwangalia Miryam kwa uelewa mwingi sana, naye aliponitazama machoni, nikasema, "Najua unawaza sana kuhusu hali yake, ila usijali. Hajaumia sana. Hao vibaka wamemkwarua kidogo tu."
"Na simu yake wamebeba," Ankia akasema.
"Kama angekaa kwa kutulia, haya yote yasingetokea... ah..." Miryam akasema hivyo kwa huzuni.
Ankia na mimi tukatazamana tu machoni, kisha tukamwangalia tena dada mkubwa.
"Sitaki akuletee shida Ankia jamani, ikiwa..."
"Hapana, hapana, Tesha siyo shida Miryam. Ni rafiki yetu, kwa hiyo lazima tumsaidie. Mbona we' umenisaidia kwa mengi magumu Miryam... sasa hiki tu ndo' kinipe shida? Hebu acha kuwaza hivyo bwana. Nenda kapumzike... asubuhi mambo yatakuwa sawa," Ankia akasema hivyo kwa upole.
Nikawa namwangalia tu Miryam, naye akashusha pumzi na kutoa shukrani, kisha akaanza kuondoka. Nikahakikisha namtoa mpaka nje na kumwacha kwenye mazingira salama mpaka alipoingia getini kwao, tukiwa hatujaongea chochote kabisa, nami nikarudi upande wetu.
Ankia akaanza kuniambia ni namna gani maisha ya hapo yalivyokuwa yakitengeneza drama moja baada ya nyingine, na hili suala la Tesha kupenda mno pombe mpaka anajikuta kwenye matatizo lingemfikisha pabaya mno ikiwa asingeangalia.
Akaniaga na kwenda kulala chumbani kwake, nami nikabaki chumbani pamoja na rafiki yangu mpya. Tayari usingizi ulikuwa umeshambeba zamani sana, si unajua alikuwa amegusa pombe? Kwa hiyo nikakaa hapo kwanza kutafakari vitu kidogo.
Alichosema Ankia kilikuwa sahihi. Tesha alikuwa kijana mzuri sana, lakini naona kuna kitu fulani kilichokuwa kikimsukuma apende mno pombe na kumfanya awe tofauti na alivyotakiwa kuwa. Kiuhakika, sisi wote tulikunywa, lakini hata sisi wengine tungeweza kuona kwamba alikuwa akipita kiasi.
Labda shauri ya msongo wa mawazo uliosababishwa na kitu fulani nisichofahamu ndiyo jambo lililofanya awe hivi, na kwa sababu nilikuwa namjali, nilitaka kuhakikisha namsaidia kwa ushauri, ikiwa ingewezekana, ili ajiepushe na mambo ambayo huenda yangekuja kumwingiza kwenye matatizo mabaya zaidi kuliko hata ya leo.
Sikutaka vitu vibaya zaidi vije kumpata huyu kijana, kwa hiyo darasa huru lingeitishwa siku ikishakucha ili kweli nisaidie kumweka huru.
★★★
Siku ikakucha. Niliamka cha kwanza ikiwa ni saa moja kasoro, nao usingizi bado ukawa unanivuta niendelee kulala. Kwa kuwa nililala na Tesha kwa kupishana miili, nilimchungulia tu na kuona kwamba bado alikuwa amesinzia, hivyo nami nikaingia usingizini tena.
Ndoto moja, mbili tena, nami nikaamka kwa mara nyingine. Zamu hii nilipoangalia muda nikakuta inakimbilia saa tatu asubuhi, nami nikamwangalia mwenzangu na kuona bado amelala kitandani, lakini macho yake yalikuwa wazi.
Tesha alitazama kuelekea juu, ikiwa kama vile anatafakari mambo fulani, nami nikampiga kidogo mguuni kwa mkono wangu.
"Oy, oy..." akasema hivyo kwa sauti ya chini.
"Uko macho muda?" nikasema hivyo na kupiga mihayo.
"Hamna... nimekata dakika 10 tu. Ankia kaja, akanicheki, ameenda sokoni kufata nyama. Wewe unalala kama umekufa mwanangu, hata hukumsikia," akaniambia hivyo.
"Ah wapi! Hahah... nimeamka kabla yako, nikakucheki, nikaona bado uko Dreamland, kwa hiyo na mi' nikarudi kulala pia..." nikasema hivyo.
"Dah, nimekunywa jana! Nashangaa sijapotea njia ya kurudi," akasema hivyo.
"Mlevi hata alewe vipi, hawezi kusahau kwake," nikamwambia.
"Ahahah... uhakika. Na mimi navyolalaga vibaya hivyo, sijakupiga mateke kweli?"
"Hamna... ila sema unajamba sana..." nikamtania.
"Aa, acha hizo mwanangu..."
Sote tukacheka kidogo.
"Unajisikiaje?" nikamuuliza.
"Dah! Kichwa kinagonga. Mbavu zinauma, hao wajinga jana walinipiga kabaroho la hatari," akaniambia.
"Kwani ulikuwa unatokea wapi kabisa? Jana nilikupigia kweli afu' baadaye ndiyo ukawa hupatikani kabisa..."
"Dah! Mwana me nilikuwa nimekasirika sana... ile ishu, si unaelewa?"
"Yeah."
"Nikaona niende zangu Tandika. Kule kuna demu wangu... anaitwa Happy... ananielewa sana. Nikaenda kwake, nikakaa pale wee... badae', jioni pale mechi imeisha, nikamwacha. Ah, afu' linapenda kunyonywa chenza!" akaniambia hivyo.
"Ahahahah... usinambie'!"
"Ah, siyo poa. Nimelila, likanigei na hela ya bia maana... linafanya kazi kwenye hoteli, kuna shift ya usiku kwo' lenyewe likaenda huko, nami ndo' nikaanza kurudi Mbagala..."
"Mm-hmm..."
"Basi mwanangu, nikaenda zangu pale Highway. Piga bia zangu kama nne hivi, wenye kushoboka wakaja, wakaongeza, nikaendelea kupiga tu. Nimekunywa jana! Halafu zilikuwa kama haziishi..."
"Haukufahamiana na hata mmoja?"
"Hamna, chawa tu zisizojulikana. Walikuwa wanafikiri me mtu mwenye hela ndo' maana..."
"Ikawaje?"
"Nimekunywa, nimekunywa, kuna demu akawa anataka niende naye Lodge ya hapo, ila me sikuwa na hela. Afu' lilikuwa la moto!"
"Wewe!"
"Acha mwanangu, bonge la pisi! Ningekuwa na 15 nisingerudi huku kabisa, ningelala nalo..."
Nilikuwa nasikiliza kwa umakini namna ambavyo kijana huyu aliongea, nikijaribu kuisoma saikolojia yake. Niliweza kutambua mambo fulani kuhusu utu wake kutokana na jinsi alivyozunguka kwenye maneno aliyotumia ili kufika kwenye pointi ya kile nilichotaka kujua. Alipenda ukweli wa mambo yote aliyofanya uelezeke mwanzo mwisho kwa msikilizaji, ili kumwaminisha zaidi.
"Nikatoka hapo, saa sita mwanangu, nikasema ah... si unajua na pombe? Nitembee tu... yaani napaona skani kama hapo tu. Nilikuwa hata siyumbi kivile mwanangu... mdogo mdogo tu mpaka lile eneo pale karibiaa... nanilii... kale ka-guest... Lasanga..."
"Ee..."
"Eee pale mbele mbele ukikaribia sasa kwenye lile dampo la machupa ya kuuzwa. Pale si ndiyo pamekaa vizuri kukojoa, nikasogea nishushe mvua. Ah!"
"Ndo' wakakuvamia hapo?"
"Yaani sijui hata walitokea wapi kaka!"
"Walikuwa wengi?"
"Kama watatu hivi. Wawili walinishika, mmoja akiwa amenikaba, afu' nikasikia nimepigwa kiunoni... hapa kwenye mbavu, ah! Isingekuwa ya pombe ningeruka nao! Wakachukua simu na wallet mwanangu, ila haikuwa na kitu hiyo..."
"Hakukuwa hata na kadi za maana? Vitambulisho?"
"Hamna. Uzuri sikuwa nimevibeba jana. Si ile nimeondoka kwa hasira, nilikuwa na buku tatu tu... ahahaha... mpaka kwa Happy huko Tandika, ndo' na yeye akanitoa kidogo baadaye. Ndiyo hivyo bro... wamenitia hasara hao wakuda..." akasema hivyo kwa kuudhika.
"Inabidi uje kwenda polisi... masuala ya laini, si unajua?"
"Ah! Nimeshachoka akili. Yaani kama nikija kukutana nao tena! Nitafanya kitu mbaya sana," akaniambia hivyo.
Nikajinyanyua na kukaa, yeye bado akiwa amelala chali huku mguu mmoja akiukanyagisha kitandani na mkono wake akiuweka kwenye paji la uso.
"Hiyo ni kama utakutana nao tena, na ni kitu kigumu sana. Hao ni watu wa kubadilisha maeneo, na wewe haukuwa target ya moja kwa moja. Walikuotea tu," nikamwambia hivyo.
"Ah... ndo' hivyo kaka. Mtihani wa kutafuta simu nyingine ni wangu... na ni mgumu kinoma," akasema hivyo.
"Unajua Tesha... nakuelewa. Vizuri sana. Wewe unavyoona mambo, ni tofauti na jinsi ambavyo dada yako au mama zako wakubwa wanayaona, kwa hiyo migongano lazima itokee msipokubaliana kwa jambo fulani, lakini...."
"Mimi ndo' nacholilia JC! Hivi kweli mwanangu, si na wewe ulikuwepo ile siku huyo mbwa ameitukana familia yetu? Tena we' hapo ilikuwa ni mara ya kwanza... me mwanangu namjua huyo mtu toka tupo wadogo, yaani hafai! Ni mchoyo, mkuda, mpumbavu, yaani ah! Halafu analeta mamae zake hapo afu' eti nimpokee 'njoo, karibu sana'? Yaani siwezi JC. Sijui Mimi anafikiria nini... ah..." akaongea kwa hisia sana.
"Hujaingia kwenye akili ya dada yako Tesha, na najua hamwezi kufanana kwa kila kitu. Unajua... we' ni mdogo wangu, sawa? Nakuelewa. Ninaelewa hasira uliyonayo haiko kwa familia yako, ila una hasira juu ya kitu kingine ambacho... ndiyo kinakufanya upende zaidi kujistarehesha... wanawake... pombe sana... ili ujipe njia ya kupotezea hizo hisia. Lakini Tesha... ushawahi kusikia kwamba huwezi kuepuka matatizo yote kwa kuyakimbia?" nikamwaongelesha hivyo kwa upole.
Akawa ananiangalia kwa macho yenye subira.
"Mimi ni rafiki yako, na nimeshakusoma. Nimeelewa kwamba kuna kitu kinachokuumiza, lakini hautaki kuki-face... unakiepuka... kwa kuishi ile... kujiachia. Inaeleweka mwanangu, sawa? Hata mimi nimeshapita kwenye nyakati za namna hiyo... kwa hiyo nakuelewa. Lakini nitakwambia kitu. Ikiwa utaendelea kuiepuka hiyo hisia na kujifikirisha kwamba uko sawa, kwamba hauna tatizo... ndiyo itaendelea kukua zaidi. Inakuwa kama unapokuwa na kinyongo na mtu... lakini unaigiza kwamba ah mko fresh. Hiyo kitu inakuwa inakutafuna ndani kwa ndani, ndiyo maana unakuwa unafanya vitu kwa njia isiyo yako kabisa, hasa... hasa kama utakasirishwa na jambo hata dogo linalohusiana na hiyo hisia uliyoificha. Unanielewa rafiki yangu?"
Tesha alionekana kuzama ndani ya hisia fulani nzito sana baada ya kunisikia nikimwambia hivyo, naye akatikisa kichwa kuonyesha uelewa.
"Sisi siyo wakamilifu mwanangu. Hakuna mtu msafi yaani. Lakini tunapoona mwenzetu anajichafua haimaanishi tumwache tu. Tunakuwa tunasaidiana hivyo hivyo, uongo?" nikamwambia hivyo.
"Ni kweli," akajibu.
"Ee. Ila sasa... kuna watu kama Joshua. Sikupingi Tesha. Huyo kaka yako... hafai. Yaani ana ule uchafu sugu kwenye utu wake hata kuusugua kwa Jik wala msasa hautoki. Sawa?"
"Kwa hilo hupingwi JC..." Tesha akasema hivyo.
"Yeah. Ndivyo hali ilivyo, haipingiki. Lakini tukija kwa dada yako... Miryam ni mtu tofauti Tesha. Anajaribu kuona kitu fulani ndani ya mtu hata kama hakipo, na hiyo inamfanya awe mtu mwelewa sana... mpole... anayetaka amani hata kama nafasi ipo kidogo sana ya kuipata. Hayo siyo makosa yake, ndivyo alivyofundwa. Na dada yenu... anawapenda sana. Nadhani anataka kufanya kila kitu kuwaunganisha, maana anajua hatakuwa nanyi siku zote..." nikaeleza hivyo.
Tesha akaendelea kunisikiliza tu kwa utulivu.
"Ma' mkubwa wako alinielewesha kuhusu huo utu wa dada yako, kwa hiyo nimemwelewa namna hiyo. Anataka kutafuta amani hata na mtu kama Joshua kwa sababu ni ndugu yenu, sawa, huyo ni Miryam. Ila wewe ni Tesha. Ukishamwelewa kwamba 'dada yuko hivi,' we' kubaliana naye, kwa njia yake ya kuona mambo, lakini unakuwa unahakikisha kwamba uko macho kwa njia yako mwenyewe ya kuona mambo ili ukiona kwamba anakaribia kuanguka... unawahi kumdaka. Maana hata yeye anaweza akawa anakosea, si ndiyo?" nikamwambia hivyo.
"Ni kweli," akajibu.
"Ee, hawezi kuona vitu kama Bi Zawadi na Bi Jamila, ama Shadya na mashoga zake. Alivyo ndivyo alivyo tayari, we' mwelewe tu, halafu utulize hisia zake hata kama bado zako zinaruka-ruka. Si unaelewa mwanangu?"
Akatikisa kichwa kukubali.
"Ee. Haumwamini kaka yako, sawa, simama na hilo. Nenda na biti la dada yako la kutafuta amani lakini jicho lako makini lisitoke kwa huyo mtu unayejua anaweza kubadilika muda wowote. Si unanipata?" nikamwambia.
"Ee mwanangu, unasema kweli. Ah... mi' nakuwa sitaki hata awe karibu yetu maana..."
"Hata akiwa mbali Tesha, uwezekano wa kufanya mambo mabaya kwenu anao. Hicho ni kitu ambacho unatakiwa uwe nacho akilini. Kwa hiyo la muhimu kuangalia ni wale unaowapenda... basi. Wewe Tesha ndiyo mwanaume hapo... hebu, i-face hiyo hisia uliyoificha... ipe za uso... kitoe hicho kitu kinachoisumbua roho yako ili uache kujikimbia we' mwenyewe... ndiyo utaona umuhimu wa haya yote niliyokwambia ili uwe namna unavyotakiwa kuwa. Simaanishi utakuwa mtakatifu, ila najua utaanza kujitahidi kutotanguliza fikira zako tu na kuangalia faida za wapendwa wako zaidi. Hilo ndo' la muhimu. Au siyo?" nikamwambia hivyo kwa busara.
"Dah! Ahahah... kaka unaongea wewe! Fungua chaneli ya documentary..."
Akasema hivyo, nasi tukacheka kidogo.
"Me nimekuelewa JC. Uko sahihi. Unajua kuna kitu..."
Kabla hajamaliza kuongea, sote tukasikia mlango wa kuingilia ndani ya sebule ukigongwa, kuashiria mgeni kafika. Ah ingekuwa Ankia ndiyo karudi si angepita moja kwa moja? Huyo hakuwa yeye.
Nikaona nitoke tu kitandani na kuchukua T-shirt la kuvaa ili nikaone ni nani, maana nilikuwa kifua wazi na nimevaa pensi tu.
"Ankia kachelewa kweli kuleta supu," Tesha akasema hivyo.
"Labda ndo' katuma mtu ailete. Ngoja nikaone ni nani," nikamwambia huku nikivaa.
"Halafu mwana una kabode simple tu, ila kifua chako kiko mbele! Unaingiaga gym?" akaniuliza.
"Kitambo, niliacha. Ila nataka nije nianze tena kujenga kinga," nikamwambia hivyo.
"Na mimi nataka nianze pia, maana nilishakuwa legelege mpaka nakabwa kijinga," akasema hivyo.
Nikatabasamu kiasi, nami nikatoka chumbani na kwenda kufungua mlango.
Macho yangu yalikuwa na uzito kiasi, lakini baada ya kumwona bibie Miryam hapo nje ikawa kama yamepata wepesi. Alikuwa amevaa nguo kama dera, ya kijani, iliyokuwa imefungwa kwa mkanda laini sehemu ya kiuno. Kichwani alizibana nywele zake ndefu alizosuka kwa juu, na uso wake usiokuwa na virembesho vya aina yoyote ulipendeza sana kwa asubuhi hii.
"Za asubuhi?" akanisalimu kwa sauti yake nzuri.
"Salama. Vipi wewe?" nikamjibu.
"Safi tu. Huyo ameamka?"
"Ee yuko macho, ila... bado yuko kitandani... ingia..."
"Hapana, mwite tu. Nataka aje nyumbani."
"Bado ni mzito, Ankia ameenda kumfatia supu pia. We'... ingia tu umwone angalau. Tafadhali," nikamwomba hivyo.
Akaniangalia kwa macho yenye utathmini, kisha akavua ndala zake na kuingia ndani. Ngozi yake nyeupe iliyoonekana nyuma ya shingo yake ilipita hadi weupe wangu yaani, ikionekana kuwa nyororo sana.
Nikaacha kumtazama baada ya yeye kufika mbele zaidi na kunigeukia, nami nikaufunga mlango na kuelekea chumbani kwangu huku nikimwambia aje. Nikakuta Tesha akiwa amejilaza bado, nami nikamwambia dada yake amekuja.
Akajinyanyua na kuketi kitandani, huku dada yake akiwa anaingia chumbani sasa, nami nikaichukua simu yangu.
"Ngoja niwapishe kidogo... njoo ukae," nikamwambia hivyo Miryam.
"Hapana..."
Tesha akasema hivyo, nasi tukamwangalia.
"Usiondoke JC. Kuna vitu nataka niongee na we' usikie," akasema hivyo tena.
Nikamwangalia Miryam na kuona jinsi alivyomtazama mdogo wake kwa hisia, naye Tesha akasimama usawa wangu.
"Mimi... dada yangu... naomba unisamehe," Tesha akaanza kwa kusema hivyo.
Miryam akaingia ndani zaidi na kumfikia mdogo wake, akamshika mkono huku akimwangalia kwa hisia, naye akasema, "Usijali Tesha. Yameshapita. Wewe... twende nyumbani kwanza uka..."
"Hapana, Mimi, nataka unisikilize kwanza," Tesha akasema hivyo.
Miryam akabaki kimya.
Tesha akaanza kujipiga kifuani kwa kidole chake na kusema, "Kuna vitu vingi sana hapa dada. Nimejikaza muda mrefu mno. Unajua nikwambie kitu? Yaani kama ingekuwa... ingekuwa ni kuzaliwa kwenye maisha mengine... ningechagua kuwa na kaka wa damu kama JC... siyo Joshua."
Miryam akanitazama usoni, nami nikamtazama tu Tesha.
"Isingekuwa ya huyu kaka, leo nisingetambua kwa nini nimekuwa hivi. Mimi, hata wewe unajua sikuwa hivi... na japo... japo umeniacha tu niishi kama navyoishi sasa hivi lakini najua huwa nakuumiza sana. Najifumbisha tu macho... lakini ni kitu nachohisi... na roho inaniuma sana kwa sababu sipendi uumie..." Tesha akaongea kwa hisia.
Miryam akaanza kulengwa na machozi.
"Lakini... iko hivyo kwa sababu... yaani... nimekuwa hivi kwa sababu... kwa sababu uliniumiza Miryam..." Tesha akasema hivyo.
Miryam akamwangalia kwa njia iliyoonyesha hakuelewa, nami nikawa makini zaidi ili kuweza kuelewa sasa funguko la huyu kijana.
"Dada una moyo. Una moyo mzuri, sawa? Lakini Joshua siyo! Siyo mtu. JC... wazazi wetu wamekufa, sawa? Kwenye ajali. Walituachia kila kitu chao... wakatugawanyishia... lakini Joshua akawa anataka hadi na vya kwetu..."
"Tesha..." Miryam akasema hivyo kama kumzuia.
"Subiri kwanza Mimi, ngoja niongee. Mwanangu... Joshua alipewa vingi kuliko hata sisi, maana mama alikuwa anampendelea sana yaani. Lakini akavitumia vibaya, halafu ndiyo akageukia kwenye vyetu. Nilikuwa nimeachiwa shamba, nalimisha na Mimi, tunapata hela zinatumika kwenye maendeleo yangu, Mariam, na ndugu zetu wengine, lakini Joshua akaliiba... akaliuza serikalini!" Tesha akasema hivyo kwa sauti ya chini.
Hiki ni kitu ambacho nilifahamu, lakini nilidhani kwamba yeye Tesha hakujua. Nilipomtazama Miryam, alikuwa anamwangalia mdogo wake kwa njia iliyoonyesha hata yeye hakutarajia hilo.
"Da' Mimi alijua, lakini hakuniambia. Alikuwa anajaribu kulinda amani, kama ambavyo sikuzote anafanya, lakini nilipojua... niliumia sana kaka! Nilihisi kama vile na yeye anampendelea, ana... anakuwa kama mama..."
"Tesha..." Miryam akamwita hivyo huku machozi yakianza kumtoka.
"No, Mimi usilie, sikulaumu. Nakuelewa, sawa?" Tesha akasema hivyo na kumfuta dada yake machozi.
"Tesha..." Miryam akaita tena.
"Usijali. Nilikuelewa, ndiyo maana nikakaa kimya. Sasa... ah... JC ndiyo kanifungua macho leo. Hiyo kitu iliniumiza mno japo nilikuelewa... ndiyo maana nikawa namna hii. Kama ulivyoniambia mwanangu... nikawa naikimbia hiyo hisia. Ila me ni mtu mwenye hasira sana kaka, na nilikuwa sitaki ziende kwa Mimi. Nampenda mno..." Tesha akasema hivyo huku machozi yakionekana machoni mwake.
Nikaingiwa na simanzi baada ya kuwa nimemwelewa vizuri sasa. Unaona? Kadarasa huru nilikompa kakawa kameleta hiyo faida.
"Kwa hiyo dah! Me... Miryam siwezi kumchukia. Lakini ninakiri leo kwamba... kulikuwa na kitu hapa... kinanisukuma nimkasirikie... ndiyo maana nikaanza kunywa sana pombe, unajua inaweza ikawa ngumu kuelewa lakini... hii kitu ipo. Mimi... wewe ni mtu mmoja nayempenda sana. Nikikwambia naweza kuua mtu kwa ajili yako, namaanisha hata Joshua! Nikimwona anakuja hapo nyumbani... nakumbuka! Nakumbuka kila kitu... ndiyo maana nafanya mambo vibaya. Eh! Nisamehe dada'ngu. Kwa jana... ah, nisamehe tu..." Tesha akasema hivyo huku amemshika Miryam mabegani.
Dada mtu akawa anamwangalia tu mdogo wake kwa huzuni.
"Ila unajua nini? Sasa hivi... nimeshaliondoa hili kaa la moto rohoni. Sitaki tena. Sitaki... hasira niliyonayo iniongoze vibaya. Nakuahidi dada, nitabadilika. Labda... ila bia nitakuwa nakunywa kidogo tu, siyo mbaya..."
Kauli hiyo ikamfanya Miryam acheke kidogo kwa pumzi ingawa alikuwa na huzuni, nami nikatabasamu pia.
"Tuyaachie haya mambo hapa. Mimi... nakuahidi. Sitakuvunja moyo. Sawa? Amani unayoitaka utaipata... tena inaanzia kwangu, yaani usikonde," Tesha akasema hivyo kwa njia ya kuchangamsha.
Miryam akaangalia chini kiasi kwa huzuni.
"Oya... ndiyo hivyo. Asante sana kwa hiyo therapy... si umeona nimefunguka daktari-mchizi wangu?" Tesha akasema hivyo.
Nikatabasamu na kusema, "Nimekuelewa. Umefanya vizuri. Kumbuka tu hili. Haijalishi uliyoyafanya, sawa? Ila yale ambayo unataka kuyafanya ndiyo ya muhimu."
"Amen," Tesha akasema hivyo kiutani.
Nikafarijika kuona namna ambavyo kijana huyu alikuwa ameweza kuufungua moyo wake na kuonyesha utambuzi, nami nikamtazama dada yake na kukuta anamwangalia mdogo wake kwa hisia.
"Ngoja nikakojoe Mimi... nakuja..." Tesha akasema hivyo.
Miryam akatikisa kichwa kukubali, naye Tesha akampita na kutoka ndani hapo.
Ni baada tu ya mdogo wake kutoka ndiyo Miryam akakisogelea kitanda na kukaa, nami nikamtazama na kuona jinsi uso wake ulivyokunjamana kwa njia ya kulia. Oh alikuwa analia, sana!
Lakini ni machozi tu ndiyo yaliyoonekana kutiririka na kwikwi zake kushtua mwili, ila huyu mwanamke hakutoa sauti. Kilikuwa kile kilio cha ndani sana kutoka kwenye moyo wake, nami kumwona akilia namna hiyo kiukweli kulinipa hisia mbaya sana. Alitia huruma.
Nikasogea mpaka hapo na kukaa pembeni yake, nami nikasema, "Miryam... jikaze tu. Mdogo wako atakuwa sawa."
"Ahh... nakosea wapi? Hhh... kwa nini najitahidi kujenga ila tu ndiyo mambo yanabomoka?" akaongea hivyo kwa sauti ya kunong'oneza, na kwa hisia sana.
"Siyo..."
"Mimi ni mpumbavu, eti?" akaniuliza hivyo na kunitazama.
Nikabaki kumwangalia kwa huruma.
"Mimi nina moyo wa kipumbavu sana. Najaribu... nafikiri kufanya hivi ndiyo inafaa, lakini kumbe ndiyo naharibu. Naangukia pua... mwisho wa siku ni mimi tu ndiyo naangukia pua. Hadi mdogo wangu nimeshindwa kumwongoza vizuri? Mpaka ana... hivi kweli jamani... ni nini kama siyo upumbavu? Ndiyo maana hata na wewe uliweza kunifanya nionekane mjinga mara ya kwanza tumekutana, siyo? Ni kwa sababu ya upumbavu wangu..." Miryam akasema hivyo kwa huzuni.
"Hapana... siyo hivyo Miryam..." nikajaribu kumtuliza.
Akaendelea kulia bila kutoa sauti sana, nami hadi nikalengwa na machozi kabisa!
Nikapitisha mkono wangu kwenye bega lake kwa njia ya kumvuta kiasi, naye akalaza kichwa chake begani kwangu. Nilipatwa na hisia ya uvuguvugu moyoni, kwa sababu hali ya huyu mwanamke ilinigusa sana, naye akawa anaendelea kulia kwa kwikwi huku mimi nikimbembeleza kwa kusugua mkono wake taratibu.
Mapigo yangu ya moyo yalikimbia kwa kasi sana na sikujua shida ni nini. Kuna kitu fulani kilichokuwa kikijijenga ndani yangu ambacho bado sikuwa nimeelewa ni nini, ila kiliweka msingi wa hisia tofauti ndani yangu ambayo ilikwenda kinyume kabisa na hali ya utu niliokuwa nimejipatia kwa kipindi hiki. Sikujua kwa sasa, lakini huenda ingekuja kueleweka baadaye.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments