MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Ile nimemwona tu jamaa, pigo la moyo lilidunda kwa nguvu kiasi kutokana na kutotarajia jambo hilo, nami nikaliachia titi la Khadija. Mwanamke huyo akautoa mkono wake kwangu pia, akijikausha kwa kutazama pembeni, na Joshua alikuwa amesimama usawa wa sofa huku akitutazama. Nikawa namwangalia kwa umakini tu, nikishindwa kuelewa alikuwa ametokea wapi.
Cha ajabu ni kwamba, baada ya kuwa amesimama na kutuangalia namna hiyo, akaachia tabasamu hafifu huku akiniangalia kwa njia ya kirafiki usoni, nami nikaendelea kumtazama kwa umakini tu. Nilikuwa na uhakika kabisa kwamba aliona kile ambacho kilikuwa kinatokea hapo baina yangu na mke wake, lakini akajifanya kama hajaona ili kuendeleza unafiki wake.
Hapo ndiyo Bi Zawadi akawa ametokea jikoni, akiwa ameshika kikombe chenye chai na kusema, "Joshu... hadi nilikuwa nimeshasahau kama uko ndani jamani."
"Eeeh, nisamehe tu mama, huko tunakotoka hatuna vyoo vya kukaa. Hiki chenu kizuri hadi kidogo nisinzie," jamaa akasema hivyo.
Kumbe jamaa alikuwa chooni anajisaidia muda wote huo? Na inaonyesha alikuwa ameshusha limzigo lizito kweli maana alikaa zaidi ya nusu saa huko. Na wengine huwa wanakaa mpaka masaa!
Bi Zawadi akacheka kidogo na kuja kunipatia chai, naye akaenda kukaa kwenye sofa lake pale alipozoea.
Nikataka kunyanyuka ili nimpishe Joshua aketi na mke wake, lakini jamaa akasema, "Ah we kaa tu bro, me niko safi hapa."
Nikawa namwangalia tu kwa utulivu, naye akakaa kwenye mkono wa sofa huku akilaza mkono wake juu ya egamio la sofa karibu na Bi Zawadi. Mke wake alikuwa ameushona tu pembeni, akitulia kama malaika mpya aliyezaliwa leo. Ni hapa ndiyo Mariam akawa amerudi tena, na sijui kwa nini tu alikawia mno.
Akaja mpaka sofani akiwa ameshika penseli, boksi lenye rangi, pamoja na counter-book kubwa, naye akasema, "Hizi hapa. Tumchore sasa."
"Mamu subiri kwanza kaka anywe chai," Khadija akamwambia hivyo.
"Eeh, ngoja kwanza. Mtachora baadaye," Bi Zawadi akasema hivyo pia.
Mariam akaweka uso wenye kuonyesha kwamba alikwazika, nami sikupenda kumwona hivyo. Lakini ningefanyaje na sukari ilikuwa imeshakorogwa kwenye chai?
"Mamu... usinune mama, eti? Anamalizia tu kunywa chai halafu ndiyo mtachora. Tena na mimi nitachora na nyie, sawa?" Joshua akamsemesha hivyo kwa kubembeleza.
Mariam akawa bado amenuna, naye akanyanyua bega lake kuonyesha kwamba hataki.
Nikasema, "Haina shida, tutachora huku nakunywa na chai. Cheupe wangu, asante. Mamu... twende."
Nikasimama pamoja na Mariam, ambaye bado alikuwa kama amenuna lakini akaridhia kwenda nami upande wa dining, nasi tukakaa vitini na kuanza kuchora.
Nilikuwa namchorea mambo rahisi kama kiti, mpira, yai, kikombe, naye angeiga kwa kujitahidi kabisa kuvifananisha. Nikawa namsifia, hata Bi Zawadi na Joshua wangekuja hapo na kuangalia kazi za binti na kumpongeza, na hii ilisaidia kumwongezea Mariam hali ya kujiamini zaidi nilipoanza kumpa michoro ya mambo tata zaidi.
Aisee Joshua alikuwa anajua kuigiza! Yaani nilikuwa nikitazama namna alivyoongea na kuwatendea wanawake hawa kana kwamba alikuwa amezaliwa kwa mara ya pili na kuwa mtu tofauti kabisa, lakini ukweli wa utu wake mbaya bado ulikuwa pale pale.
Sikupenda kabisa alipomsogelea Mariam na kumsemesha ama kumgusa, na nilikuwa nimeona niendelee kutulia tu ili amani ambayo niliiona ndani yake Mariam kwa wakati huu ibaki hapo hapo kwanza. Huyu Joshua angehitaji kuumbuliwa na kuondoshwa hapa kwa nguvu ya Miryam pekee, ambaye alikuwa ndiyo njia iliyofanya jamaa akapata kiburi cha kurudi tena.
★★
Kufikia mida ya saa saba mchana tayari mke wake Joshua alikuwa ameshaanza kufanya harakati za mapishi hapo ndani, na sijui kwa nini tu lakini mpaka sasa hivi bado tu Tesha hakuwa amefika. Hali yake Mariam kwa wakati huu ilikuwa changamfu kweli baada ya mimi kufanya kitu kilichompa furaha sana.
Alikuwa ameleta picha moja nzuri sana ya Miryam kutoka kwenye album, naye alinitaka nimchore dada yake. Nilikuwa najua kuchora lakini ikifikaga kwenye pua za watu ndiyo huwaga naharibu kabisa, ila nilipoichora pua ya Miryam niliikuza sana kwa makusudi ya kumchekesha Mariam. Na walicheka mno! Bi Zawadi, Khadija, na hata Joshua Iskariote, wote wakawa wanaiongelea mno, na kilichokuwepo ilikuwa kuja kuwaonyesha wengine na hasa Miryam, ili waone itikio lake.
Halafu huyo Khadija, tokea muda ule Joshua katushtukiza, alikuwa analeta pigo za kimahaba kunielekea kwa kunitazama kwa yale macho na tabasamu la "ninakutaka," ama kujipitisha-pitisha dining ili niangalie jinsi kalio lake lilivyonesa huko nyuma, lakini mimi bado nilikuwa tu nawaza kuhusu usalama wa Mariam kwa ujumla kwa kuwaza zaidi juu ya mume wa huyo mwanamke.
Jamaa hakuwa amenisemesha tena kwa sababu nilionyesha wazi kwamba sikutaka mazoea naye hata kidogo, lakini niliweza kuona namna alivyokuwa ananitazama sana kama vile ananichora kutambua nimekaaje-kaaje, na nadhani alikuwa ameshatambua kwamba sitaki shobo naye kabisa.
Hazijapita dakika nyingi sana toka imeingia saa saba ndiyo tukasikia mlango wa geti nje ukifunguliwa na kufungwa, na baada ya hapo mlango wa kuingilia sebuleni hapo ukafunguka pia na Tesha kuingia. Mwonekano wake ulikuwa ule ule wa jana, lakini bila shaka kwa siku hii alikuwa ametoka huko kwa Dina akiwa ameoga.
Baada ya yeye kuingia, akamsalimu mama mkubwa wake na kuitikiwa vizuri tu, lakini nikaona anamtazama Joshua kwa njia ya kusita kutoa salamu. Akawa ameniona nikiwa na Mariam hapo dining, nami nikamtikisia kichwa kisalamu. Akairudisha salamu yangu namna hiyo hiyo, naye Joshua akaona amsemeshe.
"Vipi mdogo wangu?" jamaa akamuuliza hivyo Tesha.
"Poa," Tesha akamjibu kibaridi tu na kumpita.
Akaja mpaka upande wetu na kumsalimia Mariam, na binti akamwonyesha ule mchoro wa picha ya dada yao.
Tesha akacheka na kusema, "Dah! Kaka naona unataka kutangaza vita na Mimi! Akiiona anaweza akavimba wiki nzima."
"Kweli? Itabidi Mamu asimwonyeshe," nikamwambia.
Mariam akasema, "Tamwonyesha... atacheka."
"Eeh usiache kumwonecha... atacheka chana," Tesha akasema hivyo kwa kuiga ongea ya Mariam.
"Bado hizo silabi silabi hazijakaa safi mdomoni kwa Mamu eh? Ila baada ya muda ataongea vizuri kabisa kama zamani," Joshua akadakia kwa kusema hivyo kutokea pale masofani.
Tukaangaliana na Tesha machoni kwa njia ya kukerwa na hilo. Utafikiri alijua lolote, eti silabi silabi!
Bi Zawadi akamwambia Joshua, "Eeeh mazoezi yataendelea kumsaidia sana."
Tesha akakaa kitini na kutoa simu yake huku akiniambia, "Dah! JC
mwana bora jana usingeondoka yaani Dina alipika bonge la msosi."
Nikatabasamu tu.
"Hivi Dina hajamalizaga tu kusoma?" Bi Zawadi akamuuliza Tesha.
"Eti?! Yaani mpaka Leo bado tu anakomaa na vitabu. Siyo mbaya lakini, kwao wanazo kwo' lazima aongeze mamiaka," Tesha akamwambia hivyo.
Inaonyesha wanafamilia wa Tesha walimfahamu Dina pia kutokana na jinsi ambavyo Bi Zawadi alimwongelea, labda hata alikuwa mtoto wa rafiki wa karibu. Simu yangu ikaingiwa na ujumbe, nami nilipouangalia nikakuta ni Tesha ndiyo kanitumia. Sikumtazama kwa sababu tayari nilielewa kwamba alikuwa ananisemesha bila kutaka wengine wajue amesema nini, nami nikausoma.
'Huyu fala amekuja saa ngp,' ikasomeka hivyo sms yake.
Nikajibu, 'Nimemkut mapem. Labd amekuj asubh San'
Bi Zawadi na Joshua wakawa wanaendelea na maongezi mengine, huku mke wa jamaa akiwa ameenda kukaa sofani na mume wake kwa kile kilichoonekana kuwa kumaliza kupika mboga, naye Tesha akawa anamsemesha Mariam huku akiendelea kuchat na mimi.
'Bado analet maigizo yak tu hap,' ujumbe mwingine wa Tesha ukasomeka hivyo.
Nikajibu, 'Uhakika. Ila we mtulizie tu kwanz'
'Na Bi mkubw mbn simwon?'
'Dada yako kampelek kupim, hakuw frsh'
'Aa, barid. Tunakaa hapa hapa kuhakikisha huyu bwege haondok hat na bakul'
Nikatabasamu kidogo na kumwandikia, 'Kuna kitu ntakwambia, ila baadae'
'Kuhusu Joshu?'
'Mke wake.'
'Si uniambie now?'
'Tulia. Ni ubuyu mwing'
'Au siyo? Kama vile nshaanza kunusa haruf yak. We mkal san'
'Haha akil yako hiyo'
'Kam yakwako tu. Twend hat kw Ankia tukaongee'
'Poa.'
Nilipomaliza kumjibu hivyo, nikawatazama wale wengine pale sebuleni na kusimama, kisha nikasema, "Mrembo wangu, me wacha niwakimbie sasa."
Bi Zawadi akasema, "He! JC baba, tunaivisha."
"Ahah, usijali... na ningependa sana kuenjoy mlo. Sema... kuna ka-appointment sehemu... nahitajika kwenda," nikamwambia hivyo.
Nilikuwa nataka tu kwenda kwa Ankia ndiyo nikale maana alikuwa anaandaa msosi wa ukweli! Nilikuwa nimepitisha muda sijala pilau kwa hiyo masikio yalikuwa yamenisimama.
"Una kaapointinamenti wapi na wewe? Utafikiri umeoa!" Bi Zawadi akasema hivyo.
Tesha akacheka kwa furaha na kusema, "Kaapointinamenti? Ma' mkubwa hauendi mbinguni!"
Wengine wakacheka kidogo pia.
"Kisa?" Bi Zawadi akauliza.
Tesha akasimama na kusema, "Unaharibu lugha za watu bwana. Oya... unajua ile 'what's wrong' wazungu wanayoisemaga kuonyesha wanajalii? Mwambie ma' mkubwa aiseme... utacheka! Eti 'wothilong'o mai diya!'"
Wote tukacheka kwa pamoja, naye Mariam akasimama pia huku akiniangalia kwa furaha.
"Ila Tesha! Ahahah... ananizingua tu huyu. Me naisemaga hivyo?" Bi Zawadi akalalamika.
"Hebu iseme umpinge," Khadija akamwambia hivyo Bi Zawadi.
"Whots wrongg," Bi Zawadi akaivuta kama kwa lafudhi ya mzungu.
Tesha akacheka sana.
"Sasa je! Mbona ameisema vizuri?" Khadija akamwambia hivyo Tesha.
"Eeh, umeisema vizuri sana mama. Kama mzungu uliye wewe," Joshua akampamba namna hiyo.
"Muone kwanza! We' ndiyo huendi mbinguni Tesha," Bi Zawadi akasema hivyo kimaringo.
Tesha akasema, "Haya bwana, kisura umeshinda. Twende nikutoe nje bro."
Nikiwa natabasamu tu, nikamwambia Mariam, "Tutaonana baadaye rafiki yangu. Endelea kuchora-chora hizi hapa... na hizi... halafu uje umwonyeshe dada, sawa?"
Akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, na baada ya Tesha kuyaangalia yale niliyomwambia Mariam ayachore, akatabasamu kidogo.
Nikaanza kuelekea hapo walipokaa wengine, Tesha na Mariam wakinifuata kwa nyuma, na ile tu ndiyo nataka kumpita Bi Zawadi, Joshua akasimama. Alikuwa amekaa pale ambapo niliketi na mke wake mwanzoni, Khadija akiwa pembeni yake wakati huu, kwa hiyo aliposimama ikawa ni kama vile amenizibia njia. Nikamtazama machoni kwa umakini.
"Kaka... ninaomba kuongea na wewe kabla hujaenda," akaniambia hivyo, kistaarabu tu.
Nikaendelea kumtazama kwa umakini, huku jicho pana likiona namna ambavyo mke wake alituangalia kama mtu mwenye wasiwasi.
"Maongezi tu mafupi ya kiume. Na Tesha pia. Twendeni hapo nje," Joshua akasema hivyo.
Nikatikisa kichwa kuonyesha nimekubali, nami nikamtazama Tesha na kukuta ananiangalia kwa umakini. Yale macho yanayojuana yaani. Haya, nikamuaga Bi Zawadi na Mariam kwa mara nyingine tena, na kisha sisi watatu tukatoka ndani hapo na kwenda pale kibarazani. Jua lilikuwa kali siyo mchezo!
Mimi na Tesha tukasimama kama vile tumemzingira Joshua, akiwa katikati ya ile pembetatu itengenezwayo na watu watatu kusimama pamoja, naye akawa anatuangalia kwa njia yenye upole.
"Eh bwana... nimeona nichukue hii nafasi kuzungumza na nyie kwa pamoja kwa sababu sisi wote ni wanaume, sawa? Tunaelewana kwa mapana zaidi ya vile ambavyo wanawake wanaweza kutuelewa... kwa hiyo... najua nitakayosema mtayaelewa kwa akili pana zaidi..." akaongea namna hiyo.
Alikuwa ameanza kuongea kwa njia iliyoonyesha kwamba alifanyia mazoezi kile ambacho alitaka kusema, nasi tukaendelea tu kutulia huku mimi nikitazama chini, na Tesha akimwangalia jamaa machoni kwa umakini.
"Najua kuna mambo mengi yametokea na... mengi niliyofanya ni mabaya..."
"Hapana, ni yote," Tesha akamkatisha kwa uthabiti.
Joshua akatulia kidogo, kisha akasema, "Ndiyo... yote niliyofanya ni mabaya. Siwezi kusema naweza... kufanya chochote kile kutangua mabaya yote niliyofanya, mabaya yote niliyosema, na kwa wewe Tesha... naelewa bado una hasira na mimi. Najua nimekufanya unichukie sana... na najua itachukua muda mpaka kufikia kipindi ambacho utanisamehe kabisa mdogo wangu... lakini hiyo ndiyo sababu niko hapa sasa hivi. Nimetambua kwamba niliwaumiza sana, na huwa natamani hata muda urudi nyuma ili paap, nifute yote mabaya, lakini haiwezekani kabisa. Ndiyo maana niko hapa sasa hivi... nimerudi ili tuijenge upya tena familia yetu... kuwe na amani tena. Hii yote naifanya ili niweze kuja kufa nikiwa na amani ya rohoni, siyo kuja kuingia kaburini nikiwa nachukiwa na ndugu zangu kabisa Tesha. Nyie ndiyo familia niliyonayo, niliyobakiza, na ninajua... najua nimewakosea sana kwa sababu ya kuendekeza tamaa lakini Tesha... Tesha nakuapia kwa majina ya marehemu wazazi wetu... niko hapa tena ili nirekebishe mambo upya... kwa ajili ya kumbukumbu ya wazazi wetu..." mwamba akaongea hivyo kwa upole.
Nilimtazama usoni kwa mkazo sana, nikiwa nahisi hasira ya kutaka hata kumtandika ngumi moja tu ya pua, lakini nikaendelea kutulia. Tesha akawa ameangalia pembeni baada ya kaka yake kusema hayo, naye Joshua akanitazama.
"Bro... nyie wote ni ndugu zangu. Najua mara ya kwanza tumekutana tulizinguana, na ilikuwa ni makosa yangu. Leo ndiyo nikuombe msamaha kaka. Kwa... kukutukana, kukutishia kukupiga, yaani..."
"Ahah... ungemweza sasa JC?" Tesha akamkatisha kwa kumuuliza hivyo.
Nikacheka kwa pumzi ya chini na kuangalia pembeni.
"Eee... tena unasema kweli. Nisingemuweza... angenivuruga kabisa. Unaona mdogo wangu... matatizo hayo yote ningejisababishia tu kwa kazi isiyokuwa na faida, na... Miryam ndiyo akanifanya nifungue akili yangu tena. Aliniita, akanikalisha, huyu mwenyewe alikuwepo hiyo siku ofisini kwake... aliniita, nikaenda kumsikiliza, nikamwelewa..." jamaa akaongea hivyo.
Tesha akaniangalia na kuuliza, "Da' Mimi alimwita huyu ofisini kwake? Na wewe ulikuwepo?"
Kabla sijamjibu, Joshua akadakia, "Eeh, aliniona pale, nilienda. Miryam huyu! Miryam ndiyo dada! Yaani kama nisingekuwa fala fala huko mwanzo, sasa hivi tungekuwa tunaishi bila misukosuko yote. Na ni makosa yangu..."
Aliongea, yaani, kama mtu mwenye huzuni sana, nami nikatazamana na Tesha kama vile bado hatumwelewi jamaa.
"Sikilizeni. Mimi hapa nipo... kutafuta tu amani tena... kuwaenzi wazazi wetu Tesha, na... ili Miryam na Mariam wawe na furaha. Nakuomba tu Tesha yale mapito ujaribu kuyaweka pembeni mdogo wangu. Hata kama itakuchukua muda mrefu kunisamehe, haina kwere, la muhimu tu kuwe na amani kwa muda huu wote. Mimi sitaacha kuwaonyesha jinsi nilivyobadilika... na Miryam amenisaidia sana, mpaka sasa hivi Mamu haniogopi tena, umeona? Kwa hiyo ni hivyo. Halafu nyie yaani... washkaji sana, tena huyu... JC... msomi hahah... tukiwa good hapa mambo mengi sana yatanyooka," Joshua akasema hivyo.
Alipokuwa ametamka jina langu, alinishika begani kwa njia ya kirafiki, lakini Tesha akautoa mkono wake kwangu taratibu.
"Sikia Joshua. Kama ulivyosema... kukusamehe itachukua muda. Sijui kuhusu wengine, ila mimi... itachukua muda. Kwa hiyo, we' endelea na shenanigan yako ya kutafuta amani, fresh, hakuna shida. Me nimetulia. Sikugusi, sikufukuzi tena. Ila... nitoe tu kaonyo. Ikitokea tu yaani, kale kashetani kako kakakurudia... kakakuingia tu tena ukaamsha majini-wizi yako, aisee! Siyo Mimi, ma' mkubwa, wala Mzee Hamadi watakaoweza kukusave tena. Zamu hii tutatibuana haswa... na nakwambia haya yote JC yuko hapa anasikia, kwa hiyo tusije tukalaumiana. Ushanisoma?" Tesha akasema hivyo kwa sauti ya chini lakini imara.
Kijana huyu alikuwa ameongea kile kitu ambacho hata mimi ningesema pia, lakini kwa wakati huu nilikuwa nataka kuyatimiza hayo maneno ya Tesha kwa sababu nilijua vizuri sana kwamba hako kashetani bado kalikuwa kichwani kwa huyo mwanaume.
Joshua akajichekesha kidogo na kusema, "Haina shida mdogo wangu. Usikonde. Umekuwa simba kweli, nakuaminia sana."
"Imeisha hiyo," Tesha akasema hivyo na kutazama pembeni.
Simu yangu ikaanza kuita papo hapo, nami nikaitoa na kukuta ni Ankia ndiye aliyekuwa ananipigia. Nikapokea na kumsikia mwenye nyumba wangu akiniambia niende kunywa supu ya kuku na pilau ilikuwa mbioni kuiva, nami nikamwambia poa.
Nikashusha simu na kusema, "Nahitaji kuwahi."
Niliongea hivyo bila kumwangalia Joshua hata kidogo, huku nikiona yeye ananikodolea tu, nami nikampa Tesha ishara ya kichwa kuwa anifuate. Tukatoka hapo kibarazani bila kusema lolote lile kwa huyo Joshua, tukimwacha anatusindikiza tu kwa macho mpaka tulipokwenda nje.
Nikawa nimemweleza Tesha kwa ufupi kuhusiana na lile suala la kukutana na Joshua kazini kwake Miryam, nikimwambia ilikuwa ni wakati ambao nilienda kwa dada yake ili kumzungumzia Mariam, ikionekana ni kutokea kipindi hicho Miryam ndiyo alikuwa ameanza kumvuta tena Joshua kwa ajili ya kuleta amani na ndugu yake. Lakini ndugu mwenyewe alikuwa ovyo!
Nilikuwa najihisi kuchafukwa rohoni yaani! Basi tu yaani huyo mwanaume hakuwa muungwana kabisa hata kwa jicho la kawaida tu, yaani hakufaa. Mpaka anatumia uzito wa kumbukumbu ya vifo vya wazazi wao ili tu ajionyeshe kuwa mtu mpya eti, kiukweli alinifanya nimchukie mno. Ila zake zingetimia tu, na hazingekawia.
Tukaingia kwa Ankia pamoja na kumkuta akiwa na mama Chande, best yake. Ndani palinukia kweli pilau na vitunguu swaumu na kuku, na kama kawaida yake, Tesha akaanza kutaniana na wanawake na kuwafanya wacheke kwa furaha. Inaonyesha Ankia alikuwa amepata msaada wa mapishi kutoka kwa mama Chande ndiyo maana aliwahi kutengeneza vyakula, na kwa msukumo wa jiko la gesi mambo yalikuwa fasta tu.
Wanawake wakiwa wamekaa hapo sebuleni, sisi tukaelekea chumbani kwangu ili kwanza tusimuliane mambo yetu vijana ambayo Tesha alipenda kupita maelezo. Alitaka kujua kuhusu mke wake Joshua, lakini mimi nikataka aanze yeye kunisimulia kuhusiana na yule Winny. Yaani siku wamekutana ilikuwa vipi na mpaka sasa hivi walikuwa wapi.
Ah, akasema yaani yule alikuwa na dharau sana. Eti alipokwenda kukutana naye, mwanamke huyo alimwona kuwa kama mtoto mdogo na alifikiri hangeweza kazi. Winny hakuwa wa aibu, alimpa Tesha penzi lakini alikuwa haridhiki. Tesha akasema alipiga vitano bila kutumia dawa na bado mwanamke akawa anataka waendelee!
Nikacheka na kumwambia huyo alikuwa anataka kumkomoa tu, na yeye akasema ni kweli kabisa kwa kuwa baada ya hapo alipoendelea kumtafuta kwa simu demu akawa anamkwepa tu; kumaanisha alikuwa na mishe zake nyingine za kuzungushia utamu. Ila akadai kwamba alimkubali sana huyo mwanamke kwenye ukataji wa viuno, na angalau alimla bila gharama!
Hiyo yote ilinifurahisha sana hasa kutokana na njia yake Tesha ya kuongea, na sasa ndiyo akataka kujua kuhusu mke wa kaka yake. Nikamwambia kwamba huyo mwanamke alikuwa ananitaka, nami nikamwelezea mambo yote yaliyotokea pale kwao baina yangu na huyo Khadija.
Akashangaa! Yaani haingeingia akilini mwake kufikiri huyo mwanamke alikuwa wa hivyo, akieleza sababu kuwa Khadija alikuwa mpole sana na mtulivu wa ndoa, ila ndiyo hapa akaona ukweli wa ule msemo 'kamwe usichukulie kuyajua yaliyo ndani ya kitabu kwa kuhukumu tu jalada lake.'
Nikamwambia sikuwa na uhakika wa kitu cha kufanya kuelekea suala hilo, lakini Tesha akasema ish! Piga tu! Kama mwanamke aliitaka kwa nini anyimwe? Nikacheka na kumuuliza hana kwere kwa sababu ya mwanamke huyo kuwa shemeji yake? Akaniambia hakuna kitu kama hicho, yaani hata kama Khadija angekuwa amejisogeza kwake na kuanza kumsugua-sugua miguu, hata yeye angepiga tu!
Aisee, nikamwambia ndiyo hivyo, na mimi sikuwa na ile kusema nimemtaka sana huyo mwanamke ila kama angelazimisha mambo basi ningemkoa tu na yeye. Tesha akasema tena kwa hilo aliniunga mkono wake kwa asilimia zote, akifikiri ni masuala ya kujifurahisha tu, kumbe mimi nilikuwa nataka kuchimba zaidi ndani ya suala la maovu ya Joshua.
Maongezi hayo yote yalifanywa kwa sauti ya chini ili wanawake pale sebuleni wasitusikie, na ndipo Ankia akawa ametuita twende huko. Nikamwambia Tesha huo ulikuwa ni mwito wa kunywa "thupu" ya kuku, na sikuwa nimekosea.
Kweli tukakuta Ankia akiwa ametuwekea mimi na Tesha supu pamoja na nyama kwenye mabakuli, nasi tukakaa ili kujinywea. Alikuwa kwenye harakati za kwenda kuanza kukaanga nyama za kuku ili aziunge vizuri kwa mchuzi wa nyanya na mapocho ya upishi wajuayo wanawake, nasi tukaendelea kunywa huku tukipiga story.
Mada ilikuwa sanasana kuhusiana na Simba na Yanga, jinsi timu hizi zilivyokuwa zimeingia kwenye michuano ya kimataifa barani mwetu, na mechi ya watani wa jadi iliyokuwa inakaribia kuchezwa. Ubishi na maneno ya sutu uliwajaa sana Tesha na mama Chande, hadi Tesha alikuwa anamfanyia mwanamke huyo zile pigo za kike za "ng'oo ng'oo" huku akikandamiza pua kwa kidole, nasi tukawa tunacheka sana. Wanaume tulikuwa Simba, wanawake Yanga, kwa hiyo utani wa maneno hapa ulikuwa mwingi sana.
Tukiwa tunaendelea kufurahia maongezi bwana si simu yangu ikaita? Mpigaji hakuwa mwingine ila madam Bertha, mwanamke shupavu, muuaji, na mwenye jeuri kama lote. Nikapokea hapo hapo na kumsikiliza. Alikuwa ananitaka niende kule Royal Village sasa, ikiwa ndiyo muda alioona unafaa wa mimi kutoka huku nilikokuwa. Akasema nisisahau kubeba na unyama wote niliokuwa nimetengeneza, nami nikamwambia poa. Akakata simu.
Nikaangalia muda; saa tisa kasoro. Dah! Huyo mwanamke alijua kunikatishia hamu! Yaani na hapa pilau na kuku ningezikosa tu kisa kufuata amri zake! Lakini haikuwa na noma. Nikamtaarifu Ankia kuhusu safari yangu ya ghafla kuelekea jijini zaidi, naye akaanza kununa. Eti yaani kanipikia pilau halafu naondoka? Sawa tu.
Nikacheka kidogo na kumwambia hapo naenda kusaka hela za likizo ndiyo maana, ila nikamwambia ningekuja tu kuila pilau yake baadaye. Tesha akaniuliza ikiwa hii ndiyo dharura iliyokuwa imefanya niondoke na kwao pia, nami nikakubali, nikisema kuna jamaa aliniita ili akanipange juu ya mambo fulani.
Kwa hiyo nikatoka hapo sebuleni na kwenda chumbani tena, na nilikuwa nawaza labda niende kuoga tena ila kutokana na uharakishi wa madam nikaamua tu nibadili mavazi na kuvaa kwa mtoko bomba zaidi. Nikajitengeneza vyema, kisha nikachukua lile begi langu la mgongoni na kulipunguzia vitu nilivyokuwa nimeweka humo, halafu nikachukua mifuko ile yenye madawa ya cocaine na kuitumbukiza kwenye begi.
Nilihakikisha kuacha nguo chache na vifaa nilivyochukua hospitali ili dawa zifichike pia, kisha nikavaa viatu na kutoka hatimaye. Marafiki zangu walifikiri labda nataka kusafiri kwa siku kadhaa kutoka huku, lakini nikawahakikishia kwamba ningerudi leo leo, ama kesho. Tukaagana vizuri baada ya hapo, nami nikaondoka kwenda kupanda daladala.
★★
Safari ya kuelekea Makumbusho ilidumu kwa masaa mawili kabisa. Hii ilisababishwa na msongamano wa magari hasa tulipofikia eneo la Keko, na kwenye ile round-about pale sipajui jina, lakini ilikuwa jam kali kweli mpaka kuhitaji mwongozo wa askari wa usalama barabarani. Kwa hiyo nimekuja kufika Makumbusho ikiwa ni saa kumi na moja jioni, na kwa muda wa nusu safari nilikuwa nimesimama baada ya kumpisha mwanamke mjamzito aketi kwenye siti yangu, hivyo miguu ilikuwa inaita kwa kiasi fulani.
Nikatoka Makumbusho, kama kawaida nikapanda Uber na kuanza kuitafuta Royal Village Hotel. Nikiwa njiani, nikaona nimpigie madam Bertha kumuuliza kama na leo nilitakiwa nipande lifti pale hotelini, kisha labda kwenye lifti hiyo ningekutana na mwanamke ambaye angenipa funguo ya chumba ambacho madam angekuwepo. Akaniambia niache ujinga na nifike kule tu kisha nimjulishe, na ile nataka tu kusema kwamba nimekaribia, akakata simu. Doh!
Nikajikuta tu nacheka mwenyewe, lakini hiyo haikumaanisha kwamba nilikuwa nimeshasahau dhumuni langu la kufanya haya yote. Bado, pamoja na kuwa nimejiweka upande wake, huyo mwanamke alikuwa ni adui yangu. Tumeangalia filamu nyingi zinazoonyesha kwamba mara nyingi ukitaka kufanikiwa kuwaangusha maadui zako, basi jiweke karibu nao ili uweze kufanikiwa kuwaangusha kwa njia bora.
Ndiyo nilichokuwa nikikifanya wakati huu. Ningeendelea kujichekesha tu heheh ili siku huyo mwanamke akija kunikuta serious, ajue kuna watu wasiopenda michezo kwenye maisha ya wengine kama ile aliyoifanya kwangu mpaka kuua mwanadamu mwenzetu. Na sikuwa nimempa taarifa askari mpelelezi Ramadhan kuhusu mkutano wangu huu na mwanamke huyo, ili nione kwanza huu mchezo ungenipeleka wapi kwa leo.
Nikaifikia Royal Village hatimaye, nami nikamlipa dereva na kwenda ndani ya geti. Nikatembea mpaka kufikia usawa wa bustani na kisha nikampigia tena madam. 'Haya ndiyo nimefika, niende juu au?' Akarusha dongo kwa kusema niache kuwa na kiherehere, na kwamba bado yeye hakuwa amefika hapo hotelini ingawa alikuwa anakaribia.
Nikamuuliza yuko sehemu ipi kwa sasa. Akasisitiza tu tena kwa kusema ndiyo alikuwa amekaribia kufika hotelini hapo, yaani ni dakika mbili tu angeingia, hivyo niende kumsubiri ule upande wa maegesho ya magari ya nyuma kwenye jengo hilo. Sikudhani kwenye hoteli hiyo kulikuwa na maegesho ya namna hiyo lakini hilo lilikuwa jambo hakika, hivyo nikamkubalia na kukata simu, kisha nikazungukia mpaka upande huo kwenda kumsubiri. Ah kumbe na hoteli hii ilikuwa ya ubora bwana!
Maegesho ya huku nyuma yalikuwa mapana, safi, nguzo ama ngome nyingi nene zikilibeba jengo hilo la hoteli na magari ya maana yakionekana kuegeshwa hapa na kule. Hizi ndiyo zile sehemu ambazo mara nyingi tunaonaga kwenye filamu hasa za wazungu jinsi ambavyo majambazi hupenda kuzitumia kwa ajili ya kutoroka wakishafanya maovu yao, na kweli hapa nilikuwa nimekuja kukutana na majambazi!
Nilitembea mpaka kufikia sehemu ambayo iliniruhusu kuuona mlango wa lifti ya nyuma kwenye jengo hilo, na bila shaka baada ya Bertha kufika tungeitumia hiyo kuelekea juu, hivyo nikasimama usawa wa nguzo moja na begi langu mgongoni kumsubiri madam afike.
Hakukuwa na nafsi hata moja iliyoonekana kwa upande huu, pakiwa kimya kweli, nami nikawa naangalia mpangilio maridadi wa sehemu hiyo pamoja na CCTV camera zilizowekwa kwenye kila pembe. Nikasikia kengele ya mlango wa lifti iliyoashiria kwamba kuna watu walikuwa wanatoka, na ile nimenyanyua tu uso wangu kutazama huko, nikajikuta nakunja sura kimaswali kutokana na kutotegemea kabisa kumwona niliyemwona.
Mwanamke niliyemfahamu, akiwa amevaa gauni jeupe lililo la mtindo mzito kama sweta laini, refu kufikia miguuni, lenye kubana mwili wake ulioumbika vyema. Alikuwa ameshika mkoba mkononi, na hilo gauni liliacha mikono yake myeupee wazi kutokea mabegani, na aisee alinifanya nibaki nikimtazama kwa mshangao sana. Bibie Miryam!
Yaani sikuwahi kutegemea kumwona hapo kabisa, tena akiwa ndani ya mtindo mzuri kama huo uliompendezesha vibaya mno. Alikuwa amevaa viatu vya kuchuchumia vyekundu, vikiwa vimeendana na rangi ya mkoba wake, na mwonekano huo uliniambia kwamba alikuwa sehemu hiyo kwa mkutano wa masuala binafsi; labda date na mtu wake, na huku ilikuwa ni mbali kweli!
Ila ilimfaa, nami nikaona nijibanze kwenye nguzo hiyo ili asiweze kuniona kabisa. Nisingefikiria hata mara moja kwamba ningemwona hapo hasa kwa kujua alikwenda zake kazini baada ya kumpeleka mama mkubwa wake hospitali. Alikuwa anakuja upande wangu lakini kwa kupitilizia sehemu iliyokuwa imeegeshewa magari, nami ndiyo nikawa nimeiona ile pickup yake.
Pamoja na kuwa mwanamke mwenye mvuto sana lakini hakupenda makuu mno, na kuwa mtu aliyethamini zaidi mambo yaliyokuwa na maana kwake kuliko kutafuta vitu vya kumpa sifa tu; yaani huyu hata kama angekuwa ameamua kutembelea gari aina ya Range Rover Evoque asingeshindwa, lakini aliendelea kutumia pickup iliyokuwa ya baba yake ili kumuenzi. Lakini dah! Miryam ndiyo alikuwa maana ya mwanamke. Sijui nani tu alikuwa anakula hapo!
Akawa amenipita bila kuniona maana nilijibanza vizuri, nami nikawa naangalia miondoko yake ya taratibu ambayo ingemfanya mwanaume yeyote agande kumtazama kwa jinsi alivyokuwa amebarikiwa huyo dada. Siyo kwa sura tu, siyo kwa shepu tu, hata tabia, yaani kila kitu kwake ni kama kilikuwa kamili.
Sikutaka anione maana mishe zilizokuwa zimenileta huku hazikuwa nzuri kuendana na jinsi dada wa watu alivyokuwa ananifahamu, lakini Shetani bana, akaona aniharibie tu. Sijui labda namsingizia bure? Simu yangu ikaanza kuita. Muito wa simu ulikuwa ni mdundo wa wimbo wa Ozuna uitwao "Una Lodura," wabrazili hao na ni ngoma kali, hivyo sauti ya mwanzoni tu ikawa imesikika kwa bibie. Agh!
Nimeshtuka ile nataka kuitolea sauti, sauti ya viatu vya Miryam ikakata, na hilo likaniambia kwamba alikuwa amesimama, kwa hiyo ikanibidi nitoke hapo kwenye hiyo nguzo na mimi nijifanye kwamba ndiyo nilikuwa nimetokea tu upande huo na sikuwa nimemwona. Nikaweka uso makini kweli nikiiangalia simu, na nilikuwa nimeanza kupiga hatua chache kisha nikasimama.
Mpigaji alikuwa ni rafiki yangu mmoja wa Mwanza, hivyo nikaitolea tu simu sauti huku nikimrushia laana ya kimoyomoyo huko alikokuwa kwa kusababisha nikachomeshwa namna hiyo. Nikajifanya naangalia tu pembeni kama vile sina habari na mwanamke huyo ambaye nilijua wazi kwamba alikuwa amesimama na anaangalia upande wangu, na ndipo hatua zake kunielekea zikaanza kusikika.
Nikafumba macho kwa kutotaka jambo hilo kabisa, kwa sababu nilihofia sana kuhusiana na mambo ambayo yangetokea ikiwa Bertha angefika na kunikuta nikiwa na Miryam hapo. Sijui ni kwa nini tu yaani mwanamke huyu alitakiwa kuwa hapo kwa muda huo! Ningepaswa nimwepuke upesi, kwa njia yoyote ile.
Nikamgeukia na kujifanya kushangaa, kama vile ndiyo nimemwona sasa, naye akawa ananifata huku funguo ya gari lake ikiwa kiganjani, na akitabasamu kiasi.
"Hey, vipi?" akaniuliza hivyo.
"Safi tu. Ih! Upo huku kumbe?" nikamsemesha namna hiyo.
"Ndiyo," akajibu hivyo na kusimama mbele yangu.
"Mishe gani?"
"Aa... nimekuja tu kukutana na mtu, alikuwa ameniita huku ndiyo nikaja haraka," akaniambia hivyo na kasauti kake katamu.
"Aaa... umedamshi kweli. Lazima uwe mkutano wa maana," nikazungumza kwa wasiwasi kiasi.
"Ahah... acha bwana. Ni mikutano tu ya kikazi," akasema.
"Aaa... sawa. Si ndiyo unaondoka?"
"Eeh."
"Haya sawa, basi,... baadaye. Kama kawaida tu, nitakuja kwa Mamu," nikamwambia hivyo kama namfukuza yaani.
Akauliza, "Na wewe? Mbona uko huku?"
"Kuna... na mimi kuna mtu nakutana naye... hapa. Ni rafiki. Kwa hiyo, we' nenda tu, si unaenda kuendelea na kazi? Nisikucheleweshe," nikamwambia.
Akawa ananiangalia kwa utafakari, naye akasema, "Mbona kama una wasiwasi? Kuna tatizo lolote?"
"Hapana. Kila kitu kiko sawa," nikamwambia hivyo na kutabasamu.
Akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye akasema, "Okay. Basi... tutaonana baadaye... kama ulivyosema."
Nikatikisa kichwa kukubali hilo.
Akageuka na kuanza kuondoka, nami nikaangalia pembeni na kushusha pumzi ya utulivu. Nikawaza kuwa angalau tu kama dada wa watu angeondoka, maana, hapo sikuwa sehemu nzuri kabisa ya....
Ilikuwa mapema sana kufikiri kwamba nilipata ushindi kwa kumwondoa Miryam upesi, kwa sababu alikuwa amepiga hatua chache tu kisha akasimama tena. Nikamwangalia. Akanigeukia tena na kunitazama, kisha akaanza tena kurudi kwangu. Aisee! Sijui alikuwa amesahau nini!
Akafika karibu tena, nami nikajitahidi kuonyesha utulivu usoni lakini moyoni palidundika mithili ya ngoma, naye akasema, "Nilikuwa nataka nikwambie jambo fulani."
Nikatikisa kichwa kuonyesha aendelee.
"Ni kuhusu jana... na... kila kitu ambacho kimeendelea kwa Tesha na Mamu. Huwa... sitegemei sana mtu yeyote anisaidie kwa... mambo ya familia yaani, sijazoea... ila... kwa yote ambayo wewe unafanya... nataka tu kusema asante..." akaongea hayo.
Dah! Hii ingepaswa kuwa pindi moja nzuri sana maana huyu dada alikuwa ameanza na kunisemesha kabisa, tena kunishukuru, lakini muda na sehemu ya tukio hili haikufaa. Nilikuwa naangalia upande ule wa mwingilio wa magari kwa wasiwasi kiasi, nikiomba Mungu Bertha aendelee kukawia tu.
Miryam akaendelea kusema, "Niliongea na Tesha hiyo jana... na jinsi alivyokuwa ameonyesha kutulia kiakili kwa kweli... sijaiona kwa muda mrefu kiasi. Anasema yote hiyo imewezekana eti kwa sababu ulimpa therapy ahahah..."
Nikalazimisha kicheko pia na kusema, "Eeh, ndiyo, ndiyo..."
"Yaani una effect nzuri hata kwa Mamu, mpaka ameanza na kuongea tena. Niseme tu... yaani, hatujawahi kuzungumza sana ndiyo maana nimeona nichukue hii nafasi ku..."
Maneno ya Miryam yakakatishwa baada ya sote kuona gari aina ya Harrier new model ya silver likiwa linaingia, nami nikajiambia eh Mungu! Huyu mwanamke alipaswa kutoka hapa sasa hivi!
Miryam yeye akiwa haelewi somo akaona aendelee kuzungumza tu kutoa shukrani yake, na hilo gari likaingia sehemu ya maegesho isiyo mbali sana na hapo tulipokuwa tumesimama. Dereva aliposhuka hakuwa mwingine ila yule baunsa wa madam, naye akaonekana kuufungua mlango wa nyuma wa gari.
Nikamgeukia Miryam na kumkatisha kwa kusema, "Miryam... tafadhali... tuta... tutaongea wakati mwingine... yaani, tukionana tena, sawa?"
Akaibana midomo yake taratibu huku macho yake yakiwa kwangu kwa utulivu tu.
"Unaweza kwenda tu Miryam. Naowasubiri wamefika, we'... kaingie kwenye gari dada..."
Yaani nilikuwa najaribu kumfukuza kistaarabu, na nilihitaji sana aondoke maana sikutaka Bertha amjue Miryam. Katika watu ambao sikutaka mwanamke huyo awaingie kabisa ilikuwa ni huyu dada, lakini kwa hapo nikawa nimechelewa.
"HB..." sauti ya Bertha ikasikika akiniita.
Ah!
Nikageuka kumwangalia, Miryam bado akiwa hapo hapo, nami nikamwona madam akiwa anakuja kwa mwendo wa madoido. Alikuwa amevaa gauni jeupe fupi sana lililoubana mwili wake. Mapaja yalikuwa wazi, mikono na mabega yalikuwa wazi pia, na sehemu ya mbavu zake ilikuwa wazi pia kama vile gauni hilo limechanwa humo pembeni kwa njia ya urembo.
Miguuni alivaa mabuti ya kike yenye rangi ya kahawia, na usoni alikuwa amevaa miwani pana nyeusi ya urembo. Baunsa wake alikuwa anafata nyuma huku ameitanua mikono na sura yake ikiwa makini, nao wakafika karibu yetu; Bertha akisimama karibu nasi zaidi na kuitoa miwani yake machoni.
Nikaendelea kuonyesha utulivu tu, huku nikiona jinsi Bertha alivyokuwa akimtazama Miryam kwa macho yenye udadisi, kisha akaniangalia mimi. "Za jioni?" akauliza hivyo.
"Fresh tu," nikajibu hivyo kwa sauti ya chini.
"Nimefika wakati mbaya? Mlikuwa mna..." Bertha akasema hivyo.
"Hamna, me ndiyo nimefika tu upande huu sa'hivi..."
"Sikumbuki kukwambia uje na mtu," Bertha akanikatisha kwa kusema hivyo.
Nikamwangalia Miryam kiufupi, ambaye alikuwa ananiangalia kwa utulivu tu, nami nikamwambia Bertha, "Hapana. Nimekuja mwenyewe. Sijaja na mtu."
"Huyu ni nani?" Bertha akaniuliza.
Miryam akaanza kusema, "Mimi ni..."
"Nimekutana tu na huyu dada hapa, alikuwa amedondosha funguo yake hiyo... ndo'... nikamsaidia kuipata..." nikamkatisha Miryam.
Jinsi ambavyo mwanamke huyo aliniangalia, yaani, alikuwa ndani ya mshangao mzito bila shaka, na ilieleweka kwamba hakuwa amenielewa.
Bertha akaniuliza, "Kwa hiyo ndiyo mmekutana hapa hapa?"
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Hamfahamiani kabisa?" Bertha akaniuliza tena.
Macho yake Miryam yakanitazama kwa njia ya subira, na najua alikuwa anataka kuona ningejibu nini, na aisee! Roho iliniuma sana kwa kitendo nilchokifanya.
Nikatikisa kichwa kukataa na kumwambia Bertha, "Hapana. Simjui."
Siwezi kujua undani wa mshtuko niliofanya Miryam auhisi hapo aisee! Aliniangalia kwa njia ya kawaida tu, lakini naelewa alikuwa akinishangaa sana. Sana!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments