Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Nikaendelea kumwangalia Festo kwa umakini, jinsi ambavyo alionekana makini sana na mzoefu katika hali niliyokuta yupo ndani yake, naye madam Bertha akanipita huku akisema niache kuzubaa na nimfate. Nikatii. Chumba hicho kilikuwa kipana kuliko namna ambavyo ungedhani kwa jinsi mlango wa kuingilia ndani hapo ulivyokuwa mdogo, na kiliundwa kwa njia fulani kama vile vyumba vya matumbuizo ya wanaume wahindi, au wadubai, Kamasutra-Kamasutra yaani.

Kulikuwa na nguo ndefu kama mapazia yaliyotundikwa hapa na pale kuzungukia sehemu ya sakafu lililotandikwa zulia jekundu pande zote nne za kona, yakipeperuka taratibu huku na huko kutokana na kitu kama kiyoyozi nadhani ambacho sikukiona, na sehemu hiyo ya kati ndiyo iliyokuwa na yale masofa ya chini, ungeweza kuyaita vitanda-masofa, yaliyokuwa yametengeneza umbo la mraba na kuacha nafasi ya wazi katikati ambayo ndiyo hao wanawake waliokuwa wakicheza walikuwepo. 

Kilionekana kuwa chekundu tii, yaani hadi sisi watu tulionekana kuwa na ngozi nyekundu kabisa, na ukimwondoa Festo, kulikuwa na wanaume wengine watano wenye vitambi vya pesa waliolalia masofa hapo chini huku wao pia wakipewa burudani na wanawake, ama kuvuta tu madawa ya kulevya na kunywa pombe. Nilikuwa nimeingia sehemu yenye kutatanisha zaidi tofauti hata na hiyo tuliyokuwa tumeipita muda mfupi nyuma. 

Bertha aliniongoza mpaka kufikia yale masofa, naye akakaa kwenye uwazi ambao niliweza kukisia ulikuwa spesho kwa ajili yake. Baadhi ya wale wanawake waliokuwa humo waliniangalia sana, na wale wanaume pia, na wanaume hao walikuwa wameacha vifua nje ama kubaki tu na kaushi na suruali. 

Ni Festo ndiye aliyekuwa mwenye kifua cha mwanaume mtata, kikiwa kipana na kilichokatika kimazoezi haswa, tofauti kabisa na nilivyomdhania mara ya kwanza nimemwona. Alikuwa imara. 

Nilihisi joto sana, lakini bado sikulitoa koti. Bertha akiwa amekaa kwa kuegamia kiwiko chake, akatoa kipepeo cha mkononi kwenye mkoba wake na kukifungua, tule wachina wanatopendeleaga, naye akawa anajipepea huku akielekeza uso wake juu. 

Mimi nilikuwa nimesimama nyuma yake, nikiendelea kutazama tu mambo haya, nisielewe nini kilikuwa kikiandaliwa hapa, lakini nilijua hii ndiyo ilikuwa sehemu sahihi ya kuwepo. Kama masihara tu vile mimi simba nikawa nimeingia kwenye pango la mbwa-mwitu. Na taratibu tu ningehakikisha nawanyafua wote! 

Ila huyo Festo, bado alikuwa ananifanya nikune ubongo wangu, maana sikutarajia kabisa kumkuta, na kumjua namna hiyo. Halafu alikuwa anaonekana bonge moja la mtakatifu kama ungekutana naye kule nje, yaani dah! Ikiwa Miryam angekuwa amelegeza vyuma kwa huyu jamaa basi alikuwa na kazi nzito sana. Jamaa hakuwa ameniona bado kutokana na kuzama zaidi kupiga makofi makalio ya wale wanawake.

Mimi nikaendelea tu kusimama, nami nikamwona mmoja wa wale wanaume watano akimuuliza Bertha kwa ishara kuhusu mimi kuwa nani. Bertha akaninyooshea mkono wake kutokea hapo alipojilaza, nami nikaupokea na kuja mbele yake, kisha nikakaa kwenye hilo sofa usawa wa ubavu wake. Huku yeye akiwa amejilaza kwa kuegamia kiwiko chake, na uso wake ukiwa karibu na bega langu, akaivuta shingo yangu na kunifata kinywani. 

Hakuanza kunibusu moja kwa moja, badala yake, mdomo wake ulipokuwa karibu na wangu, akasema kwamba hii ni show tu kwa hiyo niigize vyema, nami nikamwambia asihofu, ninajua. Kisha ndiyo akanipiga busu mdomoni. Najua alikuwa na madhumuni yake kunibusu hivyo mbele ya wale wanaume na wanawake, ili awape maana fulani kuhusu ukaribu niliokuwa nao kwake mpaka yeye kunileta hapo, kwa hiyo nikaona niongeze njonjo pia katika maana hiyo. 

Nikaipokea busu yake kama alivyoileta, lakini nikaanza kuinyonya midomo yake kwa hisia nzito zaidi, a.k.a sensual. Nilihisi kwamba Bertha alikuwa anataka tuikatishe, lakini mimi nikaiendeleza tu na kuula ulimi wake kama vile sikutaka kuacha, ndipo nikahisi kwamba alianza kulegea. Yaani nilimbusu kwa ufundi mpaka akaanza kujiachia ili niendelee tu, lakini mimi ndiyo nikaikatisha hapo sasa. 

Nadhani ilikuwa imekatika dakika moja ya kumpiga denda namna hiyo, naye akawa ananitazama kwa umakini baada ya kuwa nimemaliza. Nikamshika shavuni kwa wororo na kumwangalia kama vile nampenda sanaaa, yale macho yangu yale, naye akashindwa kujizuia kutabasamu. Nikawasikia wanaume wawili wakisema kwamba kwa hiyo madam alikuwa ameamua kuja na ben ten wake hapo ili awakomoe maana siku hizi hana wa kucheza naye huku chini, na ndiyo nikawa nimewatazama. 

Sasa ndiyo nikakuta Festo akiwa anaangalia upande wangu, na akinitazama kwa macho yenye umakini sana. Si ile 'mh, huyu mbona kama namjua?' Nafikiri sasa akawa amethibitisha kuwa ndiyo, alinijua. Akakaa vizuri zaidi hapo alipokuwa na kuendelea kuniangalia kwa umakini, nami nikakaa vizuri pia na kumtikisia kichwa kidogo kama kumpa salamu. Yaani nilifanya ionekane kama vile sikuwa nimeshangaa kumwona hapo, naye akanitikisia kichwa pia huku akiniangalia kama vile bado ananitathmini. 

Bertha akawa anawapiga vijembe wale wanaume kwa kumtania kuhusiana na mimi, matusi kabisa lakini walikuwa wanacheka kwa pamoja, naye Festo akatoa amri kwa wanawake wote waliokuwa humo waondoke, isipokuwa Bertha. Walimbwende wakajikusanya na kuvaa nguo zao, kisha wanaume wengine wakawapa pesa na mmoja wao kwenda nao pale mlangoni. Akawafungulia, fwii wakaondoka. 

Festo akavaa T-shirt jepesi mwilini, sura yake ikionekana makini kweli sijui shauri ya kuvurugwa na uwepo wangu ndani hapo, na najua alikuwa akijiuliza mengi ya ni kwa nini nilifika kwenye nyumba yao ya maovu. Kwa kiasi fulani, nilianza kuona ni kama vile jamaa alikuwa na sauti fulani kubwa hapa, huenda hata ndiye aliyekuwa kiongozi wa hizi operesheni zao. Ingenibidi niendelee kutulia ili nione ya kuona.

Bertha akawa ameombwa po na wale wanaume maana kwa maneno hawakumshinda, naye akasonya na kunishika begani, kisha akasema, "Honey... vua koti, hausikii joto?" 

Aliniongelesha kama vile sisi ni wapenzi kweli, nami nikamruhusu aanze kunitolea koti. Nilikuwa nimeweka uso makini kweli, hata wale wanaume walioniita ben ten hawakuwa wamenisemesha wala kunirushia ishara yoyote maana nilionyesha sikutaka shobo nao.

"Mbona mtu wako haongei madam?" mmoja wao akamuuliza hivyo Bertha.

"Umemsemesha ukaona haongei?" Bertha akamuuliza.

"Niaje dogo?" huyo jamaa akaniambia hivyo.

"Usiniite dogo. Naitwa JC," nikamwambia hivyo kwa sauti makini.

Festo akaniangalia.

"Aah, kumbe na yeye mjeuri tu kama wewe eh?" mwanaume mwingine akamwambia hivyo Bertha.

"Tena sana tu," Bertha akamwambia hivyo.

"Umemtoa wapi?" mmoja akamuuliza hivyo Bertha.

"A-ah, swali muhimu ni... anafanya nini hapa? Uliapa kutoleta wapenzi wako humu tena, maana dear kwenye wapenzi huwa unafeli sana," mwingine akamwambia hivyo.

"Kwani wewe kinachokutoa ugwadu hapa kuhusu mie kuja na mpenzi wangu ni nini?" Bertha akamuuliza.

"Hauna mume wewe?" jamaa akamuuliza hivyo pia.

"Kwani we' huna mke? Mbona mahawala zako walikuwa hapa?" nikamuuliza hivyo.

"Hahaaa... mpe vyake..." Bertha akasema hivyo.

Huyo mwanaume mtu mzima akaniambia, "Unajua unaongea na nani we' mtoto? Unanijua mimi?"

"We' unanijua?" nikamuuliza hivyo pia.

Akaangaliana na wenzake kama anashangaa, nami nikamwona Festo anatabasamu kidogo. Nikaendelea kumpa huyo jamaa aliyeanza kunichokoza utizami usio wa masihara.

Bertha akawa ananipiga-piga kwa kiganja chake kwenye bega langu na kusema, "Huyu ndiyo mwenyewe! Usifikiri nimemleta kumpa tour, ana jambo lake kuu hapa."

"Jambo gani? Kuna kitu chochote kile hapa ambacho tunaweza kumhusisha mtu mwingine zaidi yetu? Huyu mwanamke anataka kutuletea balaa, eti?" huyo jamaa akaongea hivyo na kuelekeza hilo swali kwa Festo.

"Acha kashfa Sudi! Unatumia neno 'mwanamke' ili kunishusha hadhi, au? Bila mimi usingekuwa na hilo tumbo lako kubwa sasa hivi, naomba uheshimu uwepo wangu hapa... usilete dharau," Bertha akamwambia hivyo huyo jamaa.

Huyo Sudi ndiye aliyekuwa amechomwa sana na suala la Bertha kunileta hapo, naye akasema, "We' ndiyo uache dharau! Kwani kuwa na part muhimu kwenye ishu zetu ndiyo inamaanisha tukuangalie tu ukianza kufanya makosa? Umesahau yaliyotokea ulipomweka mume wako kwenye mambo yetu? Unataka kurudia historia tena?"

"Sudi, hebu tulia. Madam ana maana yake kufanya anachokifanya, msikilize kwanza, ujue..." jamaa mwingine akajaribu kumtuliza.

"Hakuna bana! Hatuwezi kukubali mipango yetu ivurugike tena kisa kuacha mtu alete vitoto ili kuviweka kwenye mambo ya wakubwa!" Sudi akafoka.

"Huyu jamaa vipi? Mbona anakuwa kama chura-konkodi?" nikamsemesha Bertha hivyo karibu na mdomo wake kwa sauti ya chini.

"Yaani! Si lisenge tu!" Bertha akasema hivyo kwa kuudhika.

"Unasemaje we' dogo?" Sudi akauliza hivyo.

Nikamgeukia na kuanza kukunja mikono ya shati langu kuelekea viwiko, nami nikamwambia, "Unataka kujua utoto wangu uko wapi? Simama nikuonyeshe."

Jamaa akasimama kwa hasira, nami nikasimama pia. Nilikuwa naonyesha ubabe wa aina ya juu ili watu wa humu wasifikiri nilitembea tu nyuma ya mgongo wa Bertha, na baada ya kusimama hivyo, Sudi kitambi akatoa bastola kutokea nyuma ya kiuno chake na kuinyoosha kunielekea.

"Wee! Sudi!" Bertha akafoka namna hiyo.

Festo aliendelea kutuangalia huku akicheka kwa pumzi, ikionekana alifurahia sana drama hiyo mbele yake, nami nikaendelea kusimama hapo hapo huku nikimtazama Sudi kitambi kwa hasira. Bertha akanyanyuka na kutoa bastola kutokea kwenye mkoba wake, naye pia akamwelekezea Sudi. 

Mapigo yangu ya moyo yalidunda wewe! Hii ilikuwa sehemu hatari sana aisee, nami mpaka nikajiuliza sijui hawa watu walikuwa wanatoa wapi hivi vifaa vyao. Yaani sikuwa hata na wazo kwamba Bertha alikuwa na bastola mkobani, ndiyo maana kumbe hata hakukaguliwa pale mlangoni wakati tunaingia. Hawa watu walimiliki sehemu, siyo poa! 

Bastola bado zikiwa hewani na hisia angani, mwanaume mmoja aliyekuwa amelewa kiasi akasema, "Si mtusuane tu? Nimemiss kuona damu."

"Mwambie ajaribu aone namna nitakavyopasua utumbo wake na kumpa autafune!" Bertha akasema hivyo kwa hasira.

"Aisee, sisi hapa ni familia. Mambo gani haya mnafanya?" mwanaume mwingine akasema hivyo.

"Yaani huyu pussy asiyenijua ni wa kunitukana mimi?" Sudi akasema hivyo huku bado akiielekezea bastola yake kwangu.

"Hajakutukana, amekwambia unyanyuke mpigane. We' ukaingilia vyuma," mwingine akasema hivyo.

"Na ndo' nasema hivi... ajitoe akili apige hiyo risasi. Ataelewa kwa nini Twaha Kiduku hanyoagi punk!" Bertha akasema hivyo kwa mkazo.

Festo akacheka kidogo, naye akajisawazisha na kusema, "Sudi... weka silaha pembeni."

Jamaa akaendelea tu kuninyooshea mguu wa kuku huku akinitazama kama vile alikuwa anajua ningekuja kuwa-snitch.

Festo akavuta glass yenye wine na kusema, "Usitake nirudie kukwambia kwa mara ya pili," kisha akainywa wine hiyo.

Sudi akashusha mkono wake mnene huku bado akituangalia mimi na Bertha kwa chuki, naye akakaa kwenye sofa. 

Bertha akaachia msonyo mrefu na kushusha bastola yake pia, naye akasema, "Ulikuwa unafikiri nini, angekimbia au? Huyu siyo easy kama vile unavyodhani, ungekuwa mwanaume kweli ungechomoa bastola wakati kakuomba mzidunde? Lioga tu, ulikuwa unajua ungefumuliwa...."

"Basi Bertha, inatosha. Nawaomba mkae," Festo akatuambia hivyo.

Bertha akawa wa kwanza kurudi kukaa, nami nikakaa pembeni yake pia huku bado nikiwa natazamana na yule bwege. Wanaume wengine wakakaa kwa njia makini zaidi, na huyo Sudi akaanza kuvaa kaushi nyeupe.

"Wote tumekamilika sasa, ila madam umechelewa mno. Usingizi ushaanza kunivuta," Festo akasema hivyo.

Alikuwa na sauti fulani hivi, kuu, ya mamlaka, yaani ilidhihirisha wazi kwamba aliridhika na chochote kilichofanya maisha yake yawe yake.

Bertha akamwambia, "Usingizi wapi Saido... wakati nimekukuta unapagawisha macho tu hapo!"

Festo akacheka kidogo kwa pumzi.

"Kulikuwa na jam, afu' designer wangu alichelewa pia kutuletea costu...."

"Sisi hatujali hayo. Tufanye ya maana hapa, tuondoke," Sudi akamkatisha Bertha.

Bertha akamkata jicho la hasira, kisha akaigiza kukohoa na chini ya pumzi yake iliyotoka akawa amemtukana huyo Sudi. Lile tusi kubwa kuelekea mama ya huyo jamaa! Nikabana kicheko lakini kikaniponyoka puani, na huyo Sudi akawa ananitazama kwa hisia kali. Eti 'haiwezekani!'

Festo akasema, "Well, muda umeenda. Itakuwa vizuri madam... ukituambia proposal mpya uliyosema unataka kuweka mezani. Tunakusikiliza."

Bertha akairudisha bastola mkobani na kisha kuyatoa yale madawa niliyokuwa nimetengeneza, naye akamrushia Festo moja, na zile zingine kwa wanaume wengine watatu.

"Hii nini? Molly au?" akauliza mmoja.

"Sembe," Sudi kitambi akasema hivyo.

"Cocaine. Lakini kama navyopenda 
kuiita, "special cocaine,"" Bertha akasema hivyo.

"Umezinunulia wapi?" akauliza mwanaume mwingine.

"Oh, ndiyo hicho Farao. Sijanunua. Nimetengeneza," Bertha akasema hivyo.

Wengine wakabaki kumtazama kwa umakini.

"Katika kipindi chote toka tumeanza hii business, sidhani kama mmewahi kukutana na coke tamu kama hizi. Mnaweza kuonja halafu mnisimulie," Bertha akawaambia.

Wengine walionekana kutomwelewa na kuanza kuziangalia tu dawa hizo, lakini Festo alikuwa mtu wa vitendo zaidi. Akatoboa kifuko hicho kwa kidole chake kimoja na kukiingiza mpaka ndani, kisha akakichomoa na kukisogeza karibu na pua yake; akiangalia unga huo kwa umakini.
 
Akalamba kidogo, huku sisi wote tukiwa tunamwangalia, naye akatulia na kututazama tena kwa njia ya kawaida. Kisha akaangalia juu kiasi, halafu akafumba macho yake na kuyafumbua kwa kurudia-rudia, naye madam Bertha akacheka kidogo kwa kujivuna.

"Umeona muziki huo? Sekunde mbili nyingi tu, ishakugonga," Bertha akasema hivyo.

Festo akawa anaiangalia dawa hiyo kwa umakini, naye akasema, "Damn! This is good shit."

"Pigia mstari," Bertha akasema hivyo.

Wale wanaume wengine waliorushiwa hizo dawa nao pia wakatoa na kuonja, na ikawa wazi kwamba walipagawa haswa maana walidumbukiza nyingi mdomoni.

"Ei! Aloo... hii kitu mbona kali mno? Mamae... yaani mpaka raha, sss..." akasema hivyo yule ambaye Bertha alimwita Farao.

"Ah, huu ndo' unyama sasa. Madam umepata patia," akasema hivyo mwingine.

Nikaona jamaa mwingine anaanza kama kusinzia na shingo kulegea kabisa, naye Bertha akamwonyeshea kwa kidole huku akicheka. 

Huyo huyo jamaa akasema, "Kitu swafi sana. Wanigga wameziboresha au?"

"Nimewaambia hizo nimezitengeneza," Bertha akasema.

"Umezitengenezaje?" mmoja wao akauliza.

Bertha akapitisha mkono wake begani kwangu huku akiniangalia kwa kujivunia, naye akasema, "Ben ten wangu ndiyo katengeneza."

Wengine wakanitazama usoni, naye Festo akawa ananitazama kwa umakini pia.

"Kutengeneza... yaani... siyo kwamba katoa sehemu fulani market, ila katengeneza yeye mwenyewe?" Farao akauliza huku macho yake yakiwa mazito.

"Ndiyo," mimi ndiyo nikamjibu.

"How?" Festo akaniuliza hivyo.

"Ni med na chemo mixture and separation process. In simplicity... ni Kemia tu," nikamwambia hivyo. 

Festo akarudi kuyaangalia madawa hayo tena.

"Eh bwana eh! Kumbe uko na fundi?" akauliza hivyo mmoja wa wale wanaume wengine.

"Unafikiri natembea na wazembe, Tito?" Bertha akamuuliza hivyo.

"Hata me naona. Ila we' siyo kwenye Kemia tu mdogo wetu, mpaka na kwa bed unambinua huyo bibi kiufundi, au siyo?" huyo Tito akanisemesha hivyo.

"Haichomoki yaani, kwa hiyo usiulize," nikamwambia hivyo.

Bertha akacheka kidogo kwa pumzi, naye akamwambia Festo, "Nipasie na mimi, nishazi-miss."

Festo akaninyooshea kimfuko chenye madawa, nami nikakipokea na kumpa Bertha. Akachovya pia na kupitisha puani mwake, kisha akashusha pumzi ya mridhiko na kuniangalia kwa furaha.

Tito akalamba madawa tena na kusisimka, naye akaniambia, "I like you."

Bertha akamsonta kwa kidole chake kama kumpa kichwa.

"Pointi ya haya yote... ni nini?" yule Sudi kitambi akaongea hatimaye. Bado alikuwa amekaza tu, hakutaka hata kugusa madawa hayo kisa nimeyatengeneza.

Bertha akamwangalia Festo na kusema, "Festus... hiyo ni kama sample tu, HB wangu amebumba hiyo kitu ndani ya wiki moja tu bila kuwa na vifaa wala space ya kutosha. Imagine kama hiyo procedure itapanuliwa kwa kuongezewa resource... na muda. Unaona kile nachokiona?"

Festo akaniangalia kwa umakini.

"Kwa hiyo unataka kusema nini? Tum..tegemee hawala yako ndiyo awe anatutengenezea dawa, ndiyo nini, tutapata faida kubwa zaidi ya tunayopata sasa hivi?" Sudi akamuuliza hivyo Bertha.

"Kumbe akili yako bado ndogo sana Sudi. Nakushangaa, sijui umeipeleka wapi ile uliyokuwa nayo mwanzoni," Bertha akamwambia hivyo.

"Funguka zaidi Bertha," Festo akasema hivyo kwa sauti tulivu.

"Tumeshazoea kubeba mifuko ya zawadi kutoka nje, tunaisambaza vizuri kwa mabosi mpaka kuwafikia wahuni kwa sababu tuna fence imara na wazungushaji wenye akili, lakini bado hatulipwi vile tunavyostahili. Maana yangu siyo kwamba tuachane na njia zetu, a-ah, ila nataka tuongeze faida. Tunaweza kutengeneza pesa zaidi kwa kutumia kipaji kama hiki. Abra to dabra, coke mmeshazitumia sana, lakini mmeshakutana na yoyote kama hii? Hakuna. Huyu HB anajua. Fikiria sasa kama tutafanya kazi ya kutengeneza hivi vitu SISI wenyewe, vikaanza kutembea, tukavipa jina likakua, unafikiri ikishasambaa 'market' watu watataka ya nje tena? No. Watataka hii zaidi cause ndiyo nzuri, mifuko ya zawadi itatoka kwetu sisi wenyewe, faida itaongezeka mara mbili zaidi ya hii ya sasa. Na tutakuwa tunazifanya zote kwa pamoja. Sijui kama notes zimetoshea ubaoni, au niongeze chaki?" Bertha akasema hayo kwa ushawishi.

Festo akatazama pembeni akiwa kama anatafakari mambo vizuri.

"Subiri. Yaani unataka tuingize hii kitu nyingine tena ndani ya ishu zetu? Si tutachanganya mambo? Una hicho kiwanda huru cha kutengenezea hizi ishu, au unaongea tu?" Sudi akauliza.

"Ish... hivi unaujua mtonyo, ama na we' unaongea tu? Hizi ni vision za kutuongezea faida, we' kama umeridhika na ulipo tu, ni wewe. Hii ya kwetu imetusaidia tumefungua mahoteli, mabiashara, na ma-club, lakini tukijumlisha na hii ya HB wangu, sisi wote hapa tutamiliki mpaka ma-estate kabisa! Festus unajua niko sahihi... hili ni suala la kuanza kupangwa na kufanyiwa kazi ili matokeo yaje haraka," Bertha akasema hayo kwa uchochezi.

Nilikuwa nimetulia tu nikimsikiliza kwa umakini mwanamke huyo. Alikuwa na akili, akili ya kufikiria mbali sana, lakini mchecheto wake wote kuelekea mafanikio kupitia madawa ya kulevya ndiyo ambao ungemwangusha. 

Alikuwa amesema mambo ambayo yalinifanya nione kwamba hawa watu walikuwa na njia za kijanja sana za kuficha ishu zao, na ndiyo mimi kujiingiza huku kungenifunulia hizo njia ili niweze kuzifunua pia na kuwaharibia biashara zao. Hadi walikuwa wanajenga mahoteli na ma-club kwa kuwaharibia vijana wakati wao ujao kwa kuwasambazia madawa ya kulevya! 

Hapa kweli nilijiona kuwa kama askari mpelelezi aliye 'undercover,' na kipawa nilichokuwa nimebarikiwa kuwa nacho kingeendelea kusaidia kunisogeza karibu zaidi na ushindi.

Watu humo wakaanza kujadili kuhusiana na mawazo ya mwanamke huyo, isipokuwa Festo, ambaye muda mwingi alikuwa akiniangalia tu na mimi kumtazama kwa umakini. Macho yajuanayo. Mwishowe, Sudi akatoa wazo.

"Tupige kura, sisi watano tu. Mr. Festus, madam, na wewe... JC... kura zenu hazita-count," akasema hivyo.

"Kwa nini Festus na sisi tusi..."

Festo akamkatisha Bertha kwa kumnyanyulia kiganja hewani, kisha akasema, "Sawa. Pigeni kura. Nani anaiunga mkono hii kitu ipite?"

Tito, Farao na mwingine mmoja wakanyanyua viganja kuonyesha wamekubali. Bertha akatabasamu kwa kiburi.

"Ambao hawataki ipite, namba yenu imezidiwa. Kwa hiyo hii kitu imepita. Lakini... itakuwa ni ishu yetu sote. Sitaki matabaka. Ninaeleweka?" Festo akasema hivyo.

Wengine wakaonyesha kukubaliana na hilo, ingawa huyo Sudi alikuwa gubu kali sana.

Bertha akamrushia Festo busu kwa mdomo wake na kusema, "I love you too."

Festo akaniangalia na kusema, "JC..."

Nikatikisa kichwa kuonyesha nimeitika.

"Karibu kwenye club," akaniambia hivyo.

"Nimeshafika," nikamjibu hivyo.

"Kijana mtata huyu... aagn!" Farao akasema hivyo huku akivuta cocaine puani utafikiri makamasi yasiyoisha.

"Usipakie nyingi mno, utashindwa kutoka humu," Bertha akamwambia hivyo.

"Nafikiri kikao kimefikia tamati. Twende kulala sasa," Festo akasema hivyo.

Bertha akapiga mihayo na kusema, "Kweli... bora kwenda kulala ukishashinda mechi. Makolo waliopoteza wabaki kuvimbisha mashavu kama mashalavu. Ahahah... hiyo ime-rhyme vizuri sana, au siyo HB wangu?"

Nikatabasamu kidogo tu, nikiwa naelewa kwamba alikuwa anamsema huyo Sudi kitambi, na wakati huu jamaa alikuwa tu anakula hamsini zake.

"Nipe namba yako JC... in case nikakuhitaji, au ukanihitaji," Festo akasema hivyo.

Alizungumza bila kuniangalia, akiwa bize na simu yake, nami nilielewa kwamba hilo alilosema lilihusisha mengi zaidi tu ya haya yaliyotuleta hapa.

Nikasema, "Sawa."

Bertha akaniambia, "Effect yako nzuri sana HB wangu, umeona mpaka mkubwa amekuelewa?"

Nikatabasamu tu, kisha ndiyo nikaanza kumtajia Festo namba zangu. Aisee, hii ishu yote hii! 

Festo, baada ya kuwa ameitunza namba yangu kwenye simu yake, akasema, "Tutaongea baadaye Bertha. Umeshampanga kijana wako kuhusu 411 yetu?"

"Mengi bado sijamwonyesha, ila ni mjanja... mtaalamu. Nipe dakika mbili tu nimzoeshe route zetu ndiyo uje kumtumia vizuri zaidi," Bertha akasema hivyo.

Walikuwa wanaongea kwa lugha yao waliyoielewa vizuri, na japo sikujua mengi sana ila nilitambua hilo lilimaanisha mimi kuanza kufunzwa njia zao. Bao moja kwangu!

Festo akasema, "Sawa. Ismail, fanyia kazi niliyokwambia, kabla ya jua kuzama kesho niwe nimepata intel positive."

Mmoja wa hao wanaume ambaye ndiye aliyekuwa Ismail bila shaka, akatikisa kichwa kukubali.

Festo akatazama saa mkononi na kusema, "Muda umeisha. Tutaonana ikiwa muhimu tena. Kudos madam kwa wazo jipya."

Bertha akatabasamu na kutikisa kichwa kidogo kuonyesha amepokea sifa.

"Wengine endeleeni na kazi kwa umakini, mkate uingie. JC..." Festo akasema hivyo.

"Naam mkuu..." nikaitika namna hiyo.

Akatulia kidogo akiniangalia kwa utathmini, kisha akasema, "Nimefurahi kukujua leo."

"Mimi pia," nikamwambia hivyo kwa sauti makini.

Hiyo ilitolewa katika maana pana zaidi ambayo sidhani kuna mtu mwingine hapo angeweza kuitambua, naye jamaa akawa wa kwanza kunyanyuka ili aweze kuondoka. 

Bertha akanyanyuka pia pamoja na mkoba wake, huku akiwa anamtazama Sudi kwa mkazo, na jamaa pia alikuwa amekaa bado huku akituangalia kwa umakini. Hii ilikuwa chuki binafsi tu, nami pia nikasimama huku nikilishikilia koti langu mkononi. Bertha akawa anataniana na Farao na Tito ambao ndiyo walikuwa wenye urafiki kwake zaidi, kisha akawarushia busu kwa kiganja na kuanza kuondoka huku akinivuta mkono. 

Inaonekana wengine wangendelea kutulia kwanza hapo ili waendelee kulewa kwa yale madawa, kwa hiyo tuliotangulia kuondoka ikawa mimi, madam, na Festo, a.k.a Drug Lord Festus. Huyu jamaa ndiyo alikuwa maana halisi ya maneno "usilolijua ni sawa na usiku wa giza," isipokuwa tu kwa hapa hata ndani ya jicho lake alikuwa ameona kwamba na mimi nilihusiana na maana ya hiyo methali. 

Yaliyotufanya tujuane nje ya hii biashara yalikuwa ya huko huko nje, hapa ni kwamba ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kukutana, na ingepaswa kubaki kuwa namna hiyo. Yale ya nje tungekutana nayo tu tena na kuyapitia, na nafikiri hilo ndiyo lililokuwa lengo lake kuchukua namba zangu za simu. Ah nilikuwa nikiongeza marafiki na maadui tu aisee! 

Tukatoka ndani ya chumba hicho, na pale palipokuwa na unyama kama wote bado hapakuwa pamesinzia. Inaonekana kulikuwa na sheria kali ya kutowaruhusu watu ambao hawakuhusika na hiki chumba waje upande huu, na mlinzi aliyekuwa amekaa hapo bila shaka ndiyo alihakikisha hilo linatiki. Mimi niliweza kupita kwa sababu ya uso wa madam, na nadhani hata wale wanawake niliowakuta wanadensi humo ndani walipita kwa uchochezi wa timu hiyo ya Festo, vinginevyo isingekuwa rahisi kwa mbuzi yeyote kuingia. 

Tulipotoka tukaanza kuelekea upande mwingine kabisa tofauti na ule tulioingia nao, njia ikiwa ndefu na yenye kupinda, kuta zikiwa zimekaribia kuibana miili yetu shauri ya kukaribiana sana, ikionyesha kwamba hii sehemu ilikuwa ni pana mno huku chini. Tulikuwa tunatembea huku Bertha akilalamika kuhusu namna ambavyo Sudi alikuwa anamwonyesha dharau na kumwomba Festo afanye jambo fulani ili wenzao wote wamheshimu, la sivyo kuna siku angekuja kuwatibua. 

Festo hakuwa akiongea kabisa, na mimi nilitulia tu mpaka tulipofika sehemu iliyoanza kupanda juu kama ngazi lakini ikiwa ni barabara ya lami nyoofu, ndiyo tukatokezea eneo la nje lililokuwa na magari yaliyoegeshwa. Magari sita tu. Na ya kifahari. Nilipoangaza eneo zima, nikaona kwamba tulikuwa upande mwingine kutoka kwenye lile jengo la Casino, yaani lilikuwa upande wa pili wa barabara mbili za lami kutokea hapo tulipokuwa; likionekana kung'ara tu. Hawa watu walikuwa wajanja. 

Jengo la Casino ya The African Princess halikuwa sehemu halisi ya kukutanika kwa kundi lao, bali hiyo ilikuwa kama njia tu. Sikujua ikiwa wamiliki wa sehemu hiyo walijua kuhusu uwepo wa kikundi hiki na chumba chao maalumu huku chini, lakini sasa nilikuwa nimeelewa kwamba kundi la Festo liliitumia nyumba hiyo ya kamari kama ukuta wa kuficha sehemu yao ya siri. Yaani ilikuwa kama kuingia kwenye banda la kuku halafu usijue ikiwa chini ya hilo banda kuna pango dogo la nyoka. Na walijitahidi aisee, yaani ilikuwa kama vile niko kwenye nyanda za wazungu! 

Moja kati ya magari yale sita ilikuwa ni ile Range tuliyokuja nayo, nami nikaliona lile la Kluger ambalo bila shaka lilikuwa la Festo. Tulipokuwa tunayakaribia, akaja mwanaume aliyevaa kikomando fulani hivi huku akiwa ameshika bunduki nzito, naye Festo pamoja na madam wakampatia elfu kumi kumi, nafikiri ikiwa ni shukrani kwa kuwalindia magari yao labda... sikujua. 

Akaanza kuambatana nasi mpaka kufikia kwenye gari hizo, naye Festo akamwambia tu Bertha kwamba wangewasiliana maana alikuwa na uhitaji mkubwa wa kulala. Akapanda kwenye gari lake. Dereva wa madam alikuwepo hapo, ikionekana kuwa huduma ya kumwendesha ilitakiwa kuisha wakati ambao madam angerudishwa hotelini kwake, naye akatufungulia mlango wa siti za nyuma, nasi tukaingia kama mabosi vile na gari kuingia lamini.

★★

Bertha alionekana kuwa mwanamke aliyependa sana huu wadhifa wa kuwa kama "boss lady," ila mimi sikufagilia sana hizi ishu. Kwa wakati huu nilichokuwa nawaza zaidi ni kuhusu kumwangusha huyu mwanamke. Tena kwa kuwa sasa alikuwa amenitambulisha kwa kundi lake, hiyo ingetakiwa kuwa na wingi, yaani niwaangushe wote. 

Niliona kiwango fulani cha usawa katika mambo yao isipokuwa tu kwa Festo, ambaye kwa hapo alionekana kuwa kama sauti kuu. Bado nilitakiwa kujua namna njia za mitandao yao zilivyofanya kazi ili niwe na jambo kubwa la kumpatia askari Ramadhan, na nilikuwa mbioni kufikia huko, lakini kidogo angalau nilikuwa nimepata mwanga. 

Walitoa bidhaa zao nje, kupitia njia fulani za vificho ziliingizwa na kusambazwa kwa wanunuaji kupitia hilo soko waliloliita "market," kisha bila shaka waligawana faida. Bertha aliongelea fencing, aina fulani ya upitishaji wa mambo haramu kama madawa hayo kupitia mtu aliyekuwa kama ukuta usioonekana wa kuyaficha vyema, na ninafikiri huyo mtu alikuwa ndiyo Festo. 

Yawezekana yeye ndiyo alikuwa "fencer" mkuu kwenye kundi lao, ambaye aliunganisha hizi biashara kutoka hilo soko la giza mpaka kuwafikia 'wahuni na mabosi,' watu wenye pesa yaani, kuzungukia nchini na labda hata nje pia. Haloo! Hili lilikuwa bonge la homework yaani! 

Niliendelea kukaa kwenye gari huku nikitafakari, na nilihisi kichwa kikianza kunigonga kiasi. Nikaelewa hilo kusababishwa na uhitaji wa kusinzia pia, maana muda sasa ulikuwa unakimbilia kufika saa kumi usiku. Kidogo tu majogoo wangewika yaani ilikuwa kama nimetoka kwenye mkesha, na mpaka kuja kufika huko hotelini, niliomba dereva asisinzie njiani!

Kumwangalia Bertha, nikakuta amekomaa kuvuta madawa puani na mengine kuyalamba kwa mkupuo, nami nikamwambia, "Madam... inatosha. Fata ushauri uliompa Farao. Unaweza ukajiumiza... kumbuka hata haujala."

Akavuta pua yake kwa nguvu na kuniangalia kama vile ana mafua, naye akasema, "Ndiyo point yenyewe. Nataka hii kitu inipaishe mpaka nijisahau. Halafu me nina undugu na Musa? Lini nimemshauri Farao?"

Nikashusha pumzi kiutulivu, kisha nikaangalia pembeni na kusema, "Haya. Komaa."

Kidogo tu mwanamke huyu akanipamia begani, nami nikamwangalia kukuta akiwa ameniegamia huku kidole chake kimoja kikiwa kimejaa unga huo. Macho yake yakiwa mazito mno, akawa anajaribu kuyapitisha madawa hayo puani kwangu, lakini nikayakwepa na kuuzuia mkono wake usinifikie.

"Come on... fly high with me beybee..." akasema hivyo kilevi.

"A-ah... me niliyotumia inatosha..." nikamwambia huku nikiendelea kumzuia.

"Umetumia muda gani? Me siyo kolo... em' shika..."

"Acha bwana... madam... acha, sijisikii..." nikamwambia kiukali kiasi.

Akatulia na kuniangalia kama vile ameudhika, naye akasema, "Kwa hiyo hutaki, si ndiyo?"

Nikawa namwangalia kama vile nahisi kinyaa.

"Unaniangalia hivyo?" akaniuliza huku akinikazia jicho.

Nikashusha pumzi, nikiwa nahisi hasira, nami nikakishika kiganja chake na kukiingiza kidole chake mdomoni mwangu. Nikaanza kukilamba kwa njia ya kisirani cha wazi kabisa, kisha nikautoa mkono wake kwangu na kuangalia pembeni. Nilikunja sura nikijihisi vibaya baada ya kuyala hayo madawa, nami nikamsikia Bertha akicheka kidogo.

"Sasa je? HB wangu we' ndo' wa ukweli," akasema hivyo.

Kisha akalaza kichwa chake kifuani kwangu na kuusawazishia zaidi mwili wake kwangu ili nijitandaze vyema pia kumpa egamio, nami nikajinyoosha na kumruhusu anilalie.

Akawa anafinya-finya upande mmoja wa kifua changu kwa makucha yake huku akisema, "Nimekubali sana show yako pale Red Room. Umewaonyesha we' siyo mzembe hata kidogo... hasa... huyo Sudi. Ni mjinga sana... eti analeta nostalgia yangu na Chaz hapo ili anidumaze... ye' ni pumbujeo ama nini?"

Nilianza kuhisi kizunguzungu, kichefuchefu, na miguu ikivutwa nguvu nyingi mno, nami nikaegamiza shingo yangu kwenye kichwa chake Bertha nikihisi uvivu wa hali ya juu. Sikupenda kuvitumia hivi vitu kabisa, basi tu.

Bertha akaendelea kusema, "Isingekuwa... mazingira... ningembamiza risasi ya kichwa huyo malaya... anajifanyaga mjuaji sana... eti 'umesahau... wapenzi wako... mapenzi unafeli'... nafeli nini? Anayajua maisha yangu? Alishawahi hata kutoka na mwanamke wa hadhi yangu? Mimi na Charles ni mimi na Charles. Hawajui kwa nini... bado niko naye... na hayawahusu. Yule ni mume wangu, najua nilipomtoa... huyo msenge anajua nini?... Pumvabu zake. Halafu... ahah... HB... wewe... ahah... unajua sana ku... kunyonya lips yaani. Umejifunzi...a... wapi... kupiga ulimi denda... kama...."

Alikuwa anaongea taratibu, kiuchovu yaani, mpaka kusema tu pumbavu ilikuwa shida, na baada ya hapo ndiyo akawa ametulia kabisa. 

Mimi mwenyewe nilikuwa na wenge kali kweli hasa baada ya mwanamke huyu kunishurutisha nitie hayo madawa kwenye mfumo wangu, nami nikamwangalia na kuona akiwa amepitiwa na usingizi. Kwa uzito niliokuwa nauhisi, ukitegemea bado ilikuwa mbali kufika huko hotelini, nikaona ni busara tu nikifumba macho ili muda upite, na mengine yangefuata nikishayafumbua baadaye. 

Sijui hata zikawa zimepita dakika ngapi baada ya hapo, lakini kilichofanya nifumbue macho yangu tena ilikuwa ni kuhisi mvuto wa kutembea kwa gari kuacha na kusimama kabisa, kisha kishindo cha mlango wa gari kubamizwa kiasi kusikika. Nikajitahidi kufumbua macho na kuangaza vizuri zaidi mbele yangu. 

Kupaangalia nje kulinifanya nitambue kwamba bado tulikuwa barabarani, nisijue maeneo ni yapi, lakini dereva wetu hakuwa ndani ya gari. Mh? Kumwangalia Bertha, bado alikuwa amenilalia kwa usingizi mzito aliokuwa nao, nami nikaangaza huku na huko vyema zaidi na kupata kuona sasa jambo ambalo lilimfanya dereva wetu ashuke. 

Mbele zaidi ya gari hili, lilisimama gari aina ya Defender, likiwa wazi kwa nyuma, nami nikapata kumwona huyo dereva akiwa amesimama pamoja na wanaume wawili maaskari! Ohohoo, hilo lilikuwa ni balaa, bonge moja la balaa zito!

 

★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next