Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KWANZA

★★★★★★★★★★★★★★


Wiki nne zikawa zimepita baada ya mambo yale yote kutokea. Ndiyo. Mwezi mzima. Najua, najua... JC natakiwa nielezee yaliyotokea ndani ya huo muda wote, nimekoswa sana naambiwa, na kiukweli ni mengi mno yaliyokuwa yametokea mpaka kufikia sasa. Mengi yenye kuridhisha, na baadhi yenye kukwaza kwa kiasi fulani.

Tuanze na Joshua. Mwanaume huyo, baada ya kuwa amemfanyia binti Mariam vitendo vya kinyama kwa kujaribu kumuua zaidi ya mara moja na kutunga hila kibao ili tu aitaifishe mali ya binti, alikuwa amepelekwa mahakamani kwa kufunguliwa kesi ya makosa mbalimbali ya jinai. 

Ndani ya huu mwezi ulioisha yaani, alifikishwa mahakamani zaidi ya mara tatu kujibu mashtaka ya hila za udhulumaji, au uporaji mali kwa kutumia hati bandia za kimahakama, vitendo vya kijeuri kama vile kupanga mauaji, na pia kuna mtu mwingine akawa ameongezea ishu ya kumkodisha gari jamaa na kuahidiwa malipo, lakini hakulipwa na badala yake gari lilirudishwa likiwa limeharibika. 

Kesi zake mbili za kupanga mauaji na wizi hasa ndiyo ambazo zilikuwa nzito kwa huyu Joshua, ushahidi ukiwepo wa kuridhisha kabisa, naye akawa amepewa adhabu ya kwenda kutumikia kifungo cha miaka kumi jela. Siyo mchezo! Mvua ya miaka kumi! 

Waliokuwepo sanasana kwenye mahudhurio ya kesi ya jamaa ilikuwa ni mimi mwenyewe, askari Ramadhan na mwandamani wake, Tesha, Khadija, Yohana wa Kleptomaniax, Bi Zawadi mara mbili, na Miryam pia mara moja; kwenye siku ambayo jamaa ndiyo alipewa hukumu. Ushahidi alioutoa huyo Khadija na Tesha kwenye suala la yeye Tesha kutekwa pamoja na mdogo wake ili wauawe, ulikuwa nyundo nzito sana ya kuupigilia ndani zaidi msumari wa hukumu ya haki aliyopewa jamaa. Huko ndiyo angeenda kulia na kusaga mipira yake vizuri! 

Tulihakikisha haya yote hayamfikii binti Mariam kwa muda wote yalipoendelea mpaka kumalizika, na ilionekana kwamba familia yake iliridhishwa mno na hukumu aliyopewa huyo Joshua. Alistahili hata cha maisha kabisa, ila kuna vitu vitu tu vilipunguzwa, hadi nilishangaa kiasi kwamba Khadija hakula hata miaka miwili kwa sababu ya kusindikiza uhalifu ilhali wenzake wote, wale wakina Yohana wa Kleptomaniax, wote walikula mvua za miaka mitano mpaka saba jela kwa kusindikiza maovu ya Joshua. Hakukuwa na neno, la muhimu likawa kwamba mbaya wa amani ya familia yake Mariam alikuwa amewekwa mbali hatimaye.

Tukija upande wa madam Bertha sasa, mambo kweli yalikuwa 'underway' kama msemo wake. Yaani ndani ya hizi wiki tatu za mwisho zilizokuwa zimekata, tayari alikuwa ameshanionyesha sehemu ambayo biashara yake ya kutengenezea cocaine ingefanyikia, na kupitia mimi, tayari unga ulikuwa umeshaanza kutengenezwa, kuongezwa, na sasa ulikuwa kwenye harakati za kusambazwa. 

Mwanzoni ilibidi kutoa kiasi fulani kama kionjo, kidogo-kidogo, kisambazwe hapa na kule ili watumiaji waelewe kulikuwa na zigo jipya jijini, na wanajeshi wake waliofanya kazi ya usambazaji wangetangaza pia bei mpya ya kuyapata madawa hayo yaliyokuwa yameanza kushika kasi mpya kwenye soko hilo jijini. 

Kufikia wakati huu, tayari nilikuwa nimeshaona na kusoma njia zao kuu za kufanya usambazaji wa kisiri, na kiukweli zilikuwa njia ambazo sikutegemea mwanzoni, ila walikuwa wanatumia akili sana. Madawa yao yalipita sehemu na maeneo yenye hadhi za juu, mashuleni, vyuoni, mpaka kwenye makampuni, na haikuwa rahisi kwa yeyote ambaye hakuwa ndani ya hili game la uuzaji kujua jinsi ambavyo ishu hiyo iliendeshwa. 

Kwa muda wote huo, nilikuwa nimejitahidi sana kumwonyesha madam Bertha kwamba nilikuwa makini na kazi aliyotaka tuifanye, na alinifurahia mno. Hadi wale wanaume ambao tulienda kukutana nao African Princess casino siku ile walisifia sana kazi yetu mpya, kwa hiyo kuna mara ambazo tungekutana, na wao kujiachia sana mbele ya ushirika wangu. 

Lakini hawakujua kwamba kwa muda huo wote, mimi nilikuwa nafanya kazi na askari mpelelezi Ramadhan, na uamuzi wa kusubiria kwanza kabla ya kuchukua hatua dhidi ya watu hawa ulikuwa ni wake. Haikuwa tena juu ya suala la mauaji ya Joy tu, la. Sasa hivi kwa sababu mambo mengi yalikuwa yanaongezeka, ingebidi tuwe na kila kitu tulichohitaji ili yeye askari Ramadhan na wenzake wakipiga tu hatua kuwaweka chini ya ulinzi watu wote wa Bertha, iwe ni moja kwa moja. Yaani kusiwepo na njia ya kurudi nyuma tena. 

Ila kama ni kitu kilichokuwa kikinifanya nikune kichwa changu bado ilikuwa ni kutojua nitumie njia ipi ili kumkamatisha na Festo pia. Aisee, yule jamaa sikumwelewa. Yaani, alikuwepo, lakini ilikuwa kama vile hayupo. Ningemwona tu alipotaka nimwone, lakini nisingeweza kujua alifanya mambo yake kwa njia zipi. Hawa wengine walikuwa wepesi kufunguka kwa mambo mengi na hivyo ilikuwa rahisi kuwa na vitu na sehemu za kuwakamatia, lakini Festo? Hapana. 

Nilitakiwa kupata kitu cha kumnasia huyo jamaa, hasa kwa kuwa bado aliendelea kumfatilia bibie Miryam akimtaka kimapenzi. Mwanamke huyo hakuonyesha utayari wa kuwa ndani ya mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi hiki kwa kuwa kweli fikira zake zote zilielekezwa kwa Mariam. Karibia mara zote ambazo nilienda pale kwake na kuwa pamoja na mdogo wake, Miryam alikuwepo, na alijitahidi sana kuniunga mkono kwa kila jambo nililofanya ili binti Mariam aweze kukaa sawa tena. 

Wiki hizi nne za kuendelea kumsaidia Mariam zilihusisha lile suala la kumpeleka hospitali kwa ajili ya vipimo, na shukrani kwa Mola tukawa tumepata uhakika kuwa binti hakuingiwa vibaya kimwili, na hivyo alikuwa safi na salama kabisa. Hatukumwambia hilo, wala kuongelea waziwazi mbele yake mambo yaliyotokea usiku ule alipotekwa, na kadiri mazoezi ya kuuimarisha utimamu wake yalivyoendelea, ndiyo akawa anaendelea kufunguka kiutambuzi. 

Mwezi mmoja tu ukatosha kumfanya Mariam aanze kuzungumza kama ilivyokuwa awali, hata nyakati nyingine angewaita watoto wa hapo mtaani ili acheze pamoja nao ndani ya geti la nyumba yao. Alionyesha tabia za kitoto bado, lakini haikuwa kwa jinsi niliyokuwa nimemkuta mwanzoni kabisa. Wote tulijitahidi sana kumfanya afurahie maisha yake, na kilichokuwa kimebaki ikawa ni kumjuza kutambua tena yeye ni nani, na angepaswa kuwa nani kwenye maisha yake kwa mapenzi na uchaguzi wowote alioutamani. 

Chalii Gonga, mume halali wa madam Bertha, alikuwepo bado katika shughuli za biashara ambazo mke wake alimwachia, na mara kwa mara tungeonana pale Masai nyakati ambazo ningeenda na Tesha pamoja na Ankia. Mara hizo zote tulizokutana, hatukusemeshana, na alifanya iwe wazi kwamba hakutaka kunisogelea kabisa kwa sababu nafikiri kuna kitu ambacho Bertha alikuwa amefanya ili kuleta hali hiyo. 

Sikuwahi kumuuliza tena mwanamke yule kama kuna jambo lolote lilitokea baina yake na Chalii hasa baada ya jamaa kunikuta kwenye chumba cha hoteli ya madam siku ile, maana ndani ya hizo wiki chache nilikuwa nimekutana kimwili na huyo mwanamke karibia mara tano, lakini hakutaka kumzungumzia mume wake kwa undani, na mimi nisingeweza kumsukuma. 

Ila hali hii baina yangu na Chalii Gonga ilinionyesha wazi kwamba jamaa alikuwa amenyamazishwa. Lakini yote kwa yote, bado niliendelea kujitahidi kuwa makini sana mara zote ambazo ningemwona, kuepusha tu matatizo kwa upande wangu, yaani ya moja kwa moja, maana bado kuna hisia iliyokuwa ikiniambia kwamba mwanaume huyo alipanga kitu fulani. Kuwa chonjo ilikuwa lazima.

Na tukija upande wa familia yangu, haikuonekana kuwa na tatizo lolote tena upande wa mzee wangu, Mr. Frank Manyanza, tokea nilipokwenda kwenye ofisi yake kumwelezea vizuri kuhusiana na ishu ya Joshua kuihujumu familia yake ili aliuze shamba. Hakunitafuta kabisa kuongelea hilo suala tena mpaka Joshua amefungwa jela, na mimi nikachukulia kwamba mambo yalikwenda poa. 

Nilikuwa nimeshafanya safari fupi ya kuwatembelea mama na dada yangu na kuwasalimia pia, na tuliweza kuongelea mambo mengi sana na mama kuhusiana na maisha yangu, nikimwambia tu kuna vitu vya huku ningekuja kushughulika navyo nikishatoka likizo, na nikamtia moyo Jasmine asonge mbele kutoka kwa mwanaume yule ambaye hakujali hali yake. 

Mwanaume wake hakuwa mtu mwelewa, na alitoa maneno machafu sana hata alipokorofishana kidogo tu na Jasmine, na mimi nikawa nimemshauri tu dada yangu aachane na mtu ambaye hakumpa heshima, kwa kuwa bila hicho upendo ungetoka wapi sasa? Akawa ameniahidi kuwa angesonga mbele, na mimi nikamwahidi kuja kumjulia hali hapo kwetu kwa mara nyingine kabla ya wakati wake kujifungua kuwadia.

Kwa hiyo kwa ujumla ikawa ni kwamba kwenye suala la Joshua nilipata ushindi, masuala ya Mariam na Bertha ndiyo yakawa kwenye kalenda bado za kutarajia ushindi, lakini huyo Festo ndiyo bado akawa kikwazo. Ila nisingekata tamaa. Zamu hii sikutaka kumwambia bibie Miryam, oh kuna hiki, au kuna kile, hapana. Nilitaka nije nifichue kila kitu kwa vitendo tu. Na najua angekuja kushangaa mno baada ya kugundua rangi halisi ya yule mwanaume. 

Nilikuwa nimewasihi watu wa familia yake Miryam wasije kuzungumza na watu wa nje kuhusiana na ishu yote ya Joshua, na waliafikiana na hilo, lakini lengo langu hasa lilikuwa kuhakikisha habari za mimi kushirikiana na polisi mpaka kumkamata Joshua hazifiki kwa Festo; maana ingemwashia taa nyekundu ya hatari na hivyo kumfanya aanze kunifatilia zaidi. 

Ni huyu jamaa tu ndiyo aliyekuwa mwiba mgumu sana kwangu uliobaki kung'oa, na nilitaka kuhakikisha namwondoa pia maishani mwake Miryam kabla ya matatizo mengine kujitokeza....


★★★


Basi bwana, hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa. Mpaka kufikia sasa bado nilikuwa kwa Ankia, tukiendeleza maisha yetu ya mama mwenye nyumba na mpangaji wake, na urafiki wetu ulizidi kukua. Hiyo hasa ilitokana na kujuana naye kwa mengi zaidi ya story na msosi wake mtamu tu, ikiwa unaelewa namaanisha nini. Kufikia sasa mwanamke huyu alikuwa amefungua biashara nzuri sana ya duka, alipouzia vijora, suruali za wanawake, pamoja na nguo za watoto wa kike, watoto wadogo yaani, hapo hapo Mzinga maeneo ya barabarani kwenye shughuli nyingi.

Kwa hiyo kutokana na kazi yake, tungeonana kwa mida iliyoachana-achana sana, hasa jioni, usiku, au asubuhi tu. Ratiba yangu ya kutoka kwenda kwenye ishu ya madam Bertha ilikuwa kwa siku za Jumatatu, Jumatano, na Ijumaa, kuanzia asubuhi mida ya saa nne mpaka jioni. Mwanzoni ilikuwa na ulazima sana kukaa huko mpaka jioni, lakini kwa wakati huu, ningeweza hata kuondoka mapema maana wengi wa vijana wake walielewa namna ya kuunda yale madini. Sema tu ndiyo niliwekwa kama msimamizi eti!

Hivyo, nilikuwa na muda na siku za kutosha kukaa na binti Mariam na kuendelea na tiba yake. Kwa kipindi hiki, Tesha alikuwa anahangaikia zaidi kupata kazi nzuri ambayo ingemfaa, lakini hakuwa amepata kwa hiyo aliendelea kutulia huku akipata michongo ya hapa na pale mara kwa mara iliyomwingizia pesa ya matumizi yake binafsi ama kusaidia familia pia akiwa kama mwanaume. Hali kwa familia yake ilikuwa tulivu zaidi kwa wakati huu, na nilitamani sana iendelee kubaki namna hiyo hiyo bila drama nyingi kama zile za wiki kadhaa nyuma kutokea.

Sasa, leo ilikuwa ni siku ya Alhamisi, asubuhi na mapema kabisa. Kulikuwa na ishu ya maana sana kwa mrembo wangu iliyonihitaji, cheupe mwenyewe Bi Zawadi. Mwanamke huyo alikuwa na mpango wa kwenda sehemu fulani iliyoitwa Chamgando, ukiwa unaelekea Kisemvule kule sijawahi hata kufika, akiwa na lengo la kumwona mtumishi fulani wa kanisa la kilokole huko kwa ajili ya maombi "spesho" ambayo husafisha mabalaa yake, na kwa niaba ya familia yake.

Ingekuwa kama kwenda kwa Mwamposa tu lakini alikuwa anamjua vizuri sana mtumishi wa huko Chamgando, akisema ni mzuri sana, ana maono, nakwambia yaani dah! Ndiyo nikawa nimepata na huo mwaliko sasa wa kumsindikiza, na mimi ningefanyaje? Nisingeweza kumkatalia mrembo wangu. Ni kitu ambacho alikuwa ameshakililia kwa wiki chache sasa lakini kutokana na mambo ya hapa na pale nikawa sijaweza kuambatana naye, sanasana alikuwa akienda na Tesha kwa nafasi za Jumapili, hivyo leo ningeenda pamoja naye. Ahadi ni deni kama ujuavyo.

Kwa hiyo nilikuwa nimeamka mapema sana, nikajiandaa vizuri na kuvalia T-shirt langu jeupe la mikono mifupi, suruali nyeusi ya jeans, na kiatu cheusi kinachong'aa chenye muundo wa kiatu cha ballet, hutu ambato wakorea walitufanya tukawa fashion kwa kuvalia bila soksi na suruali ya kitambaa ikiwa imevaliwa kama njiwa. Nilikuwa nimetununua wiki moja nyuma, na sasa ndiyo ikawa mara ya kwanza kuvitumia.

Hii ikiwa ni mida ya saa mbili asubuhi sasa, nikatoka zangu na kuagana na Ankia, akiwa ananiambia mwonekano wangu ndiyo ungefanya watu wafikiri mimi ni mchina kweli, akisema nimependeza, nami nikamshukuru na kumwambia tungeonana baadaye. Nikatoka ndani hapo na kuanza kuelekea nje. 

Nikiwa usawa wa ukuta uliotenganisha nyumba hizi mbili, nikamwona bibie Miryam akiwa anapiga deki sehemu ya kibaraza chao kutokea kule ndani, ikiwa wazi hakuwa ameenda kazini bado, nami nikaelekea nje mpaka kufikia getini kwao. Mvua zilikuwa zikinyesha mara kwa mara hasa mwezi huu ulipoingia, na jana pia ilinyesha kwa hiyo ardhi ilikuwa mbichi. 

Nikaufungua mlango mdogo wa geti la nyumba yao majirani zetu kwa kuvuta kikamba nilichokuwa nimemsaidia Tesha kuweka siku ile, na nafikiri leo ndiyo ningekuwa mgeni wa kwanza kufika hapo ingawa hawa watu walinichukulia kuwa kama mwenyeji wao tayari.

Ile tu ndiyo nimeingia, nikamwona Miryam akijinyanyua na kusimama kutoka kwenye kuinama kwake kupiga deki, na baada tu ya kuniona pia, akaachia tabasamu la furaha lililofanya sura yake ipendeze sana. Mimi pia nikatabasamu na kujikuta nimeendelea tu kumtazama kwa furaha pia. 

Alikuwa amevaa T-shirt nyeusi ya mikono mifupi, huku kutokea kiunoni akijifunga kwa khanga safi lakini niliweza kuona kwamba ilificha suruali laini nyeusi, labda skinny, aliyokuwa amevaa kwa ndani na kuivuta juu kiasi miguuni. Nywele zake laini na ndefu alikuwa amezibana juu ya kichwa chake, na weupe wake uliomulikwa kwa jua la asubuhi ulimfanya aonekane kung'aa mikononi kutokana na umaji iliyokuwa nayo.

"Karibu." 

Akaniambia hivyo kwa sauti yake tamu sana. Na ndiyo iliyokuwa moja ya sauti za kwanza nilizohitaji kusikia kwa asubuhi hii!

Nikasema, "Asante," kisha ndiyo nikarudishia mlango wa geti na kuanza kuelekea hapo kibarazani, nikilipita gari lake huku nalipiga-piga kidogo kwa kiganja.

Akawa ananitazama kwa yale macho ya 'nakuona,' kisha akasema, "Mzee wa kung'aa!"

Nikatabasamu kidogo na kuinua viganja vyangu huku nikijiangalia kwa majivuno, nami nikamwambia, "Kama kawaida yangu."

Akacheka kidogo kwa pumzi.

"Naona unapiga usafi," nikamwambia hivyo.

"Yeah. Kama kawaida yangu," akasema hivyo pia.

Nikatabasamu kidogo huku nikiangalia ulowani wake wa jasho uliofanya nywele zake zilainike.

"Mamu bado hajaamka," akaniambia.

"Ah, hamna shida... Mamu tutaonana baadaye. Nimekuja kumpitia cheupe wangu," nikamwambia hivyo.

"Ahaa... ee kweli ameniambia... unamsindikiza kwa mtumishi, si ndiyo?" akasema hivyo.

"Mm-hmm," nikakubali.

"Ahah... alivyo na hamu ya kwenda nawe! Kama vile mnaenda date," akatania.

"Ahahah... usipime! Ila nina hamu pia ya kwenda, maana... sikumbuki mara ya mwisho nimeenda kanisani ilikuwa lini. Ndo' nafasi ya kuanza kumrudia Mzee wa Siku physically hii," nikamwambia.

"Wewe pia unataka kuponywa?" akauliza.

"Eeh, kama itawezekana... fresh. Siyo kwamba naumwa au nini, ila... najua ibada ni muhimu haijalishi dini ni ipi. Biblia inasema pale ambapo kuna roho ya Mungu watu wake wanapaswa kukusanyika pia, kwa hiyo kuwa na sehemu za ibada ni lazima ili kuwakusanya watu wamwabudu na kumsifu... na kuwaombea wengine," nikamwambia hayo.

"Wacha! Kumbe na Biblia unasomaga?" akauliza.

"Huwa nasoma kila nikipata nafasi, nina app kwenye simu. Mistari miwili, mitano, natafakari, namshukuru Mungu. Angalau kale ka-touch na muumba kanakuwepo bado... ndiyo maana ananifanya nazidi kuwa handsome," nikamwambia hivyo.

Miryam akacheka na kuinamisha uso wake, yaani kile kicheko laini cha kutoka moyoni. Alionekana kufurahi sana.

"Hahah... au nadanganya?" nikamuuliza.

Akaniangalia na kusema, "Hamna... ahahah... ni kweli kabisa."

"Sa' mbona unanicheka?" nikamuuliza huku nikitabasamu kiasi.

"A-ah... ahahah... siyo hivyo, yaani... unaongea kama Tesha," akasema hivyo.

"Ahah... eeh, akili zetu zinafanana ndiyo maana tunapatana," nikasema hivyo.

"Kweli. Ila... naona kama we' umemzidi kidogo. Atakuwa anachukua madarasa kutoka kwako," akasema hivyo.

Nikacheka kwa furaha kiasi, naye akacheka pia, kisha kwa sekunde chache tukabaki kuangaliana machoni huku tukitabasamu. Ulikuwa utizami wa uliojaa upendezi mwingi sana, sote tukiwa tunafurahia hali hii mpya ya urafiki baina yetu, naye Miryam akaibana midomo yake kiasi na kutazama pembeni, kitu ambacho kikanifanya mimi pia niache kumwangalia usoni na kushusha macho yangu kuelekea chini.

Ndipo akaniangalia na kusema, "Karibu mwaya. Karibu ndani... ma' mkubwa atakuwa anamalizia kujiandaa."

Nikawa nimemwangalia na kusema, "Sawa. Inabidi nivue viatu ili nisikuchafulie...."

"Hamna shida, pita tu," akanikatisha kwa kusema hivyo.

"A-ah, hamna bwana. Kuvua viatu lazima," nikasema hivyo na kusogea pembeni huku nikianza kuvua kiatu. 

Akawa anatabasamu na kusema, "Kumbe na we' unajali usafi eeh..."

"Uhakika. Hiyo ishu naielewa inavyochosha. Mama alipokuwaga akipiga deki halafu sisi tupite tu na miguu yetu, wee! Tungeinama kudeki nyumba yote," nikamwambia hivyo.

"Ahahah... hata kama hamjachafua kwingine?" akauliza.

"Yaani kote! Lilikuwa somo zuri ili tusirudie tena," nikamwambia nikiwa nimemaliza kuvua viatu vyote.

"Aliwapatia. Haya, ingia ndani. Me namalizia hapa," akasema hivyo.

"Sawa," nikamjibu.

Akainama tena na kushika dekio, nami nikawa namwangalia tu kwa utulivu, kisha ndiyo nikaingia ndani hapo na kurudishia mlango. 

Nilijihisi vizuri sana kuwa na hako kawakati pamoja na huyo mwanamke, yaani ile hali nzuri ya kirafiki tuliyokuwa nayo sasa ilinipa amani sana na kujenga hamu ya kutaka kuendelea kuukuza na kuukuza tu huo urafiki. Ni mengi tuliyokuwa tumepitia na huyu dada mpaka kufikia hatua hii ambayo mwanzoni nilidhani isingekuwa rahisi kufikiwa, kwa hiyo niliithamini sana.

Hakukuwa na mtu hapo sebuleni, nami nikasogea mpaka sehemu ya dining na kumwona Bi Jamila akiwa anatengeneza chai pale jikoni kwao. Na ilikuwa mapema kweli, kwa hiyo nikawaza labda hata ilikuwa ni uji. Nikaelekea mpaka upande huo wa jikoni na kumsalimu, naye akaniitikia vizuri sana huku akinikaribisha kupika. Alikuwa akitengeneza dawa ya kuchemsha, kwa ajili yake mwenyewe, kisha ndiyo angeandaa na chai pia. 

Kwa kuelewa kwamba nilikuja kumpitia mwenzake, akawa ameniambia ndiyo sasa hivi tu Bi Zawadi alikuwa ameingia chumbani ili kuvaa, na kweli nikasikia sauti ya mrembo cheupe wangu kutokea chumbani ikinisemesha, JC bwana karibu, sichelewi, natoka sasa hivi tunaenda. Nikamwambia atumie muda wote aliohitaji kumaliza kujiandaa, nami nikaendelea kusimama pembeni yake Bi Jamila na kuongelea dawa hiyo aliyokuwa akichemsha.

Baada ya dakika chache tu, Miryam akawa amerejea ndani kwa kilichoonekana kuwa amemaliza kupiga deki, naye akaelekea chumbani kwake huko. Nilikuwa nikitamani sana yaani katukio kokote kale kajiunde tu ili arudi huku na niweze kumsemesha tena, basi tu ilikuwa imeshajijenga ndani yangu kutaka kumwangalia kwa ukaribu au kunena naye mara kwa mara. 

Sifichi kuwa upendezi wangu kumwelekea mwanamke huyo ulikuwa mkubwa zaidi kwa wakati huu, lakini najua nilitakiwa kuendelea kuheshimu uhusiano wetu wa udada na ukaka tuliokuwa tumejenga, na hivyo kunizuia kuvuka mipaka kimawazo kumwelekea. Kama unaelewa namaanisha nini.

Bi Zawadi akawa ametoka hatimaye, akipendezea kwa kuvaa nguo nzuri sana ya kitenge na kuzibana nywele zake za kusukwa kwa juu, huku akishikilia mkoba mdogo ambao alisema ulikuwa maalumu kwa ajili ya kuwekea Biblia. Nikamsifia kwa kudamshi, mwenyewe akipenda kweli kujua alionekana vizuri, nasi tukiwa tayari kuondoka sasa ndiyo Miryam akawa amerejea sehemu hii ya sebule. Akatuaga vizuri pia, na ilikuwa ni yeye na Bi Jamila pekee ndiyo waliokuwa macho kutuaga, Tesha na Mariam bado walikuwa wanavuta mashuka yao huko vitandani. 

Kulikuwa na ishu ya kupangilia mambo yaliyohitajika kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa ya Bi Zawadi, ambayo sasa ilikuwa karibu zaidi kufika, na ndiyo Miryam akamwambia mama yake mkubwa kwamba wangekuja kuongelea mambo yaliyohitaji kumaliziwa tukisharudi baadaye. Inaonekana bibie asingekwenda kazini leo, kwa hiyo hapo ndiyo tukaachana nao, kisha Bi Zawadi na mie kuingia mwendoni kulifata jumba la ibada.

★★

Tulichukua daladala za kwenda Kisemvule, tukapita maeneo kadhaa mpaka kufikia sehemu fulani ambayo tulishuka na kupanda daladala nyingine tena iliyoelekea Chamgando. Watu wengi walikuwa wakitutazama sana mimi na Bi Zawadi, na mwanamke huyu alikuwa mwenye story zenye ucheshi sana; akigusia mara nyingi sana suala hilo la mie kutazamwa mno. 

Alitaka kujua ikiwa labda nilikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamke mmoja ama ikiwa na mimi sikuwa nimetulia kama Tesha, nami nikamwambia sikuwa na mtu kabisa. Aliona kwamba nampiga fix tu kwa sababu alikisia labda hata nilikuwa nimeshatoka na wanawake kama Ankia na wengine ambao hakuwajua, na kauli zake zilinifanya nicheke sana lakini kweli nikampiga fix kwa kusema sikuwa wa namna hiyo. Nilitulia kabisa. 

Akanipongeza na kusema natakiwa kujitahidi sana kubaki safi maana magonjwa yalikuwa mengi mno, na huku tulikokuwa tunaenda ndiyo ningepata kujua mengi kuhusu maisha yangu na jinsi ya kuyaendesha ili yafanikiwe zaidi. Aliifanya hali hii ionekane kama tulikuwa tunaenda kwa mganga yaani, na tulipofikia hilo eneo la Chamgando kweli ikaonekana kama vile tulikuwa tunaenda kwa mganga. 

Ilikuwa ni sehemu ambayo haijaendelea kivile, yaani utafikiri tulikuwa tumekuja kijijini kabisa. Watu waliotuona walitusindikiza kwa macho toka tumeshuka garini mpaka kuingia kwenye kijia kilichoelekea ndani zaidi ya eneo lenye uoto mwingi wa asili na miti mingi ya minazi. Ndiyo tukawa tumeifikia nyumba ndogo iliyojengwa kwa mbao sanasana na kufunikwa na Maturubai na mapazia mekundu na ya zambarau, huku kukiwa michoro ya msalaba mweupe hapa na kule. Lilikuwa ni kanisa chipukizi. 

Nikamuuliza Bi Zawadi alipajuaje huku kote, naye akaniambia mke wa mwenye hili kanisa aliwahi kuishi Mzinga, na walijuana hasa kipindi ambacho wazazi wao akina Miryam walipoteza maisha yao. Akasema kwamba mchungaji alikuwa mzuri sana na upako wake, lakini hapa tulikuwa tumekuja kuonana na mama mchungaji kwa kuwa ni yeye ndiye aliyekuwa na maono, na alitoa maneno ya ushauri na saha fulani hivi lakini kwa njia ya upako. Dah! 

Nikasema haina noma, nasi tukaifikia nyumba hii takati... taka... takatifu ya ibada. Kulikuwa na mwanamke aliyebeba mtoto mgongoni hapo nje, akionekana kuwa mtunzaji wa kanisa sijui, naye akatufata na kutusalimu kwa heshima. Yaani sana, kiasi kwamba alipiga magoti mpaka chini alipokuwa ameushika mkono wangu, nami kiukweli nilijisikia uajabu kiasi. Lakini tukaingia ndani kwa pamoja baada ya mwanamke huyo kutuongoza mpaka kufikia viti vya plastiki, nasi tukakaa. 

Mwanamke huyo akatuambia mama mchungaji alikuwa anakuja sasa hivi tu, uzuri Bi Zawadi alikuwa ameshawasiliana naye pia, na hakuishi mbali na kanisa. Kwa hiyo dakika chache za kumsubiria zikatumiwa vyema na Bi Zawadi kunielewesha mambo yalivyo kwa sehemu hii. Ilikuwa ni sehemu ya kawaida tu, ya mwanzo, hata sakafu ilikuwa ya michanga na kinara cha mbao iliyofunikwa kwa kitambaa chenye msalaba uliochorwa kwa chaki. Naelezea mengi ndiyo ili uone nilichokiona, yoh! 

Basi, mama mchungaji akawa amefika hatimaye, akiwa ni mmama ambaye hakuwa mbali sana kiumri kumfikia hata mama yangu mzazi, arobaini ya mwishoni, naye akanikaribisha vizuri sana. Leo haikuwa siku ya ibada ya pamoja, bali kama tu maombi spesho ya mtu mmoja mmoja, na Bi Zawadi akawa amemwambia kwamba mimi ndiyo "yule kijana" aliyemsema ambaye alikuwa kama baraka kubwa sana kwenye maisha ya familia yake, na alinileta ili kunisaidia nitakasiwe maisha yangu maradufu zaidi na mwenyezi Mungu.

Mwanamke huyo, mama mchungaji yaani, aliniangalia kwa umakini sana kama vile ananisoma, nami nikawa nimebunda tu kama vile sielewi somo. Kisha akaanza ghafla tu kusema kwamba anayaona maisha yangu, anajua nimetoka kwenye mazingira magumu sana lakini ni kama vile maisha yangu yote yaliongozwa na bahati kunifanya nitoke sehemu mbaya mpaka kufikia sehemu nzuri, na bado ilikuwa kwa kupambana sana. 

Akasema nina moyo mzuri mno, lakini kuna kitu fulani ambacho kilikuwa kinaihangaisha nafsi yangu na hivyo nilikuwa najaribu sana kukiepuka kwa kujifanya kama sijali, ila kutoka ndani ya moyo wangu nilikuwa najali sana. 

Mh? Alinifanya nimwangalie kwa mkazo zaidi, kwa kuwa sikatai, kuna vitu kweli nilikuwa najitahidi sana kuviepuka maishani mwangu kwa sababu zangu mwenyewe, lakini sikudhani mwanamke huyu angeweza kujua ni mambo gani. Labda aliotea tu. Ndipo akasema niache kuwaza kwamba kuliepuka jambo hilo kutanifanya niridhike, badala yake ifike wakati nitambue kwamba hilo ndiyo litakuwa chanzo kikubwa sana cha furaha ya kweli ambayo ninaitafuta. Dah!

Sawa aliongea kimafumbo fulani hivi, ile kwamba ni yangu tu mimi kujua, na kiukweli alinifanya niguswe sana kwa kuwa maneno hayo yaligusa sehemu fulani kubwa sana ya maisha yangu ambayo nilikuwa nimeiweka pembeni mno. Mbali sana yaani. Na hapa akawa amenifanya niitafakari, kitu ambacho kikanikosesha amani kiasi. 

Sijui ilikuwa ni upako kweli, ama huyu mwanamke alijua tu kusoma nyota? Kwa vyovyote vile, akanishauri nianze kuamini kwamba Mungu yupo pamoja nami, na angenipatia zawadi nzuri sana kwa mambo mengi mazuri niliyokuwa nayafanya, lakini hilo jambo aliloniambia naepuka ndiyo lingenikamilishia furaha niliyoihitaji. 

Mi' bwana nikakubali, amen kama zote, kisha mama akaanza maombi. Tukasimama kabisa, mzee nikaombewa yaani, maneno yaliyosemwa yalinigusa sana mpaka nikajihisi kutaka kulia. Sikutegemea kabisa hali iwe namna hiyo, lakini nashukuru tu mabomu ya 'fire' yaliporushwa sikuanguka chini. Nilikuwa nimevaa T-shirt nyeupe. Akili yangu hii!

Tulipomaliza maombi ya zaidi ya nusu saa, tukaketi tena, nikianza kuulizwa najisikiaje, nami nikasema nilijihisi vizuri kiasi. Bi Zawadi alifurahi sana alipotambua kuwa niliguswa mno na hii kitu. Nisingeweza kusema mengi mno kwa kuwa kuna hisia zilivurugana ndani yangu, ila nilijikuta nimeipenda sana hii kitu, nami nikaomba kujua ratiba za ibada kwa wiki. 

Wakati akiwa ameanza kuelezea, simu yangu ikaita, nami nikaitoa mfukoni ili kuiondolea sauti, lakini baada ya kuona mpigaji kuwa askari Ramadhan, nikawaomba wanawake hawa nipokee simu mara moja, nao wakakubali. Nikanyanyuka na kuelekea mpaka nje, kisha nikapokea ili nimsikilize jamaa. Sikuwa nimetegemea anitafute leo.

"Hallo..." nikasema hivyo.

"Yes, JC? Uko wapi?" Ramadhan akasikika.

"Nipo... maeneo siyo mbali sana na Mbagala. Vipi mkuu?" nikamuuliza.

"Uko na kazi, au?"

"Hapana, ni matembezi tu..."

"Naomba tukutane upesi. Nakutumia location kwa sms, ufike hapa mida ya saa sita hadi saa saba. Utaweza?" akauliza hivyo.

Nikatazama saa mkononi kukuta ni saa tano kasoro, nami nikamwambia, "Ndiyo, naweza. Ni muhimu sana?"

"Yes, ni muhimu. Na uwe cautious," akasema hivyo.

"Sawa. Nakuja," nikamwambia kwa uhakika.

Simu ikakatwa.

Nikatulia kidogo na kutafakari ni nini kilichokuwa kimezuka kwa upande wa askari huyu, ila kujua hilo ingenibidi niende huko haraka. Nikarejea pale ndani na kuwaambia wanawake wale kuwa nilipata dharura ndogo iliyonihitaji kuwahi, kwa hiyo nikaomba radhi ya kuhitaji kuondoka haraka. 

Mama mchungaji akasema haina shida kabisa, naye Bi Zawadi akasimama pia na kuahidi kuja kwa ajili ya ibada Jumapili. Mimi pia nikatoa ahadi hiyo, kisha ndiyo mama mchungaji pamoja na yule mwanamke mwingine wakatusindikiza kwa pamoja mpaka kufikia sehemu ya kupandia daladala. 

Ulikuwa ni wakati mzuri sana kuwa pamoja na Bi Zawadi huku, na nilitamani hata tupite sehemu pamoja naye ili tupate kitafunwa na nini, ila ukitegemea na muda niliokuwa nimepewa na yule askari ingetubidi tu tuchukue usafiri na kuondoka kurudi nyumbani. Kwa hiyo baada ya daladala kufika, tukaagana kwa mara ya mwisho na mama mchungaji na kupanda, haoo tukaishia.

★★

Mbinde za hapa na pale za usafiri zilisababisha tukawie kiasi, mpaka inaingia saa sita kabisa ndiyo tukawa tumeshukia Mzinga. Sasa kutokana na dirisha la wakati kuwa dogo kwa upande wangu, nikamwambia Bi Zawadi atangulie kwenda nyumbani ili mimi nipitilize mpaka huko nilikokuwa naenda, halafu tungekuja kuonana baadaye. Hakuwa na neno. Nikamwitia boda ili asisumbuke kutembea mpaka nyumbani, na baada ya yeye kupanda na kuondoka, mimi pia nikachukua boda na kuomba nipelekwa Rangi Tatu fasta.

Tayari askari Ramadhan alikuwa amenitumia ujumbe kwenye simu wa sehemu ambayo alitaka tukutane, na alitaka niwe makini sana ili nisije kufatiliwa maana sehemu hii ilikuwa ya kibinafsi mno. Nilihisi tu kungekuwa na vitu vya siri-siri kwenye huu mkutano wangu pamoja naye, kwa hiyo nikamwambia nimeelewa na niko njiani, nikaweka akilini hilo eneo na jengo alipotaka niende, kisha nikaifuta sms yake na kuzima simu pia. Mambo ya kuwa keyafuli hayo!

Nimekuja kufika kwenye eneo husika tayari saa saba ikiwa imeshaingia, lakini ya dakika za mapema, nami nikaelekea mpaka kwenye jengo nililoelekezwa. Nikaenda moja kwa moja kwenye chumba ambacho kilikuwa na namba hususa niliyopewa, kwa sababu kulikuwa na vyumba vingi vyenye namba pia kutokana na jengo hilo kuwa la upangishwaji, nami nikafungua mlango na kuingia.

Nikasimama usawa wa mlango ndani ya chumba hiki ambacho kilikuwa na hali ya ugiza sana kutokana na kutokuwa na madirisha makubwa isipokuwa sehemu nyembamba tu kwa juu zaidi za kupitishia hewa, na taa ndogo iliyomulika mwanga wa rangi ya chungwa ndiyo iliyokuwa katikati kutokea juu. Kilikuwa kipana lakini hakukuwa na vitu vingi ndani humo. Usawa wa sehemu hiyo katikati hapo sakafuni kulikuwa na meza moja tu, ambayo haikuzungukwa na viti, bali watu. Watatu.

Wawili sikuwafahamu, ila mmoja alikuwa ni askari Ramadhan. Ni yeye tu ndiye aliyekuwa amevalia kwa njia ya kawaida kama raia, lakini wenzake walivaa kwa mitindo fulani kama vile walikuwa majasusi. Na miili yao ilijengeka vyema sana, wakiwa na nyuso makini, mmoja mrefu kunifikia na mwingine mfupi kiasi, na kwenye hiyo meza kulikuwa na karatasi kubwa, pana mno, ambayo nadhani ilikuwa imeandikiwa mipango yao maalumu. 

Hapa nikajua nilikuwa nimeingia sehemu yenye hali makini sana, na huu mchezo ulikuwa wa kiwango cha aina yake.

"Karibu JC. Ingia," askari Ramadhan akanisemesha namna hiyo baada ya kuniona.

Nikaelekea mpaka hapo walipokuwa na kusimama upande mmoja wa meza, nami nikawatikisia vichwa kisalamu wenzie Ramadhan, na jibu lao likawa kwa njia hiyo hiyo.

Ramadhan akasema, "Huyu ndiyo CI wangu wa kwanza niliyewaambia. Anaitwa JC. JC..." 

"Naam..." nikaitika.

"Hawa ni maaskari wenzangu, special forces, wako nasi kwenye hii ishu. Huyu ni Richard, na huyu ni Mwitakabilamba," Ramadhan akawatambulisha wenzake.

Kudadeki! Ilikuwa karibu nimwombe arudie kulisema tena hilo jina la pili, lakini nikakaza tu na kutikisa kichwa utadhani nilikuwa nimelielewa. Yaani jina lilikuwa na "mwita," "kabila," na "lamba." Siyo poa!

"Tunajitahidi kufanya kila kitu kwa care sana, ndiyo maana tumekutana kama hivi. Una uhakika hamna mtu anakufatilia?" Ramadhan akaniuliza.

"Ndiyo, nina uhakika. Na simu nimezima," nikamwambia hivyo.

"Vizuri. Sasa... hawa hapa, ni vichwa wa vikosi maalumu ambavyo vitashughulika na round up yote ya hawa watu tunaowanyatia, na nimeona nikukutanishe nao ili wajue kwamba we' ni mmoja wetu, na part unayocheza kwenye hili game..." Ramadhan akasema hivyo.

"Sawa sawa," nikakubali.

"Tutakapowasomba watu wote wa huyo madam Bertha, itabidi iwe kwa mpigo mmoja, na hivyo hiki kikao kidogo ndiyo kitakuwa cha mwisho ili kuhakikisha kwamba tunajua kila kitu kiko sehemu husika... tukipiga tu hatua, iwe ni moja kwa moja. Si unaelewa?" Ramadhan akaniuliza tena.

"Ndiyo. Na unamaanisha kwamba hiyo round up iko karibu zaidi kufanywa?" nikamuuliza pia.

"Ndiyo. Karibu sana," Ramadhan akajibu.

"Kama lini?" nikauliza.

"Kwa upana wa sehemu zote za hiyo organization ya madawa ya kulevya, ndani ya wiki moja tu ndiyo tutapiga hatua ya kuwakusanya wote," akajibu hivyo yule mwenye jina gumu kama Ntibazokiza.

"Ila bado tunahitaji kujua ikiwa info zote za sehemu, procedure, na usambazaji, kufikia sasa... ikiwa zipo vile vile bado au kuna mabadiliko ambayo yanafanywa au yatafanywa kabla ya hiyo wiki kuisha," akasema hivyo yule Richard.

Nikamwangalia usoni askari Ramadhan.

"Anamaanisha anataka uelezee jinsi ambavyo mambo yalivyo. Kila kitu tunacho mezani, ila hawa wenzangu wanahitaji review kutoka kwako kabisa. Unaweza kuwaelezea," Ramadhan akaniambia hivyo.

Nikashusha pumzi kiasi na kuangalia mezani, nami nikaona ramani iliyokuzwa vizuri sana ya jiji la Dar es Salaam kwenye karatasi iliyokuwepo hapo. Kulikuwa na michoro-michoro ya kalamu pia, nami nikawaza bora kama kungekuwa na kifaa cha kielektroni kwa ajili ya kuonyeshana mipangilio ya mambo, lakini kwa sababu za kiusalama na uharaka nilielewa kwa nini waliamua kutumia pepa. Hakukuwa na shida.

Nikawaambia, "Okay. Hamna lolote lile lililobadilika, zaidi... ndiyo wanazidi tu kuimarisha mfumo wao mzima wa hii biashara. Iko hivi. Huyu madam Bertha na kundi lake wana vyumba maalumu kwenye majengo makubwa 21 hapa jijini, ambavyo anatumia kutunza mizigo mingi ya madawa ya kulevya. Kunakuwa na watu wake kwa hizi sehemu, na wamekaa kama watu wa kawaida tu; kama ni duka la nguo, au vitu vya rejareja, ama mashine ya kusaga nafaka... wanakuwa wanakaa kama wauzaji wa kawaida tu, lakini ikifika mida special kwa ajili ya kufanya delivery ya madawa hayo, wanaanza kuyatoa na kuyasambaza kwa kutumia system ya taka..."

Ramadhan, akiwa amekunjia mikono yake kifuani, akatabasamu na kutikisa kichwa chake, kisha akasema, "Nani angefikiria wangekuwa wanatumia njia ya kuondoa uchafu ili kusambaza uchafu wao?"

"Siyo rahisi. Kwa hiyo wanatumia system ya takataka?" Richard akaniuliza hivyo.

Nikasema, "Yeah. Bertha, na jamaa yake anaitwa Festus, wana ushirika na makampuni manne jijini yanayohusika na huduma ya kuondoa taka majumbani, maofisini, kwenye makampuni, vyuoni, everywhere yalipo available. Nafikiri mmeshayajua..."

"Yeah, tunayajua..." Mwitakabilamba akasema hivyo.

"Yes, kwa hiyo ikitegemea na pale ambapo order za hayo madawa zinatakiwa ziende, zinapelekwa kupitia hayo magari ya taka. Wanaweza feign kwamba wanaenda kupitia takataka hapa au kule, na hata kama unakuta gari linakuwa limejaa takataka halisi, kunakuwa na sehemu ya kificho kwa ndani ambayo ndiyo inakuwa imebeba mifuko yenye haya madawa. Kwa hiyo wanaoyapokea wanakuwa wanajua kabisa... ah, ikifika saa fulani, gari la taka litapita hapa. Kama kunakuwa na fuko la uchafu kwenye dustbin, wanaokuja kulitoa na kuli-empty wakimaliza, wanayatia madawa humo yakiwa kwenye mifuko safi na kurudisha fuko la kwenye kopo likiwa na hayo madawa. Kwa hiyo wanaoyategemea wanaenda upesi kuyachukua kwa njia hiyo, na malipo wanakuwa wameshafanya mapema. Njia za kuhakikisha kwamba hawaonwi tayari zimewekwa mahala pake, kwa hiyo unakuwa ni utaratibu usioshtua yeyote ambaye hahusiki," nikawaelezea.

"Na hiyo ni kwa sehemu zenye watu wenye nazo tu bila shaka," akasema hivyo Richard.

"Yes. Kinondoni, Kigamboni, Makumbusho, Kariakoo, Sinza, Mlimani, UDSM, sehemu nzuri za Mbezi, Kawe... yaani, nyingi sana kuzungukia jijini. Utaratibu wao wa malipo na delivery ni wa maana, gari liwe kubwa ama dogo, haijalishi. Wafanyakazi wapo wa kutosha, na wako fasta yaani kama tu system ya kumwita Uber... ila yao bora zaidi," nikawaambia hivyo huku nikiwaonyeshea kwenye ramani.

"Ni bora kwa uchafu zaidi. Wako smart lakini, hakuna traffic hata mmoja ambaye atasimamisha gari la takataka kuchunguza. Na wanaowasambazia lazima wawe wanalipwa vizuri ndiyo maana wanaongezeka, eh?" akaongea hivyo Richard.

"Ajira zenyewe safi mbinde. Nani atawalaumu? Pesa popote, watakwambia angalau hawafanyi ushoga," Ramadhan akasema hivyo.

"Ila ndiyo lazima huu upuuzi ukomeshwe. Shida siyo wanaonunua, ila ni wanaoyasambaza, haijalishi ni wakubwa au wadogo. Na vipi kwa walala hoi? Hivi vitu vinawafikia?" akauliza Mwitakabilamba.

"Zinafika, ila mfikishaji siyo Bertha. CI wangu mwingine anasema Bertha ni kama retailer kwa watu wakubwa, anapokea chake kikubwa, anawasambazia kipato wanajeshi wake waliohusika, na yeye anakula pesa ndefu... kama malkia vile," akasema hivyo Ramadhan.

Kauli yake Ramadhan ikanifanya nimtazame kimaswali kiasi. Alisema "CI" wake mwingine, yaani Confidential Informant, neno linalomaanisha mtu afanyaye kazi na maaskari kisiri ili kuwakamatisha wahalifu. Kwa hiyo alimaanisha kulikuwepo na mtu mwingine kwenye mtandao wa mishe zake Bertha ambaye alifanya kazi na maaskari hawa kisiri na kuwapa taarifa, kama vile mimi tu. Sikuwa najua hilo, kwa hiyo sikujua alikuwa amemwongelea nani.

"Okay sawa. Hivyo ndiyo network yao ya usambazaji inavyoenda. Vipi kuhusu ishu ya wewe kumtengenezea coke ili akuze soko lake?" Mwitakabilamba akaniuliza.

"Ndiyo, huu mwezi ulioisha ndiyo limekuwa suala la kipaumbele kwake, na wameshaanza kuyazagaza. Faida inaingia. Kwa ajili ya hiyo operation, Bertha alitafuta sehemu nzuri sana ya kuniweka mimi na watu wake ili tuyatengenezee huko bila kuvuta attention. Kwenye supermarket moja kubwa," nikamwambia.

"Ipo Riverside. Ubungo," akasema hivyo Richard.

"Yeah," nikakubali.

"Tumeshai-monitor pia, kama tu hayo majengo 21. Kilichopo hapa JC, ni kusubiri tu tuwe kwenye position nzuri ya umoja ili hiyo round up ikifanywa, iwe ni kwa siku moja ambayo Bertha, sijui Farao, Tito, Sudi, na nani... huyo Chalii... anayefanya uuzaji wa wanawake, yeah wote yaani... WOTE... tutawaweka ndani. Na itakuwa kwa siku ambayo hawatategemea," Ramadhan akaniambia hivyo.

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Kwa hiyo endelea kungoja kwa subira, uwe makini, mchezeshe Bertha karibu, ujue kabisa pale utakapotakiwa kuwepo hiyo siku ikifika. Si unaelewa?" Ramadhan akaniambia hivyo.

"Ndiyo, naelewa," nikamwambia.

"Vizuri sana, JC. Yote uliyosema yako in check. Kinachotakiwa sasa hivi tu ni kufuata mwongozo atakaokupa Rama, na hii wiki ikiisha huu mzigo utakuwa umeshautua," akaniambia hivyo Richard.

"Sawa sawa, ila...."

"Shika hii," Ramadhan akanikatisha kwa kusema hivyo.

Alikuwa ameninyooshea kifaa fulani kidogo sana cha kielektroni, nami nikakipokea na kumtazama.

"Kaa nayo muda wote, itunze vizuri. Wakati mwafaka ukifika, utajua jinsi ya kuitumia," akaniambia hivyo.

Nikatikisa kichwa na kuiweka mfukoni, nami nikamwambia, "Lakini... bado sina chochote juu ya yule jamaa, Festus. Ni fence aliye makini sana, namaanisha... anajua kujilinda, so, sijapata lolote la kumweka kwenye position ambayo wengine watakuwepo ili muwaangushe wote pamoja naye. Tutafanyaje kuhusu hilo?"

Maaskari hawa watatu wakaangaliana kwa pamoja, kisha Ramadhan akasema, "Usijali. Nitashughulika na hilo. Ni mjanja huyo jamaa, lakini atakamatika tu."

Nikatikisa kichwa kuonyesha nimemwelewa.

Ramadhan akatazama saa yake mkononi, kisha akasema, "Alright. Hii session imeisha. JC... unaweza kwenda. Be very careful. Umenielewa?"

"Ndiyo. Nakuelewa mkuu. Asante," nikamjibu hivyo.

Akanionyesha ishara kwa mkono kuwa niende sasa, na wenzake wakanitikisia vichwa vyao kama kuniaga.

Nikageuka zangu na kuanza kujiondokea sehemu hiyo, lakini kabla sijaufikia mlango nikawa nimekumbuka jambo fulani, nami nikawageukia na kusema, "Mkuu..."

Wote wakaniangalia, na Ramadhan akasema, "Ndiyo?"

"Umesema kwamba... kuna CI wako mwingine ndani ya network ya Bertha. Naweza kujua ni nani?" nikamuuliza kwa umakini.

Akatulia kidogo, kisha akaniambia, "Usiwaze kuhusu hilo. Na yeye yuko kama wewe tu, hajui kwamba uko pamoja nami, na sidhani kama anakujua."

Nikaendelea kumwangalia usoni tu.

"Ni muhimu msijuane kabisa ili mbaki kuwa salama mpaka hii yote iishe. Umeelewa?" Ramadhan akaniuliza hivyo.

Nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo, kisha ndiyo nikafungua mlango na kutoka ndani humo.

Mambo yalikuwa yanaelekea kupamba moto! Ah, yaani kuwa sehemu kama hiyo ilinifanya nijione kuwa mpelelezi fulani hivi, lakini yule mnafiki kinoma! Huo unafiki naoongelea ndiyo ambao ningetakiwa kuuendeleza kwa upande wa madam Bertha ili mambo haya nyuma ya pazia lake yashike hatamu haraka siku ambayo angetumbuliwa majipu yake ya maovu, yeye pamoja na kundi lake lote lililohusika. 

Nilijihisi vizuri sana kuwa karibu zaidi na ushindi dhidi ya kile ambacho mwanamke huyo alikuwa amemfanyia Joy na watu wengi ambao sikuwafahamu pia. Kuangusha biashara zake zote ghafla yeye na watu wake waliohusika lingekuwa ni tukio zito sana ambalo lingemuumiza, kwa hiyo nilikuwa na hamu kubwa ya kuja kushuhudia hayo yote wiki moja mbeleni. 

Lakini, bado nilikuwa namtafakari sana huyo "CI" mwingine wa askari Ramadhan. Bora kama ingekuwa najijua tu kuwa mwenyewe kama "snitch" kwa madam Bertha, lakini sasa kujua alikuwepo mwingine pia kulinipa hisia fulani za wasiwasi kiasi. Vipi ikiwa kama huyu mtu alinijua, au nilimjua, na tulijuana? Alikuwa ndani ya huu mchezo kwa muda gani mpaka na yeye awe ametoa taarifa zilezile nilizokuwa nimewapa maaskari hao? Vipi kama bila mimi kujua, huyu jamaa angekuwa "snitch" kwangu mimi pia kuelekea mipango ya maaskari na ya madam Bertha mbeleni? Angekuwa nani huyu mtu?

 

 

★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next