Reader Settings

DOSARI 

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Uhalifu, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KWANZA

★★★★★★★★★★★★★

Ni usiku wa saa tatu ndani ya hospitali moja ya mtaa, ambapo kuna watu wengi hapa na kule katika kituo hicho cha kutoa huduma za afya wanaopatiwa ama kusubiri kupatiwa huduma mbalimbali. Kuna wauguzi na madaktari wanaoshughulikia mahitaji ya wagonjwa, pamoja na ndugu ama marafiki wa wagonjwa waliopo wanaokaa kungoja taarifa za wapendwa wao. 

Miongoni mwa watu hao, kuna wanawake wawili vijana, ambao wamekaa kwenye benchi moja la kusubiri nje ya mlango unaoelekea kwenye chumba cha wodi za wanawake, wakitulia hapo pamoja huku nyuso zao zikionyesha hali ya huzuni. Mmojawapo anatazama huku na huko akiangalia watu wanaopita sehemu hii au ile, na mwingine amekaa kwa utulivu huku akiweka kiganja chake kimoja mdomoni, macho yake yakikazia sehemu moja tu kwa kuonekana kuwa ndani ya tafakari nzito sana.

Mwenzake anamwangalia kwa njia yenye huruma, kisha anamsemesha kwa kumuuliza, "Ulikuwa umeshaongea na Bony?"

Lakini mwenziye hatoi jibu lolote, na badala yake anaendelea tu kutulia vile vile akiwa ameshika tama lake.

"Sikia. Unaweza ukaongea naye, unaweza ukamwambia kuhusu hali ya mama halafu umwombe hata akusaidie kukukopesha hela kidogo, utakuwa unalipia kwa kufanyia kazi kwa muda atakaokupa," akamsemesha namna hiyo tena.

Bado mwenzake hakutoa itikio lolote lile na kuonekana kuzama tu kwenye fikira nzito.

"Pau... Pau..." akaanza kumwita.

Itikio likawa lile lile tu la ukimya.

Akamtikisa begani na kusema, "We' Paulina..."

Hatimaye akamwangalia usoni, akionekana kushtuka.

"Jamani, ndiyo imeshafikia huko?" mwenzake akamuuliza hivyo.

Mwanamke huyu anayeitwa Paulina, akafumba macho yake na kutikisa kichwa kwa kusikitika, naye akainamisha uso wake na kuufunika kwa viganja vyake.

"Usifanye hivyo, inabidi tuangalie njia yenye kukusaidia ili tumtoe mama kwenye hiyo hali..." mwenzake akamwambia.

"Nimeshajaribu mengi mno Halima, lakini naona kama hayatoshi... mpaka nashindwa kujua nafanya nini zaidi..." Paulina akasema hivyo.

"Usikate tamaa. Ni lazima tu iwepo njia, Mungu ni wetu sote, lazima atatokeza tu njia," Halima akamwambia hivyo.

"Wiki imeshaisha hivyo Halima, sijafanya ama kuleta lolote hapa la maana. Mama yangu akiendelea kukaa hivyo tu... ah..."

"Ndiyo maana ni lazima tuchangamke. Nimekuuliza kama Bony ulikuwa...."

"Nimeshaongea naye, hamna lolote kwa Bony. Kazi yangu yenyewe ndiyo hiyo, unafikiri atanikopesha hela hiyo yote? Halafu nitamlipa na nini? Nimewatafuta hata ndugu zake na mama lakini hamna anayetaka kumsaidia, hili ni langu mimi mwenyewe kubeba Halima halafu sijui cha kufanya kwa sababu mikono yangu haina nguvu. Mama yangu anaenda kufa hivyo Halima, ah!" Paulina akaongea kwa hisia na kujifuta machozi.

Halima akamwambia, "Usiseme hivyo rafiki yangu. Hebu mwamini Mungu. Mungu ni wetu sote, hawezi kutuacha. Ni lazima tuombe atusaidie, halafu tufanye jitihada zaidi ili maombi yetu yajibiwe haraka. Ona... najua hela ya tiba ya mama yako ni nyingi, lakini tuko hapa kusaidiana. Nitakusaidia pia. Nimepata-pata kidogo na kutunza kwenye kazi ya cherehani, nitakuongezea tena ili wasiache kumpa mama dawa, sawa? Wakati huo angalia-angalia na sehemu zingine pia unazoweza kupata, labda milango ikafunguliwa. Rafiki yangu, usichoke. Niko pamoja nawe, sawa? Mama yako atapona, tutamsaidia atapona," 

Halima alikuwa anamtia sana moyo rafiki yake, naye Paulina akawa anajipangusa machozi huku akitikisa kichwa kukubali faraja ya mwenzake. Simu ndogo ya Halima ikaanza kuita baada ya dakika chache za utulivu, naye akapokea na kuzungumza kiufupi na mpigaji, kisha akakata na kurudisha umakini kwa rafiki yake.

"Baba Joan huyo?" Paulina akamuuliza.

"Eeeh, amenipigia anasema ndiyo ameingia nyumbani," Halima akamwambia.

"Amekuita?"

"Hajaniita kabisa, alikuwa ananiulizia tu. Si nilikuwa nimeshamtaarifu kwamba niko huku?"

Paulina akasafisha pua na kusema, "Nenda tu nyumbani Halima. Mumeo atakuwa anakusubiri, maana ni usiku. Kwanza Joan ulimwacha na nani?"

"Yupo na dada yake, sioni kama kutakuwa na shida nikikaa na wewe...."

"Hapana Halima, nakuomba uende nyumbani. Me nitakuwa sawa hapa," Paulina akasema hivyo.

"Nitajisikia vibaya kukuacha mwenyewe..."

"Hamna, usijali. Kwa sababu leo niko off, nitalala hapa hapa kumwangalia mama, kesho nitaamkia mapambano zaidi. Asante sana kuwa nami rafiki yangu," Paulina akamwambia hivyo kwa njia imara.

Halima akatabasamu kiasi, naye akamkumbatia rafiki yake na kusema, "Usikate tamaa rafiki yangu. Tuko pamoja. Na Mungu atakusaidia wewe na mama."

"Amen," Paulina akajibu kistaarabu na kumwachia.

Rafiki yake akawa ameondoka hapo na kumwacha Paulina akiwa bado ndani ya mawazo mazito kuhusu hali ya mama yake mzazi. Aliumwa sana, akiwa na tatizo la uvimbe tumboni uliosababishwa na mambo mengi ya kijadi kipindi cha nyuma, na wakati huu lilikuwa kubwa zaidi mpaka kutishia uhai wake endapo kama asingefanyiwa upasuaji upesi; na tena kwenye hospitali kubwa zaidi. Shida ndiyo ilikuwa kwenye pesa, na hata kazi ambayo Paulina alifanya haikumpa pesa ya kutosha sana. Tayari alikuwa ametumia kiasi kingi alichotunza na kingine alichosaidiwa na baadhi ya watu waliomfahamu, katika uangalizi wa awali kitiba uliomsogezea mama yake siku, na pesa hizo zilikuwa zinaisha upesi sana. 

Alihitaji kutafuta njia ya haraka ambayo ingemwongoza kupata pesa ya kutosha ili kumsaidia mzazi wake pekee aliyemlea kwa shida sana mpaka kufikia hatua hiyo, kwa kuwa ni yeye tu ndiye aliyekuwa pamoja naye siku zote baada ya baba yake kupoteza maisha Paulina alipokuwa mdogo, na wao kutengana na wengi wa watu wa ukoo baadaye; ingawa si wote. Alitulia hapo kwenye benchi akiwaza sana nini afanye, na kweli kama rafiki yake mpendwa Halima alivyokuwa amemshauri, Paulina akaamua kufumba macho na kusali zaidi kwa Mungu ili aweze kumsaidia kuipata njia ambayo ingemwezesha kumwokoa mzazi wake mpendwa.


★★★


Ndani ya jiji kubwa zaidi katika maendeleo ya kiuchumi, tunakutana na mwanaume mtu mzima ambaye ni moja ya watu wengi waliofanikiwa kimaisha. Huyu anakwenda kwa jina la Reuben Marcus (Marko), aliye na miaka 41, mwanaume mchapakazi na aliyebeba macho yenye kutazama mbele sikuzote ili kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maendeleo ya maisha yake, na ya familia yake. Alikuwa na nafasi ya juu katika moja ya kampuni kubwa sana za kibiashara jijini, ambapo alishughulika na masuala yaliyohusiana na mapato ya jumla ya kampuni na ustawi wake akiwa mmoja wa washiriki maalumu wa bodi ya kampuni. 

Reuben alitumikia kampuni hiyo kwa miaka zaidi ya kumi na mitano, na alianza kama afisa wa mauzo katika ngazi ya chini kabisa mpaka bidii yake ya kutafuta mafanikio zaidi ilipomsaidia kuvuka madaraja na kupandishwa vyeo, na hivi sasa akawa sehemu ya juu zaidi. Alikuwa mwanaume wa malengo na kuyatimiza, mstaarabu, na mwenye akili yenye kasi katika kufanya maamuzi muhimu ambayo sikuzote yalimpa faida. 

Miaka tisa ya mwisho kufikia sasa, akiwa ameshaanza kupata mafanikio mengi ndani ya kampuni hiyo, alikutana na mwanamke mzuri sana aliyeitwa Lydia na kumpenda, na baada ya muda mfupi tu wa mahusiano, wakafunga ndoa na kufanikiwa kupata mtoto wao wa kwanza wa kike waliyemwita Larissa.

Kufikia wakati huu, binti Larissa alikuwa na miaka nane, na mama yake, Lydia, alikuwa na ujauzito wa miezi mitano, akiwa anategemea kupata mtoto wake wa pili pamoja na bwana Reuben. Lydia alikuwa mwanamke mfanyabiashara pia, akiwa na maduka mawili makubwa ya nguo na mghahawa maridadi pia ulioitwa Lydz Restaurant. Kwa pamoja walikuwa na maisha fulani ya matawi sana, uzungu yaani, na walipendana kikweli.  

Katika kipindi hiki, Reuben alikuwa anapiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo, kwa sababu alitumia pesa nyingi alizochuma kuinua mradi wake wa kujenga hoteli kubwa ambayo ingepanua zaidi uchumi wake, na ufanisi wa familia yake. Tayari alikuwa na kila kitu kilichohitajika ili kuuanzisha ujenzi huo, na ungekwenda moja kwa moja mpaka hoteli hiyo aliyotaka iwe ya kifahari ikamilike vyema na kuanza kumwingizia madola zaidi. Alitaka kujenga wakati ujao mzuri sana hasa kwa ajili ya watoto wake.

Sasa ikawa ni siku moja nzuri ya mapumziko ya kikazi kwa watu wengi, yaani Jumapili, na kwa upande wake Reuben ikawa hivyo pia ingawa kuna nyakati zingine alikuwa akihitajika kwenda kazini hata kwa siku kama hizi. Aliamka kwenye asubuhi ya saa tatu, na kitandani kwake kwa pindi hii alikuwa akilala yeye pekee. Lydia mke wake alikuwa amesafiri kwenda mkoa wa jirani ambako wazazi wake ndiyo waliishi, akiwa ameenda kuwasalimu baada ya miezi mingi kupita bila kuonana nao. 

Sikuzote kama Lydia angekwenda kwao kusalimia, alimchukua Larissa ili naye aende kuwasalimu babu na bibi, lakini kwa wakati huu Larissa hakwenda pamoja naye kwa kuwa bado alihudhuria shule. Ilikuwa mpaka nyakati za likizo ndiyo binti angeambatana naye. Lydia alikuwa amepitisha wiki kama moja tangu aende huko, na alikuwa akitarajiwa kuanza safari ya kurejea huku kwake hiyo kesho. 

Kwa hiyo Ruben akaamka tu mida hiyo hiyo ya saa tatu sasa, maana alilala kwa uchovu kutokana na kazi nyingi za siku iliyotangulia, na alipania kulala sana sema mwili wake ulikuwa na kawaida ya kumwamsha mapema ndiyo maana hakujikuta anaamka saa sita mchana. Alikuwa ameshaanza kumkosa kweli mke wake, yaani hata kama ni siku moja tu kumkosa ndani ilikuwa inampa tabu maana alimzoea sana, kwa sababu walikuwa na ule uvutano mzuri wa kirafiki uliodumu kwa kipindi kirefu kweli. Hivyo alikuwa na hamu kubwa ya ujio wake hiyo kesho. 

Lakini kwa sasa, alihitaji kushughulika zaidi na binti yake. Bila shaka Larissa bado angekuwa anakula usingizi huko chumbani kwake, na Reuben alikuwa amepanga kutumia muda mwingi wa siku hii pamoja na mwanaye kuanzia asubuhi mpaka jioni. Alitaka kuziba mapengo mengi ya wao kutoonana sana shauri ya kazi zake ambazo mara nyingine zilimbana na kufanya achelewe kurudi na kukuta binti yake ameshalala, na wakiachana asubuhi tena inakuwa ni upesi na mapema mno, hivyo alitaka kuburudika naye kwa siku nzima leo maana alihisi binti angekuwa anajihisi upweke kiasi sababu ya kukosa ushirika wa mama yake aliokuwa ameuzoea zaidi.

Kwa hiyo bwana Reuben akaingia kujisafisha bafuni kwake kwanza, kisha akaelekea chumbani kwa binti yake. Nyumba yake ilikuwa kubwa,  yenye ghorofa lenye vyumba vitatu vipana na sebule nzuri hapo chini ambapo kuelekea mbele zaidi kulikuwa na jiko na vyumba vya wafanyakazi wawili wa ndani.  Kulikuwa na uwanja mkubwa huko nje pia na nyumba ya mlinzi, wakiwa wanafuga mbwa mkali mwenye kulinda makazi yao, na Reuben na Lydia walikuwa na magari mawili mazuri ya kutembelea. 

Kiujumla walikuwa na maisha mazuri na tulivu, wakihakikisha pia kwamba binti yao anakua vyema kabisa katika mazingira safi na malezi bora, na huyu Larissa alikuwa ni hazina. Binti wa miaka nane tu, ila alikuwa na akili nzuri sana, mchangamfu lakini mwenye mwelekeo makini kama baba yake tu. Reuben alikuwa mrefu na mweusi, huku Lydia akiwa ni mweupe na mwenye urefu wa wastani uliomfaa mwanamke, na yeye Larissa alirithi uzuri wa sura ya mama yake na zaidi rangi ya baba yake, ingawa ule weupe wa mama yake ulimng'arisha sana pia kadiri siku zilivyozidi kwenda.

Reuben akakifikia chumba cha Larissa na kukuta bado amelala, hivyo akamwamsha kwa ustaarabu na kuanza kuongea naye. Kalikuwa kamechoka kweli maana kalipenda kusoma kabla ya kulala, na hata baba yake alikuta vitabu hapo kitandani kwake kuonyesha kalisinzia kakiwa kanasoma. Wakaongea kidogo, Reuben akiuliza maendeleo ya shule ya mtoto wake na kujibiwa kuwa kila kitu shuleni kipo swadakta, naye mzee akamkumbusha binti pia kuhusu mama yake kurejea kesho. 

Larissa alikuwa na shauku kweli kuhusiana na mama yake kuja maana alimkosa pia, ndiyo baba mtu akasema leo wangekwenda kuzurura, yaani wangetembelea sehemu nzuri sana jijini mpaka jioni kabisa, wanunue na vitu vingi vya kuleta nyumbani ili kesho mama yake akifika akute mambo yapo moto, na binti akafurahi kweli. Upesi akakimbilia bafu lake ili aoge, akimwambia baba yake asimtoroke. Ilimpa uradhi mwingi Reuben kuona namna ambavyo mtoto wake alikuwa na bidii sana kimasomo baada ya kupitia baadhi ya madaftari yake, na hilo likamwongezea nia ya kutaka kuhakikisha anampatia elimu bora zaidi ili aje kufika mbali sana kimaisha.

Basi, binti akawa amejiandaa vyema kabisa baada ya kuoga, akisaidiwa kuvaa nguo nzuri na msaidizi mmoja wa hapo, kisha akajiunga na baba yake sebuleni ambapo alikuwa akimsubiri. Reuben alivalia kwa njia ya kawaida tu, T-shirt na bukta, huku binti yake akivaa gauni fupi jeupe, nao wakaondoka hapo nyumbani ili kwanza ampeleke Larissa kwenye mgahawa wa mama yake huko mbele jijini; wapate kiamsha kinywa kitamu sehemu ya kibiashara ya Lydia. Mwanaume akambeba mgongoni bintiye hadi alipomweka garini, kisha akaliondoa maegeshoni taratibu na kuingia barabani kuianza safari.

Kwa mwendo wa dakika chache tu, wakawa wameufikia mgahawa huo, na kwa jinsi ambavyo ulikuwa maridadi, ungeweza kuuita hoteli nzuri ya misosi kabisa. Kulikuwa na taratibu nzuri sana hapo, wafanyakazi na wahudumu walivalia kwa njia rasmi na kutoa huduma bora kwa wateja, na watu wengi walioenda mara nyingi walifurahishwa sana na huduma hizo kuwafanya wawe wateja sugu. Yaani mgahawa haukufukuza wateja huo, na ulizidi kuwaongeza tu, hivyo uliendelea kukua sana. 

Reuben na binti yake walipoingia hapo, wakasafisha mikono na kupata sehemu ya kukaa, baba na mtoto pekee, naye akaagiza chai pamoja na maandazi magumu (half cake), na mayai ya kuchemsha, huku binti yake akiagiza chai ya maziwa, sambusa za nyama, pamoja na mayai ya kuchemsha pia. Reuben alijulikana kuwa mume wa mwenye mgahawa huo, lakini mara zote alipofika hapo kupata chakula, alilipa. Yaani alikuwa anamlipa mke wake kama mteja! 

Ilikuwa inaelekea kuingia saa tano, na watu wakiwa sehemu za hapa na kule kupata vyakula, Reuben aligundua kwamba binti yake alipenda sana kuchunguza na kufatilia kwa umakini mazingira yaliyomzunguka. Hii ilikuwa baada ya Larissa kumwonyesha kwa ishara ya mdomo atazame meza ya pembeni. 

Reuben akaangalia hapo na kuona mwanamke na watoto wake wawili wakiwa wanapata chakula, na ambacho binti alimwonyesha baba yake ilikuwa ni jinsi ambavyo mtoto mmoja wa miaka kama mitano alikula kwa njia mbaya sana na kujipakaa vyakula usoni na kuchafua nguo, na mama yake akawa anapata shida kumwongoza vyema hadi akawa akimpiga mara kwa mara, na kimya-kimya.

Reuben akamwangalia binti yake kukuta anacheka huku amefunika mdomo, naye akacheka kidogo pia. "Usimcheke mwenzio, hata we' ulikuwa unakula hivyo zamani," akamwambia hivyo.

"We! Mimi huyo?" Larissa akamwambia hivyo.

"Nani mwingine?"

"Akhaa. Me sijawahi kula hivyo maisha yangu yote baba."

"Maisha yako yote ulijiona? Wakati upo mdogo ulikuwa unakula vibaya wewe, picha zipo kwenye album, uje uangalie uone..."

"Aaah, baba unadanganya! Mama amenifunza kutumia kijiko na uma kabla hata sijazaliwa," Larissa akasema hivyo.

Reuben akacheka kidogo na kutikisa kichwa.

"Hebu ona! Linakula vibaya," Larissa akasema hivyo.

"Hey, punguza sauti. Watakusikia," Reuben akamwambia.

Larissa akakunja midomo na kusema kwa sauti ya chini, "Yaani mimi kula meza moja na mtu hivyo, siwezi baba. Uchafu-uchafu hivyo, nahama. So uncivilized!"

"Eh! We' mtoto..." Reuben akasema hivyo.

Larissa alikuwa amesuka nywele ngumu za rasta fupi, zilizovalishwa urembo wa rangi mbalimbali, naye akazipiga kidogo nyuma ya shingo yake kimadoido, eti kama mzungu.

Chakula kikawa kimeletwa huku Reuben akiwa ameanza kufurahishwa na njonjo za binti yake, nao wakajiweka tayari kuanza kula. Baada ya Reuben kuona Larissa amekaa kuziangalia sambusa kwa umakini, akahisi labda kuna tatizo.

Akamuuliza, "Darling, vipi?"

"Bee?" Larissa akaitikia na kumtazama baba yake.

"Mbona unaangalia chakula hivyo? Kuna nini?" 

"Yaani baba kuna sambusa zingine zina sura mbaya! Lakini ndiyo nazipenda," Larissa akasema hivyo.

"Sura mbaya?" Reuben akauliza.

"Eeh. Nikiziangaliaga, najua kabisa ipo sambusa ya kike, na ya kiume, na hizi tatu zilizowekwa hapa ni za kike lakini zina sura mbaya mno. Kwa hiyo zinakuwa tamu maana kama nimeshasikia ule msemo kwamba 'sura mbaya kufa hutaki, hizi za kike zikiwa na sura mbaya ni lazima ziwe zinataka kufa, na nikianza kuzitafuna zinauachia utamu wote niusikie vizuri maana zitakufa kwa raha," Larissa akaongea upesi sana kama vile hana breki.

Reuben akabaki kumtazama tu, kisha binti yake akaanza kula na kumpandishia nyusi baba yake kuonyesha anafurahia sana "kuziua" hizo sambusa. Mwanaume akacheka kidogo kwa pumzi na kunywa chai yake. Hapa alikuwa na mtoto moto kweli!

Wakati akiwa anataka kuanza kula andazi, akawa ameona watu wengine waliokuwa wakiingia mgahawani hapo, na mwanzoni hakutaka kukaza fikira kwao lakini mmoja wao akawa amevuta umakini wake. Akaendelea kuwaangalia. Walikuwa watatu, mwanaume, mwanamke, na mtoto wa kiume miaka kama minne-mitano, na ni mwanaume huyo hasa ndiye ambaye alivuta umakini wa Reuben. Alikuwa mweusi, mrefu wa wastani, na mwenye mwili mzuri wa kiume. Alinyoa kipara kichwani na kubeba ndevu hafifu kidevuni, umri wake ukionekana kuwa sambamba na rika la Reuben.

Kwa pamoja, watatu hao walionekana kuwa kama familia, na walianza kuelekea upande ambao Reuben na binti yake walikuwa wamekaa ili bila shaka kupapita na kwenda kwenye meza huru kuagiza chakula. Wakiwa wanaukaribia upande wake, Reuben akawa amethibitisha kwamba ndiyo, alimjua mwanaume huyo, na baada ya macho ya huyo mwanaume kukutana na ya Reuben, akakunja uso wake kimaswali na kuachia tabasamu la utambuzi, kitu ambacho kikafanya Reuben atabasamu kiasi pia.

Watatu hao wakaifikia meza ya Reuben, na huyo mwanaume akasema, "Eh! Mbona kama naota? Siamini yaani, ni wewe?"

Reuben akaanza kusimama huku akisema, "Labda bado ni Deja Vu. Ngoja nisimame uthibitishe."

Huyo mwanaume akacheka kidogo, naye pamoja na Reuben wakaunganisha viganja kirafiki na kukumbatiana kimabega. 

Reuben akamtazama mwanamke aliyekuwa pamoja na mwanaume huyo, naye alikuwa akimwangalia machoni kwa utulivu pia. Alikuwa na ngozi ya weusi wa maji ya kunde, mwenye mwili ulionawiri na shepu nzuri. Yaani alivalia gauni la njano lililoishia magotini, lililoubana mwili wake kwa njia iliyochoresha hips nene alizokuwa nazo na kumfanya avutie. Alikuwa na macho makubwa yaliyopendezeshwa kwa wanja, midomo minene iliyong'arishwa kuiongezea sura yake urembo, akionekana kuwa wa miaka iliyokimbilia thelathini. Na mtoto huyo wa kiume alimfanana kwa kadiri kubwa kuonyesha alikuwa wa kwake.

Baada ya wanaume kuachiana, Reuben akasema, "Habari za siku bwana?" 

"Ah, Mungu anasaidia. Ni Reuben, si ndiyo?" mwenzake akauliza.

"Yeah. Na we' ni Francis," Reuben akamwambia.

"Nilifikiri ungekuwa hata hujui jina langu, maana hatukuwa tight kivile enzi hizo," Francis akamwambia.

"Ah, ni wengi mbona nilikuwa nawajua kwa majina? Attendence yote ilikuwa kichwani," Reuben akasema.

"Hahahah... monta mpaka kiranja!" Francis akasema hivyo kwa shauku.

"Yeah, hahah... ndiyo mimi," Reuben akaongea kwa utulivu tu.

"Aisee, ni muda mrefu sana kaka. Mambo yamebadilika, mpaka na nywele umezipiga na mtindo, yaani dah!" Francis akasema.

"Hahah... kweli, ni muda sana. Upo huku kitambo?" Reuben akauliza.

Francis akasema, "Eeeh, ila siyo sana. Nimekuja huku, huu kama mwaka wa tano sasa hivi. Na wewe?"

"Ah, me niko huku muda. Toka tumemaliza shule, nilikuja huku kuendelea na masomo mpaka nilipoanza kazi," Reuben akamwambia.

"Ah, safi sana. Maisha yamekukubali kiranja, na kitambi kinavizia," Francis akatania.

"Kawaida tu. Hata we' naona yako yanang'aa," Reuben akasema hivyo huku akitoa ishara kumwelekea mwanamke yule pembeni.

Francis akamwangalia mwanamke huyo na kusema, "Ah, huyu ni dada yangu bwana. Anaitwa Josephina."

"Oooh, sawa sawa..." Reuben akaelewa.

"Eeh. Sister, huyu ni rafiki yangu, tumesoma wote shule ya msingi mpaka sekondari. Ndiyo tukaja ku-separate tulipomaliza... leo ndiyo tunakutana yaani," Francis akamwambia hivyo dada yake.

"Okay. Sawa," Josephina akajibu kistaarabu.

Alikuwa na sauti tulivu, na Reuben akamnyooshea kiganja kisalamu huku akisema, "Naitwa Reuben. Nimefurahi kukutana nawe Josephina."

Akakipokea kiganja chake huku akitabasamu na kusema, "Mimi pia. Niite tu Phina."

"Sawa sawa. Mwanao hajambo?" Reuben akasema hivyo na kukiachia kiganja cha mwanamke huyo.

"Yuko poa. Ana njaa kweli, imebidi tuwahi hapa kabla hajanitafuna," Josephina akajibu hivyo.

Reuben akatabasamu, naye akamwambia huyo mvulana, "Hujambo baunsa?"

Dogo akatulia tu kama vile hataki.

Francis akasema, "Inabidi awahishwe, maana! Atatafuna mtu kweli. Na huyu ni mwanao?"

Alikuwa akimaanisha binti yake Reuben, ambaye aliendelea kula huku akiwaangalia wengine kwa utulivu, naye Reuben akasema, "Ndiyo, mwanangu wa kwanza huyo ahahah..."

"Dah! Hujambo karembo?" Francis akamsalimu.

"Sijambo uncle. Shikamoo?" Larissa akajibu upesi huku akitikisa-tikisa mguu wake.

"Marahabaa, mtoto mzuri," Francis akamjibu kwa furaha.

"Aunty, shikamoo?" Larissa akamwamkia na Josephina.

"Marahaba dear. Unaitwa nani?" Josephina akajibu.

"Larissa," kakajibu.

"Wow! Jina zuri sana, Larissa. Eh, Hans... umemwona Larissa? Mwambie 'mambo?'" Josephina akasema hivyo kumwelekea mwanaye.

Huyo Hans akawa anamwangalia Larissa kwa njia fulani ya kujihami na kununa, kama mtoto aliye yeye, naye Larissa akampungia mkono kirafiki mvulana huyo huku akisema, "Hi."

Francis akasema, "Naona mwanao yuko sharp sana."

"Ahahah... tunakuza bwana," Reuben akaongea kistaarabu.

"Basi kaka, wacha sisi tuelekee mezani, chai yako isije kupoa kwa sababu yetu," Francis akamwambia hivyo.

"Hapana shida. Bado iko moto," Reuben akamwambia.

"Vipi tukiachiana mawasiliano kaka mkubwa? Tu-catch up na nini, maana ni miaka!" Francis akasema hivyo huku akitoa simu yake mfukoni.

"Yeah, yeah, itakuwa jambo zuri," Reuben akakubali na kupokea simu ya jamaa.

Akaandika namba yake hapo na kumkabidhi Francis simu, kisha wakaagana kwa ufupi na watatu hao kuwapita baba na binti yake, na Reuben akirejea mezani kuendelea kupata chai. Larissa alistareheka sana kwa kupata mlo wake kwa raha zote, na kwa upande wake Reuben, aliifurahia pia pindi hii pamoja na binti yake, lakini pia alipendezwa zaidi na hali mpya ya urafiki aliyohisi baada ya kukutana na mtu aliyefahamiana naye miaka mingi iliyopita. 

Bila shaka wakiwa watu waliotoka mbali na kupotezana, wangekuwa na mambo mengi ya kufurahia pamoja endapo wangeanza kufanya ushirika tena kwa kipindi hiki, mambo ya wanaume kama hivyo lakini kwa kuenzi historia ya ujana wao, ambao kama kwa maisha ya vijana wengi, huburudisha. Angewatazama pale walipokuwa wamekaa kupata chakula, na mara kwa mara macho yake yangekutana na Josephina na wao kupeana aidha tabasamu la kirafiki, ama kuangaliana tu na kuacha. 

Hii ya kuangaliana tu na kuacha ilitokana hasa na macho ya mwanamke huyo kuanza kutuma kama ujumbe fulani kumwelekea Reuben, ujumbe ambao hakujua maana yake. Yaani walipoangaliana, Josephina angekaza macho yake kwa Reuben kwa ufupi kwa namna iliyofanya mwanaume ahisi uvutano fulani baina yake na huyu mwanamke, lakini akaona aache kukazia fikira jambo hilo kwa sababu hakutaka lielekee kule ambako hapakufaa. Hakuhitaji kuiingizia akili yake majaribu.

Hivyo, mwanaume akajitahidi kuweka umakini wake kwa binti yake zaidi, akifurahia chakula na maongezi pamoja naye yenye kufurahisha, akafanya kumpigia simu na Lydia na kuongea naye pamoja na binti yao, na walipomaliza chakula kwa kushiba kabisa, Reuben akanyanyuka pamoja na Larissa tayari kuondoka. Waliona kwamba Francis na Josephina bado waliendelea kupata chakula, hivyo wakapungiana mkono kupeana kwa heri, huku Reuben akiona kwamba bado macho ya Josephina yalimtazama kwa njia yenye kutoa maana, naye akamshika tu binti yake na kuuaga mghahawa wa mke wake kwa wakati huu. 


★★★


Upande wake Paulina, mambo yalikuwa yakielekea sehemu mbaya sana, tena siyo kwa njia moja tu. Zilikuwa zimepita siku mbili tokea ule usiku ambao alikuwa hospitalini na rafiki yake, Halima, walipozungumza kwa kufarijiana kuhusu jitihada walizotakiwa kuongeza ili kuweza kumsaidia mama yake Paulina atibiwe haraka. Halima alikuwa amemwahidi rafiki yake kumsaidia na kiasi kidogo cha pesa, lakini sasa jambo hilo lisingewezekana. 

Usiku huo mwanamke huyo aliporudi nyumbani, alikuta mumewe akiwa amekasirishwa sana na kitendo chake cha kuacha kukaa nyumbani na watoto, akitanguliza mashoga zake badala ya kutimiza majukumu muhimu ya kifamilia, na katika hali iliyozidi kuwa mbaya sana mumewe akawa amempiga na kumkanya asijihusishe tena na matatizo ya Paulina. Ilikuwa kisa chenye kumhuzunisha sana Paulina, na sasa asingeweza hata kuonana wala kuwasiliana na rafiki yake baada ya mumewe kumnyang'anya simu. Mambo ya ndoa hayo.

Jambo hilo lilikuwa limeongezea utata kwenye suala la mama yake, ambaye hangeendelea kupata dawa za maji na uangalizi uliofaa kutokana na Paulina kuishiwa pesa, na hilo lilizidi kuwa baya hasa baada ya yeye kuachishwa kazi yake ghafla. Paulina alifanya kazi ya uhudumu kwenye moja ya baa kubwa za mitaa yao, na aliyemwajiri ndiye mwanaume aliyeitwa Bony. Huyu Bony hakuwa mtu muungwana sana, yaani karibia kila mhudumu aliyemwajiri hapo alitaka kutoka naye kimapenzi, kama siyo kuridhishana kimwili tu kwa jinsi alivyodhani kila mhudumu alitakiwa kujiendesha. 

Yaani, Bony kama wanaume wengi tu aliwaona wahudumu wote wa baa kuwa malaya. Na kwa upande wa Paulina hali ilikuwa vile vile. Isipokuwa tu mwanamke huyu hakuwahi kukubali ushawishi wa huyo jamaa hata kama aliahidiwa kuongezewa pesa. Kazi aliyofanya ilikuwa na mambo mengi ambayo yangefanya watu wamwone kuwa mwanamke rahisi tu kununuliwa, lakini hakuwa wa aina hiyo. Aliifanya tu kwa sababu alihitaji kupata pesa, lakini hakutaka kujitoa kuwa chombo cha starehe kwa wanaume ili tu achume pesa.

Sasa kwa siku kadhaa zilizopita hali ya mama yake Paulina ilipozidi kuwa mbaya na kuhitaji msaada wa hali ya juu, Paulina alikuwa amejaribu kumwomba huyo Bony amkopeshe pesa ili imsaidie kuendelea kumtunza mama yake, lakini mwanaume huyo alimwambia angempa hela ikiwa tu angekubali kufanya mapenzi pamoja naye, na Paulina alipoweka pingamizi, jamaa akakataa kumsaidia kwa kusema hana pesa. 

Kwa wakati huu sasa baada ya matatizo kumpata Halima ule usiku, Paulina akawa amerudi kazini na kujaribu kumwomba tena Bony msaada, lakini mwanaume huyo akamwachisha kazi. Ilimshangaza sana, hakuelewa kabisa ni kwa nini alifanyiwa hivyo hata baada ya Bony kumwambia kwamba kuna mabadiliko tu walikuwa wanafanya, na akampa kiasi kidogo cha pesa kulipia wiki za mwisho alizokuwa akifanya kazi hapo.

Lakini Paulina aliweza kung'amua sababu ilikuwa ni nini nyuma ya kitendo hicho cha Bony. Kwanza, ni yeye kukataa kujitoa kwake kimwili kwa miezi mingi, na pia, ni maneno ya chuki kutoka kwa wafanyakazi wenzake wa sehemu hiyo ambao mara nyingi walimwonea wivu Paulina, hasa kwa sababu alipendwa na wateja wengi waliofika. Paulina alikuwa mwanamke kijana mwenye sura na umbo lenye kuvutia, alijitunza, na alikuwa makini na kazi. Alivutia wateja wengi ambao hawakuwahi kupata bahati ya kumbeba na kutoka naye hata mara moja, na bado walimiminika tu hapo baa.

Lakini sasa kwa wiki ambayo hali ya mama yake ilizidi kuwa mbaya, ilianza kuonekana kama vile Paulina hatumii muda mwingi kazini na kujali mambo yake tu, na wenzake wakatumia nafasi hiyo kumchongea kwa bosi wao ili aweze kuondolewa. Kila kitu kilikuwa wazi, yaani Paulina alishangaa tu yeye pekee ndiye anayeachishwa kazi na mhudumu mwingine kuwa ameshaletwa siku hiyo hiyo, ni lazima tu shabaha iliyokuwa imewekwa nyuma ya mgongo wake kwa kitambo ndiyo ilifyatuliwa hatimaye. Hakuwa na jinsi tena. Akajiondokea tu, akirudi hospitalini na kutumia pesa kidogo aliyopewa kuongeza dawa za mama yake, na sasa akawa ameachwa mikono mitupu kabisa.

Aliendelea kujitahidi kutafuta huku na kule, akauza na kitochi chake, akawaomba baadhi ya watu aliofahamiana nao wamsaidie kumuunganisha kwa kazi zingine, lakini alielewa kwamba hata kama angepata kazi, kuja kuishika pesa ambayo ingemsaidia mama yake ni jambo ambalo lingepitisha muda mrefu. Na mama yake hakuwa na muda mrefu wa kusubiri. Hapo tena bado kulikuwa na suala la kodi ya chumba chao walichopanga, yaani aliwaza labda atafute mtu wa kumuuzia makochi yao mawili madogo haraka, wakati huo akitafuta kitu cha uhakika, lakini akaishia kuvunjika moyo tu kwa kuwa alijua hivyo ni vitu ambavyo vingegoma kuleta matokeo yenye faida iliyodumu.

Akiwa ameishiwa pesa na wazo zuri la kumpa msaada aliohitaji haraka, akaamua tu kufanya jambo ambalo hakudhani angekuja kuwahi kufanya. Kulikuwa na shangazi yake mmoja aliyeishi upande tofauti wa mji aliokuwepo, na huyo alikuwa ni mdogo wake na marehemu baba yake. Kama ndugu zao wengi tu, huyo mwanamke alikuwa amejitenga nao pia, zaidi ni watoto wake wawili tu ndiyo ambao walijuana na Paulina kipindi fulani cha nyuma na kujenga urafiki wa kindugu. Walikuwa wadogo, shule za msingi, na ni kutokea kipindi hicho cha nyuma wameonana ndiyo Paulina alionana kwa mara ya mwisho na huyo shangazi yake, hata mawasiliano pamoja naye hakuwa nayo.

Alielewa kwamba shangazi yake angekuwa na kazi iliyomsaidia kuvuna pesa nyingi, kwa sababu alisikika kuwa na maisha mazuri akiwa mzazi pekee kwa watoto wake baada ya kutengana na baba yao. Hata alitembelea gari. Hivyo Paulina akaona ajaribu kwenda kwake na kuongea naye ana kwa ana, maana kwa ndugu zao wote, angalau huyo angeweza kufikika, ikiwa kama alimkumbuka bado. Kwa hiyo akakopa hela kutoka kwa mtu aliyefahamiana naye ili aitumie kwa ajili ya nauli, akiwa hata hana uhakika wa kuweza kuirudisha upesi, lakini akajipa tu matumaini. 

Ikiwa ni siku ya Jumapili, Paulina alielewa kwamba shangazi yake angeweza kuwa nyumbani, na alipakumbuka kwake vizuri sana ingawa muda ulikuwa umepita. Hivyo akachukua daladala, mwendo ukiwa ni mrefu na kumlazimu apande ya ziada mpaka kufika hayo maeneo, na kutokea kituoni akatembea hadi kuifikia nyumba aliyojua shangazi yake aliishi. Alijua ndiyo penyewe, lakini palikuwa pamebadilika. Yaani, palipendeza zaidi ya vile alivyopaona zamani wakati yuko mdogo, ikionyesha kweli shangazi yake alikuwa amepiga hatua. Ilikuwa muhimu sasa kujaribu kumwomba amsaidie mama yake, na angejitoa hata kumfanyia kazi za ndani kwa muda wote ili kulipa deni.

Nyumba ilikuwa na uzio wa ukuta wa matofali ambayo hayajapigwa simenti, ukiwa na geti kubwa jeusi, naye akaenda na kugonga mara chache, kisha akasubiri. Eneo alilokuwepo lilikuwa na makazi mengi ya watu, nyumba za kawaida tu kwenye ujirani, na barabara changarawe iliyopitisha magari machache na waendesha baiskeli. Geti likaanza kusikika likifunguliwa, naye Paulina akaangalia hapo kwa utayari. Akatoka kijana wa kiume kwenye miaka ya utineja, akiwa mwembamba na mrefu, na huyo hakufahamika kwa Paulina, hata kijana mwenyewe alimwangalia huyu dada kigeni.

Paulina, akiwa amejishika viganja, akatabasamu kiasi na kusema, "Za saa hizi?"

"Nzuri tu. Karibu," huyo kijana akajibu.

"Asante. Samahani, eti... nimemkuta mama Inno?" Paulina akamuuliza.

Kijana huyo akamshusha na kumpandisha, akionekana kutafakari swali lake.

"Hapa si ni kwa mama innocent?" Paulina akamuuliza tena.

"Ndiyo. We' ni nani?" kijana akauliza.

"Mimi naitwa Paulina. Mama Inno ni shangazi yangu. Sijui nimemkuta?" Paulina akaongea kwa upole.

"Shangazi yako?" kijana akauliza tena.

Paulina akabaki kumtazama tu kwa kutatizika. 

Huyo kijana alikuwa akimtazama kwa njia fulani ya kudadisi eti, akiangalia zaidi kandambili nyekundu alizovaa mgeni, kisha akamwambia, "Njoo. Ingia."

Paulina akatii na kuingia ndani hapo taratibu, huyo kijana akifunga geti, naye akaanza kuongozwa kuikaribia nyumba zaidi. Ilikuwa kubwa kiasi na pana, ikipakwa rangi nyeupe, na aliona gari dogo aina ya Toyota Corolla nyeupe likiegeshwa hapo nje. Kijana akamwambia amsubirie sehemu ya varanda ili aende kumwita mwenye mji, naye Paulina akatii. Akabaki hapo nje akiwa anatoa maombi kimoyomoyo kwamba jaribio lake lizae matunda mazuri, na ndipo mlango ukafunguliwa tena na mwanamke mtu mzima kutoka humo ndani.

Paulina alimtambua huyo kuwa shangazi yake. Alikuwa mmoja wa wale wanawake waliopenda kuonekana kuwa kama wasichana bado, maana muda mwingi alijiweka katika hali ya kupendeza. Hapa alikuwa amevalia blauzi nyeupe na suruali nyekundu yenye kubana, akiwa na umbo nene kiasi, na wigi la nywele fupi likifunika kichwa chake kipana. Alikuwa na sura nene ya nyodo. Alitoka na kusimama mbele ya Paulina huku yule kijana akiwa kwa nyuma mlangoni, na alimwangalia mgeni kwa njia makini kama vile bado hajamtambua. 

Paulina akatoa ishara ya kupiga magoti na kusema, "Shikamoo shangazi?"

Huyo mwanamke akavuta fikira kwanza, kisha akajibu, "Marahaba."

Paulina akatulia na kuendelea kumwangalia usoni.

"Paulina?" mwanamke huyo akauliza.

"Ndiyo shangazi. Ni mimi," Paulina akajibu kwa unyoofu.

"Eh! Jamani! Ni siku nyingi sana, umekua! Nilikuwa hadi nimeshakusahau," shangazi akasema hivyo.

Paulina akaangalia chini tu kiwasiwasi.

"Umekuja huku mwenyewe?" shangazi akauliza.

Paulina akatikisa kichwa kukubali.

"Kulikoni? Wazima huko kwenu?" shangazi akauliza tena.

Paulina akatikisa kichwa kukanusha na kusema, "Hali siyo nzuri sana, shangazi. Nimekuja kukuomba unisaidie."

Shangazi yake akakaza macho, halafu akakunjia mikono yake kifuani na kusema, "Shida ni nini?"

Paulina akaona utata kiasi kuongelea mambo yake mazito huku kijana mdogo akiwa hapo pembeni, na shangazi yake akaelewa hilo.

"Shebby, nenda ndani. Rudi ndani!" akamwambia hivyo huyo kijana.

Baada ya kijana kuigia ndani, shangazi akafunga mlango, halafu akasimama kwa kuegamia ukuta ili amsikilize mpwa wake.

Paulina akasema, "Shangazi, kwanza naomba sama...."

"Paulina, acha kuzunguka. Ongea point iliyokuleta, maana ushaanza kunitisha. Una matatizo gani? Umefukuzwa, au?" 

"Hapana, siyo hivyo..."

"Sema sasa shida ni nini. Halafu, usiniite shangazi sasa hivi, maana mpaka tunaonekana kulingana kabisa hahahah..." shangazi akaongea kimasihara eti.

Paulina akatazama tu pembeni.

"Umesikia? We' niite Roza. Kila mtu ananijua hivyo," shangazi akasema hivyo kimadoido.

"Sawa," Paulina akajibu.

"Enhe, leta maneno," Roza akasema hivyo.

"Sha... a... yaani, mama anaumwa. Sana. Amelazwa hospitali," Paulina akamfahamisha.

"Wewe! Lini jamani?" Roza akajifanya kushangaa.

"Ana kama wiki... inaelekea ya pili..."

"Anaumwa nini?"

"Ana uvimbe tumboni."

"Eh! Masikini!"

"Anatakiwa kufanyiwa upasuaji, madaktari wanasema asipoondolewa hiyo shida, atakufa..."

"Mtume!" Roza akasema hivyo.

Paulina akaanza kulengwa na machozi.

"Ah! Pole sana mwanangu. Na, pole kwa mama yako. Sasa... eh! Inakuwaje? Umeshapata hela ya kumsaidia atibiwe?" Roza akauliza.

"Hapana. Nimetumia hela niliyokuwa nayo ili madaktari wampe... hhh... wampe utunzaji hiyo wiki, halafu...."

"Kwa hiyo yote imeisha sasa hivi?"

"Ndiyo."

"Ni shi'ngapi?"

"Niliyotumia kwake, kama laki tatu na...."

"Hapana, namaanisha... hela ya kumfanyia huo upasuaji yaani. Ni shi'ngapi?" Roza akamsahihisha.

"Inafika hadi milioni mbili shangazi..." Paulina akaongea kwa huzuni, machozi yakiwa yameanza kumtoka.

Roza akapiga ulimi wake mara nyingi kwa njia ya kusikitika, naye akasema, "Hapo itakuwa kasheshe! Hiyo ni hela nyingi!"

Paulina akajifuta machozi na kusema, "Shangazi..."

"Roza. Niite Roza," akamkatisha.

"Samahani. Roza... ninaomba unisaidie. Sina... hhh... pengine pa kupata hela ya haraka, yaani sasa hivi nimeishiwa kabisa, na...."

"Paulina natamani sana kama ningeweza kukusaidia, lakini na mimi sina. Yaani sina kabisa. Na sasa hivi, sidhani hata ukienda kwa nani ukajaribu kuomba hiyo hela utapewa. Nakwambia ukweli. Ni ngumu. Mpaka uifanyie kazi kwa muda mrefu," Roza akamwambia hivyo.

Paulina akahisi huzuni zaidi, naye akakaza kilio chake na kusema, "Naomba unisaidie shangaz... Roza... nakuomba Roza unisaidie..."

"Kwani, si unafanya kazi, au?" 

"Nilikuwa na kazi ndiyo, lakini... nikaachishwa..."

"Wapi?"

"Kwenye baa moja. Kipato chenyewe hakikuwa kingi, na niliyotunza ndiyo nikatumia kwa ajili ya dawa za mama... sasa hivi sina hhh..." 

"Kwa nini ulifukuzwa kazini?"

"Bosi wangu alikuwa ananitaka, nikamkatalia. Ndiyo akatafuta sababu ya kuniachisha mama alipoanza kuumwa. Hhh... yaani sijui la kufanya sasa hivi..."

Roza akaangalia pembeni huku akizungusha macho yake na kutikisa kichwa.

"Roza tafadhali, nakuomba. Unaweza ukawa unajua... hhh... unajuana na watu... mfff... labda kazini kwako, au popote ambapo naweza kukopa hela ili mama afanyiwe upasuaji... halafu nifanye kazi kwa huo muda wote kufidishia...."

"He! We' Paulina! Hiyo ni akili gani wewe?" Roza akamwambia hivyo.

Paulina akawa anajifuta tu machozi.

"Unafikiri itakuwa rahisi? Mambo hayaendi hivyo. Ni bora tu kama ungekubali kutembea na huyo bosi wako ili umwombe hela, usingekuwa unahangaika hivi..." Roza akamwambia.

"Shangazi..." Paulina akamwita kwa huzuni.

"Mimi sijui nakusaidiaje sasa. Hata kama ungesema upate mtu wa kukupa hela kama hivyo, umfanyie kazi, baada ya hapo nini? Mama yako atatunzwa na nani? Maana utakuwa bize kufanya kazi kwa ajili ya hela ambayo imeshatumika, mama yako atakula nini? Na wewe utaishije? Si utakuwa unatia saini mkataba wa kifo chake na chako kwa wakati mmoja?" Roza akamwambia hivyo kwa uthabiti.

Paulina akaendelea kulia zaidi bila kutoa sauti ya juu.

"Ah... me sijui kwa kweli. Sina hela yaani, sina. Na wewe hivyo unavyolia unajua haikusaidii... kulia haikusaidii lolote Paulina. Ni vema utumie tu akili nyingine," Roza akamwambia hivyo.

Paulina akajifuta machozi na kusema, "Sijui nafanyaje, shangazi. Nimeshajaribu... hhh... najaribu... nashindwa. Nakuomba unisaidie, nitafanya kazi popote, nitaenda... mff... nitakufanyia hata wewe. Naomba unisaidie. Mama yangu ndiyo pekee niliyebaki naye, amenilea kwa maumivu, ameshinda njaa ili mimi nile, amenisaidia hata nikasoma kidogo, mff... nahitaji sana kumsaidia... hhh... ninakuomba sana shangazi..." 

Mwanamke huyu mdogo aliongea kwa hisia sana, na Roza akawa anamwangalia kwa njia makini. Akamshusha na kumpandisha, akiwa ameingiwa na wazo fulani, naye akamuuliza, "Una miaka mingapi sasa hivi?"

"Ishirini na mbili," Paulina akasema hivyo upesi.

Roza akavuta fikira kwanza, kisha akamwangalia hapa na pale mwilini kama kumkagua, halafu akamshika mabegani na kumgeuza ili amtazame kwa nyuma, na hapo akawa ameridhika. Paulina hakuelewa shangazi yake anafanya nini, lakini akahisi kwamba tayari alikuwa amepata wazo la kumsaidia, hivyo akatulia tu ili angoje kuona kama matumaini yake yangezaa matunda.

Roza akamtazamisha Paulina kwake tena, na kwa sauti ya chini akamwambia, "Okay. Umenipa wazo, Paulina. Kuna kazi naijua unayoweza kufanya, ukapata hela nyingi haraka."

Paulina akaanza kucheka-kulia kwa hisia, naye akajifuta machozi zaidi na kusema, "Kweli shangazi? K-k--kama ipo... unaweza kuni...."

"Nisikilize. Siyo kwamba kama ipo, hiyo kazi ipo. Na wewe unaweza ndiyo kuifanya, kama utakuwa tayari kuifanya," Roza akamwambia hivyo.

Paulina akatulia zaidi, akibaki kumtazama mwanamke huyo kwa umakini.

"Unataka kumsaidia mama yako, si ndiyo?" Roza akamuuliza.

Paulina akatikisa kichwa kukubali.

"Sawa. Nitakusaidia uipate hii kazi. Ni rahisi sana kwa wanawake, na tena wewe... itakuwa nyepesi mno. We' siyo mtoto sasa hivi, najua unaelewa namaanisha nini," Roza akamwambia hivyo kwa sauti ya chini.

Paulina akaangalia chini kiutafakari.

"Sina njia nyingine ya kukusaidia, hii ndiyo ya haraka. Kwa hiyo, useme ikiwa kweli uko tayari, ama...."

"Niko tayari," Paulina akamkatisha kwa kusema hivyo.

Roza akashusha pumzi kwa njia ya kuridhika.

"Nitaifanya shangazi. Namaanisha... niko tayari kuifanya... Roza," Paulina akaongea kwa njia hakika.

Shangazi Roza akatabasamu kiupande, huku akimwangalia mwanamke huyo kijana kwa macho yaliyojaa... hila, naye akasema, "Vizuri. Pangusa hayo machozi sasa, nifate ndani."

Baada ya mwanamke huyo kusema hivyo, akageuka na kuufungua mlango kisha kuingia ndani kwake tena. 

Kwa sekunde chache, Paulina akabaki hapo varandani akiwa ameanza kupitisha maswali mengi kichwani kwake, kwa kuwa alielewa kwamba huenda njia ambayo shangazi yake angetumia kumsaidia isingekuwa ya kipendacho-roho kwake yeye, lakini hakuona namna nyingine ya kupata msaada ikiwa tayari hapo ofa iliibuka. Angetakiwa kuichukua tu, kivyovyote ambavyo ingekuja. Akajitia ujasiri, kwa ajili ya mama yake mzazi, naye akaanza kujifuta machozi na kujisawazisha kwa njia iliyofaa kabisa kwenda kukabiliana na hali hii mpya, kisha akaingia ndani huko pia.

★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★

Next