CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TISA
★★★★★★★★★★★★
Asubuhi iliyofuata, tayari Namouih alikuwa ofisini kwake. Kupitia na kuandaa-andaa mambo kadhaa kabla muda wa hukumu ya kesi ya Agnes mahakamani ilikuwa lazima, naye alikuwa ametafutwa na mama yake Agnes kuulizwa ikiwa mambo yangekwenda safi. Tena, na hapa Namouih akamkumbusha kwamba yeye siyo mwamuzi wa mwisho wa matokeo ya kesi hiyo, na ingawa upande wao ulionekana kuwa na nguvu zaidi ya kushinda, wangepaswa tu kusubiri matokeo huko huko mahakamani, na yeye alikuwa amejiandaa vyema kumpigania Agnes mara hii ya mwisho.
Basi, imefika mida ya saa tatu asubuhi, Blandina akawa ameingia ndani ya ofisi ya Namouih na kumkuta akiwa makini kuandika mambo fulani kwenye karatasi mezani kwake. Namouih aliponyanyua uso na kuona ni rafiki yake, akasitisha kuandika na kuendelea kumtazama. Blandina alikuwa amevalia kiblauzi cheupe kilichofunikwa kwa koti jekundu la kike, sketi nyeusi iliyoishia magotini na viatu virefu vya rangi nyekundu. Alipendeza. Akasimama tu sehemu ya mlangoni huku akitazamana na Namouih kwa hisia, kisha akapiga hatua mbili mbele na kusimama tena.
"Samahani Nam... uko bize?" Blandina akauliza kwa ustaarabu.
Namouih akalifunika kablasha lenye karatasi alilokuwa akiandikia, kisha akanyanyuka na kutoka upande wake wa meza na kuanza kumfata Blandina huku amenyoosha mikono yake mbele kuonyesha alitaka kumkumbatia. Blandina akapiga hatua chache mbele pia na kukutana naye, kisha marafiki hawa wakakumbatiana kwa upendo. Walielewana sana. Namouih alikuwa amevalia gauni refu lililoubana mwili wake kiasi kufikia kwenye supu za miguu, lenye rangi ya damu ya mzee na nyeupe, viatu vyekundu vya kuchuchumia, na nywele zake akizibana kwa nyuma kama kawaida. Wakaendelea kukumbatiana kwa sekunde chache, kisha wakaachiana na kushikana mikono kwa chini wakiwa karibu bado.
Blandina akaanza kusema, "Nam, I'm so sorry kwa jinsi nilivyozungumza jana, yaani...."
"Worry out mpenzi. Mimi ndiyo nikuombe aamahani kwa kweli. Nilivyofanya haikuwa poa. Nilidhani labda hata ungenichukia," Namouih akamwambia.
"Hapana, siwezi. Naomba tu tuyasahau eti? Ninaomba radhi tena kwa maneno yangu."
"Usiwaze mommy. Ila, nakuomba utengue kauli moja tu kwenye yale uliyosema..."
"Ndiyo... chochote."
"Usije kuacha kurudi kwangu tena," Namouih akasema.
Blandina akatabasamu na kutikisa kichwa kukubali. Namouih akaanza kuzishika nywele za rafiki yake kwa njia ya kuzichezea kidogo.
"Umechelewa kufika leo?" Namouih akauliza.
"Ee kidogo, nilipita kule garage kulifata gari. Wameshalitengeneza," Blandina akasema.
"Ahaa... sawa. Utakuwepo baadaye kusikiliza hukumu?"
"Ndiyo nitakuja."
"Okay. Oh, ona, kuna ishu moja nimepokea. Njoo," Namouih akamwambia.
Akaelekea mezani kwake tena na kuketi, huku Blandina akikaa kwenye kiti cha upande wa mbele wa meza hiyo akimtazama kwa umakini kusikiliza atakachosema.
"Kuna hii kesi mpya nimechukua, inahusu mtoto fulani wa miaka 12. Anasoma darasa la sita. Mwalimu wa somo la Historia amempiga sana na kumuumiza vibaya mno. Yuko hospitali amelazwa, na huyo teacher amefunguliwa mashtaka na wazazi wa huyo mvulana... wanataka afungwe," Namouih akaeleza.
"Huyo mwalimu ni mwanaume?" Blandina akauliza.
"Yeah."
"Kisa cha kumuumiza mtoto ni nini?"
"Huwezi amini. Yaani nasikia eti aliuliza swali darasani 'what is history?' huyo mvulana akajibu 'Clouds FM,' ndiyo kikawaka," Namouih akasema.
Blandina akaanza kucheka na kufunika mdomo wake kwa kiganja chake, naye Namouih akatabasamu na kutikisa kichwa chake kwa njia ya kusikitika.
"Acha masihara basi!" Blandina akasema.
"Well, inawezekana dogo alikuwa tu analeta ujanja, au ni utukutu kama unavyojua watoto lakini kumpiga mpaka anaenda kulazwa siyo jambo sahihi kabisa..." Namouih akaongea.
"Ila kweli..."
"Ingewezekana hii system ya kutandika wanafunzi iondolewe lingekuwa jambo bora maana walimu wengi wanaitumia vibaya na kuvuka mipaka hadi kuwatendea watoto kama ng'ombe... na sijui wanapata faida gani kuona watoto wakikaa kulialia tu..." Namouih akasema.
"Wanazitoa hasira zao hapo pia. Ng'ombe kwa jina la mwanafunzi ndiyo itikadi ya shule nyingi, na walimu watafanyaje? Wana-enjoy," Blandina akasema.
"Well, huyu jamaa lazima apewe fundisho, hili haliwezi kufumbiwa macho, na ninahitaji kukupatia ili ulishughulikie."
"Seriously?"
"Yeah. Sidhani kama litafika mahakamani huko ukili-handle vizuri kabisa kama kawaida yako. Utaweza bila shaka, si ndiyo?"
"Yeah I mean, ndiyo, nitaweza. Asante Nam-Nam," Blandina akakubali kwa shauku.
"Ahah... usijali. Ngoja nimalize kuandika mambo fulani, yapitie, then utai-handle. Ukipenda kukutana na mama yake baadaye namba yake ya simu na detail zingine zitakuwa hapa..."
"Sawa."
Namouih akaendelea kuandika huku akisema, "Baadaye nataka kuongea na Draxton, nimwombe samahani pia kwa sababu ya jana. Mliliongelea hilo mlipoondoka?"
"Hapana, na... sidhani kama alilikazia fikira sana. Potezea tu Namouih... ishapita," Blandina akasema.
"Yeah, ila bado nakuwa na kahisia kabaya moyoni maana nilitenda kitoto sana. Nitaongea naye tu kwa njia nzuri ili kuwa peace naye zaidi. Si unajua na hii kesi ya Agnes na Japheth mambo yanaweza yakawa...."
Namouih akaishia hapo baada ya kumwangalia Blandina na kuona ametazama sehemu moja kama anatafakari jambo fulani.
"Blandina..." Namouih akaita.
Akashtuka kiasi na kuitika, "Bee?"
"You good?" Namouih akauliza.
Blandina akatikisa kichwa kukubali, lakini Namouih akaona jambo fulani usoni kwake, kama huzuni.
"Kuna tatizo lingine?" Namouih akauliza.
Blandina akabaki kumtazama tu.
Namouih akaacha kuandika kabisa na kusema, "Niambie."
Blandina akashusha pumzi na kusema, "Ni Draxton."
"Amekufanyaje?"
"Hajafanya kitu... yaani... hajanifanya kitu..."
"Unamaanisha nini?"
"Jana tulirudi home... nikamkaribisha ndani... things were going great yaani... nilipoanza tu ku-make out pamoja naye, akabadilika ghafla na kuondoka," Blandina akaeleza.
"Katikati ya... in the middle yaani, akaondoka tu?"
"Tena siyo kuondoka tu, akakimbia kabisa. Sikumwelewa yaani, sijui ana shida gani? Au ndiyo yale mambo ya Yusufu na mke wa Potifa?"
"Mh... hilo nalo jipya."
"Nimejaribu kumpigia, wapi. Nimejaribu kum-text, nothing... hajajibu mpaka sasa hivi..."
"Tatizo linaweza kuwa nini? Anawezaje kuikimbia keki tamu kama hii? Anaumwa?"
"Ahah... sijui tu. We were hugging, and kissing... mara akaanza kuchemka sana, tena sana yaani. Nilipomuuliza tatizo nini, akaondoka tu," Blandina akaongea hivyo na kupiga ulimi ndani ya mdomo kwa njia ya kusikitika.
Namouih akabaki kutafakari jambo hilo kwa uzito sana.
"Just when I thought I'd wake up in bliss this morning (yaani nilipodhani tu kwamba ningeamka vizuri asubuhi hii)," Blandina akasema huku ameangalia chini.
"Ongea naye baadaye tukienda court. Lazima kutakuwa na explanation, sidhani kama yeye ni mjinga," Namouih akasema.
"Ndiyo, lakini mie ndiyo nabaki kuonekana kama mjinga. Amefanya hivyo, lakini bado nam-feel sana..."
"Yaani utafikiri siyo wewe! Unamkubali mno yaani... kupita maelezo?"
"Mno. Mpaka nashindwa kuelewa ni kwa nini."
"Mwambie. Mwambie hivyo ajue uko serious naye. Anaonekana kuwa mwerevu sana, kwa hiyo subiri tu usikie atakachosema," Namouih akamwambia.
Blandina akaupokea ushauri huo wa rafiki yake vizuri, na baada ya hapo Namouih akampa kablasha lile lenye taarifa za kesi ya mwalimu aliyemjeruhi mvulana mdogo, kisha akamuaga na kurudi kule nje kwenye ofisi yake binafsi.
Namouih aliachwa kimawazo baada ya kusikia kile Blandina alichomwambia. Alikuwa tayari kuweka pembeni maoni yake mabaya kumwelewa Draxton, ila baada ya rafiki yake kumpa ubuyu huo ikawa ni kama mashaka yake kumwelekea jamaa yakaamshwa tena. Kama tu alivyomuuliza Blandina muda mfupi nyuma, aliwaza sana ni kitu gani ambacho kingemfanya mwanaume yule amkimbie mwanamke mzuri kama rafiki yake, naye akawa anahofia kwamba huenda alificha kitu fulani kama ugonjwa au chochote ambacho kingemwathiri na rafiki yake pia endapo angeendelea kuwa naye kimahusiano.
★★
Ilitimia mida ya saa saba kamili mchana, na watu wote muhimu waliohitajika pale mahakamani wakawa wamefika. Baraza la wazee wa mahakama lilikuwepo pia, sambamba na waamuzi, na sasa ushahidi ule uliohitaji kuhakikiwa ulikuwa tayari. Agnes tayari alikuwa amefanyiwa vipimo na daktari tofauti na yule mwingine siku iliyopita, na majibu yalikuwa tayari. Video ile pia ilikuwa imehakikiwa na kuwekwa tayari kwa ajili ya maelezo ambayo yangetolewa kufikia hukumu iliyostahili.
Upande wa mtoa mashtaka, Namouih akatoa maelezo yake kuhusiana na hukumu aliyoona ilistahili kutolewa kwa sababu ya mambo yote hayo. Aliwaasa waamuzi kuona namna ambavyo vitendo vya kikatili kwa wanawake vinavyowaharibia mfumo wa maisha na kuwafanya washindwe kusonga mbele katika nyanja mbalimbali, hivyo akaomba mahakama itende kwa jicho kuu kuelekea suala hilo kwa kumpa Agnes alichostahili; haki. Upande wa mtuhumiwa, Draxton akaomba Japheth apewe hukumu ya kuachiliwa (judgement of acquittal), akisema kwamba upande wa mtoa mashtaka haujatoa ushahidi wa kutosha na sahihi kuthibitisha kwamba mtuhumiwa amefanya kosa, kwa hiyo akaiomba mahakama iamue kesi hiyo katika upande wa mtuhumiwa (favor).
Baada ya wawili hao kumaliza kazi yao hiyo, wakatulia sasa ili hatimaye vigezo vyote kupelekea hukumu ya mwisho visomwe. Hakimu akaanza kusoma marejeo muhimu kuelekea kesi hii ya ubakaji. Msichana wa miaka 19 kwa jina la Agnes Mhina alidai kwamba kijana aliyeitwa Japheth Warioba alimbaka usiku wa siku fulani wawili hao walipokutana kwenye nyumba ya wageni ili kuzungumza. Aliripoti tukio hilo kwa askari siku 3 baadaye, na ndiyo kijana huyo akakamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa sababu ushahidi wa jambo hilo ulikuwepo. Lakini kutokana na mambo fulani kuwa na dosari ndani ya ushahidi uliotolewa, baraza la waamuzi lilifikia mkataa kwamba ungepaswa kuhakikiwa kabla ya saa hii ya hukumu, na ndicho kilichofanyika.
Wakati hakimu alipokuwa akisema hayo, Agnes alionekana kuwa na wasiwasi mwingi sana kiasi kwamba ikabidi Namouih amtulize kwa kumshika viganja. Hakimu akaendelea kusema kwamba baada ya majibu ya vipimo kutoka, iligundulika kwamba msichana huyu hakuwa na vidonda sehemu zake za siri, ambavyo bado vingekuwepo endapo kama kweli angekuwa ameingiwa kimwili kwa njia iliyomuumiza sana. Akaeleza kwamba walikuwa wameshamhoji daktari yule wa maabara ndogo aliyetoa vipimo bandia na kugundua kuwa alikuwa mpenzi wake Agnes, na wawili hawa walitunga hadithi hii ya uwongo ili kumkomoa kijana yule bila kueleweka sababu ni nini ya kutaka kumfanyia hayo. Kwa jicho la haraka yeyote angeweza kusema kwamba hiyo ni kwa sababu walitaka afungwe na kuwalipa kiasi cha faini ambacho Agnes alitakiwa kupewa.
Kwa upande wa ile video, ni kweli kwamba wawili hao walifanya mapenzi siku hiyo, lakini baada ya Japheth kuwa amehojiwa pia siku iliyopita aliweka wazi kwamba usiku ule yeye na Agnes walipokutana walikunywa kileo kidogo, ila inaonekana alileweshwa kwa sababu alikuja tu kuamka asubuhi akiwa ameachwa bila nguo mwilini. Kwa hiyo, Agnes na aliokuwa anashirikiana nao wakaitengeneza vizuri na kuitia sauti kwa njia ambayo ingefanya ionekane kweli msichana huyu alibakwa, lakini Agnes akaja kujichanganya mwenyewe kwa kusema alizibwa mdomo na Japheth. Agnes alikuwa analia sana huku akimwangalia mama yake mara kwa mara kwa njia iliyoonyesha hofu, na Namouih akiwa ameshatambua hiyo ingeelekea wapi, akafumba macho yake kwa kusikitika.
Kutokana na mambo hayo, hakimu akatoa hukumu ya kumwachilia huru Japheth Warioba haraka iwezekanavyo, na kusema kwamba Agnes angetakiwa kubaki chini ya ulinzi kutokana na kutoa madai ya uwongo chini ya kiapo cha mahakama. Japheth alifurahi sana. Akapeana mikono na Draxton huku akimshukuru kutoka moyoni mwake kwa kumsaidia sana. Kwa upande wake Agnes, binti alishikwa na askari wa ulinzi hapo na kutiwa pingu, kwa kuwa alikuwa amebaki na mambo mawili ya kufanya baada ya jambo la hila yeye na wenzake walilopanga kutofanikiwa: alipie faini kubwa sana, au apewe kifungo jela.
Baada ya hakimu kuondoka, askari aliyemshikilia Agnes akaanza kuondoka pamoja naye huku binti huyo akimlilia mama yake. Mama yake mwenyewe alikuwa amekaa tu kwenye benchi huku ameifunika midomo yake kwa kiganja, akionekana kuwa na huzuni sana. Yote hayo yalikuwa kwa ajili gani? Ndugu za Japheth walimshukuru sana Draxton hapo, kisha wakaanza kuondoka kuelekea nje baada ya ushindi wao. Namouih akamfata Draxton na kumnyooshea mkono wa pongezi ya kirafiki, naye Draxton akaushika na kukubali pongezi hiyo. Kisha mwanamke akaenda kwenye meza aliyokuwa ameketi na kuanza kukusanya vilivyo vyake, ikiwa ndiyo mara ya kwanza kabisa kwake kupoteza kesi tokea alipoanza mlolongo wake wa uanasheria (career).
Blandina bado alikuwa mahakamani humo baada ya kumaliza pindi hiyo iliyokuwa na msisimuo wa hali ya juu. Wakati tu Namouih alipomaliza kupeana mikono na Draxton, wawili hawa wakatazamana kwa sekunde kadhaa. Ulikuwa utizami ulioongea mengi, na ilionekana kwamba Draxton alikuwa anajaribu kuisoma akili ya mwanamke huyu kutokana na jinsi alivyoangaliwa. Blandina akanyanyuka tu kutoka alipokuwa ameketi na kuanza kuelekea nje, naye Draxton akaanza kuelekea huko pia. Namouih aliona jambo hilo, na ingawa alitamani kujua yale ambayo yangeendelea huko nje, angepaswa tu kusubiri kuja kusikia rafiki yake angesema nini.
Yeye Namouih akatoka nje pia na kuwawahi watu wa familia yake Japheth, ambao bado walikuwa eneo hilo la nje la mahakama. Akawapa pongezi kwa kupata ushindi, na akakazia kwamba kumtetea Agnes ilikuwa ni sehemu ya kazi yake kwa sababu wanasheria hawatakiwi kuhukumu vitu kwa misingi yao binafsi tu, lakini bado akamwomba radhi Japheth kwa kilichompata. Japheth akasema Mungu amekuwa mkubwa kwake kwa kumletea mwanasheria Draxton, kwa sababu alidhani angekwenda jela na hivyo hakungekuwa na mtu wa kuitunza familia yake na mama yake ambaye alikuwa mgonjwa.
Namouih akauliza namna ambavyo kijana huyu alikutana na Draxton, akitaka kujua kama walifahamiana sana, lakini Japheth akasema hapana; hakumfahamu sana mwanasheria yule. Ni kwamba Draxton alimtafuta Japheth yeye mwenyewe na kusema angemsaidia, lakini mwanzoni hakutaka ajulikane ndiyo maana akamwambia atulie tu mpaka siku ya kusikilizwa kesi ndiyo angejitokeza, na alikuwa mtu mmoja makini aliyemwahidi kabisa ushindi. Namouih alishangazwa kiasi na jinsi ambavyo Draxton alikuja ghafla tu ndani ya kesi hii na kuonyesha kipawa kikubwa sana kilichofunua mambo kwa njia sahihi kabisa ambayo haingekuwa rahisi kwa yeyote kufanya. Yaani bila Draxton, mtu yeyote yule angeamini kabisa kwamba Japheth alimbaka Agnes, kwa hiyo mwanamke huyu akawa anataka kujua mengi zaidi kuhusu mwanaume huyo.
Wakati huo, Blandina alikuwa akielekea pale alipoegesha gari lake, bila kugeuka nyuma hata mara moja, lakini alijua wazi kwamba Draxton alikuwa anamfata. Alipoufikia mlango wa mbele wa gari lake, sauti ya Draxton ikasikika akimwita kabla hajaingia ndani ya gari. Blandina akatulia tu, lakini hakuitika wala kugeuka, naye Draxton akawa amefika nyuma yake.
"Blandina... tunaweza kuongea?" Draxton akasema kwa sauti ya chini.
"Tuongee nini? Hauna mambo mengine ya kukimbilia?" Blandina akauliza pia kwa sauti ya chini.
"Kuhusu jana. Nahitaji kuomba samahani..."
Blandina akamgeukia, kisha akasema, "Nilidhani uko tofauti na wanaume niliowapitia, na kiukweli uko tofauti. Ila ni utofauti nisiouelewa kabisa, kwa hiyo nakuomba unieleweshe nini maana ya kile ulichofanya jana."
"Sina sababu yoyote ya kujitetea kwa nilichokifanya..."
"Mmmm... kwa hiyo unataka uniacheje?"
"Utakavyoamua tu Blandina. Ona, sikufanya vile kwa nia ya... labda kukuumiza...."
"Unaumwa?" Blandina akamkatisha.
"Naam?"
"Unaumwa? Kama una ugonjwa fulani labda unaogopa kuusema, au unaogopa labda...."
"Kwamba nitakuambukiza? Nini, kama UKIMWI?"
"Me sijasema hivyo, ni wewe. Vipi, ndiyo hali halisi au?"
"La Blandina... siumwi ugonjwa wa namna hiyo."
"Sasa shida ni nini? Kwa nini uli... au labda una tatizo la kutoamsha kwa muda mrefu?"
Draxton akatabasamu na kuangalia chini.
"Niambie tu nijue. Jana Draxton, ulisema natakiwa kuonyesha kwamba nataka kutulia. Ninakwambia sasa hivi kwa uhakika kabisa. Ninataka kutulia nawe," Blandina akasema kwa uhakika.
Draxton akamwangalia tu machoni kwa hisia.
"Ahah... naonekana kama zumbu yaani... ila ndiyo ukweli. Nataka tuendelee kuwa... well, tuanzishe jambo zuri baina yetu. Na, sidhani kama tutafika mbali endapo labda una tatizo, au mwanamke mwingine, halafu hautaki kusema. Ni bora nikajua," Blandina akasema kwa hisia.
"Kama nikikwambia nina tatizo?" Draxton akauliza.
"Tatizo gani?"
"Sina tatizo Blandina, ila... niseme tu nina muda mrefu sijawa na mwanamke na... jana nilikuwa overwhelmed."
"Okay, sawa haina shida, si ilikuwa mizuka tu? Kama hauna tatizo basi...."
"La. Blandina... sidhani kama mimi na wewe tutafika huko unakotarajia," Draxton akamwambia.
"Kwa nini?"
"Iko hivyo tu."
"Ahah... sikuelewi... yaani..."
"Sitaki kukupa sababu yoyote kwa nini iko hivyo, na wala sitaki uje ujute kuwa na mtu kama mimi."
"Kwani wewe ukoje? Draxton hujanipa sababu yoyote kuhisi labda utaniumiza. In fact, sijawahi kukutana na mwanaume kama wewe, ni utofauti wako ndiyo unaonifanya nitake sana kuwa nawe..."
"Blandina..."
"Draxton mimi nimekupenda. Nimekupenda," Blandina akasema kwa hisia.
"Usiharakishe kufikiri hivyo. Kumpenda mtu huchukua muda, na kumjua, na...."
"Mimi sihitaji muda Draxton, ninajua nimekupenda. Uko sahihi. Uko sahihi. Ninataka sana kupendwa kwa dhati na ndiyo maana ni rahisi kwangu kupenda. Lakini kwa wakati huu, ninataka... ninahitaji kupendwa na wewe. Sijui ikiwa unaniona kama mjinga...."
"La..."
"... lakini nimekupenda wewe Draxton. Kama kweli hauna tatizo, ninakuomba unipende pia," Blandina akamalizia maneno yake.
Draxton akainamisha uso wake.
"Kuna njia nyingi sana za kufurahishana, si lazima sex. Nisamehe kwa kuwahi kukimbilia huko ikiwa hauhitaji hilo kwa sasa, lakini bado nakuhitaji sana. Nataka... nataka tu kuwa nawe. Unanifanya najihisi tofauti sana, na ndiyo maana nakuwa nataka kuendelea kufurahia hilo," Blandina akaongea kwa hisia.
"Hata baada ya nilichokifanya jana na kukwambia mambo haya, yaani bado...."
"Najua una sababu zako, lakini hata usiponiambia kwa sasa haitakuwa na shida. Ninakuamini. Draxton... nakupenda."
"Oh Blandina..."
Draxton aliona kweli mwanamke huyu aliamini kile ambacho alikisema yeye mwenyewe, na ingawa alikuwa anajaribu kumtolea mbali, jinsi alivyomwonyesha uhitaji wa kuwa naye ni jambo lililomvutia sana kihisia kumwelekea. Blandina akakishika kiganja kimoja cha Draxton huku akimtazama kwa hisia za mapenzi ya dhati kabisa, na mwanaume huyu akakibana kiganja cha bibie kiasi.
"Nimejaribu sana kuepuka wengi, lakini wewe... huepukiki," Draxton akamwambia.
"Najua nina mvuto kwako... sema tu unajishaua," Blandina akasema.
Draxton akatabasamu kwa mbali, kisha akasema, "Sawa. Blandina... ninajipa nafasi ya kuwa nawe, maana ukweli ni kwamba... ninatamani kupendwa pia."
Blandina akatabasamu.
"Nitajitahidi kuwa mzuri kwako, ila...."
"Achana mambo ya ila bwana. Just be you. Napenda sana jinsi ulivyo. Nitakupa furaha Draxton, mimi ni wako kuanzia sasa, na sitaruhusu chochote kinichukue kutoka kwako," Blandina akasema.
"Wow. Una maneno mazuri sana. Huwa unapiga zoezi kwenye kioo?"
"Ahahahah... practice makes perfect. Ila no, haya yanatoka moyoni. Nataka ushibe ukiwa na mimi..."
Draxton akatabasamu, naye Blandina akacheka kidogo kwa haya.
"Hongera kwa ushindi wa kesi," Blandina akasema.
"Asante. Unaelekea wapi now?" Draxton akamuuliza.
"Siendi kokote. Wewe?"
"Kuna... kazi fulani nataka kufanya... naelekea nje ya jiji."
"Mh! Unaondoka kabisa?"
"Ahahah... la. Nitarudi jioni. Vipi tukikutana muda huo?"
Blandina akatabasamu na kusema, "Sawa. Ila siyo kwamba unataka kinikimbia tena?"
"Ahahahah... sitakukimbia tena, usinikariri hivyo. Nataka kuwa pamoja nawe pia. Na-enjoy company yako."
"Mimi pia Draxton."
Draxton akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, kisha akamkumbatia kwa wororo. Blandina hakuwa ametarajia kukumbatiwa eneo hilo la mahakamani, lakini hii ikampa furaha sana na yeye kulirudisha kumbatio la mwanaume huyo kwa upendo. Draxton akamwachia na kusema angempigia baadaye, naye Blandina akakubali. Mwanaume akaondoka hapo kuelekea kwenye gari lake, naye Blandina akamtazama kwa ufupi na kisha kuishika simu yake na kuanza kupitia mambo fulani.
Alipoangalia upande mwingine wa eneo hilo la mahakama, akamwona Namouih akiwa amesimama huku anamtazama, na rafiki yake huyo akamwonyesha ishara kwa kichwa kuuliza 'vipi?' Blandina akanyanyua tu dole gumba kuonyesha mambo yako safi, na Namouih akatikisa kichwa na kuonyesha ishara ya kumwambia kwamba wangeongea baadaye, kisha marafiki hawa wakaachana na kuingia kwenye magari yao ili kuondoka hapo.
★★
Muda mfupi baadaye, Namouih akawa amerudi ofisini kwake baada ya kuvunjiwa rekodi ya kutopoteza kesi hata moja toka alipoianza kazi yake, akiwa amepigania kesi kubwa 34 na kushinda zote isipokuwa hii. Sikuzote alichukua kesi ambazo alikuwa na uhakika wa kupata ushindi, na hata kesi ya Agnes ilionekana kabisa kuwa ya ushindi kwake. Lakini mwanaume yule, Draxton, akawa amemfumbua macho zaidi kwa wakati huu ili asijiamini kupita kiasi wakati mwingine, hasa kwa kuwa jambo hilo lilifanya ionekane kama alikuwa anafanya kazi kwa mazoea.
Wakati huu, Blandina alikuwa ameondoka kwenda kukutana na mama wa mvulana yule aliyelazwa baada ya kupigwa vibaya sana na mwalimu wake, ili afahamiane naye na kuanza kushughulika na mashtaka aliyotoa. Hivyo Namouih akawa ofisini kwake akijaribu kutafuta taarifa za ndani kuhusiana na mwanasheria Draxton. Alisaka mambo mengi, lakini aliyoyapata yalikuwa yale ambayo tayari aliyafahamu. Hakukuwa na habari zozote juu ya familia yake, mahali alikoishi, wala sehemu aliyosomea sheria na kwa muda gani. Kwa kumtazama tu kijana yule alikuwa na umri mdogo sana kuweza kuwa amemaliza masomo ya sheria na kupata uzoefu wa kutetea kesi mahakamani, kwa hiyo alitaka kujua tu hata kitambulisho chake cha uanasheria kilitoka wapi.
Ilimshangaza kiasi kuona jinsi ambavyo habari nyingi za mwanaume yule ziliwekwa usiri wa hali ya juu, naye akafikiria kuja kuongea na Blandina kuhusu hilo na kuona angesemaje. Ikawa imefika mida ya jioni ya saa kumi, naye akapigiwa simu na kujulishwa kwamba Agnes alikuwa ameachiliwa kutoka rumande baada ya kulipiwa dhamana kubwa sana. Akauliza ni nani ambaye alikuwa amemlipia pesa hizo, naye akaambiwa kwamba haikujulikana ni nani kwa sababu zilipelekwa na mwakilishi ambaye hakusema mengi sana kujihusu, bali baada tu ya kumtoa Agnes, binti akafurahi sana na kuondoka pamoja naye wakisema wanaenda nyumbani.
Namouih akifikiri kwamba ilikuwa ni mtu wa karibu na familia ile, akaamua kumpigia mama yake Agnes na kumuuliza kuhusu hilo, lakini mama ya Agnes akashangaa na kuanza kuuliza kwa shauku ikiwa kweli Agnes aliachiliwa. Jambo lililomchanganya Namouih kiasi lilikuwa kwamba binti huyo alitakiwa kuwa amepelekwa nyumbani kwao lakini bado hata mama yake hakujua kama ameshatoka. Akamwambia tu mama yake kwamba amtafute, na yeye Namouih angemtafuta pia. Akawa anawaza labda aliyemtoa alikuwa mtu wake mwingine mwenye mipango naye ya kiulaghai-laghai, naye akatikisa kichwa chake kwa kusikitika baada ya kukumbuka namna ambavyo alidanganya sana kuhusu kubakwa.
Baadaye, Blandina akawa amerejea na kumwambia Namouih kwamba alikuwa amemaliza kuwapanga wazazi wote wa mvulana yule, na kwamba lazima mwalimu aliyetenda ukatili kwa mtoto angefungwa. Akamwambia pia kwamba ana mipango jioni hiyo ya kukutana na Draxton baada ya wao kuwa wapenzi rasmi sasa, naye Namouih akauliza vipi kuhusu kitendo kile cha jamaa kumkimbia, aliamua kukipotezea tu? Blandina akamwambia hilo waliliweka pembeni kwanza, na yeye alichoangalia zaidi kwa wakati huu ilikuwa kufurahia uhusiano wake mpya na Draxton kwa njia yoyote ile ambayo ingekuwepo, na akamwomba Namouih amuunge mkono kwa hilo.
Namouih akiwa hataki kumkwaza rafiki yake, akaona asimwambie kuhusu yeye kuyachunguza maisha ya Draxton na kusema anamuunga mkono kwa asilimia zote kabisa. Blandina akafurahi sana. Akamwambia kwa sababu hawakuwa na kazi za lazima basi watoke kwenda kupata kinywaji huku yeye Blandina akisubiri Draxton arejee. Akasema alikuwa ameshawasiliana naye, na leo wakikutana tena alitaka mambo baina yao yapambe moto. Namouih hakuwa na kipingamizi kwa hilo, naye akafunga kompyuta yake na kuanza kuondoka pamoja naye huku akimwambia kuhusiana na suala la Agnes kuachiliwa kutoka kifungoni.
Wawili hao wakaelekea katikati ya jiji na kuingia ndani ya kumbi moja kubwa sana iliyokuwa imechangamka. Ni sehemu ile ile ambayo marafiki hawa walipendelea kwenda mara nyingi. Wanaume kadhaa na wanawake waliwashobokea mno, lakini wawili hawa wakaketi kivyao sehemu ya pekee na kuletewa vinywaji walivyoagiza. Wakaendelea kufurahia maongezi ya hapa na pale wakikumbushia na kesi ya leo mpaka inafika saa mbili usiku, ndipo simu yake Namouih ikaita.
Akakuta namba ngeni kabisa, na baada ya kupokea na kuzungumza kidogo, akaweka uso ulioonyesha mshangao mkubwa sana. Blandina akaanza kumuuliza tatizo ni nini, naye Namouih akamalizia maongezi hayo kwa kusema ameielewa sehemu hiyo na kwamba anakwenda huko upesi. Alipoishusha simu, akamwangalia rafiki yake kwa njia ya mshangao sana, naye Blandina akauliza shida ni nini kwa mara nyingine tena.
"Agnes... Agnes ameuawa Blandina!"
"Ati?!!" Blandina akashangaa.
"Oh Allah..." Namouih akasema na kuinamisha uso wake kwa kusikitika.
"Nam... nini kimetokea?" Blandina akauliza.
"I don't know... wamenipigia simu... mwili wake umepatikana huko.... nahitaji kwenda ili nijue nini kimetokea..." Namouih akasema huku akisimama.
"Tunaweza kwenda pamoja. Ngoja nimwambie Draxton..."
"Hapana Blandina, usijali. Wewe msubiri Draxton... mengine yatafata baadaye. Nitakupigia," Namouih akasema.
"Sawa... kuwa mwangalifu..." Blandina akamwambia.
Marafiki hawa wakakumbatiana na kuagana, naye Namouih akamwacha rafiki yake hapo na kuelekea kwenye gari lake ili aende huko ambako kisa hiki kipya kilikuwa kimezuka.
Majanga yalikuwa hayaishi. Aliyekuwa amempigia alimwambia kwamba kule kwenye eneo la tukio bado maaskari hawakuwa wamefika, na namba yake Namouih ndiyo ya mwisho kuipigia simu ya Agnes walipoipata sehemu aliyouliwa. Eneo hilo halikuwa mbali sana kutokea pale Namouih na Blandina walipokuwa, kwa hiyo haikuwa ngumu mno kwa Namouih kufika huko. Ilikuwa ni kwenye nyumba ndogo tu isiyojulikana mmiliki wake ni nani, na baada ya Namouih kufika hapo aliweza kuona watu wakiwa wamekusanyika kwa nje kuzunguka sehemu ya kuingilia ndani kule.
Akalisimamisha gari lake umbali mfupi kutokea hapo, naye akashuka na kumpigia simu Efraim Donald ili amwambie alikokuwa kwa kuwa aliona kwamba angechelewa kwenda nyumbani kwa sababu ya dharura hii. Lakini alipogeuza shingo yake upande mwingine wa eneo hilo, akaona jambo fulani lililofanya mkono wake ulioshika simu ushuke taratibu mpaka chini. Huko aliweza kuona gari lile jeusi aina ya Frester, na mtu aliyefungua mlango wa sehemu ya kuingilia dereva hakuwa mwingine ila Draxton mwenyewe!
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments