MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA THELATHINI NA MBILI
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Nimekuja kuamka pakiwa pameshakucha zamani, lakini kwa hapa ingeknekana labda bado ni muda ule ule tu kutokana na jinsi ambavyo taa zilimulika sana humo ndani yaani muda wote, na kwa sababu fulani, mapazia hayakufunguliwa kuruhusu hewa na mwanga wa nje upenye ndani, ila viyoyozi maalumu vilitengeneza "fresh air."
Nikajitazama kuthibitisha, na ndiyo, bado nilikuwa kwenye sofa. Macho yalichomachoma kiasi, nami nikaanza kuyafikicha huku najinyanyua ili nikae. Mgeni nililala kwenye sofa ndani ya nyumba yenye vyumba kama vyote. Nilikuwa nahisi fukuto la ajabu mwilini, nikiwa nimetokwa jasho lenye kuchukiza, na nilihisi kichefuchefu ambacho kilikuwa kinavuruga kabisa kifua changu na kunitaka nitapike. Shauri ya kunywa bia nyingi jana halafu nikaja kuchanganya na ile whisky baadaye, asante sana Festo.
Ile tu ndiyo nimemwaza Festo, nikaanza kuangalia mazingira kwenye nyumba hiyo kutokea hapo nilipokuwa nimekaa, na macho yangu yakatulia sehemu ambayo ilikuwa ndiyo jikoni; jiko la wazi na pana lenye makolokolo kama yote ya kisasa na yaliyopangiliwa vizuri, kukiwa na mwanaume mfupi kiasi aliyekuwa amevalia kwa njia iliyoonyesha kwamba alikuwa mpishi. Tena wale "mashefu" wa kuajiriwa waliosomea upishi.
Jamaa alikuwa bize kwenye kaunta-sinki pana akiwa anakatakata nyama na maviungo-viungo mengine, akiwa anatengeneza vyakula fulani vilivyotoa aroma nzuri sana, nami nikaamua kuvuta simu yangu ili nitazame muda. Nilishangaa kukuta ni saa sita mchana, siku ya Ijumaa, na watu kama wote walikuwa wamenitafuta aidha kwa kunipigia ama kutuma ujumbe. Sikuamini kama nilikuwa nimepitisha usingizi mrefu namna hiyo, ila nadhani ni shauri ya kunywa sana jana huku nikiwa na uchovu mwilini.
Nikaona niweke simu pembeni ili kwanza nikashughulike na hiki kichefuchefu nilichokuwa nahisi, nami nikasimama na kuanza kwenda pale kwa Shefu. Alikuwa mweusi, mwenye sura makini sana ya mtu anayejua kubucha, nami nikamsalimia kistaarabu. Akaitikia vizuri, na kabla hata sijamuuliza, akasema kwamba "boss" alikuwa ameshaenda kazini, na alimwambia kwamba nikiamka nipate msosi mzuri kisha nikae kusubiri mtu ambaye angekuja kunichukua kutoka hapa ili ndiyo niondoke. Mh?
Nikamwambia asante, ila nilichokuwa nahitaji kwa sasa ni maji ya kunywa ya baridi sana, ndiyo akanionyesha friji ilipokuwa. Nikaenda hapo na kuchukua maji, nikibeba jagi kabisa, kisha nikarudi kwenye sofa kuchukua simu na kuanza kuelekea ngazini. Nikaenda mpaka kwenye chumba ambacho Festo alinielekeza ile usiku, kikiwa kipana na kisafi, cha wageni, na inaonekana hata kitanda hakikuwahi kuguswa na mtu yeyote yule.
Nikaweka simu pembeni na kuanza kunywa maji sasa. Shusha, shusha, shusha, kudadeki ikawa kama nimekiumua kichefuchefu maana ndiyo kikaongezeka sasa. Nikaliwahi bafu, nami nimeifikia tu ile siti ya choo cha kukaa nikainama kiasi na kuanza kuuondoa uchafu.
Nilijisikia vibaya sana, lakini nikaona niongeze maji tena kwenye mfumo wangu na kujitapisha kwa mara nyingine, kisha ndiyo nikapata ahueni. Uzuri kichwa hakikuuma, kwa hiyo nikavua nguo zangu na kuanza kujisafisha kabisa kimwili kwa kuoga na kuswaki. Nilitumia mswaki wa wageni humo ndani nikiombea Shefu asiwe amewahi kuutumia!
Baada ya hiyo pindi iliyoonekana kuwa nzito vibaya mno, nikakifata kitanda na kujitupia hapo ili nijisikilizie vizuri. Nikaona kuna kiyoyozi cha kielektroni juu ukutani, nami nikaamua kunyanyuka ili kwenda kukiwasha. Nikarudi kitandani tena nikiwa nimeichukua simu, na kaupepo kakiwa kananiliwaza ndiyo nikaamua kuzipitia sms sasa.
Kwanza waliokuwa wamenipigia walikuwa wengi yaani, lakini kwenye upande wa jumbe walinitumia wale waliokuwa na uvutano nami zaidi; wanawake. Ankia, Latifah, Soraya, Khadija, Ibtisam, Rukia, na wengine niliokuwa nafahamiana nao kitambo, wote walikuwa wameniachia sms, lakini baada ya kuona yule dada yake Joy aliyeitwa Adelina ametuma ujumbe pia, nikawa nimekumbuka kitu fulani. Leo ilikuwa Ijumaa. Aisee!
Nilimwahidi mwanamke huyo kwamba ningemsindikiza siku hii ikifika kwenda kule Nachingwea kuiunga mkono familia yake kwa ajili ya ujenzi wa kaburi la mdogo wake, na jumbe zake zilikuwa kadhaa kutokea asubuhi akiniuliza kama nitaenda, ikiwa niko bize au nimetingwa sana, mpaka kufikia saa tano ambayo akawa ametuma ujumbe kwamba yeye ameshakwenda na Mungu akipenda tungeonana. Dah, nilijisikia vibaya! Na alivyokuwa mstaarabu sasa!
Nikawa hadi nashindwa yaani, sijui nimtumie maneno gani, nami nikaangalia jumbe za Ankia kukuta naye ameniambia kuhusu hilo suala. Yeye mwenyewe alikuwa ameshasahau maana hakuwa amewasiliana na Adelina tena tokea ile siku ameenda pale kwake kumtembelea, ila ndiyo alipopigiwa simu asubuhi akajitahidi tu kujiandaa na kuondoa harufu za pombe, kwa hiyo sasa walikuwa pamoja kuelekea huko na rafiki yake. Alikuwa amenitafuta sana pia asubuhi kwa kupiga, lakini mimi ndiyo hivyo, sikuwa na habari.
Kwa hiyo nikaamua tu kumtumia ujumbe Adelina wa kumwomba samahani kwa kusema nilipatwa na hitilafu iliyosababisha nikashindwa kuijali hata simu, nami nikamwahidi kwamba tutayajenga zaidi wakishafika huko ama wakirudi.
Baada ya hapo, nikawapitia wengine pia, nikiona wazi namna ambavyo yule Khadija ndiyo alikuwa amenipigia mara nyingi zaidi, lakini hakukuwa na simu wala ujumbe wowote ule kutoka kwa madam Bertha. Sijui alikuwa amejichimbia wapi! Au alikuwa amenichunia? Nikaamua kumpigia. Mara mbili, kimya, ya tatu ndiyo akapokea. Akauliza nasemaje, nami nikamwambia nimemmiss. Nikasikia akisonya kidogo na kusema angenitafuta baadaye maana sasa hivi yuko bize, nami nikamwambia sawa.
Nikajikuta nacheka kidogo, kupata ile ahueni kwamba hakukuwa na noma kwa upande huo, nami nikaona sasa ndiyo ungekuwa muda mzuri kwenda kula maana kifua kilikuwa kimeanza kutulia na njaa ilikuwa inanikong'oli. Sikuwa nimekula tena tokea asubuhi ya jana nilipokula chapati mbili kwa Ankia. Sikusahau! Na labda ndiyo maana uchovu ulipita ule wa kawaida jana, na sasa nikawa nahisi mwili unarusha-rusha tu damu kwa ndani.
Nikavaa nguo zangu tena, na nilikuwa na uhitaji wa kubadili haya mavazi, hayakunukia ile "mimi" nzuri tena. Nikaenda pale sebuleni na kukuta Shefu akiwa amekaa kwenye kiti kirefu cha plastiki usawa wa ile bar ya vinywaji huku akitumia simu yake, na aliponiona akashuka na kusimama kwa 'attention,' ile ya mstalini. Nikamkaribia na kumwambia ajiachie tu, mimi sikuwa bosi wake, ila nilikuwa na njaa kali sana. Akasema nielekee upande wa meza ya chakula, kila kitu kilikuwa pale na yeye angenihudumia, nami nikafikicha viganja vyangu na kwenda upande huo.
Nikakaa kitini, meza ikiwa na vyombo kama hotpot, masahani, vijiko, chupa za chai, bakuli lenye matunda, naye Shefu akaja na kuanza kuniambia kuna hiki na kile, nichague nataka nini halafu anipakulie. Dah! Maisha hayo, tena kwa msoto wa kuuza madawa ya kulevya!
Mimi nilitaka kula kila kitu, kasoro maini tu, kwa hiyo nikamwambia aniwekee kila kitu kimoja kimoja, naye akafanya hivyo. Kwa hiyo ikawa ni hivi, half cake moja, kipande kimoja cha mkate msito, soseji moja, kipande cha nyama ya kuku, supu ya ngombe, na kipande kimoja kimoja cha matunda. Nilikula!
Shefu alikuwa amesimama pembeni, eti akitakiwa kusimama tu mpaka nimalize kula, nami nikamwambia aache ujinga na akae ili tule wote. Alikuwa anafata kile kitu wanaita protocol, utaratibu eti. Nikamwonyesha urafiki na kumfanya ajiachie pia, nasi tukawa tunakula huku tunapiga story.
Nikamweleza kwamba mimi ni rafiki ya bosi wake, na ndiyo nilikuwa nimekuja kumtembelea hiyo jana. Akasema aliambiwa hivyo pia na bosi wake, kwamba mimi ni mgeni wa muhimu sana kwa hiyo anitengenezee chakula kizuri na kunionyesha heshima, hivyo hakutegemea kwamba ningekuwa na ukarimu wa kumkaribisha ale pamoja nami maana alijua mimi mtu wa hadhi ya juu sana.
Akawa ananiambia kwamba yeye hakuishi hapo, bali alikuwa kikazi kwa ratiba, na kila baada ya kumaliza kazi yake angeondoka kabla ya saa moja kuingia. Ni mara chache angeonana na bosi wake, yaani hasa kama angekuwa ameshinda tu nyumbani ama kama akileta watu fulani kwa ajili ya party. Na akasema hajui kwa nini lakini alikuwa anamwogopa kweli bosi wake.
Nikaona kwamba mwanaume huyu alikuwa mtu mzuri, nami nikamwambia ajitahidi tu kufanya kazi yake bila kujiingiza kwenye mambo yasiyomhusu, na hangekuja kamwe kuona kwamba bosi wake ni mbaya. Kuhusu kulifanyia jengo hili usafi, akasema walikuwa wanakuja wafanyakazi wengine pia kwa ratiba kama yeye tu. Kulikuwa na mlinzi maalumu hapo nje ambaye ndiye alishughulika na yule mbwa mkali pia, kwa hiyo kabla ya hawa watu kuingia au kuondoka hapa, walitakiwa kumjulisha ili amfungie kwanza kuepuka ajali zozote za kung'atwa.
Sasa ndiyo nikawa nimetambua kutoka kwa mwanaume huyu kwamba jengo hili lilikuwa kwenye eneo lijulikanalo kama Mbezi Beach. Shefu hakujua kama sikufahamu kuhusu hilo, kwa hiyo nikawa nimemwambia iwe siri yetu tu kwamba tulikula pamoja na kuzungumza pia endapo kama bosi wake angekuja kumuuliza. Shefu akakubali. Alinikubali.
Tukiwa tunaenda kumaliza mlo, yule Khadija akawa amenipigia kwa mara nyingine. Mwanamke alikuwa na mchecheto huyo! Yaani hata Ibtisam sikuwa nimetoka naye bado ingawa alikuwa mzuri kweli, lakini yeye hakuwa king'ang'anizi kama huyu Khadija. Ila nikaona nimtolee uvivu kwa kuwa sasa mwili ulikuwa unarudisha nguvu. Nikapokea na kumsikiliza.
Alikuwa anataka tukutane leo, kwa sababu siku ya leo hakuwa amebanwa kwa lolote lile, na mume wake alikuwa na mambo mengine mpaka usiku mno. Alienda mbali mpaka kusema alikuwa ameniota kabisa, na alijisikia vibaya sana kutonipata kuanzia wakati niliompa namba mpaka sasa. Nikamwambia nilitingwa tu lakini sikuwa nimemsahau.
Sasa alikuwa anataka tukutane leo leo yaani kwa udi na uvumba, maana eti Joshua alikuwa anamwonea sana. Nilikuwa namsikiliza huyu mwanamke, yaani alikuwa mwongeaji aliyejua kupamba maneno yake ili tu apate alichokitaka, na ili kuondoa kero nikamwambia sawa; kama anakitaka sana basi atafute sehemu nzuri, siyo ya kizushi, ndiyo tukutane hapo ili tufanye alichotaka.
Akasema haina shida, yaani muda wowote kutokea sasa hivi ndiyo angekuwa amefika Mbagala kutokea Uhasibu alipokuwa na biashara zake, kwa hiyo mimi nijiandae tu kukutana naye sehemu atakayonielekeza. Alikuwa mwongo! Dakika mbili tu nyuma alikuwa amesema hajabanwa kwa lolote, eti sasa hivi tena akawa ameshafika na Uhasibu.
Nikasema poa tu na kumkatia simu, kisha ndiyo nikaenda zangu kusafisha mikono na mdomo. Sikuwa hata nikimaanisha kile ambacho nilimwambia huyo mwanamke, yaani basi tu. Kama mambo mengi ya upande wangu yasingeeleweka yaani hata kama angefanya nini baadaye, nisingeenda kukutana naye. Nilikuwa nahitaji muda wa kutuliza na haka ka mashine siyo kila siku kulima tu wanawake!
Shefu akasafisha meza, mimi hapo nikiwa nimeshamaliza usafi na kwenda kukaa sofani, kisha nikaingia mitandaoni kuangalia nini kipya. Shefu akaja mpaka sofani na kukaa, akiniuliza ikiwa ningependa kuitiwa usafiri sasa, nami nikaona niulize amemaanisha nini. Ndiyo akawa ameniambia kwamba bosi wake alimpa maagizo kuwa nikimaliza tu kula ndiyo amtumie taarifa kuwa mgeni kaishakula ili Festo atume sasa majambazi wake waje kunifata.
Nikawaza kwa ufupi, kisha nikamwambia atulie kwanza tupumzike kidogo. Nikamwomba anisimulie kuhusu maisha yake na familia kama alikuwa nayo, naye akafurahia kufanya hivyo. Nilikuwa tu nataka nile muda zaidi hapa maana hii nyumba ilikuwa nzuri balaa, na baada ya kuona kuna "console" ya kucheza game iliyokuwa imeunganishwa kwenye flat screen kubwa upande mwingine wa sebule hiyo, nikapata wazo la kucheza game pia.
Nikamuuliza Shefu, niliyekuwa nimejua sasa kwamba aliitwa Saidi, ikiwa alijua kucheza, naye akasema aliwahi kucheza PS zamani lakini hajui sana ikiwa angeweza sasa hivi. Nikamshawishi kwenda upande huo na kuwasha hilo TV kubwa kama dirisha, kisha tukawasha na hiyo deki ya game na kushika pad. Nilikuwa nimemiss hii kitu, na nilijua hii ingekuwa sehemu ya kuutafuta uchangamfu zaidi ili ule utulivu wa kiakili niliouhitaji niweze kuupata pia.
Tukaanza kucheza mpira, hao katuni wakiwafanana kweli wakina Messi na Ronaldo, hadi Siuuu waliweza kufanya! Shefu Saidi alipata shida kucheza mwanzoni lakini nikaendelea kumfundisha mpaka na yeye akaanza kujitahidi kunifunga. Nilijikuta nafurahia sana wakati huu mzuri pamoja na huyu baba, na masaa yakazidi kwenda nikiwa hapo hapo kwa Festo.
★★
Tuliendelea kucheza game mpaka kufikia saa kumi na moja, yaani Shefu Saidi alipenda sana hii kitu mpaka akawa amejisahau. Si ndiyo akapigiwa na bosi Festo sasa kuulizwa nini kilikuwa kinaendelea! Akaanza kupaniki, lakini
nikamtuliza.
Nikamwambia aseme mimi nilitaka kupumzika zaidi kwa hiyo bado nilikuwa hapa, naye shefu akamwambia hivyo Festo. Jamaa alikuwa na mambo mengi huko inaonekana, kwa hiyo akawa amemwambia shefu aniambie kwamba ameshawatuma watu wake waje na kunipeleka nilipoishi, naye shefu akakubali kufanya hivyo.
Baada ya bosi kukata simu, Saidi akaeleza namna ambavyo kweli alikuwa amefurahia uwepo wangu hapa mpaka akawa amesahau protocol. Nikamwambia asiwaze, na endapo kama akipenda tuwe marafiki nje ya kazi yake, basi tuachiane namba ili ikiwezekana tuje kufurahia pindi nyingine yenye kuburusisha kama hivi.
Nilipendezwa naye kwa sababu alikuwa mnyenyekevu sana huyu baba. Kwa hiyo akanipatia namba yake, kisha akaanza kuhakikisha kila kitu kinarudia mpangilio wake mzuri sehemu hiyo.
Haikuchukua muda mrefu sana na shefu Saidi akawa amepigiwa simu na mlinzi pale nje kuambiwa kwamba gari lilikuwa nje likinisubiria mgeni. Sijui kwa nini ingawa huyo Festo alikuwa na namba yangu hakuwa akinitumia jumbe za kunijulisha chochote kile, lakini na mimi niliona niendelee kukausha tu. Nisingejihangaisha hata kumtumia salamu yaani.
Kwa hiyo baada ya Saidi kuniambia kuhusu kusubiriwa na gari huko nje na yule mbwa kufungiwa, nikawa nimeenda kule chumbani kuvaa viatu vyangu na kuhakikisha nimejiweka sawa kimwonekano, kisha ndiyo nikatoka hapo na kumuaga mpishi huyo mwenye heshima. Lakini akaona anisindikize kabisa kuelekea nje, nasi tukaenda huku nikiangalia uzuri wa nyumba hii.
Zamu hii nisingefunikwa macho kwa kitambaa wala nini kwa hiyo labda Festo alikuwa ameanza kuniamini. Na ilikuwa ni bonge moja la jumba, ikionekana kuwa ya kununua, uwanja hapo nje ukiwa na mazingira safi pamoja na magari mawili ya kifahari tofauti kabisa na lile la Kluger ambalo Festo ndiyo alipenda kutumia alipotembelea sehemu kadha kama pale kwa kina Miryam.
Hiyo ilionyesha kwamba jamaa alificha kiasi upande huu wa maisha yake kwa watu wengi ambao hakutaka waujue, na inawezekana alikuwa na sehemu nyingine ya kukaa ambayo ingemfanya aonekane kuwa wa maisha ya kawaida tu. Kila mtu mwenye figisu ana njia zake za kujilinda, na huyu Festo alionekana kuwa makini kweli.
Kwa hiyo nikawa nimetolewa mpaka nje ya geti na kukuta Subaru Forester nyeusi ikiwa hapo, sijui ikiwa ni Uber, nami ndiyo nikampungia mkono wa kuaga Shefu Saidi na kuingia siti za nyuma. Alipenda sana kuonekana kuwa rafiki yangu.
Nikiwa ndani ya gari sasa, nikamtazama dereva na kuona alikuwa mwanaume mgeni kabisa kwangu, nami nikamsalimu kwa utulivu. Akaitikia vizuri na kuniambia amepewa maagizo ya kunipeleka Mbagala, ila tukifika huko nianze kumwelekeza mpaka kufikia mahala ambapo nilitaka kushukia. Nikakubali, nikiwa nimetambua kwamba huyu hakuwa kama wale majambazi ambao walinifata mpaka Masai kabisa, lakini huwezi kuwa na uhakika sikuzote.
Gari likaanza kutembea.
★★
Tulipita maeneo nisiyofahamu, ila kutokea Kawe pale kuelekea Mbagala sikuwa mgeni sana. Khadija sasa! Alianza kupiga simu, yaani kutokea Morocco mpaka tumefika Rangi Tatu, mwanamke alikuwa amepiga mara kumi na saba, na zote sikupokea!
Nilikuwa nahisi kero tu, yaani niliona wazi kwamba alikuwa ameanza kuniganda mno, mpaka nikawaza sijui nimpige block? Angalau hakuendelea kupiga tena mpaka nilipofika Mzinga, nami nikamwambia dereva anishushe hapo hapo; sikutaka anipeleke mpaka pale kwa Ankia kabisa.
Nikashuka, giza la saa moja likiwa limeanza kuingia, nami mdogo mdogo nikatembea mpaka kufika kwenye maskani yangu ya hii likizo. Sikuwa naziacha funguo za ziada alizonipa Ankia, na hapa nilikuwa nazo kwa hiyo nilipofika tu nikafungua geti na kuelekea ndani.
Nilikuwa nimeona gari la Miryam likiwa hapo kwake kwa nje kumaanisha mwanamke huyo alikuwepo, kwa hiyo hata wazo la kusema niwapigie mama wakubwa kuuliza hali ya Mariam nikaona nilitulize kwanza. Kwa muda huu, sikuhitaji misongo, lakini kuwa tu karibu na kwao hakungeiondoa. Yaani kwa mambo mengi akili yangu ilikuwa kwao tu. Ningefanyaje?
Nikabadili mavazi na kwenda tu sebuleni kukaa, ikiwa ni saa moja yenyewe sasa, na ile tu nataka kumtafuta Adelina ili kutuma salamu tena, simu ikaanza kuita. Khadija. Dah! Najua asingeacha kupiga kabisa huyu mwanamke, hivyo nikapokea ili nimwambie mambo yamenibana kwa hiyo sitoweza kwenda.
Kabla sijaongea, kutokea upande wa pili akasema, "Jamani wewe... nakupigia hupokei kweeli? Unajua nimeshapangilia kila kitu hapa? Kwa nini unanifanyia hivyoo?"
Nikatulia kidogo, kisha nikauliza, "Umepangilia nini?"
"Nimetafuta sehemu nzuri kama ulivyotaka, tokea saa kumi jamani... nakupigia hupokei, kweli?"
"Ndiyo, ni kweli. Nilikuwa bize..."
"Sa' si ungeniambia? Mbona kama unajisikia sana?"
"Aa wee... kama imeanza kufika huko, kata hii simu sasa hivi!"
"Me sijaongea vibaya, namaanisha tu... nimefanya kama ulivyoniambia, sasa nimekupigia kweli hata ukawa hupokei jamani! Hata kama ingekuwa ni wewe usingejisikia vizuri, lakini... nisamehe. Me... nakuomba uje," akanibembeleza.
"Uko wapi?"
"Sa'hivi niko hapa... nimesogea hapa Rangi Tatu, nimeingia hapa Highway, nakusubiri. Si unapajua?"
"Sipajui bana," nikaendelea kumwonea.
"We' njoo tu hata na bodaboda, mwambie akulete Highway... atakuleta..."
"Khadija nisikilize. Mimi sina hela, sawa? Kama unatarajia kupata hela, nakwambia mapema... mimi sina hela," nikamwambia kwa msisitizo.
"Kwani me nilikwambia nataka hela? Me nataka uje... nakutaka wewe kaka jamani, acha hizo basi. Hela ninayo, nalipia kila kitu... wewe njoo," akaendelea kubembeleza.
"Kwa hiyo nikitaka bia arobaini, utaninunulia?"
"Hata themanini, wewe njoo! Jamani, eh!" akasema hivyo.
"Umeshaanza kunywa wewe, eti? Maana naona unaongea tu..."
"Me nataka uje... kama bia utakunywa, na kama unaumwa nitakuponya. Usinifanyie uzushi jamani... uliniahidi. Njoo bwana. Kwani kuna kazi gani unayofanya sa'hivi?"
Nikatulia kidogo nikitafakari maneno hayo, nami nikamwambia, "Hamna. Hamna kazi yoyote."
"Sa' si uje? Niko free sana leo. Njoo tupeane love baby... nitakupa vyote," akasema hivyo.
Akanifanya nitabasamu kiasi, nami nikamuuliza, "Nimeshakuwa na baby?"
"Ndiyoo... we' ni mpenzi wangu. Njoo nikufurahishe bwana," akasema hivyo.
Nikafumba macho na kutikisa kichwa kidogo, nami nikamwambia, "Haya nakuja."
"Sawa. Si uko hii hii Mbagala sa'hivi?"
"Niko home kabisa."
"Sawa, we' njoo. Chukua boda kutokea hapo Mzinga ikulete mpaka hapa, nitalipia..."
"Mbona unaniwahisha sana?"
"Si unajua kuna suala la muda, my?"
"Si umesema uko free?"
"Eeh, ila ndo' mpaka saa sita tu. Nitatakiwa kurudi nyumbani. Nijali tu wangu," akaongea kwa ushawishi.
"Haya, nipe dakika kumi, nimefika," nikasema hivyo, na simu ndiyo ikakatwa.
Nilikuwa nimefikiria kumzingua huyu mwanamke, lakini sasa nikawa nimeamua kwenda ili tu kujiridhisha kidogo. Na sikumwamini. Ikiwa alitaka tuingiliane kimwili, ningefanya kitu ambacho sikupendelea kabisa kufanya pamoja na kuwa daktari na mengine mengi, yaani kutumia mpira wa kinga.
Nilitaka tu kumtumia huyu mwanamke kwa ajili ya jambo lingine, na kama ningekuwa kwenye mstari sahihi kufanya hivi, basi haya yote yalikuwa na faida kuyafanya hata kama sikuyaridhia sana. Na hata hivyo nilikuwa tu na uhitaji wa kuondoka tena ili kuyaweka pembeni kwanza haya mazingira yaliyokuwa yananilazimu kumwaza tu Mariam na dada yake.
Nikatoka hapo sebuleni na kwenda chumbani kuvaa kimtoko zaidi, pulizia manukato yangu, kisha nikaondoka kwa mara nyingine tena. Sikugeuka nyuma yaani.
★★
Nikawa nimefika hapo Highway baada ya dakika chache kutokea Mzinga, bodaboda go, na sikuwa nimesahau kuhusu kuchukua kinga; nilinunua chache dukani kabla ya kuja huku. Hii Highway ilikuwa ni kumbi ya starehe na vinywaji kama Masai tu, lakini yenyewe ilikuwa pana zaidi na yenye mtindo maalumu kikazi.
Namaanisha yaani hata wahudumu walivaa kwa sare za black and white kabisa, kitu ambacho Chalii Gonga alikuwa amefeli kuwafanyia waliopendezesha baa yake huko nilikotoka. Angalau hapa kulikuwa na kale kamvuto zaidi yaani watu walioingia wangejiona labda hata wako Kitambaa Cheupe, ila siyo kwamba ilikuwa nzuri kivile.
Kwa hiyo nilipokuwa nimefika tu, ikiwa ndiyo inaelekea kuingia saa mbili, nilimpigia huyo Khadija, naye akaja mpaka upande uliokuwa na sheli si mbali sana na hiyo sehemu, ikiwa ndiyo nilishukia hapo. Alikuwa amevaa kigauni kifupi cheusi kilichoyaacha mapaja yake wazi kiasi, yaani si mbali kutokea magotini, na kiliubana mwili wake kuchoresha umbo matata alilokuwa nalo na kufanya awe kivutio cha macho.
Tayari tu mimi mwenyewe nilikuwa natazamwa sana hapo nilipokuwa nimesimama, kwa hiyo huyu mwanamke alipofika karibu nami ndiyo karibia kila mtu aliyepita ama kusimama hapo nje akawa anatuangalia.
Khadija alikuwa amevaa kwa kujiachia sana wakati huu, yaani nilitambua kuwa hakuvaa sidiria kabisa, na chupi aliyokuwa amevaa kwa ndani ilikuwa ya aina ya kandambili ili sehemu kubwa ya makalio yake iwe nje kugusana na nguo yake iliyombana, kwa hiyo alipotembea yaani huko nyuma palitikisika kwa fujo sana. Na alionekana kupenda zile fujo fujo huyu, ndiyo maana nikawa najiuliza ni kwa kipi ambacho mume wake angekuwa anakikosa hapa mpaka kumwonea, na mwanamke naye aamue kuchepuka.
Ila sikujali sana kuhusu hayo. Nilichojali zaidi sasa ikawa kwamba baada ya kumwona namna hiyo, hamu tu hata ya kutaka kutembea naye ikawa ile ya sitaki-nataka. Alijichoresha mno, siyo kwamba kulikuwa na uajabu sana kutokana na jinsi alivyojiweka wakati huu, ila tu kwa sababu ilikuwa ni yeye yaani, sikupenda. Na hata zaidi alipokuwa amenifikia karibu, akanikumbatia ili eti tuchorwe vizuri sasa na watu wote, harufu ya pombe ikimtoka vyema mdomoni.
Nikamtoa kwangu taratibu na kumtazama kwa umakini, huku jicho lake lege kiasi likinitazama kimapenzi kabisa, ndiyo nikamwambia amependeza. Akacheka kidogo na kuuliza bodaboda aliyenileta yuko wapi ili amlipe, nami nikamwambia tayari alikuwa ameshaondoka kwa kuwa nilijilipia mwenyewe. Akasema yaani najua kweli kuzungusha, ila tutumie muda vizuri maana saa mbili inaingia, kwa hiyo akanishika mkononi na kuanza kuelekea kule kwenye Bar akitembea nami kwa ukaribu sana.
Aliona jinsi ambavyo sikuwa mtu wa kucheka-cheka sana na watu maana tulipokuwa tumeingia kule ndani, kuna wale waliokuwa wakishoboka kiasi na yeye kusimama kuwasemesha, ila mimi hata sikusimama kumsubiri. Mpaka akanifata na kuniuliza mbona namwacha kama vile niko kivyangu, ndiyo nikamwambia mimi sishobokagi na watu, akitaka kuongea na mtu hakatazwi, ila siyo lazima mpaka na mimi nijiunge naye.
Kwa kuelewa agenda yangu vizuri sasa, akawa mpole na kuniongoza mpaka alipokuwa amekaa; meza pana ya plastiki sehemu ya kona iliyojificha kiasi, na hapo walikuwa wamekaa wanawake wengine wawili rika kama la Khadija tu pamoja na mwanaume mtu mzima, mkubwa kabisa yaani kutosha kuwa mzazi kwangu, nasi ndiyo tukakaa hapo.
Tukasalimiana vizuri tu, huku nikiona jinsi ambavyo walinitazama kwa hamu, yaani labda nianze kushoboka nao sasa, lakini nikatulia tu na kuweka ubize kwenye simu yangu. Kulikuwa na bia hapo mezani, naye Khadija akawa ananinong'oneza kimakusudi tu yaani ili kujionyesha, akiniuliza nataka bia gani. Nikamwambia aagize Serengeti Lite, nikiwa makini yaani, naye akatii.
Hawa watu tuliokaa nao walikuwa ni washkaji zake Khadija eti, akiniambia hasa wale wanawake wawili alijuana nao na ile alipokuwa amekuja hapa kunisubiria, akawa amekutana nao. Ila nilijua alikuwa anadanganya tu, hao walikuwa ni mashoga zake wakipewa bia za ofa na huyo mwanaume mwingine, na hapa alikuwa amenileta ili kunioshea kwao, kwamba yuko na mtu mkali sana, si kingine. Hizi akili nazielewa sana.
Kwa hiyo nikaletewa bia tatu, nami nikamwambia Khadija nataka kuona bia themanini hapo mezani. Akacheka kwa furaha sana na kuanza kunisemesha kwa ukaribu ili tuonekane wapenzi wa dhati, na kweli, macho ya wengi hayakujizuia kutuangalia. Kulikuwa na sehemu zenye wanawake wakali kupita huyu mwanamke, na wengi waliniangalia sana. Hawa marafiki zake Khadija wakawa wanamtania eti awe mwangalifu asije kuibiwa mtu wake, naye akawa anajinadi kwa kusema haiwezi tokea maana tunapendana sana.
Nilianza kuona kwamba Khadija alikuwa amelewa zaidi, kwa sababu alikuwa ameshaanza kunywa pombe ile jioni kufikia wakati ambao nilikuja hapa, kwa hiyo mpaka namaliza bia zangu tatu yeye pia alikuwa ameongeza na kushusha zingine kooni. Aliongea na marafiki zake kwa kujiachia sana, kufikia hapo akiwa ameupandisha mguu wake mmoja juu ya paja langu, nami nikawa naona hapa siyo.
Highway ilikuwa imechangamka, lakini kwa hii kitu niliyokuwa nafanya nilikuwa napata vibe zenye kuboa tu. Khadija akataka kuniongezea bia, lakini nikamzuia. Nikamwambia imeshaingia saa tatu, tuondoke, naye akakubali. Alifikiri nina hamu sana ya kuondoka hapo pamoja naye ili tukafanye yetu, ila mimi nilikuwa nataka tu nitoke sehemu hii.
Moja, mbili, tatu, tukawa nje, Khadija akitembea nami huku ameshika kiwiko changu na pochi yake, na akionekana wazi kwa yeyote yule kwamba bia imemgonga, lakini hakuyumba. Nikamuuliza ni wapi kabisa alipokuwa amepanga twende kwa ajili ya jambo letu, naye akasema angenipeleka, ila tungepaswa kuchukua bodaboda mpaka kufika huko. Alikuwa anataka tupande kwenye boda moja eti, lakini nikamwambia hapana; tupande mbili maana sikupenda kubanana.
Kwa sababu fulani alionekana kupenda sana ujeuri niliokuwa namwonyesha maana alikuwa akicheka tu kwa kufurahia chochote nilichosema, nasi tukawa tumepata bodaboda mbili na kupanda; aliyopanda Khadija ndiyo ikiongoza kuelekea alipotuwekea makazi ya muda.
Tukiwa ndiyo tumeingia barabarani, nikawa nimepigiwa simu na askari Ramadhan, nami nikakumbuka kwamba nilikuwa na miadi ya kukutana naye leo ili tupange mikakati, lakini na hilo nikawa nimesahau. Nikapokea, naye alitaka tu kunijulisha kuwa kuna vitu vilimbana sana leo kikazi ndiyo maana akakosa muda wa kunitafuta, ila kama ni sawa basi kesho tutakutana mapema, kwa kuwa ingekuwa ni Jumamosi.
Nikamwambia haikuwa na shida kabisa, na ile amekata simu ndiyo bodaboda zikawa zimesimama. Haikuwa mbali sana kama nilivyodhani ingekuwa, tena hayo hayo maeneo ya Rangi Tatu kupita Zakhem kuelekea sehemu ya kushusha abiria usawa wa tawi la benki ya KCB, kisha kukunja kona kuiacha barabara ya lami na mbele kidogo ndiyo tukafikia jengo pana lenye ghorofa mbili. Lingefaa hata kuitwa hoteli, lakini wamiliki wakaona ni bora zaidi kuliita Lodge.
Eneo hilo lilikuwa na hali ya ugiza, kusiwe na watu wengi sana kuachana na wapita njia, mafundi wachache wa gereji walioonekana kwa mbele, na daladala kadhaa zilizotulia. Kwa hiyo tuliposhuka, Khadija akalipia usafiri, kisha ndiyo tukaelekea ndani ya hiyo lodge. Alikuwa amepitisha mkono wake kiunoni kwangu na kutembea nami akilalia bega langu, nami nikawa nimemshikilia begani pia kumwonyesha 'support.'
Tukaingia mpaka mapokezi, na mhudumu aliyekuwepo hapo, mwanamke mtu mzima pia, akawa amempa Khadija funguo ya chumba ambacho tayari mwanamke huyu alikuwa amelipia, nasi tukaanza kuelekea sehemu yenye ngazi. Tulipanda ngazi na kufika ghorofa la pili, na ilikuwa kama vile hamna watu wengi sana hapa, ila bila shaka kwa waliokuwepo walikuwa vyumbani wakifanya yao. Na ilikuwa sehemu nzuri, Khadija alijitahidi.
Akanifikisha kwenye mlango wa chumba chake, naye akatangulia kuingia huku nikifata kwa ukaribu nyuma yake; macho yangu yakitembea na mdundiko wa kalio lake. Kama ni kuondoa stress angekuwa amenisaidia sana kwa leo pia kama tu kucheza game na Shefu Saidi kulivyokuwa kumenituliza.
Chumba kilikuwa kizuri, kisafi, kitanda kipana, hadi kulikuwa na TV ndogo ya flat screen ukutani, naye Khadija akaenda kitandani na kukaa kwa kujiachia, mikono yake ikiupa mwili egemio huku ananiangalia kwa macho yenye uvutio. Ilikuwa ule mtindo kama vile anakaribia kulala chali, nami nikawa nimesimama tu huku nimeshasimamisha msuli kwa ndani tayari. Fikira tu za jambo lote.
Akaniambia, "Nimegharamika kweli kwa ajili yako leo."
"Umelipia shi'ngapi hapa?" nikamuuliza.
"Elfu hamsini," akanijibu hivyo.
"Na pombe ulikuwa unanunua. Umetoa wapi hela?"
"Ish... nina kazi, kwani unanionaje?"
"Naona kama mume wako ndiyo anakugharamia, ila hii... unaweza ukawa umemchomolea laki ama umedanga kwingine ili tuwe hapa..."
"Ahahaaa... nayedanga naye ni wewe. Na sijawahi mimi... kutoa hela kwa ajili ya mwanaume... wewe ndiyo wa kwanza," akasema hivyo kilevi.
"Kumbe?"
"Eeeh. Njoo hapa..."
Akaniambia hivyo huku akiupandisha mguu wake kwenye wakwangu akiwa ameunyoosha, mpaka kiatu f
chake kikagusa sehemu yangu ya siri na kuikandamiza kiasi. Nikaushika na kumsogelea karibu zaidi kwa kuingia katikati ya miguu yake, akiipanua sasa na kujilaza zaidi kitandani huku ananiangalia kwa hamu. Kwa hiyo sasa nikawa kama nimelala juu yake, uso wangu ukiwa karibu na wake, naye akaanza kupitisha vidole vyake kichwani kwangu taratibu.
"Yaani una sura nzuri we' kaka..." akaniambia hivyo.
"Kumbe? Mbona sikujua?" nikamsemesha kizembe.
"Ahah... nimekuelewa sana..." akaniambia hivyo.
"Na mume wako je?"
"Mzinguaji tu..."
"Kwenye kipi?"
"Mambo mengi. Tunaelewana, sema yeye tatizo lake ana gubu sana. Yeye atoke nje na mahawala, sawa tu... halafu mimi hataki nifanye jambo kama hilo. Wanaume wengi wananitaka, nawapotezea... lakini wewe hapana. Nimeshindwa kujizuia..." akaongea kwa njia fulani ya madaha sana.
Akataka kunivuta ili tuanze kupiga busu, lakini mimi nikataka nimchimbe zaidi kwanza, kwa hiyo nikaweka mgomo kiasi na kusema, "Ngoja kwanza. Hivi siku ile nimekushika nyonyo, si alituona?"
"Ahhh... eeh alituona," akanijibu hivyo.
"Mbona akawa mpole?"
"Ah... pale alikuwa anaigiza tu, we' ile familia si unaijua?"
Kauli yake ikanifanya nitambue kwamba huyu mwanamke alielewa mambo mengi sana kuhusiana na familia ya Miryam na mume wake, nami nikaona nitikise kichwa kukubali hiyo hoja.
"Alituona. Hiyo siku tumerudi nyumbani nilisemwa!" akasema hivyo.
"Wewee..."
"Acha kabisa. Alinitukana kweli. Ila huwa nikija chini tu baadaye mambo yananyooka. Mwenzako nikafikiri sitakuja kukuona tena, ila Mungu akiwa na mipango yake bwana... haipingwi..." akasema hivyo.
Nikatoa tabasamu hafifu, kisha nikaona nikoleze mambo.
Nikafunua upande wa kushoto wa gauni lake kifuani, na titi lake moja likafichuka. Nikaanza kulinyonya, nene kweli, nikinyonya chuchu yake taratibu huku navuta lile la kulia, naye akawa anapumua kwa raha na kugeukia upande kwa upande huku akichezea nywele zangu kichwani.
Nikaacha kulinyonya na kuanza tu kulivuta-vuta, kisha nikamuuliza, "Kwa hiyo mume wako bado anawa-mind sana ndugu zake, eti?"
"Ahh... eeh... wakuda tu. Wewe mwenyewe... sijui unawasaidia lakini si Miryam am
ekufukuza juzi? akasema hivyo.
Nikamtazama kwa umakini, nami nikamuuliza, "Umejuaje? Ni kweli kabisa alinifukuza."
"Mama mkwe mdogo aliniambia jana nilipoenda pale. Hadi na yeye alikuwa haelewi. Ulimfanya huyo Miryam lolote baya?"
Nikawa namwangalia kwa umakini, nami nikamwambia, "Hamna hata. Ila ni kweli kabisa... ni wakuda sana. Nilikuwa namshauri tu halafu akanifukuza. Alinikera!"
"Huyo mwanamke ndiyo alivyo, huwa hasikilizi, anajionaga anajua sana. Wote tu ni wajinga-wajinga... hata usijipendekeze kwao..."
"Kweli kabisa. Hawanipi faida yoyote, na watakuja kuishia pabaya maana wana viburi mno. Natamani kitu chochote tu kiwapate ili wajifunze," nikaendelea tu kutia chumvi.
"Si ndiyo maana Joshua yuko hapo? Atawanyoosha tu!" akasema hivyo.
"Kumbe? Basi hiyo itakuwa vizuri. Ningekuwa najua hata nisingempinga jamaa kipindi kile... basi tu," nikaongea kama vile namuunga kabisa mkono.
"Eee... alinihadithiaga... alikuwa karibu kweli kuchukua mali ila ukamvurugia. Lakini nikwambie kitu? Sasa hivi hawatoki. Yaani kipute extra kinawakuta. Utakuja kusikia," akaniambia hivyo.
"Joshua anakuja kivingine, au siyo?"
"Haswaa! Mimi hapo tu ndiyo huwaga namkubali... hakatagi tamaa. Na hivi anajua kuigiza, alinipanga fresh kweli kwa ajili ya hii show... we' subiri tu... imeshaanza kazi. Huyo mwanamke ataelewa haelewi," akaongea kwa nyodo za wazi.
Mh?
Nikajikuta naangalia tu pembeni nikiwa nawaza kuhusu taarifa hii, nikifikiria kuhusu ni nini ambacho kingekuwa kimeanza kufanywa na Joshua dhidi ya familia ile. Umeona? Nilikuwa sahihi kufikiri huyu mwanamke alijua vitu fulani kuhusu mipango ya mume wake, na hii ingekuwa nafasi nzuri ya kujua yote yaliyokuwa yamepangwa ili nitafute njia ya kuyazuia bila kujali kingine.
Khadija alikuwa amenishika mgongoni, nikiwa nimelala juu yake lakini kwa ubavu, kwa hiyo akapitisha mkono wake kwa chini mpaka kuigusa mashine yangu na kusema, "Jamani... ni(.....) basi!"
"Eh! Maneno makali dear," nikamwambia hivyo.
"Ninawashwa mwenzako..." akasema hivyo kwa deko.
Nikaingiza kiganja changu kwenye mapaja yake na kushika sehemu ya kati, naye akanyanyua mguu wake na kuutandaza vizuri ili niweze ku....
Kabla sijaanza kufanya mitekenyo yoyote ile kwa huko chini, simu yangu ikaanza kuita. Ilikuwa mfukoni, kwa hiyo nikatoa kiganja changu kwenye mapaja ya huyu mwanamke na kuanza kuivuta. Khadija akawa ananiambia niachane nayo, nami nikasema kama isingekuwa mwito kutoka kwa mtu muhimu basi ningeitolea sauti ili tuendelee na mambo yetu.
Nilipofanikiwa kuitoa nikakuta mpigaji akiwa ni Bi Zawadi, nami nikatulia na kuangalia muda hapo hapo kwenye simu. Ilikuwa ni saa tatu na nusu sasa, nami nikaona niachane na Khadija kwanza ili nimsikilize mama mkubwa. Nilihisi lingekuwa suala lililomhusu binti Mariam kama siyo tu kwamba alitaka kunisalimia. Khadija akawa ameendelea kujilaza niliposema simu ni muhimu kupokea, kisha ndiyo nikapokea na kuweka sikioni.
"Haloo... JC..." Bi Zawadi akasikika.
"Naam mrembo wangu... za jioni?" nikaitikia.
"Si salama sana baba," akasema hivyo.
Sauti yake ilijengeka kiwasiwasi yaani, nami nikamuuliza, "Kuna tatizo gani mama?"
"Tafadhali niambie umemwona Tesha..." akasema hivyo
"Tesha? Leo hapana, sijaonana naye," nikamjibu.
Khadija akajinyanyua na kukaa, akiniangalia kwa ukaribu na macho yake lege.
"Eh Mungu!" Bi Zawadi akasema hivyo kwenye simu.
"Shida ni nini?" nikauliza kwa kujali.
"Tesha ameondoka na Mamu... alitakiwa kuja muda siyo mrefu ila mpaka sasa hivi hawajarudi..."
Kauli hiyo ikanifanya nishtuke kiasi moyoni.
"Jamani tumechanganyikiwa huku JC... tumemtafuta hapatikani mpaka sasa hivi... atakuwa amempeleka wapi Mamu?" Bi Zawadi akaongea kwa hisia.
"Tesha alikuwa ameondoka naye kwenda wapi?" nikamuuliza.
"Walitoka... Tesha alikuwa ameenda kufata kitimoto... Mamu akamsindikiza, walitakiwa kurudi mapema, ila wakakawia. Tulikuwa tunampigia simu kumuuliza mbona anachelewa na usiku unaingia, akawa anasema mboga bado ni ya kusubiri sana. Imefika mpaka saa tatu tukaanza kumpigia ndiyo akawa hapatikani kabisa! Eh... mpaka Miryam na Joshu wametoka kwenda kuwatafuta... pale walipoenda kuchukua nyama hawapo tena, na Mimi bado hajarudi. Wanawatafuta..." akaeleza hayo.
Nikakaza ngumi baada ya kusikia hivyo, nami nikamuuliza, "Joshua alikuwa hapo na nyie?"
"Ndiyo, alikuja kututembelea... JC, nakuomba utusaidie kumpata Tesha. Tuna wasiwasi sana, yuko na mtoto na sasa hivi usiku baba..." akaniomba.
"Sawa, usijali. Nitaangalia cha kufanya. Nikipata lolote nitakujulisha," nikamwambia hivyo kwa upole.
"Asante sana baba," akashukuru.
Simu ikakatwa, nami nikaangalia pembeni kwa umakini.
Khadija akanitikisa begani kiasi na kuuliza, "Vipi? Ilikuwa mama mkwe wangu kama sikosei?"
Nikatazama chini na kusema, "Eeh. Ananiambia Tesha ameondoka na mdogo wake ila mpaka sasa hivi hawajarudi. Hapatikani... kwa hiyo wanawatafuta."
Khadija akacheka kidogo, kisha akasema, "Si nilikwambia?"
Maneno hayo yakanifanya nimtazame usoni, naye alikuwa anatabasamu kwa njia iliyoonyesha kwamba hilo ni jambo alilokuwa analielewa vizuri. "Unamaanisha nini?" nikamuuliza.
"Kipute extra kinawakuta! Joshu ashafanya yake, huyo msichana kabebwa," akasema hivyo.
Nikajitahidi kuonyesha kwamba hicho alichokisema hakikunishtua, na kwa kumpa kichwa ili afunguke zaidi nikasema, "Ahaa... kumbe ni Joshua! Dah, mwamba yuko vizuri... ndo' ile ishu uliyoniambia, eti?"
"Sasa je!"
"Wewe... lakini, huyu ameniambia kwamba Joshua yupo nao, sasa... kafanyaje hivyo?"
"Aah... nisikilize. Joshua ana akili. Katuma watu wake, halafu yeye yuko nao pale kwao kwa hiyo hawawezi kujua kama ni yeye. Nimekwambia Joshua anajua kuigiza wewe! Hadi anajifanya kwenda kuwatafuta ahahaaa... haki ya Mungu..."
"Ahah... heh... kwa hiyo... wamembeba Mariam... ili iweje sa'?"
"Si hako kataahira ndiyo kanasababisha Joshua asipewe mali yake? Akikaondoa ndiyo money zitaanza kuingia tena... na zamu hii nitakuwa namnyonya ka...."
"Subiri. Kwo'... unawajua waliotumwa?" nikamkatisha.
"Agh, ni huyo tu Yohana... rafiki yake. Wengine me siwajui. Ndiyo maana nilikwambia leo niko free sssana... Joshua alikuwa ameshanipanga mapemaaa. Kwa hiyo yupo huko anawa-teach, na mimi niko hapa nam-cheat... ahahahahh..." akasema hivyo na pombe yake kichwani.
"Kwa hiyo Mariam wamempeleka wapi? Wanaenda kumfanya nini?" nikamuuliza nikiwa nimeingiwa na wasiwasi.
"Watajua wenyewe! Wamtupe, wamfukie, wamchinje, sawa tu. Hakana faida yoyote hako kajinga. Ila kwa jinsi ambavyo namjua Yohana, lazima watakabaka kwanza mpaka watosheke ndiyo miamala ianze kuingia..." akasema hivyo na kuanza kucheka.
Fikira za mambo aliyoyasema huyu mwanamke zilifanya nihisi kama vile nimepigwa na kitu kizito yaani, nami nikatazama pembeni nikiwa nahofia sana. Nilichoka aisee!
Yaani niliwaza namna ambavyo hizi hali ziliendelea kuniweka katikati ya kila jambo lililohitaji suluhisho kwa njia ambayo ilikuwa kama vile imepangwa, mpaka kwa mara nyingine tena nikawa najiuliza kwa nini mimi. Lakini kwa wakati huu, nilitakiwa kukazia fikira zaidi juu ya njia ya kuweza kuwa suluhisho hilo kikweli, ili Mariam asipatwe na masaibu ambayo watu hawa walimpangia. Angekuwa kwenye hali ipi kwa sasa yule binti?
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments