MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA NNE
★★★★★★★★★★★★★★
Bertha akaona kwamba jambo hilo lilikuwa limenichanganya kiasi, naye akasema, "Unawaza challenge za kuwa baba zitakuwaje eh?"
Nikaangalia pembeni kwanza.
"Ahah... me mwenyewe ninawaza sana. Ni muda umepita toka Giselle alipofariki... sikuwaza kuwa mama tena, yaani... mambo yalikuwa mengi. Nataka kuipata hiyo furaha ya kuwa mzazi tena... na ninataka nikuzalie wewe," akaniambia hivyo.
Nikamwangalia usoni kwa umakini.
"Vipi? Ungependa tulete ka kike au ka kiume?" akauliza.
Nikaangalia chini tu.
"Au hutaki mtoto?" akaniuliza hivyo hatimaye.
Nikamwangalia na kusema, "Nafikiria hali zilizopo, Bertha. Mambo yanayotuzunguka. Kweli litakuwa wazo zuri kupata mtoto sasa hivi?"
"Unataka iwe lini?" akauliza.
Nikashindwa hata kutoa jibu.
"Unajua nina miaka mingapi?" akaniuliza.
"Thelathini na saba," nikamwambia.
"Right. Chumvi imeenda sana. Unataka nizae nikiwa na miaka mingapi sasa? Arobaini? Ili mwanangu akifikisha miaka 20 aanze kuniita bibi?"
"Sijamaanisha hivyo Bertha, najua unanielewa..."
"Sikuelewi. Niambie kama hutaki nikuzalie," akasema hivyo.
Nikashusha pumzi kiasi na kumuuliza, "Uko serious kabisa?"
"Kuhusu?"
"Kuzaa na mimi?"
"Ni kipi kinachofanya ufikiri kwamba natania?"
Nikatulia tu na kuendelea kumwangalia kwa umakini.
"Hivi unanipenda kweli?" akauliza.
"Ah, hilo swali likianzaga kutumiwa kama silaha huwa inaboa..."
"Kwa hiyo kumbe nakuboa?"
"Unataka niseme nini Bertha?"
"Nataka uniambie, utazaa na mimi, au hautazaa na mimi?" akauliza hivyo kwa mkazo.
"Me... muda bado Bertha..." nikamwambia hivyo.
Akaniachia na kutazama pembeni huku akisema, "Ah, fuckit..."
"Nisikilize. Bertha... sawa najua ume-miss kuwa mama, lakini... unaonaje ukifikiria kuzaa wakati ambao mazingira yote kwa ujumla yatakuwa salama kwa ajili ya mtoto?" nikamwambia hivyo.
"Usalama upi? Pesa si ipo?"
"Namaanisha... kila kitu kwa ujumla Bertha. Maisha uliyonayo sasa hivi, unayapata kupitia njia... harmful. Hiyo inaweza ikamwathiri na mtoto pia ikiwa bado utakuwa ndani ya hayo maisha...." nikajikuta nimeenda mbali kiasi katika kuongea.
Akaniangalia usoni kwa umakini sana, naye akauliza, "Unataka kusema nini?"
Nikafumba macho kwa ufupi, kisha nikamwambia, "Najua na wewe unatafuta nafasi ya kupata furaha, kama wanawake wote. Ila kama ni mtoto... labda ufikirie njia nyingine... salama... ya maisha, baada ya kumalizana na haya tuliyonayo sasa hivi..."
Akaendelea tu kuniangalia kwa umakini.
"Kama tu nilivyokwambia siku ile... labda kwa jambo hilo, vipi ukiamua tu kuachana na madawa halafu ukajenga kitu kingine clean kabisa, ujitoe yaani... uchukue mkondo mwingine ambao... a-ambao utakuwa salama kwa ajili yako wewe na mtoto utakayezaa? Eh?" nikamwambia hivyo.
Akaangalia tu pembeni na kucheka kidogo kwa pumzi, na kiukweli najua alikuwa akiniona kama mpuuzi fulani hivi, ila na mimi mwenyewe sijui tu ni kwa nini nilikuwa kama vile najitahidi sana kumfanya ageukie mbali kutoka kwenye biashara zake haramu na kumpa kama ukombozi. Yaani... ilikuwa ni kama vile namwonea huruma eti kwa sababu ya kutambua mambo yaliyokuwa yakija. Sijui nilikuwaje tu!
Akasimama ghafla na kisha kusema, "Unaweza kwenda sasa."
Nikasimama pia na kumwambia, "Bertha, ona... sina maana mbaya, ila ukikaa ukafikiria...."
"Sihitaji kufikiria chochote. Nimekwambia nenda. Jibu langu nimeshalipata," akanikatisha kwa kusema hivyo.
"Bertha, come on..." nikamsemesha kwa upole.
"Nenda Ubungo, sasa hivi. That's an order," akaniambia hivyo kwa uthabiti.
Nikatulia kidogo nikimtazama usoni kwa utulivu, kisha nikageuka na kwenda nje ya chumba chake. Nikajikuta nasimama tu pembezoni mwa mlango wa chumba hicho, nikiwa nafikiria lipi ni hasi na lipi ni chanya. Aloo! Hapo ndiyo nilikuwa nimejikoroga bila kujitambua.
Kweli kuchanganya mafuta na maji halafu ukategemea yaunganikane ni kitu ambacho kingefanya yeyote akuone kuwa mpuuzi, na mimi kusema kweli nilikuwa nimeanza kuonyesha huo upuuzi kwa kujikuta nachanganya vitu vilivyohusisha hisia tofauti na uhalisia tofauti sehemu moja, na kwa matokeo yenye kuvunja moyo havikuunganikana.
Hakukutakiwa kuwa na hisia yoyote ile ndani yangu ambayo ingenilazimu nimwonee mwanamke huyo huruma mpaka kujaribu kumshawishi afanye mambo mengine tofauti na uhalisia wa maisha aliyokuwa ameamua kuwa nayo, lakini hisia hiyo ilikuwepo. Ni kwamba tu labda kukaa naye huo muda wote kulikuwa kumenifanya nione uwezekano wa yeye kuacha matendo yake na kuishi maisha mengine, ila ni wazi kuwa hakutaka hilo.
Ni wazi pia kwamba hata kama kweli alikuwa akitaka kuzaa na mimi, ilikuwa ni kwa sababu za kibinafsi, si kwamba alitaka kuunda familia salama na kijana mdogo kama mimi. Lakini bado tu nilikuwa navutwa na kitu fulani kutaka kumkingia kifua, yaani... sijui tu kwa nini. Siyo kwamba nilimpenda, hapana. Labda tu ilikuwa ni suala la kumzoea, kiasi kwamba mpaka ningeweza kumsamehe kwa vitendo vyake vingi vya dharau alivyonionyesha wakati wa nyuma, lakini bado akilini nilielewa ni lazima angetakiwa kwenda chini.
Ila kwa kufikiria hasa ni namna gani watu kama wakina Sudi walitaka mwanamke huyu aende chini ndilo suala lililoupa ubongo wangu kizungumkuti ukuti kuhusu uamuzi wa mimi kuchukua. Aisee, mawazo yalikuwa mengi mno kichwani mpaka nikashindwa kuelewa niyapange vipi, hivyo nikaamua tu kuondoka hotelini hapo upesi kabla kichwa hakijapasuka.
★★
Basi, nikaondoka hayo maeneo ya Vunja Bei na kufanikiwa kupata mwendokasi ambayo ilinipeleka mpaka Ubungo, nami nikashukia huko Riverside na kupanda bajaji iliyonipeleka hadi kwenye supermarket fulani kubwa eneo hilo. Hii ndiyo ilikuwa sehemu kuu ya kazi yetu bwana, kazi ya kupikia madawa ya kulevya ya cocaine kwa njia ya kificho. Palikuwa hivi.
Supermarket kama supermarket yoyote ile, huwa zinakuwa na mpangilio wa shelfu ndefu zenye bidhaa mbalimbali, na huwekwa kwa utaratibu mzuri sana kuwafaa wateja wanaofika kujichagulia bidhaa wanazohitaji, kisha kwenda sehemu ya malipo kulipia. Kunakuwa na chumba cha ziada ndani humo ambacho kinatunza bidhaa zingine zaidi, ili baadhi zilizo kwenye manunuzi zikiisha ama kupungua kwenye shelfu, basi zinaongezwa.
Ni kwenye hicho chumba ndiyo kulipokuwa na chumba kingine kidogo, ambacho kilijengewa ndani humo humo na kufichwa mlango kwa shelfu la kutunzia maboksi ya bidhaa. Yaani kama mtu angeingia, isingekuwa rahisi kudhani kuna chumba kingine, lakini kwa sisi tuliohusika nacho, ilitupaswa tuyasogeze maboksi hayo kwa uangalifu ili kuachia njia, na kuyarudishia vile vile tena ili kuziba njia tulipoingia na kutoka. Humo ndiyo madawa yalitengenezewa sasa.
Mwenye supermarket hiyo alikuwa ameshanunuliwa na Bertha, kwa hiyo hata wauzaji na wafanyakazi wa hapo ambao hawakujihusisha na haya madawa walijulishwa kuhusu chumba hicho kuwa na biashara za watu wengine zisizowahusu, hivyo hakuna aliyetakiwa kujifanya mpekenyuzi. Oh, iliwahi kutokea mmoja wao akanusanusa yaliyokuwa yanaendelea, Bertha akamtembezea upendo wake. Ikiwa unaelewa. Kwa hiyo hata kwa wengine, ilikuwa wazi kwamba biashara hiyo ilikuwa na uhatari, na ili kutopoteza kazi na mambo mengi, walifanya iwe kama vile chumba hicho hakikuwepo kabisa.
Isipokuwa tu kwa sisi ambao tulihusika. Madam Bertha alikuwa na kawaida ya kuja hapo kila Jumatatu ya wiki, nadhani kumlipa jamaa mwenye supermarket hiyo, ambaye alikuwa mwarabu, kwa makubaliano yao waliyojua wenyewe. Zaidi yake, ni mimi tu pamoja na wanaume wengine wawili wa madam ambao ndiyo tuliruhusiwa kwenda huko nyuma, na ni sisi tu ndiyo tuliopika hayo madawa. Walikuwa wanaume wa kazi kwelikweli, hakuna mchezo yaani, ni kazi, matokeo, malipo. Na walikuwa watiifu kwa madam kwelikweli.
Kwa hiyo yalikuwa yakitengenezwa, hayo madawa, halafu yanapimwa kwa gramu ama kilo kadhaa na kutunzwa kwenye mifuko, halafu ingewekwa kwenye mapakiti makubwa ya maboksi ya vitu kama biskuti, ama sabufa, ama blenda, yaani maboksi ya vitu vilivyoonekana kuwa bidhaa safi za mauzo, kisha yangetolewa na kuanza kusambazwa kwenye kila moja ya yale majengo 21 ambayo madam alikuwa ameshasimamishia hii biashara pamoja na wenzake, ili madawa haya yaweze kurefushwa hata zaidi (yaani yaongezwe wingi), halafu baada ya hapo ndiyo usambazaji kupitia magari ya takataka ungeanza kufanywa.
Yaani lilikuwa ni shirika kubwa hili, na walienda kwa mtindo wa maana. Sudi kunifata hiyo jana usiku na kusema ishu ya madam inaharibu soko lake, ilikuwa hasa shauri ya hii supermarket. Bertha alichanganya hii ishu yake mpya na ambazo wenzake walikuwa wameshasimamisha pia kabla ya mimi kuja, na ndiyo maana haya madawa mapya yalipoanza kukolea ikabidi yaanze kurefushiwa na kwenye hayo majengo pia. Hivyo yale ambayo yalikuwa yameshazoewa yalianza kushuka kiwango cha uagizwaji, ununuzi, vyovyote vile, kwa kuwa hii mpya ndiyo iliyopendwa zaidi.
Bertha hakuwa amewaonyesha wenzake sehemu hususa ambayo madawa haya mapya yalitengenezewa, ndiyo sababu Sudi, labda na wengine pia, walikuwa wameanza kutetemeka mno kwa kuhisi soko lote lingegeukia haya madawa mapya zaidi na kuwasababishia hasara. Ndiyo maana nikafatwa. Madam alijua kuwatetemesha.
Nilikuwa sitaki ikawie mno kwa maaskari kuwamaliza hawa watu mwanzo na mwisho, kwa sababu tayari madawa hayo yalikuwa yameanza kushika kasi kubwa mno hapo jijini, na nilihofia yangetoka nje haraka. Bertha alikuwa ameshaanza kung'ara yaani, na kiukweli mwezi huo mmoja kupita ulikuwa mrefu sana kwa sababu nguvu yake na huyo Festo ilikuwa inazidi kukua; hao mapolisi wangehitaji kumaliza haya yote upesi kabla hiyo cocaine haijamaliza watu. Ooh!
Huwezi kunilaumu bwana, sasa mimi ningejua vipi kama maaskari wangehitaji huo muda wote kunyoosha haya mambo? Ni kwamba tu ushirika wote wa Bertha ulikuwa ni mkubwa sana, kwa hiyo kweli muda ulihitajika. Ila kwa kuwa isingechukua muda mrefu mno kutokea hapa mpaka muda ambao maaskari wangetoka vichakani, suala la kufanya lingetakiwa kuwa kuendelea kuigiza tu, na kutulia mpaka wakati mwafaka wa haya yote kukoma.
Mwana baada ya kufika hapo, nikashusha pumzi tu kujipa utulivu wa kiakili, kisha ndiyo nikaelekea huko ndani ya supermarket ili kuendeleza kazi ya kuliharibu taifa.
★★
Tumekuja kumaliza kazi zilizohitajika kwa siku ya leo kwenye mida ya saa kumi jioni, na ndiyo kwa pamoja, mimi na hao vijakazi wawili wa madam tukawa tumeondoka kutoka kwenye supermarket hiyo. Na tulikuwa tukifanya vitu kwa umakini, yaani hata kutoka tu tulifanya ionekane kama vile sisi ni wateja wa kawaida waliokuwa dukani, na tuliondoka kila mtu kivyake kama hatujuani. Hizo ndiyo zilikuwa "code" za madam Bertha, na tulizifata kuhakikisha usalama wa biashara zake unaendelea.
Kwa hiyo mimi nikajiondokea zangu na kwenda kutafuta mgahawa mzuri ili nipate msosi kwanza, kisha ndiyo ningerudi kule Mbagala. Na huu ulikuwa ni utaratibu kwa hizi siku za Jumatatu, Jumatano, na Ijumaa nilipokuja huku Ubungo kufanya haya mambo, lakini nilitakiwa kubadilisha sehemu na maeneo kwa ajili ya mlo kabla ya kwenda nyumbani ili kuepuka kukaririwa sehemu moja tu. Hivyo sasa nikaelekea kwenye mgahawa mmoja eneo waliloliita Fire, na hapo ndiyo nikaagiza msosi wangu na kufungua simu.
Nilikuwa nataka kuona ikiwa Bertha alinitafuta ama vipi, lakini haikuwa hivyo. Nikaamua tu kuzama Facebook kuangalia mambo mapya na nini, ndiyo nikakutana na pendekezo la urafiki kwa mwanadada Dina. Nikakumbuka kweli leo Tesha alikuwa amenipa namba yake, hivyo nikaamua kum-text mtoto. Muda si mrefu akanijibu, nasi tukaanza kuchat hatimaye baada ya utambulisho na nini, na maongezi yakahamia WhatsApp.
Inaonekana mrembo alifurahia sana mimi kumtafuta, kwa hiyo mpaka namaliza msosi bado nilikuwa nachat naye tu, maana kila mara nilipokuwa nakaribia kumuaga yeye angeanzisha mada nyingine tena iliyofanya tuendelee tu kuwasiliana namna hiyo. Kwa hiyo nikatoka hapo mgahawani baada ya kushiba ikiwa imeshaingia saa kumi na moja, na nikawaza nitembee tu kutokea hapo mpaka pale ambapo ningechukulia daladala kwa kuwa kufika huko Kariakoo stendi kuu ya mwendokasi haikuwa mbali sana kutokea Fire.
Nilikuwa nikitembea huku naendelea kuchat na Dina, utani mwingi ukiwa umeshaanza kugeukia kwenye masuala ya 'nani mchumba wako, mimi sina mtu, aah we' mwongo,' ndipo simu yangu ikaanza kuita ghafla. Aliyekuwa akinipigia ni mtu ambaye sikuwa nimetarajia kabisa anipigie, kwa sababu tulifahamiana lakini pamoja na kuwa na namba zake za mawasiliano, hatukuwa na ukawaida wa kuwasiliana kabisa. Na hasa zaidi kwa wakati huu kuna sababu mbaya iliyokuwa imesababisha hilo.
Lakini nikaona nipokee tu ili kusikiliza alichokuwa anataka kusema, na hiyo ni baada ya kumtumia Dina ujumbe mfupi kuwa nitamcheki baadaye, na sauti ya mpigaji ikasikika kutokea upande wa pili akisema, "Hallo... JC?"
"Naam..." nikaitika kama vile sitaki.
"Vipi bro, za siku?" akauliza hivyo.
"Fresh. Nani?" nikauliza hivyo kwa makusudi.
"Dah! Naona hadi na namba yangu ulikuwa umeshafuta..."
"Huwa sifuti namba nazo-save. Labda sikuku-save kwa jina."
"Aaa... haya bwana. Ni Kevin hapa," akasema hivyo.
"Kevin gani?"
"Acha hizo mdogo wangu... ni mimi Kevin, mume wa Jasmine."
"Bado unajiita mume wa dada yangu wakati umemwacha akiwa na ujauzito?" nikamuuliza hivyo.
"Ishu haiko hivyo JC, wote mmeelewa vibaya..."
"Ila ikoje?"
"Ah, kaka we' mwenyewe unajua kabisa kwamba Jas ana mood swing kali mno, hata kwa mambo madogo alikuwa anakuja juu sana... na ujauzito ndiyo ulikuwa unaongeza hilo..." Kevin akaongea kwa upole.
"Ndiyo maana ukaanza kum-cheat, si ndiyo?" nikamuuliza.
"Una uhakika gani na hilo? Kwa sababu tu yeye ndiyo amesema hivyo?"
"Hawezi akakusingizia tu, Kevin. Ni lazima kuwe na ukweli kwenye hilo..."
Akasema, "Nisikilize JC. Nilikuwa nimekutana na sonara mmoja hivi, mwanamke, kumwomba anitafutie mkufu special sana kwa ajili ya Jasmine. Kumbe wakati huo kuna rafiki yake Jasmine alikuwa kwenye mazingira hayo, akatuona, halafu akatupiga picha akamtumia mke wangu. Nimefika home nakuta Jas kavimba, nikijaribu kumwelezea haelewi, na tena nilikuwa nimetoka kunywa kidogo na wakina Banza ndiyo maana ugomvi ukawa mkubwa sana... mpaka nikaamua tu kuondoka ili nisije kusababisha hali yake iwe mbaya..."
"Na ilikuwa mbaya! Unajua kwamba mimba ilikuwa karibu kutoka?" nikamuuliza hivyo.
"Ndiyo, nilisikia, nikaenda hospitali kumwona, lakini alinifukuza kwa kunilaumu kwamba yote ni makosa yangu. Me JC sikupenda kumwacha Jas kwa... njia ya kufanya ionekane kama labda tumeachana kabisa, nilikuwa nataka tu kumpa space atulie kwanza, maana kama unavyojua mambo ya mimba na nini...."
"Nisikie Kevin. Me ni mwanaume, najua mambo mengi ambayo huwa tunafanya, kwa hiyo hata ujiteteeje... najua hayo yote uliyosema siyo kweli. Wewe kiri tu kwamba ulikuwa na mwanamke mwingine, then tafuta utaratibu wa kufanya amani na...."
"No, JC I swear to God... sikudanganyi. Kama unataka kuthibitisha...."
"Mimi nithibitishe ili iweje? Nimekuwa Jasmine? Kwanza kwa nini unanipigia mimi kuniambia haya mambo wakati ni ya wewe na mke wako ku-solve?" nikamuuliza hivyo kistaarabu tu.
Akaniambia, "Unafikiri sijafanya hivyo? Tokea Jasmine aliponifukuza hospitalini, kila nikimpigia simpati, namtumia sms kibunda, hajibu. Nikimtafuta na mama, call zote zinaenda voicemail, najua hata na yeye ana hasira na mimi japo hatukuwahi kuzungumzia haya. Na Mr. Frank... yaani, sijui hata kama naweza kuongea naye, ndiyo maana nikakutafuta wewe mdogo wangu ili nipate njia ya kusema na Jas tena... nimem-miss sana JC... hayupo nyumbani kwangu zaidi ya mwezi sasa hivi, na najua atakuwa kwa mama mkwe huko... natamani hata kwenda, lakini...."
Wakati nikiendelea kusikiliza maombi ya mume huyu wa dada yangu, bado nilikuwa natembea hapo hapo Kariakoo, nikipishana na watu wengi sana, lakini jicho langu likawa limeweza kukamata uwepo wa mtu fulani ambaye ilionekana kama alikuwa akinifuatilia. Sikuweza kuuona uso wake vizuri, ila alikuwa upande wa pili wa barabara, na kwa muda fulani sasa tokea nilipokuwa nimepokea simu ya Kevin, alionekana tu kutembea sambamba na mimi akijifanya kama mpita njia wa kawaida tu.
Alikuwa ni mwanaume, mwenye mwili mkubwa uliolelekea kuwa wa ubonge, akiwa amevalia sweta jepesi jeusi pamoja na suruali ya jeans nyeusi, na sandals za kahawia miguuni. Kofia yake nyekundu kichwani ilisogezwa mbele sana usoni kuuziba vizuri, na kilichofanya nisiuone vyema ni hasa kutokana na umbali, watu, na pia mimi mwenyewe kujitahidi kujifanya kama vile sikuwa nimemtilia maanani mwanaume huyo.
Baada ya Kevin kumaliza kutoa kilio chake kilichoonekana kuwa kilitoka moyoni, nikamuuliza, "Umem-miss eh? Sawa. Nimekuelewa. Kwa hiyo... wewe unachotaka sasa hivi ni nini?"
"Nataka kurudiana na dada yako mapema, JC. Space kwa huu mwezi mzima imetosha, siwezi kusema niendelee kukaa kimya tu halafu aje kujifungua me hata sipo, hiyo italeta picha gani mbele ya wazazi? Hatujafunga ndoa kihalali bado, sawa, lakini moyoni mwangu yule tayari ni mke wangu. Nakuomba ujaribu kunisaidia niongee naye tena," Kevin akasema hivyo.
Huku nikiwa naendelea kuibia kwa jicho langu kumwona jamaa aliyekuwa sambamba nami, nikamuuliza Kevin, "Uko wapi kwani sasa hivi?"
"Nipo kwangu, nimesharudi..."
"Sa' si ungetulia tu mpaka Jasmine ajifungue?"
"Hata hilo nitakubaliana nalo, ila me nachotaka ni kwamba tuwe kwenye mstari mzuri mpaka kufikia siku atakayojifungua. Eh? Haina shida hata akiendelea kukaa na mama huko, la muhimu tu uhusiano wetu uwe sehemu nzuri kwanza, pamoja na wazazi pia... lakini bado simpati yaani... najisikia vibaya..."
Kevin alipokuwa ananiambia hayo, nilikuwa nimeamua kuachana na barabara na kuingia ndani ndani kwenye majengo na sehemu zenye shughuli nyingi, nikitembea kawaida tu, ili nione kama kweli yule jamaa angeendelea kusonga na mimi. Sikukosea. Alikuwa ananifatilia, kwa sababu ningejifanya kugeuza shingo huku na huku kuangalia hiki na kile, na yeye angeonekana kuja nyuma yangu taratibu. Hapo nikaelewa kulikuwa na hatari.
"JC? JC vipi, bado upo?"
Kevin akauliza hivyo baada ya kuona nipo kimya, na kiukweli nilikuwa sijasikiliza mengi zaidi aliyokuwa amesema kwa sekunde chache za mwisho, hivyo nikamwambia, "Yeah, nimekusikia. Nimekuelewa Kevin. Ona... niko... Kariakoo sasa hivi, vurugu, kelele, nitakutafuta bro. Sawa?"
"Nataka unifanyie mpango JC... Jasmine..." Kevin akaongea kwa msisitizo.
"Yeah, nimekuelewa. Tutaongea vizuri baadaye," nikasema hivyo kiuharakishi.
"Haya poa. Nashukuru br..."
Nikakata simu kabla hajamaliza kuongea, nami nikaiweka mfukoni upesi.
Bado mfatiliaji wangu alikuwa akija taratibu tu, na mimi nikaelewa wazi kwamba huyo alikuwa ametumwa kwa mambo mawili; aidha anifatilie tu na kuona ningekwenda wapi mpaka wapi, ama anifatilie mpaka kufikia sehemu ambayo ingekuwa rahisi zaidi kunidhuru. Sikufikiria mtu mwingine yeyote ambaye kwa wakati huu angekuwa na nia ya kutaka lolote baina ya hayo mambo mawili isipokuwa Sudi.
Huenda machale yangu ya kukisia kwamba ningeanza kufatiliwa na watu wake kwa kipindi hiki ndiyo yalikuwa yameanza kuzaa matunda yake, lakini kama siyo hivyo, basi hapa ningekuwa nikishughulika na adui mwingine ambaye sikufahamu wazi alikuwa nani. Kwa vyovyote vile, ningepaswa kumwepuka haraka sana, hivyo nikaamua kuanza chenga.
Kwa mwendo wa kawaida tu, nikaanza kupita huku na kule na kuibukia sehemu ambazo hata sikuwa na ujuzi kuzihusu kufahamu nilikuwa wapi, na bado katika hizo zote huyo jamaa aliendelea kuwa mkia wangu. Nilijitahidi sana kuhakikisha sifanyi agundue kwamba nilitaka kumwepuka, lakini najua wazi kwamba angetambua muda siyo mrefu kuwa nilimpiga chenga kwa makusudi.
Hivyo nikawa nimefikia sehemu fulani ya ndani zaidi iliyokuwa na soko la vyakula na mbogamboga, pakiwa na ardhi yenye matope mazito na uchafu mwingi, watu wakipishana kwa shida, nami nikaona sehemu ndogo sana iliyokuwa na uwazi uliotenganisha milingoti ya miti minene, iliyoshikilia maturubai ya wafanyabiashara. Nikafanya kuingia hapo na kujibananiza huku nikiigiza kuweka simu sikioni na kuficha uso wangu kiasi, na baada ya sekunde chache, nikamwona jamaa akitokea upande niliotokea pia, naye akapitiliza zaidi kwa kufikiri niliendelea kwenda huko mbele.
Hapo hapo nikatoka upesi sana na kuanza kurudi haraka kule nilikotoka, na ingawa hizi kona na chocho za Kariakoo zilichanganya, nikafanikiwa kufika mpaka eneo lililoegeshewa daladala, lakini siyo kule nilikokuwa nadhamiria kwenda kuchukua daladala za kuelekea Mbagala, na sikuwa nimemwona yule jamaa tena.
Haraka mno nikapanda gari ambalo lilikuwa linaelekea sehemu ambayo hata sikuangalia na kujali, yaani nikapanda tu na kukaa. Likaendelea kusimama hapo hapo kwa dakika kadhaa hata baada ya kujaza abiria, na kupitia kioo cha dirisha nikawa nimemwona yule jamaa akiwa anakuja upande huu.
Bila hata ya kuwa nimeuona uso wake, ikanibidi nijifiche zaidi kwa kuinamisha uso wangu, na mpaka kufikia dakika ambayo daladala ilianza kuondoka hapo, ningemwona mwanaume yule pale nje akiwa amesimama pembezoni mwa duka fulani kubwa, akiangaza huku na kule bila shaka kunitafuta, lakini bado sikuweza kuuchora uso wake vizuri sana, ingawa sasa nilitambua kwamba alikuwa na ndevu nyingi kwenye mashavu mpaka kidevuni. Aloo! Siyo poa.
Nikakaa vizuri zaidi baada ya gari kuondoka eneo hilo, huku nikiwaza ni nini hasa ambacho niliponea chupuchupu kwa muda huo. Huu mchezo ulikuwa umeanza kuwa hatari zaidi kwangu, na kama nisingekuwa mwangalifu, basi ningejikuta najipoteza mapema mno. Kuna maamuzi fulani magumu ambayo ningehitaji kuchukua haraka kabla mambo hayajaniharibikia kwa sababu ya kukaa kusubiri tu, nami nikaamua kuvuta simu yangu na kumpigia mtu ambaye sikufikiri ningekuja kuwahi kutaka kumpigia mimi mwenyewe, naye akawa amepokea.
"Hallo..." sauti yake ikasikika.
"Yes, hallo..." nikaitikia hivyo.
"JC. Habari gani?" akauliza.
Nikamwambia, "Ninaomba kuonana na wewe tafadhali... Festo."
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments