MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Nikafumba macho yangu kidogo tena na kufumbua, na haikuonekana kama nilikuwa naota. Maaskari hao, hawakuwa maaskari wa usalama barabarani, ila wale ambao huwa wanavaa kofia fulani hivi nyekundu kichwani zilizopindia upande mmoja wa kichwa. Kudadadadadeki!
Nikaanza kujitahidi kunyanyuka, lakini nilikuwa mzito vibaya mno, na Bertha kunilalia ndiyo kuliniongezea uzito. Nikajaribu kumwamsha, wapi. Hadi mate laini yalikuwa yanadondoka kutoka mdomoni mwake! Nikaangalia tena hapo nje na kuona kwamba askari mmoja alikuwa ameanza kuja huku kwenye gari, akishikilia libunduki hilo, nami nikasema "Toba!"
Hakukuwa na muda wa kufikiri aisee. Nikauchukua mkoba wa madam upesi sana na kutoa bastola na kifuko chenye cocaine, kisha nikaurusha kwenye siti na kuinama. Nikalifunua kanyagio la miguu upande wangu na kuvisukumia vitu hivi kwa chini, kisha nikalifunika na kuweka miguu yangu hapo hapo, huku nikijikalisha tena kwenye siti kwa kumweka Bertha aniegamie vile vile. Nikajifanya kuwa ndiyo nimetoka usingizini kwa kufikicha macho yangu taratibu, huku mapigo yangu ya moyo yakifanya riadha hiyo! Siyo poa.
Ni hapo hapo mlango wa upande wake Bertha ukafunguka, nami nikatazamana ana kwa ana na njemba iliyokuwa inaonekana makini kweli. Alikuwa mwanaume mtu mzima, mwenye mwili wa mazoezi bila shaka kutokana na mafunzo yao ya kivita, naye akawa anaangalia mbinuko wa paja la Bertha kwa jinsi alivyokuwa amejilaza, kisha akanitazama na mimi pia. Yaani hapa kama isingekuwa kurukishwa vichura! Sijui tu.
Nikajitoa akili na kumpungia jamaa mkono kiasi, kisha nikasema, "Habari ya kazi mkuu?"
Hakujibu salamu yangu na kuendelea kunitazama kwa umakini, kisha ndiyo akasema, "Mnafanya nini kutembea usiku wote huu?"
"Ah... kumradhi mkuu. Tumetoka kwenye sherehe, sasa... tukachelewa kidogo, ndiyo..."
"Kuchelewa kidogo? Unajua sa'hivi saa ngapi?" akanikatisha kwa kuuliza hivyo.
Nikaona yule dereva akianza kuletwa na yule askari mwingine, nami nikamwambia huyu wa mlangoni, "Najua muda umeenda... na najua kuna sheria, ila... imeenda tu nje ya uwezo wetu yaani... ni kwa sababu sisi tuna...."
Mlango wa upande wangu kufunguliwa ukakatisha maneno yangu, nami nikawatazama waliokuwa nje hapo.
"Habari za kazi mheshimiwa?" nikamsalimu hivyo huyo askari.
Ke! Nilikuwa najikaza kiume yaani, ila hofu iliyokuwepo!
Huyo askari wa pili akauliza, "Wewe ndiyo mmiliki wa hili gari?"
Nikasema, "Ni usafiri wa kulipia kutoka makampuni."
Dereva wetu akaanza kusema, "Boss... tuna... tumesimamishwa shauri ya kuwa mwendoni kwenye hii barabara muda ukiwa umeenda, ila nilikuwa najaribu kuwaelezea kwamba kuna hali zilizosababisha tukachelewa..."
"Haina shida... usijali," nikamtuliza, nikijifanya kuwa bosi kweli.
Yule askari wa kwanza akasema, "Endelea na uliyokuwa unasema."
Halafu nahisi alikuwa mhaya huyo jamaa, nami nikamwambia, "Ndiyo, yaani... tunaishi huku Sinza, sherehe ilikuwa pale Kigamboni na ni mwendo mrefu kama mjuavyo. Ugeni wetu ulikuwa rasmi kwa hiyo... tulitegemewa kukaa mpaka mwisho, so... ndiyo hivyo..."
Askari wa kwanza akauliza, "Huyu ni nani?"
Alielekeza swali lake kwa kunionyesha Bertha, nami nikamwambia, "Mke wangu."
"Amefanyaje? Mbona yuko hivyo?" akauliza tena.
"Ahah... uchovu tu. Amekunywa-kunywa pia, kwa hiyo hapo yupo ndotoni," nikamwambia hivyo.
Yule askari wa pili akasema, "Nionyeshe vitambulisho vyako."
Doh! Nikaitoa wallet yangu kutoka mfukoni mwa suruali, kisha nikapekua na kuvichomoa vitambulisho vyangu viwili; kimoja cha utaifa, kingine cha kikazi. Nikampatia.
Yule askari wa kwanza akafanya kitu ambacho nilikuwa nimehofia zaidi mwanzoni baada tu ya yeye kuingiza mkono wake ndani ya gari na kuuchukua mkoba wake Bertha, kisha akaanza kutafuta-tafuta ndani yake. Kijasho hicho nilichohisi! Niliombea tu asikute fuko lingine la unga ama hapo ndiyo ingekuwa mwisho wa safari!
Yule askari wa pili akasema, "Wewe ni daktari kumbe? Muhimbili?"
Nikamwangalia na kutikisa kichwa kukubali.
"Mnakaa wapi?" akaniuliza tena.
"Tuko hapo... siyo mbali na Makumbusho, tuna apartment Royal Village..." nikasema hivyo kwa kujiamini zaidi wakati huu.
"Ile hoteli kubwa?" akauliza tena.
"Eeh," nikajibu.
Nilitengeneza mazingira ya kuonyesha kwamba tulikuwa na hela sana, na huyo askari wa pili akanirudishia vitambulisho vyangu.
"Aisee, niwaombe radhi kwa mara nyingine tena. Najua hii haifai, na mnatimiza wajibu wenu kutulinda. Sema... inabidi hata niwape pole ya usumbufu, maana... mnapiga kazi sana..."
Niliongea hivyo huku nikiomba kwa ishara kumwelekea askari wa kwanza kuwa anipe mkoba wa Bertha, naye akanipatia. Sikuwa hata na uhakika kama kulikuwa na pesa lakini nikatafuta na kukuta kuna kakibunda ka laki moja. Oh shukrani kwa Mungu!
Nikaifungua huku nikisema, "Siyo mbaya mkiendelea kupiga kazi na ka kitu ka kuwapa boost baadaye mkija kutazama mechi ya watani wa jadi, au siyo?"
Nikamnyooshea askari wa kwanza elfu hamsini, naye akazipokea huku akisema, "Huo muda tunaupata sasa? Hahahah..."
Nikajichekesha pia utafikiri hata alikuwa ametoa utani mkubwa zaidi ya vituko vya Joti! Si unajua wahaya kwa sifa?
Nikampa na yule askari wa pili hamsini pia, naye akazipokea huku akisema, "Hii tuiiteje? Rushwa au?"
"Faini hiyo mkuu. Nimewakosea. Na tena mmenikuta vibaya, yaani ilitakiwa kutoka kubwa zaidi. Na nimemchomolea huyu ya kwake, kwa hiyo mnajua tu tukifika huko akaamka, heee ataniwashia moto huo!" nikawaambia hivyo.
Wakacheka kidogo, mibichwa sasa ikiwa imewajaa.
"Haya bwana. We'... ingia tu kwenye gari uwawahishe huko," askari wa pili akamwambia hivyo dereva wetu huku akimrudishia kadi iliyoonekana kuwa leseni yake.
Dereva na suti yake huyo akazungukia mpaka upande wa usukani. Saa kumi hiyo.
"Kuweni waangalifu next time. Wengine siyo waelewa sana, mngefanya tu hata kulala huko huko kwenye sherehe," askari wa kwanza akasema hivyo.
"Ah, imeeleweka mheshimiwa. Sema na masuala ya kazi si unajua nikaona kurudi home muhimu kwa ajili ya kesho. Na tena siyo kesho, ni leo, yaani dah!"
Wakacheka kidogo tena, na yule wa pili akasema, "Haya nendeni sasa. Lakini huyo akiamka akauliza pochi yake imeenda wapi? Utamwambiaje?"
"Nitamwambia niliinywea wine. Akininyonga sawa tu," nikasema hivyo kama vile sijali.
Wakacheka na kutikisa vichwa vyao, kisha ndiyo wakanitakia safari njema na kutuacha tuondoke. Raa!
Mwendo ulipoanza tena, dereva akawa amenisimulia kuhusu namna ambavyo maaskari hao walimsimamisha na jinsi ambavyo hali hiyo ilimfanya ahisi hasira kutokana na kutoona jambo lolote lile baya tulilokuwa tumefanya, nami nikamwambia tu haikuwa na haja ya kuangalia tena kisa hicho maana ilikuwa ishapita. Nikamwambia tu awe makini asije kutupitisha njia yenye watu wa namna hiyo tena.
Tukaipita Shekilango, na sijui ni kwa nini alikuwa amezungukia mpaka huku, ila labda ndiyo ilikuwa kufuata agizo la kupita sehemu ambazo hatungesimamishwa na yeyote tena. Akachanganya njia ya hapa na pale mpaka tukalifikia jengo la hoteli ya Royal Village hatimaye. Ah, nilikuwa nimechoka!
Tukawapita walinzi getini na kuelekea mpaka maegesho, na jitihada ya kumwamsha Bertha ikagonga mwamba kwa sababu alikuwa mbali mno kiusingizi. Hivyo nikaamua kumbeba tu mikononi, na kufikia wakati huu tayari nilikuwa nimesharudisha bastola na yale madawa mkobani mwake na kuufunga vizuri.
Dereva akasaidia kubeba vitu vyetu na kutusindikiza mpaka kufikia kwenye lifti, nasi tukaanza kuelekea ghorofani mpaka tukaingia chumbani kwake madam kwa msaada wa jamaa nilipomwongoza kutumia kadi ya kufungulia mlango wa kuingilia ndani hapo.
Nikamlaza mwanamke huyo kitandani, na inaonekana dereva huyu alikuwa akifikiri mimi ni mume wake Bertha kiukweli, kwa hiyo mpaka sasa alikuwa akiniita boss. Akaaga hatimaye, ikionekana kuwa huduma yake ndiyo ilikuwa imefikia mwisho, na nadhani tayari alikuwa ameshalipwa na Bertha; labda kupitia njia fulani ya kampuni jamaa aliyofanyia kazi.
Akatuacha, nami nikafunga mlango na kutazama muda. Ilikuwa saa kumi na moja alfajiri, na kiukweli hapa sikutaka kujali kingine tena. Nikavua ushenzi wote aliokuwa amenivalisha huyo mwanamke na kuzima taa, kisha nikawasha kiyoyozi na kwenda kujitupia kitandani hapo; pembeni ya madam. Muda haukupita mwingi sana usingizi ukawa umenibeba pia.
★★★
Nimekuja kuamka asubuhi nisiyofahamu muda wake, na tena hata sikuwa na uhakika ikiwa ni asubuhi. Macho yalikuwa mazito mno, usingizi bado ukiendelea kuyatongoza ili yafumbe na kulala tena, lakini nikajitahidi kutulia kwanza na kuufukuza usingizi kistaarabu.
Matukio yote ya usiku uliotangulia yakacheza vyema tena kichwani kwangu, na aisee, nilikuwa nahisi kiu kikali na njaa! Na hivyo vitu viwili ndiyo vilifanya nihisi uchovu mzito hata kusema ninyanyuke kwenda kutafuta maji, na ndiyo nikawa nimegeukia upande wa pili wa kitanda na kumwona madam Bertha akiwa amelala bado.
Sura yake nyeupe ya Rose Ndauka ilitazama upande wangu, akiwa amelala kwa ule mtindo chali huku mguu mmoja akiwa ameukunjia usawa wa kiuno kwa kujiachia. Hii ilifanya gauni lake lililokuwa na mpasuo matata liwe limefunuka kwenye huo huo mguu uliokunjwa, kwa hiyo wote ulionekana wazi mpaka kuionyesha nguo yake ya ndani nyeupe.
Nikajigeuza vizuri na kumtazama kwa umakini. Alikuwa amelala kama amekufa, pua yake ikionekana kutoa umafuta wa jasho ingawa kiyoyozi cha kitaalamu kilikuwa kinatupuliza, na hiyo ilionyesha kwamba alikuwa na joto kali mwilini kutokana na kutumia madawa mengi jana; ama niseme leo.
Nikaona niachane naye tu na kujinyanyua, nami nikakaa na kuikanyagisha miguu sakafuni. Mapazia yaliyotundikwa kwenye madirisha yalikuwa yameyafunika kwa hiyo mwanga wa hapo ndani ulikuwa hafifu kuelekea kuwa giza, na ni kitu kilichofanya macho yangu yatulie japo kulikuwa na kizunguzungu kichwani.
Nikaichukua simu yangu kutoka kwenye meza ndogo yenye taa pembeni, nikiwa niliiweka hapo kabla sijajitupia kitandani ile alfajiri, na ndiyo kutazama muda nikakuta ni saa sita mchana, siku ya Jumatano.
Nilikuwa nimekuta wapendwa wangu wengi wakiwa wamenitafuta, wa huku nilikotoka na kule Mbagala, na ujumbe wa salamu kutoka kwa yule Ibtisam ndiyo ulionifanya nitabasamu baada ya kukumbuka kile ambacho Bertha alimwambia jana. Nikamtumia ujumbe wa salamu pia, kisha nikaweka simu pembeni.
Nikasimama na kuelekea kwenye dirisha la upande mmoja, kubwa kweli, nami nikasogeza pazia kiasi na kuangalia nje. Kutokea hapo juu, niliweza kuona pande todauti-tofauti za jiji, watu, majengo, magari, na nilitambua kwamba mvua ilikuwa imenyesha kutokana na ardhi zenye lami kulowana na mawimgu kuwa mazito. Jua halikuonekana pia.
Nikaanza kusikia sauti za miguno kutokea nyuma yangu baada ya kusimama hapo kwa sekunde chache, nami nikageuka na kumwona madam akiwa anajinyoosha na kuviringika hapo kitandani mpaka kufikia upande niliokuwa nimelala mimi. Lakini alikuwa anaendelea tu kuviringika kuelekea mwishoni kabisa, nami nikakimbilia hapo ili kumwahi asije kuanguka.
Ilikuwa imebaki kidogo tu apigize likisogo lake, ila nikawa nimemdaka, na nafikiri mshtuko wa jambo hilo ukafanya aamke. Akawa ananitazama kwa kutoelewa-elewa nini kinaendelea, nami nikamsaidia kurudi kitandani tena huku nikimwambia alikuwa karibu kudondoka. Akajilaza chali tena na kukandamiza pua yake kwa vidole, huku akifumba macho kwa mkazo, nami pia nikaona nijilaze tu pembeni yake.
Nikawa nimeangalia juu tu nikiwaza kwenda kuoga kisha niondoke hapa, lakini ingekuwa muhimu kwanza kusikia propaganda za huyu kiumbe. Inaonekana alikuwa anajisikia ovyo tu, nami nikamuuliza ikiwa kuna chochote alihitaji. Cha kwanza kabisa alichotaka ilikuwa ni kujua kwa nini nimelala pamoja naye kwenye kitanda chake, na Dotto alikuwa wapi.
Nikamwambia sijui habari za Dotto, lakini kuhusu kwa nini nimelala hapa, nikamwelezea kila kitu kuanzia wakati alipolewa sana mpaka tukakutana na maaskari na kufika huku hotelini alfajiri ya saa kumi na moja. Aliniangalia kwa mkazo sana, asielewe kwa nini haelewi. Akajilaza kwa ubavu ili aniangalie vizuri zaidi, nami nikamtazama pia kwa kujiamini ingawa nilielewa alitaka kuanza kuangusha mabomu yake.
"Yaani ukawapa laki moja kabisa, hivi we' una akili au matope?" akaniuliza hivyo.
"Kwa hiyo ulitaka nifanyeje? Wale walikuwa FFU, siyo migambo," nikamwambia hivyo.
"Ndo' uwape laki yangu? Hivi wewe... na toka lini FFU wakakubali rushwa, walikuwa mashoga au?"
"Ah, me sijui bana. Ilikuwa tu bahati ya ngekewa..."
"Ama umeiminya hiyo hela, halafu unawasingizia tu hapa FFU?"
"Aa wee... mtafute dereva wako wa jana akusimulie yeye mwenyewe. Me siyo boya kama unavyofikiria."
"We' dogo mbona unazingua mapema sana?"
"Tumia akili yako vizuri basi sometime na we' naye!" nikamwambia hivyo kwa kuudhika.
Akaniangalia kwa umakini na kuuliza, "Unamaanisha nini?"
"Wale polisi siyo wa mchezo, sawa? Kidogo tu hadi walikuwa washashika mkoba wako kupekua, wangetusondeka kwenye Defender je? Ungepimwa wakaona unakula unga je? Ile bastola wangeiona tu kama wangetushusha pale, we' ulikuwa mawinguni madam, nilihitaji ku-act fasta ili wasitutoe mule. Sa'hivi ingekuwa story nyingine hapa, ah..." nikaongea hivyo kwa mkazo.
Akawa ananitazama kwa umakini, kisha akafanya ile cheko ya pumzi huku midomo akiikunja, naye akasema, "Kwa hiyo ndiyo umekuza sauti sasa... eti hero..."
"Ni lazima mpaka useme hivyo? Si uniambie tu asante?"
"Asante ya nini wakati umewapa hela yangu? Kwani hawalipwi? Na utairudisha, bogus wewe... nilikuwa nimeipangia mambo mengine halafu we' uje uwape tu hao wajinga!"
"Asa' madam, kweli, laki moja tu? Unanilalamikia hivyo wakati unajua nitakutengenezea mamilioni kabisa? Huoni kama unanionea?" nikamwambia hivyo kwa kujiamini.
Akabaki kunitazama huku midomo yake ikikunjamana kwa njia ya kuzuia tabasamu lake lisionekane wazi, lakini najua alikuwa akifurahi sana. Nikakunjia mikono kifuani na kutazama juu, naye ndiyo akacheka kidogo na kushusha pumzi kwa sauti kabisa.
"Watu wengine ni wakuda tu. Hawakuona magari mengine ya kusimamisha ila letu tu?" akasema hivyo.
Nikabaki kimya tu.
Akanitazama usoni na kuuliza, "Umekunywa chai?"
Nikamwangalia na kusema, "Itoke wapi? Ndiyo nimeamka tu na mimi... na ni saa sita sasa hivi, ngoja nijimwagie halafu nisepe."
"Wewe, unaenda wapi?"
"Ku... naondoka, naenda nyumbani. Nasikia njaa."
"Hivi wewe mbona una mashauzi sana? Mbona ulikuwa umekaa hapa huo muda wote kama ulikuwa unasikia njaa sana?" akaniuliza kwa njia ya kuhukumu.
"Nilikuwa nataka kuhakikisha naondoka nikikuacha upo sawa. Umeshaamka sasa, na uko good. Kwa hiyo ndiyo naenda..." nikamwambia hivyo kistaarabu.
Alibaki akiniangalia kwa macho yenye utulivu kiasi, nisijue ni sehemu ipi ya maneno yangu ndiyo alikuwa anaitafakari.
Nikajikalisha na kuashiria kutaka kutoka kitandani huku nikisema, "Utanisamehe kwa kulala kitandani kwako, lakini sipendi kulala chini. Ngoja nikuache tu, tuta..."
"Wewe, em' subiri," akanikatisha na kuushika mkono wangu kabisa.
Nikamwangalia usoni.
"Hebu kaa hapo utulie," akaniambia hivyo.
Alionekana kuwa makini zaidi wakati huu, ule u-madam ukiwa umerudi, nami kweli nikaona nitulie na kumsikilizia.
Akageukia kule pembeni na kuchukua kimkono cha simu ya mezani, kisha akakiweka sikioni na kubofya namba tatu tu. Baada ya sekunde chache, akaanza kuongea na mtu fulani, akimwambia anahitaji huduma ya vyakula vitamu kwenye chumba hiki namba 101, kisha ndiyo akairudisha simu mahala pake.
Akanitazama na kusema, "Uwe unaacha kujiendekeza na we' naye. Vitu vingine siyo mpaka uanze 'natako kuondokoo'... si unasema tu uletewe chakula, we' vipi?"
Aliongea kwa njia ya michambo na kunitazama kwa mkazo wa kiutani, nami nikatazama tu pembeni bila kutabasamu wala nini.
Akajinyanyua kutoka kitandani na kusimama karibu na kitanda, nami nikamtazama machoni na kukuta ananitazama pia. Tulikuwa tunapeana utizami makini sana, naye akaanza kuitoa mikanda ya nguo yake mabegani, akiishusha huku bado macho yake yakiwa kwangu. Ilipomtoka mikononi, ikafanya nguo yake idondoke mpaka chini, mwili wake mweupe ukiwa wazi, lakini sikuacha kumtazama machoni.
Sidiria na nguo yake ya ndani vilimsitiri vyema kwa mbele, na najua alikuwa amefanya hivyo kwa makusudi, ila mimi nikaendelea tu kumwangalia usoni na si mwilini mwake. Akatoa tabasamu la upande kwa kiburi, kisha akavua mikufu, mabangili, na pete zake na kuzirusha kitandani, halafu akageuka. Hapo sasa ndiyo macho yangu yakashuka. Hiyo nguo ya ndani aliyokuwa amevaa iliacha mashavu ya kalio lake nje, na yalikuwa meupe kama tu mwili wake.
Nafikiri Bertha alikuwa na makusudi iliyokithiri sana, kwa kuwa alianza kutembea kuelekea upande wenye mlango wa kioo kizito, ikiwa ni bafuni bila shaka, naye alitembea taratibu huku akifungua sidiria yake kutokea mgongoni kwake, kisha akaitupa chini. Nilikuwa nimeshaanza kuvimba bila kupenda, japo sikuona kifua chake kwa mbele, hali hiyo tu alivyoitengeneza ilisisimua.
Alipoufikia huo mlango, akavua nguo yake ya ndani huku akiwa ameibana miguu yake kwa uangalifu ili nisiweze kuona mengine zaidi ya kalio lake na miguu tu, naye akaitoa miguuni pake huku akiwa amenigeuzia shingo kunitazama kwa macho ya uchokozi. Huyu alikuwa ni mtu mkubwa ananifanyia hivyo! Ingekuwa ni bwege mwingine hapo tayari angekuwa ameshavua nguo akifikiri huo ni mwaliko, ila mimi nilikuwa na akili bwana.
Haya yote yalikuwa majaribio ya huyu mwanamke ili kuona akili yangu inatik-tok sehemu gani zaidi, nami nikaacha kumwangalia na kuchukua tu simu yangu. Nilijitahidi kuukazia msuli ulale upande mmoja ili asije kuona kwamba alichokuwa amefanya kilinisisimua, maana ni boksa laini tu ndiyo iliyokuwa mwilini bado, naye akawa ameingia mule bafuni kuoga.
Alipokuja kutoka, alikuwa amejifunika kwa taulo fupi kutokea kifuani, na alikuwa amezivalisha nywele zake kimfuko fulani cha kuzuia zisiguswe na maji, naye akasema naweza kwenda kuoga sasa. Alikuwa kama ameshapotezea kile alichotoka kufanya muda mfupi nyuma, nami kweli nikaelekea bafuni kuoga.
Damu ilikuwa inakimbia kweli shauri ya njaa, nami nikawa nimemaliza na kujikausha maji kwa taulo nyingine, kisha nikajifunga hiyo hiyo kiunoni na kutoka. Nikakuta kukiwa na mtu mwingine ndani hapo, mwanamke mhudumu wa vyakula hotelini, ambaye alikuwa ameleta vyakula vya ukweli na chai za chocolate kama vile bado ilikuwa asubuhi.
Wakati huu Bertha alikuwa amekaa kitandani akiwa amevaa nguo ya taulo iliyoufunika mwili wake wote, na nywele zake kuziachia, na mhudumu huyo alikuwa amesimama pembeni yake akiwa ameshika kifaa cha kielektroni cha kupokea pesa. Yaani, Bertha akawa amempa kadi yake ya benki, na huyu mhudumu akaipachika tu hapo kwenye hicho kifaa ili kivute hela ya malipo kwa ajili ya chakula. Mambo hayo!
Huyo mhudumu aliponiona nakuja upande wao nikiwa kifua wazi, akaendelea tu kuniangalia, nami nikamsalimia. Akaitikia vizuri, nami nikafika hapo kitandani na kukaa upande mwingine karibu na pale chakula kilipowekwa.
Nikiwa najali zaidi hamsini zangu, nikashtuka kiasi baada ya Bertha kufoka kwa sauti ya juu, akiwa amempigia kelele huyo mhudumu kuwa aache kuzubaa na akaendelee na kazi zake. Nikawaangalia wote na kukuta huyo mhudumu akiwa ameanza kusukuma katoroli kake ka kubebea vyakula huku akiniangalia mara kwa mara, naye Bertha akasonya. Dah!
Inaonekana dada wa watu alikuwa amezubaa kuniangalia mpaka Bertha ndiyo akampigia huo mwano, nami nikaendelea kumtazama tu mpaka alipoondoka masikini. Nikamwangalia Bertha, ambaye alikuwa akinitazama kwa macho yenye kukerwa, nami nikacheka kidogo kwa pumzi na kuangalia pembeni.
Haikuwa muda mrefu baada ya hapo nasi tukaanza kula kwa pamoja. Ugali mzuri, nyama hizo, mboga mchanganyiko zilizokaangwa, soseji, chai ya kupashia matumbo mwanzoni, pamoja na maji ya kunywa. Nilifikiri huyu mwanamke alishindia madawa tu lakini kumbe alijua nini maana ya mlo pia.
Hatukusemeshana kwa lolote tena mpaka tuliposhiba kabisa, ndiyo nikampa shukrani na kuanza kuvaa nguo zangu nilizokuja nazo jana. Akawa bize tu na simu yake, akiwa hajamuulizia Dotto tena, nami nikaweka vifaa vyangu begini na kulibeba, kisha ndiyo nikamuuliza ikiwa kuna jambo lolote alitaka nifanye kuhusiana na zile ishu zetu; nikiwa hasa namaanisha kutengeneza madawa mengine.
Alichoniambia ikawa 'nenda tu, nitakwambia,' nami huyoo nikageuka zangu na kunyoosha njia. Hata hakuwa akinilipa! Ila siyo mbaya, maana nilikuwa nimeshajazwa matumaini ya kuja kumtoza malipo makubwa sana kwa kukomesha maovu yake, na angelipia bila kupenda.
★★
Ilinichukua masaa karibia matatu kabisa kutokea huko kwa madam Bertha mpaka kuja kufika kwa Ankia. Nilipoondoka hotelini pale, nilichukua usafiri wa bodaboda mpaka kwenye kituo cha mabasi ya mwendokasi ili nielekee Muhimbili kwanza.
Nilikuwa na lengo la kwenda kurudisha vifaa nilivyochukua hospitali pamoja na kumwona Latifah, lakini pia, nilitaka tu kuonana na daktari Roshan ili nizungumze naye kwa machache. Hayo machache yalikwenda kwa jina la Mariam. Nilitaka nimweleze kwa ufupi kuhusu maendeleo ya binti ili anipe mawazo zaidi juu ya mambo ambayo ningeweza kuboresha katika zoezi langu la kumsaidia binti, nami nilitekeleza hilo baada ya kufika hospitalini hapo.
Latifah ndiye aliyekuwa mlaji wa muda wangu zaidi maana hakuishiwa maneno na malalamiko kuhusu mimi kumweka pembeni sana, na alifanya kunikutanisha na watu wengine tuliofanya nao kazi hospitalini hapo ili tu niendelee kukaa pamoja nao kwa muda mrefu.
Ila Tesha kunipigia na kuniuliza kama ningeenda kwao leo ndiyo iliyokuwa njia yangu ya kumtoroka mwanamke huyo, nikiitumia kama dharura fulani iliyonihitaji kuwahi kuondoka. Nikamwambia rafiki yangu kwamba ndiyo nilikuwa njiani kurudi Mbagala, naye akasema sawa. Latifah alikuwa anajua kung'ang'ania mtu wewe, siyo poa!
Ndiyo nikafanikiwa kumkimbia baada ya kumwachia vifaa vile, nami nikaenda kupanda daladala pale Kariakoo zilizoandikwa Gerezani mpaka Mbagala. Na aisee! Sikutaka tena kuja kurudia kupanda hizo daladala, yaani mshono ni mshono, watu tulikuwa tumebanana haswa mpaka kupumua ilikuwa ni mateso. Sijui shida ilikuwa ni nini tu, yaani gari zinakuja watu wamejaa kinoma, na hapo ni jioni ya mapema tu, sikupata picha usiku hiyo biashara ilikuwa vipi! Na hii ilikuwa ni mara ya pili kuzipanda.
Kwa hiyo baada ya kuwa nimefika kwake Ankia, mida ya saa kumi na nusu hivi jioni, nilimkuta akiwa pamoja na wale marafiki zake wawili vijana, wale wavaa pini puani kama yeye pia, nami nikapokelewa kwa salamu nzuri na kuzirudisha, kisha nikaenda zangu chumbani. Ankia alikuwa amenimiss huyo! Akaja chumbani nilipokuwa nimeanza kutoa nguo mwilini, naye bado akawa analalamika kuhusu mimi kuikosa pilau yake jana.
Nikalikamata kiuno na kuanza kulipiga denda laini, na kidogo tu nilikuwa nimeshaamka maana nilikuwa na hamu kweli, hasa baada ya madam kunianzishia uchokozi wake usiokuwa na maana kule hotelini, lakini nisingeweza kwenda na Ankia mazima kwa wakati huu. Alikuwa na wageni, halafu bado alikuwa "mgonjwa," kwa hiyo mbio hiyo ya dendani ikaishia midomoni tu.
Lilikuwa limelegea kweli, likiniangalia kwa hamu pia, nami nikamwambia asiwaze; akipika msosi mzuri tena kwa ajili yangu tutakula pamoja, yaani mimi na yeye tu.
Nikamwambia kwamba nilihisi uchovu kiasi maana nilitokea hospitalini kutimiza wajibu fulani, ila na sasa nilitaka kuvaa ili kwenda kumwona Mariam pia. Ndiyo akawa ameniambia kwamba alikuwa amekuja chumbani humu ili kuwaumiza mioyo hao rafiki zake, akisema eti wote walikuwa wananitaka. Nikamwambia amefanya jambo la maana, naye akacheka kidogo na kisha ndiyo akatoka ndani hapo.
Kweli bado nilikuwa nikijihisi mzito mzito, kama vile nilitakiwa kuendelea kulala, na kukiangalia kitanda kulinifanya nitamani kweli kukirukia ili nijisinzishe kidogo, lakini nisingeweza kuvunja ahadi yangu ya kwenda kumwona Mariam. Na nilikuwa nawaza kuhusu dada yake pia, ikiwa alikuwa amewaambia mama zake labda kuhusu jinsi nilivyomkana jioni ya jana, ila ndiyo ningetakiwa kwenda huko na kujua.
Nikatia viwalo vingine safi mwilini, kisha nikatoka hapo tena na kuwapita wanawake wakiendelea kukaa pamoja. Akili yote ilikuwa kwa Mariam wakati huu. Nikafika hapo kwao, nami nikaelekea mpaka ndani na kupiga hodi mlangoni. Aliyekuja kunifungulia mlango hakuwa mwingine ila binti Mariam mwenyewe, naye akanikaribisha kwa tabasamu la furaha na kunikumbatia.
Nikaingia ndani hapo huku bado akiwa amenikumbatia, na ndiyo nikawakuta wenyeji wangu wengine wakiwa wamekaa kwenye masofa na wakiniangalia kwa furaha. Warembo wangu wawili walikuwepo, Tesha, pamoja na Shadya pia, nami nikasalimiana nao na kuanza mazungumzo yenye kufurahisha pamoja nao wote. Walikuwa wamenikosa tokea jana, hasa Mariam, ambaye hakutaka kuniachia yaani mpaka nikahisi aibu.
Kwa hiyo nikakaa naye sofani, nami nikamwambia nimekuja sasa na kama kawaida, leo pia tungechora. Akafurahi sana na kwenda chumbani upesi kama mshale, ili akalete vifaa vya kuandikia. Tesha akasema yaani dogo alikuwa kama hana amani kutoniona leo, ila kufika kwangu ndiyo kukamrudishia furaha yake, nami nikamwambia huo ni uhakika. Nikawa nimeulizia hali yake Bi Jamila na kujua kwamba aliendelea vizuri zaidi wakati huu, akiwa alipata dawa za kutumia walipokwenda hospitali jana na Miryam kuangalia afya yake.
Angalau sasa nikawa nimehakikisha kwamba hali ilikuwa shwari kwa upande wa familia nzima ya bibie Miryam kunielekea, kitu ambacho kilionyesha kwamba hakuwa amenitibulia kwa lolote. Ila kuongea naye bado lingekuwa jambo la lazima; kwanza nimweleweshe kuhusu suala la jana, halafu nimwambie ukweli wote wa matendo ya Joshua ambayo yangekuja kuivuruga amani hii niliyoikuta hapa.
Najua angenielewa tu, kwa sababu aliipenda familia yake, kwa hiyo ningepaswa kumsubiri bibie afike ili nisahihishe mambo. Kila kitu kingekuwa sawa.
★★
Mambo yakaendelea kuwa mazuri tu sehemu hii baada ya masaa machache kupita mpaka kufikia saa mbili usiku. Nilikuwa nimefanya michezo ya uchoraji wa herufi pamoja na Mariam, yaani kuzichora alfabeti na kuzipamba kwa rangi zake binti pia.
Nilikuwa namwelekeza apangilie herufi kadha wa kadha kwa mtiririko hususa ili kutokeza maneno kama "MY NAME IS MARIAM," "MY BROTHER IS TESHA," na mengine mengi kwenye karatasi nyingi, kisha mimi na Tesha tungemsaidia kuyatamka kwa kusoma pamoja naye. Alifurahia sana huyu binti na kuwaonyesha mama zake kila mara, nao wangempongeza sana.
Shadya alikuwa amekwishaondoka kwenda kwake kwenye mida ya saa kumi na mbili, kwa kuwa kipindi hiki tayari mume wake alikuwa amesharudi kutoka safari. Alikuwa hapa leo kwa ajili ya kupangana na mama wakubwa na hata Tesha pia kuhusu kufanya sherehe ndogo ya siku yake Bi Zawadi ya kuzaliwa, iliyokuwa ikikaribia kufika, na walikuwa wamepanga ije kufanyiwa hapa hapa nyumbani maana eti mama wakubwa walikuwa wazito mno kwenda kumbini.
Walikuwa wameshaanza kupanga bajeti, nani aje, nani asije, na katika watu wa kuja mmoja wao alikuwa yule Dina tuliyeenda kumtembelea siku fulani ya juzi pamoja na Tesha. Kijana ndiyo akawa ameniambia sasa kwamba alikuwa amewasiliana na Dina leo leo, na mdada huyo alisema eti alikuwa ameumia baada ya mimi kutotimiza ahadi ya kwenda pale kwake kumtembelea tena.
Tesha akasema inaonekana Dina alikuwa amenielewa sana, lakini hata alipomjaribu kumpa namba zangu, alikataa, mwanadada huyo akiona hiyo kuwa siyo busara, ama labda tu aliogopa. Nikamwambia Tesha inaonekana huyo Dina alikuwa na usawaziko mzuri wa kiakili, nami nikasema tungepanga kwenda kumtembelea siku nyingine tena.
Basi, tukiwa tunaendelea kufurahia wakati huu kwa pamoja hapo sebuleni, honi ya gari nje ya geti la nyumba hii ikaashiria kuwa mkurugenzi alikuwa amefika. Tesha akanyanyuka na kwenda nje ili amfungulie dada yake, nami nikawa najiandaa kwa yale ambayo yangefuata nikionana na Miryam tena.
Kale ka hisia ka msisimko wa hofu kiasi kalikuwepo, siyo hofu ya woga bali ya kutarajia mengi mno. Sikujua mwanamke huyo angenitendea vipi baada ya kile kilichotokea baina yangu, yeye, na Bertha ile jana jioni, na ndiyo nikawa nasubiri kuona. Sijui ingekuwa vipi endapo kama angefika na gia ya kwanza kuingiza ikawa kunifukuza!
Baada ya gari kuingia na geti kufungwa, bibie Miryam akawa wa kwanza kuingia ndani, kisha Tesha akafuata nyuma yake. Mwanamke huyo alikuwa amevalia shati jeupe la kike lenye mikono mirefu lakini iliyokunjwa mpaka usawa wa viwiko, pamoja na suruali nyeusi ya kitambaa iliyokuwa imembana kiasi usawa wa hips zake na kuchanua kwa upana zaidi kufikia miguuni. Nywele zake ndefu za kusukwa alikuwa amezilaza upande wa mbele kwenye bega la kushoto, na mkononi alishikilia mkoba mweusi.
Alipokuwa ameingia tu na kuniona, nilitambua upesi sana kwamba hakufurahishwa na uwepo wangu hapo kwa sababu hakunitazama tena na kuelekeza fikira zake kwa wengine hapo sebuleni. Akakaa kwenye sofa pamoja na Mariam, huku akizungumza na mama zake wakubwa kuhusu masuala ya hapa na pale yaliyokuwa yametokea kwa muda aliokuwa kazini. Tesha alikuwa amepeleka mifuko fulani jikoni, bila shaka Miryam akiwa ndiyo amekuja nayo, kisha akarudi na kukaa karibu nami tena.
Mariam akafata karatasi moja aliloandikia na kwenda kumwonyesha dada yake, naye Miryam akatabasamu kiasi. Akamuuliza ikiwa aliandika yeye mwenyewe, na Mariam akatikisa kichwa kukubali. Miryam akamwomba ayaseme maneno hayo kwa sauti, naye Mariam akayatamka vizuri sana. "I LOVE YOU MIRYAM." Sisi wengine tukacheka kidogo, na nilikuwa nimemkaririsha kwelikweli hayo maneno, naye Miryam akaonekana kufurahi sana.
Bi Zawadi alipoanza kumzungumzia Mariam kwa kugusia namna ambavyo nilichangia kumfanya achangamke namna hiyo, Miryam hakuniangalia, wala kunisemesha hata kidogo, akikwepa kuendeleza mazungumzo kwenye mada ambazo ningehusika zaidi. Alikuwa na hasira mimi, na ilieleweka kwa nini. Nikaona nitulie kimya tu mpaka Tesha akauliza kwa nini sikuwa nikiongea, na ndiyo nikawa nimemtazama Miryam. Nikakuta akiwa ameniangalia, kisha akaacha na kumtazama Mariam tu.
Ah, hii hali sikuipenda kabisa, na kwa sababu haikutakiwa kuendelea kuwa namna hiyo, ningepaswa niongee na huyu dada. Ningepaswa nimweleweshe. Miryam alikuwa mstaarabu na mwelewa kwa hiyo najua angenisikiliza na kuelewa maana ya yale niliyoyafanya jana. Haingekuwa busara kumwacha anikasirikie na kujenga kitu kama uadui wakati bado mdogo wake alinihitaji, kwa hiyo ningetakiwa kuongea naye; sasa hivi.
Baada ya Tesha kuniuliza kwa nini nilikuwa kimya tu, sikutoa jibu lolote kutokana na kuwa ndani ya fikira zilizozama kwa dada yake, naye akanishika mkononi na kusema, "JC? Vipi bro, mbona umezubaa?"
"Uko sawa JC?" Bi Jamila akaniuliza pia.
"Ndiyo, niko sawa," nikajibu hivyo kwa utulivu.
Wengine wakawa kama wameelekeza umakini wao kwangu, isipokuwa Miryam tu, aliyekuwa anapekua mkoba wake kutafuta nini sijui.
"Miryam..." nikamwita.
Mkono wake ukakatisha kutafuta alichokuwa anasaka mkobani, na macho yake mazuri yakapanda taratibu kunitazama usoni.
"Naomba kuongea na wewe... tafadhali..." nikamwambia hivyo.
Akaendelea kuniangalia kwa umakini, na Mariam akamwangalia pia kwa njia makini. Hata binti alionekana kuelewa kwamba kulikuwa na jambo zito, siyo mama wakubwa na Tesha pekee tu walioonekana kuhisi hilo kutokana na jinsi ambavyo wao pia walimwangalia Miryam.
Sikuhitaji mwanamke huyo anipe jibu. Nikanyanyuka tu kutoka sofani na kuuelekea mlango, nami nikatoka hapo na kwenda kibarazani. Nilielewa kwamba bila shaka niliwaacha wengine pale ndani wanajiuliza tatizo lilikuwa nini, ila lilikuwa langu na Miryam pekee kutambua na kutatua.
Sekunde tatu tu na mwanamke huyo akawa amekuja nje pia, naye akasimama umbali mfupi kutoka pale nilipokuwa nimesimama.
"Kuna mambo mengi sana ambayo nataka.... nashindwa kujua nianzie wapi yaani..." nikaanza kwa kumwambia hivyo.
Akawa ananitazama tu machoni kwa umakini.
"Miryam... kwanza... kile ambacho kimetokea jana najua hukukielewa vizuri, kwa hiyo..."
"Nilielewa vizuri sana," akanikatisha kwa kusema hivyo.
Nikatulia kidogo na kumuuliza, "Ulielewaje?"
"Mimi na wewe hatufahamiani," akasema hivyo.
Nikaishiwa pozi kiasi. Lakini nikamwambia, "Haiko kama unavyofikiria. Pale yaani... yale mazingira hayakuwa mazuri, sikutaka wale watu wakufahamu kwa sababu...." nikashindwa kuendelea.
Akasogea karibu zaidi na mimi, naye akasema, "Unakuwa mtu mwingine kabisa mbele yetu halafu unapokuwa na watu wako unabadilika, si ndiyo? Sasa nitakwambia kitu fulani. Sijali kuhusu nani unakutana naye, na sijui ni nini unafanya, lakini kuanzia wakati huu sitaki tena ujihusishe kwa lolote lile linalohusu familia yangu. Umenielewa?"
Alinifanya nibaki nikimtazama kwa mshangao mzito bila hata kuachama mdomo na kukodoa macho. Aliongea kwa sauti ya chini lakini ilipiga roho ya masikio yangu mpaka kufikia hisia kwa kishindo chenye nguvu sana, naye akaashiria kutaka kurudi ndani tena.
Nikamwambia, "Miryam, subiri. Unamaanisha nini?"
Akaniangalia na kusema, "Sitaki tena uwe karibu na mdogo wangu!"
"Kwa nini?"
"Ahah... "kwa nini?""
"Miryam haujui sababu iliyonifanya nikatenda kama vile jana..."
"Na sijali. Nimekwambia sitaki tena u..."
"Miryam, em' kwanza... tulia. Sawa? Huo uamuzi unaufanya kwa sababu tu ya hasira, hauoni utam-cost mdogo wako?"
Akaniangalia kwa macho makali na kunisogelea karibu zaidi, naye akasema, "Kwani nilikuomba huo msaada wako?"
Nikatulia kidogo, ikiwa imechoma hiyo, nami nikamwambia, "Ndiyo, hukuniomba. Nilijitolea mwenyewe, kwa sababu ninataka kumsaidia Mariam... apone. Haya mambo mengine hayahusiani naye."
"Lakini si ni mambo yako? Kwa hiyo nini... ukiwa hapa unajifanya daktari mwema, unajali, halafu ukiwa na watu wako ndiyo hatujuani? Ya nini uendelee kumzunguka mdogo wangu ikiwa hata na yeye unaweza ukamkana mbele ya watu kwamba humjui?" akaniambia hivyo kwa hisia kali kiasi.
"Miryam hapana, hiyo siyo maana ya kile nilichokifanya jana," nikamwambia hivyo kwa sauti yenye hisia.
Akabaki kuniangalia tu kwa mkazo.
"Wale siyo watu wazuri Miryam. Ndiyo waliosababisha kifo cha Joy, na mimi niko nao ili nije kusaidia kuwakamatisha... wakalipie kwa maovu wanayofanya..."
"Kwa hiyo na we' umekuwa askari sasa hivi?" akanikatisha.
"Hapana, ila ninafanya kazi na maaskari," nikamwambia hivyo.
"Ahah... unbelievable. Yaani unaweza kusema chochote, na kufanya chochote ili kudanganya tu. Uko hapa, unamsaidia mdogo wangu, sijui ili uthibitishe kwamba wewe ni mtu mzuri wakati siyo! Sitaki tena... we' kaka... sitaki tena ujihusishe na Mamu. Hiyo influence yako... na mashirikiano uliyonayo na hayo makundi yafanyie huko huko, sitaki tujuane tena kama ulivyokataa kunijua. Unafikiri nitakuwa na amani kujua unafanya mambo hatari wakati uko na mdogo wangu? Ili na yeye aje apelekwe kwenye hizo biashara zenu za kusagana?"
"Miryam..." nikamwita kwa upole.
Akanyanyua kidole chake na kusema, "Uliyoyafanya kwa ajili ya Mamu yanatosha. Kama kukushukuru nimeshakushukuru, kwa hiyo nakuomba... utajua mwenyewe namna ya kuwaelezea hawa wengine lakini nakuomba uache... mazoea na familia yangu."
"Yaani Miryam kweli... unaongea haya yote kama vile hunijui?"
"Ninajua nini kuhusu wewe kwani? Zaidi ya kwamba ikiwa sitachukua hatua haraka basi utasababisha matatizo kwenye familia yangu?"
"Mimi? Mimi niwasababishie matatizo? Siyo mimi nitakayewaletea shida Miryam, ila usipoangalia, ni wewe mwenyewe ndiye utakayefanya familia yako ianguke," nikamwambia hivyo.
Akakaza sura yake na kuuliza, "Unasemaje?"
"Usiwaze kuhusu mimi kuwa mbaya kwako kwa sababu hujui hata kwa kile nilichokifanya jana, nilikifanya ili kukulinda. Siwezi kuwatakia nyie mabaya hata kidogo. Ila huyo Joshua wa sasa siye mtu unayemdhania Miryam. Bado ana lengo la kuwaharibu nyie kama familia... na atafanya kitu kibaya tena kwa Mariam ili achukue shamba lake," nikamwambia hivyo.
Akawa ananitazama kwa hisia kali kiasi, naye akauliza, "Umemaliza?"
"Sikutanii Miryam. Nina uhakika na ninachosema. Kaka yako siyo mtu, hana uthamini wa familia, anajali tumbo na koo lake tu. Mtu anaweza kubadili matendo lakini kubadili utu huwa ni ngumu, na utu wa Joshua umeshaharibu mpaka dhamiri yake kiasi kwamba hawezi akabadili matendo yake tena. Anachofanya ni maigizo tu. Nafikiri hayo yote unayajua Miryam, lakini sidhani kama unajua kwamba ni yeye ndiyo alipanga Mariam agongwe na gari siku ile nimemwokoa... hiyo ilipofeli ndiyo akaja hapo getini na zile paper, na alipofeli tena ndiyo sasa hivi ameona aje kivingine. Unaona? Anataka kufanya Mamu atoweke Miryam, na usipoangalia... atatoweka kweli. Ni yeye ndiyo unapaswa kujihadhari naye Miryam... siyo mimi," nikamweleza hayo kwa hisia.
Akawa ananitazama kwa umakini tu, naye akasema tena, "Umemaliza?"
Nikabaki nikimwangalia kwa utulivu.
"Wewe ni mwongo sana. Sawa? Nakwambia leo... wewe ni mwongo, halafu mnafiki," akaniambia hivyo.
Dah!
Nikaendelea kumwangalia kwa macho yenye umakini.
"Unajua kila mara ambayo nilikuwa najitahidi kuona kwamba labda nilikujaji vibaya mwanzoni... umerudi tena kunithibitishia kwamba nilikuwa nakosea. Wewe ndiyo mwongo. Unaweza mpaka kudanganya mtu kwamba uko karibu kufa ili tu upate lifti, unashindwa vipi kudanganya kuhusu matendo ya mtu mwingine ambaye hata humfahamu?" akaniambia hivyo.
"Ahh... God!" nikasema hivyo kwa sauti ya chini huku nikitikisa kichwa kwa kutoamini jinsi ambavyo jambo hili lilizidi kwenda upande mbaya tu.
"Unadanganya kwamba Joshua alitaka kumgonga Mariam kwa gari, ulimwona? Oh, kama una ushahidi utoe. Utaniaminishaje? Kwa kuanza kukohoa na kusema unaumwa kifua, au?" akaniuliza hivyo.
Nikamwangalia kwa mkazo kiasi na kusema, "Kwa hiyo kumbe bado tuko kule kule tu? Mpaka leo bado hujanielewa vizuri kiasi kwamba unatumia hicho kisa nilichokifanya mara ya kwanza tumekutana ili kufumbia macho mambo mazito ya wakati huu? Ningekuwa nataka kuwaletea matatizo ningemsaidia mdogo wako?"
"Kwa hiyo nini... unanisimangia Mamu? Kwamba niamini kila kitu unachosema kwa sababu unamsaidia mdogo wangu bila kulipwa, si ndiyo?" akaniuliza hivyo kwa hisia kali.
"Okay Miryam, sijamaanisha hivyo unavyofikiria... no," nikamwambia hivyo kwa ukali kiasi.
Hisia zilikuwa zimeanza kupanda!
"Sikukuomba umsaidie Mamu, ulikuja mwenyewe kwangu. Ukitaka kuacha, acha... na sitaki tena uendelee. Acha niibebe familia yangu mwenyewe, haikuhusu kwa lolote," akanisemesha hivyo kwa sauti ya juu kiasi.
Inaonekana sauti yake ilisikika mpaka pale ndani, kwa kuwa mlango ulifunguka na wa kwanza kutoka akawa ni Tesha.
"Hakuna anayekuzuia Miryam, lakini hata wewe ni mwanadamu. Hutabeba kila kitu peke yako, kuna vitu vingine vitakushinda na utahitaji msaada. Huwezi kuona kila kitu..."
"Nimesema uniache! Sihitaji msaada wako kwa lolote!" Miryam akanikatisha kwa ukali.
Tesha akawa amesimama nyuma yake, akionekana kushangaa, na mama zao wakubwa wakawa wamekuja nje pia na kusimama karibu na Miryam.
"Mimi... kuna tatizo gani?" Bi Zawadi akamuuliza hivyo.
"Nakuomba uondoke," Miryam akaniambia hivyo.
"Da' Mimi... JC kaka, ishu ni nini?" Tesha akauliza hivyo.
Nikasema, "Miryam nakuomba utulize akili... ili uone mambo kama...."
"Nimekwambia ondoka, ushauri wako siuhitaji. Mizigo yangu ni yangu kubeba, haikuhusu," Miryam akaniambia hivyo.
Nikamwambia, "Miryam, unavyofikiria siyo. Hicho kimeanza kuwa kiburi sasa...."
Miryam akanitandika kofi zito shavuni ghafla sana!
"Mimi!" Bi Zawadi akaita hivyo kwa mshangao.
Nilibaki nikiwa nimeinamishia uso wangu pembeni baada ya mwanamke huyu kunilabua namna hiyo, na kiliuma kweli! Ila maumivu ya hicho kibao kwangu mimi hayakuwa shavuni, bali moyoni. Mambo yalikwenda tofauti kabisa na matarajio yoyote niliyokuwa nayo.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments