CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA NANE
★★★★★★★★★★★★★★
Basi, jioni haikukawia kufika siku hii, naye Blandina akawa amejiandaa kwa ajili ya muda ambao angeutumia na mwanasheria kijana kwa jina la Draxton usiku huo. Alikuwa na matarajio mazuri sana, hivyo alihakikisha anapendeza na ananukia vizuri sana ili jamaa asimchukulie poa hata kidogo. Alitaka kumwonyesha leo kwamba anajua.
Alijiremba vizuri sana usoni, nywele zake za kusukwa akiziachia mpaka mgongoni, mwilini akivaa nguo fulani yenye muundo kama wa shati refu lililoishia sehemu za chini za mapaja yake, likiwa kama limekatwa mipasuo midogo kwa pembeni na hivyo mapaja yake kwa upande kuonekana vyema. Lilikuwa refu lakini kutokana na hips zake nene na kalio kubwa ilifanya linyanyukie juu kidogo namna hiyo. Sehemu ya kifuani liliacha uwazi mpana kwenye mstari uliotenganisha matiti yake na hivyo kuyaonyesha kwa juu kiasi. Lilikuwa na rangi ya blue kwa ujumla mchanganyiko na rangi zingine, na ni hilo pekee ndiyo alilovaa pamoja na nguo za ndani. Miguuni alivalia viatu vyeusi virefu vyenye kamba zilizoifunga miguu yake kwa kupanda mpaka sehemu za supu. Alipendeza.
Akiwa anajiweka sawa zaidi, simu yake ikaita, na tabasamu la furaha likatoka midomoni mwake baada ya kuona ni yule yule aliyemtarajia. Akapokea, naye Draxton akaongea kutokea upande wa pili, akisema tayari alikuwa nje ya nyumba aliyoishi bibie, hivyo achukue muda wote aliohitaji kujiandaa, naye angekuwa hapo nje akimsubiri. Blandina akavutiwa na huu utendewaji wa kama vile yeye ni malkia, naye akamwambia angetoka muda si mrefu. Baada ya maongezi hayo, Blandina akajigusa hapa na pale kuhakikisha anatoka nje kuua macho ya mtu, kisha akaelekea nje ya nyumba aliyoishi.
Alipotoka nje ya geti, akaliona gari la Draxton, aina ya Forester nyeusi, likiwa limeegeshwa upande wa pili wa barabara iliyozitenganisha nyumba za maeneo hayo, na Draxton mwenyewe akiwa amesimama nje kwa kuliegamia. Akatembea taratibu mpaka alipomfikia jamaa, naye akatabasamu kwa hisia. Draxton alikuwa amevaa sweta jepesi la mikono mirefu, lililokuwa na rangi ya blue iliyolowana, na lilimbana vizuri kuonyesha jinsi kifua chake kilivyojengeka vizuri kilivyokuwa. Alivalia suruali nyeusi ya kardet na viatu vyeusi chini, naye akatabasamu pia kwa kupendezwa na mwonekano wa Blandina.
"Umependeza," Draxton akaongea kwa sauti tulivu.
"Asante," Blandina akamjibu huku akitabasamu.
"Hawajambo huko ndani?"
"Niko mwenyewe hapo na dada wa kazi..."
"Aah... sawa. Naona hii mitaa imetulia."
"Yeah kidogo. Hakuna fujo sana."
"Sawa. Twend'zetu," Draxton akasema.
Blandina akatikisa kichwa kukubali, kisha Draxton akamfungulia mlango wa gari sehemu ya mbele, naye Blandina akapita karibu yake na kuingia kukaa. Ndani ya gari la Draxton palinukia vizuri sana, na jamaa akazungukia mpaka upande wa usukani na kuingia pia. Akaliwasha gari lake na kulitia mwendoni huku Blandina akimwangalia tu kwa jinsi alivyokuwa kimya sana, naye akachekea kwa chini.
"Vipi?" Draxton akauliza.
"Hamna kitu. Unaonekana makini kweli," Blandina akasema.
"Ahah... ndiyo hivyo. Usinilaumu sana nikikuboa mpaka ukahisi kufa," Draxton akamwambia.
"Ahahahah... sifikirii kama utaboa sana. Jinsi ulivyokuwa unaongea mahakamani leo yaani... nilijua u-special wako ni wa hali ya juu."
"Usiwahi kufikiri hivyo maana bado hujanijua vizuri."
"Ndiyo nataka sasa kukujua. Sijakutana na wanaume wengi ambao wako tayari kuninunulia chupa nyingine baada ya kuivunja..."
"Chupa tu? Hujui kwamba wapo watakaokununulia mpaka majumba na magari?"
"Magari hayajawahi kunibabaisha..."
"Mmm... kwa hiyo kumbe ni hapo kwenye chupa ndiyo palikukamata eh?"
"Pamoja na mambo mengine."
Draxton akatabasamu kidogo na kusema, "Well, Blandina, hii ni kama apology tu kwa kuku..."
"Wewe unaiona kama apology tu na siyo kitu kingine zaidi?" Blandina akamkatisha.
"Mambo mengine huja baada ya muda. Ndiyo tumekutana tu kwa mara nyingine," Draxton akamwambia.
"Mmmm... napenda jinsi ulivyo on point. Bila shaka umewapangisha wanawake wengi foleni," Blandina akasema.
Draxton akacheka huku akiwa amefumba mdomo.
"Angalau nimepata bahati ya kuendeshwa nawe leo," Blandina akasema.
"Kwa nini uione kama bahati?" Draxton akauliza.
"I don't know. Labda we' ndo' uniambie. Ni nini kimenifanya nisiweze kuku-resist?"
"Mmm... nimependa jinsi ulivyo on point pia. Napenda mwanamke asiyeficha hisia zake na kutarajia mwanaume tu ndiyo awe mwenye kufunguka kwake."
"Kumbe? Hujakutana na wengi walio hivyo kwani?"
"Wapo wengi. Sema, mimi siyo mtu wa kukaa kutafuta..."
"Oooh kwa hiyo mpaka wewe ndiyo utafutwe..."
"Wewe ni tofauti Blandina. Unajua unachotaka, uko care, na ukisharidhika unatulia. Ungeweza kunipotezea tu na kuamua kujitafutia mtu mwingine lakini inaonekana fikira zako zimeridhishwa na mimi. Kwa hiyo niko hapa kujaribu kutokuzivunja moyo."
"Ahahah... fikira zina moyo?"
"Ni tamathali tu..."
"Me naziona kama swagger. Unaongea kwa njia fulani tofauti... nzuri sana..."
"Wewe pia."
"Kwa hiyo umeshakuwa na wanawake wengi eeh? With that charm who could resist you?"
"Ahahahah... usinione vibaya lakini kuhusu hilo..."
"Mhm... hapana wala, mimi pia nimepita kwa wanaume kadhaa. But kila mara inakuwa ni kama sijui kuchagua, au labda mimi ndiyo mwenye tatizo kwenye...."
"La, siyo wewe," Draxton akamkatisha.
Blandina akamwangalia kwa utulivu.
"Wewe Blandina unataka kupendwa, ndiyo maana moyo wako ni rahisi kupenda. Sema, watu wengi huwa wanalipenda tu wazo la kupenda na hawafilirii nini kiendelee zaidi wakishapenda, ndiyo maana muda ukipita hilo wazo wanalichoka kumwelekea mtu waliyedhani walimpenda. Wewe unataka kutulia, ila watu unaowapata wanafikiri unataka kucheza, kwa sababu huwaonyeshi mapema kwamba unategemea watulie nawe, kwa hiyo baadaye ukija kuwaonyesha... wanazingua. Hilo si tatizo lako kwa sababu ni wenyewe ndiyo wanakuwa wanashindwa kuona jinsi mambo yalivyo kihalisi," Draxton akamwambia kwa ustaarabu.
Blandina akamwangalia sana, kisha akauliza, "Unawezaje kuongea hivyo kuhusu mimi wakati ndiyo tumekutana tu?"
"Niliwahi kusoma saikolojia kidogo," Draxton akamwambia.
Blandina akatabasamu na kuangalia mbele.
"Samahani kama nime...."
"No, no, nimependa maneno yako. Ulichosema ni kweli, maana hata me nwenyewe nilikuwa sijafikiria hivyo ila ni kweli kabisa," Blandina akamwambia.
"Usijali sana, ni kitu cha kawaida," Draxton akasema.
"Kwa hiyo... unasema kwamba nikikuonyesha nataka kutulia nawe, na wewe utatulia na mimi?" Blandina akauliza.
"Ahahah... huko bado sana kufika Blandina. Ndiyo tumekutana tu, kama nilivyosema," Draxton akaongea.
"Sawa," Blandina akajibu kiupole huku akiangalia mambo fulani kwenye simu yake.
Wakaendelea na mwendo, huku Blandina akimwelekeza pa kwenda, na sasa giza lilikuwa linavizia kwa mbali baada ya jua kutua.
"Tunaenda mahali fulani hususa? Maana huku sijawahi fika," Draxton akamuuliza, wakiwa mwendoni bado.
"Ndiyo. Rafiki yangu anaandaa mlo wa jioni pamoja na mume wake, wanataka ku-share pamoja nami kwa sababu sikuwa nimeonana na mume wake muda mrefu... ni rafiki yangu pia, yaani wananikaribisha," Blandina akasema.
Draxton akabaki kimya, lakini Blandina akatambua ni kama jambo hilo halikumfurahisha.
"Vipi? Haujapenda kwamba... tunaenda huko?" Blandina akauliza.
"La, si hivyo. Nilifikiri ingekuwa mimi na wewe tu, sikuwa... sikudhani kungekuwa na wengine."
"Haupendi mijumuiko eeh?"
"Kawaida tu. Ungeniandaa mapema."
"Usiwaze. Ni watu wazuri sana na... nitafurahi kukutambulisha kwao," Blandina akamwambia.
Aliongea hivyo utadhani tayari alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume huyu, naye Draxton akampa tu tabasamu na kuendelea kuendesha na maongezi mengine kuendelea. Blandina alikuwa akiuliza mambo fulani kuhusu maisha ya Draxton, lakini mwanaume huyu angekwepa kujibu moja kwa moja na kugeuza mada zimwelekee Blandina, ambaye angeongea kwa uhuru kuhusu mambo yake mengi.
★★
Nyumbani kwa wanandoa Efraim Donald na Namouih, maandalizi kwa ajili ya kumkaribisha rafiki yao yalikuwa yamekamilika kufikia wakati huu, katika maana ya msosi. Namouih ndiye aliyetengeneza chakula kizuri kwa ajili ya rafiki yake na mume wake, lakini bado wazo la Blandina kuhusu kumleta Draxton hapo lilimkera. Lilimkera hasa kwa sababu mtu huyo alikuwa upande pinzani wa kesi waliyopigania, akiwa mtetezi wa mbakaji wa msichana mdogo, na jinsi alivyotoa kauli mbalimbali mahakamani zilizoonwa na wengine kuwa zinapatana na akili kulimfanya Namouih amchukulie Draxton kwa njia fulani kama adui. Ingawa Blandina kumleta mwanaume huyo hapo kulimkera sana Namouih, kungempatia pia nafasi ya kumsoma zaidi, kwa sababu alipanga kuona mwanaume huyo alijengekaje kiutu.
Efraim Donald tayari alikuwepo nyumbani, akiwa amekaa zake kwenye sofa huku akipitia mambo kadhaa kwenye simu, na TV kubwa ukutani ikionyesha habari za saa, ikiwa ni saa moja tayari. Namouih alipokuwa amemaliza kusaidizana na Esma katika masuala ya mapishi, akaelekea juu ili kujiweka sawa zaidi kimwili. Alijiwekea mwonekano wa kawaida tu kama mke wa nyumbani kwa kuvaa dera refu lenye urembo mwingi, naye akarejea kwa mume wake na kuketi karibu yake sofani, akipiga naye story na kujipiga picha za selfie pamoja naye. Angalau yale yaliyotokea jana baina yao walikuwa wameyaweka pembeni kwa wakati huu.
Hazikupita dakika nyingi na simu yake ikaita, ikiwa ni Blandina anayepiga, naye akapokea na kujua sasa kwamba rafiki yake alikuwa nje ya geti tayari. Namouih akamwambia sawa, kisha akanyanyuka na kwenda mpaka mlangoni, naye akamwita Alfani akimwambia kuna mtu nje hivyo akafungue geti kumruhusu aingie. Baada ya Alfani kufanya alichoambiwa, gari lisilo geni sana machoni mwa Namouih likaingia, akitambua ni la Draxton kwa sababu alimwona mapema leo akiondoka nalo kutoka mahakamani. Akawa amesimama tu hapo huku akilitazama mpaka lilipoegeshwa nyuma ya magari yao, kisha milango ikafunguka na wawili wale kutoka.
Namouih akawa amemkazia macho Draxton, ambaye alionekana kuangalia umaridadi wa eneo la nyumba hiyo mpaka Blandina alipomfata na kukishika kiganja chake, kisha wakaanza kutembea kwa ukaribu kumwelekea Namouih. Blandina alionekana kuwa mbingu ya 18 maana aliongea na jamaa huku akicheka kwa furaha, na Namouih akajiambia tu moyoni 'haya.' Efraim Donald naye akawa ametoka na kusimama pembeni ya mke wake, na baada ya Blandina na Draxton kufika karibu, Namouih akamkumbatia rafiki yake huku wakisemeshana kwa uchangamfu.
"Nakuona shemeji," Blandina akamwambia Efraim baada ya kuachiana na Namouih.
"Nakuona na wewe, yaani huachi tu kunenepa! Ni kilo, kilo, tani..." Efraim akasema, nao wakacheka na kukumbatiana pia.
Namouih akawa amempuuzia kabisa Draxton, hata kumwambia tu 'karibu' hakutaka.
"Donald, huyu ni Maximilian Draxton," Blandina akamtambulisha hatimaye.
"Vipi kaka?" Efraim akamsalimu.
"Safi," Draxton akajibu.
Wanaume wakapeana mikono kirafiki, naye Efraim Donald akatambua kwamba mikono ya Draxton ilikuwa na nguvu sana.
"Karibu sana. Naitwa Efraim. Ukipenda niite Donald," Efraim akamwambia.
"Nimefurahi kukufahamu Efraim. Niite Draxton," naye pia akajitambulisha.
Efraim akasema, "Draxton ni jina lenye nguvu. So, wewe na huyu kibibi mna...."
Blandina akacheka na kusema, "Umeanza!"
"Ahahah... gesture ya kwanza. Mnapendezeana," Efraim akamwambia.
"Well, bado siye ni marafiki tu, ila kwenye kupendezeana uko sahihi..."
Blandina ndiye aliyesema maneno hayo huku akimlalia Draxton begani, naye Efraim akatabasamu, huku Namouih akizungusha macho kikejeli.
"Karibu dear. Ulivyovaa utafikiri unataka kuua mtu," Namouih akamwambia Blandina.
"Na bado..." Blandina akajibu.
Wawili hawa wakaongoza kuingia ndani, huku wanaume wakiwafuata nyuma.
Ndani hapo palikuwa pazuri sana, Draxton aliona hilo, nao wakaelekea mpaka masofani na kukaa. Blandina aliongea kwa uchangamfu sana alipozungumza na Efraim Donald. Maongezi yalipohamia kwa Draxton, hakuongea sana kujihusu zaidi ya kusema yeye ni mwanasheria anayejitegemea tu na siyo kwamba ameajiriwa sehemu yoyote binafsi au serikalini. Akasema ni muda mrefu kiasi ulikuwa umepita tokea mara ya mwisho aliposimamia mtu kwenye kesi, kwa hiyo wakati huu alikuwa amerudi tena upande huo ili kufanyia kazi kipawa chake cha uanasheria. Namouih hakumsemesha hata kidogo ingawa wote kuwa wanasheria kungefanya wawe na mengi ya kuongelea, na kwa kiasi fulani suala la Draxton kuchuana naye kwenye kesi likazungumziwa, lakini kwa njia nzuri tu kwenye maongezi yao changanyikeni.
Basi, imefika saa mbili hivi, Namouih akawaongoza wengine kwenda kuketi kwenye meza ya chakula, naye Blandina akamshika tena Draxton kiganjani na kutembea karibu yake mpaka walipoketi vitini. Kulikuwa na vyakula vingi vilivyofunikwa ndani ya vyombo vya kutunzia, naye Blandina akatania kuhusu kutoa sala kabla ya kula, akimwambia Efraim afanye hivyo. Efraim Donald akasema kwamba chakula kilikuwa kimeshabarikiwa pindi tu mke wake alipomaliza kukipika, kwa hiyo haikuwa na haja ya kusali, na hilo likafanya wengine wacheke. Esma alikuwepo pia hapo akisaidia kupangilia mambo vyema, naye akakaa pia kwenye kiti kimoja. Ni Namouih pekee ndiye aliyekuwa amesimama sasa, akimimina juice (sharubati) ya mchanganyiko wa parachichi na ndizi kwenye glasi za wengine. Alipomaliza ya Efraim, akaifata ya Esma, kisha ya Blandina. Lakini alipoifikia ya upande wa Draxton, akamwangalia kidogo na kuona jambo fulani.
Mwanaume huyo alifumba macho taratibu na kuinamisha uso wake, akivuta, au akitoa hisia fulani hivi. Hii ilikuwa ni mara ya pili Namouih kumwona anafanya hivyo, ya kwanza ikiwa ni mapema ya leo walipokuwa mahakamani, naye akashindwa kuelewa alikuwa na tatizo gani. Wengine hawakutambua jambo hilo, naye Namouih akaghairi kumwekea jamaa juice na kwenda kuiwekea glasi ya sehemu ambayo angekaa yeye. Blandina alikuwa anaongelea vituko vya shuleni pamoja na Esma na Efraim, naye akawa ametambua kwamba Namouih hakumwekea mtu wake juice. Hii haikukaa sawa machoni pake, na kwa kuhisi Namouih alifanya hivyo kwa makusudi, akalichukua jagi lenye juice na kuanza kummiminia Draxton kwenye glasi bila kumtazama Namouih, lakini Namouih akawa anamtazama tu mwanaume huyo kwa jicho la chini.
Sasa Draxton akawa ameketi sawa baada ya Blandina kumaliza kumwekea juice, akisikiliza maongezi baina ya marafiki sehemu hiyo.
"Ahahah... basi ikifika somo la Mathe kila mtu anachoka," akasema Efraim Donald.
"We, acha! Utajaribu kuchagua combi yoyote ile ili kuiepuka, lakini ndiyo ilikuwa imeziganda zote," akasema Blandina.
"Ma-pythagoras theorem na ma-logarithm yalikuwa yananiacha hoi," Esma akaongea.
"Me yaani hata nilikuwa siyakumbuki hayo majina," Namouih akasema na kumfanya Esma acheke.
"Halafu sasa ikifika wakati wa paper, mtu anaomba ile, kuna kitabu fulani kidogo cha mahesabu..."
"Four Figure," Esma akamkumbusha Efraim.
"Ee Four Figure. Unaiomba kama show tu yaani hauifanyii kitu, unajikuta uko makini kweli kufanya ma-calculation," Efraim Donald akaongea hivyo na kufanya wengine wacheke kidogo.
Wakati huu, wanawake walikuwa wanajipakulia vyakula, kisha Namouih akaanza kumpakulia mume wake. Blandina naye akaanza kumpakulia Draxton, na ilikuwa ni kama alifanya hivyo ili kumchengua rafiki yake ingawa hilo halikuwa lengo lake kihalisi. Alitaka tu kumwonyesha Draxton kwamba alimjali sana, naye Draxton akamwonyesha tabasamu la shukrani. Blandina alipotaka kumwekea mboga za majani, mwanaume huyu akamwambia asiweke.
"Hauli majani?" Efraim Donald akamuuliza.
"Ndiyo, huwa... sili mboga za majani," Draxton akamwambia.
"Kwa nini?" Namouih akauliza.
Hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza anamsemesha tangu alipofika hapo, naye Draxton akamwangalia tu.
"Una allergy?" Blandina akamuuliza Draxton huku akiwa ameacha kumwekea.
"Yeah, unaweza kusema hivyo," Draxton akajibu.
Namouih akafanya ile cheko kwa pumzi wanayofanyaga wanawake ya bila kutoa sauti huku akiangalia chini, kwa njia fulani ya dharau, na Blandina akawa amemwona.
"Nafahamu jamaa fulani mhindi... alikuwa akila majani tu, hey! Asubuhi anaamka na mapele shingoni mpaka mgongoni. Unajua kuna allergy ambazo huwa zinaua," akasema Efraim.
"Yeah ni kweli. Mimi nikila huwa najihisi vibaya sana... kama kuumwa," akasema Draxton.
"Kwa hiyo we' ni nyama tu... eti?" Namouih akamuuliza.
"Pamoja na vyakula vingine," Draxton akajibu na kuanza kula.
"Watu wanaokula majani tu na siyo nyama huwa kwa kiingereza wanaitwa vegetarians, eti?" akauliza Esma.
"Ndiyo," akajibu Efraim Donald.
"Vipi wale wanaokula nyama tu?" Esma akauliza tena.
"Nyamatarians," Blandina akamjibu kiutani.
Hilo likafanya wengine wacheke.
"Unaiga ile ya took inakuwa tookunti?" Efraim Donald akamwambia Blandina, naye akacheka kidogo.
"Nakutania mwaya. Ila sijui wanaitwaje labda mpaka tutafute Google," Blandina akamwambia Esma.
"Wanaokula nyama pekee hufuata mlo unaoitwa carnivore diet. Kwa hiyo wanaitwa carnivores," Draxton akamwambia Esma.
"Ahaa... umesema cani...." Esma akauliza.
"Carnivores," Draxton akamwambia.
"Halafu kweli, hiki kitu kama tuliwahi kusoma kwenye biology," akasema Blandina.
"Nitayakumbuka sasa?" Efraim Donald akasema, nao wakacheka kidogo.
Namouih akamtazama Draxton akila taratibu, kisha akamuuliza, "Unakulaga nyama za aina zote?"
Draxton akatulia kidogo, kisha akatikisa kichwa kukubali.
"Hadi za watu?"
Blandina akashusha kijiko alichokuwa karibu kuingiza mdomoni na kumtazama Namouih kwa mkazo baada ya yeye kuuliza swali hilo.
Draxton akakiangalia tu chakula chake bila kutoa jibu kwa hilo swali.
"Hahah... honey, matani gani tena hayo?" Efraim akamuuliza mke wake huku akiendelea kula.
"Ahah... yeah, nilikuwa natania tu. Manyamatarian wengi sana siku hizi," Namouih akaongea, ikiwa ni kwa njia ya kejeli.
"Ahahahah... natamani ningeweza kuwaona mnavyochuana kwenye hiyo kesi ya Agnes, nione moto wenu. Ulisema ana miaka mingapi?" Efraim Donald akamuuliza mke wake.
"Ana 19. Mbakaji wake ana 26," Namouih akajibu huku akimtazama Draxton kama vile anamwambia yeye.
"Mechi za kombe la dunia zinaanza hivi karibuni. Unafatilia?" Draxton akamuuliza Efraim, akiwa amebadili mada upesi.
"Yah! Haloo, ninaitabiria mambo makubwa sana Senegal ingawa Mane atakosa, wana kikosi kizuri sana," Efraim Donald akasema.
"Ndiyo ni kweli. Hata Morocco pia, wanacheza vizuri sana," Draxton akamwambia.
Efraim Donald akaanza kuzungumzia mambo fulani kuhusu soka, huku Draxton akimsikiliza, naye Namouih akaendelea kula. Aliponyanyua macho yake kumwangalia Blandina, akakuta anamtazama tu, kwa njia iliyoonyesha kwamba alikasirishwa na jambo fulani. Namouih akauliza kupitia macho 'vipi,' naye Blandina akaacha kumwangalia na kuendelea tu kula huku akionekana kukosa shangwe aliyokuwa nayo mwanzoni. Esma aliona hilo pia, lakini akakausha tu na kuendelea kula.
Namouih hangehitaji kukisia kuhusu ni nini kilichomkwaza rafiki yake, alijua kabisa kwamba Blandina alikasirishwa na jinsi yeye alivyomtendea Draxton. Akaendelea tu kula pia, huku maongezi ya hapa na pale yakiwasindikiza vizuri mpaka walipomaliza mlo na kushiba. Draxton alionyesha ustaarabu mzuri sana kwenye kula, na Blandina alifurahia sana uwepo wake hapo. Wanaume wakaelekea tena kwenye masofa huku sasa Efraim akimwambia Draxton kuhusu usafirishaji wa mizigo na magari kwenda nje ya nchi, na wanawake wakasaidiana kupeleka vyombo sehemu ya jikoni.
Walipofika tu huko, Namouih akimwambia Esma awapishe yeye na Blandina kwanza, na dada huyo akatii na kuwaacha.
"Okay, najua kuna kitu kiko kifuani kwako kwa hiyo, ropoka," Namouih akasema.
"Usifikiri sijui ulichokuwa unajaribu kufanya," Blandina akasema kwa mkazo.
"Kufanya nini? Nimetukana mtu?"
"Namouih naomba tuheshimiane. Kama shida ni mimi kumleta Draxton hapa ungeniambia nikaacha, siyo kuanza kumfanyia vile..."
"Hivi kweli Blandi... yaani unanikasirikia mimi rafiki yako wa miaka mingi over a guy you just met yesterday? Na uko tayari kabisa kugombana nami kisa nini, nime...."
"Ni maisha yangu. Mimi huwa siji kutoka sehemu yoyote kukuamulia namna unavyotakiwa kuiendesha ndoa yako, kwa hiyo naomba uyaache maamuzi yangu kuwa yangu," Blandina akaongea kwa hisia kali.
Namouih akabaki kimya, kwa kutambua kwamba Blandina alikasirika sana.
"Ulivyomfanyia imekupa faida gani? Ili iweje? Tena unafanya hivyo mbele yangu bila kujali nitakavyohisi?"
"Blandi...."
"Unauliza kama anakula nyama ya mtu kumaanisha ye' ni mchawi au? Unamfanyia hivyo kwa kuwa mnapingana kwenye kesi au ni chuki tu isiyokuwa na maana yoyote ile? Namouih sijapenda. Ulivyofanya ni vibaya, na sitawahi tena kuja kukanyaga hapa," Blandina akasema.
"Blandina... sikia... mimi... sioni kama huyo kaka anakufaa... kabisa... sidhani kama yuko...."
"Naomba uniache tu Namouih. Niache nichague yeyote nayetaka. Wewe siyo mama yangu kuniamulia nitakayekuwa naye kama wa kwako alivyokuamulia wa kukuoa!" Blandina akasema kwa mkazo.
Namouih akaishia tu kumwangalia rafiki yake kwa huzuni, ambaye alitoa maneno hayo kuonyesha ni jinsi gani alikuwa amevunjwa moyo na yale aliyomtendea mtu wake. Blandina akampita Namouih na kuondoka kutoka hapo jikoni, akimwacha mwanamke huyu bila amani moyoni.
Efraim Donald na Draxton walipatana vizuri sana, na mume huyo wa Namouih hata akamwomba namba za simu kijana huyu mwenye akili iliyompendeza mno. Muda wa dakika kadhaa ambazo Blandina na Draxton waliendelea kuwa hapo, walipiga story tu na kushushia vinywaji taratibu mpaka Blandina aliposema alitaka kuondoka na "rafiki" yake, yaani Draxton. Hakuwa amedhamiria waondoke mapema sana, lakini kwa sababu ya kilichotokea, mwanamke huyu hakujihisi vizuri kuendelea kubaki hapo. Namouih alikuwa akitafuta hata nafasi ndogo tu ya kuongea na Blandina tena, lakini aliona wazi jinsi rafiki yake huyo alivyomkwepa ingawa si moja kwa moja, kuonyesha bado alikuwa amekasirika. Hivyo mwishowe wakaagana, ikiwa ni saa nne ya saa tano sasa, na wawili hao waliofika hapo kama wageni wakaondoka hatimaye.
Wakiwa wamerudi ndani baada ya wageni kuondoka, Efraim Donald akamuuliza Namouih kuhusu suala la yeye kumsemesha Draxton kwa njia mbaya, akimwambia kwamba alijifanya tu kama hakuona matendo yake, ila aliyaona. Namouih, tayari akiwa hana amani baada ya Blandina kumwonyesha ameudhika, akasema tu kwamba hakuwa na nia mbaya, lakini Efraim Donald akamrekebisha na kusema hiyo haikuwa sahihi kwa kuwa huenda kijana yule alijihisi vibaya. Lakini akamwambia tu apotezee jambo hilo kwa kuwa bila shaka lingesahaulika, nao wakaanza kufanya maandalizi ya kujipumzisha.
★★
Wakiwa mwendoni kuelekea kwake Blandina, Draxton alimwambia mwanamke huyu namna ambavyo alifurahia ushirika wake (company). Akaweka wazi jinsi alivyofurahia chakula na ushirika wa marafiki zake Blandina, na mwanamke huyu akawa anatafuta njia ya kumwombea Namouih samahani kwa jinsi alivyotenda kumwelekea, lakini akawa anashindwa. Alihisi jambo hilo lingeharibu maongezi yao mengine, lakini pia alitaka tu lisahaulike.
Wakiwa wamefika kwake Blandina hatimaye, Draxton akasimamisha gari usawa wa geti la nyumba hiyo, naye akamtazama machoni mwanamke huyu aliyekuwa anamwangalia kwa upendezi mwingi.
"Hii ndiyo part tunayosema 'goodnight,' siyo?" Draxton akamwambia.
"Mbona bado mapema kusema 'goodnight?'" Blandina akasema hivyo huku akilaza kichwa chake kwenye siti aliyokalia, na akimtazama mwanaume kwa uvutio.
Draxton akatabasamu na kusema, "Okay. Good-before-night."
Blandina akatabasamu na kusema, "Bado haitoshi."
"Nini huwa kinatosha kwenye hii dunia?"
"Kwangu mimi... labda ni kujua tu kwamba hii haitakuwa mara ya mwisho tunafanya hivi..."
"Una matarajio mengi sana juu yangu eti?"
"Ndiyo. Niambie unataka nifanye nini ili yatimie..."
"Sitarajii chochote Blandina. Wewe ni mwanamke mzuri, lakini kwenda unakotaka nahisi itakuwa kuharakisha mno."
"Unaogopa mapenzi ya mwendokasi eeh?" Blandina akaongea hivyo huku akianza kutembeza kidole chake kwenye mkono wa Draxton taratibu.
"Nilikuwa hata sijafikiria ikiwa ungetumia hilo neno leo," Draxton akamwambia.
Blandina akamsogelea karibu na uso wake, naye Draxton akaupitisha mkono wake usawa wa ubavu wa mwanamke huyu ili aegamie hapo.
"Ulikuwa hujafikiria ningesema neno... mapenzi?" Blandina akamwambia hivyo karibu kabisa na mdomo wake.
Draxton akatulia kidogo, kisha akatikisa kichwa kukanusha huku akimwangalia mdomoni.
"Ungependa nikuonyeshe linamaanisha nini?" Blandina akasema kwa sauti ya deko.
"Tayari najua linamaanisha nini, ila...."
"Bado hujalijua kutoka kwangu," Blandina akamalizia maneno ya jamaa.
Draxton akahisi kiganja cha Blandina kikitembea taratibu kutokea pajani kwake na kuelekea mpaka sehemu ya kati ya suruali yake. Hisia murua zilikuwa zimeanza kuwavaa wawili hawa, naye Blandina akawa anafurahia sana pumzi za taratibu kutoka kwa Draxton karibu na mdomo wake, na akihisi jinsi mtambo wa jamaa ulivyoanza kuwa mgumu pole kwa pole.
"Twende ndani..." Blandina akasema kwa sauti iliyoonyesha hisia nzuri sana.
Draxton akaacha kumtazama mdomoni na kuangalia mkono wa bibie ulioshika sehemu yake ya kati, kisha akasema, "Nahisi ni kama... nitaharakisha... sijui kama niko tayari..."
"Mhmhm... basi mimi nitakuongoza..." Blandina akasema kwa maringo.
Kisha mwanamke huyu akaanza kuibusu midomo ya Draxton taratibu, naye Draxton akawa anamruhusu aendelee kufanya hivyo. Blandina alikuwa ameingiwa na hamu kubwa sana ya kutaka kulionja penzi la mwanaume huyo kijana kiasi kwamba akaendelea kumbusu kimahaba sana na kuongeza kasi, lakini Draxton akaivunja busu yao na kuketi sawa zaidi. Blandina akawa anamwangalia usoni kwa hamu sana, lakini akijiuliza kwa nini aliivunja busu ghafla.
"Draxton... kuna tatizo?" Blandina akauliza huku akitembeza kiganja chake kidevuni kwa Draxton.
Draxton akiwa amefumba macho, akatikisa kichwa kukanusha.
"Mbona hivyo?" Blandina akauliza.
Draxton akamtazama kwa ufupi, akiona jinsi mwanamke huyo alivyokuwa na hamu kweli, naye akasema, "Hamna tatizo. Nafikiri... itakuwa... itakuwa vizuri zaidi tukienda ndani."
Blandina akaachia tabasamu la furaha na kuung'ata mdomo wake wa chini kidogo, kisha akatikisa kichwa kukubali na kutoka ndani ya gari. Draxton akashika usukani kwa nguvu sana na kufumba macho yake, naye akawa anapumua kwa nguvu kiasi ili kujipa utulivu. Alipofumbua macho, akamwona Blandina akiwa amesimama getini huku akitazama upande wa gari, hivyo mwanaume akajiweka sawa na kutoka pia. Akafunga gari vyema na kumfata Blandina, nao wakaingia ndani kule baada ya msichana wa kazi kufika na kuwafungulia geti. Aliitwa Hamida.
Nyumba aliyoishi Blandina ilikuwa ya kupanga, yaani yote kwa ujumla alikuwa analipia yeye akiwa mpangaji pekee. Ilikuwa nzuri yenye rangi ya blue na madirisha yenye vioo vyeusi vikubwa, na ndani palikuwa pazuri sana pia, kukiwa na vifaa vingi vya kisasa vilivyopangiliwa vyema kwenye vyumba vyote hapo. Akawa anamwambia Draxton jinsi ambavyo hakuwahi kuwa na mpango wa kujenga nyumba, lakini ikiwa angepata pesa za kutosha kununua nyumba kabisa, angenunua. Muda wote Blandina aliozungumza, Draxton alikuwa kimya, akimfuata tu kwa ukaribu mpaka walipoingia ndani kwenye sehemu ya sebule na msaidizi wake wa kazi kusimama pembeni yao kama vile anasubiri kuambiwa kitu fulani.
Blandina alipomwangalia msichana wake wa kazi, akatambua kwamba alikuwa anamtazama Draxton kwa upendezi mwingi, na hilo likamkera.
"Ulikuwa umeshalala?" Blandina akamuuliza.
"Ndiyo nilikuwa nime..nimejilaza, ila sikusinzia," Hamida akajibu.
"Haya we' rudi ukalale. Tutaonana kesho," Blandina akamwambia na kuweka pochi yake ndogo mezani.
Draxton akamtazama Hamida na kukuta anamwangalia kwa njia fulani hivi ya uvutio, naye Blandina akaona hilo.
"Haujanisikia au?" Blandina akauliza kwa sauti ya juu kidogo.
"Sawa dada..."
Hamida akajibu hivyo haraka na kuondoka, huku kalio lake nene kiasi likitikisika kwa nyuma ndani ya dera alilovaa. Blandina akasonya kidogo, naye Draxton akatabasamu.
"Usiwe hivyo," Draxton akamwambia.
"Nini, we' hujaona alivyokuwa anafanya hapo? Sijui yukoje," Blandina akasema kwa kukereka.
"Unakasirikia hicho tu, je ukinikuta nimesimama na mwanamke mwingine?"
"Namuua, halafu wakinikamata unakuja kupiginia kesi yangu ili nitoke."
Draxton akacheka kidogo na kutazama pembeni.
Blandina akamsogelea na kupitisha mikono yake kiunoni mwake, akiigundisha miili yao huku anamwangalia usoni. "Tulikuwa wapi kweli?" akauliza kwa sauti ya chini.
Draxton akapitisha mikono yake mgongoni kwa Blandina, akifanya kama kumkumbatia, kisha akaanza kuilamba shingo ya mwanamke huyu kwa njia fulani kama vile anataka kuitafuna... taratibu. Blandina hakuwa ametarajia kabisa kwamba Draxton angeanzia hapo, lakini msisimko uliomwingia ukamfanya ahisi kulegea na kuanza kutoa miguno kwa pumzi za mdomo. Mwanamke naye hakuwa nyuma; akapeleka mkono wake wa kushoto mpaka sehemu ya kati ya suruali ya jamaa na kuanza kupavuta-vuta, na sasa Draxton akawa analiminya kalio la bibie kwa nguvu na kulizungusha-zungusha kwa njia iliyompa mhemko mwingi sana Blandina. Alikuwa amewaza kwamba labda wangefanyiana haya wakiwa chumbani, ila hata kuanzia hapa hapa haikuwa mbaya, kwa sababu tayari penzi lilikuwa mwendoni.
Draxton akaiacha shingo ya Blandina na kuifata midomo yake sasa, nao wakaanza kunyonyana ndimi kwa uzito, huku sasa Blandina akiwa anafungua kifungo cha suruali ya Draxton na kuelekea kuishusha zipu yake. Draxton alikuwa anaongeza kasi katika busu zake na tomasa, akiwa kama anamsukuma Blandina kuelekea ukutani, na kwa kukosa mhimili kidogo Blandina akaitoa mikono yake kwa chini na kumshika kiunoni na shingoni. Lakini ni baada ya kumshika shingoni ndiyo mwanamke huyu akafumbua macho na kuvunja denda yao ili amwangalie Draxton vizuri. Alipoigusa shingo ya mwanaume huyu, Blandina alihisi joto kali sana kama vile alikuwa ameshika nguo iliyopigwa pasi kwa muda huo huo. Draxton akawa anapumua kwa uzito kiasi, huku sasa akiangalia chini, na bado miili yao ikiwa karibu.
"Draxton... uko sawa?"
Blandina akamuuliza hivyo, lakini Draxton akamwachia na kurudi nyuma kidogo, akipumua vile vile, na akijishika magotini kama mtu aliyechoka baada ya kukimbizwa kwa muda mrefu. Blandina akamsogelea na kuishika shingo yake tena, lakini joto kali la hapo likamfanya aiachie upesi sana.
"Draxton... mbona unachemka hivi... shida ni nini?" Blandina akauliza hivyo akiwa haelewi kilichokuwa kinaendelea.
Draxton hakujibu lolote, bali akageuka tu na kuanza kuondoka. Tena hadi akaanza na kukimbia kabisa kuelekea nje. Ajabu!
Blandina akaanza kumfata huku akimwita sana, lakini mwanaume huyo akatoka mpaka nje kabisa na kwenda kwenye gari lake. Blandina alipofika nje, tayari Draxton alikuwa ameshaligeuza gari na kulitia mwendoni kutoka maeneo hayo. Dada wa watu akabaki kusimama hapo nje akiwa ameachwa na butwaa zito, hisia nzuri za kimahaba zilizokatizwa, na maswali mengi sana kichwani. Alijihisi vibaya sana kwa sababu ya kitendo cha Draxton, naye akawa anataka kujua ni nini kilichomsibu mwanaume huyo mpaka akaamua kukimbia namna hiyo.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments