SEHEMU YA 02.
MWAKA 2002-SUMBAWANGA.
Ni mwezi wa kwanza wa mwaka 2002 katika kijiji cha Kizwite mkoani Rukwa Wilayani Sumbawanga alifika mwanamke mmoja ambaye alijipatia umaarufu sana kwa watu wote wa kijiji hicho na vijiji vya pembeni , umaarufu wa mwanamke huyo ulitokana na kuwa na watoto wengi ambao walikuwa wamepishana kwa miaka michache sana kwa namna ambavyo walikuwa wakilingana kwa muonekano wa nje, lakini kubwa zaidi ni namna walivyokuwa na rangi zinazotofautiana ikidhihirisha baba zao kuwa tofauti tena wa makabila tofauti duniani.
Yaani kwa maneno marahisi kati ya watoto hao kuna waliokuwa na mchanganyiko wa Kiarabu , Kizungu , Kichina , kijapani na Kiafrika.
Kwa maelezo ya awali ya wanakijiji wanasema mwanamke huyo tokea afike hapo haikuwahi kujulikana alitokea wapi na kuhusu watoto aliokuwa nao aliwapata pata vipi au baba yake alikuwa ni nani haikujulikana , kitu pekee ambacho wanakijiji wa Kizwite walijua kuhusu mwanamke huyo ni jina lake lake tu ambalo lilifahamika kama Chakwe.
Wanakijiji wanaelezea kwa kusema kwamba Chakwe alionekana kama mwanamke ambaye alikuwa hana akili nzuri sana na walikuwa na makisio hata watoto aliokuwa nao walitokana na kubakwa , hayo yalikuwa ni makisio tu ya wanakijiji hao lakini ukweli wote alikuwa nao Chakwe mwenyewe lakini kutokana na hali yake ilivyokuwa haikuweza kufahamika moja kwa moja maisha ya nyuma ya Chakwe yalikuwa kuwaje mpaka akawa katika hali kama hio na alipelekea stori nyingi kumuhusu zikitungwa ndani ya kijiji hicho.
Chakwe mara baada ya kufika katika kijiji cha Kizwite hakujali kushangawa na watu bali alifuatishana na watoto wake huku na huko kujipatia chakula ,alikuwa na mbinu za kipekee sana katika kujipatia chakula, mbinu yake ya kwanza ilikuwa ni kuamua kwenda kukaa na watoto wake nje ya nyumba ambayo ameichagua kwa siku na mwenye nyumba asipowapa chakula basi Chakwe na watoto wake hawawezi kuondoka.
Mbinu ya Chakwe kukaa nje ya nyumba ya watu ilikuwa ikimsaidia sana , kwani watu wengi kutokana na ile hali ya kumnyanyapaa yeye na watoto wake ilibidi tu kuwapa chakula ili kuwaondosha katika eneo lao.
Mbinu yake nyingine ilikuwa ni ya kuiba , lakini mbinu hio haikumsaidia sana kukidhi mahitaji ya watoto wake wote kumi ambao alikuwa nao hivyo mbinu ambayo ilikuwa ikifanya kazi ni ile ya kupewa chakula.
Chakwe hakuwa na nyumba ya kuishi hivyo hakuweza kupika na mara nyingi sehemu ambayo waliishi ni sehemu ambayo alijenga yeye mwenyewe kama hema chini ya mti na kuishi na watoto wake.
Aliweza kujenga nyumba hio kwa kutumia turubai ambalo aliiba kwa mwanakijiji mmoja ambaye alikuwa akilitumia kufunikia matofali yake na hata mwanakijiji huyo alipokuja kugundua Chakwe ndio alieiba hakuwa na la kufanya zaidi ya kusamehe..
Baada ya wanakijiji kuona Chakwe alikuwa akiteseka na watoto wake ndipo wanakijiji hao wakiongozwa na mwenyekiti wao waliamua kumpatia Chakwe nyumba ambayo ilisemekana alikuwa akiishi mwanaume ambaye hakuwa na familia , lakini mwanaume huyo alifariki kwa kuwekewa sumu.
Nyumba ambayo Chakwe alipewa na wanakijiji hao ilikuwa mbali kidogo na makazi ya wanakijiji , yaani ilikuwa imejitenga kidogo lakini haikuwa mbali sana , ni nyumba ambayo ilikuwa karibu sana na barabara ikizungukwa na miti,baada ya Chakwe kupewa nyumba hio angalau sasa aliweza kupata sehemu ya kuwasitiri watoto wake.
Maisha ya Chakwe na watoto wake ambao hawakufahamika majina yaliendelea ndani ya kijiji cha Kizwite kwa miezi mitano kamili na baada ya hapo ndipo Chakwe na watoto wake walipokumbwa na janga la Asili ambalo lilimuua yeye mwenyewe na takribani watoto wake wote kasoro mmoja tu.
Ilikuwa ni mwezi wa masika yaani mwezi wa tano kwenda wa sita ndani ya kijiji hicho sasa usiku mmoja Chakwe akiwa amejisitiri na watoto wake ilipiga Radi ambayo haikuwa ya kawaida katika nyumba ambayo alikuwa akiishi Chakwe.
Kama ujuavyo Radi inavyotokea hupiga mara moja au mara mbili na kisha hupotea na kuacha madhara basi hicho ndio kilichotokea.
Sasa mara baada ya Radi ile kupiga , yaani zikiwa zimepita kama dakika mbili kilionekana kivuli kikifika katika maeneo ya nyumba ya Chakwe.
Alikuwa ni mtu lakini mtu huyo hakuonekana sura kutokana na mavazi yake ambayo alivaa yalikuwa ni mavazi flani kama ya kininja lakini hayakuwa ya kininja yalikuwa ni mithili ya mavazi ambayo kwa kingereza hufahamika kama Cloak, mavazi flani hivi kama majoho ya rangi nyeusi ambayo huunganishwa na kofia kama vile ni Sweta lakini Kofia flani hivi ambayo mtu akijifunika huwezi kuona sura yake.
Sasa kivuli cha mtu huyo kilionekana hivyo na kwa namna mtu huyo alivyoweza kutokezea katika eneo hilo haikujulikana ametokea upande upi lakini aliweza tu kuonekana akiwa amesimama pembeni ya nyumba ya Chakwe ambayo ilikuwa imeharibiwa na Radi.
Yule mtu mara baada ya kusimama kwa dakika kadhaa katika eneo hilo , akiwa anamulikwa na mwezi uliokuwa ukitoa mwanga hafifu alipiga hatua kusogea mbele na sasa hata kile alichovaa miguuni mwake kiliweza kuonekana , alikuwa amevalia aina flani ya buti ndefu za rangi nyeusi mithili ya zile za mvua lakini hizo zilikuwa ni za kubana miguu kiasi na kisigino kirefu.
Nyumba ile haikuwa imeharibika yote , upande mmoja ulikuwa umebomoka na mwingine ulikuwa umesimama na yule mtu aliingia upande ule uliosimama na ndani ya dakika chache tu baada ya kupotelea kwenye uharibifu ule wa nyumba aliweza tena kuonekana kutokana na mbalamwezi,
Katika mikono yake alionekana akiwa amebeba kitu na kwa maelezo ya shuhuda ambaye aliweza kuona kila kitu anasema kwamba mtu huyo alionekana kama amebeba mtoto, kwa mara ya kwanza hakuweza kujua kama ni mtoto lakini baada ya wanakijiji kuweza kufika katika nyumba hio ili kuangalia kama kuna aliebakia hai ndipo walipobaini Chakwe mwenyewe amekufa na maiti yake ilionekana pamoja na ya watoto tisa.
Shuhuda alieshuhudia kila kitu alikuwa ni mwanakijiji wa hapo hapo na anaendelea kusema kwamba baada ya yule mtu kutoka akiwa ameshikilia mtu palepale hakuweza kumuona tena , anasema ni kama vile alipotea mara baada ya yeye kupepesa macho.
Haikuwa mara ya kwanza kwa watu kufa kwa kupigwa na radi lakini tukio la Chakwe lilizua gumzo , moja ya sababu ambayo ilipelekea kuzua gumzo ni maelezo ya mzee Kabwela ambaye alishuhudia kila kitu , ukweli ni kwamba kwa stori yake hio alioelezea kuna ambao waliamini na kuna ambao hawakuamini ,walioamini waliamini kutokana na kutokuonekana kwa mwili wa kumi wa mtoto wa Chakwe mwenye asili ya kizungu na wale ambao hawakuamini ni kwasababu ya stori ya Kabwela ambayo ilikuwa ni ya kufikirika.
“Mimi siwezi kuamini kabisa , Mzee Kabwela ametupiga kamba labda alikuwa amelewa kama kawaida yake”
“Lakini hata kama hamumuamini kutokana na tabia yake , je vipi kuhusu kupotea kwa maiti nyingine?”
“Swali zuri Kizito, huenda mtoto hakulala na mama yake au alipona na kukimbia”
“Mimi naamini maneno yake , mambo mengi ya ajabu yalitokea ambayo yalikosa maelezo mpaka leo hii , naendelea kuamini kutokana na kwamba niliweza kuulizia katika kijiwe cha pombe ambacho Mzee Kabwela hupendelea kwenda na niliambiwa siku hio hakuweza kufika , hivyo moja kwa moja inaniaminisha kwamba siku hio hakulewa”
Yalikuwa ni malumbano ya vijana ambao walikuwa wakicheza Draft ndani ya kijiji hicho ambao walikuwa wakizungumzia tukio lililotokea juzi yake mara baada ya kukamilisha kumzika Chakwe na watoto wake.
Vifo vya watu kumi na moja wa kijiji hiko vilizua gumzo sio kwa wanakijiji tu lakini hadi kwa taifa mara baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari, huku maelezo ya Shuhuda Mzee Kabwela yakiamsha msisimko wa hali ya juu.
Ukweli ni kwamba kila watu waliokuwa wakiongelea tukio hilo na hata baadhi ya waandishi wa habari waliweza kufika katika kijiji hicho na kujaribu kuwahoji wananchi na habari walizoambiwa zilikuwa zikichanganya kidogo lakini kutokana na kutumia usomi wao kuna wengine ambao waliondoka kwa kuona maelezo ya wanakijiji hao hayakuwa na mantiki na kuna wengine waliweza kuamini kutokana na sifa kuu ya vijiji vingi vya Sumbawanga kwa kusifika na uchawi,
Hata wanakijiji wengine walienda mbali na kusema kwamba huenda hata radi hio ilikuwa ni ile ya kutengenezwa na walozi wakubwa wa kijiji hicho lakini hata hicyo hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja, hivyo jalada la tukio hilo likafungwa rasmi na tukio likasahaulika.
******
Hamza ambaye alikuwa kwenye gari alikuwa akikumbuka kwa uchache sana maisha ya utoto wake , yaani yeye na mama yake na ndugu zake , alikuwa akikumbuka kabisa alikuwa na wadogo zake wengi na walikuwa na maisha magumu sana , maisha ya kutanga tanga huku na huko wakimfuata mama yake, Hamza anakumbuka kabisa katika akili zake japo kwa uchache katika watoto wa mama yake yeye ndio aliekuwa mkubwa , ambaye kwa kiasi flani alikuwa akijitambua kutokana na kuwa wa kwanza , kumbukumbu zake nyingine ambazo alikuwa akikumbuka ni namna ambavyo aliweza kushuhudia namna wadogo zake walivyopoteza maisha mara baada ya kumulikwa na mwanga wa ajabu.
Hamza hakukumbuka kwa usahihi sana kuhusu maisha yake ya utoto lakini baadhi ya kumbukumbu ambazo zilikuwa ngumu aliweza kuzikumbuka, hakuwa akijua alikuwa na miaka mingapi katika kumbuukumbu zake za utoto akiwa na mama yake.
Baada ua janga la asili kumkumba Hamza na kusalimika maisha yake yaligeuka na kuwa msururu wa matukio ya kusisimua sana , huku mtu anaefahamika kwa jina la Mzee akichukua nafasi kubwa katika msururu wa matukio hayo.
******
Hamza hakuwa akishukia kituo cha karibu na chuoni kwake, ni utaratibu aliokuwa amejijengea , alipenda kuchangamsha mwili wake kwa kutembea umbali mrefu kidogo
Sasa mara baada ya kushuka wakati akiwa anatembea kando ya barabara akipishana na watu wengi ambao walikuwa katika harakati za maisha palepale alijikuta akiitwa kwa nyuma na sauti ambayo alikuwa akiitambua .
Nyuma ya Hamza alionekana kijana wa rika lake aliekuwa amevalia suruali ya kitambaa nyeusi , shati la rangi ya mikono mirefu jeupe na moka ya rangi ya kahawia , alikuwa amependeza kwa namna ambavyo alikuwa amechomekea ukijumlisha na mwonekano wake kwa ujumla , alikuwa na kila sababu ya kuitwa mwanaume mtanashati au Handsome , kama utamfananisha na Hamza basi moja kwa moja kijana huyo angeshinda upande wa nanmna mavazi yake yalivyo lakini katika upande wa sura ilioumbwa vyema Hamza alikuwa akichukua nafasi kubwa.
Hamza alikuwa na mchanganyiko wa rangi na kwa kumuangalia tu kwa haraka haraka lazima ungejua ni mchanganyiki wa mzungu na mwafirka, kinachomfanya Hamza kutoonekana wa kuvutia ni namna ambavyo anajiweka , alikuwa akivaa kawaida sana pengine kuliko mwanafunzi yoyote wa chuo cha FEMU na hilo lilimfanya kuonekana wa kawaida sana macho ya watu wengi.
“Muuza vyungu mwenyewe nakuona kama kawaida yako”Aliongea Hamza huku akiuonyesha tabasamu kwa rafiki yake afahamikae kwa jina la Alex..
“Kwa namna ambavyo unataongea , ni kama kazi ninayofanya ni ya hali ya chini , lakiini ukawaida unaoniona nao leo ndio unatokana na kazi yangu”Aliongea na kumfanya Hamza kutoa tabasamu la uchungu na kuendelea kutembea.
“Imekuwaje leo hii ukatembea kwa miguu, nilitegemea muda kama huu upo njiani ukiwa umempa mtoto wa kike lift”
“Hahaha.. sio kila siku nampa mwanamke lift siku nyingine ni washikaji kama nyie , gari imezingua kuwaka asubuhi ya leo, nimekuja kwa lift kutoka kwa jirani yangu na aliniacha kule upande wa chini ndio maana nikaamua kutembea tu”Aliongea Alex na kumfanya Hamza kutingisha kichwa.
Baada ya kukaribia getini Alex aliungana na watu wengine waliokuwa wakimfahamu na kuingia huku wakiongea kwa kucheka lakini kwa upande wa Hamza alionekana kuwa na mawazo yake kichwani kwani hakujichanganya katika stori za watu hao ambazo mara nyingi zilihusisha wanawake.
Hamza alikuwa na muda mrefu kidogo tokea aanze kusoma ndani ya chuo hicho lakini mpaka kipindi hicho hakuwa amezoeana na watu wengi , pengine ni kutokana na hulka yake ya ukimya.
Licha ya Hamza kufahamiana na Alex ukaribu wao huwezi kusema ni ule wa kirafiki, ukweli ni kwamba Alex alikuwa ni mcheshi mno kiasi cha kuongea na kila moja na kucheka nae , alikuwa amezoeana karibia na darasa zima.
Umaarufu wa Alex ndani ya chuo hicho hutokana na biashara yake ya uuzaji wa vyungu vya aina mbalimbali , Alex alikuwa akihusika katika uuzaji wa vyungu vya kupikia , vyungu vya kuwekewa maua ambavyo vina urembo wa aina yake na bidhaa nyingine za aina hio na hili ndio ambalo lilimpatia umarufu kwani biashara yake ilikuwa sio ya kawaida na imekaa vibaya lakini ukweli ni kwamba ndio biashara ambayo ilimfanya Alex kuonekana mtu mwenye pesa na alikuwa akimiliki kabisa gari aina ya IST gari ambayo ilimpatia umaarufu na kufanya ashobokewe na wanawake wengi chuoni.
“Alex mambo?”Sauti nyororo iliweza kusikika nyuma ya vijana wa kiume wa chuo hicho cha FEMU akiwemo Hamza ambaye muda wote alionekana kuwa kimya akiwa sio mwenye kusikiliza stori za wenzake.
“Anitha..!!!”
Alex aliitikia kwa kubabaika kiasi huku kundi la wenzake likikaa kimya kumwangalia mrembo Anitha.
Alikuwa ni mwanadada mrembo mno , huenda ndio ambaye alikuwa akishika namba moja kwa uzuri ndani ya chuo chote cha FEMU ni mwanadada huyo huyo ambaye alimfanya Hamza kuwa maarufu ndani ya chuo cha FEMU.
“Niambie mamii ,, uko poa?”Aliongea Alex kwa mbwembwe huku akianza kulamba midomo yake na kusugua sugua mikono kiswaga na kumfanya Anita kutabasamu kiasi cha kupelekea mashavu yake kutengeneza vishimo.
“Niko poa”Alijibu Anitha huku akiangalia kundi la watu hao na ilishangaza kwamba licha ya wanaume waliokuwa wametangulizan na Alex kuwa wanadarasa lakini hakujihangaisha kusalimiana nao , lakini hata hivyo ni jambo la kueleweka.
Hakuna ambaye hakuwa akijua tabia ya maringo aliokuwa nayo Anitha ndani ya chuo hicho na ni kupitia maringo hayo ndio yaliomfanya Hamza kudhalilika na kujipatia umaarufu wa aina yake baada ya kukataliwa waziwazi.
Anitha alionekana kuwa na maongezi na Alex hivyo wale wengine kila mmoja alijiongeza na kupiga hatua za kuelekea darasani , isitoshe ni muda mfupi uliobaki mpaka kipindi kuanza.
*******
Shauku ni msingi wa kitabia ambao ni muhimu kwa binadamu kuwa nao ili kumuwezesha kujifunza na kukua.
Tukiwa na shauku inatupelekea kupata motisha ya kujifunza vitu vipya jambo ambalo linaweza kutupelekea kupata gunduzi za vitu vingine vipya ambavyo hatujawahi kuvifikiria.
Shauku ya muda mfupi inaweza kukupeleka kupata shauku ya muda mrefu na mwisho wa siku kujibu maswali uliokuwa ukijiuliza kwa muda mrefu, kwa mfano unaweza ukawa na shauku ya kumjua mtu kwasababu mtandaoni kaandika jambo ambalo ni fikirishi mwisho wa siku shauku yako inakupa motisha ya kutaka kuonana na huyo mtu na anakuelezea kwanini aliandika vile na katika maneno yake unajikuta unapata kitu kipya ambacho hujawahi kufikiria na shauku nyingine kuanza.
Ni muhimu kuwa na shauku inayoendana na vipaumbele vyetu ili tuweze kukua na kujifunza zaidi na zaidi na mwisho wa siku kuyafikia mafanikio.
Kumbuka kila kitu kilianza kama shauku na shauku ikaibua mawazo na hatimae ikaipelekea dunia kuwa kama inavyoonekana leo.
“Paaa.. Paaah”Wanafunzi walijikuta wakipiga makofi ya nguvu.
Alikuwa ni Profesa Issai Stephano a.k. a Mr Bonus point, alikuwa amepewa jina hilo la utani kutokana na mwishoni mwa kipindi chake lazima atoe ushauri nje ya somo lake kwa wanafunzi wake ambao mwenyewe anaita Bonus point na siku hio alikuwa akielezea kuhusu Shauku.
Ijapokuwa mara nyingi mwishoni mwa kipindi chake aliongea kama utani lakini maneno yake yalikuwa na maana kubwa kwa wale ambao walikuwa wakimchukulia siriasi.
Katika watu ambao walikuwa wakipenda kipindi chake kiishe na kuweza kusikiliza Bonus Point ni Hamza , alipenda sana kumsikiliza Profesa Stephano kwani maneno yake licha ya kuyaweka kimatani zaidi lakini alikuwa akifikisha ujumbe wenye maana nzito ambayo kwa mtu aliekuwa siriasi kwa kile anachoelezea basi pengine angepiga hatua kubwa katika ukuaji wa kifikra.
Hamza wakati wenzake wakitawanyika katika ukumbi kwa ajili ya kusubiria kipindi kingine , yeye alikuwa akifikiria neno Shauku , maneno ya Profesa Stephano ni kama yamegusa kile kinachoendelea katika maisha yake.
“Ili kutimiza shauku yako ya muda mrefu unapaswa kufanyia kazi shauku yako ya muda mfupi , pengine majibu utakayoyapata kwenye shauku yako ya muda mfupi ndio mlango wa kutimiza shauku yako ya muda mrefu”Maneno hayo yalijirudia rudia katika kichwa chake.
“Shauku yangu ya muda mfupi kwa sasa ni ipi?”Alijiuliza Hamza lakini alishindwa kujibu swali lake mara baada ya kuja kushituliwa na moja wapo ya rafiki yake wa karibu afahamikae kwa jina la Amiri au Pacha mdogo.
“Mzee unawaza nini tena , ushasahau mpango wetu wa jana?”Aliuliza Amiri mara baada ya kumsogelea Hamza.
“Hamna nilikuwa nayawazia maneno ya Profesa , yanaonekana kuwa na uhalisia”
“Hahaha… Profesa watu wanamchukulia kama mzee wa Komedi kwa aina yake ya ufundishaji lakini yule mzee ni mtu ambaye ana uzoefu wa mambo mengi, kuna tetesi ambazo nimesikia pia jamaa inasemekana ni jasusi mstaafu”Aliongea Amiri na kumfanya Hamza kumwangalia kwa mshangao.
“Unasema kweli?”
“Nimesema ni tetesi tu mzee , kama swali lako ni kuthibitisha hizo tetesi basi naweza kukujibu ndio, ni tetesi ambazo zinazungumzwa na watu wengi”Aliongea na kumfanya Hamza kutoa tabasamu la uchungu na aliona ameuliza swali la kijinga.
“Oya halafu mwana unaonekana kuwa na mawazo mengi ujue , vipi tunaenda au hatuendi?”Aliuliza Amiri mara baada ya kuona utayari mdogo wa Hamza.
“Tunaenda ili mradi tu malipo yawe ya uhakika”
“Haha.. hilo ondoa shaka ili mradi tu ufanye kazi kama ulivyosema maana bado hata siamini kama unaweza tengeneza”
“Siwezi kusema naweza halafu nikashindwa, ongoza njia tuondoke”Aliongea na Amiri alitabasamu na kisha walianza kutoka kwenye Hall 5 hiio kupitia mlango wa nyuma na kutoka.
Dakika chache mbele walitokea katika maegesho ya chuo ya muda mfupi na kusogelea gari aina ya Ford.
Ilikuwa ni gari ambayo anatumia Amiri ambayo ni ya kwake kabisa , Amiri hakuonekana mnyonge, ijapokuwa alikuwa akisoma chuo cha kawaida kama hicho lakini maisha yake yalikuwa ni yale ya juu lakini licha ya hivyo hakua akibagua watu wa kufanya nao urafiki.
Pengine kutokana na maisha yake ya juu angechagua marafiki wenye pesa kama yeye lakini ajabu alimchagua Hamza kama moja wapo ya marafiki zake ,
Kwa mara ya kwanza Hamza na Amiri kujenga urafiki wao ni siku ambayo Hamza alitokea kuweka wazi hisia zake mbele ya mrembo Anitha, Hamza anakumbuka siku kilichompelekea mpaka kuweka hisia zake wazi ni kutokana na kuamua kutumia Bonus Point zilizotolewa mwisho wa kipindi na Profesa Singano.
Pointi ambazo zilimpa ujasiri Hamza na kuomba kuongea na Anitha pembeni na kumweleza hisia zake kwamba anampenda na bla blah kibao lakini mwisho wa siku Hamza aliambulia kejeli na kusonywa tena mbele ya Kadamnasi ya wanafunzi wenzake , ilikuwa ni kama vile Anitha alimfanyia makusudi kwani licha ya kwamba alikuwa na uwezo wa kumjibu kistaarabu lakini mwisho wa siku akaamua kumjibu kwa sauti kubwa ili mradi tu kumdhalilisha huku akimwita Hamza mtu masikini ambaye hana hadhi kabisa ya kutoka na yeye kimapenzi na aende kutafuta wa hadhi yake.
Amiri ambaye alikuwa ni sehemu ya wanafunzi hakuchulia swala la Hamza kama la aibu bali alichukua katika upande wa Chanya na kumuona Hamza kama mtu jasiri hususani pale alipoweza kumsikia Hamza na yeye kiropoka mara baada ya kukataliwa na kumwambia Anitha:
“Anitha unaweza usinipende leo , lakini mimi ni mbishi kufa na siku moja wewe mwenyewe ndio utanifuata na kutaka mahusiano na mimi , ndio itakuwa wakati wangu wa kukukataa”Aliongea Hamza bila ya aibu na kisha akapangua watu na kuondoka.
……..
“Oya mzee sasa sikia , inshu niliokuambia jana ni complex kidogo lakini malipo yake ni ya kueleweka”
“Unamaanisha nini , si kufunga tu kwanini iwe Complex?”Aliuliza Hamza kwa mshangao kidogo.
“Ni kama nilivyokuambia Kamera ambazo unapaswa kufunga ni za siri sana na anaeishi hapaswi kujua”Aliongea na kumfanya sasa Hamza kuelewa anachotaka kumaanisha.
“Kwahio unamaanisha unataka nikusaidie kufunga spy Camera?”
“Ndio nilichokuwa nikimaanisha , najua tulikubaliana ni kufunga tu kamera lakini sijakuambia ni wapi na kwa ajili gani , ndio maana nikasema ni inshu Complex lakini ambayo ina malipo makubwa kama utafanikisha”
Kwa jinsi ambavyo Amiri alikuwa akiongea ilimfanya Hamza kuona pengine hamjui vizuri rafiki yake kwani ombi lake lilionekana kuwa na utata lakini ambalo limekaa kijasusi zaidi.
“Amiri kama ndio ulikuwa mpango wako najitoa , nina shida kweli ya pesa lakini vipi kuhusu usalama wangu , ninaweza kufanya kama unavyotaka lakini kama itagundulika ni mimi inaweza kuniletea matatizo”Aliongea Hamza.
Ukweli ni kwamba siku ya jana mchana Amiri alimuuliza Hamza kama alikuwa na ujuzi wowote wa kufunga CCTV Kamera amsaidie na Hamza alimjibu Amiri kwamba alikuwa na uwezo huo jibu ambalo lilimfurahisha sana Amiri na kumwambia kwamba kuna kazi anataka kumpatia na ina malipo mazuri kama tu atamsaidai katika jambo hilo.
Hamza alimwambia atamsaidia kwasababu ni rafiki yake lakini Amiri akagoma na kusema lazima amlipe na Hamza mara baada ya kuona Amiri analazimisha malipo hakutaka kukataa isitoshe alikuwa na shida ya pesa.
Sasa walikubaliana kesho yake ambayo ndio siku hio sasa , lakini ajabu ni kwamba Amiri anampatia Hamza maelezo tofauti na ya jana yake na kusema Kamera ambazo anapaswa kufunga ni Spy Camera , yaani sio kamera za ulinzi bali kamera za kiuchunguzi tena katika nyumba ya mtu, jambo hilo linamfanya Hamza kuona ni swala la hatari kwani inaweza ikabainika yeye ndio muhusika na kujiingiza matatizoni.
“Sikia Hamza najua ni kweli nimekuahidi malipo , lakini nimekuchagua kunisaidia hii kazi kwasababu wewe ni rafiki yangu , kuna kitu muhimu sana nataka kufatilia ili niweze kupata majibu ya wasiwasi wangu na shauku ya muda mrefu”
“Shauku gani na majibu gani?”Aliuliza.
“Ni stori ndefu rafiki yangu , lakini jua ni maswala ya kimapenzi ndio yananifanya niende mbali namna hii, nataka Kamera hizi zifungwe katika Apartment anayoishi demu wangu , kuna vitu ambavyo sivielewi kuhusu Mellisa ndio maana”Aliongea huku akianza kutia huruma kidogo.
“Kama nitakuwa sawa basi naweza kusema ni kwamba humuamini mpenzi wako , lakini sidhani kama kufunga Kamera sehemu anayoishi inaweza kukupa majibu ya kile unachokitaka , wenzako sehemu ambayo wanatakiwa kuweka umakini ni kwenye simu na sio mambo ya Kamera”
“Upo sahihi , lakini hayo unayoyasema ni kwamba nishayafanya tayari na ni mwaka sasa tokea nianze kumfatilia Mellisa kuhusu mawasiliano yake lakini sijawahi kuona kitu cha tofauti lakini bado hisia zangu zinaniambia Mellisa ananisaliti tena ananisaliti ndani ya nyumba ambayo nimempangishia mimi , Bro hebu nisaidie katika hili ni swala la dakika chache tu kulifanya na mimi lazima nikulipe” Aliongea na kumfanya Hamza kuanza kukuna kicha chake kwa namna flani alianza kumwelewa Amiri lakini bado kuna kitu hakipo sawa katika maelezo yake.
“Kama ni hivyo hisia zako zinakuambia nini na kwa nini ubahisi anakusaliti ndani ya nyumba uliompangishia , kuna viashiria vyovyote ambavyo umevipata?”
“Ni stori ndefu ambayo ina mlolongo wa matukio ambayo hata kama nitakuelezea hapa huwezi kunielewa bro , ila ninachojua ni kwamba Mellisa ananisaliti tena usaliti anaufanyia ndani ya Apartment niliompangia mimi , sina uhakika wa hisia zangu na hizo Kamera zitanipa majibu ya kile ninachotafuta , Bro nikipata ushahidi wa hisia zangu nitakuambia kila kitu kwasasa naomba unisaidie”
Amiri alimbembeleza Hamza kwa kila namna ili tu aweze kumsaidia na mwisho wa siku Hamza alikubali , isitoshe Amiri alikuwa amemsaidia katika mambo mengi sana ambayo yalihitaji pesa.
“Okey nitakusaidia katika hili lakini lazima tukubaliane jambo moja”
“Nipo tayari kukubaliana na chochote unachotaka , Hamza ili mradi tu unisaidie katika hili”Aliongea Amiri na kumfanya Hamza kutoa tabasamu la uchungu.
“Sikia nitakusaidia lakini sihitaji malipo ya aina yoyote ile”Aliongea na kumfanya Amiri kushangaa kidogo lakini alijikuta akilipukwa na furaha isiokuwa ya kawaida haikuwa furaha kwamba hatolipa bali ni furaha kwamba ataweza kufungiwa hizo Kamera maana Amiri hakuwa na shida ndogo ndogo za pesa.
Comments