MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA PILI
★★★★★★★★★★★★★★
Nilikuwa namuwaza sana huyu CI mwingine kwa kuwa sikupenda tu hii hali ya kuwekwa gizani, ila kama tu askari Ramadhan alivyokuwa ameniambia, huenda sababu kuu na nzuri ilikuwa ni ili tuwe salama. Ni kweli kutojuana ingesaidia tuwe salama, ila ndiyo huwezi kuwa na uhakika sikuzote kwamba uko salama kwa sababu tu mwingine anadhani upo salama. Kuna kitu kilikuwa kikiniwasha sana kutaka kujua huyu mtu alikuwa nani, na ningejitahidi kuhakikisha namjua.
Baada ya kuondoka hiyo sehemu, nikaelekea mpaka eneo la kupanda daladala ili nirejee Mzinga kushughulika na mgonjwa wangu wa muhimu sana, Mariam. Akili ilikuwa imehamishwa sana kutoka kwenye upande mzuri wa kiroho kwa msaada wa Bi Zawadi ile asubuhi, na sasa ilikuwa kwenye ule mbaya kutokana na kuwaza mambo mengi ambayo yangefanyika hizi siku chache zijazo kwa upande wake madam Bertha.
Kulikuwa na ka hisia ka sintofahamu kalikozunguka sana ndani yangu, hali fulani ya kujihukumu kutokana na kujiingiza katika hayo yote tokea Joy alipouawa. Sawa, sehemu kubwa ya hiyo ishu ilikuwa ni ili kukomesha matendo yasiyo ya kiungwana ya Bertha na watu wake, ila huu mwezi mzima, kuwa naye karibia kila mara, yaani sikatai kwamba nilikuwa nimeshamzoea yule mwanamke kwa njia ambayo ndiyo ilisababisha sehemu fulani ya hisia zangu ihisi kujuta kiasi shauri ya kujua kile ambacho kingempata mbeleni akikomeshwa matendo yake.
Ila si ilikuwa kwa nia nzuri? Si nilifanya hivi ili akome kufanya vitu haramu na hivyo kumwangusha kama nilivyokuwa nimetazamia toka mwanzo? Kwa hiyo sikupaswa kabisa kuhisi hivi. Kazi ingepaswa kuendelea. Ndani ya wiki moja haya yote yangekuwa yamekwisha, na nikaombea tu yaishe kiwepesi kabisa.
Kuwaza vitu vingi vya namna hiyo kukawa kumeifanya akili yangu irudie jambo fulani ambalo mara nyingi nilikuwa naliweka pembeni sana, yaani dada yake Joy, Adelina. Mwanamke huyo mwenye kujali alikuwa na kawaida ya kunitumia jumbe za salamu mara kwa mara, na mimi kutokana na kuwa na mambo mengi nilishindwa kumjali hata mara moja. Yaani kwa huo mwezi mzima uliopita, alikuwa amenitumia jumbe kadhaa za salamu, lakini sikuwahi kujibu hata moja.
Sasa wakati huu nikiwa naelekea huko kwa Mariam ndiyo nikaona ingekuwa vyema nikimtafuta, kumsalimu tu na kuomba radhi kwa kutingwa na mambo mengi. Inawezekana hata familia yake ilidhani suala la kuwasaka wasababishi wa kifo cha Joy ndiyo lilikuwa limezikwa, maana muda ulikuwa ukienda upesi sana.
Nikawa nimeifikia Rangi Tatu kwenye mida ya saa nane ya saa tisa hivi, nami nikaingia Zakhem kupata msosi kabla sijatimkia Mzinga. Ilikuwa ni kwenye mgahawa ule mzuri wa Zakhem, sehemu ya nje kwenye uwazi uliojengewa mabenchi-meza mapana kwa ajili ya wateja, nami nikakaa na kuagiza msosi mzuri. Kutazamwa mno na baadhi ya watu ilikuwa kama kawaida, na mimi nikaendelea kula hamsini zangu tu.
Nilikuwa nimeshaboresha vizuri ratiba yangu ya ulaji, ila siku ya leo ilipaswa kunisamehe tu kwa kukosa mlo wa asubuhi kwa kweli. Mambo yaliingiliana. Nikiwa nasubiria msosi uletwe ndiyo nikaamua kumpigia Adelina sasa, naye hakukawia kupokea.
"Halloo..." sauti yake ikasikika upande wa pili.
"Hallo. Vipi dada?" nikamuuliza hivyo.
"Safi. Za masiku JC?"
"Ah, Mungu anasaidia. Nimeona nikujulie hali leo maana... kwa kweli mambo yamekuwa mengi, wakati mwingine mpaka nakosa kukujibu ukinijulia hali dada'angu..."
"Kweli aisee, mambo lazima yatakuwa mengi. Me nikafikiri labda hata ulipoteza simu ama hutaki tu kujibu..."
"Ahahah... hapana, na... nisamehe tu kwa hilo..."
"Haina shida. Mapumziko yako yanaendaje?"
"Namalizia-malizia siku za likizo then nitarudi kwetu. Bado si upo Mbezi toka umeondoka Nachingwea?" nikamwambia.
"Kinyerezi, ndiyo," akajibu.
"Yeah, Kinyerezi kweli. Vipi kazi?"
"Ah, sasa hivi nipo tu. Ile kazi niliiacha," akasema hivyo.
"Kumbe?"
"Eeeh, ilikuwa hailipi kivile, kwa hiyo nikaamua kuachana nayo. Ninatarajia kuanza nyingine pale airport..."
"International?"
"Eeeh."
"Ah, hongera sana. Unaenda kupaisha ndege?"
Akacheka kidogo kwa furaha, kicheko chake kizuri kikinifanya nitabasamu, naye akasema, "Ni uhudumu tu. Niliona nisomee haya masuala miaka miwili mitatu iliyopita bwana, sasa hivi ndiyo majibu ya sala za kupata hiyo kazi yamejibiwa. Nitapangiwa labda... kama ni nje au ndani ya ndege."
"Vyema sana Adelina. Utakuwa sehemu nzuri sana... na ndiyo inakufaa."
"Eti eeh?"
"Kabisa."
"Asante," akasema hivyo.
Ni hapa ndiyo msosi wangu nilioagiza ukawa umeletwa, nami nikaanza kula taratibu huku simu ikiwa sikioni bado.
"Mama mzima?" nikamuuliza Adelina.
"Hajambo. Anaendelea vizuri sasa hivi. Vipi na wewe? Mkeo hajambo?" akaniuliza pia.
"Ahah... yupo. Siku hizi na ye' amekuwa bize kweli..."
"Eeh, aliniambia amefungua duka, nitapanga nije kuliona siku moja."
"Itakuwa vizuri sana. Tena sasa hivi kwa sababu umetulia, kwa nini tu usije kututembelea? Ni kitambo hatujaonana..." nikamwambia hivyo.
"Kweli. Unataka tuonane tena?" akauliza.
"Ndiyo. Nimekukumbuka," nikamwambia hivyo.
"Hata mimi JC," akasema hivyo kwa njia fulani ya taratibu.
Nikatabasamu kiasi, kisha nikasema, "Unaweza kuja hata Jumamosi ikiwezekana."
"Mmm... Jumamosi hapana, ninaenda sehemu fulani kusaidia maandalizi ya harusi jioni hiyo hiyo. Labda kesho. Au... kesho una mipango mingine?"
Kesho ilikuwa ni Ijumaa, kwa hiyo ndiyo nilikuwa na mipango mingine, hivyo nikamwambia, "Eeh, kesho nitakuwa location nyingine. Vipi ukija Jumapili basi?"
"Ni sawa. Tutaangalia na Kariakoo Derby," akasema hivyo.
"Hahahah... kumbe na we' shabiki wa mpira?" nikamuuliza.
"Ndiyo, naangalia pia. Wewe Simba au Yanga?"
"Simba."
"Wow! Mimi pia," akasema hivyo kwa shauku.
"Safi sana. Uje sasa ili tumzomee vizuri Ankia Yanga ikitandikwa 10," nikaongea kiutani.
"Hahahahah... sawa nitafika," akasema hivyo.
"Haya bwana. Me ndo' naweka msosi mahala pake hapa. Karibu," nikamwambia hivyo.
"Asante, me mwenyewe ndo' napakua," akasema.
"Haya, tutachekiana mida eh?"
"Poa. Badae," akaniaga.
Nikakata simu baada ya kumaliza maongezi hayo na mwanamke huyo, nami nikawa nimejisikia vizuri kiasi. Inaonekana kufikia wakati huu Adelina alikuwa ameshaizoea ile hali ya kumpoteza mdogo wake, na nilikuwa nimetaka kuuliza lolote kuhusu upande wa suala la kifo cha Joy, ila nilighairi baada ya kuhisi namna ambavyo alitulia kihisia wakati huu. Kama ni kumwongelea Joy, basi tungemwongelea akifika huku hiyo Jumapili.
Na hakuwa amekosea aliposema kwamba Jumapili ilikuwa ni siku ya mechi ya watani wa jadi, almaarufu Kariakoo Derby. Kulikuwa na msisimko mkubwa kutoka pande zote za mashabiki kwa kuwa ni mechi iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu kubwa sana, na nilitazamia pia kuitumia pindi hiyo kufurahia wakati mzuri zaidi pamoja na marafiki zangu wa huku; kujumuisha na ujio wa Adelina pia. Na sijui kwa nini tu, ila kuongea naye hivyo, kulinipa hisia fulani tamu sana. Ila sikutaka kupeleka mawazo mbali mno. Yajayo nisiyoyajua ndiyo yangefurahisha.
★★
Nikawa nimemaliza msosi baada ya dakika chache, kisha nikalipa na moja kwa moja nikaelekea kupanda daladala ili nifike Mzinga. Kama kawaida tu, haikuchukua dakika nyingi sana nami nikawa nimeshafika huko, kisha nikaelekea pale ambapo duka lake Ankia lilikuwa ili nimsalimie kwanza. Alifurahi kuniona, naye akasema alikuwa na mpango wa kwenda nyumbani mapema, kwa hiyo nikamwambia angenikuta kwao Mariam ikiwa asingenikuta kwake.
Basi, nikaendelea na safari yangu mpaka nilipofika kwao Mariam, nami nikaingia getini hapo na kumkuta Tesha akiwa amekaa pamoja na binti Mariam varandani. Alionekana kumwonyesha mdogo wake vitu fulani kwenye simu, na baada ya Mariam kuniona, akanyanyuka na kunifata huku akitabasamu kwa furaha. Akanikumbatia kwa nguvu kweli utadhani hakuwa ameniona miezi, nami nikatoa viashirio vya bandia kumwelekea Tesha kwamba ningekufa kutokana na jinsi nilivyobanwa na binti, naye akatabasamu kiasi na kusimama.
Mariam akaniachia na kunitazama machoni huku akitabasamu, naye akasema, "Shikamoo JC?"
Nikatabasamu pia na kusema, "Marahabaa. Aisee! Unalisema jina langu vizuri sana sasa hivi. Nikupe maua yako bwana..."
Nilipomwambia hivyo, nilikuwa nimenyanyua kiganja changu kwa upande wa juu, naye akaweka chake karibu na changu kwa upande wa chini, vidole vyetu vikiwa vimegusana kiasi, kisha tukavichezesha haraka-haraka kwa pamoja huku tukisema "Broooop," halafu ndiyo sote tukapiga vidole viwili kiganjani kwa njia iliyotoa sauti. Sijui kama hii taswira imeeleweka vizuri!
Huu ulikuwa mtindo mpya wa kisalamu ya kishkaji niliokuwa nimemfundisha binti, na alikuwa ameupenda sana zaidi ya ule wa "Hi-five" niliomzoesha kipindi kile, na hii mpya tuliitamka 'bruup.' Kwa hiyo nyakati zozote alipojisikia furaha kwa kufanya jambo zuri, ningetumia mtindo huu pamoja naye ili kuikuza zaidi furaha yake na hisia ya kujiamini, na yeye alipenda mno kusifiwa kwa kuendelea kujitahidi kuimarika zaidi kiutimamu.
Mariam alikuwa anafanya maendeleo upesi sana, yaani ni kama yale mabaya yote yaliyokuwa yametokea hayakutokea kabisa, na hilo lilikuwa jambo jema. Niliona wazi kwamba si muda mrefu sana huyu binti angeacha kuwa "binti" tu, na hatimaye angerudia hali yake ya kawaida ya kujitambua kuwa mwanadada aliyeelekea kuwa mwanamke kikamili.
Baada ya kupiga hiyo 'Broop,' Mariam akasema, "Nimechora na kuandika leo, JC. Nimeandika."
"Wow! Kweli? Umeandika nini?" nikamuuliza.
"Alph, alpha-beti..." akasema hivyo.
"Zote?"
Akatikisa kichwa kukubali.
"Safi. Enhe... na nini kingine?" nikamuuliza.
"Majina yetu wote," akasema hivyo.
"Wewee... kweli? Nani kakuelekeza?" nikauliza.
"Kaandika mwenyewe. Mama, Tesha, JC, Miryam... kaandika hayo yote mwenyewe," Tesha akaniambia hivyo baada ya kutufikia.
"Aisee! Safi sana Mamu. Vipi kusoma? Unasoma-soma?" nikamuuliza binti.
"Yes. I am... studying..." Mariam akasema hivyo.
Nikajikuta natabasamu kwa furaha sana baada ya binti kusema hivyo, nami nikamwekea kiganja ili tufanye 'Broop' tena. Eti na Tesha pia akataka kuweka kiganja chake kwenye vyetu aliunge, lakini Mariam akamsukuma kwa nguvu ili asituharibie, mpaka nikashangaa. Tesha akacheka na kunyanyua mikono juu kama kusema yaishe, kisha Mariam akarudi kwangu na kunipa 'Broooop' ndefu kwa raha zote.
"Tufanye mazoezi ya kinanda, eh?" Mariam akauliza.
"Kweli, nenda kakiandae tuje tupige zoezi," nikamwambia hivyo.
Mariam akaanza kuelekea kule ndani, huku akitazamana na kaka yake kwa njia ya chuki eti, naye Tesha akamfanyia ishara kwa vidole vyake viwili kuwa anamtazama kwa umakini.
Tesha akanisogelea tena, nasi tukagongesha viganja vyetu kirafiki, kisha akasema, "Nakuona mchungaji. Leo kitakatifu kweli, au siyo?"
"Ahahah... ma' mkubwa wako amenipeleka huko Chamgando aisee, nimepapenda!" nikamwambia.
"Katusimulia. Anasema umeguswaaa..."
"Kasema na nini kingine? Kwamba nimeanguka?"
"Hahah... labda siyo JC. Tena umevaa nyeupe kabisa, hata kama ungekuwa na mapepo usingeanguka ili tu kulinda nguo yako isichafuke..."
"Unanijua vizuri kumbe."
"Mbona ukamkimbia sa'? Ulienda wapi?"
"Niliitwa sehemu mara moja."
"Na demu?"
"Ahah... akili zako hizo..."
"Aa, we' sema tu. Huwa kuna tumambo-mambo unaficha sana, ila me huwa najua mbona..." akasema hivyo.
"Mambo kama yapi?"
"Kama wewe na Soraya," akaniambia hivyo.
Nikamkazia macho.
"Najua ulimla Tausi mwanangu, wala hamna noma," akasema hivyo.
"Umejuaje?"
"Mwezi mzima umetosha kunifanya nijue, we' unanionaje? Anakukubali mno, naonaga anakupigia wee... ila we' unamkaushia tu. Nikajua tayari ushakula na kutema..."
"Mbona unaongea kama vile imekuuma sana?"
"Ah, toka hapa! Kiniume nini, kwani me sina demu?"
Nikacheka kidogo kwa pumzi.
"Sema una mambo kubwa sana we' jamaa, unatoka-toka sana kwa mishe kali inaonekana. Ungenipa michongo basi na mimi," akasema hivyo.
"Siyo mambo kama hayo, ni... masuala tu ya kifamilia narekebisha," nikamwambia hivyo.
"Ahaa..."
"Eeh. Nani yupo huko ndani?" nikamuuliza hivyo huku tukianza kuelekea mlangoni.
"Mama hao... na Shadya. Wanapiga tu umbea kuhusu ishu ya Doris," akasema hivyo.
"Doris ndo' nani?" nikamuuliza.
"Ih! Hivi kumbe nilikuwa sijakwambia?" Tesha akasema hivyo.
"Kuniambia nini?" nikauliza.
"Kuna sherehe ya harusi, ya huyu dada anaitwa Doris. Ni ndugu yetu pia, sijafatilia kivile ila nadhani tunatakiwa kumwita binamu. Anaolewa," akasema hivyo.
"Ooh, sawa. Yeye anakaa wapi?"
"Kijitonyama. Si unamkumbuka nanilii... yule Dina... tuliyeendaga kwake kule Uhasibu?"
"Ee, namkumbuka..."
"Ee, Dina ni mdogo wake Doris sasa..."
"Okay... sawa. Ndo' maandalizi ya harusi yameanza..."
"Eee, wamewaweka da' Mimi na Shadya wanakamati... wanaanza na kitchen party kabisa... halafu..."
Kabla Tesha hajamaliza kuniambia kuhusu suala hilo, Mariam akatokezea mlangoni kwa kasi mpaka tukashtuka kiasi, naye akasema, "JC, njoo. Nimeshaweka kinanda."
Nikatabasamu na kumwambia sawa, kisha ndiyo kwa pamoja tukaingia ndani.
Mama wakubwa walikuwa hapo na Shadya wakipata mazungumzo yao wanawake, nasi tukasalimiana vizuri sana na Bi Zawadi akaanza kukumbushia jinsi mambo yalivyokuwa asubuhi tulipokuwa tumekwenda kwa mama mchungaji. Mariam akaniondoa sehemu ya warembo wangu upesi na kunipeleka dining, maana aliona kama vile anacheleweshwa sana, kwa hiyo nikakaa naye pamoja na Tesha ili kuendelea na utaratibu wetu kama kawaida.
★★
Nilitumia muda mrefu nikifanya michezo na mafunzo pamoja na Mariam, mpaka inafika mida ya saa mbili usiku, bado nilikuwa hapo kwao. Kufikia wakati huu Tesha alikuwa ameondoka kwenda kutembea sijui, na wakina Bi Zawadi na Shadya walikuwa wakisaidizana kupika.
Mapishi ni kitu kilichokuwa kikimvutia sana Mariam, alipenda hata kucheza nami kwa kujipikilisha kipindi cha nyuma, lakini kwa sasa kila mara alipoona wakubwa wanaandaa misosi, alijitahidi kuhusika kwa lolote ili kuwasaidia. Kwa hiyo alikuwa akienda jikoni na kurudi kwangu mara kwa mara, na mida hii nilikuwa sehemu ya sebuleni nikingojea Miryam arejee ili nimsalimu kabla ya kuwaaga wa hapa na kwenda kupumzika huko kwa Ankia.
Nilikuwa nikiwaburudisha mama wakubwa kwa story za hivi ama vile, huku na wenyewe wakiwa wamenipatia madokezo kuhusiana na sherehe ya huyo mwanamke aliyeitwa Doris iliyokuwa inakaribia. Kulikuwa na hamu kubwa kutoka kwa Bi Zawadi hasa kuelekea hafla hiyo kwa sababu alisema yeye na mama yake Doris walikuwa marafiki sana, na alimwona Doris wakati alipozaliwa pia. Huyo Doris hakuwa mbali sana kiumri kumfikia Miryam, akiwa kwenye thelathini ya mapema, na mama zao walikua pamoja kutokea udogoni.
Kwa hiyo hapa mbele kungekuwa na sherehe mbili; hiyo ya Doris, pamoja na sikukuu ya kuzaliwa ya Bi Zawadi, ambayo ingeitangulia harusi ya Doris. Mambo yaliyokuwa yakija kwa upande wa familia hii yalionekana kuwa mazuri, na wakaniomba nihusike pia kwenye lolote ili kupendezesha hafla hizo kwa mguso wangu waliouona kuwa baraka sikuzote. Nikawahakikishia kwamba hilo lingetimia kwa asilimia mia.
Basi, saa mbili ikiwa inaendelea kutembea, nikawa nimepigiwa simu na Ankia, na nilipopokea akaniambia alikuwa kwake muda mrefu tayari, na alinimiss, hivyo niende upesi maana alikuwa akiandaa msosi mtamu kwa ajili yetu; na sikupaswa kutoa kisingizio sijui Mamu, sijui nini, na yeye alikuwa wa muhimu. Dah! Nikaona nimkubalie tu, nami nikawaambia mama wakubwa pamoja na Shadya kuwa kuna ishu nilihitaji kufanya hapo kwa Ankia mara moja hivyo ningeondoka sasa ili kwenda kuiandaa.
Kama kawaida, malalamiko kutoka kwa Shadya na Bi Zawadi ya mimi kutaka kuondoka wakati tu msosi ulikuwa unaivishwa yakaanza, lakini nikawatuliza na kuwaahidi ningetenga muda mzuri wa kufurahia mlo pamoja nao; sema kwa wakati huu mambo yalikuwa mengi kidogo. Yaani nilikuwa napendwa na hawa watu hadi kujigawa ilikuwa tabu kiasi, lakini Ankia na yeye aliihitaji ushirika wangu kwa hiyo zamu hii ingekuwa yake.
Mama wakubwa na Shadya wakaridhia, nami nikamuaga na Mariam pia nikisema kesho kama nitawahi kutoka huko "mjini," basi nitakuja ili tucheze tena. Hakuwa na neno. Tukapiga 'Broop' kama kawaida, kisha nikawaambia wote wampe Miryam salamu zangu akirejea, nami ndiyo nikawaacha.
Nikaelekea upande wetu na kumkuta Ankia akiwa sebuleni, mwili wake ukiwa ndani ya nguo za unyumbani, kilemba kichwani, na akiwa anaangalia tamthilia runingani. Tukasalimiana vizuri, nami nikaelekea chumbani na kuvua T-shirt na suruali, nikavaa pensi nyepesi na kaushi tu, kisha nikarudi sebuleni kukaa pamoja naye sofani na kuanza story.
Ankia akaanza kunisimulia kuhusu jamaa fulani aliyekuwa anamsumbua sana kwa kwenda pale dukani kwake kumtongoza kila siku, nami nikaanza kumtania ile ya 'Ankia kapata mchuumba, Ankia kapata mchuumba.' Akacheka sana na kuniambia niache mambo yangu ya kipuuzi.
Kweli nilikuwa tu nina hamu ya kutaka kukaa na Ankia ndiyo maana hata kusema niendelee kuwa pale na mama wakubwa kumsubiria Miryam haikuwa kitu nilichowazia sana tena, kama kumwona bibie ningemwona tu tena, huu sasa ungekuwa ni muda wangu na Ankita. Alikuwa anatoa kero zake mwenyewe na mimi nikimpa ushauri kwa utani mwingi, huku mboga ya msosi mtamu uliolekea kuiva ikihisika vyema puani mwangu kutokea huko jikoni.
Katika zile pindi ambazo angenyanyuka kwenda kukoroga-koroga mapishi yake na kurudi kukaa tena, nilikuwa nikijibu jumbe tofauti-tofauti kwenye simu yangu na kuperuzi mitandao ya kijamii, hii ikiwa ni saa tatu, na wakati Ankia alipokuwa amenyanyuka kwa mara nyingine tena na kwenda jikoni, simu yangu ikaanza kuita.
Nilipoangalia mpigaji, nikakuta ni yule Dotto, kikaragosi mtiifu wa madam Bertha, ndiye aliyekuwa akinipigia. Kufikia kipindi hiki nilikuwa na namba zake pia, kwa sababu na yeye alikuwa na sehemu muhimu kwenye upande tofauti wa biashara za Bertha kama tu ilivyokuwa kwangu, kwa hiyo wakati mwingine tulikuwa tukifanya collabo na nini... hasa kutokana na yeye kuyapenda madawa niliyokuwa nawatengenezea.
Lakini haikuwa kawaida yake kunipigia ama mimi kumpigia, isipokuwa tu iwe ni jambo muhimu, sanasana madam Bertha akihusika; yaani sikuwa na kitu chochote na huyu jamaa ambacho kingefanya aonekane kama mshkaji wa karibu sana mbali na kujuana tu kwa sababu ya biashara zetu na madam. Hivyo kupiga kwake simu muda huu kukaniweka katika hali ya umakini, nami nikapokea nikiwa hapo hapo sofani na kumsikiliza.
"Halloo..." sauti yake ikasikika.
"Yeah, niaje?" nikasema hivyo.
"Poa. Upo kitaa?"
"Cha Masai, yeah. Vipi?"
"Njoo hapa Masai," akaniambia.
"Bar? Upo hapo?" nikamuuliza.
"Ee, njoo."
"Ishu gani? Maana ndo' msosi unawekwa mezani sa'hivi," nikamwambia hivyo.
"Achana na njaa wewe, njoo hapa sasa hivi kuna ishu ya muhimu. Fanya haraka," akasema hivyo kwa sauti makini.
Mh?
Nikamwambia, "Poa. Dakika tano basi."
"Zisipite," akasema hivyo, kisha akakata simu.
Nikatulia kidogo kutafakari ni nini ambacho kingekuwa kinaenda kutokea hapo Masai, na ni mawazo mawili yaliyoingia hasa kwenye fikira zangu.
Kwanza, inawezekana tu kwamba Bertha alikuwa amefika hapo na kutaka niende, ama hakuwa amefika hapo na ndiyo Dotto akawepo kusimama kwa ajili ya ishu niliyohitajiwa. Lakini cha pili, nikawaza vipi ikiwa labda kwa njia fulani yale mambo yangu ya pembeni na maaskari yalikuwa yamewafikia hawa watu? Je kama waliniona, ama kuhisi kuwa ninaelekea kuwa-snitch, na huu ungekuwa mwito wa kwenda kubainisha upande gani niliokuwa hasa, ama labda hata kuumizwa?
Ingenibidi niwe makini mno maana chochote kile kingeweza kutokea, na nikikumbukia vizuri kabisa kwamba askari Ramadhan alikuwa amenipa kifaa fulani maalumu cha kutumia wakati wa hali ya dharula, nikanyanyuka kutoka hapo na kwenda kuvaa suruali pamoja na kofia yangu, ile kama kibandiko ambayo Tesha alininunuliaga kipindi kile ndiyo nimejuana naye. Kifaa kile nikakitia mfukoni.
Baada ya kuvaa hivyo nikatoka na kumuaga Ankia kwa kusema naenda hapo Masai mara moja. Alifikiri nimeitwa labda kwenda kunywa na hivyo ningekimbia msosi aliokuwa akiandaa, lakini nikamwambia hapana, ningeenda tu kuongea na mtu mara moja kisha ningerudi kula. Kwa hilo hakuwa na neno, nami nikatoka na kuanza kuelekea huko Bar.
★★
Nikiwa ndiyo naikaribia Masai, pembezoni mwa geti la mbele kwenye mwingilio wa jengo hilo niliweza kuliona gari la madam Bertha, ile Harrier yake ya silver, likiwa limeegeshwa usawa huo na Dotto mwenyewe akionekana kusimama karibu nalo. Alikuwa amevaa tracksuit kubwa ya blue kama jezi ya klabu ya Chelsea, huku akiwa amesimama na wanaume wengine wawili wa mitaa hii hii akionekana kuongea nao vitu vya kihuni tu, nami nikakaribia sehemu hiyo na kusimama pembeni.
Aliponiona, akanisogelea na kugongesha tano pamoja nami, na wenzake vilevile, kisha akaniambia kwamba kuna sehemu natakiwa kwenda naye si mbali sana na hapa, kwa hiyo niingie kwenye gari ili anipeleke. Nikamuuliza wapi, lakini akasema twende kwenye gari ndiyo tutaongea vizuri, naye akawaaga wenzake na kwenda kuingia kwenye gari, huku akinionyeshea ishara kwa kichwa kuwa niwahishe.
Nilikuwa nimeshapandisha mashaka hata zaidi, lakini hakukuwa na nafasi ya kuwa mwoga hapa. Nilikuwa tayari kwa lolote, kwa hiyo nikaingia upande wa mbele pia pembeni yake, naye akatia gari moto na kuanza kulitembeza. Taratibu tu tukaiacha Masai, tukielekea lamini huko, nami nikaamua kuongea sasa maana jamaa alikuwa kimya tu.
"Mishe zinaendaje?" nikamsemesha.
"Ah, fresh. Fresh. Mambo ni wali nazi," akasema hivyo.
"Haujaja Masai muda. Kulikoni leo? Umewamiss wa huku?"
"Haamnaa. Nilikuwa nimekufata wewe tu," akaniambia hivyo.
"Kwa nini?" nikamuuliza.
"Si nimekwambia kuna sehemu nakupeleka?" akasema hivyo.
"Eeeh, ila hujasema ni wapi," nikamwambia hivyo.
"Tulia sasa. Ni surprise," akaongea namna hiyo.
Nikamtazama kwa umakini sana, kisha nikaangalia pembeni na kuuliza, "Madam anajua kuhusu hii... surprise?"
"Mhmhm... unataka sana niiharibu hiyo surprise, eti?"
"Oh, kumaanisha kwamba yeye ndiyo anafanya hii surprise, si ndiyo?"
"Tutajuaje? Inabidi kulifungua kwanza boksi ndiyo uione. Tulia. Boksi lako unaenda kulifungua muda si mrefu," akaniambia hivyo.
Nikamtazama usoni kisomi zaidi, naye akaniangalia na kutabasamu kiujeuri kiasi, na safari ikaendelea tu.
Tulikuwa tumeingia lami na kuelekea upande wa huko Rangi Tatu, lakini yaani bado ilikuwa ni hapo hapo Mzinga gari likawa limeingia kwenye barabara ya changarawe upande wa pili wa lami hiyo kutokea huko tulikotoka. Yaani, tukawa tumeivuka lami na kwenda upande wa pili wa Mzinga. Akaliendesha gari taratibu kupitia barabara ya changarawe kuelekea sehemu ya ndani zaidi ya mitaa hiyo ambayo sikuwahi kuwa na kawaida kabisa ya kuitembelea, mpaka alipolifikisha eneo lililokuwa na kumbi ya vinywaji na starehe kama tu Bar ya Masai.
Lakini huku palikuwa na hali ya ugiza sana, hapakuwa na watu wengi hapo. Sehemu alipoegeshea gari, kulikuwa na gari lingine aina ya Toyota Vanguard nyeusi, nasi tukashuka kwa pamoja nikiwa sijauliza kingine chochote mpaka wakati huu. Mambo mawili yakawa hakika. Moja, ni kwamba hakudanganya aliposema kuwa hatungeenda mbali, yaani hapa hata kwa mguu tu tulikuwa tunafika na kurudi tulipotoka upesi, na mbili, kilichokuwa kinanisubiri kama "surprise" ndiyo kilikuwa huko ndani.
Dotto akakutana nami mbele ya gari na kuniambia, "Karibu Facebook. Ushawahi kuja hapa?"
Nikatikisa kichwa kukanusha, nami nikamwambia, "Masai pamekuboa sana? Mpaka ukaamua kuja kunipea surprise yangu huku..."
Akacheka kidogo na kunishika begani huku akisema, "Masai kuna macho mengi mno. Huku ndo' pametulia. Twende."
"Subiri. Si uniambie tu kuna nini? Unanipa hali ya wasiwasi bro," nikamwambia hivyo.
"Ah, usiogope..."
"Siogopi..."
"Ee, ndo' twende sasa. Tumekaa pamoja mwezi mzima tunapiga mishe safi halafu huniamini bana? Come on," akanisisitizia huku akitangulia.
Nikafata nyuma yake.
Sehemu hii kimwonekano haikuwa na ule ubora wa kadiri kuifikia hata Masai; jengo lilishikiliwa na kupambwa na mbao nyingi, isipokuwa tu sehemu ya kaunta, na hata waliofika kulewa hapo hawakuwa wengi kivile. Yaani ilikuwa kama vile hamna umeme, taa pekee zikiwa zile za kuwaka-waka kwa mapambo, hapakuchangamka kabisa, lakini ni wazi Dotto hakuwa amenileta ili tujichangamshe hapo.
Tukaipita tu sehemu ya kaunta na kuelekea ndani zaidi mpaka kufikia mlango ambao nilikisia ndiyo ulikuwa wa chumba kama cha VIP kwa hapa Facebook, naye Dotto akafungua mlango na kuingia. Nikajitia ujasiri zaidi na kumfata pia, na kweli kilikuwa chumba kwa ajili ya maVIP, ingawa hakikuwa bora kwa lolote lile ambalo niliwahi kuona. Mwonekano wake ulikuwa wa kujitahidi, lakini sikukazia fikira zangu kwa vitu vilivyokuwa humo, bali watu niliowakuta.
Wanaume. Wawili. Na niliwafahamu vizuri sana. Wote walikuwa wameketi kwenye masofa ya humo, huku katikati kwenye meza kukiwa na sahani yenye kitimoto nyingi, pamoja na chupa chache za bia na K-vant; wakiwa wanatazama upande wangu kwa kuridhika. Ilikuwa ni Chalii Gonga, pamoja na mshirika wa kundi la Festo kutokea kule Red Room, yule jamaa aliyeitwa Sudi!
Mh? Sikutakiwa kuonekana kwamba nilishangaa, lakini nilishangaa. Sikuwa nimetarajia kabisa. Chalii Gonga alionekana makini akiwa ndani ya Manga pana nyeusi na suruali ya jeans, pamoja na buti za kaki miguuni, huku kichwani akivaa kofia kama alivyopendelea. Sudi yeye alikuwa amevaa T-shirt la mikono mifupi lenye rangi mchanganyiko pamoja na suruali ya kijani, nyepesi kwa michezo, huku kiatu cheupe kama vile ametoka sehemu fulani kufanya ukocha wa netiboli kikiificha miguu yake chini.
Nikasimama tu nikiwaangalia watatu hawa, namaanisha na Dotto, ambaye akaenda mpaka alipokaa Chalii Gonga na kuketi kwenye mkono wa sofa, kisha naye akawa ananitazama kwa utulivu kama wawili hao tu. Kofia yangu ilikuwa imeficha kiasi sehemu ya juu ya uso wangu, kwa hiyo kwa jinsi nilivyowaangalia kwa umakini na kuchanganywa kwa wakati mmoja, ilionekana kama nimekuja kigaidi zaidi.
Sudi akasema, "Karibu JC. Kaa hapo tuongee."
Huyu huyu jamaa ndiyo yule ambaye mara ya kwanza kabisa madam Bertha kunipeleka kule Red Room alikuwa ananitendea vibaya kwa chuki binafsi, lakini sasa akawa eti ananikaribisha kama vile tuna amani sana wakati hata sikuwahi kuwa na habari naye. Kumkuta hapa akiwa na Chalii kuliwasha taa nyekundu ya hatari kali kwenye hisia zangu, lakini zaidi ni kwa nini Dotto awe pamoja nao na kutumiwa kunileta kwao. Baada ya kukaribishwa hivyo, nikaendelea tu kusimama na kuwaangalia.
"Wewe ndiyo... kaa hapo tuongee," Chalii akaniambia hivyo.
Nikamtazama Dotto na kuuliza, "Nini kinaendelea?"
Chalii Gonga akatabasamu na kuvuta pombe yake, naye Dotto akasema, "Boksi ndiyo limefunguka. Surprise!"
Nikatabasamu kiasi na kusema, "So... uko kwenye Kahoot na hawa watu, ama labda ni mkutano wa wote na madam hajafika?"
Chalii akamwambia Sudi, "Ahah, si unaona? Yaani kashachizika mno kuwa kibenteni wa mke wangu, unafikiri ataambilika?"
"Zipo njia nyingi za kushawishi watu, lakini ana akili. Tumpe tu ukweli aji-adjust, mengine yatafata," Sudi akasema hivyo.
"Kaa chini dogo. Hakuna mabunduki humu, wala usijali," Dotto akaniambia hivyo.
"Niko sawa nikisimama. Semeni mlichoniitia," nikawaambia hivyo kwa ujasiri.
Sudi akaniangalia usoni kwa umakini, naye akasema, "Toa hiyo kofia."
Nikaishika kofia yangu na kuirekebisha vizuri zaidi kichwani, halafu nikaendelea kumwangalia.
Dotto akatabasamu na kutikisa kichwa chake kiasi.
"Hapa dharau hazitakusaidia kwa chochote mdogo wangu. Ungekuwa unajua ni namna gani unaweka maisha yako hatarini kuwa na Bertha, usingejifanya una kiburi sana," Sudi akaniambia hivyo.
"Yangu me na Bertha, ni yangu me na Bertha. Nimekujulia kwake, na sina ishu yoyote na wewe. Na pia yako wewe na yeye hayanihusu mimi. Sa' sijui unataka nini," nikamwambia hivyo
"Nataka utumie akili yako, na kipaji chako... vizuri. Bertha anakutumia tu, lakini ukiisha faida kwake atakutupa sehemu mbaya mno," Sudi akasema hivyo.
"Okay, kwa hiyo we' unataka nini? Ndo' unataka kusema kwamba unajali sana... utaumia mno nikitupwa, au?" nikamuuliza hivyo.
Chalii akasimama na kuja karibu nami huku akisema, "Acha kujifanya mjuaji dogo. Hivi unaelewa ni namna gani nimetamani sana kukushika na kukutufua-tufua, nikukatekate kila kiungo cha mwili wako kwa kufanya uhawala na mke wangu mimi... tena mpaka unanionyesha kabisa hilo waziwazi? Unataka kujifanya unajua sana dharau, kamwonyeshe mtu mwingine asiyejua nini maana ya kudharauliwa, na siyo mimi. Naijua dharau vizuri sana. Na una... una bahati tu JC. Una bahati tu kwamba ninakuona kama mimi, la sivyo usingekuwa unaivuta hiyo pumzi hata sasa hivi..."
Maneno yake yalieleweka katika kuyasikia, na domo lake likinuka pombe kiasi, lakini sikuelewa alikuwa anamaanisha nini kiujumla. Nikabaki nimemtazama usoni kwa umakini tu.
"Uko sehemu mbaya sana, hujui tu. Nilipokujuaga kipindi kile, nilikukubali sana, lakini ukaamua kuonyesha we' ni mbwa zaidi ya mbwa. Hapa... chukulia yaani ni kama vile tunataka kukusaidia, kwa sababu we' ni mbwa kipofu mwenye faida, na Bertha kakushika mkono akikudanganya kwamba anakuongoza, lakini ni yeye ndiyo unamwongoza pamoja na kwamba huoni. Advantage aliyonayo ni wewe, na akishafika anapotaka, anakuachia uangukie shimoni..." Chalii Gonga akasema hayo.
"Unataka nini Chalii? Unataka nikuombe msamaha? Mke wako ndiye aliyenitaka, muulize ukipenda. Me nilikwenda kwake kikazi, mengine yaliyotokea yalitokea tu... sa' sijui unaongea haya yote ili iweje," nikamwambia hivyo.
"Ahah... yaani bado haelewi tu," Chalii akamwambia Sudi hivyo.
"Well, labda uache kutumia methali nyingi ndiyo nitaelewa unachotaka. Sema mnataka nini," nikawaambia hivyo.
Sudi akasimama pia na kutusogelea, naye akasema, "Tunataka kumwangusha Bertha."
Kauli yake ya moja kwa moja ikanifanya niendelee kumtazama tu utadhani sikusikia alichokuwa amesema.
"Hicho ndiyo tunachotaka," Sudi akasema hivyo.
"Na mnaniambia mimi? Kwa nini?" nikamuuliza hivyo.
"Kwa sababu wewe ndiyo kitu ambacho kinampa nguvu zaidi sasa hivi, ilianza kama masihara tu... lakini siyo wewe tunayetaka kumwangusha. Ikiwa unaelewa nachomaanisha," Sudi akasema hivyo.
Nikawaangalia wote kimaswali kiasi, Dotto akiwa amekaa kule kule tu akitutazama kwa utulivu, nami nikauliza, "Unataka ni-flip? Unataka ni... nijiunge na nyie kumwangusha Bertha?"
Sudi akatikisa kichwa kukubali.
Nikacheka kidogo nikiwa nimeshangazwa kiasi na jambo hili, huku wao wakinitazama kwa umakini tu, kisha nikasema, "Samahani... ahah... nimeshangaa tu. Okay. Kwa hiyo, mnataka kumwangusha madam, halafu mnasema mimi ndiyo nguvu yake. Kwa nini tena mnafanya ionekane kama mnaniomba nijiunge nanyi? Kama me ndo' nguvu yake, si ni mimi ndiyo napaswa kuondolewa, au?"
"Hapana. Wewe utabaki kuwa na nguvu uliyonayo, na utaitumia ukiwa pamoja na sisi," Sudi akaniambia hivyo.
"Nguvu gani unaongelea?" nikamuuliza.
"Uwezo wako wa kutengeneza cocaine hii ambayo imeanza kuagizwa zaidi, ndiyo nguvu anayoongelea," Chalii Gonga akasema hivyo.
Nikamwangalia Sudi usoni.
"Bertha ametumia akili, kukutumia wewe, na watu wake wachache, kutengeneza hiyo kitu bila kutuhusisha sisi wengine; yaani ukiondoa Festus, mimi na wenzetu hatujui mnapozitengenezea, na delivery mnazotoa ni za maana... lakini najua haupati chochote unachostahili zaidi ya kuendelea kulamba tu tako lake kama Charles alivyokuwa akifanyiwa. Tunataka kumwondoa Bertha kwenye picha, ujiunge nami, na manufaa utakayopata yatakuwa mara mia zaidi ya huyo mwanamke anayokupa. Trust me, hautajuta," Sudi akasema hivyo.
Nikatazama chini kwa ufupi, kisha nikasema, "Kumbe ni hicho? Yaani... hofu yako ipo kwenye suala kwamba Bertha ameanza kuichukua market kwa kasi sana, si ndiyo? Unaogopa vile mnavyouza nyie vitapigwa chini muda siyo mrefu maana watu wengi watakuwa wanataka hizi cooking mpya, si ndiyo?"
"Siogopi chochote mimi," Sudi akaniambia hivyo.
"Sasa shida ni nini? Bertha si ni mwenzako? Mpo kundi moja, kwa muda mrefu, hata me sijui mmeanza lini hizi mambo mpaka nilipozikuta, kwa nini sa...."
"Acha kujitoa akili JC! Nisikilize. Mimi nimeshaona mengi nikiwa na yule mwanamke, najua jinsi anavyoweza kubadilika haraka, sasa hivi anakuchekeaa unajiona umefika, ila utakuja kujuta. Nakwambia utakuja kujuta usipoamua kusimama nasi mdogo wangu," Chalii Gonga akasema hayo.
"Huo muda wote ulikuwa wapi Chalii? Kwa nini sasa hivi ndiyo unaonyesha... ujasiri, wa kusimama dhidi ya Bertha?" nikamuuliza.
Sudi akasema, "Unajua kwamba Bertha ana nguvu..."
"Exactly! Ana nguvu, ndiyo maana nyie wote hapa mnamwogopa. Wewe Sudi unaonekana kuwa rebel, sijapinga, lakini hata zile stunt... kuninyooshea bastola ili nikuogope, ulikuwa tu unataka kujitutumua mbele ya wengine lakini unajua huwezi kumgusa. Halafu mnanifata eti mnataka ni-flip? We' Chalii umeshindwa huo muda wote, mimi ndiyo niweze? Na wewe Dotto unakubaliana na haya yote?" nikawaambia wote hivyo.
Wakaangaliana na kucheka kidogo, naye Sudi akasema, "Tumia akili dogo. Sisi, hatumwogopi Bertha... ila, ni aliyesimama mbele zaidi kumpa hiyo nguvu."
Nikatulia kidogo, kisha nikasema, "Festo."
"Mm-hmm. Na, uko sahihi, nina... me ni mjeuri. Sana. Festus ana control kubwa over what we do na tumeheshimu chain yake ya command kwa muda mrefu sana, ila inatakiwa ufike muda mwanaume ujue kwamba huwezi sikuzote kusimama nyuma ya mgongo wa mtu. Bertha... ni kikwazo. Ni... ni kunguni, anayehitaji kutumbuliwa haraka sana. Angekuwa anajali maslahi ya group zima, ange-share mipango yake kwa sisi wote, lakini anaifanya kwa siri zaidi, anaiba mpaka na wateja waliokuwa loyal kwetu, faida zetu sisi zinaporomoka kwa sababu ya ubinafsi wake. Nimeangalia hilo kwa wiki mbili zilizopita, na hasara aliyotupatia mimi, Tito na Farao ni kubwa; anaiba wateja wetu, tena hadi nilisikia wakati anafanya tangazo la biashara yake mpya na we' mbwa wake ulikuwa naye... lakini wengine hawana kifua cha kukoroma kwa madam kwa sababu tu anamfurahisha Festus. Well not me. Sitaruhusu ushindi wake umaanishe me nianguke, that's why inatakiwa yeye ndiyo aanguke haraka sana," Sudi akasema hayo yote kwa mkazo.
Nikawa nimeelewa vizuri shida yake, na sikupenda walivyokuwa wananiita mbwa, ila nikamuuliza, "Kwa hiyo... unataka nitoke upande wa madam Bertha, nije kwako, si ndiyo? Ili nikuongezee faida kama navyofanya kwake, ili tena na wewe iwe vile vile kama yeye, halafu Farao... au nani, aje kwangu tena baadaye kunishawishi nikusaliti na wewe?"
Sudi akacheka kidogo.
Chalii Gonga akasema, "Haitakuwa hivyo. Tukishamwondoa Bertha, kila kazi utakayofanya na sisi itakuwa kwa malipo unayostahili. No monkey business."
"Na kwa kusema 'kumwondoa,' unamaanisha?" nikamuuliza hivyo.
"Tutamuua," Dotto akaongea hivyo.
Nikamtazama kwa umakini sana, kisha nikasema, "Ni Dotto kabisa ndiyo amesema hivyo? Ahah... I can't believe this. Hii... coup imeanza lini kaka?"
"Dotto ni mdogo wangu. Usifikiri amefurahia sana kufanya kazi ndani ya kiganja cha yule mwanamke, na mambo mengi mabaya ambayo Bertha amenifanyia, Dotto ameona. Imetosha sasa," Chalii Gonga akasema hivyo.
"Mabaya? Chalii kaka, si umepewa na hoteli mbili kabisa?" nikamwambia hivyo.
"Acha usenge, malaya wewe! Ulikuwepo? Unajua ni kwa nini alinipa? Muda wote niliokaa nalipia makosa yake lakini kwa wengine inaonekana kama nafurahia maisha... unafikiri ninafurahia kweli? Kama alikwambia alinipa hizo hoteli na bar, alikwambia pia ni kwa nini? Alikwambia kwamba alisababisha mtoto wetu afe? Halafu mimi ndiyo nikalipia makosa yake mwenyewe kwa kulishwa nyama mbichi ya mtu? Eh?" Chalii akaongea kwa hisia.
Nikakaza uso kimaswali kiasi. Hadithi aliyoitoa ilikuwa tofauti kidogo na jinsi nilivyosimuliwa na Bertha, nami nikamuuliza, "Bertha alimuua mtoto wenu?"
"Alikuwa anataka kumnywesha juice yenye sumu mwanamke aliyefikiri ninatoka naye kimapenzi, lakini mtoto wetu akainywa kimakosa na kufariki. Huyo mwanamke nilikuwa hata sitoki naye! Halafu bado akanilaumu mimi kwa kifo cha mtoto wetu, ikawa ni masimango, vitisho, ujeuri... unafikiri ni mwanaume gani anaweza kukaa kuvumilia hayo yote kutoka kwa mwanamke, eh? Kisa tu amepewa kanguvu fulani na Festus na watu wao? Ndiyo nitetemeke forever?" Chalii akasema hivyo.
Mh?
Nikatazama tu chini huku nikitafakari mambo kwa kina.
"Bertha ana mpango mwingine, JC nakwambia. Huo mpango ukikamilika wewe ukiwa umeshamaliza kumsaidia kuutimiza, anakuua. Tena vibaya zaidi ya alivyomuua Joy, bila hata sababu. Hujaujua ulimwengu wake vizuri mdogo wangu, usijione umefika. Utakufa vibaya sana," Chalii akasema hivyo.
Nikatulia kidogo na kushusha pumzi taratibu, kisha nikawauliza, "Kwa hiyo mnachotaka ni nini? Nifanye nini yaani? Me ndo' nimuue Bertha, au?"
Sudi akasema, "Mbona unaenda mbali sana? Tulia. Hapa tunachotaka tu ni wewe kusema kama utajiunga nasi, au la. Mengine baadaye."
"Na kama jibu ni la?" nikamuuliza hivyo.
Wakaangaliana kwa ufupi.
"Ahah... kwamba ndiyo mtaniua? Ikiwa ni hivyo, hata msichelewe. Karibuni," nikawaambia hivyo.
"Nah, kukuua haitupi faida, zaidi ni hasara. Baada ya kukueleza hayo yote, we' ndo' unapaswa uamue. Kubali kuja upande wangu, utapata faida kubwa. Lakini ukiendelea kukaa kwa Bertha kisa anakupa titi unyonye, utaumia sana mwanangu. Hauko peke yako anayenyonyesha," Sudi akasema hivyo.
"Kwamba nini, unanijali sana?" nikamuuliza hivyo.
"Hapana. Najali biashara zangu tu, na nimeona wewe unaweza kuwa asset nzuri. Huko uliko, wanakufichia kile unachostahili, na we' unaendekeza ujinga kufikiri utakuwa mfalme wa malikia anayetaka kukaa kwenye kiti cha ufalme peke yake. Hiyo haipo. Ni muda wa kuamka. Na ni sasa," Sudi akaniambia hivyo.
"Ahah... hivi kweli! Dah, kwa hiyo... tuseme natoka hapa, naenda kumwambia Bertha kila kitu ambacho mmesema. Hapo itakuwaje?" nikawauliza.
"Bertha atakuua vibaya mno ukienda kumwambia haya!" Chalii Gonga akasema hivyo.
Nikamtazama kwa umakini.
"Anamwamini Dotto mara mia zaidi yako, wewe amekujua kwa miezi miwili tu. Ukisema ninajaribu kukufanya umgeuke nikiwa pamoja na Sudi, labda atakuamini. Lakini hatua yoyote atakayotaka kuchukua lazima itapita kwa Dotto, na anafikri Dotto hawezi kumsaliti hata kwa ajili ya kaka yake. Imagine ni namna gani hiyo itakuwa ni rollercoaster juu yako mwenyewe," Chalii akaniambia hivyo kwa uhakika.
Nikamwangalia Dotto kwa umakini, ambaye alikuwa akila tu nyama za kitimoto huku pia akinitazama kama vile siyo yeye aliyekuwa akiongelewa. Nikatabasamu kiasi na kutikisa kichwa kwa kutoamini haya yote.
"Every man's gotta think for himself. Utakaa nyuma ya mgongo wa Bertha mpaka lini wakati wewe ndiyo mwenye nguvu? Oh, usijali kuhusu yale tunayopanga kumfanya. Wewe jali zaidi juu ya ni wapi utasimama. Tumekuita ili uione picha kwa ukamili; we' ni mwanaume, tumia akili, utakachoamua baada ya hapo ni juu yako... na uamue kwa busara," Sudi akaniambia hivyo.
Nikaendelea kumtazama tu kwa utulivu.
Sudi akarudi pale alipokuwa ameketi, huku Chalii Gonga akiendelea kusimama karibu yangu na kuniangalia kwa umakini, na jamaa akachukua simu yake pamoja na kitu kama mkanda wa kuvaa kiunoni sijui, kisha akaja tena upande wangu na kusimama.
Akasema, "Usichukue muda mrefu kunipa jibu. Mambo yatabadilika kwa kasi. Umenielewa?"
Nikabaki tu kumtazama usoni, naye akanipita na kuelekea nje. Chalii Gonga naye akachukua chupa zake za bia pale mezani na kunipita pia, na hapo ndani nikawa nimebaki mimi na Dotto.
Nilimwangalia mwanaume huyo kwa utathmini wa hali ya juu sana, na kwa kweli hakuonekana kuwa na tatizo lolote na yale yote yaliyokuwa yamesemwa humo muda mfupi nyuma. Akatafuna kipande kimoja cha nyama, na kunionyeshea sahani eti na mimi nichukue, lakini nikaendelea tu kumwangalia usoni kwa umakini.
Akanyanyuka pamoja na hiyo sahani yenye kitimoto na kuja mpaka niliposimama, naye akasema, "Game on."
Kisha akanipita na kuelekea nje pia.
Kwa sekunde chache nikabaki nikiwa nawaza huu mchezo ungeelekea wapi zaidi baada ya haya yote, maana ni mengi sana yalikuwa yakiongezeka, na kwa kasi. Yaani kama ni kuwa snitch, basi ningetakiwa kuwa snitch kwa kila upande, mpaka nikaanza kuchanganyikiwa juu ya ni upande upi ambao nilistahili kusimama nao zaidi.
Watu wake Bertha mwenyewe walikuwa wameanza kuunda njama za kutaka kumuua, halafu wanichukue mimi kwa ajili ya mipango yao. Maelezo yote waliyotoa kuhusu kwa nini nisingeweza kumwambia madam kuhusiana na hili yalionekana kuwa utumbo tu kwangu, lakini najua nisingeweza kumwambia yule mwanamke kwa sababu nilielewa kuwa maaskari walikuwa kwenye nyendo za karibu mno kufanikisha zoezi la kuwakamata watu hawa WOTE; haijalishi ikiwa na wao walianza kutangaziana vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hivyo uamuzi sahihi kwa wakati huu ungetakiwa kuwa kuendelea kutulia tu na kuona ni mkondo gani ambao mambo haya yangeelekea mpaka kufikia siku ambayo yote yangekomeshwa, na ningepaswa kujitahidi kuwa mwangalifu kutojikuta naumizwa vibaya mno na matokeo ambayo yangekuja.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments