FOR YOU
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA NNE
★★★★★★★★★★★★★★★★
MIAKA... NANE... BAADAYE...
Miaka hupita haraka, na katika kisa hiki hali haikuwa tofauti. Miaka nane ilikuwa imepita tokea wakati ule mbaya sana kuwahi kuikumba nchi. Watu wengi waliuawa kipindi kile ambacho kama ungemuuliza mtu fulani siku za wakati huu kuhusu kipindi hicho, angekwambia kilikuwa kinaitwa "enzi za Demba Group," ijapokuwa haukuwa umepita hata muongo (miaka 10).
Raisi Paul Mdeme bado alikuwa madarakani, pamoja na wasaidizi wake wengi kwenye vyeo vyao vya kisiasa ambao walikuwa wafisadi na wanafiki kama yeye tu. Kipindi cha miaka miwili nyuma kilikuwa kipindi cha uchaguzi mkuu wa viongozi nchini, naye kama kawaida yake alisaidiwa kushinda tena uraisi kupitia udanganyifu uliofanywa na watu waliomuunga mkono na aliowalipa kuchakachua matokeo. Alipenda kutupa pesa za sifa kwa "chawa" wake wengi na kufurahia anasa sana.
Kuna vitu vipya alivyovijenga kwenye nchi ambavyo vilifanya ionekane kwamba yeye ni Raisi mzuri sana, lakini ukweli ni kwamba alikuwa akiwanyonya watu kwa njia ambazo hawakutambua kirahisi. Si wote waliokuwa na maisha mazuri, kwa sababu matajiri wangeendelea kubaki matajiri, na masikini, masikini. Sera yake ya kuboresha maisha ya wananchi WOTE ilikuwa imeshindwa sana, naye aliendelea kufanya mambo mengi haramu (illegal) bila kujulikana, kama tu kipindi kile cha Demba Group.
Jenerali Jacob Rweyemamu. Ah! Shetani wa mashetani. Bado alikuwa kwenye cheo chake hicho, naye pia aliendelea kufurahia anasa kutokana na unyonyaji walioufanya yeye na kundi lao lote lililoshiriki vitendo vile vya ukatili miaka nane iliyopita. Alikuwa pia aina ya kiongozi wa jeshi mwenye kuogopwa sana, na hata ingeweza kupita mwaka kaonekana hadharani mara mbili au mara tatu tu, kwa sababu kazi nyingi aliwaachia wengine wafanye huku yeye akifurahia starehe na wanawake tu. Bado waliendelea kuungana mkono na Raisi Paul Mdeme, hivyo kihalisi taifa lilikuwa kwenye hali inayoweza kuitwa "siyo sawa."
Weisiko naye alikuwepo, akiwa bado na cheo chake cha Luteni Jenerali kilichofuata cha Jenerali Jacob. Bado alikuwa mtu makini sana, aliyetekeleza mambo yote ambayo Raisi na Jenerali walimwagiza kufanya. Alifurahia pia mali nyingi alizojichumia kwa kuwa upande wao, na mambo ya kikatili hakuwa ameacha. Nyakati ambazo watu fulani wangezingua utendaji wa Raisi au Jenerali, Weisiko aliongoza mauaji yasiyo ya moja kwa moja kwao ili kuwanyamazisha, na hivyo kufanya kelele ziwaondokee wakuu wake.
Kulikuwa na maoni mchanganyiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na utendaji wa viongozi na maendeleo ya nchi. Kwa asilimia kubwa, wengi waliona ni kama walikuwa wakinyonywa na hakukuwa na maendeleo ya aina yoyote, huku ile ndogo ikiwa yenye kuiunga mkono serikali hiyo na uongozi wake. Asilimia hii ndogo ndiyo ya wale "chawa" ambao walikuwa wanapenda tu kushabikia viongozi ili wapate faida. Wabunge wengi, mawaziri, madiwani, na hata maaskari walitenda kwa njia zenye ubinafsi sana zilizowaumiza wananchi wengi. Kwa wengi wa viongozi ilikuwa ni kufanya tu safari za nje ya nchi na kuishi maisha ya gharama sana, huku watu sehemu mbalimbali wakipitia magumu ambayo yalihitaji uangalizi wao lakini hawakupata.
Kwa hiyo hivyo ndivyo jinsi maisha yalivyokuwa chini ya utawala wa Mdeme ambao kwenye runinga ulisifiwa sana lakini kwenye uhalisia ulikuwa ukikashifiwa sana. Lakini muda si mrefu, mambo mengi yangebadilika kwa njia ambayo haingetazamiwa.
★★★★
Ikiwa ni ndani ya kipindi hiki hiki cha utawala wa Mdeme, jambo fulani lenye kushangaza sana lilitokea. Majengo ya benki kuu ya nchi yalivamiwa na kundi la wezi lisilojulikana, na kundi hilo lilibeba pesa nyingi sana kupita maelezo. Yaani, hakukuwahi kutokea kitu cha namna hiyo popote pale, kwa sababu ziliibiwa jumla ya pesa taslimu za kitanzania TRILIONI 20! Yaani trilioni 1 ni sawa na bilioni 1000, sasa piga hesabu trillioni 20 ni sawa na billioni ngapi. Haloo... si mchezo! Hizo zilikuwa ni pesa nyingi sana, na ilishangaza wengi kuhusu ni jinsi gani ziliweza kutolewa kwenye majengo hayo, zikiwa za karatasi kabisa (cash), na watu hao wasikamatwe.
Kwenye majengo hayo siku hiyo ya wizi yalilipuka mabomu mawili, moja kwenye kila jengo. Zilipita SIKU MBILI bila ya waandishi wa habari kuruhusiwa kuingia maeneo hayo ili kujua ni nini hasa kiliendelea, ndipo baada ya hapo wakaruhusiwa na taarifa hizo zikaanza kusambaa sasa. Viongozi walichanganyikiwa balaa. Yaani maneno yalisemwa na kusemwa mpaka ikawa kama kituko. Raisi Paul Mdeme alikuja kutoa tamko lake la hadharani na kusema wezi hao wangekamatwa tu, kwa sababu hawangeweza kutoroka na kitita kikubwa namna hiyo cha pesa. Sehemu za mipaka zilifungwa kutoruhusu yeyote kuondoka mpaka wahakikishe wanawakamata watu hao.
Lakini wadau wengi bado waliuliza; iliwezekanaje kweli, eti wezi waibe trillioni 20 kwenye makao makuu ya pesa yenye ulinzi mkali, wasikamatwe, halafu waje kukamatwa baadaye? Wengi waliona huenda kuna mchezo umefanywa na viongozi kuiba pesa hizo na kusingizia wezi, kwa sababu ni kitu ambacho hakikupatana na akili kabisa, lakini hakuna aliyekuwa na uhakika. Msako ulioendelea ulihusisha maaskari na wanajeshi, wataalamu wa mambo ya teknolojia na mitandao ili kuweza kuwapata wezi hao, lakini hawakufanikiwa hata kidogo!
Kama ni kitu ambacho kiliachwa na wezi hao nyuma, ilikuwa ni kibandiko (sticker) chenye mchoro wa sura ya mnyama kama simba mweupe anayeonyesha meno yake kwa ukali, na chini ya mchoro huo yalikuwa maneno "MESS MAKERS." Kwa hiyo wezi hao walikuwa kama wameacha alama ya utambulisho wao, kama kundi fulani hivi la kigaidi, na jina lao lilikuwa likimaanisha "watu wanaochafua mambo." Watu wengi, hasa wahuni, waliwaita "chafu." Mitandao ya kijamii ilifurika kwa mijadala yenye ucheshi mwingi kuhusiana na tukio hilo, na haikupita siku yoyote ile bila jina "Mess Makers" kutajwa kwenye vipindi vya habari kwenye runinga.
Ilikuwa ni jambo liliohitaji kufanyiwa ufumbuzi mapema sana, kwa sababu pato la nchi liliporomoka kwa asilimia kubwa kuwahi kutokea, na mipango mingi ya kimaendeleo iliyokuwa imewekwa isingefanikiwa hata kidogo......
★★★★
DAR ES SALAAM
Ndani ya jengo la makao ya muda mfupi ya viongozi wa Jeshi la nchi, kulikuwa na mgeni maalumu kutoka kwenye Wizara ya Polisi, ambaye alikuwa ni "Principal Secretary" wa mambo ya ndani yaliyohusiana na jeshi la polisi. Aliitwa Joachim Uwesu, naye alikuwa amefika hapo ili kuwapatia taarifa muhimu Kanali Oswald Deule na Kapteni Erasto Shimuye wa Jeshi la Nchi, iliyogusiana na suala zima la msako wa wezi wale kwenye makao makuu ya benki kuu nchini. Alikuwa amefika kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Donald Ngassa, ambaye alikuwa sehemu nyingine ya mkoa akiendesha operesheni zingine maalumu.
"Zimepita siku kumi na moja toka watu hao walipoiba mabilioni ya pesa na mpaka sasa hawajajulikana na kukamatwa. Maneno mengi yanazagaa, na hali ya kiuchumi nchini imeanza kuporomoka kwa huge estimates za asilimia.... jamani, ndani ya mwezi mmoja mambo mengi kimiradi yataanza kuporomoka zaidi na zaidi. Nimeagizwa kukuletea pendekezo katika suala la kuwakamata watu hao..." akasema Secretary Joachim.
Akampatia faili fulani Kanali Oswald, naye baada ya kulifungua, akalitupa mezani kwa kukerwa.
"Principal Secretary... unafikiri mimi sijui jinsi ya kufanya kazi yangu?" Kanali Oswald akamuuliza.
"Hapana mkuu, siyo hivyo, ni kwamba...."
"Sijali umeagizwa na nani. Sihitaji msaada wake kwa kuwa kila kitu kiko under control. Nenda kawaambie waliokuagiza kwamba ninashughulikia mambo yote ipasavyo, sihitaji babysitter," Kanali Oswald akasema.
"Kumradhi mheshimiwa Kanali, lakini hili ni pendekezo muhimu sana. ACP Lois...."
"Hakukuwa na haja ya kumwita hapa! Hili suala tunaweza kulishughulikia sisi wenyewe, kwa kuwa tunajua zaidi ya hao maaskari," akasema Kanali Oswald.
"Ninaelewa Kanali, na ninaheshimu sana kila jitihada ambayo mmeweka katika hilo. Lakini tunahitaji sana msaada wake kwa kuwa kwenye masuala ya namna hii amethibitisha kuwa na kipawa kikubwa sana, na mbinu nzuri katika kuwakamata wahalifu sugu. Ni kwamba...."
"Ninajua anachoweza kufanya. Lakini kama nilivyosema, tunalishughulikia hili suala sisi wenyewe. Nimepewa mamlaka yote na Jenerali kuongoza operation nzima ya kuwakamata wezi hao, kwa hiyo ninachosema ni kwamba simhitaji ACP hapa," akasema Kanali Oswald.
"Hii siyo kuhusu wewe Kanali..." akasema Secretary Joachim.
"Nini?" Kanali Oswald akauliza.
"Ni amri kutoka kwa Raisi kwamba ACP Nora Lois ajiunge katika kuwasaidia na operation hii," akasema Joachim.
"Raisi? Una uhakika na unachokisema? Una uthibitisho gani?" Kanali Oswald akauliza kiukali.
"Kila jambo liko kwenye hilo faili ulilotupa mezani," Secretary Joachim akasema kwa uthabiti.
Kanali Oswald akalichukua tena na kuanza kulipitia. Kweli aliona pendekezo hilo lilikuwa limetoka kwa Raisi kwa kuwa hata muhuri wake ulikuwepo hapo. Akamwangalia Kapteni Erasto ambaye alikuwa akimtazama kwa umakini pia, naye akalitupa tena mezani faili hilo na kumsogelea karibu Secretary Joachim.
"Kwa hiyo wanataka kumleta huyo mtoto mdogo ndiyo afanye kazi yangu? Kwa nini? Wanafikiri nimeshindwa?" Kanali Oswald akauliza.
"Hapana. Unatakiwa tu kushirikiana naye kwa sababu ana level nzuri ya ujuzi katika kushughulika na masuala haya. Bado nguvu ya command utakuwa nayo, lakini yeye ataongoza mbinu zote zitakazohitajika kufuatwa," akasema Joachim.
"Ataongoza? Yaani mimi Colonel niongozwe na ACP wa Jeshi la Polisi?" Kanali akauliza.
Secretary Joachim akashusha pumzi, kisha akasema, "Kama nilivyosema, hii siyo kuhusu wewe Kanali. Ni kuhusu nchi yetu sote. Shida hii inapaswa kupatiwa utatuzi haraka sana, na hii ni kati ya njia zitakazosaidia kufanikisha hilo. Ikiwa una tatizo lolote na badiliko hili unaweza submit lalamiko kwa General. Lakini nakuhakikishia hata yeye...."
"Of course, of course. Hata yeye atasema ni sawa tu. Hawa wezi washenzi wamekuwa mwiba kwangu na sasa naongezewa mwingine... ahah... eti kisa damu ni nzito kuliko maji," Kanali Oswald akasema kwa kejeli.
"ACP yuko wapi sasa?" akauliza Kapteni Erasto.
"Alikuwa agency moja ya CHRAGG kule Dodoma juzi, lakini tayari amepokea mwito huu hivyo atafika kesho," akasema Joachim.
"Wow! Kumbe tayari ilikuwa imeshapigwa na tiki kabisa kwamba mtoto wa mwenyewe aje kujipodolesha huku, halafu ndiyo ningepewa taarifa baada," akasema Kanali Oswald kwa kuudhika.
Wote wakamwangalia Kanali kwa sekunde chache, kisha Kapteni Erasto akauliza, "CHRAGG alikuwa anafanya nini?"
"Alikuwa tu akisaidia kuwafundisha baadhi ya maafisa wa level za juu. Anaweza akawa "mtoto" kama Kanali asemavyo, lakini atakuwa msaada mkubwa sana katika hili," Secretary Joachim akasema.
Kanali Oswald alimwangalia kwa kukerwa sana. Hivyo bila kukawia, Secretary Joachim akawaaga wakuu hawa na kuondoka kwenye jengo hilo. Kanali Oswald akapiga meza kwa ngumi yake.
"Msako nchi nzima, zaidi ya wiki nzima wa wajinga wachache tu lakini mpaka sasa hatujawashika... najua hii ni njia ya Weisiko ya kutaka kuniharibia,' akasema Kanali Oswald.
"Kwa nini unasema hivyo?" Kapteni Erasto akauliza.
"Toka kitambo hakupenda kabisa kwamba na sisi tulijiingiza kwenye mambo yao na General, kwa hiyo kwa sababu yuko tight naye anataka tu kunishusha ili General asini-favor."
"Kwa hiyo huu mpango wa kumleta ACP ni wazo la Weisiko? Unajuaje hilo?"
"Aagh... sijui Erasto, lakini ninahisi ndiyo iko hivyo. Hivi kweli operation ya namna hii wamtume huyo.... aah..."
"Si amempendekeza Raisi?"
"Mdeme hana muda wa kufatilia nani ni mjuzi kwenye haya masuala, yeye atakubaliana tu na lolote ambalo General atapendekeza. Na aliye nyuma ya General kumfanyia haya yote ni nani kama siyo Weisiko?" Kanali Oswald akasema kwa ukali.
"Mh... ngoja tuone kama kweli kataweza kuleta kitu kipya hapa. Nafurahi tu hatujazinguliwa kwa kutoweza kuwashika hao washenzi..."
"Umeshafikiria ni nini kitatokea ikiwa tutawashika na huyo ACP akiwa hapa?"
"Kwamba credit yote itaenda kwake?"
"Kwamba tutaonekana wapuuzi tu wasiojua kazi wanayoifanya!"
"Kanali... nimefatilia kazi zake... na kiukweli yuko vizuri. Ngoja tumpe nafasi tuone..."
"Nafasi siyo yetu kumpa, kashapewa... mbona huelewi Erasto? Muda si muda tutakuwa tunafanya mambo chini ya kivuli chake," Kanali Oswald akasema.
"Sawa mkuu, nimeelewa. Lakini hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kwenda na muziki," akasema Kapteni Erasto.
"Wanafikiri kwa kuwa kamefanikiwa kwenye mambo kadhaa ya kipelelezi basi kataweza kuipindua na hii meza... ngoja waone ikiwa itakuwa rahisi kama wanavyofikiria," Kanali Oswald akasema.
Kanali Oswald alikuwa amekerwa sana na uamuzi huu wa kumleta ACP Nora Lois katika utatuzi wa wizi huo kwenye makao makuu ya benki ya nchi, kwa sababu alitaka sana kujionyesha kuwa bora zaidi ya yeyote endapo angefanikisha kuwakamata wahalifu wale kwa njia zake. Kwa hiyo alihisi ni kama alishushwa thamani kutokana na hili kwa kuwa yeye alikuwa Kanali kwenye Jeshi la Nchi, huku ACP Nora Lois, yaani Kamishna Msaidizi wa Polisi, akiwa wa cheo cha kadiri kwenye Jeshi la Polisi, lakini akaendelea kuamini kwamba ikiwa wangefanikiwa kuwashika wezi hao, basi isingekuwa kwa jitihada yoyote ila ya kwake tu.
Wakajiweka tayari kwa ajili ya kumpokea ACP Nora Lois ili waweze kuona ni nini ingekuwa hatma ya msako huo.
★★★★
Siku iliyofuata, viongozi hao wawili wa jeshi pamoja na Secretary Joachim walikuwa ndani ya chumba maalumu cha mkutano kujadili suala hili la wizi wa matrilioni kwenye benki kuu. Aliyekuwepo hapo pia ni Luteni (Lieutenant) wa cheo kilichofuata cha Kapteni Erasto, aliyeitwa kwa jina la Michael Mwakasiba, ambaye alikuwa mwanajeshi (na jasusi) mwenye mwili wa kikomando na mwenye uzoefu katika masuala ya kivita. Katika operesheni hii ya kuwasaka wezi wale, alikuwa ameitwa pia ili kuongoza timu yake maalumu katika msako huo, kwa kuwa alikuwa na kiwango cha huu cha umakini kwenye kazi. Alikuwa ni mtu wa kamata, piga, weka ndani, na asingesita kuua mtu yeyote ambaye angejaribu kumletea ushenzi mbele ya kazi yake.
Secretary Joachim alikuwa amewaambia viongozi hawa (Kanali Oswald na Kapteni Erasto) kuwa IGP Donald Ngassa angefika hapo pia pamoja na ACP Nora Lois, na kwa kejeli Kanali Oswald akasema bila shaka wangewasubiri maana muda wote duniani wa kusubiri walikuwa nao. Kapteni Erasto alimfahamu vizuri sana Luteni Michael, naye alijua mara tu atakapotia nyayo zake katika msako huu, basi matokeo yangekuja vizuri. Luteni Michael ndiye aliyekuwa amevalia T-shirt yenye rangi nyeusi na suruali ya kijeshi, huku wengine wakiwa wamevalia suti za kazi zenye nembo za vyeo vyao. Kapteni Erasto alikuwa akizungumza na Luteni Michael, huku Kanali Oswald akizungumza na watu fulani kwa simu.
Baada ya muda mfupi, akaingia ndani humo IGP Donald Ngassa, akiwa amevalia nguo za kipolisi na kofia. Nyuma yake alifuatwa na mwanamke fulani aliyevalia T-shirt nyeupe yenye kubana na suruali ya jeans, naye alikuwa na umbo lililonawiri kiasi lakini siyo nene sana. Nywele zake ndefu na laini zililazwa kufikia mabegani, naye alikuwa na macho mazuri pia. Mikononi hakubeba chochote kile zaidi ya 'tablet' ndogo ambayo alitunzia mambo yake muhimu kwa ajili ya kazi. Huyu alikuwa ni ACP Nora Lois.
IGP Donald alipiga saluti ya heshima kwa wakuu hapo, naye ACP Nora akafanya hivyo hivyo, kisha wote wakaanza kuwasalimu wa hapo ndani. Luteni Michael alibaki kumwangalia tu mwanamke huyu, na kwa haraka akawa amevutiwa naye sana. Secretary Joachim ndiye aliyefanya kama kuwatambulisha kwa waliokuwa ndani hapo, na wakati ACP Nora alipotambulishwa kwa Luteni Michael, Luteni akamfata na kumnyooshea mkono ili waiunganishe kwa salamu. ACP Nora akatabasamu na kukubali hilo, naye Luteni Michael akawa anamwangalia kwa macho yaliyoonyesha upendezi mwingi.
Baada ya hapo, wote wakaketi na kumwacha Kanali Oswald aelezee mambo kwa ufupi kwa wote.
"Na sasa, sijui kama kuna jambo jipya ambalo mnaweza kuleta hapa kwa kuwa kila njia tumeipitia... kwa hiyo uwanja ni wenu sasa," akasema Kanali Oswald.
"Bado inasugusha kichwa kuhusu ni jinsi gani waliweza kuingia na kutoka sehemu kama ile... hawajaacha clue zozote, fingerprint, wala nini... ndiyo maana imekuwa ngumu sana kuwajua. Ni jambo la ajabu sana trilioni 20 kubebwa bila kuonekana! Walitumia njia gani hawa watu?" akasema Secretary Joachim.
"Speculation za juu zikiwa ni kwamba huenda wameshirikiana na baadhi ya waliofanya kazi pale ndiyo zimefanya mpaka sasa wafanyakazi wa hapo waendelee kushikiliwa na kuhojiwa. Lakini hakuna chochote kilichopatikana chenye kusaidia," akasema Kapteni Erasto.
"CCTV camera zote zilichekiwa?" akauliza Luteni Michael.
"Mara mia," akajibu Kapteni Erasto.
"Timu zetu zina mafunzo ya hali ya juu. Watu wako makini sana, wanatumia mbinu zote kwa kuwa wana uelewa mzuri kutokana na taarifa wanazopata hata kama ni chache ili kutatua hii kitu... lakini mpaka sasa hakuna matokeo... tunafeli wapi? Unaweza ukasema labda hao wajinga walitumia uchawi lakini hakuna kitu kama hicho. Labda tu walichagua siku na wakati ambao bahati ilikuwa upande wao, because this is impossible," akasema Kanali Oswald.
"Hapana siyo impossible, kwa sababu wameshathibitisha kwamba ni possible," akasema ACP Nora.
"Well hatujaja hapa ili kuwasifia hao wajinga ACP. Ongea point yako," akasema Kanali Oswald kwa kukereka.
"See, hilo ndiyo tatizo Kanali. Unafikiri kwamba ni wajinga, lakini kihalisi hawa watu wana akili nzuri sana ya kile wanachokifanya," akasema ACP Nora.
"Katika vita, viongozi wenye experience kama sisi sikuzote huwa tunapangilia mambo kwanza kwa ufasaha kabla ya kuishinda, na siyo kwenda kichwa kichwa tu," akasema Kanali Oswald.
"Ndiyo lakini, mara nyingi viongozi wanaojenga uelewa wa haraka na kuchukua hatua za vitendo mapema ndiyo hupata mafanikio kwa kuwa wana faida ya kukimbizana na adui kwa ukaribu, siyo kusubiri afike mbali. Huu muda wote uliopotea unafanya hao watu wazidi kukimbia tu na kutuacha mbali. Kinachoangaliwa hapa sikuzote huwa ni mambo makubwa makubwa tu, lakini mki-pay attention kwa detail hata ndogo nawaambia mtaona mambo mengi sana," akasema Nora.
Kanali Oswald alimwangalia ACP Nora kwa mkazo sana. Ilikuwa ni kama mwanamke huyu alikuwa akishindana naye, lakini kihalisi alikuwa anamwambia tu ukweli.
"Umeona nini ACP?" Luteni Michael akamuuliza Nora.
"Nilipitia tape za CCTV za nje. Sijui waliwezaje kuingia kule ndani na hata kutoa zile pesa, lakini nafikiri natambua walichofanya ili kutoka," akasema ACP Nora.
Wote wakabaki kumwangalia kwa umakini.
"Bomu la kwanza lilipolipuka, clamor zilikuwa nyingi, vurugu na sintofahamu kubwa. Ukifatilia utagundua kuwa bomu la kwanza lililipuliwa karibu kabisa na...."
"Milango ya vault, ambazo baadae zikawa tupu," akamalizia Luteni Michael.
"Ndiyo. Sijui ikiwa walikuwa wameshatoa pesa au la, lakini bomu la kwanza halikuumiza yeyote pale; wote walitoka salama. Ilichukua dakika zaidi ya 20 kwa maafisa kuingia kule ndani bomu la pili lilipolipuka, na hata hapo hakuna kifo kilichotokea, sana sana baadhi yao na wafanyakazi kadhaa waliumizwa. Timu special ilipotumwa kwenda kule ndani kuwatoa nje na kuwapeleka hospitali, haijulikani kama bado pesa zilikuwepo ama zilikuwa zimeshaondolewa..." akaeleza ACP Nora.
"Kwa nini unarudia kutuambia mambo ambayo tunajua?" Kanali Oswald akauliza.
"Kanali, zilifika ambulance 13 kuwaondoa waliojeruhiwa. Lakini hospitali zilikoelekea zilikuwa ni ambulance 12 tu," akasema Nora.
Luteni Michael akamtazama kwa umakini sana ACP Nora, na kwa kuelewa alichomaanisha, akachekea kwa chini. Wote wakawa wameelewa alichomaanisha.
"Unataka kusema kwamba... yaani... hao wezi walikuwa hapo hapo?!" akauliza Kapteni Erasto kwa mshangao.
"Ndiyo," Nora akajibu.
"Unbelievable!" akasema Secretary Joachim.
"Kwa hiyo... walikuwa ndani... wakiwa wamevaa kama wanajeshi au walinzi au wafanyakazi... wakati walipokuwa wanawatoa waliojeruhiwa na wenyewe walikuwepo, halafu wakaingia kwenye ambulance fake ambayo labda iliendeshwa na mwenzao... wakatoroka wakiwa hapo hapo!" Kapteni Erasto akasema.
"Hiyo mbona kama ni kitu ambayo haiwezekani? Kama ni hivyo basi pesa zingekuwa pale pale... maana wasingeweza kuzibeba huku wakijifanya kujeruhiwa," akasema Luteni Michael.
"Kuhusu kuziondoa pesa, ni kwamba kuna njia fulani walitumia ambayo... bado haijaelezeka. Lakini hata kwa njia ndogo namna hiyo ya kutoroka wameonyesha wanaweza ku-toy na defence zinazojiita za hali ya juu. Siyo wajinga hawa watu... wanajua wanachokifanya," akasema ACP Nora.
"Kwa hiyo kujua haya yote kutatusaidia vipi kuwakamata?" akauliza IGP Donald.
ACP Nora akaanza kubofya kwenye tablet yake, kisha akampa IGP Donald ili ampatie Kanali Oswald.
"Nilichukua copy tape za CCTV za nje kuzunguka majengo hayo na kuzipitia kuangalia watu waliopita maeneo hayo ndani ya wiki tatu za nyuma. Kwa kawaida kama ni watu wanaojirudia kupita eneo fulani, huwa ni nadra kukaa sehemu moja kwa muda mrefu, au hata kubadili sehemu ya kukaa IKIWA tu walikuwa wapita njia; isipokuwa huyo," akasema ACP Nora.
Kanali Oswald alikuwa anaangalia picha kwenye tablet hiyo, nayo ilikuwa ya mtu mwenye mwonekano mchafu sana na nywele zilizovurugika. Kwa haraka Kanali Oswald akatambua huyu alikuwa mtu kichaa.
"Nini hiki?" Kanali Oswald akauliza.
"Huyo mwanaume anayeonekana kama mwehu hapo, ndiye ambaye ame-appear mara nyingi zaidi eneo hilo kuliko mtu yeyote, na sehemu anazopitia ni tofauti KUZUNGUKA majengo yale, halafu anakaa sehemu moja akijifanya kama anapumzika. Hilo linakwambia nini?" ACP Nora akasema.
"Kwamba ni mmoja wao ndani ya disguise?" Kanali Oswald akauliza.
"Ndiyo," akajibu ACP Nora.
"Unawezaje kuwa na uhakika na hilo?" Secretary Joachim akamuuliza.
"Hakuhitajiki uhakika hapo. Hili ni kweli kabisa. ACP anachotaka kusema ni kwamba watu hawa wamekuwa wakifanya kama... reconnaissance ya maeneo haya kwa muda mrefu ili kujua udhaifu wa eneo hilo na kupangilia jinsi ya kuingia na kutoka. Wanajua wanaofanya kazi hapo, walinzi, wakuu, na kadhalika. Ili kuficha utambuzi wao wanatumia disguise. Hapa tunadili na ma-professional, siyo mchezo," akasema Luteni Michael.
"Na huo ulikuwa ni mwanzo tu," akasema ACP Nora.
"Subiri kwanza. Huyu anaweza akawa ni chizi kama machizi wengine tu. Hivi kweli unataka kuleta ndani chizi, si utaonekana chizi?" akauliza Kapteni Erasto.
"Hivyo ndivyo wanavyotaka kuwafikirisha Captain. Baada ya hiyo... heist... huyo chizi hajaonekana eneo hilo tena, wakati alikuwa anafika hapo kila siku kwa wiki tatu mfululizo, and then the next day kabla wizi kufanyika poof... akapotea," akasema ACP Nora.
"Ikiwa walikuwa wanajiamini kupita mpaka ndani na kuiba pesa zile zote kama vile siyo kitu, kwa nini watumie njia ya namna hii... kama kweli ni ma-professional?" akauliza IGP Donald.
"Kwa sababu haikuwa rahisi kwao kupata blueprint za ndani ya jengo. Kujua pesa zinakaa wapi, watumie muda gani, na njia gani kulihitaji planning za hali ya juu, ndiyo maana wakamweka huyu 'chizi' hapo nje. Huwezi kujua... labda hata walitumia disguise za sura kwa baadhi ya wafanyakazi wa pale ili kuingia ndani kule... anything is possible," akasema ACP Nora.
"Ahahah... ACP unaigeuza hii kuwa kama movie," akasema Kapteni Erasto.
"Hapana, yuko sahihi," akasema Kanali Oswald.
"Kanali, kweli hapa nchini kuna mtu anayeweza kufanya hayo yote na tukashindwa kugundua mapema?" Kapteni Erasto akauliza.
"Tumeshindwa kugundua mapema kwa sababu tumekuwa tukiangalia mambo mengi kwa juu-juu. Ilitupaswa tutulie, tuangalie njia walizotumia kwanza ndiyo tujue jinsi ya kuwakamata. ACP Nora umefanya kazi nzuri sana. Na imenishangaza kwa sababu umepewa ishu hii ndani ya siku mbili tu, umewezaje kutambua haraka mambo yote hayo?" akasema Kanali Oswald.
"Kama nilivyokwambia Kanali, yuko vizuri sana," akasema Secretary Joachim.
"Kweli. Unastahili cheo cha juu zaidi ya hapo aisee," akasema Luteni Michael.
ACP Nora akatabasamu na kusema, "Shukrani, lakini niko sawa na nilipo kwa sasa."
"Kwa hiyo picha hii inahitaji kusafishwa vizuri ili huyu mpumbavu akamatwe na awataje wenzake," akasema Kanali Oswald.
"Ndiyo. Lakini... tunahitaji kufanya mambo kwa umakini zaidi. Hawapaswi kutuona tukija kwa sababu wanaweza kubadili nyendo zao haraka," akasema ACP Nora.
"Tunajuaje kwamba hawajaondoka nchini?" akauliza Secretary Joachim.
"Kwa sababu ya pesa walizoiba. Kuziondoa nchini haingekuwa rahisi, kwa hiyo ni lazima kuwe na sehemu fulani wamezificha, na wao kujificha," akasema Kanali Oswald.
"Ndiyo ni kweli," akasema IGP Donald.
"Hii taarifa tumfikishie General haraka," akasema Kapteni Erasto.
"Hapana, nataka tufanikishe kwanza zoezi hili. Luteni, utakuwa ukifanya kazi hii sambamba na ACP Nora. Chochote mtakachopata mnanipa taarifa haraka. Na hakikisha unawafunkurunyua hao jamaa huko waliko na kuwaleta kwangu mapema, inaeleweka?" akasema Kanali Oswald.
"Ndiyo mkuu. Ondoa shaka," akasema Luteni Michael.
"Kwa hiyo kila sehemu atakayokwenda Luteni...."
"ACP Nora atakuwa pamoja naye. Kuna tatizo na hilo?" Kapteni Erasto akamkatisha IGP Donald.
"Ah... hapana, Itakuwa sawa kabisa," akasema IGP Donald.
"Sawa. Kusanya timu yako mwanze kazi Luteni. Nileteeni nyama jioni," akasema Kanali Oswald kitamathali.
Luteni Michael akasimama pamoja na wengine, nao wakapiga saluti za heshima. Kanali Oswald akamrudishia ACP Nora tablet yake, kisha ACP Nora, IGP Donald, pamoja na Luteni Michael wakatoka ndani ya ofisi hiyo.
"Mtoto yuko vizuri," akasema Kapteni Erasto.
"Yeah, Raisi anajua machaguo yake," akasema Secretary Joachim.
"Just to be clear, hii mission siyo ya ACP Nora. Ameletwa kusaidia tu kwa sababu ana kichwa kikubwa na siyo command, lakini hapa kila jambo nitaongoza mimi, sijui mnanielewa?" akasema Kanali Oswald.
Secretary Joachim na Kapteni Erasto wakatazamana kwa kutopendezwa na wivu usio na maana yoyote wa Kanali Oswald. Alikuwa anaona ni kama vile ACP Nora angepata sifa kubwa badala yake endapo mission hii ingefanikiwa kwa sababu ya akili yake nzuri ya kuchanganua mambo, kwa kuwa kihalisi alichotaka ilikuwa ni kujinufaisha tu yeye mwenyewe na matokeo mazuri kwa upande wao. Baada ya muda, Secretary Joachim akawaacha viongozi hao wa jeshini na kurudi kwenye harakati zingine.
★★★★
Luteni Michael aliambatana na ACP Nora kwenye gari lake kuelekea kwenye jengo dogo ambalo timu yake yenye watu saba wenye uzoefu wa kijeshi/kijasusi walikuwa. Hapo walikuwa na vifaa vya kiteknolojia vya ufatiliaji na taarifa mbalimbali ambazo walikuwa wanafanyia kazi ili kuweza kubaini wezi wale walikuwa wapi. Kihalisi Luteni Michael pia pamoja na timu yake walikuwa wameshaanza kufanyia kazi suala hili siku chache za nyuma, lakini hata wao hawakuwa wamepata ufumbuzi mzuri. Kwa hiyo kile ambacho Nora alikuwa amegundua wangeanza kukifanyia kazi ili kufanikisha zoezi la kuwakamata watu wale.
Wakiwa njiani, waliongelea mambo kadhaa waliyofikiria kuhusiana na matukio haya yote ambayo kwenye vichwa vya watu wengi yalikuwa yenye kushangaza sana.
"Kwa hiyo ulikuja huku kwa usafiri kumbe?" Luteni Michael akamuuliza wakiwa bado mwendoni.
"Yeah. Gari yangu ilipatwa na trouble kidogo, nikaiacha itengenezwe. Ila kuna mtu ataileta huku kufikia kesho," akasema ACP Nora.
"Okay. Nimefatilia kazi zako. Uko vizuri sana. Najua pia huwa haupendelei kuvalia sare za kaki, na kiukweli inakupendezea," Luteni Michael akamwambia.
ACP Nora akatabasamu.
"Hawa jamaa wanaumiza vichwa," Luteni Michael akasema.
"Wanajiita eti Mess Makers. Waliacha sign yenye hayo maneno ili waonekane kama kundi fulani jipya la kigaidi," akasema ACP Nora.
"Ni utoto wenye utoto wa kitoto," akasema Luteni Michael.
"Ila mchezo wao ni wa kikubwa," akasema Nora.
"Unajua... ni sawa kwamba wanafanya mambo kitaalamu na nini... lakini, bado najiuliza hizo pesa walizitoje pale... it just doesn't make sense yaani wangehitaji lori au malori kabisa," akasema Luteni Michael.
"Tukiwashika watasema tu," akasema Nora.
Luteni Michael akamtazama kwa makini. Aliona jinsi mwanamke huyu alivyokuwa makini sana. Uso wake ulizama kwenye tablet yake, akifanya tafiti zake na kuchanganua mambo.
"Ulini-impress sana leo," akasema Luteni Michael.
Nora akamwangalia.
"Kuona umetambua mchezo wa hawa jamaa ndani ya siku moja wakati bado Kanali inamwasha huko chini kwa wiki nzima... kiukweli uko vizuri sana," akasema Luteni Michael.
"Ahahah... watu wako hao wanapenda kujikweza sana lakini jambo dogo namna hiyo hata Koplo angeona mbona," Nora akatania.
"Ahahahah... yeah, ni vyeo vyao tu ndo' vinawasumbua akili, hawana tena ile passion waliyokuwa nayo mwanzoni iliyowafikisha hapo... zaidi tu ni kusema 'kawafunkurunyueni' hao watu... sijui hata hilo neno linamaanisha nini," akasema Michael.
"Ahahahah... me sisemi sana, isije ikawa naongea na mmoja wao..."
"Ahahahah... me siko hivyo. Kazi kazi. Hawa mafala wanasumbua vichwa sana, lakini ndiyo nafurahia hivyo. Mwizi anapenda kukimbizwa, siyo kukamatwa. Kwa hiyo tukishawakamata unakuwa unataka kupumzika kwa kuwa ulikimbiza haswa. Lakini mimi sijui ni kwa nini tu ila...."
"Huwa ni kama bado unataka kuendelea kuwakimbiza," Nora akamalizia.
"Yeah. Ndo' nafurahia," akasema Luteni Michael.
"Mimi napenda zaidi ku-solve puzzle. Kwa hiyo nilipopigiwa tu simu, nikakubali hii ishu. Tunakoelekea sidhani kama itakuwa ngumu sana, ikiwa tu tutakuwa makini," Nora akamwambia.
"Alikupigia simu huyo Secretary?"
"Hapana. Ilikuwa ni Mdeme."
"Una ukaribu sana na Raisi eeh?"
"Siyo kihivyo."
"Mmmm... okay. Kwa level yako ya intelligence ungekuwa sehemu pana zaidi. Kwa nini unabaki kuwa ACP?"
"Napenda hivyo. Napenda... kuwa chini ya mwongozo. Sijui nisemeje yaani... vyeo vya juu huwa viko off sana kwangu. Nafurahia zaidi position niliyonayo," akasema Nora.
Luteni Michael aliweza kuona kama kuna historia fulani nzito ndani ya maisha ya mwanamke huyu. Lakini hakutaka kupeleka mambo sehemu ya kibinafsi zaidi wakati huu kwa kuwa walikuwa wamekutanishwa kikazi, hivyo akaona aiendeleze tu safari yao na mazungumzo zaidi wangefanya wakati mwingine.
Baada ya kufika kwenye jengo ilipokuwepo timu yake, Luteni Michael akawatambulisha watu wake kwa ACP Nora. Wote walikuwa ni wanaume, kwa majina ya Vedastus, Omari, Bobby, Alex, Mishashi, Mario, na Hussein.
Walimkaribisha kirafiki na kwa heshima, kisha Luteni Michael akawajuza kuhusiana na taarifa mpya aliyowaletea ACP Nora. Bila kukawia, Bobby akaanza kuifanyia kazi picha ile, akiisafisha kwa kompyuta ili kuweza kuuona vyema uso wa "chizi" yule. Kisha akaanza kutafuta ulingani na sura za watu ambao walikuwa mkoani hapo kwa miezi michache iliyopita zilizoendana na hiyo, na moja ikawa ndiyo "perfect match," yaani yenyewe kabisa.
Kwa kutumia kompyuta zao maalumu waliweza kubaini mtu huyo alikuwa ni nani kwa kitambulisho alichotumia kama mwananchi. Aliitwa Kevin Dass, miaka 34, naye alifanya kazi ya ujenzi wa nyumba za kisasa kwa muda wa miaka zaidi ya kumi nchini. Huyo ndiyo aliyekuwa chizi wanayemtafuta! Kupitia namba zake za mawasiliano, waliweza kubaini kwamba kwa sasa hakuwa ndani ya mkoa huu, bali mkoa mwingine kabisa wa mbali, yaani Mwanza. Hivyo Luteni Michael akaamuru upesi kwamba waondoke na kuelekea kule ili kumshika haraka sana.
Kwa msaada wa ACP Nora wakawa tayari wamepiga hatua ya haraka mno katika msako huu, na ambacho kilitarajiwa baada ya hapo ingekuwa ni kumaliza kabisa utata uliokuwa umeanzishwa na hao "Mess Makers."
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments