Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Miryam akaacha kuniangalia na kumtazama Bertha, ambaye alikuwa amesimama kama vile amemzibia njia. 

"We' dada mzuri. Unamwonaje HB wetu, umempenda?" Bertha akamsemesha hivyo Miryam.

Miryam akabaki kimya, nami nikamtazama usoni kwa hisia za hatia. 

Bertha akacheka kikejeli na kusema, "Nisamehe shoga, nilikuwa nakutania tu. Ila... kama mlikuwa bado hamjapeana namba, nisiwe kikwazo. Chukua tu namba za HB boy. Hana baya."

"Madam, acha bwana. Ni..." 

Nikaishia hapo tu huku nikimwonyesha Bertha kwa ishara za mikono kwamba kumzingua mtu mzima namna hiyo haikuwa jambo zuri, lakini huyu mwanamke alijali sasa? Miryam alipotaka kupiga hatua kuondoka, Bertha akamwahi na kumzibia njia kwa kusimama mbele yake zaidi, nami nikapandwa na hisia zilizofanya nikunje ngumi kwa chini. 

Mwanamke huyo mbabe akawa anamwangalia Miryam huku akitabasamu kichokozi, na yule baunsa wake akaja karibu yangu na kupitisha mkono begani kwangu kirafiki. Eti ile kwamba kwa sababu madam alikuwa ameanza kumzingua mtu, basi lilikuwa ni jambo letu moja, nami nikaendelea tu kutulia huku nikiwatazama wanawake.

Bertha akazishika nywele zake Miryam kwa chini, naye akasema, "Mbona haraka hivyo? Unawahi wapi? Tuongee kidogo."

"Naomba unipishe," Miryam akamwambia hivyo.

"Hee! Nyie... mmeisikia hiyo sauti? Dada, em' ongea tena..." Bertha akasema hivyo.

Miryam akabaki kimya tu.

"Ongea baasi... hata kidogo. Nitakupa pesa. Nisemeshe tu walau kidogo," Bertha akaendelea kumshurutisha.

"Labda tukusaidie kumfanya aongee?" baunsa Dotto akasema hivyo.

"Wewe... mmfanye nini tena? Mtoto mzuri kama huyu siyo wa kulazimisha. Huoni alivyo wa moto? Darling... nitakupa pesa yoyote unayotaka yaani. Wewe unaweza kuwa sehemu muhimu sana ya biashara yangu kuubwa kuliko... yaani unafaa kabisa. Uko perfect sana."

Miryam akabaki kumwangalia Bertha kwa njia iliyoonyesha hakuelewa, nami nikawa nimeelewa ni biashara ya aina gani mwanamke huyo alikuwa akimaanisha. Aisee! Yaani kule kule ambako sikutaka tufike ndiyo Bertha akawa anatupeleka kabisa!

"Nimekuelewa sana yaani... nataka tuwe karibu. Ushawahi kusagana?" Bertha akamuuliza hivyo.

Nikafumba macho na kuinamisha uso, huku baunsa Dotto akicheka kidogo.

"Una matatizo ya akili?" Miryam akamuuliza hivyo.

"Ahahah... inawezekana yamenipata nilipokutana tu na wewe. We' unaonaje mpenzi?" Bertha akasema hivyo na kumshika kiunoni.

Miryam akaupiga mkono wake kwa nguvu ili asiendelee kushikwa, na akiwa anamnyooshea Bertha kidole akasema, "Jichunge we' mwanamke! Siyo kila mtu anaishi maisha ya kibatili kama wewe. Katafute malaya wengine wa kusagana nao, sikujui, hunijui, kwa hiyo nikome!"

Aliongea kwa uthabiti kabisa, na akiwa bado amemnyooshea Bertha kidole, Dotto akataka kwenda hapo sijui kumpiga, lakini nikamshika mkono kumzuia, na hata Bertha akawa amenyanyua kiganja chake kumzuia jamaa asiende hapo.

"Madam... achana naye tu. Kwanza... pisi kali nyingi, tutatafuta hata baadaye. Muda unaenda, si unajua?" nikamwambia hivyo.

Bertha akaniangalia, kisha akamtazama Miryam kwa macho makini.

"Nimekwambia nipishe. Usifanye nikakuitia polisi sasa hivi," Miryam akamwambia hivyo Bertha.

"Ahah... wacha! Kwa hiyo hutaki kabisa tuchezee mito, darling?" Bertha akasema hivyo kwa sifa.

Miryam akasonya na kutaka kumpita tena, lakini Bertha akamzuia kwa kutumia nguvu zaidi. 

Hali ikaonekana kutaka kuingia sehemu mbaya zaidi ya nilivyokuwa nimetarajia, nami nikashindwa kujua pa kusimama kabisa. Miryam ndiyo angekuwa chaguo la kwanza katika kutetewa na mimi lakini hilo lingenifanya nipoteze mchezo wote niliokuwa nimeanzisha kwa Bertha. 

Miryam akamshusha na kumpandisha mwanamke huyo kwa hisia kali, naye Bertha akamsogelea dada wa watu karibu zaidi kama anataka kuanzisha ndondi. Ilikuwa ni ile chick Vs chick kama kwenye WWE, na inaonekana Dotto alitaka kuwa mwamuzi kabisa kwa jinsi alivyotaka kuona wanawake hao wakianza kutoboana! 

Ila Mungu si Athumani bwana? Watu kadhaa kutoka kwenye lifti wakaanza kuja huku, na hata magari mengine yakaingia pande hizi. Hiyo ikawa ni ponea chupu chupu niliyohitaji sana itokee, naye madam akasogea nyuma kiasi na kuachia tabasamu ili bila shaka watu waliopita waone mambo yalikuwa shwari hapo.

"Una bahati. Huwa sipendi kusemeshwa kama ulivyonisemesha. HB angekupa mawaidha ya nini naweza kukufanya... ila muda hautoshi sweety. Kwa hiyo... nenda," Bertha akamwambia hivyo Miryam huku akitabasamu kinafiki.

Niliona wazi kwamba Miryam alikuwa amekasirishwa na haya yote, naye akanigeukia na kunitazama kwa mkazo. 

Kama ilivyokuwa siku fulani ya nyuma, nilipatwa na ile hisia ya hofu, sijui woga, yaani ni kitu ambacho kilitokea tu pindi ambayo Miryam angeniangalia namna hiyo. Sijui ilikuwa kwa nini tu, lakini ni kitu kilichofanya hadi ujasiri wa kumtazama machoni unitoke, nami nikaangalia pembeni kama vile simjali.

"Ondoka," Bertha akamwambia hivyo Miryam.

Miryam akamtazama na kumshusha kwanza, kisha huyoo akaenda zake mpaka kwenye gari.

Bertha alikuwa anamwangalia tu Miryam mpaka alipoingia garini, na kiukweli nilikuwa najihisi vibaya kusimama tu hapo na kuangalia hayo yote yalipokuwa yakiendelea. Yaani sijui hata ningemtazama vipi tena huyo dada wakati ambao ningerudi kule nyumbani.

Nilijisikia vibaya sana kumkana namna ile, lakini sikuwa na jinsi. Hakuelewa, ila nilikuwa namlinda. Sikutaka Bertha aanze mambo yake ya kufatilia huyo alikuwa nani maana sikuwa na uhakika ikiwa alikuwa ameshaniamini kwa asilimia zote, na kunikuta hapo na mtu bila shaka kungempa shuku. Bora kama ingekuwa ni mtu mwingine tu lakini Miryam, hapana. Sikutaka aguswe pabaya kabisa. Nilimheshimu mno.

Gari la Miryam likatoka sehemu ya maegesho huku sisi wote tukiliangalia, naye Dotto akasema, "Pisi la maana, lakini akili hamna."

"Kinajikuta kisafi, eti 'malaya wenzako...' unafikiri kimekuja huku kufanyaje kama siyo ku(.....)? Bado kitaendelea kudrive mistubishi mpaka kitakufa. Na ni kweli, hana akili kabisa. Demu wa wapi mkali namna hiyo akandesha usenge kama huo? Mpuuzi mkubwa tu!" Bertha akasema hivyo kwa dharau.

Aisee, nilisikia hasira! Basi tu. 

Nikashusha pumzi na kusema, "Harakati zinaendaje sasa? Maana saa moja inaingia."

Bertha akaanza kuelekea upande wa lifti huku na sisi tukimfuata, naye akasema, "Utajua huko juu. Na iwe mara ya mwisho kukuona umesimama na mpumbavu yeyote tukiwa tunakutana, sijui unanielewa?"

Nikasema, "Yes madam."

Tukaifikia lifti na kuingia, kisha tukaanza kuelekea juu. Bado nilikuwa nikimwaza Miryam tu, yaani ni jinsi gani ambavyo tukio la muda mfupi nyuma lingefanya nipoteze kabisa kiasi chochote cha imani alichokuwa nacho kunielekea kwa wakati huu. Sijui alikuwa ananifikiriaje! Lakini hakukuwa na njia ya kuepuka yaliyotokea maana nilikuwa na malengo kwenye haya yote niliyofanya, kwa hiyo ningepaswa kuendelea kujitahidi kuyafikia. 

Tukiwa bado ndani ya lifti, Bertha akapigiwa simu na mtu fulani, naye akaanza kuongea naye kwa shauku. Alikuwa anamwambia kwamba asiogope, hangekawia kufika huko na alikuwa na zawadi nzuri sana ambayo ingewafanya wote wa huko wachanganyikiwe ile mbaya, nami nikaelewa hilo lilimaanisha sehemu ambayo mwanamke huyu ndiyo alikuwa anataka twende muda huu. 

Kwa sababu sikujua mengi ya kutegemea japo nilijiandaa kwa lolote lile, nisingeweza kufanya kitu cha ujanja-ujanja mpaka niwe na uhakika wa kile ambacho kingetokea. Yaani namaanisha kama siku ile huyu mwanamke ameniita nije hapa kwa mara ya kwanza, nilifanya kurekodi sauti za mambo tuliyozungumzia na kumpelekea yule mpelelezi, lakini kwa sasa hivi nisingefanya kitu kama hicho mpaka nihakikishe mazingira ambayo ningekuwepo yangeruhusu. 

Mpaka tumetoka ndani ya lifti na kwenda kwenye kile kile chumba kwenye ghorofa ya saba, madam bado aliendelea kuongea na huyo mtu wake kwenye simu, naye akaenda kukaa kwenye sofa lililokuwa na muundo kama kitanda, kwa hiyo akawa amekaa kama amelalia ubavu wake mmoja na kuendelea kuongea kwa madaha. 

Mimi nikaweka begi langu kitandani, huku Dotto akiwa amesimama pembeni yangu kama vile anasubiria nimpe kitu fulani, na nilijua tu kile ambacho alikuwa anataka. Nikachomoa dawa ya kwenye kifuko kidogo na kumpatia, naye akakipokea na kunigongea tano kuonyesha furaha. Nikamwangalia Bertha, ambaye bado alikuwa kwenye raha ya maongezi yake, nami nikakaa kitandani hapo. 

Dotto alikuwa kwenye kiti kimoja kati ya viwili karibu na meza fupi, vyote vikiwa vya plastiki, naye akawa ameifungua dawa na kuweka kiasi mezani, kisha akaitenganisha kwa mistari mifupi na kujisawazisha vizuri. Akaniangalia na kunitolea ishara ya kwenda hapo ili nijiunge naye, lakini nikamwonyesha kwamba niko vizuri tu, hivyo yeye aendelee. 

Akaiinamia meza na kuziba tundu moja la pua yake, kisha akavuta mstari mmoja wa madawa hayo mpaka ukaisha. Kwa jinsi ilivyokuwa kali, hiyo ingempaisha mbali sana kiasi kwamba sidhani kama angeweza kuendesha gari vizuri tena. Akawa anakunakuna pua huku akitikisa kichwa kuonyesha msisimko, nami nikampa tabasamu hafifu tu aliponitazama machoni. 

Nikamwangalia na madam, ambaye sasa alikuwa amemaliza kuongea na simu na kuonekana akichat sijui? Bado sikuwa nikiambiwa yatakayofuata lakini nikaona nibaki tu kimya na kutoa simu yangu pia. 

Wakati huu, nilikuta yule mwanamke mwislamu aliyeitwa Ibtisam akiwa amenitumia ujumbe, akisema kuwa anataka tukutane tena na angeandaa mazingira yeye mwenyewe, lakini sikumjibu jumbe hata moja. Alikuwa amenichunia toka nilipomwambia nimemwelewa, na sasa ghafla tu akawa anataka tukutane. Je kama ilikuwa ni mume wake au ndugu zake wa Mafia? Isingekuwa busara kufia ujinga, kwa hiyo nikaamua kumweka pembeni. 

Nikaanza tu kucheza "game" maana niliona wazi kwamba hapo ingekuwa ni kusubiri tu; Bertha alikuwa bize na mambo yake, na Dotto alikuwa kwenye raha ya vibe la madawa niliyotengeneza. Kidogo tu ndiyo jamaa akaanza kuongea, akisifia hayo madawa na kunipigisha story za mambo mengine ambayo hayakuwa na umuhimu wowote ule kwangu. 

Niliangalia kwa umakini namna ambavyo mwanaume huyo alizungumza kwa njia huru sana mbele ya Bertha, kitu kilichoonyesha kwamba walikuwa na mazoea ya muda mrefu. Kwa jinsi alivyokuwa na ukaribu naye, bila shaka alijua siri nyingi za mambo ya huyo mwanamke, na kama alishiriki katika mauaji ya Joy basi na yeye angekuwa amejiweka ndani ya shabaha yangu ya maangamizi. Siyo mbaya kujipa kichwa kidogo! 

Nikawa nasindikiza tu mongezi yake na kumwambia mambo yaliyomchekesha, naye akaendelea tu kushusha madawa puani kila robo saa.

★★

Bertha kama boss alikuwa kivyake tu mpaka inaingia saa tatu usiku, nami nikajiuliza ikiwa kweli ningewahi kutoka huku. Na hapo bado kuna sehemu tulitakiwa twende, kuna kitu tulikuwa tunasubiria, kwa hiyo bila shaka hiyo sehemu ingekuwa ya mambo yaliyohitaji giza nene. 

Ah nikaona hii kuwa usumbufu tu maana huyo mwanamke aliniwahisha kweli kuja huku mpaka nikajikuta nakutana na Miryam, wakati tu angeweza kuniambia nianze kuja hata jioni ili nifike huku usiku. Hakukuwa na namna ya kubadili mambo tena, ila kiukweli bado ishu ya kukutana na Miryam hapo hotelini mpaka Bertha kumwanzishia fujo ilinisumbua sana akilini.

Nikawa nimeanza tena kumwaza mwanamke huyo pale mlango wa kuingilia ndani hapo ulipogongwa kwa nje. Nikamwangalia madam usoni, naye akaninyooshea kiganja kuuelekea mlango kuashiria nikaufungue, hivyo nikanyanyuka na kuchukua kadi ya kufungulia kisha kwenda mlangoni. 

Bila shaka aliyekuwa anasubiriwa ndiyo alikuwa amefika, na baada ya kufungua mlango, nikakutana uso kwa uso na mwanaume kijana aliyekuwa amevalia suti iliyombana haswa, na alikuwa na kipara huku akivalia miwani pana yenye kuonyesha macho yake. Alikuwa amesimama mbele ya wanaume wengine wawili wenye miili mikubwa na warefu, waliokuwa wamevaa suti pia, na wakiwa wamebeba maboksi mapana ya kutunzia nguo pamoja na fuko la kutunzia suti; likiwa na suti. 

Huyu mwanaume aliyevalia miwani akawa ananiangalia kwa njia fulani kama ananishangaa, lakini jinsi ambayo alifanya hivyo yaani sikuielewa-elewa. Alikuwa kama anarembua kwa mbali, shingo yake ikinesa-nesa kwa maringo utadhani alikuwa.... subiri kwanza, nini? 

"We' nyau ndo' unafika sasa hivi?"

Swali hilo liliulizwa na Bertha humo ndani, nami nikaelewa kwamba lilimhusu mmoja wa hawa watu waliofika hapa. Ila ni huyu wa mbele tu ndiye aliyekuwa akifanana na nyau kwa hiyo bila shaka swali lilikuwa lake kujibu!

Huyo jamaa akacheka kidogo kwa pumzi na kusema, "Jamani dear, nisamehe. Kazi zilikuwa piled up, na msongamano wa magari hukutuacha salama."

Eh! Alisema hivyo huku akinipita na kuingia ndani, nami kiukweli sikuwa nimetegemea kabisa namna yake ya kuongea. Yaani aliongea kike, 'jomooni deear,' hivyo! Wale jamaa wengine wakaingia pia, nami nikaufunga mlango na kuwatazama wote kwa umakini. 

"Utakuja kuni-cost wewe, unajua nimesubiria kwa muda gani hapa?" Bertha akamwambia hivyo huyo jomooni deear. 

"Mmmm, shoga, acha ukali bwana. Ilikuwa nje ya uwezo wetu," jamaa akamwambia hivyo.

Aisee! 

"Kwenda huko! Nje ya uwezo wapi, ukinikosesha alama leo? Hee. Mizigo ndiyo hiyo?" Bertha akamuuliza.

"Hundred percent! Yaani kama uliyoagiza darling, parcel za ukweli, suti na hizo dress, yaani unakoenda na mume wako itakuwa kama nyie ndiyo mnaimiliki Bongo nzima! Hahahaaah..."

Nikajikuta tu natabasamu na kutikisa kichwa kwa kutoamini huu upuuzi. Kumbe tulikuwa tumekaa hapa muda huo wote kumsubiri huyu bwege alete nguo za kuvaa ili ndiyo twende tulikopaswa kwenda, naye akawa amezileta kwa mbembwe zile za yule jamaa anayependaga kusema dhambi za fashoon. Na walikuwa ni wale wale kabisa!

Bertha akasema, "Huna lolote Eliya."

Eliya, ikiwa ndiyo jina la huyo jamaa, akasema, "Si utaona? Kwani me huwaga nafeli? Insta kote nafahamika, hata wa duka la Mobetto hawawezi kufikia hizi design. We' mwenyewe unanijua, ndiyo maana bado umezama kwa fashion designer Eliyah! Hahaaa mtoto vaa, ng'ara, pendeza, hakuna atakayefikia show yako huu usiku, yaani hakuna yeyote yule atakayefikia mng'ao wako kwa hii kitu. Au nadanganya Mandonga zangu? Sasa! Kitu ng'ari ng'ari, yaani ukivaa kila mtoto wa mjini unamgeuza mshamba... yaani ndoigee!"

Dotto na wale mabaunsa wakacheka kidogo, hata Bertha pia akacheka huku akitikisa kichwa taratibu, kwa sababu jamaa aliongea huku amenyanyua tatu hewani kana kwamba alikuwa anachamba mtu kama mwanamke! 

Inaonekana Bertha alipenda sana misifa ya namna hiyo, tabasamu lake la kiburi lilithibitisha hilo, naye akawa amesimama na kufungua maboksi kuziangalia nguo hizo. Akazitoa kabisa, moja baada nyingine, akizipima-pima mwilini kwake, na huyo Eliya akaendelea kusifia tu kama kawaida yake. 

Hivi huwa ni lazima watengenezaji mitindo ya wanawake ambao ni wanaume sikuzote wawe namna hiyo, ama? Tena jamaa hadi akawa ananiangalia kwa yale macho yaani dah! Kungekuwa na mawe humo!

Bertha sasa akawa ameshika nguo hizo mbili mikononi mwake, akiwa anajishauri atumie ipi maana zote zilikuwa nzuri, naye akaniangalia na kusema, "Njoo mpenzi."

Wengine wakanitazama usoni, na mpaka kufikia hapo bado nilikuwa nimesimama karibu na mlango. Bertha alikuwa na michezo yenye kushtukiza maana alifanya iwe ngumu kwangu kujua namna ya kuitikia masuala fulani ambayo yangekuwa tofauti na misingi ya uhusiano tuliokuwa nao, lakini mimi ningekwenda tu na mabiti namna hiyo hiyo.

Nikatembea taratibu mpaka kufikia aliposimama, naye akaniuliza, "Eti honey... nivae lipi?"

Wakati huu huyu mwanamke alikuwa anatumia sauti fulani kama vile anadeka kwangu eti, bila shaka akiwa ananioshea kwa hawa wengine walioingia, nami nikajitoa tu akili na kumwonyesha gauni aliloshika mkono wa kulia. 

Lilikuwa ni gauni lenye kubana bila shaka, lililokuwa na rangi ya maroon, na lilipambwa kwa vitu kama vialmasi vingi kulizunguka vilivyofanya limeremete sana kwa mng'ao wa mwanga wa taa. Lile lingine lilikuwa la blue-bahari, likiwa la mtindo ambao sikuuelewa na sikujali; mimi nilimwonyesha tu la maroon avae, tuondoke.

Akaliangalia gauni nililomchagulia na kuniuliza, "Kwa nini unataka damu ya mzee? Kwa nini nisivae hili?"

Khh! Kero!

Nikamwambia, "Ngozi yako ni nyeupe, mpenzi wangu. Ukivaa hii inayomeremeta halafu usiku... ndiyo utaonekana kuwa zaidi ya malaika kabisa."

Bertha akabaki kunitazama kwa umakini baada ya mimi kumwambia hivyo. Nafikiri sifa ikawa imemwingia.

Eliya akasema, "Kweli shem, si umeona? Atang'ara vibaya mno! Madam... vaa maroon upendeze, hata mwanaume wako amesema... utakuwa zaidi ya malaika. Yaani watu watakaposema 'haki ya Mungu,' watamaanisha wewe! Wape vitu vyao heshima yako iendelee."

Jamaa alikuwa anasifia kwa bidii kweli bidhaa zake, kitu kilichoonyesha kwamba pesa ambayo madam angeitoa ilikuwa ndefu. Bertha akaonekana kuridhia gauni hilo, naye akamwambia Eliya kwamba angeyachukua yote na pesa angemwekea kwenye namba yake ya akaunti ya benki ikifika kesho, na kwa hilo Eliya hakuwa na neno. 

Mimi nikakaa kitandani tena, nisitake shobo na mtu yeyote hasa baada ya huyo Eliya kuanza kunisifia-sifia kwa Bertha akisema kwamba alikuwa amepata mtu aliyeendana na hadhi yake kutokana na mimi kuwa na sura nzuri, naye akasema tungezaa watoto waliofunika uzuri wa watoto wa mastaa kama wa Hemedy PhD. 

Aliongea huyo kaka, na hivi alikuwa shoga! Mpaka Bertha akakatisha kelele zake na kumwambia aondoke sasa ili sisi tuvae na kwenda kuenjoy. Eliya na mabaunsa wake hawakuwa na neno, nao wakaondoka hapo ikiwa ni mida ya saa nne wakati huu. Dotto akawa amesimama huku akionekana wazi kuwa amelewa, naye akampa ishara Bertha kama kumuuliza 'niende?' naye Bertha akazungusha macho yake kidogo na kumruhusu aende. 

Nikawa nimeelewa kwamba jamaa alitaka kumwahi Eliya ili bila shaka aende kuchukua namba kama siyo kupiga sound, ikionekana alipenda mashoga. Maisha haya! Ndiyo maana nilisema mwanzoni kwamba maisha hutofautiana, na kila mtu ana namna ya kuyaendesha kwa uchaguzi wake, kwa hiyo nisingehukumu lolote na kuendelea kuangalia tu pale ugali wangu ulipo. Basi.

Baada ya Dotto kuondoka, Bertha akasema, "Chukua hiyo suti uvae. Tumeshachelewa."

Nikauchukua mfuko wenye suti hiyo, ikiwa ni ya zambarau, safi, mpya, yenye tai maridadi, na boksi la pembeni lilikuwa na viatu vyeusi vipya pia. Yaani haya mambo yote, bure bure tu? Bertha alikuwa anataka kunipeleka wapi?

Nikamuuliza, "Suti na hili joto lote kweli? Tunaingia pande gani?"

"Kigamboni. Na ni lazima uonekane smart, siyo sehemu ya watoto," akajibu hivyo.

"Ahaa, sawa. Kigamboni... ndo' kwenye ile ishu uliyoniambia?"

"Yeah. Twende tukacheze karata," akasema hivyo.

Mh?

Mwanamke huyo akaanza kuvua kigauni kifupi alichokuwa amevaa, nami nikabaki nikimwangalia. Alikuwa amebaki na sidiria nyeupe ambayo ilikuwa na urembo uliofanya rangi ya 'chukuchuku' zake ionekane kwenye matiti yake yenye ujazo mkubwa, na hata nguo yake ya ndani ilikuwa ya mtindo huo huo lakini kito chake kilifichwa vyema kwa mbele. 

Nikaona nitie umakusudi wa kuendelea kumtazama, ili aone kwamba nilikuwa nimezubaishwa na mwili wake. Alikuwa na tumbo dogo la mazoezi, hips nene kiasi ingawa alikuwa na mwili mwembamba, naye akaanza kulivaa gauni aliloletewa na Eliya huku akiniangalia kwa umakini pia.

"Unavaa ama?" akaniuliza hivyo.

Nikajifanya kushtuka kiasi na kuliondoa T-shirt langu mwilini, kisha nikalirushia kitandani na kuanza kuitoa suti. 

"Hauendi kujimwagia?" nikamuuliza hivyo bila kumtazama.

"Nimekwambia tumechelewa... kwani hujaoga?" akasema hivyo.

Nikatabasamu kidogo tu. 

Nikamwangalia na kukuta ameshalivaa gauni lake, lililokuwa refu na lenye mpasuo mpaka kufikia pajani usawa wa kalio kabisa, huku likiwa na mikanda myembamba iliyopitishwa mabegani. Kwenye kifua chake kulikuwa na uwazi mpana ulioonyesha mstari uliotenganisha matiti yake, na kiukweli lilimpendezea.

Akawa ananitazama kifuani kwangu, naye akasema, "Una kamwili kazuri. Gym inakuhusu eh?"

"Ah... hamna hata. Nimenyanyua chuma zamani sana, sa'hivi nimeacha, labda push-up za mara moja moja tu," nikamwambia hivyo kwa kujishaua.

Akawa ananitazama kwa yale macho ya kuhukumu.

Nikafanya kuanza kuivua suruali yangu taratibu huku nikisema, "Angalau lakini nilijaribu-jaribu kuukata mwili... kidogo. Ila... hauna ile sifa ya kuniruhusu niwe bodyguard wa mtu, au siyo?"

Nikawa namwangalia sasa baada ya kuvua suruali yangu, nikiwa nimebaki na boksa pekee, nami nikamchezeshea matiti ya kifua changu kwa uchokozi kidogo.

Akatabasamu kiasi na kutikisa kichwa kuonyesha utani umemwingia, naye akasema, "Hauna baya. Umeumbwa kwa ajili ya mwanamke kweli."

"Siyo yeyote tu lakini... wale wa maana," nikamwambia.

"Kama nani vile?"

"Hamisa Mobeto."

Akacheka kidogo na kusema, "Unamkubali sana eh?"

"Mno. Ni kipenzi changu toka niko la saba. Mademu wote niliotoka nao walikuwa wakali ila bado sijapata anayefikia pale..."

"Ni mpaka uje umpate yeye mwenyewe, na ukishampata utamwona wa kawaida sana," akasema hivyo.

Kisha akaanza kunifata mpaka niliposimama huku akiniangalia usoni kwa umakini, nami nikatulia tu. Akageuka na kunipa mgongo, na ni kweli alinipa maana mgongoni palikuwa wazi, akiwa anataka nimsaidie kupandisha zipu ya nguo hiyo.

Nikatii na kuanza kumpandishia, taratibu, nikifanya makusudi kwa kusugua kucha ya kidole changu mgongoni kwake kadiri nilivyokuwa napandisha. Nikaona ameinamisha uso wake kiasi na shavu lake kunyanyuka kidogo, kitu ambacho kilionyesha kwamba alikuwa anatabasamu, nami nikamaliza kumfungia na kuachia zipu hiyo. 

Akanigeukia tena na kuniangalia machoni, mimi nikiwa nimesimama kwa utulivu tu, kisha akashusha macho yake mpaka usawa wa boksa yangu na kusema, "Fanya haraka kibamia. Hatuna muda wa kupoteza."

Dah! Yaani huyu mwanamke! 

Nikatabasamu kidogo tu na kutikisa kichwa, naye akaniacha hapo na kwenda pamoja na mkoba wake sehemu yenye kioo ili ajitengeneze usoni na kichwani. Akavaa na mikufu, mabangili, na pete zingine zilizoonekana kuwa za gharama, ama inawezekana zilikuwa ghoroka.

Mwanaume mimi nikatia suti na tai mwilini, na ilinikaa vyema sana japo sikuwa nimepimwa. Ilikuwa ya ki-modo yaani, koti na suruali za zambarau pamoja na kizibao, shati jeupe, kiatu cheusi, na kwa kujumuisha na saa yangu kali mkononi ilinifanya nitokelezee ile mbaya. Lakini joto sasa! 

Nikawa nimemwomba Bertha chanuo ili nisawazishe nywele zangu vizuri, naye akanipa huku akinitazama kwa umakini. Nikajitengeneza vyema kisha nami nikamwangalia, nikiona wazi namna alivyokuwa anatathmini mwonekano wangu.

"Hapa vipi? Nakimbilia kuifikia hadhi yako, au siyo?" nikamuuliza hivyo.

Akatoa tabasamu la kiburi kiasi, naye akachukua manukato yake yaliyoonekana kuwa ya gharama na kunipulizia hapa na pale kwenye nguo nilizovaa, kisha ndiyo akaniangalia machoni na kusema, "Unakaribia."

Nikatabasamu kidogo, naye akaacha kuniangalia na kuifuata simu yake.

Jinsi ambavyo mwanamke huyu alikuwa ameanza kujiachia kiuhusiano kunielekea tofauti na mwanzoni ilionyesha alitaka kunizoea, na mimi nilikuwa na nia ya kuendelea kulisukuma hilo kwa kuwa ningemfanya azidi kuweka imani kwangu zaidi, na hivyo iwe rahisi kuzielewa kazi zake na kuziporomosha. Akawa anaongea na mtu kwenye simu, akisema aweke gari tayari kwa kuwa tungeshuka sasa hivi mpaka huko chini. 

Alipokata simu, nikamuuliza ikiwa huyo aliyekuwa anazungumza naye ni Dotto, maana jamaa alionekana kuwa anga ya 18 kuweza kuendesha gari vizuri tena. Akasema hapana, huyo alikuwa dereva mwingine ambaye usafiri wake ulikuwa ni wa kulipia, na ndiyo angetutoa hapo hotelini mpaka Kigamboni. 

Nikamuuliza kwa nini ilimpasa alipie usafiri ikiwa alikuwa na gari lake kabisa, naye hakunijibu lolote isipokuwa kunishusha na kunipandisha tu. Akanipita na kulifuata begi langu, naye akalifungua na kukunguta kwa nguvu mpaka kila kitu kikadondokea kitandani. Hadi vile ambavyo nilipaswa kumrudishia Latifah hospitali. Alikuwa na fujo! 

Akayaona yale madawa, yakiwa kwenye mifuko minne kama tu glucose zikaavyo, naye akayaweka kwenye mkoba wake uliokuwa mpana vya kutosha kuyaweka. Akaniambia nibebe kadi/funguo ya mlango, nami nikatii na sote tukaelekea nje ya chumba. Ningekuja kulirudia begi langu baada ya kutoka huko alikokuwa ananipeleka. 

Tulikuwa tumependeza sana, yaani tulipendezeana mbele ya macho ya wengi ambao wangetuona, hukumu ya kwanza kwa yeyote ikiwa ni sisi kuwa wapenzi. Bertha alitembea kwa mwendo uliofanya ionekane ni kama vile kiuno chake kinazunguka, na kalio lake lililotokeza nyuma ya hicho kigauni lilionekana kuwa jeupee. Yaani kwa jinsi ambavyo mpasuo ulikuwa umefikia hadi karibu na kiuno chake, kama tu ungeuvuta upande wa nyuma wa hiyo nguo basi ungeona tako lake lote!

Tukachukua lifti ile ile ya upande wa nyuma, nasi tukaelekea maegesho. Kufika hapo kulinifanya nimwaze tena bibie Miryam, jinsi niliyokuwa nimemkana. Ke! Nahisi angekuwa amenikasirikia si sababu tu nilikana kumjua, ila hasa kwa jinsi ambavyo Bertha alimtendea. Lakini hilo lingekuwa la kusuluhisha baadaye. 

Hapa tulikuwa tukielekea pale ambapo nakumbuka Dotto aliegesha Harrier ya madam, lakini wakati huu haikuwa hapo na badala yake lilisimama gari jeusi aina ya Range Rover, safi kinoma. Pembeni alisimama mwanaume aliyevaa suti kabisa, ikiwa ndiyo dereva bila shaka, na aisee huu ungekuwa ni usafiri wa gharama. 

Huyu mwanamke hakuonekana kuwa mraibu tu wa madawa ya kulevya, bali inawezekana alihusika katika masuala ya kununua na/ama kusambaza, "Drug Lord" wa kike, na ni huko huko nilikokuwa nataka anipeleke ili nikapaumbue maana alionekana kufanya vitu hivi kwa mpangilio makini sana. 

Tukalifikia gari hllo, jamaa akafungua mlango wa siti za nyuma, naye madam akatangulia kisha nikafuata. Gari maridadi siyo mchezo! Na nilijua pointi ya kulitumia hili ilikuwa ni kuoshea huko tulipokuwa tunaenda kucheza karata, nami nikamuuliza ikiwa tungekutana na Dotto huko lakini akakanusha. 

Akasema tu Dotto alielekea sehemu nyingine kwa masuala yake binafsi, nami nikaelewa tu kwamba jamaa alikuwa ameenda kula misele na mupenzi wake! Haya bwana, nikatulia tu. Dereva akaingia kwenye usukani, ndinga ika-vruum, safari ikaanza.

★★

Tulizunguka barabara za hapa na kule jijini, tukipita maghorofa, nyumba, maduka, magari, na sikuwa nikikazia fikira sana kuhusu njia tuliyotumia kuelekea Kigamboni, kwa sababu mwendo ndani ya gari hilo ulitengeneza hali fulani tulivu iliyonipa nafasi ya kutumia simu kwa muda mrefu. Ndani ya saa kama moja na nusu hivi tayari tukawa tumeingia Kigamboni kwenye majengo mengi maridadi sana hapa jijini, na ndiyo huyo dereva akawa anaitafuta sehemu tuliyopaswa kuelekea. 

Nilikuwa nikiwasiliana na marafiki WhatsApp, pia na mama yangu aliyekuwa akinijulia hali, na yule mwanamke mwislamu aliyeitwa Ibtisam. Bado alikuwa ananitafuta, na wakati huu nikawa nimemwambia kwamba mambo yalikuwa yameingiliana kwa hiyo kukutana isingekuwa rahisi mpaka wakati mwingine. Yaani alikuwa anataka tukutane saa hii hii. 

Angalau muda huu nilithibitisha kwamba ni yeye maana tulihamishia maongezi WhatsApp, ndiyo akapiga video call ili nimwone. Sikuona noma kupokea nikiwa pamoja na Bertha maana alikuwa bize na simu yake pia, nami ndiyo kwa mara ya kwanza nikawa nimeiona sura ya Ibtisam bila kificha uso. Alikuwa mwarabu, mweupee, macho mazuri kweli, naye alikuwa na ongea ya taratibu sana kama hataki yaani. 

Nikawa namwambia vitu vya kujenga mazoea zaidi, akiwa anasema anapenda sana macho yangu na anatamani anione tena ana kwa ana, nami nikamsisitizia kwamba tungekutana muda mwingine uliofaa. Aliona kwamba nilikuwa nimependeza kwa kuvaa suti, na alitambua nilikuwa kwenye gari, hivyo akauliza ninaelekea wapi kwa wakati huu. Nikamwambia ni matembezi tu, lakini ndiyo ule utani wa 'ama uko unaenda kula bata na wanawake wengine' ukawa umeanza. 

Nikamwambia mimi sina hizo, ila nilikuwa naelekea sehemu muhimu sana ndiyo maana nilivaa mpaka na suti, naye eti akawa anataka kujua ni wapi kabisa. Nilikuwa nataka hata nimkatie simu kwa sababu alianza kuonyesha kuniganda mno, lakini ndiyo hapo akauliza ikiwa labda niliogopa kumwambia kwa sababu nilikuwa na mke wangu. Bila matarajio, nikashtukia simu yangu inakwapuliwa upesi na Bertha, nami nikamtazama. 

Sasa alikuwa akiangaliana na Ibtisam hapo kwenye video call, naye akasema, "Ndiyo, yupo na mke wake, malaya wewe! Lione kwanza, hadi Kanumba alikwambia una minywele kama fidudidu lakini hukomi tu kutoka na waume za watu! Zima simu ukalale, shenzi wewe!"

Kisha mwanamke huyu akasonya na kuirusha simu yangu kwenye uwazi wa katikati kwenye siti tulizokalia. Nikabaki namwangalia tu usoni, yeye akiwa amerudia ubize wake kwenye simu yake, nami nikaichukua ya kwangu na kukuta kweli Ibtisam amekata mawasiliano. Nikamtazama tena Bertha usoni.

Akaniangalia kwa jicho kali kiasi, naye akauliza, "Nini?"

Nikashindwa kujizuia kuanza kucheka, nami nikageukia upande wa kioo na kuendelea kucheka tu.

"Nini kimekupa raha?" akaniuliza hivyo tena.

Nikamwangalia na kusema, "Yaani kumbe ulikuwa unasikiliza ya huku?"

"Kwani niko nje ya gari?" akauliza hivyo. 

Nikacheka tena kidogo.

"Unaongea na malaya zako ukiwa na mimi, una akili sawa sawa?" akaniuliza hivyo.

Aisee! Yaani yeye kila kitu kwake ni kibaya tu.

Nikamwambia, "Basi yaishe. Sitarudia."

Akasonya kidogo kuondoa kero.

Nikaendelea kumwangalia kwa jicho makini sana, yeye asijue ni namna gani nilivyokuwa nawaza mengi mno juu yake, nami nikaipumzisha simu yangu na kuendelea kutulia.  

★★

Si dakika nyingi kutokea hapo nasi tukawa tumeingia upande wa jengo moja maridadi sana, na gari likapelekwa eneo la maegesho ambalo lilikuwa limejaa magari ya watu wengine. Ikanibidi nihakikishe ikiwa sehemu hiyo ndiyo iliyokuwa yenyewe, na kweli ilikuwa ni yenyewe. Wapi? Jengo la Casino ya The African Princess! 

Mh? Nikamtazama Bertha kwa umakini, ambaye alikuwa akiongea na dereva kuhusu kutuacha malangoni mwa jengo hilo kisha akatafute sehemu nyingine ya kuegesha gari kutokana na maegesho ya hapo kujaa. Sikushangaa kuja sehemu kama hii, lakini sikufikiria hata kidogo kwamba ingekuwa hapo. Msemo wa Bertha kuhusu kuja kucheza karata ukawa umeeleweka vizuri zaidi sasa, ila najua hilo halikuwa lengo pekee la kufika hapo. Nikatulia tu. 

Dereva akalisogeza gari usawa wa malango ya jengo hilo maridadi sana, kisha akatoka na kutufungulia mlango, nasi tukashuka. Niliigiza vyema kuwa "gentleman" kwa kukishika kiganja chake madam kama wazungu vile, naye dereva akaliondoa gari hapo baada ya sisi kuanza kuyaelekea malango. 

Haipingwi kwamba hii ilikuwa ni sehemu ya watu wenye pesa, na angalau Bertha alijitahidi sana kutufanya tuonekane kuwa pea moja ya watu wa majuu. Na mpaka mwanamke huyu kunivalisha vizuri namna hii na kunileta hapo kwa njia fulani kama vile sisi ni wanandoa, ilionyesha alikuwa amenikubali sana. Ila akili yangu ilikuwa imetekwa zaidi na yale ambayo yangetokea huko ndani ya jumba hilo la kamari.

Hakukuwa na wengi tulioingia nao, na hata kuona kwamba eneo la maegesho lilijaa ilimaanisha ni kweli kabisa yale Bertha aliyokuwa akisema kuhusu kuchelewa. Ikiwa ni saa tano ya saa sita sasa, tukafikia hapo malangoni, nasi tukakutana na mabaunsa wawili, tena nafikiri walikuwa kama wale makomando wa jeshi kabisa, naye Bertha akasalimiana nao kwa njia iliyoonyesha kwamba walimfahamu. 

Mwanamke alikuwa amepitisha mkono wake ndani ya kiwiko changu nilichokunjia usawa wa ubavu, nami nikiwa makini, nikawatikisia jamaa kichwa kisalamu. Mmoja wao akatumia kile kifaa cha kupima vitu vyovyote hatarishi mwilini kwa kukipitisha kuanzia mabegani kwangu mpaka viatuni, kisha akaturuhusu tupite bila hata kumkagua Bertha. Alifahamika hapo. 

Tukaingia. Hii ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia sehemu hii, na aisee! Walioijenga walifanya kweli. Palikuwa pazuri. Sana. Watu wengi wenye pesa zao walikuwa hapa na kule, aidha wakifanya michezo tofauti tofauti ya kamari, ama kujitumbuiza kwa muziki, pombe, na wanawake. 

Aisee, wanawake! Yaani... PISI! Sikuona mzembe hata mmoja humo, yaani wote walikuwa wazuri, shepu hizo, sura, vinguo walivyovaa sasa, ai! Tesha angezimika sana kuwa sehemu kama hii. Yaani kuna mambo mengi kiasi kwamba siwezi kuyaelezea yote hapa!

Kuingia kwetu hapo kulifanya wengi wao watutazame sana. Unajua kutokana na Bertha kuwa amezoeleka hapo sidhani kama yeye ndiyo alikuwa kitovu cha hayo macho kodo, ila juu ya ni nani aliyekuwa pamoja naye wakati huu. Mzee mwenyewe. Niliendelea kuweka mwonekano wangu makini usoni kama sijali lolote lile kabisa, naye Bertha akaninong'oneza sikioni akisema kwamba niendelee kuwapa mikazo ya namna hiyo hiyo. Alikuwa anataka tupite kwenye kona na kumbi zenye watu ambao wangetutazama sana, na kwa hilo niliridhia. 

Tukaendelea kutembea, kwa mwendo wa taratibu wa wapendanao, na nilikuwa namwambia mambo yenye kufurahisha sana ingawa hakuwa mwanamke chekelea, ili nijenge mazingira yenye ukaribu zaidi kadiri ambavyo mchezo huu ungeendelea kusonga. 

Tukaanza kufatwa na washobokaji japo wenye hela, wakitusalimia, huku wanawake wakali wakipita-pita karibu nami na wengine wakinitazama mno. Samaki mpya kwenye bahari ya papa, yaani wote wanataka kuning'ata! Mpaka kuna watu kadhaa wakawa wameomba kupiga picha na sisi, wakituona kuwa kama watu maarufu, naye Bertha akawakubalia na kuniruhusu nimshike kiunoni na kumbusu shavuni. Nilikuwa sahihi kabisa, alikuwa ananioshea huyu. 

★★

Baada ya kuchangamana na mataita wawili watatu waliomwelewa madam na kushusha wine kali pamoja nao, Bertha akaniambia sasa ulikuwa umefika muda wa kunipeleka sehemu ambayo ilidili na suala la unyama wetu, ili aweze kuniingiza kundini. 

Wakati huu ilikuwa ni saa saba usiku, naye akanishika mkono na kunitoa sehemu ya VIP tuliyokuwa tumekaa, kisha akaanza kunipeleka upande mwingine wa jengo ambao ulitufikisha kwenye ngazi zilizoelekea chini. Haikuonekana kama tulikuwa juu, kwa hiyo bila shaka kulikuwa na sehemu iliyojengwa chini ya ardhi kwenye jengo hilo, nasi tukashuka. 

Bertha alikuwa ameshachangamka kutokana na wine alizopiga, na najua huko tulikoenda ndiyo kungekuwa na mizuka zaidi. Hata huko tulipotoka palikuwa pamechangamka, ila tulipofika huku chini, hadi mimi mwenyewe nikakubali. Palikuwa pa moto! Watu waliokuwepo walifanya kila aina ya ujinga, waziwazi, bila aibu, bila vizuizi. Yaani ilikuwa ni kama nimeingia kwenye zile zama za waroma na Spartacus! Sikuamini. 

Kumbi ilikuwa inalindwa hiyo, na Bertha alitoa pesa fulani ndefu inayofanana na dola, kama kiingilio sijui, kisha ndiyo tukapita. Kulikuwa na taa za rangi mchanganyiko. Moshi ulitawala. Harufu zilikuwa nyingi sana; harufu si ya bangi, shisha, mirungi, manukato, madawa ya kuchoma, makalio, na bila kusahau makwapa! Zote zilichanganyika huku.

Joto lilikuwa kali ukitegemea na nilikuwa nimevaa suti, naye Bertha akaendelea kunivuta kuelekea upande mwingine wa mbele zaidi. Tulikuwa tunawapita watu huku nikishikwa-shikwa na kuvutwa kabisa, si na wanawake, si na wanaume, yaani ah! Mola nisaidie!

Mimi na madam tukafika mpaka kwenye mlango mmoja mfupi sana, kukiwa na baunsa mmoja aliyekaa kitini akitutazama kwa umakini, na akiwa na bunduki ndefu, naye Bertha akatoa ufunguo fulani mkobani mwake na kisha kuuchomeka kwenye tundu lisilo na kitasa, nami nikaona kitaa fulani cha kijani kinawaka kwa juu. 

Akasukuma huo mlango, nasi tukaingia kwa kuinama, kisha akaufunga tena. Bila shaka hii ndiyo ilikuwa sehemu ya "Top Secret," na ile nimesimama vizuri na kupaangalia ndani humo, nikajikuta nashangaa kiasi baada ya kumwona mtu fulani niliyemfahamu. Oh, kulikuwa na watu kadhaa ndani hapo lakini ni huyu tu ndiye aliyevuta umakini wangu zaidi. 

Mwanaume mtu mzima, akiwa amekaa kwenye sofa la sakafuni, yaani yale ya chini bila mbao, na wanawake wawili wakiwa nusu uchi huku wakimtikisia makalio na matiti yao kumzunguka usoni na mwilini, na alikuwa anayalamba. Ilikuwa ni mchumba Festo! Yule yule jamaa aliyekwenda kwake Miryam ili kumtolea mwanamke huyo posa, na ambaye nadhani mpaka kufikia kipindi hiki bado alikuwa anajibebisha kwa mwanamke huyo, ndiyo alikuwa sehemu hii ya madhambi akipewa burudani. 

Lakini kwa nini awe ndani ya sehemu hii iliyokuwa ya maovu zaidi na ya siri sana? Alihusika wapi kwenye haya yote ambayo Bertha alitaka kunionyesha?

 

★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next