CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI
★★★★★★★★★★★★★★
Namouih akaendelea kumwangalia na kumwona anaingia ndani ya gari lake hilo, kisha likawaka na kuanza mwendo kutoka eneo hilo. Alishangaa sana. Draxton alikuwa anafanya nini huku? Si Blandina alisema kwamba mtu wake huyo alikuwa anarejea kutoka safari fupi nje ya mji wao na kwenda kumpitia ili wakajivinjari? Alikuwa anafanya nini huku karibu kabisa na nyumba ya tukio la mauaji ya binti ambaye ni yeye mwenyewe Draxton ndiye aliyemfichua leo kuwa mwongo? Kulikuwa na uhusiano wowote kati yake na jambo hilo lililokuwa limetokea?
Maswali mengi sana yakaendelea kupita kichwani kwake Namouih, na hakuwa ametambua kwamba wakati huo aliokuwa amezubaa, mume wake upande wa pili alikuwa amepokea simu wakati ule Namouih ameushusha mkono wake, na baada ya Efraim Donald kuona kimya tu, akakata na kumpigia tena. Namouih akashtushwa na mtetemo wa simu yake, ndipo akapokea na kumwambia Efraim yaliyojiri. Mume wake akatoa pole na kusema ajitahidi kuwa mwangalifu na asisogelee chochote mpaka maaskari wafike hapo, ndipo simu ikakatwa baada ya hapo.
Namouih akatulia kidogo na kutazama upande ule ambako Draxton alionekana muda mfupi nyuma. Yaani kama ni mashaka basi yalikuwa yameongezeka zaidi hata sasa, naye akatazama tena kule kwenye ile nyumba ambayo alijua binti yule angekuwemo. Hakujua hata ni jinsi gani alivyokuwa ameuawa, hivyo akatafuta namba ya mama yake Agnes na kumpigia ili ampe taarifa hizo. Lakini akasitisha kufanya hivyo baada ya gari tatu za maaskari kufika hapo, na nyingine aliyoitambua upesi sana baada ya kuzisoma namba zake za usajili. Ilikuwa ni Toyota Prado nyeupe ya yule rafiki yake mpelelezi, yaani Felix. Mwanamke akaanza kulielekea pale lilipoegeshwa, huku sasa baadhi ya waandishi wa habari wakianza kufika eneo hilo na kamera zao.
Maaskari waliofika hapo wakaanza kuwaambia watu wasogee pembeni ili waingie kule ndani, na waandishi wa habari wakielekea huko pia ili kuchukua tukio hilo. Felix akawa ameshuka kutoka kwenye gari lake akiwa pamoja na wapelelezi wengine wawili, naye akamwona Namouih akimfata. Akamuuliza alikuwa anafanya nini hapo, ndiyo Namouih akamweleza kwamba msichana aliyetaarifiwa kwamba ameuawa ni mtu aliyetoka kumsimamia kwenye kesi mapema ya siku hii, hivyo alikuwa hapo kujua ni nini kilichotokea. Felix akamwambia angoje hapo ili aende kule ndani kuona kama tukio hilo lilikuwa na uhusiano na mambo yale aliyokuwa anapeleleza, naye akaelekea huko pamoja na wenzake akimwacha Namouih anasubiri hapo nje.
Baada ya muda mrefu kupita, Namouih akaanza kuwaona maaskari wale wakiutoa mwili wa aliyeuawa ukiwa umefunikwa kwa shuka kuuzunguka wote, nao wakaupeleka kwenye moja ya magari yao ili bila shaka upelekwe mochwari. Hatimaye Felix akawa ametoka ndani huko pia, huku akijitahidi kuwakwepa waliokuwa wanawauilza maswali, naye akamfata Namouih mpaka karibu ili aanze kumweleza kilichotokea.
"Vipi Felix? Nini kimempata Agnes?" Namouih akauliza.
Felix akashusha pumzi na kusema, "Yale yale mambo niliyowaambia Namouih."
"Nini?!" Namouih akasema kwa mshangao.
"Mwili wake wa baridi sana. Sehemu ya chini ya tumbo lake imekatwa na... hana ulimi mdomoni. Ni mambo yenye kutisha sana," Felix akasema.
Namouih akawa ameuziba mdomo wake kwa kiganja, akionekana kuhuzunika sana.
"Kibaya zaidi ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyemwona wakati anaingia hapo, na haijulikani aliingia na nani. Tumeuchunguza mwili wake lakini hauna fingerprint zozote wala clue yoyote iliyoachwa ambayo inaweza kutusaidia kumkamata anayefanya haya... inakera sana..." Felix akaongea kwa hasira.
"Ina maana... Felix jamani... haya mambo yataendelea mpaka lini?" Namouih akauliza.
"Yaani hata sielewi. Hii ndiyo mara ya kwanza kisa kama hiki kimetokea ndani ya nyumba. Namaanisha... kwa kawaida tungewakuta wakiwa wamefukiwa au sehemu za nje kama mara ya mwisho... lakini huyu... inaonekana muuaji wake alikuwa na haraka sana leo... lakini bado hatujawa na njia ya kutambua ni nani hasa," Felix akamwambia.
"Felix... chunguzeni kwa umakini zaidi. Kwa watu wengi hili litakuwa jambo jipya, lakini unajua kabisa kwamba limeendelea kwa muda mrefu sana. Hawa watoto wanakufa hivi kwa nini? Tafadhali... fatilia kwa kina ujue ni nani ambaye alimtolea dhamana huyu msichana leo, kwa sababu ndiyo huyo huyo aliyemleta huku. Yaani me hata sikupewa taarifa yoyote ile, mama yake hajui mtoto yuko wapi, halafu sasa hivi apewe tu taarifa kwamba amempoteza? Aah!" Namouih akasema hivyo kwa mkazo.
"Ondoa shaka Namouih, tutazama zaidi kwenye hili. Nikwambie tu kiukweli... naona afadhali sasa hivi kwamba jambo hili litakuwa wazi kwa wengi maana sikuona faida yoyote ya kulificha kwa muda mrefu... ni hasara kubwa tu ndiyo tuliyoendelea kupata. Kila kitu watashughulikia watu hawa kwa hiyo... wewe nenda nyumbani kapumzike..." Felix akamwambia.
"Lakini vipi kuhusu.... "
"Usijali Namouih. Wewe nenda tu. Tutawasiliana," Felix akasema.
Namouih alionekana kuwa ndani ya taharuki nzito sana, kwa sababu jambo hilo lilimfanya aumie mno. Kuna ile hali fulani ya kuhisi hatia iliyompata kwa sababu hakufatilia mambo vizuri baada ya kupewa taarifa kwamba Agnes ametolewa kifungoni na mtu asiyejulikana mpaka janga hilo kutokea. Lakini pia ni suala la Draxton kuonekana eneo hilo ndiyo lililomchanganya zaidi. Kama kwa kufikiria tu labda alipata taarifa za kifo cha Agnes na kuja huku lingekuwa wazo la haraka kuingia akilini, basi ni nani aliyempa taarifa? Hapana. Hapa alihisi kabisa kwamba mwanaume yule alikuwa akifanya mchezo mbaya sana, na kama angeendelea kuachiliwa hivi hivi tu basi huenda mambo haya mabaya yangeendelea kutokea.
Akaingia ndani ya gari lake akiwa ameghafilika sana, naye akaona ampigie Blandina simu ili amjuze kuhusu mambo yaliyokuwa yametokea. Baada ya Blandina kupokea na kuuliza kulikoni, Namouih akaeleza wazi namna Agnes alivyouawa, na rafiki yake huyo akahuzunika sana na kutoa pole. Namouih akamuuliza ikiwa wakati huu tayari alikuwa na Draxton, naye Blandina akakubali, akisema kwamba Draxton alikuwa akimpeleka yeye Blandina kumwonyesha alipokaa jijini hapo. Namouih aliingiwa na wasiwasi sana. Ni ile fikira ya kwamba huenda Blandina angejikuta ndani ya hali kama iliyomkuta Agnes kwa sababu ya kupelekwa asikokujua na mwanaume huyo mwenye njia fulani za siri mno, lakini angeweza vipi kumwambia rafiki yake huyo kwa njia ambayo isingemuudhi au kumkwaza kama ilivyotokea usiku wa jana?
Namouih akamwambia Blandina awe mwangalifu sana kwa sababu vitendo hivi vya kikatili vingeweza kutokea sehemu yoyote ile, naye Blandina akamwambia asiwaze kwa sababu alikuwa salama mikononi mwa Draxton. Namouih akakata simu na kuinamisha kichwa chake kwenye usukani kwa kusikitika sana, na akihofia mengi. Hakuwa na uhakika kuhusu kile alichokihisi kumwelekea Draxton, lakini machale yake yalimwambia kwamba yule hakuwa mtu mzuri kabisa. Na sasa huenda rafiki yake kuwa pamoja naye kungeleta matatizo hata zaidi. Akasali kwa Mungu ili ampe ulinzi Blandina, naye akawasha gari lake na kuanza kuondoka eneo hilo ili aende nyumbani.
★★
Upande wa wapendanao, yaani Blandina na mpenzi wake mpya kwa jina la Draxton, walikuwa mwendoni ndani ya gari la mwanaume huyu baada ya kukutana. Muda ule ambao Namouih alimwacha Blandina na kwenda kufuatilia tukio la Agnes, mwanamke huyu alimtafuta Draxton kwa simu na kuuliza kama alikuwa amesharejea jijini, naye Draxton akasema hakuwa mbali sana hivyo Blandina ajiandae tu naye angempitia kwake. Kwa hiyo Blandina alitoka hapo na kwenda nyumbani kwake ili kujiweka vizuri zaidi kimwili kwa ajili ya kukutanika kwake na mpenzi wake huyo.
Baada ya Draxton kumfikia Blandina saa kama moja baada ya hapo, mwanamke akapanda ndani ya gari lake akiwa amependeza sana na kuuliza ni wapi walipokuwa wanaenda. Ndiyo Draxton akamwambia alitaka kumpeleka akapaone pale alipoishi, na alikuwa na mpango mzuri sana kwa ajili ya mrembo huyu. Hisia nzuri sana za Blandina kumwelekea mwanaume huyo zilimfanya asahau hata ishu ya Agnes kuuawa na kufurahia tu nafasi hiyo ya kuwa pamoja na Draxton, na ndipo walipokuwa mwendoni kuelekea huko akapigiwa simu na Namouih, ambaye alimjuza kuhusu yaliyotokea na kumwambia awe mwangalifu.
Alipokata simu, Blandina akamwangalia Draxton na kusema, "Hivi umeshasikia?"
"Kusikia nini?" Draxton akauliza.
"Agnes ameuawa Draxton," Blandina akasema.
Draxton akatulia kidogo, bila hata kuonyesha mshangao wowote wa kinafiki, naye akasema, "Ndiyo. Nafahamu hilo."
"Mbona hujaniambia?"
"Nilijua tayari ungekuwa unafahamu, na sikutaka kuharibu wakati wetu huu mzuri..."
"Mm... Draxton! Yule mtoto unajua tumetoka tu kumwona leo mahakamani halafu unasema hivyo?"
"Samahani. Ila ni kweli... sikutaka hilo jambo liingilie mambo yetu. Itakuwa mbaya sana tukifurahia usiku huu kwa sababu Agnes amekufa? Ikiwa unataka tunaweza kuahirisha...."
"No, Draxton sijamaanisha hivyo. Roho tu inaniuma. Namouih ndiyo ananiambia sasa hivi kwamba ameuliwa kikatili sana, kama tu wasichana ambao...."
Blandina akaishia hapo baada ya kukumbuka kwamba kitu alichotaka kusema hakutakiwa kukisema.
Draxton akamwangalia na kuuliza, "Kama wasichana ambao?"
Blandina akaangalia mbele ya gari na kubaki kimya.
"Kuna jambo fulani ambalo ni kuu sana hapa eti?" Draxton akauliza.
"Hapana," Blandina akasema.
"Niambie Blandina. Unaweza kuniamini," Draxton akasema.
Blandina akamtazama, kisha akaanza kumwambia mambo yote ambayo rafiki yake mpelelezi, yaani Felix, alikuwa amewaambia yeye na Namouih siku kadhaa nyuma kuhusiana na vifo vya wasichana matineja waliouawa kwa kukatwa matumbo yao. Akamweka wazi kuwa muuaji hakuwa amepatikana mpaka sasa, na watu waliokuwa wanafanya upelelezi walificha tu mambo hayo mpaka wakati huu. Draxton alikuwa anamsikiliza kwa umakini sana, naye akasema kwa kweli mambo yote hayo hayakuwa mazuri hata kidogo, na ingehitajika nguvu ya ziada kwa waliofanya uchunguzi kuweza kumbaini msababishi wa mambo hayo ili watu wasiendelee kupoteza maisha.
Basi, baada ya mwendo wa dakika kadhaa, Draxton akalisimamisha gari lake nje ya nyumba fulani kubwa iliyozungushiwa uzio wa ukuta mrefu. Akamwambia Blandina kwamba hapo ndipo alipoishi, ikiwa ni nyumba ya kupanga, na kulikuwa na wapangaji wengine watatu na familia zao. Yaani ilikuwa ni kubwa sana kutoshea vyumba zaidi ya vinne au zaidi kwa kila mpangaji hapo, lakini yeye Draxton alikuwa amechukua vyumba vitatu tu na choo na bafu. Akamkaribisha Blandina kwenda ndani, na mpenzi wake huyo akaanza kuongozana naye mpaka ndani ya geti la nyumba hiyo.
Kweli walikuta baadhi ya watu hapo, nao wakawasalimia vizuri na kuwapita kuelekea mpaka upande wenye vyumba vyake Draxton. Wanawake watu wazima waliokuwepo hapo walimwangalia mno Blandina, tena kwa njia za husuda, na mwanamke huyu alilitambua hilo wazi lakini ndiyo kwanza hakuwa na muda nao. Wawili hawa wakaufikia mlango wa chumba cha Draxton, na jamaa akaufungua na kumwambia mrembo apite ndani. Blandina alipenda sana jinsi ambavyo ndani kwa mwanaume huyo kulipangiliwa vyema sana. Kuanzia zulia kubwa chini, vitu vya samani, TV ndogo ya bapa (flat screen) ukutani, masofa matatu yenye rangi nyekundu, yaani palikuwa pasafi sana.
Blandina akawa anapaangalia huku akitabasamu, kisha akamgeukia Draxton na kuuliza, "Unaishi na nani humu?"
"Peke yangu tu," Draxton akasema.
"Mmmm..." Blandina akaguna hivyo huku akimwangalia kwa njia iliyoonyesha hamwamini.
"Ahahahah... nini sasa?"
"Sidhani. Hao wamama walivyokuwa wananiangalia hapo nje, yaani kama siyo mmoja wao basi wote umeshawanyandulia humu ndani," Blandina akasema.
Draxton akaipitisha mikono yake kiunoni mwa mrembo na kuusogeza mwili wake karibu naye huku akitabasamu na kusema, "Mbona una wivu sana?"
"Mm... yaani me niwaonee wivu hao? Nitakuwa nimekosa kazi ya kufanya labd...."
Kabla Blandina hajamaliza maneno yake, Draxton akaifata midomo yake na kuanza kumtandika denda ya taratibu sana, naye Blandina akazungusha mikono yake nyuma ya shingo ya jamaa akijibu busu hiyo kwa upendo. Kisha Draxton akaikatisha na kumwangalia usoni.
"Nimekuchagua wewe tu. Usiwaze kabisa kuhusu mambo ya nje," Draxton akamwambia kwa ukaribu.
"Unanipenda Draxton?" Blandina akauliza kwa njia ya deko.
Draxton akatikisa kichwa kukubali.
"Basi kwa nini ulinitesa?"
"Kumaanisha?"
"Siku ile... ulipoondoka tu ghafla... nilipata shida sana... ulinlacha pabaya..."
Draxton akainamisha uso wake.
"Draxton... niambie tu shida ilikuwa nini. Sitakusumbua tena juu ya hili. Ni nini kilikupata?" Blandina akauliza kwa hisia.
Draxton akamwachia na kukishika kiganja chake, kisha akaanza kumvuta kuelekea ndani ya chumba ambacho alitumia kulala. Palikuwa pazuri sana pia, nao wakafika na kukaa kwenye kitanda chake kikubwa chenye godoro laini; lililofunikwa kwa shuka jeupe na safi sana. Blandina alikuwa anamwangalia sana kwa subira, akiwa anataka kusikia angesema nini.
"Nahitaji kukuomba samahani Blandina... kweli nilivyofanya siku ile haikuwa vizuri. Kuna... hali fulani ambayo huwa inanipata... unaweza kuchukulia ni kama jinsi allergy yangu kwa mboga za majani inavyofanya nihisi kuumwa... ni hivyo hivyo pia inapokuja kwenye suala la sex...." Draxton akamwambia.
Blandina akawa ameshindwa kuelewa. "Unamaanisha... kila mara ukitaka... au mwanamke anapotaka kufanya sex nawe, unaanza kuumwa?"
"Ni kama hivyo."
"Kwa nini? Una allergy na sex?"
Draxton akabaki kimya na kuangalia tu chini.
"Nielezee Draxton. Hiyo hali yako inakuzuia kuwa na mwanamke kwa nini? Ni nini kinakusumbua? Umeshawahi kwenda kwa daktari...."
"Blandina..."
"... ukajaribu kuona tatizo ni nini? Labda kuna tiba, Draxton... unamaanisha hauwezi ku-share nami mapenzi?" Blandina akauliza kwa hisia.
"Najua vitu hivyo havieleweki vizuri, lakini... ndiyo hali halisi. Nikijaribu kukupa penzi... sitafanikiwa. Nimekuja nawe hapa kukuweka wazi juu ya hilo kwa kuwa Blandina... nimevutiwa nawe pia. Nina... nina hisia za kimapenzi kwako. Ila nahitaji kujua kama utakuwa tayari kuendelea kuwa nami nikiwa namna hii... kwa sababu nilijaribu kukukwepa ila nikashindwa kwa kuwa umeniingia sana. And this is ridiculous yaani... najua kabisa haitapatana na akili wewe kuwa nami kama hatutaweza...."
Blandina akamkatisha kwa kumkumbatia kwa upendo, naye Draxton akafumba macho taratibu.
"Hakuna kinachoshindikana Draxton. Nilikwambia mimi ni wako, na sitaruhusu chochote kinichukue kutoka kwako. Unaamini hilo?" Blandina akaongea akiwa bado amemkumbatia.
Draxton akabaki tu kimya.
Blandina akamwachia na kumwangalia usoni. "Unaamini kwamba nakupenda Draxton?" akamuuliza.
"Naamini. Sema... naogopa Blandina..." Draxton akasema.
"Ahah... unaogopa nini mpenzi wangu?" Blandina akauliza huku anaushika uso wake.
Draxton akatulia kidogo na kisha kusema, "Naogopa kukupoteza Blandina."
Blandina akaachia tabasamu la hisia, kisha akasema, "Hautanipoteza. Usijali. Sijakupenda tu kwa sababu ya jambo hilo, nimekupenda wewe kama ulivyo. Hilo tatizo lako... labda tutalipatia ufumbuzi baadaye... lakini nina imani mimi nawe tutafika mbali."
Draxton akabaki kumtazama kwa njia iliyoonyesha hisia nyingi sana kwake, naye Blandina akamsogelea mdomoni mwake na kuanza kumbusu kimahaba sana. Ingawa alitaka jambo hilo lielekee mbele zaidi, akajitoa mdomoni mwake na kuendelea kumshikilia usoni.
"Ninafahamu mtu mmoja ambaye hajawahi kupeana mapenzi na mume wake toka walipooana... na wanapendana vizuri tu. Sijui hiyo huwa inakaaje lakini... kwangu mimi haitakuwa na shida sana Draxton," Blandina akasema.
"Kweli? Hata tuseme miaka ikipita? Utaweza kuvumilia?"
"Mhmhmhm... tutapaswa kusubiri kuona mambo yatakavyokuwa. Ila ninajua upendo wangu kwako ni mkubwa kuliko hata sex..."
Kauli hiyo ikamfanya Draxton acheke kwa chini.
"Blandina... sitataka kukuumiza. Ikifika hatua ukaona kwamba hautaweza kuendelea nami wewe achana nami tu... najua kuna wanaume wengi watakaoweza kukupa vile mimi nimeshindwa...."
"Hivi Draxton kwa nini unapenda kuwa negative sana? Si nimetoka kukwambia kwamba hilo siyo tatizo? Usiongee hivyo tena, me sipendi. Kwani hao wanaume siwaoni? Mimi nimekuchagua wewe regardless... ungekuwa hauna mkono, au mguu, au jicho, jua nimekupenda wewe. Please..." Blandina akaongea kwa uhakika.
Draxton hakuwa na namna ila kumwacha mwanamke huyu aamue kwa namna ambavyo moyo wake ulimsukuma. Yeye pia alivutiwa naye, lakini hali yake isiyoeleweka ilimfanya ahisi labda angemwonea sana kama wangeendelea kuwa na uhusiano kwa njia hii, lakini kwa sababu mwanamke alionyesha kuwa na uhakika kwenye uamuzi wake, basi mwanaume akaona asimkwaze.
Kwa hiyo wawili hawa wakaendelea kupata maongezi, na kuna mambo fulani ambayo Draxton alisema kujihusu yaliyomshangaza sana Blandina, lakini bado hisia zake kwake zilikuwa zenye nguvu mno na hivyo aliyachukulia mambo yote hayo kuwa kawaida. Mwanaume hata akapika kwa ajili yao wote, nao wakala na kulala pamoja usiku huo uliokuwa mzuri sana kwa Blandina kutokana na kuweza kulala ndani ya kumbatio la mwanaume wake.
★★★
Usiku huo ulipita, na sasa ikiwa ni siku mpya ya Alhamisi, tayari vyombo vingi vya habari vilikuwa vimeshatangaza tukio lile la mauaji lililompata Agnes Mhina, na tayari mama na ndugu zake walikuwa wamezipata taarifa. Maaskari kama kawaida yao walitoa ahadi kwamba muuaji angepatikana tu, lakini bado ukweli kuhusu vifo vya namna hiyo kuwa vimetokea kwa muda mrefu ukafichwa, yaani haikuwekwa wazi kwamba tukio kama lililompata Agnes limekuwa likiendekea kwa muda mrefu sana. Maandalizi ya msiba wa Agnes yalianza upesi, kukiwa na watu wengi wa familia yake na marafiki waliokwenda kumfariji mama yake.
Namouih pia alikuwa amepanga kwenda msibani huko siku ya leo na kesho ili kutoa pole yake. Usiku uliotangulia baada ya yeye kufika nyumbani, alieleza kile alichoona kwa Efraim Donald kuhusiana na Draxton, akimwambia alimwona mwanaume yule eneo la tukio kisha akaondoka upesi sana. Aliwaza kwamba huenda alikuwa pale kwa sababu fulani, lakini ni kwa nini awe hapo wakati alikuwa amemwambia Blandina kwamba ameenda nje ya jiji? Akasema alihisi jamaa alificha jambo fulani, naye angetakiwa kumwambia Felix kuhusu ishu hiyo. Mume wake akamwambia Namouih aache kuwaza mbali sana kwa sababu hiyo ingesababisha aanze kufikia mikataa asiyokuwa na uhakika nayo. Jambo hili lingetakiwa kuachwa mikononi mwa polisi, na kama alikuwa na mashaka basi amuulize Draxton mwenyewe kabla ya kuongea na askari.
Bado moyo wa Namouih haukujihisi wepesi kuelekea pigo za yule mwanaume. Akawasiliana na Blandina kumuuliza ikiwa mambo upande wake yalikwenda vizuri, na rafiki yake huyo akasema angalau leo ameamkia pazuri ingawa ilikuwa siku ya huzuni kwa wengine. Akamwambia kwamba alilala kwa Draxton na alifurahia sana kuwa naye. Kwa hiyo Namouih akaona aache kwanza kumwambia kuhusu ishu ya jana, kisha akasema wakikutana ofisini wataongea mambo mengine kabla ya wote kwenda kumpa pole mama yake Agnes kule msibani. Blandina akakubali, kisha baada ya hapo simu zikakatwa.
★★
Muda wa saa tatu asubuhi hii tayari marafiki hawa wakawa ndani ya ofisi yake Namouih. Blandina alikuwa amevaa nguo nyeupe kwa juu kama sweta lililombana mpaka kufikia shingoni na sketi nyeusi iliyoishia magotini, naye Namouih alivaa blauzi nyepesi ya njano na sketi nyeusi pia kufikia magotini, wakiwa na mionekano maridadi kwenye nyuso zao. Namouih alikuwa amemuuliza Blandina kwa nini alivaa nguo ya namna hiyo wakati jiji lao lilizungukwa na joto kali, naye Blandina akasema hakuhisi joto kabisa, na sasa maongezi yakageukia kwa mpenzi wake mpya.
"Kwa hiyo akakupeleka kwake... ni pazuri?" Namouih akawa anauliza.
"Pasafi! Acha! Mwanzoni nikafikiri labda kuna demu mwingine huwa anaenda kumtengenezea hapo..." Blandina akasema.
"Inawezekana."
"Aa wapi... anajielewa tu."
"Kwa hiyo zamu hii mambo yakaenda fresh kabisa tofauti na mara ya kwanza?"
"Mmm... yeah."
"Mmm yeah, inamaanisha mka... arrr?" Namouih akauliza, akimaanisha kufanya mapenzi.
Blandina akatikisa kichwa kukanusha.
Namouih akakunja sura kwa njia ya maswali.
"Draxton anasema ana shida fulani inapokuja kwenye suala hilo. Ni kama vile ana allergy na sex," Blandina akasema.
"Excuse me?!" Namouih akashangaa.
"Yeah."
Namouih akaanza kucheka, naye Blandina akamtazama kwa njia ya kukerwa.
"Ahahahah... sorry. Sijaelewa yaani..." Namouih akasema.
"Asa' mbona umecheka kama hujaelewa?"
"I'm sorry... okay? Si... sijategemea ungesema kitu kama hicho..."
"Ndiyo hivyo. Inachekesha sawa lakini ndiyo hali halisi. Draxton anapatwa na shida fulani kila akijaribu tendo... inakuwa kama anaumwa. Na anasema akipitiliza anaweza kuzidiwa," Blandina akamwambia.
"Kuzidiwa? Kwamba akifanya sex anaweza hata kufa au?"
"Sijajua."
"Kwa hiyo utafanyaje sasa? Utaendelea kuwa naye?"
"Well, nimemshauri tuje kwenda kwa daktari kujua ana shida gani lakini bado anachekecha kichwa chake. So in the meantime... na mimi nitakuwa kama wewe," Blandina akasema.
"Unamaanisha nini?"
"Na wewe si haupewi haki yako? Lakini mbona bado uko na Donald na anakupenda sana? Me mwenyewe... nampenda Draxton yaani... kwa asilimia zote. Kwa hiyo nitaendelea kuwa naye regardless ana hali gani... na hiyo haitakuwa na shida kubwa kwangu."
Namouih akainamisha uso wake na kusema, "Unajua kwamba baada ya muda utachoka?"
"Kama wewe?" Blandina akauliza.
Namouih akamwangalia usoni.
"Ahah... usijali. Ndiyo tumeanza tu... you never know," Blandina akasema.
"Sawa. Fuata tu moyo wako Blandina, ila tafadhali nakuomba uwe mwangalifu sana," Namouih akasema.
"Kuwa mwangalifu na Draxton? Usijali. Ninamjua. Ana... amepitia changamoto nyingi maishani. Anastahili kuwa na mtu wa kumpenda..."
"Kila mtu ana mtu wa kumpenda, na...."
"Siyo Draxton," Blandina akamkatisha.
"Nini?"
"Draxton hana mtu yeyote Namouih. Yuko mwenyewe tu. Hana ndugu wala dada, hata watu wa kiukoo. Wote wameshakufa."
"Wote?!" Namouih akauliza kwa mshangao.
"Yeah, aliniambia jana. Kwa hiyo... unaweza kuelewa ni mtu mpweke. Hana hata marafiki yaani..."
"Huyo ni mtu wa aina gani Blandina? Hana ndugu, hana marafiki, ina maana anaishije?"
"Kama unavyomwona."
"Hata hajaajiriwa, sehemu yoyote ile, anategemea tu pesa za mtu mmoja mmoja, si ndiyo? Lakini ana gari, analipia vyumba, halafu hana wazazi wala ndugu, mara sijui hawezi ku-sex...."
"Unataka kusema nini Nam?" Blandina akamkatisha.
"Blandina, najua umempenda sawa, lakini unahitaji kuwa mwangalifu. Haya... jana alikwambia alikoenda?" Namouih akauliza.
"Ndiyo alisema. Alienda kuonana na yule jury wa siku ile mahakamani maana alihitaji msaada wake kumkutanisha na kiongozi wa masuala ya jurisprudence nje ya mkoa, walikuwa na mambo yao maana wanafahamiana... ndiyo akarudi na kunipitia," Blandina akasema.
"Alikwambia chochote kuhusiana na Agnes?"
"Ndiyo, aliniambia. Alikuwa anajua Agnes aliuawa. Namouih mbona umeanza tena kuwa judgmental namna hii?" Blandina akauliza kwa kufadhaika.
Namouih akafumba macho yake kwa kujihisi vibaya baada ya kutambua alipitiliza mno, naye akasema, "Samahani Blandina. Ninawaza tu kuhusu usalama wako. Ninakupenda sana rafiki yangu."
"Usijali Nam. Me nitakuwa sawa. Namwamini Draxton. Nakuomba tu na wewe uniamini mimi," Blandina akimwambia.
Namouih akavishika viganja vya rafiki yake na kuomba samahani kwa mara nyingine tena, naye Blandina akasema ilikuwa sawa. Baada ya hapo, wawili hawa wakaanza kupitia masuala ya kazi mpaka inafika saa saba hivi mchana, kisha ndiyo wakaondoka kwa pamoja kwenda kule msibani hatimaye.
★★
Baada ya Namouih na Blandina kwenda msibani, walitumia muda wa kama masaa matatu huko mpaka inafika saa kumi na moja ndiyo wakaamua kuondoka. Walikuwa wameonana na mama yake Agnes na kumpa pole kwa rambirambi kubwa, nao wakamwahidi kurudi tena kesho kwa ajili ya mazishi. Blandina alikuwa amewasiliana na Draxton mapema akimtaka aje nao pia lakini kwa sababu fulani mwanaume huyo alishindwa kuja. Alisema tu kwamba angekuja kesho, naye Blandina akaridhia hilo.
Ingawa hakusema lolote tena, Namouih bado alikuwa na mashaka kumwelekea Draxton, na kama tu mume wake alivyokuwa amemshauri, akawa ameamua kwamba angeongea naye yeye mwenyewe kuhusiana na uwepo wake jana kwenye tukio la mauaji ya Agnes. Ikiwa kile ambacho rafiki yake alikiona kwa Draxton kilikuwa kizuri kweli, basi naye angehitaji kuondoa mashaka yoyote kumwelekea ili mambo yawe shwari, na njia pekee ya kufanikisha hilo ni kuongea naye ili aache kumhukumu vibaya kama hakukuwa na sababu ya kufanya hivyo.
Katika maongezi yao wakati wanapata chakula, Namouih akawa ameulizia kule ambako Draxton aliishi, naye Blandina akamwelekeza bila ya kutambua kwamba rafiki yake alikuwa na lengo la kwenda huko. Walikuwa wanakula kwenye mgahawa mmoja maeneo ya huko huko kwa kina mama yake Agnes, na baada ya kumaliza, Blandina akasema alihitaji kwenda kumtumia pesa mama yake mzazi kwanza, kisha ndiyo wangeondoka kurudi upande wao wa jiji. Lakini Namouih akamwambia atangulie tu kwa sababu yeye alipanga kwenda sehemu nyingine kwanza, hivyo aidha wangekutana baadaye au wangewasiliana tu maana hakukuwa na mpango wa kurudi ofisini tena, na Blandina alitaka kwenda nyumbani.
Hivyo, Blandina akamwacha Namouih hapo na kutangulia kuondoka, kwa kuwa wote walikuja na magari yao. Ni baada tu ya Blandina kuwa ameondoka ndiyo Namouih akanyanyuka pia na kwenda kwenye gari lake. Sehemu aliyokuwa amepanga kwenda ni moja tu; kwa Draxton. Hakuwa na uhakika kama anngemkuta, lakini kutokana na maelezo ya rafiki yake alielewa kwamba nyumba ile ilikuwa na watu wengine kama wapangaji kwa hiyo angejaribu hata kuwauliza kuhusu jinsi walivyomwona mwanaume huyo kimtazamo endapo kama asingemkuta. Yaani na yeye leo angekuwa kama mpelelezi kwa njia yake mwenyewe.
★★
Mwanamke huyu aliendesha gari lake mpaka maeneo sahihi kabisa kama alivyoelekezwa na Blandina, naye akawa amefika karibu kabisa na nyumba ambayo Draxton alikuwa anaishi. Ilikuwa rahisi kwake kupatambua baada ya kuliona gari la mwanaume huyo nje ya geti la nyumba, na hilo likamwambia kwamba kijana yule alikuwepo. Kwa hiyo angehitaji kwenda huko kuonana naye moja kwa moja. Akaliegesha gari lake nyuma ya gari la Draxton, naye akashuka na kulifunga. Kisha akaelekea mpaka getini na kuligonga kistaarabu, naye akasimama kwa utulivu.
Eneo hilo lilikuwa na nyumba kadhaa zilizoachana, na maduka machache ya bidhaa. Baadhi ya watu waliokuwepo walimtazama Namouih sana, hasa wakina mama, na ni jambo ambalo mwanamke huyu alikuwa ameshazoea hivyo akawapuuzia tu. Hazikupita sekunde nyingi na geti hilo likafunguliwa, akiwa amefungua mvulana mdogo, naye akamwamkia Namouih na mwanamke huyu kumwitikia vizuri. Akamuuliza kuhusu Draxton, lakini mvulana huyu alionekana kutolitambua hilo jina, hivyo Namouih akamnyooshea kidole gari la Draxton na kumuuliza kama mwenye nalo alikuwa ndani.
Baada ya mvulana huyo kukubali, Namouih akamwambia amwelekeze mlango wa chumba cha Draxton, naye akaingia ndani ya geti hilo akiongozwa na huyo mtoto. Sehemu ya ndani hapo kulikuwa na wanawake wawili watu wazima waliomzidi Namouih umri kiasi pamoja na msichana mwingine rika kama la Agnes tu, naye akawasalimu na wenyewe kuitikia. Mvulana yule akaendelea kumwongoza mpaka kufikia kona iliyoelekea upande mwingine wa nyumba hiyo, uliokuwa na njia fupi kama korido, naye akamwambia ni vyumba vya huko mwishoni ndiyo huyo "mkaka" aliishi.
Namouih akamshukuru, kisha akaanza kwenda taratibu mpaka alipofikia mwisho wa kona ile na kufika sehemu iliyokuwa na uwazi zaidi. Palikuwa na stendi zenye kamba za kuanikia nguo, zikiwa na nguo chache, naye akasimama hapo hapo alipokuwa baada ya kumwona Draxton sehemu hiyo. Alikuwa amesimama kwa njia ya kuinama, chini kukiwa na ndoo yenye nguo alizokuwa anafua. Yaani alikuwa anaonekana kwa upande wa utosi wake wa kichwa; ikiwa angesimama wima basi angetazamana na Namouih moja kwa moja, na hakuwa amevaa kitu chochote kwa juu, bali pensi nyepesi na viatu vyeupe vya kushindia.
Kwa sekunde hizo chache ambazo Namouih alibaki kumwangalia, Draxton alikuwa anaendelea tu kufua, kisha mara ghafla, akaacha na kutulia. Namouih akaendelea kumwangalia kwa umakini, na jamaa akasimama wima sasa na kumtazama mwanamke huyu usoni sawia. Hapa ndiyo Namouih alipata kukiona kifua cha mwanaume huyo kwa mara ya kwanza kabisa, na kiukweli hangebisha, kilikuwa kifua cha mwanaume halisi. Draxton alikuwa na kifua kilichotuna na kujikata vyema, na tumbo lake, tumbo lake lilikuwa limetunisha mifuko yake sita ya nguvu (six packs) kwa uimara wa hali ya juu mpaka kufanya hadi ile miwili ya chini zaidi kuonekana (kitu ambacho kingefanya ziitwe eight packs); na zilichoreka vizuri mno mpaka Namouih akashindwa kujizuia kumtazama hapo.
Lakini alipomtazama mwanaume huyo usoni, akakuta akiwa anamwangalia kwa njia ya kawaida kabisa, yaani hakushangaa kumwona hapo hata kidogo ingawa hakujua amefikaje, na wala hakuonyesha nia ya kutaka kumkaribisha. Hivyo Namouih akapiga hatua chache mbele na kusimama huku anamwangalia kwa njia iliyoonyesha kujiamini.
"Habari Draxton?" Namouih akamsalimu
Draxton akabaki kimya na kuendelea kumwangalia tu.
"Hautaki salamu yangu? Nimekushtua sana kufika hapa?" Namouih akauliza.
"Habari ni nzuri, Namouih," Draxton akamwambia.
Namouih akatabasamu na kuangalia pembeni huku anatikisa kichwa chake.
"Karibu. Umetoka msibani, siyo?" Draxton akamuuliza.
"Ndiyo. Mbona wewe hukuja?" Namouih akauliza.
Draxton akaiangalia ndoo yenye nguo alizokuwa anafua, kisha akamwangalia tena Namouih.
"Aaaa... ulikuwa unafanya usafi... hongera," Namouih akasema.
Draxton akatulia kidogo, kisha akasema, "Samahani Namouih, huu siyo muda mzuri sana. Ikiwa una maongezi na mimi tunaweza kupanga wakati mwingine."
"Kwa nini huu usiwe muda mzuri? Kwa sababu uko kifua wazi? Umejikata kweli... uko vizuri," Namouih akamwambia.
Draxton akaangalia pembeni na kutabasamu kwa mbali sana.
"Mgeni ndiyo nimefika halafu unanifukuza jamani?" Namouih akasema.
"Sijakufukuza. Ninajua umekuja huku kufanya kama... uchunguzi," Draxton akamwambia
"Unajuaje hilo? Uchunguzi wa nini sasa... je kama nimepita kukusalimia tu?" Namouih akauliza.
"Mimi ni mwanasheria pia Namouih. Nakuelewa vizuri," Draxton akasema.
"Unaelewa nini? Mbona unajishtukia sana wakati me sijasema lolote...."
Namouih akaacha kuongea baada ya Draxton kuanza kupiga hatua kumwelekea mpaka akafika mbele yake kabisa. Mwanaume alikuwa anamwangalia kwa njia fulani yenye umakini, utadhani alimsogelea ili kumpiga, naye Namouih akaendelea kumtazama machoni kwa kujiamini.
"Unataka kusema nini Namouih?" Draxton akauliza kwa sauti tulivu.
Namouih akamshusha taratibu mpaka tumboni na kumpandisha mpaka machoni tena, kisha akasema, "Nilikuona jana. Jana usiku... nilikuona pale kwenye nyumba ambayo Agnes aliuawa."
"And with that... unafikiri nimefanya kitu fulani kinachohusiana na kifo chake?"
"Mbona unajiwahi hivyo?"
"Si ndiyo unachowaza?"
"Sijasema hivyo, hayo ni mawazo yako. Nataka kujua ulikuwa unafanya nini pale wakati ulimwambia Blandina umeenda wapi sijui na jury wako..."
Draxton akatabasamu kidogo.
"Nini kinakuchekesha?" Namouih akauliza kwa uthabiti.
"Hujanichekesha. Navutiwa tu na jinsi unavyopenda haki," Draxton akamwambia.
"Well, sijaja hapa kutoa burudani kwako. Nataka ukweli," Namouih akasema.
"Ukweli ni kuwa, nilikwenda na huyo jury wangu nje ya jiji kumsaidia na mambo fulani, kwa sababu aliniomba. Wakati narudi, Japheth akanipigia simu na kuniambia kwamba Agnes alimtafuta muda si mrefu kabla ya kifo chake, na alionekana kuwa kwenye shida fulani... ila hakujua ni shida gani maana mawasiliano yalikata. Ndiyo ikabidi nimwombe Japheth namba za Agnes... nilipojaribu kumtafuta sikumpata, kwa hiyo nikaamua kuifuatilia namba yake kwa kutumia app fulani ya simu yangu. Nilipofika eneo lile ndiyo nikakuta ameshauawa..." Draxton akaeleza.
Namouih akamtazama sana usoni, kisha akaanza kutikisa kichwa kwa kukataa yale aliyosikia.
"Ndiyo ukweli huo Namouih."
"Hapana, unadanganya. Yaani umeibuni hiyo story vizuri sana mpaka...."
"Kwa nini nibuni chochote?"
"... umejichanganya kwa kusema ooh sijui Japheth akanipigia, wakati namba yangu ndiyo iliyokuwa ya mwisho kufanya mawasiliano na simu ya Agnes! Unaongea nini?" Namouih akasema kwa mkazo.
"Namba yako ndiyo ya mwisho kumpigia yeye, siyo yeye kukupigia wewe. Aliyempigia simu Japheth alikuwa ni Agnes mwenyewe... inaonekana wewe ulikuja kumpigia baadaye..." Draxton akamwambia.
"Hapana... umeitunga hii story Draxton...."
"Chukua mambo yote niliyosema uende kuyafanyia utafiti wewe mwenyewe... ndiyo utajua kama nasema ukweli au la... lakini siyo kuja tu hapa na kuanza kunirushia madai yasiyo ya kweli. Tafadhali Namouih. Wewe kama mwanasheria unatakiwa kujua kwamba hupaswi kufikia conclusion bila kuwa na uthibitisho kamili... so please use some sense," Draxton akamwambia kwa ustaarabu lakini kwa uthabiti pia.
Namouih alikuwa amekuja kujua ukweli wa kile kilichompa mashaka kumwelekea mwanaume huyo kutokana na kifo cha Agnes, lakini kwa jinsi Draxton alivyojieleza ilimfanya aanze kuona kwamba huenda alimhukumu vibaya mno, tena kupita kiasi. Akaangalia tu chini akiwa anafikiria maneno ya mwanaume huyu, naye Draxton akaamua tu kurudi pale alipokuwa ameweka ndoo yenye nguo ili amalizie kuzifua, kwa kuwa jioni ya giza ilikuwa imeshaanza kuingia. Ni pale tu mwanaume huyu alipogeuka nyuma na kumpa mgongo Namouih ndiyo mwanamke akamtazama na kuona jambo lililomfanya atoe macho kwa mshangao.
Nyuma ya mgongo wa Draxton, usawa ule ule kabisa, Namouih aliweza kuyaona maneno yale ya mchoro wa tattoo aliyoyaona usiku ule ambao yeye na Blandina waligonga kiumbe fulani cha ajabu, ambacho kilikuwa na mwonekano kama wa mtu kabisa. "LIVING IN MY HEART YOU ARE, SO YOU AREN'T DEAD."
★★★★★★★★★
ITAENDELEA...
★★★★★★★★★
Comments