Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Nikiwa naendelea kumpa Miryam bembelezo kwa kusugua mkono na bega lake taratibu, mlango wa kuingilia hapo chumbani ukafunguka, nami nikatazama hapo na kumwona Ankia akiwa amesimama. Bila shaka ndiyo alikuwa amerudi, na inaonekana alikuja moja kwa moja mpaka humu chumbani kutuangalia mimi na Tesha, lakini akakuta niko na dada mtu. 

Miryam akawa amemwona pia, naye akajitoa begani kwangu na kuanza kujifuta machozi kwa viganja vyake. Ankia alikuwa amesimama hapo mlangoni akitutazama kama vile anasubiri maelezo.

"Ndiyo umerudi?" nikamuuliza hivyo.

"Ee... ndiyo nimefika. Kila kitu kiko sawa jamani?" Ankia akauliza hivyo kwa kujali.

Miryam akasimama baada ya kujikausha machozi, nami nikasimama pia. Akasema, "Ndiyo, nimemwijia Tesha."

"Yuko wapi?" Ankia akamuuliza.

"Ameingia uani. Ngoja niende nikamsubiri hapo nje," Miryam akasema hivyo.

Nilikuwa namtazama tu kwa utulivu, naye akaanza kuelekea mlangoni lakini Ankia akamshika mkono kumzuia. Sote tukamtazama.

"Nime... nimeleta supu. Kaa basi tunywe pamoja na mdogo wako, eti?" Ankia akamwambia hivyo.

Miryam akasema, "Sitaweza Ankia. Naingia kazini, nataka nikajiandae. Ila Tesha anaweza kubaki, na...."

"Ankia umerudi?" Tesha akawa amefika na kusema hivyo.

"Eee. Namwambia dada yako tunywe supu, nimeleta nyingi, ila anataka kuwahi kazini..." Ankia akasema.

"Aaa, Mimi... kunywa tu hata bakuli moja. Sikumbuki mara ya mwisho tumekunywa supu pamoja..." Tesha akamwambia hivyo dada yake.

Ankia akatabasamu na kusema, "Ee bwana, hata bakuli moja tu. Ngoja nikaweke, sawa?" 

Miryam akaonekana kutaka kumridhisha mdogo wake, hivyo akatikisa kichwa kukubali.

"Haya twendeni jamani. JC... njoo," Ankia akaniita.

Nikatikisa kichwa kukubali, nami nikafata nyuma yao wote mpaka hapo sebuleni.

Hakukuwa na ile hali changamfu sana iliyozoeleka kutokana na uwepo wa Tesha, kwa sababu wakati huu alikuwa chini ya mvurugo wa kihisia. Angalau Ankia angeongea kwa njia nyepesi ili kurudisha hali iliyosawazika zaidi kwa sehemu hiyo. Kulikuwa na hotpot mezani na mfuko wenye kitu kwa ndani, naye Ankia akawa ameleta sahani ya udongo na mabakuli manne pamoja na vijiko. 

Kwenye ule mfuko akatoa chapati sita za kusukumwa na kuziweka kwenye sahani, akisema ndizo zilizofanya akakawia kiasi kwa sababu ya kuhitaji kusubiri. Akaweka na supu kwenye mabakuli, nyama zikiwa zile zifananazo na maini (wanaita mapupu), naye akatusogezea kila mtu sehemu yake na kumsisitizia Miryam anywe na kula chapati. 

Nilikuwa namwangalia mwanamke huyo na kuona namna alivyojitahidi kusitiri hisia zake. Kuna kitu kilichokuwa kinaisumbua nafsi yangu kutokana na kushindwa kumwambia maneno yenye kufariji alipokuwa anajilaumu kwa sababu ya matatizo yaliyokuwa yanatokea kwenye familia yake. 

Hii ndiyo iliyokuwa mara ya pili kwangu kuweka ukaribu wa namna hiyo kwa huyu mwanamke, yaani vile nilivyombembeleza kidogo akiwa amenilalia begani, nikiwa nakumbukia mara ya kwanza aliponikumbatia kwa kutoa shukrani ya moyoni nilipomsaidia mdogo wake. Nilihisi kama ningeweza kujiweka karibu naye zaidi ili tushirikishane katika mambo yenye kujenga zaidi, lakini tatizo alikuwa wa kivyake mno. 

Tukawa tunakunywa thupu, taratibu tu, naye Tesha akawa anasimulia kwa wanawake jinsi alivyojikuta anakabwa na vibaka na kuibiwa simu; bila kuongelea masuala ya wanawake aliokutana nao bar lakini. Akatania kwa kusema alitaka kurudi huko leo na kisu ili akawatafute hao vibaka, nasi tukamwambia awe mwangalifu kisije kikageuziwa kwake. 

Kwa hiyo maongezi hapo yalikuwa mepesi tu mpaka tulipomaliza supu, Miryam na mimi tu ndiyo tukiwa tumekula chapati moja moja, kisha yeye na mdogo wake wakatuaga na kuelekea kwao. Tesha alikuwa anataka kwenda kuuweka mwili wake sawa zaidi ili baadaye nimsindikize kwenda kituo cha polisi kuangalia suala lake la simu, nami nilikuwa nimemwambia haina tatizo. 

Bila shaka, wawili hao wangeenda kujaribu kuweka hali vizuri zaidi pale kwao, lakini bado nilikuwa na hofu kuelekea suala la huyo Joshua. Sikutaka kuwachanganyia habari kwa kuwaambia mambo niliyosikia huyo mjinga akisema, maana najua ningeizidisha tu hofu ya Miryam kutokana na vitu ambavyo mdogo wake angeweza kufanya. 

Kwa sasa ingekuwa busara kutulia tu, lakini ningehakikisha nakuwa makini ili kuiepusha familia hiyo kutoka kwenye matatizo ambayo Joshua alitaka kuyaendeleza; hasa kumlinda Mariam. 

★★

Muda mfupi baada ya Miryam na Tesha kuwa wameondoka hapa kwa Ankia, nikawa nimefanya usafi wa chumba na mwili, kisha nikavaa vizuri ili niweze kwenda pale kwao kushughulika na binti Mariam. 

Ni leo ndiyo nilitaka kumpa Ankia hela ya kodi kwa ajili ya mwezi uliofuata, basi tu yaani ili wiki ambazo zingefuata nisiwaze kabisa kuhusu hilo suala. Nilipotazama matumizi yangu ya pesa za pembeni toka nimekuja mapumziko, nikaona nilikuwa nimetafuna nyingi kiasi, lakini hakukuwa na shida sana juu ya hilo. 

Baada ya kupangilia mambo vyema, nikamfata Ankia na kumpatia pesa. Kama kawaida yake, alianza kujishaua mara JC mbona hivi, mbona vile, nami nikalazimisha azichukue na kumwambia akate mashauzi yake. Nikamuaga baada ya hapo, nikisema ndiyo naenda kwenye wajibu wangu wa kidaktari, nami nikaelekea mpaka kwa jirani yetu. 

Tesha akawa amekuja kunifungulia geti, naye akasema kitu ambacho hata Bi Zawadi aliwahi kuniambia mapema sana kuhusu geti hilo. Ni kwamba kama mlango mdogo wa geti ungekuwa unaweza kufungukia kwa nje basi ningekuwa naingia tu badala ya kusumbuka kupiga hodi, hivyo nikaona nisaidie kuirekebisha hali hiyo kidogo. 

Nikamwomba Tesha atafute kamba nyembamba, msumari, na nyundo ikiwezekana ili tujigeuze mafundi hapo. Akatii na kufata kamba nyembamba iliyoendana na zile walizoweka hapo nje kwa ajili ya kuanikia nguo, msumari mrefu, lakini hakukuwa na nyundo. Akaleta tu jiwe. 

Nikaikata kamba hiyo kwa urefu uliotoshea upana wa kimlango hicho, kisha nikaifunga kwenye kale kadude ka kuvuta kwenye kifungio cha geti na kuipitisha nje kupitia uwazi mdogo mwanzoni mwa ukuta ambapo geti lilianzia. Nikatoka nje na kuugonga msumari ukutani, mwanzoni kabisa karibu na geti, kisha nikaifunga kamba hapo. 

Tukaanza kufanya majaribio kwa kufunga kimlamgo cha geti, kisha naivuta kamba kiasi nikiwa kwa nje ili ikikivuta kile kidude kwa ndani, kiachie, na huo mlango ukafunguka. Akili mtu wangu! Ilikuwa ni njia ndogo tu ya kurahisisha kazi kwa sisi tuliozoea kuja hapo, naye Tesha akasema ilikuwa ni njia nzuri sema aliona uvivu tu kushughulika na geti hilo. 

Nikaingia tena, na wakati huu ndiyo nikatilia maanani kuwa gari la Miryam halikuwepo, kumaanisha alikuwa ameshakwenda kazini. Nikamuuliza Tesha hali kwa sasa ilikuwaje, naye akaniambia tu twende ndani ili tukaongelee huko. 

Kweli tukaenda, nami nikakuta hali isivyo kawaida na nilivyokuwa nimezoea. Sikuwakuta Bi Jamila na Bi Zawadi wakiwa wamekaa kwenye sofa lao kama kawaida, na sikumwona Mariam pia. Nikadhani labda wapo chumbani maana kulikuwa na hali ya utupu hapo.

Tukakaa na Tesha sofani, nami nikamuuliza, "Mariam yuko poa?"

"Eeh, ila ndo' hayupo. Wote hawapo," akasema hivyo.

"Wapi tena?"

"Da' Mimi kawachukua kuwapeleka kwa Joshua. Wakaongee huko," akasema hivyo kwa njia ya kukerwa.

Nikamwangalia kwa umakini na kuuliza, "Kampeleka Mariam kwa Joshua?"

"Ndo' maana yake."

"Lakini si Miryam amesema anaenda kazini?"

"Ndiyo, kawapeleka huko wote na mama wakubwa, halafu ataenda kazini... labda na baadaye ataenda tena huko... kuwafata."

"Mbona we' hujaenda?"

"Kwani haiko wazi? Sitaki tu. Lakini nimesingizia kwa dada kwamba sijisikii fresh bado. Hapo wanaenda kudanganywa-danganywa tu na huyo fala."

"Aisee! Yaani akimgusa Mamu, atanitambua," nikajikuta nimesema hivyo kwa hasira.

"Nini? Nani, Joshua? Anataka kumuumiza Mamu?" Tesha akaniuliza hivyo kwa mkazo.

Nikamwangalia na kusema, "Aa... hapana, yaani namaanisha... hali ya Mariam siyo nzuri kivile bado, ikiwa ataogopeshwa sana na kaka yako itakuwa kurudi nyuma tena. Nimeongea tu vibaya."

"Siyo vibaya, me mwenyewe nitamuua huyo mjinga ikiwa Mamu atarudi hapa bila unywele hata mmoja. Sema ndiyo nimemwahidi dada kuwa mpole, kwa hiyo natulia tu."

"Ila ungeenda nao Tesha, huwezi kujua," nikasisitiza.

"Usiogope bro. Me najua Joshua anachokifanya hapa mwanzoni ni kuigiza tu, kwa hiyo lazima na mimi niigize pia. Hawezi kumgusa mtu yeyote sa'hivi, utaona," akanihakikishia.

Nikaangalia pembeni nikiwa nimeudhika kiasi. Sikujua nifanye nini maana hali hii ilikuwa ya kushtukiza, na hii ikanipa somo kuhusu kuwa chonjo zaidi na hii familia ili Joshua asije kufanikiwa kwenye mipango yake, mimi nikabaki tu mdomo wazi.

"Wanarudi saa ngapi?" nikamuuliza hivyo.

"Jioni. Hapa doro tu kaka. Nataka nikazurure wee mpaka hiyo jioni," akaniambia hivyo.

Nikatulia tu na kushusha pumzi.

"Oy... kama vipi tuoshe, ama nini?" akaniuliza.

"Kuelekea wapi?"

"Nataka nikazunguke Kigamboni leo. Halafu baadaye tutazamia kwa mshkaji fulani hivi, nina siku sijamwona. Unasemaje?" akasema hivyo.

Lengo la kuja hapa ilikuwa kuendelea na mazoezi yangu pamoja na Mariam, lakini hakuwepo. Sikuwa na jambo lingine muhimu la kufanya kwa hiyo nikaona nimkubalie tu rafiki yangu. Labda na matembezi yangeleta jambo jipya mbali na yale niliyokuwa natazamia yafike. 

Alikuwa ameshaoga kwa hiyo nikakaa kumsubiri alipokwenda kuvaa. Alivalia kawaida tu kama mimi, na kofia yake kama kibandiko kichwani ikanifanya na mimi nitake kwenda kuichukua ya kwangu, lakini nikaahirisha. 

Tukatoka pamoja, akafunga milango na geti, nasi tukaenda kwa Ankia ili Tesha amwachie funguo za kwao ili endapo kama ndugu zake wangewahi kurudi kabla yake basi wazikute hapo. Ankia akatutakia matembezi mema huku akisema tukirudi tumletee zawadi, nasi tukaingia barabarani baada ya hayo.

★★

Basi, tukawa tunatembea mdogo mdogo kuelekea Mzinga. Baada ya kufika Mzinga, kibishoo tu yaani, tukaamua kuifata Kongowe kwa kutembea pia. Mwendo wa taratibu tu, huku tukipeana story nyingi za mambo yetu wanaume ukatufikisha mpaka hapo Kongowe, na hii ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika eneo hilo tokea nimepajua Mzinga; na hata Mbagala pia. 

Mwanzoni mwa eneo hilo kunakuwa na sehemu nyingi zenye biashara ndogo na kubwa za wajasiriamali sanasana, nasi tukaelekea upande ambao daladala zingesimama kwa ajili ya kubeba abiria. Tukakuta moja ambayo ilikuwa ikielekea Kigamboni ndiyo, nasi tukaingia na kukaa siti za nyuma kabisa. Mwonekano wangu na Tesha ungefanya watu wafikiri sisi ni ndugu wa damu labda, maana kuna sehemu kubwa ya pigo zetu iliyokuwa inafanana sana. 

Tukiwa tu ndiyo tumekaa, Tesha siti ya dirishani kabisa na mimi pembeni yake, nikapokea ujumbe kutoka kwa mtu ambaye sikuwa nimetarajia kabisa kwa muda huu. Ilikuwa ni Adelina, dada mkubwa wa Joy; ama niseme marehemu Joy. 

Yaani tokea tumebadilishana namba pale msibani sikuwahi kumtumia salamu hata mara moja, ijapokuwa nilikuwa kwenye harakati za kumtafutia mdogo wake haki kwa mauaji yaliyomsibu. Alikuwa ametuma salamu fupi, 'habari yako,' nami nikatuma jibu kuwa 'niko salama' na kuuliza yeye aliendeleaje. 

Nikaanza kumsikia konda kutokea nje akisema kwa abiria fulani waingie kukaa, kwamba siti hazikuwa zimeisha. Yaani alikuwa anawashawishi kwa kusema tena kuna waarabu ma-handsome wamekaa huko mwishoni, na ndiyo Tesha akanishtua nitazame nje. 

Nikaangalia kupitia kioo na kuona wanawake wawili pamoja na mwanaume kijana mmoja, wote wakiwa ni waislamu, na mwanamke mmoja alivalia yale manguo meusi yanayoficha mpaka uso kasoro macho, lakini kale kengine uso ulikuwa wazi tu na kuzungukiwa kwa hijab kichwani. Kalikuwa kembamba, keupe, kenye macho mazuri kweli, na nahisi wao walikuwa waarabu kasoro huyo mwanaume kijana aliyekuwa mweusi kabisa; akionekana kuwa mwandamani wao. 

Huyo mwanamke aliyeficha uso alikuwa kama hataki kuingia kwa kuwa labda hakupenda kukaa mwishoni, naye Tesha akawa ananishurutisha tufanye jambo ili hako kadada kaingie maana alikuwa amekaelewa tayari. Adelina akawa amenitumia ujumbe akisema yuko poa na kuuliza kama bado nilikuwa Mbagala, naye Tesha akaendelea kunibonyeza-bonyeza mpaka nikahisi kero. 

Agh, nikasogea kufikia uwazi wa kioo na kuwaangalia wanawake hao, nami nikasema, "Dada, ingieni tu. Nafasi ziko tatu, yaani kama vile zimebaki kwa ajili yenu tu."

Mwanamke aliyekuwa amefunika mpaka uso akawa ananiangalia sana, naye konda akaongeza spidi ya kuwashawishi. 

Nikakaa sawa tena na kumwambia Tesha, "Nimeweka jitihada hiyo kama ulivyotaka. Umefurahi?"

Akacheka kidogo na kusema, "We' ni chizi! Ndo' mpaka utuchoreshe? Ona washamba wanavyotuangalia."

"Unasumbua mno," nikamwambia hivyo nikiwa makini na simu.

Nikamjibu Adelina kwamba bado niko Mbagala ndiyo, na kumuuliza kama alisharudi Mbezi. Tesha akanibonyeza kidogo, nami nikaangalia mbele na kuona wale wanawake wameshapanda na kuja upande wa nyuma. Yule mwanaume kijana hakupanda, inawezekana labda alikuwa anawasindikiza tu, nao wakaja kukaa pamoja nasi; nafasi iliyobaki ikiwa imetutenganisha katikati.

Kale kadada kenyewe kakawa dirishani kabisa, huyo mficha uso akiwa pembeni yangu, nami nikamtazama Tesha na jamaa akajikausha tu kama vile siyo yeye aliyenisisitiza kuwashawishi waingie. Inaonekana kwa muda huu abiria waliokuwa wanataka kuelekea huko mbele walikuwa wachache, kwa sababu hakukuwa hata na mtu aliyesimama na safari ikaanza. 

★★

Vuuu, mwendo ukaendelea huku na mimi nikiendelea kuchat na Adelina. Ilianza kidogo kidogo tu lakini mpaka ikafika hatua tukaanza kutaniana, kirafiki yaani. Akawa ameniambia kuwa kwa sasa hivi alikuwa amekwenda pale Mbagala kwa rafiki yake mmoja kumsalimia na ndiyo alifikiria uwezekano wa kupata nafasi ya kuja kunitembelea mimi na Ankia pale nyumbani. 

Unajua, mpaka leo Adelina alikuwa anafikiri mimi ni mume wake Ankia, ndiyo ikabidi nimwambie kwamba ile ilikuwa danganya toto tu niliyofanya pamoja na Ankia; wala hata hakuwa mke wangu, na ndiyo matani baina yangu na Adelina yalianzia hapo. 

Mwendo ulikuwa mrefu kiasi kuelekea Kigamboni, mara kwa mara watu wakiongezeka kwenye gari na kupungua, na uvumilivu ulikuwa unamshinda Tesha. Alitaka sana kuipata namba ya kale kadada keupe pembeni yetu, lakini alihofia kwamba huenda huyo mwanamke mwingine alikuwa mama yake kwa hiyo kungekuwa na utata. 

Lakini akawa ananishawishi kwa kunitumia sms nijaribu kumsemesha maana alikuwa na uhakika kwamba mwanamke huyo aliingia tu kwenye gari kwa sababu yangu, nami nikamwambia Tesha aache umalaya la sivyo ungekuja kumuua siku moja. 

Kama ninavyosemaga, mimi siyo mtu wa kuogopa mtu kabisa, na kama ningekuwa nataka kupata namba za mwanamke yeyote niliyekutana naye, ningezipata. Ila kuanza kumwelezea Tesha kwamba nilikuwa sitaki tu najua ingegonga mwamba, na hata hivyo nilikuwa nataka rafiki yangu huyu ajisikie vizuri tu baada ya mambo yote aliyokuwa amepitia jana, kwa hiyo nikamwambia atulie ili nimrekebishie mitambo. 

Adelina bado nilikuwa nachat naye, akiwa amesema kwamba anaweza hata akaja leo kunitembelea mimi na Ankia pale nyumbani, nami nikaona nimjibu kwanza. Nikamwandikia kuwa kwa sasa nilielekea Kigamboni kwa hiyo endapo kama alikuwa na mpango wa kwenda kwa Ankia muda huu, asingenikuta, lakini labda kama ni jioni ndiyo tungeweza kuonana. 

Ilishangaza kiasi kwamba hakuwa hata amemtafuta Ankia bado kuongelea suala la kwenda kumtembelea ilhali walikuwa ni marafiki, lakini labda ni kwa sababu tu hakuwa amewahi kuwasiliana nami kabisa, na kule kudhani mimi ndiyo kichwa sasa pale kwa Ankia. 

Nilipomaliza kumweleza, nikamtazama mwanamke yule mwislamu. Hilo baibui jeusi alilovaa lilificha uzuri wa ngozi nyeupe aliokuwa nao, maana nilitazama vidole vyake vyenye kucha ndefu kidogo na nyekundu, vilivyoshikilia simu ya macho matatu, na kiuhakika nikaona kwamba havikuwa na hata chembe ndogo ya sugu nyeusi. Sijui walikuwa waarabu kweli? 

Tesha akanibonyeza tena na kunipa ishara kwamba eti nichangamke, nami nikatabasamu kiasi na kufungua simu yangu tena upande wa sms. 

Nikaandika pale patupu hivi, 'Habari? Naomba namb yako kam hutojal'

Nikanyoosha simu kwa chini kumwelekea mwanamke huyo, naye akaitazama. Sikuwa hata nikimwangalia lakini nikamwona akinyanyua uso wake kuniangalia, hivyo na mimi nikamwangalia. Huwa naweza kuweka macho fulani hivi ya kumvuta mwanamke aamshe upendezi kunielekea, macho ya ushawishi yaani, nami nikawa namtazama kwa hiyo njia. 

Akaangalia mbele tu kama vile hataki, kisha akaichukua simu yangu kichinichini na kuiunganisha na yake. Nilikuwa nimeweka uso makini, nikiona wazi jinsi Tesha alivyojikausha kwa kujifanya anatazama nje tu, na kwa jicho la mbali nikaweza kuona mwanamke huyo anaandika kitu fulani kwenye simu yangu. 

Kisha, akaitelezesha simu kwenye hiyo siti kuelekea upande wangu bila kuitazama, kukiwa na pete nene zenye kuonekana kuwa kama za dhahabu kwenye vidole vyake viwili, nami nikaipokea nikiwa nimeweka mwonekano makini bado. Mambo ya siri hayo, na Tesha ndiyo akawa ameniingiza majaribuni! 

Wanawake wa hivi nawaelewa sana, yaani wanapoamuaga kujitafutia vitulizo vya nje huwa wanapenda mno usiri wa hali ya juu, na huyu inaonekana alikuwa amenielewa sana ndiyo maana akakubali kufanya hivyo akiwa pembeni ya binti yake, sijui mdogo wake, sikujua.  

Tesha akakunja ngumi yake karibu na paja langu, akiwa anataka tugonge tano ya ushindi, nami nikaweka kiganja changu hapo huku nikimnyanyulia kidole cha kati. Nikatazama simu yangu na kukuta namba za simu zikiwa zimeandikwa hapo, nami nikazitumia ujumbe.

'Jina lako mremb?'

Nikajikausha kama simwangalii, nami nikaona anaandika kitu fulani kwenye simu yake kisha akatazama pembeni.

Ujumbe ukaingia kwenye simu yangu, namba hiyo hiyo, ukisomeka, 'niambie lako na wew.'

Nikajibu, 'JC'

'Ndiyo nn'

'Ndiyo my name'

'Me naitw Ibtisam'

'Ooh saw. Jina lako zur kam wew mremb'

'Uremb wang umeon wp'

Nikiwa bado sijajibu ujumbe wake huo ndiyo tukawa tumeingia maegesho ya daladala kwenye eneo la Kigamboni, na watu wakawa wanasimama ili washuke.

Nikamwandikia hivi, 'Ngj tushuke nikwambie'

Kweli tukaanza kushuka mpaka nje, nami pamoja na Tesha tukaenda upande wa nyuma wa gari na kuwaangalia wanawake hao waislamu. Wenyewe wakaelekea upande mwingine kwa pamoja, huku kale kembamba kakigeuka kututazama mara moja.

Nikaangalia simu na kukuta ujumbe wa huyo mwanamke akiwa amejibu, 'Saw, lkn ntakuchek badae. Kun shm naend sahiv'

Tesha akaniuliza, "Oy, umemwambiaje? Anasemaje?"

"Kaka utakuja kuniweka matatizoni siku moja!" nikamwambia hivyo.

Tukaanza kutembea kuelekea sehemu iliyoturuhusu kuiona vyema Bahari ya Hindi.

"Kwani vipi?" akaniuliza.

"We' kila demu unataka tu, wengine ni majini."

"Ahahahah... me kwani nilikwambia namtaka huyo jini wako? Mimi nilikuwa nakataka kale kengine, we' si umechukua namba ya huyo maza'ake kwa upendo wako?"

"Nimeomba namba yake ili uje kuipata ya hako unakokataka. Halafu Tesha!"

"Hahahah... JC bana! Kwo' jini linasemaje?"

"Atanicheki baadaye, na linaonekana limeolewa. Ah, sijui hata kwa nini nimemwomba namba!"

"Si kwa ajili yangu? We' ukishamzuzua utanifanyia unyama na mimi nipate ya hako kengine. We' utakula mazeli, mimi kimweli. Tena tutafanyia kwenye double deka kabisa."

Nikacheka kidogo tu na kusema, "Tesha tunaingia Kigamboni, wanawake wazuri kama wote, utawasahau hao uliowaona. Tulia mdogo wangu."

"Ah, kwenda huko! Huu ndiyo wakati wangu, we' ushazeeka ndo' maana. Twende tukapande meli huko."

Nikacheka na kutikisa kichwa, nami kweli nikaanza kumfata.

Tukapita sehemu nyingi zenye biashara, watu wengi, wadada wazuri ndiyo usiseme, nasi tukaelekea sehemu ya kununulia kadi za tiketi kwa ajili ya kuvuka bahari kwenda upande wa pili wa Kigamboni; ule wenye majengo ya ukweli. Tesha akapata kadi, nasi tukaenda kuvuka kwa kupanda meli ndogo ya uvukishaji abiria na magari. Watu walikuwa wengi kufikia kiasi kilichohitajika, na wakati tukiwa tumeanza kuvuka mvua ikaanza kunyesha. 

Mpango ulikuwa kwenda kuzurura sehemu kadha wa kadha kwa eneo hilo, lakini mvua ikaongezeka mno kiasi kwamba jambo hilo likaingiwa na utata. Yaani ile tumeshuka tu, ikatubidi tuingie kwenye daladala ambazo zilielekea Kariakoo, na safari ikaanza tena. Hii haikuwa mara ya kwanza kutembelea Kigamboni na hata niliwahi kutoka na mwanamke fulani aliyekuwa wa pande hizi, ila hiyo ni hadithi nyingine, ya kusimuliwa kwa wakati mwingine. 

★★

Mwendo wa dakika kadhaa ukatufikisha mpaka Kariakoo, na kwa huku mvua ilikuwa ishakatika. Tukashuka, Tesha akiwa bado anawashwa kutembea, hivyo tukachukua mwendokasi na kwenda pande za Ubungo. Tukazurura wee, Tesha hata akanipitisha kule alikokuwa anaenda kufata wanawake wa kulipwa, chimboni yaani, naye akawa akisema hizo mishe siku hizi hafanyi. 

Tukatoka huko na kuzunguka mpaka Uhasibu, nasi tukashukia hapo. Tesha alikuwa na rafiki yake mwanachuo aliyekaa eneo la Uwanja wa Benjamin Mkapa, hivyo tukatembea mdogo mdogo kuelekea huko. Alikuwa ameshawasiliana naye. Yaani safari hii yote leo ilikuwa ni kwa udhamini wa Tesha, mimi ndiyo nilikuwa kama mtalii wake, nasi tulipokuwa tu ndiyo tumeyapita malango ya uwanja nikaanza kuona mdada fulani akija upande wetu taratibu. 

Tesha alikuwa ameniambia kwamba tunaenda kumsalimia tu mshkaji wake, kwa hiyo sikuwa nimetarajia kwamba ingekuwa ni mwanamke mpaka mdada huyo alipotukaribia na kukumbatiana na Tesha kirafiki. Alikuwa mfupi kiasi, mweusi, mwili wa kawaida tu, na tabasamu lake lilionyesha mwanya mdogo katikati ya meno yake ya mbele. 

Wakawa wanasemeshana kirafiki sana, naye akaniangalia na kunisalimu pia. Alikuwa mchangamfu sana, jina lake ikiwa ni Dina, naye akatuongoza kuelekea pale alipoishi. Ilikuwa ni kwenye zile nyumba za wapangaji zilizojaa hasa wanafunzi wa chuo, nasi tukaingia kwenye chumba chake. 

Kilikuwa simple tu, safi, godoro chini kwenye sakafu ya vigae, friji ndogo, begi la nguo pembeni ya shehena ndogo ya vyombo, vifaa vya mapodozi na manukato, viti vitatu vya plastiki. Jiko dogo la gesi lilibeba sufuria lenye chakula kwa ndani bila shaka, nasi tukakaa na kuanza kupiga story. 

Mimi nilikaa kwenye kiti, Tesha na Dina wakakaa kwenye godoro, na ni wao sanasana ndiyo walioongea huku mimi nikichangia mada mara moja moja kukoleza ucheshi. Dina akaniuliza natumia soda gani, nami nikamwambia Pepsi. Tesha vilevile akasema Pepsi ingawa alitania kutaka bia. 

Dina akatoka kwenda kufata soda, nasi tukabaki hapo, nikisikiliza maneno ya kipuuzi ya Tesha kuhusu jinsi nilivyotakiwa kubaki hapa leo ili nifanye jambo fulani na Dina. Ni hapa ndiyo nikawa nimepokea ujumbe kutoka kwa yule mwanamke mwislamu tuliyekutana kwenye daladala, akiwa ametuma tu 'mambo,' nami kabla hata sijamjibu, simu yangu ikaanza kuita. Mpigaji? Bertha. Hatimaye! 

Sikutaka Tesha asikie jambo lolote ambalo lingemfanya atambue nani naongea naye, hivyo nikapokea nikiwa nimejihakikishia kutosema lolote litakalomshtua jamaa.

"Hallo?" sauti yake Bertha ikasikika.

"Hello, vipi?" nikasema hivyo.

"Poa. Uko wapi?"

"Niko kwa Mkapa hapa."

"Unafanyeje huko?"

"Nimekuja kwa mshkaji wangu, niambie..."

Tesha akaniuliza kwa ishara, "nani?" nami nikamwonyesha ishara pia kuwa atulie.

"Nataka uje. Au biashara uliyonayo sasa hivi huko ni muhimu sana?"

"Hakuna chochote muhimu zaidi yako dear."

"Usiniite dear, mazoea ya hivyo sitaki."

"Sawa dear," nikasema hivyo makusudi.

"Halafu wewe!" akasikika kwa ukali.

Nikajikaza nisicheke na kumwambia, "Pole, nimejikwaa tu. Ulimi hauna mfupa."

"Na nitakuja kuuwekea mfupa usipoangalia."

"Sorry."

"Toka huko sasa hivi. Niko Masai," akaniambia hivyo.

Ni muda huu ndiyo Dina akawa ameingia ndani tena, lakini wakati huu alikuwa pamoja na mwanadada mwingine mweupe, mwembamba, mrefu kiasi, aliyekuwa amevalia T-shirt nyeusi na suruali ya jeans ya samawati iliyobana. Nywele zake zilisukwa kwa mtindo wa dread nyeusi na fupi, naye akaenda kukaa godoroni baada ya Tesha kunyanyuka na kukaa kwenye kiti.

"Umeelewa?" Bertha akasikika kwenye simu.

Nikasema, "Eeh, nimeelewa. Ila... niko mbali kama hivi, naweza kuchelewa kidogo."

Dina akawa ametufungulia soda zetu na kutupatia, na ukimya mfupi uliofuata kwenye simu ukanifanya nitambue kwamba Bertha alikuwa amekasirishwa na maneno yangu.

Nikamwambia, "Ila nakuja. Nitakuwa nimeshafika muda siyo mrefu."

Likakata simu!

Kazi nilikuwa nayo. Nikashusha pumzi na kumwangalia Tesha, aliyekuwa akinitazama kama anasubiri nijielezee. 

"Kuna dharura bro. Natakiwa nifike location mara moja," nikamwambia hivyo.

"Tumekuja wote, unataka kuondokaje mwenyewe bana?" Tesha akaniuliza kwa uthabiti.

"Iih, unataka kutukimbia?" Dina akaniuliza hivyo.

"Kuna dharura imetokea, nahitajika sehemu haraka ndo' maana..."

"Acha bangi! Hautoki hapa. Keki tamu kama hizi unakimbia kweli?" Tesha akasema hivyo kiutani.

Tukacheka kidogo, na Dina akamsonta huku akisema, "Afu' wewe!"

"Inanibidi tu kaka," nikamwambia Tesha.

"Jamani, mbona ghafla? Chakula hiki napakua," akasema Dina.

"Oh usijali Dina, niko poa. Labda umpakulie huyu mbwa," nikamwambia hivyo.

Akacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Em' pakua mama, tule."

"Basi kunywa hata soda, imeshafunguliwa," akaniambia hivyo yule mdada mwingine.

"Ee, kunywa soda ndiyo uende kaka," Dina akaniambia.

"Poa," nikajibu.

Ingenibidi nipige hii soda fasta maana huyo Bertha hakuwa mtu wa subira hata kidogo, na hiki ni kitu ambacho nilikuwa nimekisubiria sana kwa hiyo wiki nzima kwa hiyo nisingeweza kuchezea nafasi hata kama ningepewa ofa ya utatu na hawa wadada! 

Nikawa napiga fundo ndefu ndefu, huku nikiwa nimeanza kuchat na yule mwanamke mwislamu pia. Alikuwa mmoja kati ya wale wanawake ambao walipenda mtu aende moja kwa moja kwenye pointi ya kitu ambacho alitaka kutoka kwake, nami nikamwambia ndiyo, nilimkubali sana kutokana na kupenda macho yake na ngozi yake. 

Akaniambia ooh nimeshaolewa, kwa hiyo ukinitaka lazima upande ngazi, nami nikamwambia hakuna ngazi za kupanda; ikiwa alinikubali pia basi tuje kucheza, lakini asipotaka basi sitalazimisha. Kwa kauli hiyo akawa ametulia kwanza, nami nikawa nimemaliza soda. 

Nikamshukuru Dina na kusimama, Tesha bado akiwa analalama kuhusu mimi kuondoka, hivyo ikanibidi nitoe ahadi ya kuja naye tena kesho ikiwezekana kumtembelea rafiki yetu. Dina alipenda sana hilo wazo na kusisitiza nisije kuacha kuja, nami nikamwambia aondoe shaka. Huyo rafiki yake mwingine alikuwa akiniangalia sana kwa sura yake ya kiupole, nami nikamuaga pia nikiwa hata simjui jina. 

Nikawaacha marafiki hao hapo na kuanza kuelekea barabarani, nikiwa natumaini kuwahi, na Tesha asijue kwamba sehemu niliyokwenda ilikuwa ni Masai. Angeshangaa sana!

★★

Nilifanikiwa kupata usafiri wa daladala zilizoelekea Mbagala, na mpaka kufikia huko tayari ilikuwa inaelekea kuingia saa moja. Nilikuwa nikijiuliza ni kwa nini madam Bertha alikuwa ameamua kuja Masai mapema sana leo, lakini hayo yote ningeyajua nikishafika pale. 

Badala ya kuchukua daladala tena kutokea Rangi Tatu, nikaamua kupanda bodaboda ili niwahi zaidi, brrrr mpaka Mzinga, nami nikaunganisha moja kwa moja kufikia Masai, lakini nikaona nielekee kwa Ankia kwanza. 

Nikafika hapo dukani kwa Fatuma na kumkuta huyo dada pamoja na wanawake wengine wengine wakiwa wamekaa kama kikundi cha kupiga umbeya, nami nikamwambia bodaboda anisubirie nikachukue mzigo ndani kisha anirudishe Masai upesi. Nikawapita hao wavaa dera kama siwaoni, nami nikaelekea mpaka ndani na kuingia. 

Akili yangu ilikuwa imekazia fikira jambo moja tu kiasi kwamba mpaka nikashtuka kiasi moyoni baada ya kuingia na kumkuta Ankia akiwa amekaa pamoja na Adelina! Ile hali ya kutotegemea kumkuta mwanamke huyu hapa ingawa tulikuwa tumewasiliana ilikuwepo yaani, halafu nilikuwa kwenye kasi kwelikweli. 

Wawili hao, baada ya kuniona, wakatabasamu kwa pamoja, nami nikatabasamu pia na kusogea karibu zaidi na walipokaa.

"Mume amerudi," Adelina akasema hivyo.

"Ee, baba mwenye nyumba ndiyo kafika," Ankia akasema hivyo pia.

Nikajikuta tu natenda bila kufikiri sana kwa kuinama na kumkumbatia Adelina, nami nikamwambia, "Karibu."

Nafikiri alikuwa ameshangaa kiasi lakini akaweza kucheka kidogo kwa pumzi, naye akasema, "Asante."

Nikamwachia na kusema tena, "Karibu sana."

Kisha nikaelekea chumbani, bila shaka nikiwaacha wanawake hao wanatazama haraka yangu. 

Nikaingia chumbani na kutoa yale madawa niliyotengeneza, nami nikachukua kiasi kidogo na kukiweka kwenye karatasi tu baada ya kuwa nimekosa pa kuwekea, kwa kuwa sehemu niliyohifadhia dawa yote ilikuwa ndani ya mifuko minene; madawa yakionekana kama glucose. Nikachomeka hicho kikaratasi mfukoni, kisha nikaelekea sebuleni tena.

"Unatoka?" Ankia akauliza hivyo.

"Ndiyo, kuna sehemu nafika mara moja lakini... sikawii, nakuja. Sawa?" nikaongea hivyo nikiwa nimeelekeza fikira zangu kwa Adelina.

Akatikisa kichwa kukubali, naye Ankia akasema, "Unawahi nini kinachokutoa kijasho hivyo? Tuambiane..."

"Utajua tu, ngoja nirudi," nikasema hivyo na kuelekea mlango.

Nikawaacha wanawake hao wakicheka kidogo, nami nikaenda mpaka nje tena. Nikapanda bodaboda na kugeuza kuirudia Masai, nasi tukafika hapo huku sasa giza likiwa limeshaingia. Nikamlipa jamaa na kumwambia atokomee, kisha nikaelekea pale ndani. 

Wanywaji walikuwepo na nafikiri kuna wahudumu wapya waliokuwa wameongezwa hapa na wachache niliowajua kuondoka, nami nikawa nimemwona Bobo pamoja na DJ fulani hivi wa hapo Masai. Nikamfata.

"Oyo, mchina..." akaniambia hivyo tukiwa tunagonganisha mabega yetu kirafiki.

Nikagongesha tano kwa yule DJ pia, kisha nikamwambia Bobo, "Oya umepotea kweli."

"Ah, mimi, wewe? Yaani hutokei Masai siku hizi mwanangu. Check watu wanavyokuangalia kama vile hujawahi kuonwa hapa," akasema hivyo.

Nikatabasamu na kusema, "Na mimi nimetingwa kaka, ila mdogo mdogo narudi. Ishu zinakwendaje?"

"Kama kawa budha. Oy... mtu wako yupo huko ndani," akaniambia hivyo kwa kuninong'onezea sikioni.

"Eeh, nimeona gari nje," nikamwambia.

"Yuko VIP, kamchangamkie..."

"Ndo' mpango mzima," nikasema hivyo.

Tukacheka tena pamoja, kisha nikamwacha hapo na kuelekea pande ya VIP. Na Bobo alikuwa sahihi kabisa, watu walikuwa wananiangalia kweli, lakini umakini wangu wote ulikuwa kumfikia huyo madam. 

Nilipofika mlangoni, nikajiwekea hali ya utulivu, kisha nikaingia ndani hapo. Nikamkuta madam Bertha akiwa amekaa sofani, glasi yenye wine kiganjani, na kwenye sofa la pembeni alikaa yule baunsa wake; a.k.a shemeji. 

Kama kawaida ya mwanamke huyo, alikuwa amependeza kwa kuvaa kigauni kifupi chekundu, kilichoyaacha mapaja yake meupe wazi kutokana na namna alivyokuwa amepiga nne, na inaonekana kilikuwa cha mgongo wazi. Wakati huu alishonea wigi la nywele za kizungu kichwani, na baunsa wake alikuwa amevaa kaushi tu na suruali nyeusi, akionyesha misuli yake imara. 

Nikasogea usawa wa meza moja hapo, nami nikamtikisia kichwa jamaa kama salamu, naye akairudisha. Nikamwangalia Bertha, ambaye alikuwa akinitazama tu kwa utulivu, nami nikamwambia, "Nimefika madam."

"Umechelewa," akaniambia hivyo.

"Kweli? Mbona naona kama bado party haijaanza?" nikamuuliza hivyo.

Baunsa wake akamwangalia na kucheka kidogo, naye Bertha akawa amenikazia macho yake.

"Tupishe," Bertha akamwambia hivyo jamaa.

Baunsa akasimama na kuja upande wangu, naye akaniuliza, "Una ule unyama jembe?"

"Nakosaje labda?" nikamuuliza hivyo.

Akatabasamu huku akitikisa kichwa taratibu, nami nikaitoa ile dawa na kumfungulia. 

"Si iko kama ile?" akaniuliza hivyo.

"Kwa asilimia zote," nikamwambia.

Akachovya kwa kidole na kulamba, kisha akatikisa kichwa kwa nguvu kiasi na kunishika begani. "We' dogo ni nyoko!" akaniambia hivyo.

Nikatabasamu kidogo, naye akanipita na kutoka ndani humo. 

Nikabaki na madam. Alikuwa ananitazama kwa yale macho ya kuhukumu bado, naye akasema, "Njoo."

Nikatii na kumfata. Sikuwa na hofu kumwelekea huyu mwanamke, ila kujifanya mnyenyekevu sana ilikuwa lazima. Nikasimama usawa wa sofa alilokalia na kubaki mtulivu. 

"We' vipi, si ukae?" akaniambia hivyo.

Nikasogea na kukaa kwenye sofa karibu yake.

Akawa ananitazama sana, naye akasema, "Yaani hiyo sura! Kama mwanamke!"

Dah! Kashfa hizo. 

Nikatabasamu kwa kujilazimisha na kusema, "Asante. Moja kati ya silaha zinazonisaidia kupita huku na kule ni hii sura."

Akacheka kwa mguno, kisha akaweka glasi yake pembeni.
"Nimekufatilia kwa hiyo wiki dogo, naona una maisha magumu sana mpaka ukaamua kutoka Goba Center kuja kuishi Mbagala," akaniambia hivyo.

Umeona sasa? Nilikuwa sahihi. Huyu mwanamke alikuwa amefanya uchunguzi kunihusu mpaka kujua kitu ambacho bado sijaelezea kujihusu. Nikataka kujua anaelewa mambo mengi kadiri gani kuhusu maisha yangu.

"Ahah... eeh... maisha magumu. Nimekaa sehemu nzuri lakini... hazijanifiti ndo' maana nimeangukia huku sasa hivi," nikaongea hivyo kiupole, ikiwa kimtego zaidi.

Akasema, "Me sijali ulikuwa unaishi vipi. Nataka tu ujue nikiamua kukuharibia maisha yako endapo kama utanigeuka basi sitosita kuanza hata na familia yako."

"Usiwe na hofu juu ya hilo madam. Siwezi kukusaliti. Kwanza... familia yangu iko Mwanza, mimi huku ni mtafutaji tu kwa hiyo niko mwenyewe," nikamdanganya.

"Una uhakika na kile ulichojiingiza kukifanya huku dogo?" akaniuliza.

"Ndiyo najua. Nina ujanja mwingi, usinichukulie poa. Sema mambo huko Goba hayakwenda fresh tu ndo' maana nikaja huku kujitafuta, na najua nimejipata tena kwa kuwa chini yako. Sitakuangusha madam. Najua nachokifanya, na nitafata utakachonielekeza kufanya," nikamwambia hivyo.

Akatulia kidogo, kisha akasema, "Sawa. Nipe hiyo kitu nionje."

Nikamfungulia kikaratasi chenye dawa ya cocaine, naye akachovya na kulamba kidole chake huku akinitazama kwa macho makini. Kidogo tu yakalegea naye akawa ananiangalia utadhani ananitaka kimapenzi. Ah mimi nilikuwa mtaalamu bwana! 

Na angalau kufikia hapa nikawa nimetambua kwamba hakujua mengi zaidi kuhusu maisha yangu isipokuwa tu kuwa amefatilia na kujua nilikotokea kihalisi kabla ya kufika huku, kwa hiyo mchezo wangu kwake ungeendelea taratibu.

Vibe likiwa limemgonga, akaniambia, "Unyama mzuri huu."

Nikatabasamu kidogo.

"Kuna ishu nataka nikushirikishe," akasema hivyo.

Pasi ndefu hiyoo! Nikatikisa kichwa kuonyesha namsikiliza.

"Kesho utakuja pale pale ulipokuja siku ile, uje jioni," akasema hivyo.

"Sawa. Nije na unyama wetu?" nikamuuliza.

Akaweka macho ya udadisi, naye akauliza, "Unamaanisha kwamba unao mwingi?"

"Nimetengeneza kiasi fulani. Hakijazi mifuko mikubwa lakini si unajua ni tamu mno, kwa hiyo kidogo tu...."

"Ni nyingi," akamalizia maneno yangu.

Nikatikisa kichwa kukubali.

Akaninyooshea kidole chake na kunipiga kofi laini shavuni, naye akasema, "Safi sana. Kumbe we' kweli wa faida. Uje nao kesho. Nitakuelekeza mengine ukishafika."

"Imeisha hiyo," nikamwambia hivyo.

Akawa ananitazama kwa njia fulani utadhani alikuwa ananisoma, naye akasema, "Nataka kuona kama we' siyo mwanaume sura tu."

Nikamsogelea karibu zaidi na uso wake na kumuuliza, "Kivipi?"

"Kesho. Kesho ndiyo nitaona," akasema hivyo huku akipindisha shingo yake kiasi, midomo yetu ikiwa karibu sana.

Nikasema, "Ahaa... nilidhani unataka nikuonyeshe sasa hivi."

Akatabasamu na kuangalia chini, kisha akatoa tusi kunielekea bila kuniangalia. 

Nikatabasamu pia baada ya kuona kwamba alikuwa ameanza kuonyesha roho ya kuniamini kiasi, na bila shaka ishu hiyo ya kesho ingehusiana na mengi ya vitu nilivyotaka kuhakikisha vinaporomoka kwa msaada wa askari Ramadhan. Ingebidi kusubiri kuona.

Akawa amekivuta kinywaji chake tena na kuikunjua miguu yake, naye akaniangalia usoni. "Kwa hiyo toka mpenzi wako amekufa, haujaingiza substitute?" akaniuliza hivyo.

Nikatazama chini kwa ufupi, nikielewa alimaanisha Joy.

"Oh, nimegusa pabaya? Mhm... inawezekana ulikuwa unampenda sana."

"Joy na mimi ilikuwa kama biashara tu. Wala hakukuwa na kitu tense kivile," nikamwambia.

"Mm? Unanidanganya mimi? Ahah... unajua bado natakiwa niwe mwangalifu sana juu yako maana inaweza ikawa unataka kumlipizia kisasi mpenzi wako," akasema hivyo.

Dah! Lina akili!

Nikatoa kicheko cha kujilazimisha na kusema, "Madam una vituko. Najua hauamini hilo kwa sababu tayari unaniamini mimi."

"Unajuaje?"

"Usingemwambia bodyguard wako atoke nje kama ungeamini naweza kukufanyia kitu kibaya. Hadi dawa nayotengeneza unakula, kama ingekuwa kukuua si ningewekea hata sumu?"

Akatulia kidogo akiniangalia kwa umakini, naye akasema, "Huwezi kuwa na uhakika sikuzote. Ndiyo maana bado nataka nikupime."

Nikaegamia sofa, huku nikimwangalia kizembe na kusema, "Fanya chochote madam... JC ni mali yako sasa hivi."

"Nhhaa... unanifurahisha. Bado akili yako ni ndogo sana."

Nikamshika kiunoni taratibu, naye akawa makini na kuniangalia machoni. "Ndiyo unifunze sasa. Mi' wa faida kweli," nikamwambia hivyo kwa sauti ya chini.

Akabaki kuniangalia tu huku akizungusha-zungusha kinywaji ndani ya glasi aliyoshika, na ni hapo ndiyo mlango wa kuingilia ndani humo ukasikika ukifunguka. Kwa sababu nilikuwa nimeupa mlango mgongo, nisingeweza kujua nani kaingia upesi, lakini nikaona macho yake Bertha yakimtazama aliyeingia kwa njia ya kukerwa. 

Nikiwa nafikiri ni mhudumu labda au yule baunsa, nikageuka bila kuwa na utayari wa kumchukulia serious huyo mtu aliyeingia mpaka nilipojikuta nashangaa kiasi baada ya kuona ni Chalii Gonga mwenyewe!

 


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA 

★★★★★★★★★

Previoua Next