Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA TATU

★★★★★★★★★★★★★★


Nikatoka hapo walipopaita Facebook nikiwa nimeanza kuwaza mambo mengi, na baada ya kufika nje sikuyakuta yale magari mawili pale ambapo yalikuwa yameegeshwa, kuonyesha kwamba wale jamaa walikuwa wameshaondoka. Ingenibidi kurudi makwetu kwa kutembea, na haikuwa na tatizo. Kutembea mdogo mdogo mpaka huko kungenipa dakika chache za kutafakari vizuri yale ambayo hasa Chalii alikuwa ameyasema.

Kwenye hiki kisa haikujalisha nani alikuwa anasema ukweli na nani alikuwa anadanganya, lakini jamaa aliponiambia upande wake wa story kuhusu jinsi mtoto wake na Bertha alivyopoteza maisha, nilihisi kama hakuwa akidanganya. Wakati ule Bertha aliponisimulia kwa upande wake nilimwamini kabisa maana si unajua uchungu wa mama na nini, lakini inawezekana alikuwa ananidanganya., 

Hivyo nikaanza kutilia mashaka mambo yote aliyokuwa amesema kuhusu yeye kwenda jela, sijui akatoka, sijui akamuua nani, kwa sababu ndiyo vitu ambavyo vilikuwa hata vimenipa hali ya kumwona kuwa mtu aliyepitia mambo magumu mpaka kusababisha awe jinsi alivyo. Ikiwa alikuwa amedanganya tu kuhusu kifo cha mwanaye na kumtesa Chalii kwa makosa yake yeye mwenyewe, basi alikuwa wa daraja lingine la ubaya huyo mwanamke. Baya sana.

Na siyo kwamba nilikuwa nimepuuzia kila kitu ambacho Sudi na Chalii waliniambia kuhusiana na mwanamke yule kuniua akishafika pale anapotaka afike baada ya kunitumia, hicho kilikuwa ni kitu ambacho nilitakiwa kuchukua kwa tahadhari. Ningetulia kuona jinsi ambavyo mambo yangeenda, lakini mpaka kufikia siku ambayo askari Ramadhan na wenzake wangepiga hatua kuwakamata watu hawa, ningepaswa niwe chonjo sana. Yaani LOLOTE lingeweza kutokea, huenda hata ningeuliwa lakini bado nikawa hai kiroho kuendelea kusimulia hiki kisa!

Kesho ingekuwa Ijumaa, kwa hiyo najua ningeonana na Bertha tu. Hatukuwa tumeonana tokea Jumatano, zaidi tuliwasiliana tu kwa sms fupi na yeye kuonekana ana mambo mengi aliyokuwa anapika, kwa hiyo sikujifanya mbwa sana wa kunusanusa aliyofanya kila muda. Tulikuwa tunashiriki mapenzi, lakini hatukuwa wapenzi kabisa. 

Mimi kuendelea kuigiza kwamba nampenda sana Bertha ilikuwa muhimu kwa faida yangu, na nilifurahi tu kwamba hakutaka ipitilize maana hata na mimi kiukweli sikutaka ipitilize. Ah, yaani nilikuwa naombea siku ya askari Ramadhan iwahi kufika! Na tena na hapo bado hata sikujua ingekuwa vipi kuhusu kiongozi Festo, jamaa mtata aliyekuwa akiogopwa na akina Sudi, sijui ikiwa na yeye angeshikwa? Ingebidi kuendelea kungoja tu.

Dakika kadhaa kupita na saa tano ikawa imeingia baada ya kuwa nimefika hapo kwa Ankia. Wakati nikija nilikutana na Bobo nje ya Masai Bar, tukaongea kidogo na akanitambulisha kwa mpenziwe hatimaye kwa mara ya kwanza kabisa. Alikuwa mdada mdogo tu tena kukaribiana rika na Mariam kabisa, lakini alionekana kuwa mjanja mno, na Bobo alipendelea wenye umri kama wa huyo demu wake. 

Kwa hiyo ndiyo nikafika na kuingia hapo getini, na yule Fatuma wa dukani alikuwa ameshafunga. Wakati nilipotazama upande wa jirani zetu nikaliona gari la Miryam hapo nje, lakini ni uwepo wa mwanamke huyo nje hapo ndiyo ukafanya nisitishe hatua zangu na kuendelea kumwangalia kupitia vitundu vya ukuta wa uzio. Alikuwa ameketi kitini sehemu ya varanda lao pale, akiwa ametazama tu simu yake akionekana kusoma ama kuchat.

Nikasogea kwenye tundu la ukutani na kumchungulia vizuri, na kama kuotea tu, akanyanyua uso wake na kutazama sehemu hiyo hiyo, hivyo akawa ameniona. Nikatabasamu kiasi na kumpungia mkono, naye akatabasamu pia na kunipungia mkono pia. Nikatoa ishara kwa kiganja kumuuliza jambo fulani, lakini nafikiri kwa kutoelewa vizuri, akaamua kunionyesha ishara kuwa nimfate hapo ili tuweze kupeana salamu vyema zaidi.

Ikabidi nizunguke, moja kwa moja mpaka getini kwao na kuingia, nami nikaanza kukielekea kibaraza hapo alipokuwa. Alikuwa ndani ya kiblauzi chepesi cheupe, ambacho kilifunika kifua chake vizuri kabisa, na kinguo laini na kirefu kwa juu kilimsitiri vyema mikononi mpaka chini kama vile koti la kike, ila jepesi. Alikuwa amevalia na suruali pana ya kulalia pia, akiketi kwa kukunja nne, na nywele zake laini alikuwa ameziachia zimwagikie mgongoni kwake. 

Nikafika karibu zaidi na hapo huku nikitabasamu kirafiki, naye akawa ananiangalia machoni kwa utulivu tu. 

"Vipi?" nikamuuliza hivyo.

"Safi. Ndiyo umetoka mizunguko?" akaniuliza hivyo na kasauti kake katamu ambako walahi nisingewahi kuja kukakinai.

Nikamwambia, "Yeah, ila sikuwa mbali sana. Hapo tu Mzinga. Nilikuwepo hapa mpaka mida saa mbili kabla hujafika. Umeingia muda umeenda sana?"

"Saa tatu ndiyo nimefika. Sijachelewa sana," akasema hivyo.

"Wengine?"

"Wameshaingia kulala."

"Na Tesha amelala sasa hivi?"

"Hapana. Hayupo. Nimerudi sijamkuta. Ameniambia yupo njiani kutokea Tandika huko kwa rafiki yake... alikuwa amemwalika," akanijulisha.

"Ahaa... ningeshangaa," nikasema hivyo.

Akatabasamu kiasi na kusema, "Nyie wote mida hii ndiyo sahihi kwa mambo yenu kufanywa."

"Ahahah... me siyo sana..."

"Aa wapi..." akasema hivyo, nasi tukacheka kidogo kwa pamoja.

"Mbona hujaingia kulala bado? Au unakula upepo hapa shauri ya joto eh?" nikamuuliza.

"Ee joto pia. Ila huwa napenda kukaa nje mara moja moja... kufikiria vitu," akasema hivyo huku akiangalia pembeni.

Niliona kuwa kuna "vitu" ndiyo alikuwa anafikiria, nami nikataka nijue kama ningeweza kusaidia kwa njia yoyote.

"Umekula lakini?" nikamuuliza.

Akaniangalia na kutikisa kichwa kukubali, naye akasema, "Mapema tu wote tumekula, ndiyo hadi na Mamu akalala. Wewe je?"

"Mimi pia," nikasema hivyo ingawa bado sikuwa nimekula.

Akaonekana kutafakari kitu, kisha akasema, "Ngoja nikuletee kiti."

Sikuwa hata na mpango wa kutaka kukaa kabisa, na kabla hata sijasema lolote lile akawa amenyanyuka na kuelekea ndani. Baada ya sekunde chache akarejea akiwa amebeba kiti kimoja, nami nikamsaidia kukipokea na kukiweka chini, kisha sote tukakaa vitini kwa pamoja tukiwa tumeacha uwazi katikati yetu, na tukiwa tumetazama upande wa gari lake. Hali nzuri ya utulivu na kaupepo ka hapo nje vilifanya nipate hisia nzuri, nami nikamwangalia bibie.

"Ulikuwa umeenda kuzungukia wapi leo baada ya kuachana na ma' mkubwa?" akauliza hivyo.

"Kwenye ile ishu," nikamwambia hivyo.

"Mmefikia wapi sasa hivi?"

"Karibu sana. Yaani ni kesho, kesho-kutwa... hawa watu wanakamatwa," nikamwambia hivyo.

"Ni bora. Jitahidi sana kuwa mwangalifu, eti?" akaniambia hivyo.

"Ah, ondoa shaka. Kila kitu kinaenda kwa mpangilio," nikamwambia hivyo.

Akatikisa kichwa na kuangalia pembeni. 

Ni Miryam pekee ndiye aliyekuwa anajua kuhusiana na ishu ya mimi kushirikiana na maaskari kisiri ili kuwasaidia wawakamate wakina Bertha, kwa kuwa baada ya yale mambo yote kutokea ule mwezi uliopita, aliniuliza ikiwa nilimaanisha kile nilichosema kuhusu suala hilo siku ile aliponipiga kibao kwa kutoniamini, ndiyo nikakiri ukweli huo. Ila kuhusiana na Festo kuingiliana na haya mambo pia sikuwa nimemwambia, na inawezekana jamaa alikuwa bado akimfatilia huyu mwanamke lakini nilitumaini kuwa mwisho wake ungefika hivi karibuni, na Miryam angejionea mwenyewe.

Nikamtathmini kidogo baada ya yeye kuendelea kutazama pembeni tu, nami nikasema, "Vipi huko dukani? Wateja kama wote wanafurika eh?"

Akasema, "Eeh, angalau. Mungu anasaidia. Mambo yanaenda."

"Hivi... kabla haujaja huku, ulikuwa unafanya kazi wapi?" nikamuuliza hivyo.

"Dodoma. Nilikuwa mhasibu kwenye benki ya Exim kule Area D," akanifahamisha.

"Wow! Sikujua. Kumbe una expertise ya uhasibu?"

Akatabasamu na kusema, "Yeah."

"Kwa hiyo kama usingekuja huku... mpaka sasa hivi ungekuwa bado unafanya hiyo kazi ya uhasibu?" 

"Labda. Sijui kwa kweli," akaniambia hivyo.

"Haukutafuta sehemu nyingine hata ulipofika Dar?"

"Hapana. Nilitaka tu ku-focus kwenye duka aliloniachia baba," akasema hivyo.

"Okay. Haujutii kuiacha kazi yako lakini? Haujawa-miss uliokuwa umefanya nao kazi, ama eneo ulilokuwa unaishi... marafiki wa huko?"

"Ah, kama ni marafiki, tunafanya mawasiliano. Nilipokatisha mkataba wangu kuja huku, waajiri na wafanyakazi wenzangu walielewa... so hatujaachana pabaya, kuna ambao nakutana nao mitandaoni, wananijulia hali, utani kidogo, basi. Ni miaka michache imepita hata hivyo... siwezi kusema sija-miss kazi niliyokuwa nayo, lakini sijuti kuiacha. Huku niko sawa pia," akasema hivyo.

Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.

"Kwa nini umeuliza?" akaniuliza hivyo.

"Oh... yaani, huwa nafikiria tu, kwa mambo yote ambayo umepitia toka umekuja kwa familia yako, ingekuwa mwingine angekata tamaa na kurudi alikokuwa kwa sababu labda ni pazuri zaidi. Lakini wewe uko imara sana... ni jambo zuri mno," nikamwambia hivyo.

Akatabasamu kiasi na kusema, "Asante. Hata wewe pia."

Nikamwangalia usoni.

"Kuamua kujitoa ili kuwasaidia maaskari wawakamate hao watu wabaya, kuacha kwenda kufanya mambo yako ili ubaki kumsaidia mdogo wangu, tena kwa kupoteza gharama na muda wako... wewe ni imara pia," akaniambia hivyo.

"Ahah... asante. Lakini me gharama gani nimepoteza sasa? Mbona unatia chumvi?"

"Wakati wako wa mapumziko, na ujuzi wako ambao ni wa kulipwa unautumia kwa mdogo wangu bure kabisa... hiyo ni gharama. Unamsogeza Mamu sehemu nzuri sana yaani... sikufikiria kwamba ingeweza...."

"Imeshawezekana Miryam. Mdogo wako yuko imara kama wewe, kwa hiyo hata hilo atalishinda tu," nikamwambia hivyo kwa uhakikisho.

Akashusha pumzi na kuangalia pembeni.

"Kuna vitu kuhusu Mamu bado vinakuhangaisha, Miryam?" nikamuuliza kwa upole.

Bila kuniangalia, akasema, "Nawaza tu kuhusu ufahamu wake. Tunamwita mtoto, lakini Mariam ni msichana mkubwa tayari. Anaelekea kuwa mwanamke kamili. Nilikuwa nataka hali hii imwondoke mapema... arudi shule... a... asomee jambo fulani, yaani... sijui kama itawezekana..."

"Itawezekana, Miryam. Taratibu tu."

"Lakini hiyo taratibu itaisha lini? Najua nilikuomba ubaki, ila hautaendelea kuwa hapa sikuzote, na ukiondoka sijui ndiyo itakuwaje..."

"Haina shida Miryam. Hata kama nikiondoka, Mamu tayari ame-progress... kile ambacho nimefanya naye, hata kama ni Tesha anaweza kukifanya. Kikubwa tu ni kumbukumbu yake kuwa imara zaidi... basi. Hata akija kwenda shule tena, la muhimu linatakiwa kuwa tumeifanya kumbukumbu yake ikae vizuri sana. Akili anayo, na atafanikiwa," nikamtia moyo.

"Kwa hiyo kikubwa ni kuifanya kumbukumbu yake iwe imara... na ndiyo unachofanya sasa hivi?"

"Yes."

"Lakini... tutajuaje kwamba imetosha?"

"Haihitaji kutosha, ila kuanza tu kuonekana. Anatakiwa yeye mwenyewe aanze kuona kwamba kucheza rede na watoto, ni utoto. Anatakiwa aje akwambie 'dada, nataka kwenda kutembea huko Kigamboni,' yeye mwenyewe, siyo mpaka asindikizwe na mtu, kwa sababu anajua jinsi ya kujiongoza kwenda na kurudi. Zipo ishara tu zitajionyesha kwamba yuko tayari... tena... najua siku siyo nyingi zitaanza kujionyesha," nikamwambia hivyo.

"Eti eh?"

"Mmm," nikakubali.

"Sawa. Nimeelewa. Na... unaongea kama vile mwalimu wa falsafa, siyo wa biology," akatania.

Nikacheka kidogo na kusema, "Napenda kusoma vitu vingi, tia ndani falsafa pia."

"Kumbe?"

"Eeh. Unafikiri ilikuwaje sharobaro kama mimi akawa daktari?"

Akatabasamu na kusema, "Kwa kupenda kusoma sana."

"Ndiyo hivyo."

Akiwa ananiangalia kwa utulivu, akasema, "Haya nielezee jinsi unavyoiona kumbukumbu ya Mamu kwa sasa toka umeanza kumfundisha. Kifalsafa zaidi."

"Ahah... unapenda kusikiliza falsafa?" nikamuuliza.

Akatikisa nyusi kuonyesha "ndiyo" huku akitabasamu kwa mbali.

Nikasafisha koo kiasi, nami nikamwambia, " Well... naweza kusema yuko kwenye hatua nzuri, siyo kama mwanzo, ila... kifalsafa ya biology na sayansi yake zaidi, iko hivi..."

Akatabasamu zaidi huku akiniangalia kwa utulivu. 

"Niliwahi kusoma makala fulani. Inaeleza jinsi kumbukumbu ilivyo complex sana, hasa kwa kuwa ubongo ni mtata, na inapotokea mtu anakuwa amepoteza kabisa kumbukumbu, kuirudisha kunakuwa na mitihani yake. Lakini kwa case kama ya Mamu, ikiwa amepatwa tu na usahaulifu shauri ya trauma, ama nini, ndiyo unakuta tunafanya hizi harakati sasa... kumsaidia... arejeshe... ahahah..."

Nikajikuta nacheka tu kutokana na jinsi Miryam alivyokuwa akinitazama kwa njia iliyoonyesha usikivu, naye akatabasamu na kusema, "Endelea."

Nikamwambia, "Unakuta pale ubongo unapokuwa unajaribu kuvuta kumbukumbu, zile kumbukumbu imara ndiyo zinakuwa zinaimarika zaidi, halafu zile dhaifu..."

"Zinafifia zaidi," akamalizia.

"Eeeh. Maana yake sasa mtu anapojipa challenge ya kuvuta kumbukumbu ya mambo aliyojifunza, iwe ni leo, jana, juzi... ndiyo inakuwa njia nzuri ya kuuondoa ule udhaifu ili kuupa ubongo nafasi nzuri ya kuboresha kumbukumbu. Mazoezi ninayofanya na Mamu ndiyo yana lengo hilo la mwanzo. Hatakumbuka kila kitu ambacho amewahi kuona au kujifunza, kama tu wewe huwezi kukumbuka kila sura uliyoiona ulipoenda mizunguko na kurudi nyumbani. Yale mambo ambayo yanaongezeka kwenye ubongo wake; vitu anavyojifunza, anavyoona, na kuhisi, iwe vipya au vya zamani, ndiyo vinakuwa kama gharama inayofunika yale ambayo aliyajali zamani, na kumbukumbu yake inaimarika zaidi kwa haya ambayo... inayapata sasa na kuendelea. Umeelewa?"

Akatikisa kichwa taratibu kukubali huku akinitazama kwa utulivu.

"Kumbukumbu ya Mamu imekuwa ikishindana yenyewe kwa yenyewe, na kwa sababu ilimtawala kwa muda mrefu akiwa namna hiyo, haikuwa rahisi kwa ubongo wake kuzingatia... au niseme... yaani kutilia maanani yeye ni nani, ikiwa itafaa arudishwe nyuma kiufahamu ama asonge mbele... ubongo wake ukaamua ah, ngoja tumrudishe huyu nyuma, halafu abaki hivyo hivyo. Kwa hiyo ili kumtoa huko, ingehitajika kuuchezesha ubongo wake kwa kumbukumbu za vitu vinavyodumu kupitia njia za kipekee... namaanisha vitendo, sauti, na hisia. Kumshikamanisha Mamu hasa na vitu vinavyoteka hisia zake, kwa njia nzuri, ndiyo kutamfanya akumbuke mambo mengi vyema zaidi, popote pale atakapoenda. Haimhitaji JC peke yake kwa ajili ya hilo. Ni nyie wote," nikamwambia hivyo kwa sauti tulivu.

Miryam alikuwa ameganda kunitazama usoni tu na macho yake mazuri, naye akaachia tabasamu hafifu lililoonyesha upendezi. 

Nikabana midomo yangu nikitabasamu pia, hapo nikijiona kama mwambaaa, kisha nikasema, "Ndiyo falsafa ya daktari hiyo."

Akafumba macho yake taratibu na kuyafumbua tena huku akiangalia pembeni, naye akaniambia, "Una akili... na maneno mengi."

Nikiwa nimejisikia vizuri baada ya kusifiwa, nikamwambia, "Ndiyo Jayden huyo."

Akarudia kunitazama machoni huku akitabasamu kiasi, nami pia nikamwangalia usoni. 

Tulikuwa tunaangaliana kama vile tumegandishwa, na aisee hisia ya hapo niliipenda sana. Ilikuwa kama vile mwanamke alitaka niendelee kuongea, lakini mimi nikawa nimekosa cha kuendelea kumpa, hivyo ni macho yetu tu ndiyo yakabaki kuambiana kitu fulani kwa lugha ambayo sidhani kama sisi kwa pamoja tuliielewa. Ndipo akawa amekatisha utizami huo na kujiweka sawa zaidi kwa jinsi alivyokuwa ameketi, nami nikaacha kumwangalia pia.

"Sawa. Nashukuru kwa company. Falsafa imeeleweka vizuri. Asante pia," akasema hivyo huku akizilaza nywele zake kwa kiganja.

Nikasimama, naye pia akasimama, kisha nikamwambia, "Nina kausingizi kananivuta, nataka nikakawahi hahah..." nikaongea kwa kujishaua.

"Hata me nausikia. Kesho mapema kazini," akasema hivyo.

"Yeah... mimi pia. Namaanisha... nitawahi kuamka, nije kumcheki Mamu," nikamwambia hivyo.

Akatikisa kichwa kukubali hilo huku akiniangalia kwa macho yenye subira fulani hivi, sijui nini tu.

Nikamwambia, "Sawa. U-usiku mwema. Ngoja nikusaidie kupeleka kiti ndani..."

Mwanamke hakuwa na neno, naye akageuka na kukibeba kiti chake, mimi pia nikibeba nilichokuwa nimekalia, nasi tukaviingiza ndani pamoja mpaka sehemu ya dining. Nikawa nimemuaga kwa mara nyingine tena, nami huyoo nikaelekea mpaka kwa Ankia nikimwacha bibie anafunga geti la nje.

Nilimkuta Ankia akiwa sebuleni bado, anatazama tamthilia za Azam Two, na eti alikuwa amenuna shauri ya mimi kuchelewa kurudi. Nikaanza kumtekenya baada ya kukaa naye ili mood yake nzuri irudi, naye akaacha kununa na kudeka kwake nilipomwambia nimejitahidi kuwahi ili nile msosi wake mtamu. Eti hakuwa amekula bado, akinisubiri mpaka nirudi, na kwa kweli alikuwa akitaka tu tule pamoja maana aliandaa pilau na nyama vizuri sana utafikiri ilikuwa sikukuu.

Kwa hiyo mwenye nyumba wangu akapakua, nasi tukala na kushiba na kusaza. Story mbili tatu zikafata mpaka mida ya saa sita usiku, ndiyo sote tukaanza harakati za kwenda kujipumzisha vyumbani kwa amani; kuoga kidogo kwanza, kuhakikisha milango na mageti yamefungwa, kisha ndiyo tukaagana na kwenda kujitupia vitandani. 

Bado mawazo yaliyohusiana na mkutano wangu pamoja na Sudi, Chalii Gonga, na Dotto yalikuwa yakizunguka kichwani, lakini nikajitahidi kuulazimisha usingizi unibebe upesi ili mambo mengine yafuate siku ikishakucha.


★★★


Na hatimaye ikakucha. Hii ikiwa ni Ijumaa, asubuhi na mapema tu nikajiandaa vizuri kwa ajili ya kutoka, Ankia akiwa ameshaandaa chai na kuweka mambo mezani ili tukamue na kiporo cha moto cha pilau na nyama aliyotengeneza jana. Nikavaa T-shirt langu jipya la mikono mifupi lenye rangi ya maroon (napenda sana hii rangi), pamoja na suruali ya jeans nyeusi, na kiatu cheupe miguuni kikakamilisha mwonekano wangu wa daktari sharobaro. Nikanywa chai pamoja na Ankia na kuagana naye ikiwa inakaribia kufika saa nne, nami nikaelekea kwao Mariam upesi.

Nikiwa tu ndiyo nimefika getini kwao na kuingia, hapo hapo simu yangu ikaanza kuita; Bertha. Nikapokea. Mwanamke akawa anauliza nilikuwa wapi, kwa nini nilichelewa mno kufika kule Riverside Ubungo kwa ajili ya mishe yetu, nami nikamwambia ndiyo nilikuwa njiani lakini nilikuja kwa uangalifu maana nilihisi kuna watu wangekuwa wananifatilia. Kauli hiyo ikamfanya aniulize kwa nini nilidhani hivyo, ila nikamtuliza kwa kusema asiwe na wasiwasi, ilikuwa ni hisia tu na nilijitahidi kuwa makini.

Dakika hiyo hiyo, kutokea mlango wa pale ndani akawa ametoka Tesha, bila shaka akiwa amesikia geti lilipofunguliwa, naye akanitikisia kichwa kisalamu na mimi kumrudishia pia. Nikamwambia madam Bertha kwenye simu kuwa ningemtafuta baadaye nikishafika kule, lakini akanibadilishia mpango. 

Akasema niende moja kwa moja kule hotelini kwake, yaani nisiende Ubungo, na mimi kuona Tesha anaanza kuja upande wangu kukanifanya tu nimkubalie madam haraka-haraka, kisha ndiyo nikamuaga na kukata simu. Sababu za yeye kunibadilishia mkondo wa safari ningezijua huko huko.

Tesha akawa amenifikia karibu zaidi na kusema, "Demu... na najua sijakosea!"

Nikacheka kidogo na kumwambia, "Zamu hii sitakataa."

Akacheka pia na kugongesha tano pamoja nami, kisha akasema, "Umeng'aa mwanangu. Wapi hiyo?"

"Naingia Vunja Bei mara moja..."

"Unaenda kumnunulia manzi kijora, nini?"

"Aa wee... hiyo haipo. Ni business za maana naenda kufanya, nipate ya kutosha kwa ajili ya mechi Jumapili."

"Aa, hapo umeongea! Kariakoo Derby bonge moja la dude Jumapili. Katafute mwanangu tuje tunywe haswa!"

"Ahahahah... tafuta ya kwako, fala wewe! Me namtengenezea mambo Adelina," nikamwambia hivyo.

"Adelina? Yule sista'ake Joy?"

"Eeh, atakuja huku kuangalia Derby."

"Ahaa... kumbe ushaanza kutoka naye?"

"Hamna, rafiki yangu tu. Nimemwalika. Tutakaa naye Jumapili, labda tutaenda Masai, au siyo?"

"Uhakika. Na sisi kesho nanilii, Doris... anakuja hapa kututembelea," akasema hivyo.

"Ahaa, Doris anayeolewa?"

"Eeh. Halafu atakuja na Dina."

"Okay. Afu' Dina kitambo! Yuko poa?" nikamuuliza hivyo.

"Ah, kwanza we' mwana si unafanya mambo siyo fresh," akaniambia hivyo.

"Nimefanyaje tena?"

"Mpaka leo mwanangu hujaenda kumwona Dina... wakati ulimpaga promise kabisa, mwenzio akaiweka moyoni..."

"Ah, ahahahah... dah!" nikajikuta nachoka.

"Ananicheki sana kaka, kila mara lazima JC uuliziwe. Sema, huwa tu nasahau, inabidi nikupe namba yake ili ndo' upate motisha zaidi. Unamtesa mtoto wa watu," akasema hivyo.

"Ah, basi unadhani shida ni namba Tesha?"

"Ee, ni namba. Hauchukulii serious maana huna contact zake kabisa... mpaka mwezi umepita."

"Hamna bro, hiyo siyo shida. Shida ni muda. Mambo yanakuwa mengi. Hivi... unamkumbuka yule mwanamke mwislamu ambaye... tulikutana naye kwenye daladala ile siku tunaenda Kigamboni, alikuwa na kale kadem keupe ulikokuwa unataka namba yake?" nikamuuliza.

"Eeh, afu' kweli, dah! Kitambo! Ulizipata?"

"Hamna, lakini si nilizichukua za yule mama yake?"

"Ee. Mnawasiliana? Ushapiga?"

"Ndo' hicho nachotaka kukwambia. Toka hiyo siku tunawasiliana, ananielewa, anataka show... lakini mpaka sasa hivi hatujawahi kukutana tena. Kwo' ishu siyo mawasiliano, ni muda tu," nikamwambia hivyo.

"Ah, mwanangu una raha wewe! Kumbe maza mtu akakukubali?"

Nikacheka kidogo.

"Afu' dili si lilikuwa umpate kisha uniletee namba za mtoto wake yule? Ulizipata sasa?"

"Aa wapi, we' mwenyewe si ulikuwa umeshasahau? Ndo' imeisha hiyo..."

"Unazingua. Kwani shi'ngapi kukutana tena Kigamboni na huyo maza? Kwanza uliwahi kumwona uso wake kabisa?"

"Tunaongeaga video call, anavua zile mask zao."

"Anaitwa nani?"

"Ibtisam."

"Mzuri?"

"Mzuri ee. Mwarabu."

"Dah, sa' unafeli wapi?"

"Yaani wewe Tesha wewe... ahah. Wewe umetoka tu sasa hivi kuniambia simtendei Dina haki, halafu kidogo tu na Ibtisam ushaanza kumwakilisha. Kwa nini hauna msimamo?" nikamuuliza.

Akacheka na kusema, "Ndo' nilivyo. Kama raha za UKIMWI zinakutaka wewe tu, lazima nikusapoti ili ulazwe pema peponi, kamanda! Mapema..."

"Ahahahah... endelea kuota. Au ndo' kusema Dina anao sasa?"

"Hamna. Dina yuko clean kama sahani nyeupee..."

"Unajuaje?"

"Najua tu. We' ngoja nikupe namba yake, umtafute tu ajisikie vizuri... ile kwamba wewe ndiyo umemtafuta yeye. Atafurahi sana. Tena na kesho akija mkaonana, fresh zaidi," akasema hivyo.

"Haya, nipe. Sifagilii wenye umri mdogo, ila ilete," nikasema hivyo.

"We' si unapenda mashangazi tu, badala utafute viembe bado vibichii unakalia hayo madude yaliyoiva mpaka yanatepeta byeee..." akaniambia hivyo, nasi kwa pamoja tukacheka kidogo.

Akanipatia namba za huyo Dina, nami nikazitunza na kumwambia ningemtafuta baadaye.

Ikawa ni kwenda huko ndani kuwasalimu wakina Bi Jamila na Bi Zawadi baada ya kuongea hivyo kidogo na Tesha, pamoja na Mariam pia ambaye ndiyo alikuwa ametoka tu kuamka kama binti ya mfalme. Nikawaaga pia dakika chache zilipopita za maongezi mafupi kuhusiana na sherehe ya bibi harusi mtarajiwa Doris, ambaye alikuwa ameanza kunijengea hamu ya kutaka kumwona bila hata ya mimi kuelewa sababu kihalisi, na baada ya hapo ndiyo nikaondoka kuelekea kwa madam Bertha.

★★

Safari ya kunipeleka huko ilichukua muda wa kama saa moja hivi kutokana na msongamano wa magari mara kwa mara, na hatimaye nikafika hoteli ya Royal Village. Huku nikiwa nakumbukia ishu yote ya jana usiku pamoja na yule Dotto, nikaelekea hadi chumbani kwa madam nikiwa nimehakikisha sikuwa na mkia wowote nyuma yangu, yaani sikufatiliwa. 

Hii haikuwa kama sinema ya wamarekani ambao muda wote hutembea na bastola kiunoni ili kujilinda, hapa palikuwa Bongo, kwa hiyo ni macho pekee ndiyo yaliyotumika kuangaza huku na kule kujihakikishia usalama maana kwa sasa sikujua nani angekuwa akiniangalia zaidi. Hata ulinzi ambao ningeahidiwa na maaskari najua haukutosha kwa asilimia zote, nilipaswa kuwa na macho makali ya utambuzi wa kilichonizunguka na kujua hatua za kuchukua kuepuka mabalaa mapema.

Baada ya kufika kwenye chumba hicho, madam Bertha akawa anenifungulia mlango. Nilimwangalia  kwa njia ya kawaida tu usoni, lakini yeye alikuwa akinitazama kwa upendezi na tabasamu hafifu midomoni mwake. Wakati huu alikuwa amebadilisha mwonekano wake kichwani kwa kusukia nywele za rasta nene na nyekundu, ambazo zilitengenezwa kwa njia fulani kama minyororo mirefu iliyofikia mpaka usawa wa hips zake. Na hapa alikuwa amevaa T-shirt la mikono mirefu kama sweta, lenye rangi ya kijivu, refu mno mpaka kufikia magotini, na zaidi ya hilo hakuwa amevaa kingine.

Nikamtikisia nyusi moja kiuchokozi kiasi, naye akanyoosha mikono yake yote kunielekea kama kuniita niende kumkumbatia. Nikaingia na kumkumbatia kweli, nikiwa makini kutokana na mawazo yaliyokuwa yakizunguka akilini, naye akaniachia mgongoni na kuendelea kuyashika mabega yangu huku akiniangalia usoni kwa macho yenye raha, na mie nikiendelea kukishika kiuno chake.

"Nimekumiss," akaniambia hivyo.

"Mimi, wewe?" nikamuuliza hivyo kiutani.

"Mhm... mdogo wako anaendelea vizuri?"

"Ee, anasukuma-sukuma angalau."

Bertha akanisogelea karibu zaidi usoni na kunibusu mdomoni mara mbili, kisha akaniangalia na kusema, "Mbona uko serious hivyo?"

"Hamna, kawaida tu," nikamwambia hivyo.

Akiwa anasugua-sugua mabega yangu kwa viganja vyake vyenye makucha marefu, akasema, "Hujapenda nilipokubadilishia safari ghafla eh?"

"Hapana, nimefurahi. Nilifikiri ningekuja kukuona jioni... ila now ndo' ntakuwa nawe mpaka jioni," nikamwambia hivyo.

Akatabasamu kidogo na kunibusu mdomoni tena, kisha akaniachia na kusema, "Haya, funga mlango. Njoo tuongee."

Akaanza kulielekea sofa, nami nikaurudishia mlango na kumfata pia. Alikuwa akifanya utafiti fulani mtandaoni inaonekana kwenye laptop yake iliyokuwa kwenye meza hapo pembeni, nami nilipofika karibu naye, akakaa kwenye sofa huku akiuvuta mkono wangu ili nikae pamoja naye. Ikawa hivyo. Akawa amenitazama usoni sawia huku akiegamiza mwili wake kwenye egemeo la sofa, nami nikawa namwangalia kwa utulivu.

"Ulikuwa umefika wapi nilipokupigia?" akaniuliza hivyo.

"Nilikuwa... maeneo ya Kariakoo. Ndiyo nilikuwa nataka tu kupanda mwendokasi," nikamdanganya.

"Nini kilifanya ukafikiri kuna mtu alikuwa anakufatilia?"

"Sijasema hivyo, yaani... nilikuwa tu najitahidi kuwa mwangalifu..."

"Na ndo' ungefanyaje hivyo?"

"Nisingeenda Ubungo moja kwa moja. Ningepitiliza kabisa mpaka mbele huko, niangalie mazingira, halafu ndo' niende kwa spot yetu hata kwa boda... precaution tu," nikamwambia.

Akatikisa kichwa na kusema, "Sawa."

Nikaiangalia laptop yake na kumuuliza, "Ulikuwa unatafuta kitu fulani hapo?"

Akaitazama na kisha kuifunika huku akisema, "Yeah, nimemaliza. Achana nayo."

"Kwa hiyo supermarket leo sitaenda, eti? Au nitaenda baadaye?"

"Achana na ishu za kazi, HB. Nimekuita hapa tuongee... mimi na wewe," akasema hivyo.

Nikajiweka kiumakini zaidi na kushika nywele zake, kisha nikasema, "Niambie."

"Kwa hizi wiki zilizopita... umefanya kazi nzuri sana kunionyesha kwamba kweli uko serious na mimi, na najua bado sijakupa tuzo yako unayostahili," akaniambia hivyo.

Nikamwangalia kwa njia ya ufikirio.

Akasema, "Usipandishe mzuka, simaanishi nitaanza kukupa mpalange!"

"Ahahahah... huwa unawaza vitu vya ajabu madam!" nikamwambia hivyo.

"Well, great minds think alike. Hata wewe una akili ya ajabu sana. Yaani tumeanza kuuza coke yako muda mfupi tu lakini neema kubwa imeanza kushuka mikononi mwetu..." akaniambia hivyo.

"Unajiongelea wewe na nani?"

"Sisi wote. Festus hasa. Na hivi ndiyo nilivyokuwa nataka HB wangu. Umeni-impress kweli kama ulivyoahidi," akaongea kwa njia yenye hisia sana.

Nikalazimisha tabasamu na kusema, "Usiwaze. Nilikwambia chochote kwa ajili yako."

"Kweli eh?" 

"Kabisa. Kila kitu nilichofanya... ni kwa sababu yako. Na kila kitu nitakachofanya, ni kwa sababu yako wewe tu," nikamwambia hivyo kwa njia ya fumbo.

Akatabasamu na kunishika usawa wa sikio, naye akasema, "Unataka niwe wako peke yako, ndiyo maana umefanya kila uwezacho mpaka kuwa hapa. Unataka nifungue moyo wangu kwako na kukuweka ndani zaidi, si ndiyo? Huu ndiyo wakati wako sasa."

Maneno hayo yalisemwa kwa njia ya hisia za kweli kabisa, yaani Bertha hakuwa akijaribu kunitania wala nini, niliona wazi kwamba alimaanisha kile ambacho alikisema. Nikaendelea kumwangalia usoni kwa umakini, huku fikira zangu zikiendelea kupingana kwelikweli na hisia zangu.

"Sidanganyi kwamba tayari nilikuwa nimeshakuelewa pia, ila ndo' sitaki tu yale yale ya Chaz yanipate tena maana nawaelewa nyinyi vizuri mno..." akasema hivyo.

"Mimi siyo..."

"Wewe siyo Charles, najua. Ndiyo maana nimeweza kufungua tena milango ya moyo wangu kwa ajili yako. Nimekukubali kwa asilimia zote JC," akasema hivyo.

Dah! Alikuwa akiongea kwa hisia yaani, sikutegemea. Haya yote yalikuwa yanatokea wapi?

"Nataka tu nikuombe... msamaha. Nisamehe kwa jinsi nilivyokuwa nakutendea mwanzoni mpaka sasa, nilikuwa sijagundua tu thamani yako. Ila sasa hivi nimeijua, sitaki inipotee kabisa. Nakuhitaji sana... uendelee kuwa upande wangu... siyo kwa sababu ya kazi tu, yaani... kama hivi... ni... najua unaelewa..."

Aliongea kwa kubabaika kiasi, akionyesha kuwa na udhaifu wa wazi mbele yangu, na tayari nilikuwa nimeshaelewa alichokuwa anajaribu kuniambia.

Nikaangalia pembeni kwanza na kusema, "Ndiyo... nimekuelewa."

"Umeelewa nini?" akauliza.

Nikamwangalia na kusema, "Kuna neno unataka kusema, lakini unashindwa kulisema."

"Ahahah... haujakosea," akaniambia hivyo.

Nikiwa makini, nikamuuliza, "Kinachokufanya ushindwe ni nini?"

"I guess... siyo mtu wa tamthilia-tamthilia mimi, hayo maneno nayaona kuwa ya kipuuzi..."

"Lakini si ndiyo ukweli wa kile unachohisi?"

"La muhimu ni kwamba umenielewa, kwa hiyo siyo lazima niyaseme."

"Sawa. Haina shida," nikamwambia hivyo.

"Haina shida? Yaani nimeongea hayo yote halafu unasema haina shida?" akauliza.

"Ee, si nimekwambia nimeelewa? Kwa hiyo poa. Haina shida. Nimekuelewa," nikamwambia hivyo.

Akanikazia macho yake.

"Ahah... mbona unaniangalia hivyo sa'?" nikamuuliza.

"Hata dakika mbili hazijaisha tayari umeshaanza kunionyesha dharau kisa tu nimekwambia...."

"Umeniambia nini?" nikamkatisha.

Akanikazia macho yake tena, naye akasema, "Kwa hiyo kumbe ni mpaka niseme?"

Nikatabasamu na kusema, "Haujasema. Mpaka useme."

Akashindwa kujizuia kutabasamu kwa hisia, naye akaniangalia kwa macho yaliyojaa upendezi na kusema, "Nakupenda."

Mh? 

Nikabaki nikimwangalia kwa njia ya kawaida, kwa sababu kihalisi mwenzake hapa nilikuwa naigiza, lakini yeye alionekana kuwa mahali palipompoteza kabisa kihisia. Yaani alionyesha ile ya kufa na kuoza kabisa, na mimi hapo nikawa natafakari mambo mengi kinoma.

Kila kitu ambacho niliambiwa jana na wale wanaume kilikuwa kikizunguka kichwani, hasa vitu alivyosema Chalii. Kwa hiyo hapa asilimia kubwa ya kile ambacho akili yangu iliniambia ilikuwa kwamba mwanamke huyu alikuwa akinidanganya tu ili niendelee kulainika zaidi kwake, nimpe mafanikio zaidi, halafu mwisho wa siku ndiyo aje kuniangamiza. Tena bila sababu. 

Nikashindwa hata kutoa itikio lolote la maigizo na kuendelea kumwangalia usoni kwa umakini sana, kwa sababu akili yangu ilikuwa ikinishawishi kuweka kigingi cha kutoamini kabisa maneno hayo, lakini tena ikawa kama hisia zangu zinaniambia aliyamaanisha. Na yaani ilikuwa ni kwa nini wakati huu huu tu ambao mambo yangeenda kumharibikia eti ndiyo akaanza kuleta swaga za 'nakupenda sana?'

Alipoona nimeishia kumtazama tu, akasema, "Nini wewe? Si ndiyo ulichotaka nikiseme, au? Out loud. Nimekisema."

Nikatazama pembeni tu na kushusha pumzi kama mtu aliyeishiwa raha.

"HB... vipi? Haujafurahi?" akaniuliza hivyo.

Nikamwangalia na kusema, "No, siyo hivyo. Sikutegemea tu..."

"Kwa nini? Kutokana na jinsi ulivyonizoea, yaani hauwezi kuamini kabisa eti?"

"Siyo... ahah... siyo kabisa, yaani... ni ngumu tu kidogo. Nilikuwa hadi nimeshaanza kuzoea kuwa toy wako tu," nikamwambia hivyo.

Akanishika shingoni na kuniambia, "Usiseme hivyo bwana, namaanisha nayokwambia. Umeshaniteka kihisia, mbali tu na kuwa mzuri kitandani..."

Nikatabasamu na kutikisa kichwa kiasi.

"Ona, kuanzia sasa hivi... nataka tuwe serious. Umenipigania kwa vingi, na umeshinda. Nataka nikupe unachostahili sasa. Labda ndiyo itakuwa njia nzuri ya kukuthibitishia kwamba nimekupenda pia..." akasema hivyo.

"Na ni nini hicho kitakachonithibitishia?" nikamuuliza.

Akatabasamu na kusema, "Nataka kuzaa na wewe."

Nikamtazama kimaswali kiasi, na kwa sauti ya chini nikasema, "Nini?"

"Yes. Nataka kukuzalia JC. Niko tayari kuwa mama wa mtoto wako," akaniambia hivyo.

Raa!

Nikabaki nikimtazama machoni kwa umakini sana utadhani alikuwa amenipiga kwa kitu kizito kupita uzito wenyewe. Nilishindwa kuelewa ikiwa mpaka kufikia hapa mwanamke huyu bado alikuwa akicheza na mimi, ama ilikuwa vipi. Huyu alikuwa Bertha, ama nilikuwa naota?

 


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next